Jumapili, 28 Mei 2023

Siri katika Ukuta wa kulia Machozi


1Nyakati 7:12-16 “Bwana akamtokea Sulemani usiku, akamwambia, Nimesikia uliyoyaomba, na mahali hapa nimejichagulia kuwa nyumba ya dhabihu.  Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao. Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa. Maana sasa nimeichagua nyumba hii na kuitakasa, ili kwamba jina langu lipate kuwako huko milele; yatakuwako na macho yangu, na moyo wangu daima.”

 

Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa hakuna eneo muhimu sana duniani kwaajili ya maombi kama mahali paitwapo ukuta wa kulia machozi The wailing wall au ukuta wa Mashariki The Western wall, Mahali hapa ni mahali ambapo pana siri kubwa sana ya mafanikio ya kiroho kwa mujibu wa biblia na moja ya siri kubwa sana ya mahali hapa ni pamoja na kujibiwa maombi, Maelefu ya Wayahudi na viongozi wengi wakubwa Duniani, kwa karne nyingi  wamekuwa wakipatembelea mahali hapa kwaajili ya Maombi, Ukuta uliitwa jina ukuta wa Machozi kwa sababu wayahudi hufika mahali hapa na kulia au kuomboleza kwaajili ya kukumbuka kubomolewa kwa Hekalu lililokuwa limesimama mahali hapa, Lakini pia huomba mahali hapa kwaajili ya kumsihi Mungu kwaajili ya ujio wa Masihi, wengine huandika maombi yao katika vikaratasi na kuyachomeka katika nyufa za ukuta huo ili Mungu aweze kuyakumbuka maombi yao daima!. Leo tutachukua Muda kuangalia siri iliyoko katika ukuta huu wa kulia machozi kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-


·         Historia fupi ya Ukuta wa kulia Machozi

·         Siri ya Ukuta wa kulia Machozi

·         Kila mtu anaweza kwenda kuomba katika ukuta wa kulia machozi

 

Historia ya Ukuta wa kulia Machozi.

Ukuta wa kulia machozi ni sehemu ya ukuta uliojengwa na Mfalme Herode, Mnamo karne ya Kwanza kwa makusudi ya kuzingira na kutunza eneo la Mlima Moriah ili kwamba eneo la juu yake lipate kujengwa Hekalu lililokuwako Yerusalem, wote tunafahamu ya kuwa Hekalu la Yerusalem liliharibiwa mnamo mwaka wa 70 baada ya Kristo na kuwa mpaka sasa halikuwahi kujengwa tena!, Wayahudi wamekuwa wakihofia kukwea moja kwa moja kwenye eneo hilo kwa kuogopa kumkosea Mungu, na badala yake sasa wamegundua kuwa wanaweza kufanya maombi katika eneo la ukuta huo ambao ulikuwa ni msingi au ukingo wa lililokuwa hekalu ilikuwa ngumu kulipata eneo hilo kwa uhuru zaidi mpaka mara baada ya vita ya siku dita iliyopiganwa mwaka 1967 na kuwapa uhuru mpana wa kupafikia mahali hapo, na tangu wakati huo ndio ilipatikana uwezo usioweza kutikisiaka wa kupatumia mahali hapo Muhimu kwa maombi duniani. 


Siri ya ukuta wa kulia Machozi

Kwa mujibu wa maandiko Mlima wa Hekalu ni mahali muhimu sana ambapo Hekalu la Kwanza la Suleimani lilijengwa na kisha Hekalu la pili ni mahali penye kutazamwa sana na Mungu kwa Mujibu wa Maandiko, Hivyo ukuta wa kulia machozi ni sehemu ya Hekalu lililokuwepo ni msingi, eneo hili kibiblia lina ahadi za ajabu sana,  watu wa Mungu wakiomba katika eneo hilo lazima Mungu atasikia na kufanya:- 


 2Nyakati 7:14 “ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao.” 


Mungu pia ameahidi kuwa macho yake na masikio yake yatafunguka kuelekea maombi yatatakayotolewa kutoka katika mahali hapo  ona 


2Nyakati 7:15-16 “Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa. Maana sasa nimeichagua nyumba hii na kuitakasa, ili kwamba jina langu lipate kuwako huko milele; yatakuwako na macho yangu, na moyo wangu daima.” 


Mahali hapo kama vile tu ilivyokuwepo Nyumba ya Mungu maandiko yameashiria kuwa Mungu ataliweka jina lake mahali hapo milele, eneo hili ni la Wayahudi na lilinunuliwa kwa fedha na Mfalme Daudi ili aweze kutoa dhabihu mahali hapo kwa sababu malaika wa Bwana alisimamisha upanga wake mahali hapo ili asiwaangamize watu ona 


2Samuel 24:18-25 “Basi Bwana akawaletea Israeli tauni tangu asubuhi hata wakati ulioamriwa; nao wakafa watu toka Dani mpaka Beer-sheba sabini elfu. Lakini huyo malaika aliponyosha mkono wake kuelekea Yerusalemu ili auharibu, Bwana akaghairi katika mabaya, akamwambia huyo malaika mwenye kuwaharibu watu, Yatosha, sasa ulegeze mkono wako. Naye yule malaika wa Bwana alikuwako karibu na kiwanja cha kupuria cha Arauna, Myebusi.Daudi, alipomwoma malaika aliyewapiga watu, akanena na Bwana, akasema, Tazama, ni mimi niliyekosa, ni mimi niliyepotoka; lakini kondoo hawa, wamefanya nini? Mkono wako na uwe juu yangu, na juu ya nyumba ya baba yangu. Siku hiyo Gadi akamwendea Daudi, akamwambia, Haya! Kwea wewe, ukamwinulie Bwana madhabahu penye kiwanja cha Arauna, Myebusi. Basi Daudi akakwea sawasawa na neno la Gadi, kama Bwana alivyoamuru. Huyo Arauna akatazama, akamwona mfalme na watumishi wake wakimjia; Arauna akatoka, akasujudu mbele ya mfalme kifulifuli hata nchi. Arauna akasema, Bwana wangu mfalme amemjia mtumwa wake kwa kusudi gani? Naye Daudi akasema, Makusudi ninunue kwako kiwanja hiki, ili nimjengee Bwana madhabahu, ili kwamba tauni ipate kuzuiliwa katika watu.  Arauna akamwambia Daudi, Bwana wangu mfalme na akitwae, akatolee yaliyo mema machoni pake; tazama, ng'ombe hawa kwa sadaka ya kuteketezwa, tena vyombo vya kupuria, na vyombo vya ng'ombe, viko kwa kuni, vitu hivi vyote, Ee mfalme, mimi Arauna nakupa wewe mfalme. Kisha Arauna akamwambia mfalme, Bwana, Mungu wako, na akukubali. Lakini mfalme akamwambia Arauna, La, sivyo; lakini kweli nitavinunua kwako kwa thamani yake; wala sitamtolea Bwana, Mungu wangu, sadaka za kuteketezwa nisizozigharimia. Hivyo Daudi akakinunua hicho kiwanja cha kupuria na wale ng'ombe kwa shekeli hamsini za fedha. Naye Daudi akamjengea Bwana madhabahu huko, akatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. Basi Bwana aliiridhia nchi, na tauni ikazuiliwa katika Israeli.” 


Historia ya mahali hapo inaonekana wazi katika kifungu hicho hapo juu, kwamba ukiacha historia ya kimaandiko, kuwa ni mahali ambapo Mungu alimuamuru Ibrahim akamtoe Isaka kama sadaka katika Mlima Moriah lakini pia unaweza kuona kuwa Daudi alikuja kupanunua kwa kusudi la kumjengea Mungu madhabahu sawa na maelekezo ya kiungu, aidha eneo hili ambalo baadaye Suleimani alijenga Hekalu, na pia Daniel alipokuwa mbali utumwani huko Babeli hata pamoja na kutokuweko kwa hekalu alifungua madirisha ya chumba chake kuelekea mahali hapa kwaajili ya dua na maombi yake yaliyompa mafanikio ona 


Daniel 6:10 “Hata Danieli, alipojua ya kuwa yale maandiko yamekwisha kutiwa sahihi, akaingia nyumbani mwake, (na madirisha katika chumba chake yalikuwa yamefunguliwa kukabili Yerusalemu;) akapiga magoti mara tatu kila siku, akasali, akashukuru mbele za Mungu wake, kama alivyokuwa akifanya tokea hapo.” 


Daniel kupiga magoti na kuelekeza maombi yake katika mji wa Yerusalem miaka mingi hata kabla ya kuweko eneo hili, ni wazi kuwa hakuwa anaelekea Yerusalem peke yake bali mahali hapa muhimu ambapo leo ndio uko ukuta huo wa kulia Machozi kumbuka Daniel alikuwa akifanya hayo wakati Hekalu lilikuwa limebomolewa na Mfalme Nebukadreza, Daniel alifanya hivyo kwa imanina maelekezo ya kimaandiko yaliyoko katika 


1Wafalme 8:35-36 “Ikiwa mbingu zimefungwa, hata hakuna mvua, kwa sababu wamekukosa wewe; kama wakiomba wakikabili mahali hapa, na kulikiri jina lako, na kuiacha dhambi yao, wakati ule utakapowatesa; basi, usikie huko mbinguni, ukaisamehe dhambi ya watumwa wako, na ya watu wako Israeli; unapowafundisha njia iliyo njema, iwapasayo kuiendea; ukanyeshe mvua juu ya nchi yako, uliyowapa watu wako iwe urithi wao.” 


Unaona kumbuka neno wakiomba wakikabili mahali hapa, hii maana yake kama mtunanapana neema ya kufika Yerusalem anaweza kwenda kwenye eneo hili la ukuta wa kulia machozi na kuomba, lakini kama uko nchi ya mbali unaweza kuomba kuelekea eneo hili, hii iko wazi kimaandiko, nafahamu kuwa Yesu ni zaidi ya hekalu, na kuwa maombi yanapaswa kupelekwa kwa Mungu baba kupitia jina la Yesu, lakini hata hivyo ukweli wa kimaandiko unabaki wazi kuwa Mungu alipachagua mahali pale katika ardhi ile aapaweke jina lake mahali hapo hivyo maombi kuelekea mahali hapo bado yanalipa, mtu mmoja alisema unapopata nafasi ya kwenda kuomba mahali hapo usiende na maombi mepesi na ya kawaida bali mazito na ukiwa na imani kubwa kuwa Mungu atayaelekea maombi yako, kutokana na siri hii watu wengi na viongozi wengi wakubwa duniani wamewahi kufika na kufanya maombi katika ukuta wa kulia machozi. 


Kila mtu anaweza kwenda kuomba katika ukuta wa kulia machozi

Kwanini mahali hapa pana mvuto mkubwa sana kwa watu wa aina mbalimbali, na watu maarufu wa aina mbalimbali na wanasiasa na watu kadhaa wa kadhaa hufika mahali hapa ni kwa sababu mahali hapa ni kwaajili ya watu wote na sio Israel Peke yao, wakati Mfalme Suleimani alipokuwa akiweka wakfu mahali hapa, alimuomba Mungu kwaajili ya waisrael na vilevile kwaajili ya wageni ambao watasikia habari za jina la Bwana Mungu wa Israel na kutoka mbali nao wakihitaji kuomba kuelekea katika nyumba ya Mungu au eneo husika basi Mungu awajibu na kuwasikia mpia ona 


2Nyakati 6:32-33 “Hata na mgeni naye, asiyekuwa mmoja wa watu wako Israeli, atakapokuja kutoka nchi iliyo mbali sana kwa ajili ya jina lako kuu, na mkono wako ulio hodari, na mkono wako ulionyoshwa; hao watakapokuja na kuomba wakiielekea nyumba hii; basi usikie huko mbinguni, toka makaoni mwako, ukatende yote atakayokuomba huyo mgeni; ili watu wote wa dunia wapate kulijua jina lako, na kukucha wewe, kama watu wako Israeli, tena wajue ya kuwa nyumba hii niliyoijenga imeitwa kwa jina lako.”


Kifungu hicho cha maandiko kinafungua mlango, kwa kila mtu ambaye sio myahudi anaweza kwenda kuomba katika ukuta wa kulia machozi, kwa kusudi la kumtafuta Mungu na kumcha Mungu, na uzuri wake ni kuwa dua hii ya mfalme Suleimani dua nyake na maombi yake yote yalikubaliwa na Mungu, ni kwaajili ya siri hizi watu wengi wamekuwa wakienda Yerusalem kwa ziara mbalimbali wakipata nafasi hawakosi kufika katika ukuta huu na kufanya dua zao na maombi yao na Mungu anajibu maombi, na utafurahia ahadi zote za Mungu ambazo nyingi ya hizo chanzo chake ni hapa

 

Rev. Innocent Mkombozi Kamote.

 

Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima!

Hakuna maoni: