Jumatatu, 8 Mei 2023

Kupigwa kwa ukuta uliopakwa chokaa!


Matendo 23:1-3 “Paulo akawakazia macho watu wa baraza, akasema, Ndugu zangu, mimi kwa dhamiri safi kabisa nimeishi mbele za Mungu hata leo hivi. Kuhani Mkuu Anania akawaamuru wale waliosimama karibu naye wampige kinywa chake. Ndipo Paulo akamwambia, Mungu atakupiga wewe, ukuta uliopakwa chokaa. Wewe umeketi kunihukumu sawasawa na sheria, nawe unaamuru nipigwe kinyume cha sheria?



Utangulizi

Leo tutachukua muda kwa kutosha kujifunza na kuchambua kwa kina maneno yaliyozungumzwa na Paulo Mtume dhidi ya Kuhani mkuu waliyekuwako wakati huo kama tulivyoweza kuona katika mstari wa msingi

Matendo 23:1-3 “Paulo akawakazia macho watu wa baraza, akasema, Ndugu zangu, mimi kwa dhamiri safi kabisa nimeishi mbele za Mungu hata leo hivi. Kuhani Mkuu Anania akawaamuru wale waliosimama karibu naye wampige kinywa chake. Ndipo Paulo akamwambia, Mungu atakupiga wewe, ukuta uliopakwa chokaa. Wewe umeketi kunihukumu sawasawa na sheria, nawe unaamuru nipigwe kinyume cha sheria?

Katika tafakari yetu leo kuhusu kifungu hiki cha maandiko tunajifunza somo hili KUPIGWA KWA UKUTA ULIOPAKWA CHOKAA Kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

·         Agizo la kutenda haki

·         Paulo hakutendewa haki

·         Kupigwa kwa ukuta uliopakwa chokaa

Agizo la Kutenda haki

Mojawapo ya maagizo ya Mungu kwa mtu awaye yote mwenye mamlaka, ni kuhakikisha kuwa anatenda haki, kila ngazi ya mamlaka duniani ni ngazi ya maamuzi, kwa msingi huo ni muhimu kwa kila mmoja mwenye mamlaka kuhakikisha kuwa anatenda haki, Kutokutenda haki ni kinyume na mapenzi ya Mungu, Mungu aliagiza watu wasitende yasiyo haki katika hukumu ona

Mambo ya walawi 19:15 “Msitende yasiyo haki katika hukumu, usimpendelee mtu maskini, wala kumstahi mwenye nguvu; bali utamhukumu jirani yako kwa haki

Mungu ndiye hakimu wetu mkuu atakayemuhukumu kila mmoja sawa na kutenda kwake na hivyo ni muhimu kwetu tunapokuwa katika ngazi za maamuzi kutenda haki au kuhakikisha kuwa haki inatendeka bila kufanya upendeleo tukikumbuka kuwa Mungu ndiye mtoa sheria na ndiye mwenye kuhukumu, hivyo kila aliye kwenye ngazi ya maamuzi na ajiangalie.

Yakobo 4:12Mtoa sheria na mwenye kuhukumu ni mmoja tu, ndiye awezaye kuokoa na kuangamiza. U nani wewe umhukumuye mtu mwingine?

Na ndio maana maandiko yanatuonya kwamba tujihadhari na hukumu kwa kuwa nasi tutahukumiwa, na kujihadhari na kipimo kile tukipimacho kwani kipimo kilekile tupimacho ndicho tutakachopimiwa,  Mungu ndiye Muhukumu wa ulimwengu mzima na kwake ni lazima atatenda haki na kuisimamia na kuhakikisha kuwa inakuja kufanyiwa malipizo kwa namna yoyote (Karma)

 Mwanzo 18:25 “Hasha usifanye hivyo, ukamwue mwenye haki pamoja na mwovu, mwenye haki awe kama mwovu. Hasha; Mhukumu ulimwengu wote asitende haki?

Ulikuwa ni utambuzi kamili wa Ibrahimu kuwa Mungu wa Mbinguni Mungu wake ana sifa kadhaa wa kadhaa lakini mojawapo yeye ni Muhukumu wa Ulimwengu ni Jaji mkuu nani mwenye haki hivyo alimsihi Mungu kutenda haki wakati anapotaka kuangamiza watu wote katika miji ya Sodoma na Gomora ya kwamba kwa vyovyote hataangamiza watu wema pamoja na waovu, Tabia hii ya uungu ya kutenda haki inapaswa kuwa na kila kiongozi aliyeko katika nafasi ya kufanya maamuzi duniani kwamba ni lazima atende haki, kutenda haki huambatana na Baraka kubwa sana.

Lakini kutokutenda haki ni hatari sana Katika imani ya Kiislamu, Kitabu chao Quran kina Sura maalumu inayoitwa Al – Qariah  maana yake hukumu au mizani, mkazio wake ni kuhukumu kwa haki au kutenda usawa kama inavyofanya mizani, Katika kitabu cha Mithali, Maandiko yanaonya kuhusu Mizani ya hadaa ikiwa na maana ya kutokutenda haki ni chukizo kwa Mungu ona

Mithali 11:1 “Mizani ya hadaa ni chukizo kwa Bwana; Bali vipimo vilivyo sawasawa humpendeza.”

Kwa msingi huo maandiko yanatukumbusha hapa umuhimu wa kutenda, haki na kuhukumu kwa haki, na kufanya mambo sawasawa na Mapenzi ya Mungu na kutokuwahukumu wenzetu katika namna isiyo sahihi

Paulo hakutendewa Haki!

Matendo 23:1-3 “Paulo akawakazia macho watu wa baraza, akasema, Ndugu zangu, mimi kwa dhamiri safi kabisa nimeishi mbele za Mungu hata leo hivi. Kuhani Mkuu Anania akawaamuru wale waliosimama karibu naye wampige kinywa chake. Ndipo Paulo akamwambia, Mungu atakupiga wewe, ukuta uliopakwa chokaa. Wewe umeketi kunihukumu sawasawa na sheria, nawe unaamuru nipigwe kinyume cha sheria?

Mahakama ya kitahudi ambayo huongozwa na kuhani mkuu ikiwa na wataalamu wapatao 70  ambayo ilijulikana kama baraza la wazee (Sanhedrin) ilikuwa imeketi kusikiliza mashauri ya Paulo mtume yaliyoletwa kwa hila na masingizio ya wayahudi, wakati Paulo anapewa nafasi ya kujitetea alianza kwa kuonyesha wazi kuwa ameishi kwa dhamiri safi maana yake yeye hana hatia hata sasa, Neno hilo likiwa kinywani mwa Paulo alipokuwa akianza utetezi wake mara moja hatujui ni kwa chuki au kwa dhamiri gani Kuhani mkuu Anania hakufurahishwa na neno hilo akaamuru waliosimama karibu naye wampige mara moja makofi katika kinywa chake, kwa kitendo hiki Paulo alimwambia Mungu atakupiga wewe, ukuta uliopakwa chokaa, kwa sababu ameketi katika kiti cha hukumu ili ahukumu sawa na sharia lakini anaamuru apigwe kinyume cha Sheria, haki haikutendeka mahali hapo! Paulo kwa ujasiri mkubwa na ushuhuda kuwa anaifanya kazi ya injili sawasawa na wito wake katika Kristo kwa hiyo kimsingi hakuwa na hatia zaidi ya upofu uliokuweko katika baraza ka wazee wa kiyahudi kuhusu mtazamo wao kinyume na injili ya Bwana Yesu! Paulo hakutendewa haki ni kutokana na  na jambo hili Paulo mtume alijua wazi kuwa Mungu atasimama  na kumtetea bila kujali kuwa Anania alikuwa kuhani mkuu andiko linasema hivi

Zaburi 12:5 “Kwa ajili ya kuonewa kwao wanyonge, Kwa ajili ya kuugua kwao wahitaji, Sasa nitasimama, asema Bwana, Nitamweka salama yeye wanayemfyonya.”

Kama haki haipatikani mahali ambapo haki inatakiwa ipatikane maana yeke mahali hapo hapana ustaarabu na yanayofanyika hayana tofauti na yanayofanywa na wanyama, Mwanadamu anapaswa kuwa kiumbe kilicho staarabika na kama hakuna ustaarabu maana yake hakuna tofauti na ulimwengu wa wanyama Mungu anataka haki itendeke

Muhubiri 3:16 “Zaidi ya hayo, nikaona tena chini ya jua ya kwamba, Mahali pa hukumu upo uovu, Na mahali pa haki upo udhalimu. Nikasema moyoni mwangu, Mungu atawahukumu wenye haki na wasio haki; kwa kuwa kuna wakati huko kwa kila kusudi na kwa kila kazi. Nikasema moyoni mwangu, Ni kwa sababu ya wanadamu, ili Mungu awajaribu, nao waone ya kuwa wao wenyewe wafanana na wanyama.”

Muhubiri 4:1 “Kisha nikarudi na kuona madhalimu yote yanayotendeka chini ya jua; na tazama, machozi yao waliodhulumiwa, ambao walikuwa hawana mfariji; na upande wa wale waliowadhulumu kulikuwa na uwezo, walakini wale walikuwa hawana mfariji.”

Dhuluma inapotendeka na haki inapopotoshwa Mungu hataweza kutulia ataingilia kati na kuileta hukumu kwa haraka kama ilivyosema Zaburi 12:5 kwa hiyo ni muhimu kufuatilia na kuona kuwa haki inatendeka katika jamii, Je swala la kumpiga kofi mtume Paulo mdomoni ili asijitetee na  na asiendelee kusema kuwa hana hatia je ni swala dogo? Mbele za Mungu haikuwa jambo jema na hata mbele za Paulo mwenyewe na ndio maana Paulo aliamua kumuachoa Mungu na kumhakikishai kuhani mkuu kuwa Mungu Atampiga! Je kuhani mkuu alipigwa  na Mungu kama Paulo alivyosema?

Kupigwa kwa ukuta uliopakwa chokaa!

Kabla ya kuangalia kama Kuhani mkuu alipigwa na Mungu au la jambo la kwanza ni jina alilopewa na Paulo mtume kwa kuitwa ukuta uliopakwa chokaa! Hii ilikuwa na maana gani, kwa kawaida usemi huu hauna tofauti na ule usemi wa Yesu Kristo alipokuwa akiwakemea Mafarisayo kutokana na tabia zao za kinafiki aliwaita makaburi yaliyopakwa chokaa

Mathayo 23:27-28 “Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mmefanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, nayo kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu, na uchafu wote. Vivyo hivyo ninyi nanyi, kwa nje mwaonekana na watu kuwa wenye haki, bali ndani mmejaa unafiki na maasi.”

Unaona mwanadamu awaye yote anayeketi katika kiti cha hukumu na kuhukumu wengine wakati nay eye mwenyewe akiwa sio mkamilifu, ana dhambi tena chafu kuliko za wale anaowahukumu huyo ni ukuta uliopakwa chokaa ni kaburi ambalo limepakwa chokaa kwa nje linaonekana kuwa jema lakini kwa ndani limejaa mifupa ya wafu, ukuta uliopakwa chokaa ni wa watu ambao ndani ni waovu wana hatia, lakini hawatendi haki, wanajidai haki lakini ni wanafiki wakubwa! Paulo alimkemea kuhani mkuu kwa tabia ya kinafiki ya kuamuru apigwe kinyume cha Sheria wakiwa katika mahakama ya kiyahudi kwaajili ya kutafuta haki lakini pamoja na hayo alitabiri kuwa Mungu atampiga kuhani mkuu je hili lilitimia?

Kwa mujibu wa Historia Mwana historia Mashuhuri aitwaye A.C Harvey anamuelezea Ananias kuwa alikuwa mtu Jeuri sana, mwenye kiburi, mroho mwenye uchu, akiamua ameamua na mwenye utawala wa kiimla maneno anayotumia kumueleza katika ikiingereza ni a Violent, Haughty, gluttonous and rapacious man. Japo alikubalika kwa wayahudi,kwa maelekezo hayo na kwa vyovyote vile mtu huyu hakuwa na wema ndani yake, Mungu alimpiga kwa maelezo ya Mwanahistoria mashuhuri wa kiyahudi wa karne ya Kwanza alitwaye Flavious Josephus , Annania alijihusisha na uasi dhidi ya serikali ya kirumi na kushutumiwa vikali na gavana wa Syria alishitakiwa huko Roma na kupelekwa kwa Kaisari Claudius kati ya mwaka wa 52 baada ya Kristo, Claudius alimuongeza muda wa kuendelea na ukuhani mpaka mwaka wa 58, akiwa kibaraka mkubwa wa warumi, alikamatwa na kuuawa na wayahudi wenye msimamo mkali mwanzoni mwa vita kati ya wayahudi na warumi, Na hivyo kutimizwa kwa maneno ya Mtume Paulo kuwa Bwana atakupiga ukuta uliopakwa chokaa, Mungu hatawaqacha watu wake hususani watumishi wake waonewe, haki tasimama hata kama hao wanaoonea watumishi wa Mungu ni wenye mamlaka ya kifalme au la Zaburi 105:14-15 “Hakumwacha mtu awaonee, Hata wafalme aliwakemea kwa ajili yao. Akisema, Msiwaguse masihi wangu, Wala msiwadhuru nabii zangu.”

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima!

Hakuna maoni: