Luka 24:46-49 “Akawaambia, Ndivyo
ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba
mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi,
kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya. Na tazama,
nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe
uwezo utokao juu.”
Utangulizi:
Ni muhimu kwa kila mmoja kuwa na
ufahamu, ya kwamba uhai wa kanisa unategemeana sana na jinsi au namna Kanisa
linavyompa nafasi Roho Mtakatifu kufanya kazi pamoja nasi, Endapo kanisa
litaendelea na kazi zake za kutimiza agizo kuu bila kutoa nafasi kwa mwenye
kanisa yaani Roho Mtakatifu, itakuwa ni rahisi sana kanisa kupoteza nguvu zake
na kubaki na hekima ya kibinadamu, jambo ambalo linaweza kutuletea aibu na
kushindwa vibaya, ni kwa kuzingatia hilo leo katika siku ya Pentekoste ni
muhimu kwa kila mmoja wetu kujikumbusha tena umuhimu wa kumpa nafasi Roho Mtakatifu
kufanya kazi pamoja nasi vinginevyo au kinyume chake usiende bila Roho
Mtakatifu au uwezo utokao juu!.
Mathayo 28:18-20 “Yesu akaja kwao, akasema
nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni,
mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana,
na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na
tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.”
Tutajifunza somo hili kwa
kuzingatia vipengele viwili muhimu vifuatavyo:-
Agizo la
kwenda kuihubiri injili
Agizo la
kutokwenda bila uwezo utokao juu
Agizo la kwenda kuihubiri injili.
Moja ya agizo muhimu sana na
ambalo ndio msingi wa uwepo wa Kanisa duniani ni kuihubiri injili, Yesu Kristo
aliwandaa wanafunzi wake kwa muda wa kutosha ili hatimaye aweze kuwatuma kwenda
kuihubiri injili
Marko 3:13-15 “Akapanda mlimani, akawaita
aliowataka mwenyewe; wakamwendea.
Akaweka watu kumi na wawili, wapate kuwa pamoja naye, na kwamba awatume
kuhubiri, tena wawe na amri ya kutoa pepo.”
Unaona kusudi kubwa na Yesu
Kristo kuwaita mitume au wanafunzi wake ni ili awafundishe waweze kuwa pamoja
naye wakae katika uwepo wake kisha baada ya hayo aweze kuwatuma kwenda
kuihubiri injili, haya ndio makusudi makubwa zaidi ya uwepo wa kanisa, kila
kanisa linawajibu wa kuihubiri injili, kuhubiri injili ya Bwana wetu Yesu
Kristo kwa watu wote ndio mapenzi ya Mungu, kanisa lisilo hubiri injili ni
kanisa lisilo na utii kwa kazi ya Kristo ni kanisa linalozimika katika moto wa
injili, nachelea kusema ni kanisa lililokufa; lakini ni wazi kuwa litakuwa ni
kanisa lililopoteza mwelekeo, ni lazima tuihubiri injili, ni lazima tuwafikie watu
wa mataifa yote na vile vile na kuwafungua kutoka katika nguvu za giza yaani vifungo
vya shetani na kutoa pepo wachafu kwa wanaoonewa nao,
Marko 16:15-18 “Akawaambia, Enendeni
ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa
ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio;
kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata
wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya
wagonjwa, nao watapata afya.”
Agizo hili kubwa ni la muhimu
sana watu waokolewe na kufunguliwa kutoka katika nguvu za giza ili wahamishiwe
kwenye ufalme wa mwana wa pendo lake, kila kanisa na kila mtu anayetambua
umuhimu wa agizo hili kuu anapaswa kulitii na kuhakikisha kuwa linafanyiwa kazi
na hayo ndio mapenzi ya Mungu. Kuna changamoto kiasi Fulani katika kanisa la
leo, ya kuwa watu wengine wamejikita sana katika kuwafungua watu bila kuhakikisha
kuwa watu hao wanatubu dhambi zao na kumwamini Bwana Yesu, mambo haya
yanahitaji uwiano, lakini kubwa zaidi tunapolitimiza agizo kuu Bwana mwenyewe
atakuwepo kulithibitisha neno kwa ishara na miujiza, hivyo miujiza iwe ni
sehemu tu ya kuthibitishwa kwa neno na sio biashara ya kuponywa tu kwa miili ya
watu hao ili hali nafsi na roho zao zingali kifungoni, ni muhimu sana kuihubiri
injili sawa na agizo la Bwana wetu Yesu Kristo na hayo ndio mapenzi ya Mungu
Agizo la kutokwenda bila uwezo utokao juu.
Pamoja na umuhimu mkubwa wa agizo
hili kuu na msisitizo wake ni muhimu sana tukatilia maanani kuwa ndani ya agizo
kuu Yesu mwenyewe vilevile alisisitiza wanafunzi wake wasiende bila kuvikwa
uwezo utokao juu! Ona
Luka 24:46-49 “Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa
na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake
habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi ndinyi
mashahidi wa mambo haya. Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini
kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu.”
Uwezo huo utokao juu ni nini na
unapatikanaje? uwezo huu utokao juu ni matokeo ya nguvu za Mungu kuwa juu ya
wale waliomuamini Bwana Yesu na waliotayari kulitimiza agizo kuu, uwezo huu
unapatikana baada ya Roho Mtakatifu kuja juu yetu ona
Matendo 1:8 “Lakini mtapokea nguvu, akiisha
kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika
Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.”
Kwa nini Yesu Kristo alisisitiza
kwamba wanafunzi wake wasiende bila uwezo huo kutoka juu yaani Bila kupokea
nguvu kutoka kwa Mungu Roho Mtakatifu? Sababu kubwa mojawapo ni kuwa kazi ya
kuihubiri injili ina upinzani, ina upinzani wa aina mbalimbali, kutoka kwa
watu, dini zao, tamaduni zao, serikali zao na miungu yao na nguvu za giza,
hivyo kuna nguvu za upinzani ambazo ni ngumu kuzikabili katika hali ya kawaida
ya kibinadamu bila neema na msaada wa Mungu, kujaribu kufanya kazi za injili na
hata kukemea pepo bila kuwa na nguvu za kukabiliana na mapepo hayo na upinzani
huo ni hatari sana na rahisi kujikuta unakata tamaa na kuingia katika kuabishwa
na upinzani wa kishetani, hatuwezi kuigiza kwa kuwa shetani anaogopa wazi nguvu
ya Mungu na anajua watu wanaotumiwa na Mungu na wale wanaoigiza!
Matendo 19:11-20 “Baadhi ya Wayahudi wenye
kutanga-tanga, nao ni wapunga pepo, wakajaribu kutaja jina la Bwana Yesu juu
yao waliopagawa na pepo wachafu, wakisema, Nawaapisha kwa Yesu, yule
anayehubiriwa na Paulo. Walikuwako wana saba wa mtu mmoja Skewa, Myahudi,
kuhani mkuu, waliofanya hivyo. Yule pepo mchafu akawajibu, akawaambia, Yesu
namjua na Paulo namfahamu, lakini ninyi ni nani? Na yule mtu aliyepagawa na
pepo mchafu akawarukia wawili, akawaweza, akawashinda, hata wakatoka mbio
katika nyumba ile hali wa uchi na kujeruhiwa. Habari hii ikajulikana na
Wayahudi wote na Wayunani waliokaa Efeso, hofu ikawaingia wote, na jina la
Bwana Yesu likatukuzwa. Na wengi wa wale walioamini wakaja wakaungama,
wakidhihirisha matendo yao. Na watu wengi katika wale waliotumia mambo ya
uganga wakakusanya vitabu vyao, wakavichoma moto mbele ya watu wote; wakafanya
hesabu ya thamani yake, wakaona ya kwamba yapata fedha hamsini elfu. Hivyo
ndivyo neno la Bwana lilivyozidi na kushinda kwa nguvu.”
Unaona kutoka katika kifungu hiki
cha maandiko tunaona mambo makubwa mawili, watu waliojaribu kukemea mapepo kwa
jina la Yesu huku wakiwa hawajavikwa uwezo ule utokao juu, wala hata kuokoka! na matokeo yake walipigwa na kujeruhiwa vibaya
kwa sababu hawakuwa na nguvu wala mamlaka ya kutoa Pepo, lakini Paulo mtume
alitumiwa na Mungu kwa miujiza Mingi na zaidi sana hata watu waliotumia uganga
walibadilika na kuchoma moto vitabu vyao vya uchawi vyenye gharama kubwa sana,
Paulo mtume hakufanya haya kwa nguvu zake, alijaa Roho Mtakatifu alitumiwa na
Mungu, ikiwa kanisa linataka kuona nguvu za Mungu ni lazima tutii agizo kuu
lakini wakati huo huo tusiende bila uwezo utokao juu, yaani bila nguvu za Mungu
Roho Mtakatifu ndani yetu!
Mungu hajawahi kumtuma mtu katika
kazi fulani bila nguvu zake, nguvu za Roho wake Mtakatifu zinamuwezesha mtu huyo
kukabiliana na upinzani kutoka kwa maadui wa injili, alipomtuma Musa dhidi ya Farao,
kwa kusudi la kuwaokoa wana wa Israel katika nchi ya Misri, alimpa nguvu za
kupambana na serikali ile iliyokuwa ikitumainia miungu na nguvu za giza
zilizoongozwa na wachawi maarufu walioitwa Yane na Yambre ambao kimsingi
walishindana na Musa na Haruni kwa kufanya kiujiza ya kuigiza ona
2Timotheo 3:8 “Na kama vile Yane na Yambre
walivyopingana na Musa, vivyo hivyo na hawa wanapingana na ile kweli; ni watu
walioharibika akili zao, wamekataliwa kwa mambo ya imani.”
Unaona hawa walikuwa wachawi
wakuu wa serikali pinzani ya Farao ambayo ilijawa na kuabudu miungu na
kutegemea uganga na uchawi, Musa na Haruni na wazee wa Israel wangewezaje kudai
uhuru katika serikali ya aina ile bila Nguvu za Mungu? Hatuwezi kuwasaidia watu bila nguvu ya Mungu
izidiyo nguvu zote!
Kutoka 7:20-22 “Musa na Haruni wakafanya
hivyo, kama BWANA alivyowaambia; naye akaiinua ile fimbo, na kuyapiga maji
yaliyokuwa mtoni, mbele ya Farao, mbele ya watumishi wake; na hayo maji yote
yaliyokuwa katika mto yakageuzwa kuwa damu. Hao samaki waliokuwa mtoni nao
wakafa; na ule mto ukatoa uvundo, Wamisri wasipate kunywa maji ya mtoni; na ile
damu ilikuwa katika nchi yote na Misri. Lakini waganga wa Misri wakafanya mfano
wa hayo kwa uganga wao; na moyo wake Farao ukawa mgumu, wala hakuwasikiza, kama
BWANA alivyonena.”
Mwinjilisti Filipo alipokwenda
kuihubiri injili katika eneo la Samaria alikutana na mtu aliyekuwa mchawi na
aliyekuwa na nguvu za giza ambazo watu wengi waliamini ni uweza wa Mungu, mtu
huyu aliiamini injili na kubatizwa lakini bado alikuwa na moyo wa kichawi mpaka
alipokuja kushughulikiwa na Roho Mtakatifu wakati Petro na Yohana walipokwenda
kutoa msaada wa kihuduma kule Samaria, ni hatari sana kama kanisa litafanya
kazi chini ya kiwango cha nguvu za Mungu zinazohitajika na ndio maana leo kuna
shuhuda za kuwepo kwa wachawi makanisani wakiingia na kutoka na kujifanyia
uchawi wao na kanisa linaogopa tunawezaje kukabiliana na haya usiende bila
uwezo utokao juu, lazima tujae ngvu za Roho Mtakatifu katika kiwango cha
kufurika ona :-
Matendo 8:5-21 “Filipo akatelemka akaingia
mji wa Samaria, akawahubiri Kristo. Na makutano kwa nia moja wakasikiliza
maneno yale yaliyosemwa na Filipo walipoyasikia na kuziona ishara alizokuwa
akizifanya. Kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia
kwa sauti kuu; na watu wengi waliopooza, na viwete, wakaponywa. Ikawa furaha
kubwa katika mji ule. Na mtu mmoja, jina lake Simoni, hapo kwanza alikuwa
akifanya uchawi katika mji ule, akiwashangaza watu wa taifa la Wasamaria,
akisema ya kuwa yeye ni mtu mkubwa. Wote wakamsikiliza tangu mdogo hata mkubwa,
wakisema, Mtu huyu ni uweza wa Mungu, ule Mkuu. Wakamsikiliza, kwa maana
amewashangaza muda mwingi kwa uchawi wake. Lakini walipomwamini Filipo,
akizihubiri habari njema za ufalme wa Mungu, na jina lake Yesu Kristo,
wakabatizwa, wanaume na wanawake. Na yeye Simoni mwenyewe aliamini akabatizwa,
akashikamana na Filipo; akashangaa alipoziona ishara na miujiza mikubwa
inayotendeka. Na mitume waliokuwako Yerusalemu, waliposikia ya kwamba Samaria
imelikubali neno la Mungu, wakawapelekea Petro na Yohana; ambao waliposhuka,
wakawaombea wampokee Roho Mtakatifu; kwa maana bado hajawashukia hata mmoja
wao, ila wamebatizwa tu kwa jina lake Bwana Yesu. Ndipo wakaweka mikono yao juu
yao, nao wakampokea Roho Mtakatifu. Hata Simoni alipoona ya kuwa watu wanapewa
Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono ya mitume, akataka kuwapa fedha akisema,
Nipeni na mimi uwezo huu, ili kila mtu nitakayemweka mikono yangu, apokee Roho
Mtakatifu. Lakini Petro akamwambia, Fedha yako na ipotelee mbali pamoja nawe,
kwa kuwa umedhania ya kuwa karama ya Mungu yapatikana kwa mali.”
Nadhani sasa unaweza kumuelewa
Bwana Yesu kwanini alisisitiza usiende bila kuvikwa uwezo utokao juu, upinzani
wowote katika injili unaweza kuzimwa endapo tu tutamruhusu Roho Mtakatifu Mungu
kuwa pamoja nasi katika kazi hii, sio tu katika nguvu za giza pekee bali hata
kuitetea imani na kukubali kuwa mashahidi na kufa kwaajili ya Kristo bila nguvu
hizo ni vigumu kustahimili hata majaribu na upinzani dhidi ya injili na
watumishi wa kweli ona
Matendo 6: 8-10 “Na Stefano, akijaa neema
na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu. Lakini baadhi
ya watu wa sinagogi lililoitwa sinagogi la Mahuru, na la Wakirene, na la
Waiskanderia, na la wale wa Kilikia na Asia, wakaondoka na kujadiliana na
Stefano; lakini hawakuweza kushindana na hiyo hekima na huyo Roho aliyesema
naye.”
Katika kila kazi ambayo Mungu
anampa mtu na au kumtuma mtu anampa nguvu hizo za Roho Mtakatifu ili
kukabiliana na upinzani wake Samsoni aliitwa kuwa mwamuzi dhidi ya wafilisti
waliokuwa wakiwaonea Waisraeli wakati huo hakuenda Samsoni bila uwezo huo
utokao juu Nguvu za Mungu zlimfanya
samsoni kuwa wa kipekee ona
Waamuzi 15:14-16 “Alipofika Lehi, Wafilisti wakapiga kelele walipokutana
naye; ndipo roho ya Bwana ikamjia kwa nguvu, na zile kamba zilizokuwa juu ya
mikono yake zikawa kama kitani iliyoteketezwa kwa moto, na vile vifungo vyake
vikaanguka mikononi mwake. Naye akaona mfupa mbichi wa taya ya punda, akautwaa,
akapiga watu elfu kwa mfupa huo; Samsoni akasema, Kwa taya ya punda chungu juu
ya chungu, Kwa taya ya punda nimepiga watu elfu.”
Vilevile Mungu alipomuinua Eliya
dhidi ya manabii wa baali Mungu alimpa Eliya uwezo utokao juu ulioweza
kudhihirisha nguvu za Mungu aliye hai na kuwafanya watu waliokuwa wanasita sita
kumgeukia Mungu na kurejea kwake 1Wafalme
18:21-40, Pia Paulo mtume alikutana na Elima yule mchawi kule Cyprus Matendo 13:6-12 na Daniel aliweza
kuonekana kuwa mwenye majibu katika serikali ya Nebukadreza na Belshaza kuliko
wanajimu na wachawi kwa sababu Roho Mtakatifu alikuwa juu yake
Kwa hiyo unaweza kuona ni hatari
na aibu kubwa kwenda bila uwezo utokao juu, kanisa tunapaswa kumuomba Mungu
wakati wote na kuhakikisha kuwa wakati wote tunajaa nguvu za Mungu, kwaajili ya
usalama wetu, na kwaajili ya kuthibitisha uwepo wa Mungu na kukabiliana na
nguvu za kipinzani, Roho Mtakatifu ni ahadi ya Mungu, ahahdi za Mungu
zimehakikishwa, na Mungu ni mwaminifu katika ahadi zake, yeye huliangalia neno
lake ili aweze kulitimiza ni muhimu kwetu kuhakikisha kuwa kama kuna jambo la
Muhimu la kuliombea ni kujaa Roho Mtakatifu, Nguvu hizi ndio silaha yetu ya
ushindi wakati wa upinzani, kazi ya Mungu ina vita katika ulimwengu wa roho,
ziko protoko za kipepo zinazoshindana na injili na watenda kazi wote kwa hiyo
ni muhimu kukumbuka na kumkumbusha Mungu
atupe neema hii tusiende bila uwezo utokao juu, nguvu hii ni moja ya silaha
muhimu katika vita zetu za rohoni!
2Wakorintho 10:3-4 “Maana ingawa tunaenenda
katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; (maana silaha za vita vyetu si
za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;)”
Unaona iko vita katika ulimwengu
wa roho, haionekani katika macho ya kawaida lakini wakati mwingine hujitokeza
katika ulimwengu wa mwili asili ya kila kitu ni rohoni, hivyo lazima tuwe hodari
katika Bwana na katika uwezo wa nguvu zake kwa kuvaa silaha zote mojawapo ikiwa
nimkusali katika Roho, tunawezaje kufanya hivyo lazima tuwe pia tumevikwa uwezo
kutoka juu ona
Waefeso 6:10-18 “Hatimaye, mzidi kuwa
hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu,
mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu
ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili,
juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu,
mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.
Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani,
na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani; zaidi ya yote mkiitwaa
ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule
mwovu. Tena ipokeeni chapeo ya wokovu,
na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu; kwa sala zote na maombi mkisali kila
wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea
watakatifu wote;”
Usiende bila uwezo utokao juu,
wanafunzi wa Yesu walimuelewa Bwana na walikaa katika maombi katika chumba cha
juu pale Yerusalem wakafunga na kuomba kwa siku kumi, siku ya 50 Pentekoste
Roho Mtakatifu alikuja juu yao na kuwafanya kuwa na ujasiri, watu ambao awali
walikuwa wakijifungia kwa hofu ya wayahudi, sasa walikuwa tayari kukabiliana na
kila aina ya upinzani wakivikwa ujasiri na wakaipeleka injili kwa ujasiri bila
kujali mazingira magumu waliyokutana nayo. Injili hiiambayo kanisa limeipokea
duniani kote hata leo, ilitokana na kanisa la kwanza kuzingatia sana swala zima
kuhusu ujazo wa Roho Mtakatifu, endapo tutafuata nyao zao kanisa halitakuwa na
kitu cha kupoteza! Injili itawafikiwa watu, maisha ya watu yatabadilishwa na
hakutakuwa na utata kwa miujiza inayofanywa chini ya utendaji wa Mungu
mwenyewe, ukomavu wa wakristo na watumishi wa Mungu utaonekana na matunda ya
Roho Mtakatifu yataonekana katika maisha yetu ya kila siku! Asante kwa
kufuatilia mafundisho yangu uongezewe neema kumbuka usiende bila uwezo utokao
juu!
Na Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni