Jumapili, 14 Januari 2024

Tazama mwana kondoo wa Mungu!


Yohana 1:26-30 “Yohana akawajibu akisema, Mimi nabatiza kwa maji. Katikati yenu amesimama yeye msiyemjua ninyi. Ndiye yule ajaye nyuma yangu, ambaye mimi sistahili kuilegeza gidamu ya kiatu chake. Hayo yalifanyika huko Bethania ng'ambo ya Yordani, alikokuwako Yohana akibatiza. Siku ya pili yake amwona Yesu anakuja kwake, akasema, Tazama, MWANA-KONDOO WA MUNGU, aichukuaye dhambi ya ulimwengu! Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Yuaja mtu nyuma yangu, ambaye amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu.”




 

Utangulizi:

Nyakati za agano la kale, Watu walipotaka kumuabudu Mungu, na aidha kurejesha au kuendeleza uhusiano na Mungu, kwa vile Mungu ni Mtakatifu, uovu na dhambi ulikuwa umemtenga mwanadamu mbali na uwepo wa Mungu, hivyo njia ya kumfikia Mungu ilikuwa ni lazima imwagike damu, na ndipo Mungu aweze kuridhia uhusiano unaotafutwa na mwanadamu, kupitia damu ya Mwanakondoo, ambaye alikuwa anakufa kwa niaba ya Mwanadamu au wanadamu ili aweze kuwakubali, kwa msingi huo utaweza kuona kuwa utamaduni wa kuchinja kama njia ya kuwasiliana na Mungu unazingatiwa sana pia katika makafara ya dini za kienyeji ambazo ziko maelefu kwa maelfu katika jamii ya aina binadamu. Hii ndio ilikuwa njia ya kwanza kabisa ya mwanadamu kuridhiwa na Mungu unaona?

Mwanzo 4:2-5 “Akaongeza akamzaa ndugu yake, Habili. Habili alikuwa mchunga kondoo, na Kaini alikuwa mkulima ardhi. Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa BWANA. Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. BWANA akamtakabali Habili na sadaka yake; bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana.”

Kwa hiyo utoaji wa sadaka/kafara za wanyama na kuteketeza ndio ilikuwa njia ya zamani zaidi ya mwanadamu kuuakaribia uwepo wa Mungu na kuridhiwa, wanyama wote yaani wanyama safi wasio najisi wangeweza kutumika kwa jambo hili lakini Kondoo ndiye aliyekuwa mnyama bora zaidi aliyenona na ambaye angeweza kufaa kwa sadaka au kafara za wanadamu kwa Mungu.  Je mwana kondoo alikuwa akimaanisha nini katika lugha ya kinabii? Hilo linatupa nafasi ya kuchukua muda leo, kutafakari kwa kina na mapana na marefu, kuhusu somo hili Tazama mwana kondoo wa Mungu kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo!

·         Mwanakondoo katika unabii

·         Nguvu ya Damu ya mwanakondoo

·         Tazama mwanakondoo wa Mungu


Mwanakondoo katika unabii

Ni muhimu kufahamu kuwa katika lugha ya kinabii, kondoo alikuwa akimwakilisha Mwanadamu, yaani kimsingi, mwanadamu ndiye aliyetakiwa kufa, lakini kwa rehema za Mungu alikuwa anaridhika kwa muda pale inapopatikana damu mbadala, lakini kwa uwazi kabisa kondoo alikuwa akimaanisha mwanadamu au kusimama kwa niaba ya mwanadamu katika lugha ya kinabii unaweza kuona kwa mfano katika kifungu cha maandiko kifuatacho:-

2Samuel 12:1-6 “Ndipo Bwana akamtuma Nathani aende kwa Daudi. Naye akamwendea, akamwambia, Palikuwa na watu wawili katika mji mmoja; mmoja wao alikuwa tajiri, wa pili maskini. Yule tajiri alikuwa na kondoo na ng'ombe wengi sana; bali yule maskini hakuwa na kitu, ila mwana kondoo mmoja, mdogo, ambaye amemnunua na kumlea; naye akakua pamoja naye, na pamoja na wanawe; hula sehemu ya posho lake, na kukinywea kikombe chake, na kulala kifuani mwake, akawa kwake kama binti. Hata msafiri mmoja akamfikilia yule tajiri, naye akaacha kutwaa mmoja wa kondoo zake mwenyewe au mmoja wa ng'ombe zake mwenyewe, ili kumwandalia yule msafiri aliyemfikilia, bali alimnyang'anya yule maskini mwana-kondoo wake, akamwandalia yule mtu aliyemfikilia. Ndipo hasira ya Daudi ikawaka sana juu ya mtu yule; akamwambia Nathani, Aishivyo Bwana, mtu huyo aliyetenda jambo hili, hakika yake astahili kufa; naye atamrudishia yule mwana-kondoo mara nne, kwa sababu ametenda neno hili, na kwa sababu hakuwa na huruma.”

Unapoangalia kifungu hiki cha maandiko, utaweza kuona Lugha ya kinabii inayotumiwa na nabii Nathani katika kuikabili dhambi ya Mfalme Daudi, Daudi alikuwa amefanya dhambi ya zinaa na dhambi hii iliambatana na ujauzito, na ili kuuficha ule ujauzito wa mke wa mtu, alitumia hila mbalimbali ambazo zilishindikana kumlaghai mume wa Bathsheba yaani Uria ili akalale kwa mkewe kwa kusudi la kumchomekea lakini alikataa, na hivyo kwa hila aliwekwa mstari wa mbele katika vita ili afe, na kisha yeye akamuoa mwanamke yule akiwa na mimba yake, kitendo cha kumuua Uria ni kitendo cha kuchinja Kondoo wa mtu masikini na katika habari hii Daudi alihukumu kuwa mtu huyo anastahili kufa yaani yeye, lakini pia anapaswa kulipa yule mwana kondoo mara nne! Hii ilikuwa ina maana Daudi alitakiwa afe, lakini vilevile walitakiwa wafe watu wanne katika familia yake, sasa ingawa Daudi alisamehewa baada ya toba na kifo kiliondolewa kwake hata hivyo watoto wake wanne Walikufa sawasawa na lugha ile ya kinabii:-

1.       Mtoto wa Daudi aliyezaliwa na Bathsheba – 2Samuel 12:15-23 “Naye Nathani akaondoka kwenda nyumbani kwake. Basi Bwana akampiga yule mtoto ambaye mkewe Uria alimzalia Daudi naye akawa hawezi sana. Basi Daudi akamwomba Mungu kwa ajili ya mtoto; Daudi akafunga, akaingia, akalala usiku kucha chini.Nao wazee wa nyumba yake wakaondoka, wakasimama karibu naye, ili wamwinue katika nchi; lakini hakukubali, wala hakula chakula pamoja nao. Ikawa siku ya saba, yule mtoto akafa. Nao watumishi wa Daudi wakaogopa kumwambia ya kuwa mtoto amekufa, maana, walisema, Angalieni, yule mtoto alipokuwa angali hai, tulisema naye, asitusikilize sauti zetu; basi hatazidi kujisumbua, tukimwambia ya kuwa mtoto amekufa? Lakini alipoona ya kuwa watumishi wake wananong'onezana, Daudi alitambua ya kuwa mtoto amekufa; basi Daudi akawauliza watumishi wake, Je! Mtoto amekufa? Nao wakasema, Amekufa. Ndipo Daudi akainuka pale chini akaoga, akajipaka mafuta, akabadili mavazi yake; akaingia nyumbani mwa Bwana, akasali; kisha akaenda nyumbani kwake, na alipotaka wakamwandalia chakula, naye akala. Watumishi wake wakamwambia, Ni neno gani hili ulilolitenda? Ulifunga na kulia kwa ajili ya mtoto, alipokuwa hai; lakini mtoto alipokuwa amekufa, uliinuka ukala chakula. Akasema, Mtoto alipokuwa hai, nalifunga, nikalia; kwa maana nalisema, Ni nani ajuaye kwamba Bwana atanihurumia, mtoto apate kuishi? Lakini sasa amekufa nifungie nini? Je! Naweza kumrudisha tena? Mimi nitakwenda kwake lakini yeye hatanirudia mimi.”        


2.       Mtoto wa Daudi aitwaye Amnoni - 2Samuel 13:28-33 “Kisha Absalomu akawaamuru watumishi wake, akasema, Angalieni basi, moyo wake Amnoni utakapofurahiwa kwa mvinyo; nami nitakapowaambia, Mpigeni Amnoni, ndipo mwueni, msiogope; si mimi niliyewaamuru? Iweni hodari, iweni na ujasiri. Basi watumishi wa Absalomu wakamfanyia Amnoni kama alivyoamuru Absalomu. Ndipo wakaondoka wana wote wa mfalme, wakapanda kila mtu nyumbu wake, wakakimbia. Ikawa, walipokuwa njiani, habari zikamwasilia Daudi, kusema, Absalomu amewaua wana wote wa mfalme, wala hata mmoja wao hakusalia. Ndipo mfalme akainuka, akararua nguo zake, akalala chini; nao watumishi wake wote wakasimama karibu naye, wenye nguo zao zimeraruliwa. Akajibu Yonadabu, mwana wa Shama, nduguye Daudi, akasema, Asidhani bwana wangu ya kwamba wamewaua vijana wote, wana wa mfalme; maana ndiye Amnoni peke yake aliyekufa; yakini haya yamekusudiwa kwa kinywa chake Absalomu tangu siku ile alipotenzwa nguvu umbu lake, Tamari.Basi sasa bwana wangu mfalme asilitie neno hili moyoni, kudhani ya kwamba wana wote wa mfalme wamekufa maana ni Amnoni peke yake aliyekufa.”

               

3.       Mtoto wa Daudi aitwaye Absalom – 2 Samuel 18:9-15 “Na kwa bahati Absalomu akakutana na watumishi wa Daudi. Naye Absalomu alikuwa amepanda nyumbu wake, na yule nyumbu akapita chini ya matawi manene ya mwaloni mkubwa, hata kichwa chake kikakwama katika mwaloni huo, akanyakuliwa juu kati ya mbingu na nchi; na yule nyumbu aliyekuwa chini yake akaenda mbele. Basi mtu mmoja akaona hayo, akaenda akamwambia Yoabu, akasema, Tazama, mimi nalimwona Absalomu ametundikwa katika mwaloni. Naye Yoabu akamwambia mtu yule aliyempasha habari, Je! Wewe umeona haya; Mbona, basi, hukumpiga hata nchi papo hapo? Nami ningalikupa fedha kumi na mshipi. Yule mtu akamwambia Yoabu, Kama ningalipata fedha elfu mkononi mwangu, hata hivyo singalinyosha mkono wangu juu ya mwana wa mfalme; kwa maana mfalme masikioni mwetu alikuagiza wewe, na Abishai na Itai, akisema, Angalieni sana mtu awaye yote asimguse yule kijana, Absalomu. Na tena, kama ningaliitendea roho yake kwa hila; (wala hapana neno lo lote liwezalo kufichwa mbele ya mfalme); ndipo wewe mwenyewe ungalijitenga. Ndipo Yoabu akasema, Siwezi kungoja na kusema nawe hivi. Akachukua vyemba vitatu mkononi mwake, akamchoma Absalomu moyoni, alipokuwa akali hai katikati ya ule mwaloni. Kisha vijana kumi, waliomchukulia Yoabu silaha zake wakamzunguka, wakampiga Absalomu, na kumwua.”

 

4.       Mtoto wa Daudi aitwaye Adonai – 1Wafalme 2:22-25 “Akajibu mfalme Sulemani akamwambia mamaye, Na mbona wamtakia Adonia Abishagi, Mshunami? Umtakie na ufalme pia; kwa kuwa yeye ni ndugu yangu mkubwa; naam, umtakie yeye, na Abiathari kuhani, na Yoabu mwana wa Seruya. Ndipo mfalme Sulemani akaapa kwa Bwana, akasema, Mungu anifanyie hivyo, na kuzidi, isipokuwa Adonia amenena neno hili juu ya uhai wake mwenyewe. Basi kwa hiyo, Bwana aishivyo, aliyenithibitisha na kunikalisha katika kiti cha enzi cha Daudi baba yangu, akanifanyia nyumba, kama alivyoahidi, hakika atauawa leo hivi Adonia. Mfalme Sulemani akatuma kwa mkono wa Benaya mwana wa Yehoyada: naye akampiga, hata akafa.”

 

Unaweza kuona ni kwanini tumechukua muda kufuatilia vifo vinne vya wana wa mfalme Daudi, ni ili kuthibitisha neno la Nabii Nathani kuwa Daudi kwa dhambi yake ya kuua mwana kondoo mmoja (URIA) alipaswa kulipa kondoo wanne, (WATOTO WAKE). Kwanini kwa sababu kulipa mara nne ilikuwa ni sehemu ya fidia ya agizo la kitorati kuwa kama umedhulumu kitu unapaswa kulipa mara nne kama malipizi 

 Kutoka 22:1 “Mtu akiiba ng'ombe au kondoo, na kumchinja, au kumwuza; atalipa ng'ombe watano badala ya ng'ombe mmoja, na kondoo wanne badala ya kondoo mmoja.”

Luka 19:8-10 “Zakayo akasimama, akamwambia Bwana, Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang'anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne. Yesu akamwambia, Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu. Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.”               

Kwanini nimechukua muda kuchambua kwa undani swala la Daudi na kulipa mara nne na vifo vya watoto wake kusudi langu kubwa ni kuonyesha tu picha ya kibiblia kuhusu kondoo, Kwamba kondoo husimama badala ya mtu na mtu husimama badala ya kondoo katika lugha ya kinabii, na ni katika picha hii ya kinabii tunapata wazi picha ya Mwana kondoo aliyetolewa kwa niaba ya Isaka wakati agizo la msingi la Mungu kwa Abraham lilikuwa ni kumtoa Isaka  mwanaye wa Pekee (AHADI) kama sadaka ya kuteteketezwa kwa Bwana:-

Mwanzo 22:1-14 “Ikawa baada ya mambo hayo Mungu alimjaribu Ibrahimu, akamwambia, Ee Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa. Akasema, Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia. Ibrahimu akaondoka alfajiri, akatandika punda wake, akachukua vijana wawili pamoja naye, na Isaka mwanawe, akachanja kuni kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa, akaondoka, akaenda mpaka mahali alipoambiwa na Mungu. Siku ya tatu Ibrahimu akainua macho yake, akapaona mahali pakali mbali. Ibrahimu akawaambia vijana wake, Kaeni ninyi hapa pamoja na punda, na mimi na kijana tutakwenda kule, tukaabudu, na kuwarudia tena. Basi Ibrahimu akazitwaa kuni za hiyo sadaka, akamtwika Isaka mwanawe; akatwaa moto na kisu mkononi mwake, wakaenda wote wawili pamoja. Isaka akasema na Ibrahimu baba yake, akinena, Babangu! Naye akasema, Mimi hapa, mwanangu. Akasema, Tazama! Moto upo, na kuni zipo, lakini yuko wapi mwana-kondoo kwa sadaka ya kuteketezwa? Ibrahimu akasema, Mungu atajipatia mwana-kondoo kwa hiyo sadaka, mwanangu. Basi wakaendelea wote wawili pamoja. Wakafika mahali pale alipoambiwa na Mungu, Ibrahimu akajenga madhabahu huko, akaziweka tayari kuni, kisha akamfunga Isaka mwanawe, akamweka juu ya madhabahu, juu ya zile kuni. Ibrahimu akanyosha mkono wake, akakitwaa kisu ili amchinje mwanawe. Ndipo malaika wa BWANA akamwita kutoka mbinguni, akasema, Ibrahimu! Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa. Akasema, Usimnyoshee kijana mkono wako, wala usimtendee neno; kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee. Ibrahimu akainua macho yake, akaangalia, na tazama, kondoo mume yuko nyuma yake, amenaswa pembe zake katika kichaka. Basi Ibrahimu akaenda akamtwaa huyo kondoo, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe. Ibrahimu akapaita mahali hapo Yehova-yire, kama watu wasemavyo hata leo, Katika mlima wa BWANA itapatikana.”

Unaweza kuona tukio hili ni tukio la kinabii, Ibrahimu na Mwanae Isaka ni manabii, Mungu anaposema na Ibrahimu kwenda kumtoa mwanae wa Pekee Isaka ni swala la kinabii, mwendo wao wa siku tatu, Isaka kubeba kuni mabegani mwake, kondoo mume amenaswa pembe zake katika kichaka zote hizi ni lugha za kinabii, ni picha ya kitu halisi ambacho Mungu alikuwa amekikusudia kwa ulimwengu, Ibrahim anamwakilisha Mungu,Isaka anamwakilisha Mwana wa pekee wa Mungu, kubeba kuni kunawakilisha Kubeba Msalaba, na mwendo wa siku tatu unamaanisha siku za mateso ya Yesu kufa na kufufuliwa kwake, Kondoo yule aliyenasa pembe zake ndiye aliyetolewa kwa niaba ya Isaka kondoo huyo pembe zake zilikuwa zimenasa katika kichaka ni picha inayomwakilisha Yesu Kristo aliyekufa msalabani huku akiwa amevikwa taji ya miiba kichwani mwake, kwa msingi huo tunaona wazi kuwa lugha ya kinabii hapa inaelezea, namna kondoo huyo alivyosimama kwa niaba ya Isaka, ni ni Picha ya kinabii kuhusu Mwanadamu mkamilifu atakayekufa kwa niaba ya wanadamu kama watamuamini Mungu na kuhesabiwa haki.

Lugha nyingine ya kinabii inaonekana katika torati ya Musa Kitabu cha Kutoka 12:3-7 “Semeni na mkutano wote wa Israeli, mkawaambie, Siku ya kumi ya mwezi huu kila mtu atatwaa mwana-kondoo, kwa hesabu ya nyumba ya baba zao, mwana-kondoo kwa watu wa nyumba moja; na ikiwa watu wa nyumba ni wachache kwa mwana-kondoo, basi yeye na jirani yake aliye karibu na nyumba yake na watwae mwana-kondoo mmoja, kwa kadiri ya hesabu ya watu; kwa kadiri ya ulaji wa kila mtu, ndivyo mtakavyofanya hesabu yenu kwa yule mwana-kondoo. Mwana-kondoo wenu atakuwa hana ila, mume wa mwaka mmoja; mtamtwaa katika kondoo au katika mbuzi. Nanyi mtamweka hata siku ya kumi na nne ya mwezi ule ule; na kusanyiko lote la mkutano wa Israeli watamchinja jioni. Nao watatwaa baadhi ya damu yake na kuitia katika miimo miwili na katika kizingiti cha juu, katika zile nyumba watakazomla.”

Hili ni tukio lingine ambalo linakolezea unabii wa Ibrahimu katika kitabu cha Mwanzo, Kwa maelekezo ya Mungu kwa Musa na Haruni, kwa wana wa Israel ili kwamba waweze kuokolewa na mauti ya kuuawa kwa kila mzaliwa wa Kwanza katika nchi ya Misri, Maelekezo ya Mungu ni kuwa lazima imwagike Damu, damu ya mwana kondoo asiye na hila yaani lazima awe mkamilifu, asiwe na marakaraka, na damu yale ikawekwa juu ya miimo ya milango, hii pia ilikuwa ni picha ya kinabii ya ukombozi wa Mwanadamu kupitia mtu ambaye hana dhambi ambaye ni Yesu Kristo, swala la unabii sio khadithi tu ni picha halisi ambazo Mungu alikuja kuzitimiza baadaye kupitia Masihi Mwana wake

Nabii Isaya naye katika namna ya kushangaza sana anamuona Masihi kama kondoo akipelekwa Msalabani, machinjoni kwa unyenyekevu mkubwa kwaajili ya ukombozi wa mwanadamu, ili wanadamu wasamehewe dhambi zao

Isaya 53:2-9 “Maana alikua mbele zake kama mche mwororo, Na kama mzizi katika nchi kavu; Yeye hana umbo wala uzuri; Na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani.Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu. Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona. Sisi sote kama kondoo tumepotea; Kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe; Na Bwana ameweka juu yake Maovu yetu sisi sote. Alionewa, lakini alinyenyekea, Wala hakufunua kinywa chake; Kama mwana-kondoo apelekwaye machinjoni, Na kama vile kondoo anyamazavyo Mbele yao wakatao manyoya yake; Naam, hakufunua kinywa chake. Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa; Na maisha yake ni nani atakayeisimulia? Maana amekatiliwa mbali na nchi ya walio hai; Alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wangu. Wakamfanyia kaburi pamoja na wabaya; Na pamoja na matajiri katika kufa kwake; Ingawa hakutenda jeuri, Wala hapakuwa na hila kinywani mwake.”

Kwa msingi huo tunaweza kuona wazi kuwa lugha zote za kinabii zinamzungumzia kondoo huyu, na kwa ujumla sikukuu zote za kuchinja na makafara yote zilikuwa ni picha za kinabii zinazomzungumzia Yesu kristo, Yeye ndiye mwana kondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu kama ilivyotabiriwa katika maandiko. Damu yake ina nguvu ya kuondoa na kufunika kabisa makosa yetu, Mungu anapoiangalia  au kuikumbuka Damu ya mwanae anaacha kutughathibikia na damu yake inatangaza rehema kwa niaba yetu na kutununua na kutulipia deni ili sisi nasi tuweze kuwa mali ya Mungu na kuufikia uwepo wa Mungu katika njia iliyo rahisi zaidi bila kuhitaji tena damu ya wanyama. Hilo linatuleta katika kutafakari kwa kina sasa kuhusu nguvu ya Damu ya Mwana kondoo.

Nguvu ya Damu ya mwanakondoo

Tunaweza kujiuliza ni kwanini Damu? Ya mwana kondoo? Wote tunakumbuka namna na jinsi Mwanadamu alivyopoteza nafasi ya kuwa na ushirika na Mungu, baada ya dhambi, Mungu alimueleza wazi mwanadamu kuwa siku atakapoivunja sharia yake yaani kula tunda alilokuwa amekatazwa kwa hakika atakufa!

Mwanzo 2:16-17 “BWANA Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema, Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula, walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.”               

Kwa hiyo kwa maana nyingine kila mwanadamu akiivunja sheria ya Mungu kwa kujua au kwa kutokujua anajingiza katika dhambi na anaileta mauti katika maisha yake, dhambi kwa kawaida malipo yake ni kifo tu na sio vinginevyo

Warumi 6:23a “Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti;…………….Unaona kwa msingi huo ili Mungu asiweze kuiona dhambi, ilikuwa ni lazima uhai mwingine utolewe kwa niaba ya muhisika ili Mungu asiikumbuke dhambi yake unaweza kuona na uhai huo unakaa katika Damu, Damu ndio kiwakilishi kiuu cha uhai wa Mwanadamu na wanyama,

 Waebrania 9:22 “Na katika Torati karibu vitu vyote husafishwa kwa damu, na pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo.”

Kwa hiyo Dhambi zinapofanyika zinadai kifo, zinadai mauti, zinadau uhai, kwa hiyo adhabu ya uhai wa kitu kingine kinapouawa kwa niaba yako Mungu huiona damu na kwa muda huo anaacha kughadibika kwa hiyo kwa rehema za Mungu na kwa upendo wake wanyama walikuwa wanakufa kwa niaba ya Mwanadamu, kwa hiyo unapofanya dhambi Mungu hukasirishwa na kwa kuwa Mungu ni mwenye wiu kwaajili yetu tamshi lake ni sheria siku utakapokula matunda ya mti huu hakika utakufa! Sasa kwa kuwa Mungu ni Mtakatifu hatuwezi kumkaribia hivihivi Mungu akaweka njia mbadala ambayo ni dhabihu ya damu ili hasira zake zisiwake kwetu na badala yake Damu ya mwanakondoo aliyeuawa kwa niaba yetu inamfanya Mungu aturehemu hivi ndio ulimwengu wa roho ulivyo na kanuni zake  Damu husimama kwa niaba ya uhai wetu na adhabu zetu Damu ni uhai  na damu ina uhai

Walawi 17:10-12 “Kisha mtu awaye yote wa nyumba ya Israeli, au miongoni mwa hao wageni wakaao kati yao, atakayekula damu, ya aina yo yote, nitakunja uso wangu juu ya mtu huyo alaye damu, nami nitamkatilia mbali na watu wake. Kwa kuwa uhai wa mwili u katika hiyo damu; nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu; kwani ni hiyo damu ifanyayo upatanisho kwa sababu ya nafsi. Kwa hiyo naliwaambia wana wa Israeli, Hapana mtu miongoni mwenu aliye na ruhusa kula damu, wala mgeni aketiye kati yenu asile damu.”               

-          Kumwagika kwa damu ni ufuno halisi kuwa dhambi ni swala nyeti na linagharimu sana mfumo wa maisha yetu.

-          Kumwagika kwa damu ni ufunuo wa Moyo wa Mungu kwetu kuwa Mungu anahitaji kurejesha uhusiano wake na mwanadamu na hataki watu wafie dhambini.

-          Kumwagika kwa damu ulikuwa ni ufunuo unaoonyesha ya kuwa tunahitaji mbadala wa kitu kingine kuchukua mizigo kwa niaba yetu.

-          Kumwagika kwa damu ni alama ya kitu kinachoweza kufanya upatanisho kati yetu na Mungu

-          Kumwagika kwa damu ni ufunuo wa uzito wa haki ya Mungu kupatikana kwa neema

-          Kumwagka kwa Damu ni ufunuo wa namna mwanadamu anavyoweza kurejesha uhusiano wake na Mungu

Kwa njia hii Mungu alikuwa akijifunua kwa wana wa Israel namna anavyoweza kuwa na ushirika nao, lakini Mungu sio wa Israel pekee ni Mungu wa Ulimwengu mzima na mataifa yote Je sadaka hizi za mafahari ya kondoo na mbuzi zingeendelea hata lini? hizi zote zingegharimu mamilioni ya wanyama duniani leo, hizi zilikuwa ni picha ni alama ya kinabii kuonyesha nguvu ya Damu, inavyoweza kurudisha uhusiano wetu na Mungu, inavyoweza kupatanisha inavyoweza kurudisha ushirika na Mungu, inavyoweza kusababaisha kutangaziwa rehema na kusamehewa dhambi, damu za mafahari zilifanya kwa muda tu Lakini Damu ya Yesu ingetolewa mara moja kwa kazi za milele.

Tazama mwanakondoo wa Mungu

Yohana 1:26-30 “Yohana akawajibu akisema, Mimi nabatiza kwa maji. Katikati yenu amesimama yeye msiyemjua ninyi. Ndiye yule ajaye nyuma yangu, ambaye mimi sistahili kuilegeza gidamu ya kiatu chake. Hayo yalifanyika huko Bethania ng'ambo ya Yordani, alikokuwako Yohana akibatiza. Siku ya pili yake amwona Yesu anakuja kwake, akasema, Tazama, MWANA-KONDOO WA MUNGU, aichukuaye dhambi ya ulimwengu! Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Yuaja mtu nyuma yangu, ambaye amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu.”

Kimsingi manabii walikuwa wakitabiri kuja kwa Mwana kondoo halisi wa Mungu, Lakini nabii Yohana Mbatizaji yeye alikuwa akiwaonyesha wazi jamii ya watu kwamba yule aliyekuwa akitazamiwa, kusubiriwa na kuhubiriwa na manabii ndiye huyu, na sasa watu wote wanapaswa kumwamini, kuamini kazi yake atakayoifanya pale msalabani kwamba, itafanya kazi zaidi ya zile zilikuwa zikifanywa na wanyama jana leo na hata milele, mwana kondoo huyo ni Yesu Kristo ambaye kama alivyotabiriwa ndivyo ilivyokuwa

Isaya 53:7-10 “Alionewa, lakini alinyenyekea, Wala hakufunua kinywa chake; Kama mwana-kondoo apelekwaye machinjoni, Na kama vile kondoo anyamazavyo Mbele yao wakatao manyoya yake; Naam, hakufunua kinywa chake. Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa; Na maisha yake ni nani atakayeisimulia? Maana amekatiliwa mbali na nchi ya walio hai; Alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wangu. Wakamfanyia kaburi pamoja na wabaya; Na pamoja na matajiri katika kufa kwake; Ingawa hakutenda jeuri, Wala hapakuwa na hila kinywani mwake. Lakini Bwana aliridhika kumchubua; Amemhuzunisha; Utakapofanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi, Ataona uzao wake, ataishi siku nyingi, Na mapenzi ya Bwana yatafanikiwa mkononi mwake;”

Hakuna kiongozi mwingine yeyote wala muazilishi wa dini nyingine yeyote aliyeweza kuhitimisha unabii wake katika hali kama hii, Isipokuwa Yesu Kristo, dini na taratibu nyingine zozote duniani ambazo hazina kiongozi aliyetimiza unabii hivi ni dini za uongo, kama unaweka Imani yako kwa nabii marehemu ambaye hajawahi kumwaga damu yake wala kutoa uhai wake kwaajili ya wanadamu basi fahamu kuwa huyo siye aliyetabiriwa katika maandiko, Na deni lako la dhambi linabakia vile vile, Ni Yesu pake yake anayeruhusiwa kuwa na mamlaka na kupokea Enzi na utukufu kutokana na kazi hii ya ukombozi aliyoifanya na upendo mkuu wa Mungu alioufunua kwetu

Ufunuo 5: 11-12 “Nikaona nikasikia sauti ya malaika wengi pande zote za kile kiti cha enzi, na za wale wenye uhai, na za wale wazee, na hesabu yao ilikuwa elfu kumi mara elfu kumi na elfu mara elfu, wakisema kwa sauti kuu, ASTAHILI MWANA-KONDOO ALIYECHINJWA, kuupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu na heshima na utukufu na baraka.”                

1Yohana 4:9-10 “Katika hili pendo la Mungu lilionekana kwetu, kwamba Mungu amemtuma Mwanawe pekee ulimwenguni, ili tupate uzima kwa yeye Hili ndilo pendo, si kwamba sisi tulimpenda Mungu, bali kwamba yeye alitupenda sisi, akamtuma Mwanawe kuwa kipatanisho kwa dhambi zetu. .”

Yohana 15:13 “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.”

1Petro 1:18-21 “Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; BALI KWA DAMU YA THAMANI, KAMA YA MWANA-KONDOO ASIYE NA ILA, ASIYE NA WAA, YAANI, YA KRISTO.NAYE amejulikana kweli tangu zamani, kabla haijawekwa misingi ya dunia; lakini alifunuliwa mwisho wa zamani kwa ajili yenu; ambao kwa yeye mmekuwa wenye kumwamini Mungu, aliyemfufua katika wafu akampa utukufu; hata imani yenu na tumaini lenu liwe kwa Mungu.”

Mungu aliona aikamilishe kazi ile ya kinabii kupitia Mwanaye, yaani kama Ibrahimu alithubutu Kumuachia mwanaye Isaka kwaajili ya Mungu, Mungu sasa katika hali halisi hakumzuia mwanaye Yesu Kristo kwaajili yetu, upendo huu ni mkubwa sana kwani unahuisha ushirika wetu na Mungu, unatupa kibali cha kuwa na ushirika na Mungu na hivyo inafungua njia ya ajabu kwetu ya kuwa hakuna lolote ambalo Mungu anaweza kutunyima 

Warumi 8: 32 “Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye?              

Maana yake ni nini? Kila changamoto tunayoweza kukutana nayo duniani iwe ndogo au kubwa, iwe dhambi au mauti, iwe hatari, iwe ya kimwili, au ya kiroho, iwe ya kiuchumia au ya kisaikolojia kamwe haitaweza kuushinda upendo wake yeye kwani anasamehe dhambi kisha anashughulika na magonjwa yetu na mateso yetu na fadhaa zetu yeye amemleta Mungu karibu na sisi, amerejesha uhusiano wetu na baba hivyo ili tuwe na uhai ili tuwe na uzima ili tufanikiwe hatuna budi kuhakikisha kuwa tunamtazama yeye katika maisha yetu yote na ndio maana Yohana mbatizaji aliwanyooshea kidole kwamba yeye hana majibu ya kutosha amekuja anayestahili na hakuna njia nyingine akawaambia watu TAZAMA MWANA KONDOO WA MUNGU, Leo nakutangazia ya kuwa chanzo cha mafanikio yako, sio sabuni, sio chumvi, sio maji ya Baraka wala mafuta ya upako, wala udongo, wala nyayo zako, wala kula keki mimi wala kukombolewa kwa adhri yako, wala kupeleka kucha zako, wala nyele zako, Leo Roho Mtakatifu amenituma kwako nikiwa na ujumbe kama wa Yohana Mbatizaji TAZAMA MWANA KONDOO WA MUNGU, Nasema hivi kwa changamoto zozote, kwa vita ya aina yoyote, kwa majungu ya aina yoyote, kwa  fuitina za aina yoyote, kwa dhuluma ya aina yoyote, kwa mapito ya aina yoyote, kwa njaa, kwa aibu, kwa kupungukiwa kwa lolote lile leo nakuelekeza neno moja nimepewa kwaajili yako TAZAMA MWANA KONDOO WA MUNGU, kwa changamoto zozote zile, kwa laana zozote zile, kwa usumbufu wa mizimu, kwa usumbufu wa wachawi, kwa matatizo ya nuksi laana mikosi na balaa, kwa changamoto za kurogwa, damu ya Yesu ni zaidi ya ndele, ni zaidi ya zindiko lolote lile liwe kwamsisi, au kwasemangube au milima ya rwengera au Nchedebwa, au Liwale, na kadhalika Damu yake inamaliza yote, yeye ndio suluhisho la changamoto zetu zote na jina lake linatosha sana ni jina kuu kuliko yote, lina nguvu na mamlaka yote hivyo kwa suluhu zozote za changamoto zako nasema TAZAMA MWANA KONDOO WA MUNGU basiiii.  Rbashakarabasiote rikabashakarabasabo, yekerekishitaraka sata Yete tara sata! TAZAMA MWANA KONDOO WA MUNGU. Naema TAZAMA MWANA KONDOO WA MUNGU nasema TAZAMA MWANA KONDOO WA MUNGU Haleluyaaaaa Ukimtazama yeye unapomtazama yeye hakuna kuchoka wala kukata tamaa wala kuzimia moyo


Waebrania 12:2-3 “tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu. Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu.”


Rev. Innocent Samuel Jumaa Kamote


Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima

Hakuna maoni: