Jumapili, 21 Januari 2024

Unatenda mambo hayo kwa mamlaka gani ?


Luka 20:1-8 “Ikawa siku moja, alipokuwa akiwafundisha watu hekaluni, na kuihubiri habari njema, wakuu wa makuhani na waandishi pamoja na wazee walimtokea ghafula; wakamwambia, wakisema, Tuambie, unatenda mambo hayo kwa mamlaka gani? Tena, ni nani aliyekupa mamlaka hii? Akajibu akawaambia, Nami nitawauliza ninyi neno moja; niambieni, Ubatizo wa Yohana, je! Ulitoka mbinguni au kwa wanadamu? Wakahojiana wao kwa wao, wakisema, Kama tukisema ulitoka mbinguni, atasema, Basi, mbona hamkumwamini? Na tukisema ulitoka kwa wanadamu, watu wote watatupiga kwa mawe, kwa kuwa wamemkubali Yohana kuwa ni nabii.  Wakajibu, kwamba, Hatujui ulikotoka. Yesu akawaambia, Wala mimi siwaambii ninyi ni kwa mamlaka gani ninatenda mambo haya.”




Utangulizi:

Yesu alikuwa akiifanya kazi kubwa ya kuhubiri, kufundisha neno na kufanya kazi mbalimbali ikiwemo uponyaji, pamoja na makemeo na makaripio ya aina mbali mbali pale ilipobidi, siku moja akiwa anafundisha, na kuihubiri habari njema, wakuu wa makuhani, waandishi na wazee walimtokea na kuhoji mamlaka yake, kwamba anafanya kazi hii kwa mamlaka gani? Na ni nani aliyempa mamlaka hii? Kwa ujumla kundi hili la watu walikuwa ni wajumbe wanaowakilisha baraza la utawala na mahakama ya juu ya maamuzi ya kiyahudi linalojulikana kitaalamu kama “SANHEDRIN” swali lao kwa Yesu lilikuja hasa baada ya tukio la Yesu kutengeneza kikoto cha mkambaa na kupindua meza za watu waliokuwa wakifanya biashara Hekaluni, huku akikemea na kuonyesha namna Hekalu linavyopaswa kuheshimiwa na sio swala la kufanyiwa biashara!

Luka 19:45-48 “Akaingia hekaluni, akaanza kuwatoa wale waliokuwa wakifanya biashara, akiwaambia, Imeandikwa, Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala; lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi. Naye akawa akifundisha kila siku hekaluni. Lakini wakuu wa makuhani, na waandishi, na wakuu wa watu walikuwa wakitafuta njia ya kumwangamiza; wasione la kutenda, kwa kuwa watu wote walikuwa wakiandamana naye, wakimsikiliza.”

Jamii kubwa ya watu waliokuwa wakihusika na biashara hizi walikuwa ni jamii ya wazee, waandishi na makuhani, hawa ndio waliokuwa washika dau la kisiasa, na ndio mara nyingi sana walikuwa wakikutana na makemeo ya Yesu kwa uwazi na ndilo kundi la watu waliokuwa wakimtafuta ili waweze kumwangamiza, kimsingi hawakuwa wasikivu kwa injili wala mafundisho ya Yesu lakini walikuwa wakimtaka Yesu na kutafuta namna wanavyoweza kumkwamisha ili wamuue au kumshitaki, kwa sababu Yesu alikuwa maarufu kuliko wao na jamii kubwa ya watu walikuwa wakiandamana naye na kumsikiliza! Baraza hili la “SANHEDRIN” kimsingi ndilo lilokuwa na haki au lililojipa haki ya kuidhinisha jambo lolote lile ikiwa ni pamoja na kutoa kibali kwa marabi, majaji na waalimu kufundisha au hata kibali cha kushughulika na watu wanaominiwa kuwa wako kinyume na mafundisho sahihi ya kiyahudi!

Matendo 9:1-2 “Lakini Sauli, akizidi kutisha na kuwaza kuwaua wanafunzi wa Bwana, akamwendea Kuhani Mkuu, akataka ampe barua za kuenda Dameski zilizoandikwa kwa masinagogi, ili akiona watu wa Njia hii, waume kwa wake, awafunge na kuwaleta Yerusalemu.”

Ni katika Mtazamo kama huu ndipo walipojivika ujasiri wa kumkabili Yesu na kumuhoji kuwa anayafanya haya kwa mamlaka gani?  Leo nataka tuchukue Muda kujifunza mambo ya msingi muhimu katika somo hili UNATENDA MAMBO HAYA KWA MAMLAKA GANI kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

1.       Ufahamu kuhusu Baraza la wazee wa kiyahudi (Sanhedrin)

2.       Unatenda mambo haya kwa mamlaka Gani?

3.       Ufahamu kuhusu Mamlaka ya Yesu Kristo!

Ufahamu kuhusu Baraza la wazee wa kiyahudi (Sanhedrin)

Baraza la wazee wa kiyahudi liliundwa na kusanyiko la wazee au wataalamu wa sheria wa aina mbalimbali wapatao 71, ambapo Kuhani mkuu ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa baraza hilo, akisaidiwa na wazee sabini, Baraza hili lilikuwa na mamlaka ya kimahakama katika jamii ya kiyahudi, na hivyo ilikuwa ni kama mahakama ya juu zaidi ya kiyahudi, iliyokubaliwa na serikali ya kikoloni ya Warumi kwaajili ya kushughulika na maswala ya Kidini, kiraia, kisiasa, kijamii na kudhibiti uhalifu unaoweza kufanywa na watu wa jamii ya kiyahudi, pia walikuwa na mamlaka ya kutoa kibali kwa marabi waliokubalika na baraza kuwa na wanafunzi na kufundisha, walikuwa pia na kibali cha kuruhusu au kumtangaza mtu kuwa hakimu, yaani mwamuzi, Rabi na Mzee, kwa hiyo katika wakati wa Yesu rabi ndio walikuwa na kofia zote tatu na hivyo waliweza kufanya kazi zote, za kufundisha, kutoa hukumu na maagizo ya kiutawala, hawa walipatikana kwa idhini ya baraza hilo,  kwa hiyo hata walimu wa kidini walipaswa kuwa na kibali cha Baraza hilo la wazee,  kwa hiyo swali lao la hadharani kwa Yesu Kristo lilikuwa lina makusudi ya wazi ya kumdhalilisha Yesu Kristo, wakiwa na maana ya kwamba anayoyafanya anayafanya kwa idhini ya nani na kwa sababu hiyo watu wangesikia na kujua kuwa Yesu ni Mwalimu (Rabbi) ambaye hajaidhinishwa na mahakama hiyo!

Neno hilo SANHEDRIN Ni neno la kiyunani SUNEDRION au SANHEDRIM neno hili limetokana na muunganiko wa maneno mawili SUN na HEDRA ikiwa na maana ya TOGETHER na SEAT yaani Kukusanyika pamoja, Kwa hiyo ni baraza la wazee wenye hekima walioalikwa chini ya kuhani mkuu kumsaidia kufanya kazi za kitawala katika jamii hiyo

Kwaasili kundi hili kwa mujibu wa maandiko ya kiyahudi yaitwayo MISHNA liliundwa kama matokeo ya wazee waliokuwa pamoja na nabii Musa nyakati za agano la kale, ambao Mungu aliwaita kwa kusudi la kumsaidia Musa katika maamuzi mbalimbali na usaidizi wa kulibeba taifa la Israel wazee hao walikuwa muhimu sana angalia:- 

Hesabu 11:16-17 “Kisha Bwana akamwambia Musa, Nikusanyie watu sabini, miongoni mwa wazee wa israeli, ambao wewe wawajua kuwa ndio wazee wa watu hawa, na maakida juu yao; ukawalete hata hema ya kukutania, wasimame huko pamoja nawe. Nami nitashuka niseme nawe huko, nami nitatwaa sehemu ya roho iliyo juu yako na kuiweka juu yao; nao watachukua mzigo wa watu hawa pamoja nawe, ili usiuchukue wewe peke yako.”

Wazee hao waliwekwa kwa maelekezo ya Mungu kwa nabii Musa kwaajili ya maswala ya kiserikali katika Israel japo kwa Muda na hakuna agizo la kuendeleza mfumo huo lililotolewa na Mungu, Kwa hiyo hakuna historia ya kutosha kuhusu uanzishwaji huu wa SANHEDRIN lakini inajulikana tu kuwa walipata Baraka za warumi kushughulika na maswala  wayahudi isipokuwa idhini ya kuua Muhaini wa kisisasa ilishughulikiwa na mahakama ya Kirumi, tunaliona katika maandiko wakiwa katika utendaji tangu wakati wa Yesu hata wakati wa Nyakati za kanisa la Kwanza.

Mathayo 26:57-59 “Nao waliomkamata Yesu wakampeleka kwa Kayafa, Kuhani Mkuu, walikokuwa wamekutanika waandishi na wazee. Na Petro akamfuata kwa mbali mpaka behewa ya Kuhani Mkuu, akaingia ndani, akaketi pamoja na watumishi, auone mwisho. Basi wakuu wa makuhani na baraza yote wakatafuta ushuhuda wa uongo juu ya Yesu, wapate kumwua;”

Marko 15:1 “Mara kulipokuwa asubuhi wakuu wa makuhani walifanya shauri pamoja na wazee na waandishi na baraza nzima, wakamfunga Yesu, wakamchukua, wakamleta mbele ya Pilato.”

Matendo 5:21 “Nao waliposikia wakaenda alfajiri hekaluni, wakaanza kufundisha. Akaja Kuhani Mkuu nao waliokuwa pamoja naye, wakawakutanisha watu wa baraza, na wazee wote wa wana wa Israeli, wakatuma watu gerezani ili wawalete.”

Ni baraza hili ndilo lililohusika kumshitaki Yesu na kutoa ushawishi wa kuuawa kwake na ni baraza hili pia lililohusika kwa kiasi kikubwa katika upinzani dhidi ya Kanisa nyakati za karne ya kwanza, na ni wengi jamii hii iliyokuwa wanamiliki biashara zilizokuwa zikiendeshwa pale Hekaluni na ambazo Bwana Yesu alizikemea na kupindua meza.   

Unatenda mambo haya kwa mamlaka Gani?

Kama nilivyogusia awali kwamba swali hili lilikuwa na makusudi ya kumdhalilisha Yesu Kristo, Baraza la wazee SANHEDRIN ndio waliokuwa na mamlaka ya kuruhusu watu wafundishe neno baada ya wao kuidhinisha jambo hili liliwapa upofu na uziwi na kiburi kwa kujidhani kuwa wao ndio mamlaka ya mwisho na kuwa rabi anayekubalika na wao na aliyepita katika viwango vyao ndiye sahihi na anayepaswa kusikilizwa na watu!

Lilikuwa ni swali la kumuhukumu Yesu Kristo Tena, ni nani aliyekupa mamlaka hii? Swali hili halikuulizwa ili kupata taarifa bali liliulizwa kuwa hii mamlaka ya kufundisha wewe umeitoa wapi kusudi kubwa lilikuwa ni kumvunjia Yesu heshima ili watu wajue kuwa anafanya kazi hiyo bila kibali chao, aidha Kama Yesu angejibu kuwa anafanya hayo Kama Mwana wa Mungu kwa kuwa Yeye ni masihi basi wangepata nafasi ya kumuhukumu kwani angekuwa kama amekufuru na kimsingi Yesu hakutaka hata pepo wamdhihirishe yeye kuwa ni nani! Hakutaka kujifunua kama Masihi

Baraza hili hili pia lilimfanyia hujuma hiyo hiyo hivyo hivyo Yohana Mbatizaji, kwani ni baraza hili ndilo lililotuma wajumbe kwenda kumuuliza swali YOHANA MBATIZAJI kuwa yeye ni Kristo au ni nani? Lakini hawakuhusika katika kumuamini hii ni kwa sababu hakuonekana kupitia pia katika mikono yao na pia walimpuuzia hawakumuamini!

Yohana 1:19-22 “Na huu ndio ushuhuda wake Yohana, Wayahudi walipotuma kwake makuhani na Walawi kutoka Yerusalemu ili wamwulize, Wewe u nani? Naye alikiri, wala hakukana; alikiri kwamba, Mimi siye Kristo. Wakamwuliza, Ni nini basi? U Eliya wewe? Akasema, Mimi siye. Wewe u nabii yule? Akajibu, La. Basi wakamwambia, U nani? Tuwape majibu wale waliotupeleka. Wanenaje juu ya nafsi yako?

Ni watu wa kawaida ndio ambao walimuamini Yohana Mbatizaji na kutambua kuwa ni nabii, na ndio maana Yesu aliwauliza swali kwa swali lao, kuwa Ubatizo wa Yohana mbatizaji ulitoka wapi na waliogopa kujibu kwa sababu hawakuamuamini, na watu walimuamini, kukaa kimya kwao na kutokujibu swali la Yesu kuwa hawajui mamlaka ya Yohana mbatizaji ilitoka wapi, ilikuwa ni kuonyesha ujinga wao kuwa kama hawajui mamlaka ya Yohana mbatizaji imetoka wapi ni wazi kuwa Hawawezi kujua mamlaka ya Yesu Kristo ambayo ni pana zaidi  na ni wazi kuwa baraza hilo hawana mamlaka ya kumzuia au kumpangia nabii cha kufanya. Nabii ni msemaji kwa niaba ya Mungu, ni mdomo wa Mungu, kama mtu hajui mamlaka ya nabii inatokea wapi ni vigumu kujua mamlaka ya Mwana wa Mungu.

Hakuna mwanadamu mwenye mamlaka ya kuhoji mamlaka ya Yesu, wala kwa muhubiri wa injili, kundi la makuhani na wazee wa Sanhedrin walikuwa na ujinga katika vichwa vyao na ufahamu wao hawakuwa hata wamefunuliwa maandiko kuijua mamlaka ya Kristo ambayo ilitabiriwa pia katika maandiko Nabii Isaya anaeleza kuhusu mtoto mwanaume mwenye uweza wa kifalme mabegani mwake yaani mwenye nguvu za kiserikali huyu Ndiye Yesu ona

Isaya 9:6-9 “Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani. Maongeo ya enzi yake na amani Hayatakuwa na mwisho kamwe, Katika kiti cha enzi cha Daudi na ufalme wake; Kuuthibitisha na kuutegemeza Kwa hukumu na kwa haki, Tangu sasa na hata milele. Wivu wa Bwana wa majeshi ndio utakaotenda hayo.”

Yakobo alitabiri kuwa huyu ana fimbo ya Enzi yaani mamlaka na utawala na mataifa watamtii Mwanzo 49:10 “Fimbo ya enzi haitaondoka katika Yuda, Wala mfanya sheria kati ya miguu yake, Hata atakapokuja Yeye, mwenye milki, Ambaye mataifa watamtii.”

Kama Sanhedrin wangelijua maandiko yanasema nini kumuhusu Kristo, ukweli ni kuwa wasingelithubutu hata kidogo kuhoji ni kwa mamlaka gani anayatenda hayo anayoyatenda wao walikuwa  wakitafakari ubatili na kumfanyia ghasia wakiwa wamesahau kuwa yeye ndiye mfalme wa wafalme na bwana wa mabwana na kuwa wafalme wote wa dunia wanapaswa kwenda kwa kicho mbele zake

Zaburi 2:1-12 “Mbona mataifa wanafanya ghasia, Na makabila wanatafakari ubatili? Wafalme wa dunia wanajipanga, Na wakuu wanafanya shauri pamoja, Juu ya Bwana, Na juu ya masihi wake.Na tuvipasue vifungo vyao, Na kuzitupia mbali nasi kamba zao. Yeye aketiye mbinguni anacheka, Bwana anawafanyia dhihaka. Ndipo atakaposema nao kwa hasira yake, Na kuwafadhaisha kwa ghadhabu yake. Nami nimemweka mfalme wangu Juu ya Sayuni, mlima wangu mtakatifu. Nitaihubiri amri; Bwana aliniambia, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa. Uniombe, nami nitakupa mataifa kuwa urithi wako, Na miisho ya dunia kuwa milki yako.Utawaponda kwa fimbo ya chuma, Na kuwavunja kama chombo cha mfinyanzi. Na sasa, enyi wafalme, fanyeni akili, Enyi waamuzi wa dunia, mwadibiwe. Mtumikieni Bwana kwa kicho, Shangilieni kwa kutetemeka. Shikeni yaliyo bora asije akafanya hasira, Nanyi mkapotea njiani,Kwa kuwa hasira yake itawaka upesi,Heri wote wanaomkimbilia.”

Ni Dhahiri kama wangetambua mamlaka iliyoelezewa kuhusu masihi na aliyokuwa nayo Yohana mbatizaji na kama wangemuamini na kumsikiliza ilikuwa ni rahisi kwao kuwa wanyenyekevu na kuwa na hofu na Yesu Kristo kwa sababu hakuwa wa kawaida hata kidogo

Mathayo 3:11-12 “Kweli mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba; bali yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, wala sistahili hata kuvichukua viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto. Ambaye pepeto lake li mkononi mwake, naye atausafisha sana uwanda wake; na kuikusanya ngano yake ghalani, bali makapi atayateketeza kwa moto usiozimika.”

Yohana alikuwa amekwisha kueleza wazi kuwa yeye hastahili hata kuwa mtumwa wa Yesu Kristo wala hata kulegeza gidamu ya viatu vyake, mwenyewe alisema ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, na zaidi ya yote ndiye atakayehukumu wanadamu na kuwatupa motoni wale wasiomuamini, Yalikuwa ni maneno ya kutisha sana ambayo Yohana alizungumza kuhusu Yesu, kuhoji kuwa Yesu anafanya hayo kwa mamlaka gani ni upofu na uwendawazimu wa hali ya juu sana, Kama wangemuamini na kumsikiliza Yohana alivyokuwa akizungumza kuhusu Yesu basi walipaswa kujificha  na kukoma kabisa kuhoji jambo lolote alilokuwa akilifanya bwana Yesu wala wasingelithubutu hata kumsogelea. Yohana anasemaje tena kuhusu Yesu? Angalia andiko hili:-

Yohana 3:26-31 “Wakamwendea Yohana, wakamwambia, Rabi, yeye aliyekuwa pamoja nawe ng'ambo ya Yordani, yeye uliyemshuhudia, tazama, huyo anabatiza na watu wote wanamwendea. Yohana akajibu, akasema, Hawezi mtu kupokea neno lo lote isipokuwa amepewa kutoka mbinguni. Ninyi wenyewe mwanishuhudia ya kwamba nalisema, Mimi siye Kristo, bali nimetumwa mbele yake. Aliye naye bibi arusi ndiye bwana arusi; lakini rafiki yake bwana arusi, yeye anayesimama na kumsikia, aifurahia sana sauti yake bwana arusi. Basi hii furaha yangu imetimia. Yeye hana budi kuzidi, bali mimi kupungua. Yeye ajaye kutoka juu, huyo yu juu ya yote. Yeye aliye wa dunia, asili yake ni ya dunia, naye anena mambo ya duniani. Yeye ajaye kutoka mbinguni yu juu ya yote.”

Ni wazi kuwa Yesu ni kama alikuwa anawaambia kwamba mngemuelewa vizuri Yohana mbatizaji, isingekuwa ngumu kumuelewa yeye, lakini tatizo la baraza walimkataa Yohana mbatizaji na ndio maana ilikuwa ngumu kwao kumuelewa Yesu, Yohana anasema AJAYE KUTOKA JUU HUYO YU JUU YA YOTE  Yohana aliwaeleza kuwa yeye sio Kristo lakini ametumwa mbele yake ni wazi kuwa watu wenye akili nyingi wangeweza kumpa kipaumbele nabii aliyefuata baada ya Yohana kwa vile huyo ndiye masihi na ambaye Yohana alikuwa ametumwa mbele yake, huyu ana mamlaka kubwa ana mamlaka nzito sana yuko juu ya yote, na manabii walinena habari zake unawezaje kuhoji mamlaka yake?     Yohana anasema sistahili hata kulegeza gidamu (Kamba) za viatu vyake!                                            

Ufahamu kuhusu Mamlaka ya Yesu Kristo!

Neno mamlaka katika maandiko ni moja ya neno maarufu sana na wakati mwingine linatafasiriwa kama Nguvu na Uweza, Neno Mamlaka, kwa Kiebrania ni Mamlakah na katika kiyunani ni EXOUSIA neno hili limetumika zaidi ya mara 102 katika agano jipya pekee, Mamlaka ni itifaki ya Kiungu,  na linapotumika humaanisha UFALME, NGUVU, UTAWALA,  na AMRI au mamlaka  kwa kiingereza KINGDOM, DOMINION, REIGN AND SOVEREIGNTY or AUTHORITY RIGHT, PRIVILEGE and ABILITY Hii ni Tabia ya uungu, Yesu Kristo Ana mamlaka pana sana na hatuwezi kuizungumzia katika somo moja kama hivi, unapozungumzia habari za Yesu unazungumzia serikali ya kiungu, haitaji kibali cha mwanadamu kufanya jambo, anaweza kumshirikisha mwanadamu au kumjulisha kwa upendo wake lakini huwezi kuingilia mamlaka yake huwezi kuhoji utawala wake, huwezi kuzuia matakwa yake anauwezo wa kufanya lolote! Na zaidi ya yote maandiko yanaonyesha kuwa Yesu amewekwa juu ya hayo yote ona

Wakolosai 1:15-20 “naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake. Naye amekuwako kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hushikana katika yeye. Naye ndiye kichwa cha mwili, yaani, cha kanisa; naye ni mwanzo, ni mzaliwa wa kwanza katika wafu, ili kwamba awe mtangulizi katika yote. Kwa kuwa katika yeye ilipendeza utimilifu wote ukae; na kwa yeye kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake akiisha kufanya amani kwa damu ya msalaba wake; kwa yeye, ikiwa ni vitu vilivyo juu ya nchi, au vilivyo mbinguni.”   

Unaona ikiwa Yesu na Mamlaka hii inayoelezewa katika maandiko basi hakuna jambo la kipuuzi na la kijinga na kukosa nidhamu duniani kama kupuuzia mamlaka aliyo nayo Kristo, kwa hiyo nadhani baraza hili ambalo lilikuwa linasheheni watu wenye akili na taaluma mbalimbali na uwezo wa kuhukumu mambo inasikitisha kuona kuwa wanakosa akili na hekima ya kutambua mamlaka ya Yesu Kristo na ulikuwa ni mshahara mzuri sana kwa Yesu kutokuwafafanunulia anafanya yale kwa mamlaka gani na badala yake aliwarudisha darasa la kwenda kwanza kujifunza ilikotoka mamlaka ya Yohana mbatizaji

Ni mpaka macho yako yatiwe Nuru tena kwa maombi ndipo uweze kujua mamlaka inayotenda kazi katika Kristo ni mamlaka ya juu sana

Waefeso 1;18-23 “macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo; na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo; kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wake; aliotenda katika Kristo alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho; juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia; akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote.”

Hebu niambie kuna mamlaka gani ambayo inaweza kuzidi mamlaka ya Yesu Kristo? Na ndio maana hata tunapotumia jina lake kuamuru lolote linatokea kwa idhini yake yaani kwa mamlaka yake, Jina lake maana yake ni mamlaka yake, licha ya kuwa na mamlaka yote Yesu amejidhihirisha kuwa na mamlaka katika maeneo kadhaa kama yanavyonena maandiko:-

Yesu Kristo ana mamlaka Yote Mbinguni na Duniani hii ni mamlaka kubwa sana ni mamlaka ya kiungu - Mathayo 28:18-20 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.”

Yesu Kristo ana mamlaka juu ya watu wote - Yohana 17:2-3 “kama vile ulivyompa mamlaka juu ya wote wenye mwili, ili kwamba wote uliompa awape uzima wa milele.  Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma.”

Yesu Kristo ana mamlaka ya kusamehe dhambi - Mathayo 9:2-6 “Na tazama, wakamletea mtu mwenye kupooza, amelala kitandani; naye Yesu, alipoiona imani yao, alimwambia yule mwenye kupooza, Jipe moyo mkuu, mwanangu, umesamehewa dhambi zako. Na tazama, baadhi ya waandishi wakasema nafsini mwao, Huyu anakufuru. Naye Yesu, hali akijua mawazo yao, akasema, Mbona mnawaza maovu mioyoni mwenu? Kwa maana rahisi ni lipi, ni kusema, Umesamehewa dhambi zako, au ni kusema, Ondoka, uende? Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (amwambia yule mwenye kupooza) Ondoka, ujitwike kitanda chako, uende nyumbani kwako.”

Yesu Kristo ana mamlaka juu ya Pepo - Marko 1:23-27 “Na mara palikuwapo ndani ya sinagogi lao mtu mwenye pepo mchafu; akapaza sauti, akisema, Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je! Umekuja kutuangamiza? Nakutambua u nani, Mtakatifu wa Mungu. Yesu akamkemea, akisema, Fumba kinywa, umtoke. Yule pepo mchafu akamtia kifafa, akalia kwa sauti kuu, akamtoka. Wakashangaa wote, hata wakaulizana, wakisema, Nini hii? Ni elimu mpya! Maana kwa uweza awaamuru hata pepo wachafu, nao wamtii! ”   

Yesu Kristo ana mamlaka dhidi ya Kifo - Ufunuo 1:17-18 “Nami nilipomwona, nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho, na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu.”    

Yesu Kristo ana mamlaka dhidi ya Magonjwa yote - Mathayo 8:2-3 “Na tazama, akaja mtu mwenye ukoma akamsujudia, akisema, Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa. Yesu akanyosha mkono, akamgusa, akisema Nataka; takasika. Na mara ukoma wake ukatakasika.”        

Yesu ana mamlaka juu ya malaika - Mathayo 13:41-43 “Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watakusanya kutoka katika ufalme wake machukizo yote, na hao watendao maasi, na kuwatupa katika tanuru ya moto, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Ndipo wenye haki watakapong'aa kama jua katika ufalme wa Baba yao. Mwenye masikio, na asikie.”

Yesu Kristo ana mamlaka dhidi ya sheria ya Musa - Yohana 1:16-17. “Kwa kuwa katika utimilifu wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema. Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo.”

Yesu ametupa mamlaka ya kufunga au kufungua lolote – Mathayo 18:18-20 “Amin, nawaambieni, yo yote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yo yote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni. Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lo lote watakaloliomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni. Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao.”

Yesu ametupa mamlaka dhidi ya Shetani na wajumbe wake – Luka 10:17-19. “Ndipo wale sabini waliporudi kwa furaha, wakisema, Bwana, hata pepo wanatutii kwa jina lako.  Akawaambia, Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme. Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru.”

Unapoitambua mamlaka ya Kristo unapata ujasiri mkubwa, na swali  hilo hilo wakituliiza sisi wakati tunapoifanya kazi ya Yesu aliyotutuma unaweza kujua kuwa ni madhara gani yanaweza kumkuta mtu anayeshindana na mamlaka hii ona Luka 10:16Awasikilizaye ninyi anisikiliza mimi, naye awakataaye ninyi anikataa mimi; naye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma.” Unaona katika protokali za kibiblia tunapoifanya kazi ya Mungu alafu mtu akahoji unayatenda mambo haya kwa mamlaka gani mtu huyo anamtafuta pweza aliko na yatakayomkuta atashindwa kusimulia hata wajukuu wake kwa nini? Kwa sababu tunafanya kazi chini ya mamlaka kubwa sana sana sana !

Hitimisho!

Kuna mambo mengi sana ya kuzungumzia kuhusu mamlaka ya Yesu, lakini Muda hauwezi kutosha Mamlaka ya Bwana wetu Yesu Kristo ndio mamalaka ya juu zaidi kuliko zote duniani na mbinguni na haipaswi kuhojiwa na mtu awaye yote, Kimsingi Yesu alikuwa mnyenyekevu mno hata kuweza kuwasikiliza wajumbe wa kundi la makuhani na wazee waliohoji mamlaka yake, Eti unayatenda mambo hayo kwa mamlaka gani?  Watu wote tuliopewa agizo la kuihubiri injili tuna mamlaka kubwa na kibali cha kwenda kila mahali kuihubiri njili na kila kitu kimetiishwa chini yetu hakuna kitakachoweza kusimama mbele yetu siku zote za maisha yetu, kwa unyenyekevu inatupasa kutii sheria za kila nchi na taifa zilizowekwa zisizokingana na Mamlaka ya kiungu, kwaajili ya unyenyekevu, lakini mamlaka inayotenda kazi ni kubwa na iko juu yetu. Ni baraza hili ambalo Petro na Yohana aliwahoji yupi wa kumtii Mungu au wanadamu, wako watu wenye mamlaka za duniani ambao hutumia mamlaka zao vibaya wakitaka kudhibiti watumishi wa Mungu,  lakini hatuna budi kufahamu ya kuwa Mungu ametupa mamlaka iliyokubwa sana kupitia Yesu Kristo ni mamlaka ile ileiliyotenda kazi ndani ya Kristo ndiyo inayotenda kazi ndani yetu! Hatupaswi kuogopa

Matendo 4:17-19 “Lakini neno hili lisije likaenea katika watu, na tuwatishe wasiseme tena na mtu awaye yote kwa jina hili. Wakawaita, wakawaamuru wasiseme kabisa wala kufundisha kwa jina la Yesu. Petro na Yohana wakawajibu wakawaambia, Kwamba ni haki mbele za Mungu kuwasikiliza ninyi kuliko Mungu, hukumuni ninyi wenyewe;”

Matendo 5:26-29 “Ndipo yule jemadari akaenda pamoja na watumishi, wakawaleta, lakini si kwa nguvu, kwa maana waliogopa watu wasije wakawapiga kwa mawe.Walipowaleta, wakawaweka katika baraza. Kuhani Mkuu akawauliza,akisema, Je! Hatukuwaamuru ninyi kwa nguvu, msifundishe kwa jina hili? Nanyi, tazameni, mmeijaza Yerusalemu mafundisho yenu, na mnataka kuileta damu ya mtu yule juu yetu. Petro na mitume wakajibu, wakisema, Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu.”

Mathayo 28:18-20 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.”

Kwa msingi huo tunapokwenda kuifanya kazi ya Mungu huku tukiwa tumefuata taratibu zote basi sasa asitokee mtu kututishia na kutaka kuizuia kazi ya Mungu, na wote wanaojihusisha na ushirikina na uchawi na kutaka kushindana na mamlaka ya kiungu tuliyopewa nawaamuru katika jina la Yesu waharibikiwe katika kila mpango wao wa maisha mpaka waokoke katika jina la Yesu, kwa mamlaka niliyopewa kila mahali ambako kuna kizuizi kwaajili ya injili nakiamuru kizuizi hicho kusambaratishwa na kuharibika hata kisiwepo tena katika jina la Yesu Kristo aliye hai, tumia mamlaka hii katika kila jambo lililo kinyume na ustawi wa maisha yako katika mapenzi ya Mungu Kumbuka kuwa ni mamlaka ile ile iliyomtuma Yesu ndiyo tuliyopewa, unaweza kuitumia mamlka hii kukemea lolote lililo kinyume naustawi wako na ustawi wa Ufalme wa Mungu, Yesu ana mamlaka kubwa sana, Hata lile hekalu alisema Imeandikwa NYUMBA YANGU hekalu lile pia lilikuwa ni nyumba yake hata wewe ni mali yake ni aibu kubwa kuhojo mamlaka ya Kristo kwani YU JUU YA YOTE. Asante kwa kufuatilia masomo haya Uongezewe neema !

 

Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!      

Hakuna maoni: