Jumatatu, 8 Januari 2024

Kwanini Yesu alijiita Mwana wa Adamu?


Mathayo 16:13-17 “Basi Yesu akaenda pande za Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani? Wakasema, Wengine hunena u Yohana Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii. Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani? Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni.”

 

 



Utangulizi:

 

Moja ya njia pekee ya kutambua mtu au kitu kwa kina na mapana na marefu ni pamoja na kuangalia majina ambayo mtu huyo anaitwa au anajiita, katika somo la uungu, unapomzungumzia Mungu baba na mwana na Roho Mtakatifu, moja ya nafsi ambayo inasumbua sana wanazuoni wengi wa Kikristo na zaidi wasio wakristo ni kujua asili ya Kristo, na ni kutokana na kuwepo kwa utata mwingi sana kuhusu asili ya Yesu, kumekuwepo na somo katika vyuo vya Biblia linalojaribu kuchambua kwa undani ili kumjua Yesu ni nani, somo hilo kitaalamu huitwa CHRISTOLOGY  ambalo ni muunganiko wa misamiati miwili ya kiyunani CHRIST na LOGOS ikiwa na maana ya MAARIFA KUHUSU KRISTO – Knowledge about Christ, Somo hilo kimsingi linahusika na kuchambua kwa undani sana kuhusu Yesu Kristo na asili yake, kumjua Yesu na Mungu baba yetu wa Mbinguni yalikuwa ni moja ya sehemu ya muhimu ya maombi ya Yesu Kristo kwetu!.

 

Yohana 17:1-3 “Maneno hayo aliyasema Yesu; akainua macho yake kuelekea mbinguni, akasema, Baba, saa imekwisha kufika. Mtukuze Mwanao, ili Mwana wako naye akutukuze wewe;             kama vile ulivyompa mamlaka juu ya wote wenye mwili, ili kwamba wote uliompa awape uzima wa milele. Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma.”

 

Kumjua Yesu Kristo kwa kawaida sio swala Jepesi kama tunavyofikiri, huwezi kumjua Yesu bila msaada wa Mungu, maandiko au Yesu Mwenyewe na katika maandiko pia wakati mwingine ni mpaka yeye mwenyewe ahusike kukufunulia andiko husika kwa neema yake. Leo tutachukua muda kujifunza somo hili muhimu KWANINI YESU ALIJIITA MWANA WA ADAMU tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

 

·         Jinsi kuijua asili ya Yesu Kristo kulivyowasumbua wasomi

·         Jinsi ya kumjua Yesu Kristo

·         Kwanini Yesu alijiita mwana wa Adamu

 

Jinsi kuijua asili ya Yesu kulivyowasumbua wasomi

 

Moja ya swala ambalo lilisumbua sana mnamo karne ya kwanza mpaka karne ya tatu kwa wanazuoni wakubwa sana katika kanisa la Mungu, ilikuwa ni pamoja na kuijua nafsi ya Mungu mwana, utata kuhusu Yesu ni nani sio tu ulisumbua vichwa vya wasomi, lakini hata wakati wa Yesu mwenyewe kila mmoja alikuwa akisema lake kuhusu Yesu ni nani ona :-

 

Mathayo 16:13-17 “Basi Yesu akaenda pande za Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani? Wakasema, Wengine hunena u Yohana Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii. Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani? Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni.”

 

Katika karne ya tatu swali kuhusu Masihi ni nani bado liliendelea kuwasumbua wasomi na kila mtu alikuwa na maoni yeke kuhusu asili ya Yesu kuwa ikoje na ni nani? Kama tunavyoweza kujionea maoni mbalimbali ya wanazuoni wakiumiza kichwa kumjua Yesu.

 

1.      Waebionite – (Ebionites) – Hili ni kundi la wakristo wa kiyahudi ambao walikuweko karne za mwanzoni wakiishi maisha ya kimasikini wakiwa na Imani kuwa umasikini una uhusiano na maisha matakatifu, waoa walikuwa wakiamini kuwa YESU NI MASIHI LAKINI SIO MUNGU na kuwa kuzaliwa kwake na Mariamu kunasisitiza umuhimu wa kuishika na kuitii Torati ya Musa, Hivyo Yesu ni Mwanadamu aliyetii torati yote ya Musa na kutunukiwa kuwa masihi.

 

2.      Waanostisizim – (Gnosticism) – Hili ni kundi la watu walioamini kuwa Maarifa yanaleta wokovu na dhambi ni ujinga, kundi hili liliamini kuwa YESU ALIKUWA NI ROHO NA HAJAWAHI KUUTWAA MWILI Fundisho la aina hii lilipingwa vikali na Mtume Yohana na alilionya kanisa kuwa makini na aina ya fundisho kama hilo ona

 

 1Yohana 4:1-3 “Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani. Katika hili mwamjua Roho wa Mungu; kila roho ikiriyo kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili yatokana na Mungu. Na kila roho isiyomkiri Yesu haitokani na Mungu. Na hii ndiyo roho ya mpinga Kristo ambayo mmesikia kwamba yaja; na sasa imekwisha kuwako duniani.”            

3.      Waariyan – (Arianism) – Ni kundi la Wakristo waliofuata fundisho la Mwanatheolojia aliyeitwa Arius ambaye alikuwa mwangalizi na msomi wa chuo kikuu cha Kikristo huko Alexandria nchini Misri kati ya mwaka 256-336 Baada ya Kristo, wao waliamini kuwa Yesu sio Mungu ni kiumbe cha kwanza kuumbwa na Mungu na hivyo hayuko sawa na Mungu lakini yuko chini kidogo ya Mungu na juu ya malaika, walimuita Yesu Mwanzo wa kuumba kwa Mungu sawa na

 

Ufunuo 3:14c “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, MWANZO WA KUUMBA KWA MUNGU.”

 

Pia wanatumia andiko hili kutoka injili ya Yohana Yesu akisema baba ni Mkubwa kuliko Yeye

 

Yohana 14:28 “Mlisikia ya kwamba mimi naliwaambia, Naenda zangu, tena naja kwenu. Kama mngalinipenda, mngalifurahi kwa sababu naenda kwa Baba, KWA MAANA BABA NI MKUU KULIKO MIMI.”

 

4.      Wanestorian – (Nestorianism) – Hili ni kundi lingine la wasomi wa Kikristo, waliokuwa na mtazamo tofauti kuhusu asili ya Yesu, wao waliona kuwa uungu na ubinadamu hauwezi kuwa na muunganiko kwa hiyo Yesu hawezi kuwa Mungu mwanadamu, au kuwa Mungu wakati huo huo na wakati huo huo mwanadamu.

 

5.      Waapolonari – (Apollinarian) – Aplonari alikuwa ni askofu kijana wa kanisa la Laodekia lililokuwako huko Syria mwaka wa 361 baada ya Kristo, yeye aliamini pamoja na watu wake kuwa Yesu alikuwa mwanadamu lakini akili yake ilikuwa akili ya kiungu, kwa hiyo asili hizi mbili hazikuweza kujitokeza kwa pamoja ni kama anataka kusema kuwa kuna wakati Yesu alikuwa mwanadamu na alisema na kundenda kibinadamu na kuna wakati alikuwa Mungu na alitenda na kusema kama Mungu.

 

6.      Waeutiko – ( Eutychians)  - Hili ni kundi la Wakristo waliofuata mafundisho ya Eutychus ambaye aliishi huko Constantinople, kati ya mwaka  380 - 456      baada ya Kristo, wao walikuwa na fundisho kuwa Yesu alikuwa na asili mpya yaani Mungu + Mwanadamu = Asili mpya, kwa hiyo Yesu sio Mungu wala sio Mwanadamu

 

7.      Waorthodox – (Orthodox) – Hili ni Kundi la wakristo wanaoamini kuwa wanafundisho sahihi neno Orthodox maana yake ni Right opinion  wao waliamini kuwa Yesu ni Mungu mwanadamu na kwa sababu hiyo Yeye ni Mwanadamu kwa asilimia 100% na ni Mungu kwa asilimia 100% fundisho hili ndilo lililosalia kuwa fundisho sahihi mpaka sasa kwa mujibu wa kanisa la Mungu  wao wanasimamia andiko la Yohana 1:1-3, 13-14

 

Yohana 1:1-3 “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika.”

 

Yohana 1:14 “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.”

 

Unaweza kuona makundi hayo yalikuwa na mijadala mikali sana kuhusu Asili ya Kristo, na hii inatufundisha wazi kuwa kumjua Yesu Kristo sio kazi nyepesi kama watu wengi wanavyodhani inahitajika neema maalumu ya kiungu kuweza kumjua Yesu, na ndio maana watu wengi sana huwa wanachanganyikiwa kuhusu, nafsi na asili ya Yesu mpaka leo, Ni muhimu sana tunapoendelea kujifunza somo hili kuwa na maombi ya kutaka kumjua Yesu zaidi, kama mwandishi wa Tenzi za injili namba 92 alivyoimba kuwa anataka kumjua Yesu na azidu kumfahamu, tunahitaji neema ya Mungu kumjua bwana wetu Yesu.

 

Jinsi ya kumjua Yesu Kristo

           

Kumjua Yesu Kristo kamwe hakuwezi kuja kwa akili za kawaida za kibinadamu, wala kwa kujenga hoja za kisomi, maandiko na Yesu Kristo Mwenyewe anaonyesha wazi kuwa kumjua Yesu Kristo kunaweza kuletwa kwetu kwa msaada wa Mungu na ufunuo wa Mungu Baba mwenyewe kwetu kupitia Roho wake Mtakatifu, maandiko au Yesu Kristo mwenyewe moja kwa moja tunaweza kupata ushahidi wa jambo hili kwa kuangalia tena andiko letu la Msingi

 

Mathayo 16:16-17 “Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni.”

 

Unaona? Yesu alipouliza swali watu wanasema kuwa mwana wa Adamu ni nani, kulikuwa na majibu mbali mbali kuhusu Masihi, lakini hatimaye Simioni Petro akajibu, wewe ndiwe Kristo Mwana wa Mungu aliye hai, na mara baada ya jibu hili ambalo lilikukuwa jibu sahihi Yesu alijibu kwa kumwambia HERI WEWE SIMONI BAR-YONA; KWA KUWA MWILI NA DAMU HAVIKUKUFUNULIA HILI, BALI BABA YANGU ALIYE MBINGUNI Maneno haya yana maana gani? Rahisi tu huwezi kumjua Yesu bila kufunuliwa na Mungu mwenyewe, na kule kusema mwili na damu havikukufunulia hili, Yesu alikuwa akimaanisha Akili ya kawaida ya kibinadamu na uweza katika uhai wa mwanadamu hauwezi kutambua siri hii ya kuwa Yesu Kristo ni nani, na ndio maana umeweza kuona wasomi wengi walisumbuka kutambua asili ya Kristo na hata leo, watu wa dini nyingine hususani wakiwemo waislamu wanahangaika sana na kutatizwa mno na ukweli kuhusu asili ya Yesu Kristo,  na huwa wanadhani tuna haja ya kumkuza sana au kukufuru kwa kumpa Heshima ambayo wanadhani haistahili, jambo kubwa la Msingi ni kuwa tunamjua Mungu kupitia ufunuo kutoka kwa Mungu mwenyewe! Na neema yake wakati tunapotafakari na kumruhusu yeye atufunulie maandiko!

 

Au wakati mwingine Yesu mwenyewe huwa anahusika kutufunulia yeye mwenyewe ili tuweze kumjua au kutufunulia maandiko ili tuweze kuelewa, jambo hili linadhihirika wazi kuwa hata wanafunzi wa Yesu, waliomuona mubashara alipokuwa hai, alipofufuka ilikuwa ngumu kwao kumjua na hata kujua kile ambacho kimeandikwa kumuhusu, lakini kwa msaada wake yeye mwenyewe waliweza kubaini ukweli uliokuweko na kwa hiyo kwa kupitia ufunuo wake katika maandiko unaweza kumjua kumhusu! Angalia maandiko hapa:-

 

Luka 24:13-32Na tazama, siku ile ile watu wawili miongoni mwao walikuwa wakienda kijiji kimoja, jina lake Emau, kilichokuwa mbali na Yerusalemu kama mwendo wa saa mbili. Nao walikuwa wakizungumza wao kwa wao habari za mambo hayo yote yaliyotukia. Ikawa katika kuzungumza na kuulizana kwao, Yesu mwenyewe alikaribia, akaandamana nao. Macho yao yakafumbwa wasimtambue. Akawaambia, Ni maneno gani haya mnayosemezana hivi mnapotembea? Wakasimama wamekunja nyuso zao. Akajibu mmoja wao, jina lake Kleopa, akamwambia, Je! Wewe peke yako u mgeni katika Yerusalemu, hata huyajui yaliyotukia humo siku hizi? Akawauliza, Mambo gani? Wakamwambia, Mambo ya Yesu wa Nazareti, aliyekuwa mtu nabii, mwenye uwezo katika kutenda na kunena mbele za Mungu na watu wote; tena jinsi wakuu wa makuhani na wakubwa wetu walivyomtia katika hukumu ya kufa, wakamsulibisha. Nasi tulikuwa tukitumaini ya kuwa yeye ndiye atakayewakomboa Israeli. Zaidi ya hayo yote, leo ni siku ya tatu tangu yalipotendeka mambo hayo; tena, wanawake kadha wa kadha wa kwetu walitushitusha, waliokwenda kaburini asubuhi na mapema, wasiuone mwili wake; wakaja wakasema ya kwamba wametokewa na malaika waliosema kwamba yu hai. Na wengine waliokuwa pamoja nasi walikwenda kaburini wakaona vivyo hivyo kama wale wanawake walivyosema, ila yeye hawakumwona. Akawaambia, Enyi msiofahamu, wenye mioyo mizito ya kuamini yote waliyoyasema manabii! Je! Haikumpasa Kristo kupata mateso haya na kuingia katika utukufu wake? Akaanza kutoka Musa na manabii wote, akawaeleza katika maandiko yote mambo yaliyomhusu yeye mwenyewe. Wakakikaribia kile kijiji walichokuwa wakienda, naye alifanya kama anataka kuendelea mbele. Wakamshawishi wakisema, Kaa pamoja nasi, kwa kuwa kumekuchwa, na mchana unakwisha. Akaingia ndani kukaa nao. Ikawa alipokuwa ameketi nao chakulani, alitwaa mkate, akaubariki, akaumega, akawapa. Yakafumbuliwa macho yao, wakamtambua; kisha akatoweka mbele yao. Wakaambiana, Je! Mioyo yetu haikuwaka ndani yetu hapo alipokuwa akisema nasi njiani, na kutufunulia maandiko?      

 

Kwa hiyo hata maandiko kumbe tunaweza tu tukayasoma lakini kama Mungu Baba, au Mwana au Roho Mtakatifu hatakufunulia jambo au utafichwa jambo huwezi kulibaini au kulijua, wanafunzi wa Yesu ni mpaka yalipofumbuliwa macho yao ndio wakaweza kuelewa na macho yao yakafunguliwa wakamtambua, lakini pia alipokuwa akiwafunulia maandiko tena akiwakemea ENYI MSHIOFAHAMU WENYE MIOYO MIZITO YA KUAMINI YOTE WALIYOYASEMA MANABII, ukifungwa ufahamu, ukawa na moyo mzito huwezi kuelewa na kuamini hata kilichoandikwa na manabii, Yesu akikufunulia maandiko utamuelewa kwa undani, na anaweza kufanya hivyo kwa wale waliokuwa pamoja naye n ahata kwa wale wasiokuwa pamoja naye yaani hata sisi leo Yesu yu aweza kutuelekeza kitu kupitia Roho wake Mtakatifu na tukaweza kuelewa yale yaliyofichika ona hii:-

 

Wagalatia 1:11-12 “Kwa maana, ndugu zangu, injili hiyo niliyowahubiri, nawajulisha ya kuwa siyo ya namna ya kibinadamu. Kwa kuwa sikuipokea kwa mwanadamu wala sikufundishwa na mwanadamu, bali kwa ufunuo wa Yesu Kristo.”

 

Paulo Mtume pia katika kifungu hiki anatuhakikishia kuwa aliihubiri injili ambayo haikuwa ya namna ya kibinadamu kwa sababu aliipokea na kufundishwa na Yesu Kristo mwenyewe kwa ufunuo, kwa hiyo unaweza kukubaliana nami wazi kuwa bila kufunuliwa jambo kuhusu Kristo ni vigumu kwa akili za kawaida kuweza kutambua kitu au jambo kuhusu Yesu Kristo, Hasa kama Bwana amekusudia kulificha au kama hatuna muda wa kusoma na kutafakari na kutaka kumjua. Bwana ampe neema kila mmoja wetu kuwa na ufunuo kumhusu Kristo ili tuweze kuwa na uelewa mpana kwa kina na mapana na marefu kumuhusu Yesu!, katika somo hili sio nia yangu kumuelezea Yesu Kristo labda nitafanya hivyo wakati mwingine leongo langu kuu ni kujibu swali la Msingi kwanini Yesu alijiita mwana wa Adamu hili tutalitafakari kwa kina katika kipengele kinachofuata:-

 

Kwanini Yesu alijiita mwana wa Adamu

 

Kama umeweza kunifuatilia tangu mwanzo, leo sitaki kujibu swali Yesu ni nani, lakini nataka kujibu na kuweka wazi kwanini Yesu alijiita Mwana wa Adamu, moja  ya njia ya kumjua Yesu ni pamoja na kuyajua maandiko, kwamba yanasema nini Kumuhusu yeye, kwa hiyo katika somo la ufahamu kuhusu Yesu Kristo yaani Christology waalimu wanafanya kazi kubwa sana ya kuchambua majina yoote ya Yesu Kristo yaliyotumika katika maandiko kumuelezea, na moja ya majina hayo ni MWANA WA ADAMU tena inaonekana wazi kuwa jina hili Yesu Kristo mwenyewe ndiye aliyelitumia zaidi kuliko wanafunzi wake wala watu wengine, kwa hiyo kuna swali kubwa sana la msingi la kujiuliza kwanini Yesu alikuwa akijiita mwana wa Adamu? Na kabla ya kuangalia swala hilo tuone sehemu kadhaa katika maandiko Yesu akijiita mwana wa Adamu na tukio hili la kujiita mwana wa Adamu limeonekama mara zaidi ya 82 katika maandiko hususani agano jipya

 

Mathayo 12:31-32 “Kwa sababu hiyo nawaambia, Kila dhambi na kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu, ila kwa kumkufuru Roho hawatasamehewa. Naye mtu ye yote atakayenena neno juu ya MWANA WA ADAMU atasamehewa, bali yeye atakayenena neno juu ya Roho Mtakatifu hatasamehewa katika ulimwengu wa sasa, wala katika ule ujao.”            

 

Mathayo 13:37 “Akajibu, akasema, Azipandaye zile mbegu njema ni MWANA WA ADAMU;”

 

Marko 14:62 “Yesu akasema, Mimi ndiye, nanyi mtamwona MWANA WA ADAMU ameketi mkono wa kuume wa nguvu, akija na mawingu ya mbinguni.”

 

Luka 12:8-10 “Nami nawaambia, kila atakayenikiri mbele ya watu, MWANA WA ADAMU naye atamkiri yeye mbele ya malaika wa Mungu;          na mwenye kunikana mbele ya watu, huyo atakanwa mbele ya malaika wa Mungu. Na kila mtu atakayenena neno juu ya MWANA WA ADAMU atasamehewa, bali aliyemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa.”

 

Yohana 1:51 “Akamwambia, Amin, amin, nawaambia, Mtaziona mbingu zimefunguka na malaika wa Mungu wakikwea na kushuka juu ya MWANA WA ADAMU.”

 

Yohana 3:13-15 “Wala hakuna mtu aliyepaa mbinguni, ila yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani, MWANA WA ADAMU. Na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo MWANA WA ADAMU hana budi kuinuliwa; ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye.”

 

Mathayo 8:20 “Yesu akamwambia, Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana viota; lakini MWANA WA ADAMU hana pa kulaza kichwa chake.”

Marko 10:45 “Kwa maana MWANA WA ADAMU naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.”

 

Luka 5:24 “Lakini, mpate kujua ya kwamba MWANA WA ADAMU anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (alimwambia yule mwenye kupooza). Nakuambia, Ondoka, ujitwike kitanda chako, ukaende zako nyumbani kwako.”

 

Mathayo 26:64 “Yesu akamwambia, Wewe umesema; lakini nawaambieni, Tangu sasa mtamwona MWANA WA ADAMU ameketi mkono wa kuume wa nguvu, akija juu ya mawingu ya mbinguni.”

 

Hayo ni baadhi ya maandiko machache tu ambayo yanamtaja Yesu kama Mwana wa Adamu,  na baadhi ya mikazo hii aliitaja yeye mwenyewe, swali kubwa linabaki kwanini Yesu anajiita Mwana wa Adamu?  Na ni watu wachache sana ambao walimuita Yesu mwana wa Adamu baada ya kumuona akiwa amesimama mkono wa kuume wa Mungu ona

 

Matendo 7:55-56 “Lakini yeye akijaa Roho Mtakatifu, akakaza macho yake, akitazama mbinguni, akauona utukufu wa Mungu, na Yesu akisimama upande wa mkono wa kuume wa Mungu. Akasema, Tazama! Naona mbingu zimefunguka, na MWANA WA ADAMU amesimama mkono wa kuume wa Mungu.”            

 

Kwa mujibu wa utafiti wa kimaandiko na michango ya wanazuoni wengi kuhusu tafasiri ya kwanini Yesu alijiita Mwana wa Adamu kwa mkazo na msisitizo mkubwa? Ziko sababu kadhaa ambazo wanatheolojia wanajaribu kuelezea Kama nitakavoainisha hapa

 

1.      Kusisitiza uhusiano wake na wanadamu

 

Moja ya tafasiri inayoelezwa na wanazuoni ni kwanini Yesu alijiita mwana wa Adamu inasemekana ni kusisitiza uhusiano wake na wanadamu, hii ni kwa sababu neno Mwana wa Katika Kiibrania linasomeka BEN ambalo lina maana kubwa mbili, Mtoto wa, na uhusiano na, Kwamfano watu waliookoka wao huitwa wana wa Ufalme ona

 

Mathayo 8:11-12 “Nami nawaambieni, ya kwamba wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi pamoja na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo katika ufalme wa mbinguni; bali wana wa ufalme watatupwa katika giza la nje, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.”        

 

Wakati wale watakaofufuliwa na Bwana wetu Yesu Kristo wanaitwa wana wa Ufufuo

 

Luka 20: 35-36 “lakini, wale wahesabiwao kuwa wamestahili kuupata ulimwengu ule, na kule kufufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi; wala hawawezi kufa tena; kwa sababu huwa sawasawa na malaika, nao ni wana wa Mungu, kwa vile walivyo wana wa ufufuo.”

 

Hali kadhalika wale wanaopenda Amani, Yesu aliwaita wana wa Amani unaweza kuona katika

 

Luka 10:5-65. “Na nyumba yo yote mtakayoingia, semeni kwanza, Amani iwemo nyumbani humu; na akiwamo mwana wa amani, amani yenu itamkalia; la, hayumo, amani yenu itarudi kwenu.”

 

Na mtu ambaye ameandikiwa hukumu ya Mungu, huitwa mwana wa uharibifu mfano ni Yuda ona

 

Yohana 17:12 “Nilipokuwapo pamoja nao, mimi naliwalinda kwa jina lako ulilonipa, nikawatunza; wala hapana mmojawapo wao aliyepotea, ila yule mwana wa upotevu, ili andiko litimie.”

 

Kwa hiyo Yesu anapotumia neno Mwana wa Adamu anammaanisha kimsingi uhusiano wake na wanadamu, au uhusuano wake na Adamu aliye baba ya wanadamu wote, kwa msingi huo katika mkazo huu Yesu ambaye ni Mungu anataka kuonyesha ushirika wake na wanadamu, anataka kutuonyesha kuwa aliacha enzi na utukufu na kukubali kuwa mwanadamu ambaye kimsingi ni dhaifu na hivyo ni jambo la unyenyekevu sana    

 

Wafilipi 2: 6-8 ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.”

 

Kwa msingi huo jina hili Mwana wa Adamu linaunganisha au kuonyesha ubinadamu wote wa Bwana Yesu, akiwa anakula, anachoka, analala, anasalitiwa, anateswa, anadhihakiwa, anateswa na anauawa na hatimaye Mungu anamfufua kutoka kwa wafu, kwa hiyo moja yaw azo la kitheolojia ni kuwa Yesu ambaye ni Mungu alikuwa anafurahia kuushiriki ubinadamu na akawa anaweza mkazo Mwana wa Adamu.

 

2.      Kwaajili ya Kutimiza unabii

 

Jambo lingine linalozungumzwa na wanazuoni kwamba ni kwanini Yesu alijiita Mwana wa Adamu ilikuwa ni kujitambulisha kuwa yeye ndiye Masihi sawa na nabii mbalimbali katika maandiko ukiwemo unabii wa Daniel tunaweza kuliona hilo wazi katika

 

Daniel 7:13-14 “Nikaona katika njozi za usiku, na tazama, mmoja aliye mfano wa mwanadamu akaja pamoja na mawingu ya mbingu akamkaribia huyo mzee wa siku, wakamleta karibu naye. Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa.”

 

Ni uwazi kuwa unabii huu wa Daniel pamoja na maeneo mengine umesema wazi kuwa masihi atakuwa ni wa namna gani, ni aliye mfano wa Mwanadamu na akapewa Mamlaka na utukufu na ufalme, hivyo ni vya milele, kwa hiyo wanatheolojia wengi wanahisia ya kuwa Yesu alupokuwa akijiita mwana wa Adamu alikuwa pia akijidhihirisha kuwa yeye ni Masihi sawa na namna na jinsi alivyotabiri nabii Daniel.

 

Kwa ujumla kupitia Yesu kuwa mwanadamu, ameweza kufanya kazi kubwa ya kuandaa njia ya ukombozi wa mwanadamu, ukiacha kuja kuwa na Enzi na mamlaka ya utawala wa kiungu duniani lakini Masihi ameweza kufanya mengi kwaajili ya wanadamu, ameweza kuufunua uungu na wema na tabia ya Mungu kupitia uanadamu wake kwa hiyo kuna faida kubwa sana ya Yesu kuwa mwanadamu mfano

 

Kusamehe dhambi wanadamu kwa sababu ameonja unanadamu anajua udhaifu wa mwanadamu – Marko 2:10 “Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (hapo amwambia yule mwenye kupooza),”

 

Kumtafuta mwanadamu na kumuokoa – Luka 19:9-10 “Yesu akamwambia, Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu. Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.”

 

Kushiriki mateso kwa niaba ya wanadamu ili kuleta ukombozi – Marko 8:31  Akaanza kuwafundisha kwamba imempasa Mwana wa Adamu kupatikana na mateso mengi, na kukataliwa na wazee, na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na baada ya siku tatu kufufuka.”

 

Kumfunua Mungu kwetu – Yesu alipokuwa na mwili wa kibinadamu alisema wazai kuwa kazi ananozifanya na maneno yote aliyokuwa anawafundisha yalikuwa yanafunua matendo ya Mungu kwa wanadamu

 

Yohana 5:19-20 “Mwana hawezi kutenda neno mwenyewe ila lile ambalo amwona Baba analitenda; kwa maana yote ayatendayo yeye, ndiyo ayatendayo Mwana vile vile.Kwa kuwa Baba ampenda Mwana, naye humwonyesha yote ayatendayo mwenyewe; hata na kazi kubwa zaidi kuliko hizo atamwonyesha, ili ninyi mpate kustaajabu.”

 

Kuonyesha shauku ya Mungu kushirikiana na wanadamu – Mathayo 1L22-23 “Hayo yote yamekuwa, ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii akisema, Tazama, bikira atachukua mimba, Naye atazaa mwana; Nao watamwita jina lake Imanueli; Yaani, Mungu pamoja nasi.”           

 

3.      Kwaajili ya Kufunua asili yake ya uungu

 

Tunaelewa wazi kuwa Yesu ni Mungu, kule kuitwa mwana wa Mungu maana yake anashiriki uungu, kwa hiyo Yesu alikuwa akijionea fahari kuushiriki uanadamu, huku yeye akiwa na asili ya uungu, Mungu anamjua mwanadamu kama kiumbe dhaifu na mara kadhaa alilitumia neno mwanadamu akimuita Ezekiel, inasemekana Mungu anamtaja Ezekiel kama mwanadamu mara 93 kwa msingi huo Mungu alikuwa akimaanisha Ezekiel ni mwanadamu lakini sivyo Ilivyo Kwa Kristo. Yesu hakuwa dhaifu Kama Ezekiel Yeye alikuja kumfunua Mungu kwetu, alikuwa Mungu aliyeishi katika ubinadamu

 

Wakolosai 2:9 “Maana katika yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili.”

 

Kwaajili ya haya aliweza kusamehe dhambi, aliweza kuonyesha ubwana dhidi ya sabato, aliweza kuonyesha kuwa amekuja kumuokoa mwanadamu, aliweza kuonyesha kuwa ana uwezo wa kufufua wafu, aliweza kuonyesha kuwa anamamlaka ya kuhukumu, na kuonyesha kuwa atarudi tena siku moja duniani, aliweza kuonyesha kuwa ana mamlaka ya kubadili sharia ya Musa kwa kuitimiza na ana mamlaka ya kumuweka huru Mwanadamu na kumkomboa kama mwana wa Mfalme wa Mbinguni

 

Mathayo 26:64 “Yesu akamwambia, Wewe umesema; lakini nawaambieni, Tangu sasa mtamwona Mwana wa Adamu ameketi mkono wa kuume wa nguvu, akija juu ya mawingu ya mbinguni.”

 

Kwa sababu hizi na nyinginezo nyingi wanatheolojia wanazitumia kumuelezea Yesu na kujaribu kujibu kuwa ndio sababu kubwa na za Msingi za Yesu kujiita mwana wa Adamu. Kwa hiyo katika tafiti nyingi na vitabu vingi na wajenga hija wengi wanaishia kwenye jambo hilo na sababu hizo kwanini Yesu alijiita mwana wa Adamu!

 

Hitimisho:

 

Kwa mtazamo wangu mimi ambao ndio umenisukuma kuandaa somo hili, Yesu alipokuwa akijiita Mwana wa Adamu, kuna tofauti kabisa na Mungu alivyokuwa akimuita Ezekiel nabii Mwanadamu, Yesu alikuwa akijiita Mwana wa Adamu, katika mtazamo uleule wa namna anavyojiita au alivyoitwa Mwana wa Abraham, au Mwana wa Daudi, unapoangalia maandiko katika Kitabu za Ezekiel Mungu anapomuita Ezekiel Mwanadamu kuna tofauti na neno Mwana wa Adamu linavyotumika katika Agano jipya tunaweza kuona kwa kitambo kiasi

 

Ezekiel 3:1-4 “Akaniambia, Mwanadamu, kula uonacho; kula gombo hili, kisha enenda ukaseme na wana wa Israeli. Basi nikafunua kinywa changu, naye akanilisha lile gombo. Akaniambia, Mwanadamu, lisha tumbo lako, ulijaze tumbo lako kwa hili gombo nikupalo. Ndipo nikalila, nalo kinywani mwangu lilikuwa tamu, kama utamu wa asali. Akaniambia, Mwanadamu, haya! Waendee wana wa Israeli ukawaambie maneno yangu.”

 

 

Mathayo 12:31-32 “Kwa sababu hiyo nawaambia, Kila dhambi na kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu, ila kwa kumkufuru Roho hawatasamehewa. Naye mtu ye yote atakayenena neno juu ya MWANA WA ADAMU atasamehewa, bali yeye atakayenena neno juu ya Roho Mtakatifu hatasamehewa katika ulimwengu wa sasa, wala katika ule ujao.”

 

Katika kiingereza wakati kwa Ezekiel wanatumia son of man au a son of man kwa Yesu linatumika neno The Son of Man, kwa Ezekiel ikimaanisha mwanadamu, na Kwa Yesu Kristo ikimaanisha Mwana wa Adamu, hii maana yake ni nini?  Huyu ni mwana wa Adamu wa Ahadi ambaye Adamu alikuwa ameahidiwa, kama ilivyokuwa kwa Abrahamu ambaye alikuwa ameahidiwa na Daudi ambaye naye alikuwa ameahidiwa, mwana huyu wa Ahadi aliyeahidiwa Adamu katika kitabu cha Mwanzo:-

 

Mwanzo 3:14-15 “BWANA Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha yako; nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino.”

 

Ijapokuwa mwana huyu wa ahadi anaitwa uzao wa Mwanamke, lakini kwa uwazi kabisa alikuwa ni mtoto wa Adamu kwa hiyo Tangu wakati huu katika wazo la Adamu na wazo la Mwanamke walikuwa wanafahamu kuwa kuna moja ya mtoto wao ambaye atakuwa suluhisho la mgogoro kati yao na Shetani, Kwa hiyo alikuwa ni mtoto wa ahadi za kinabii, fahamu kuwa katika agano la kale mwanzoni kabisa hakukuwa na nabii na hivyo Mungu baba mwenyewe ndiye aliyekuwa nabii kwa Adamu na Eva na unabii wa kwanza ni Mwanzo 3:15 uzao wa mwanamke,

 

kwa hiyo Yesu alipokuwa akijiita mwana wa Adamu alikuwa akimaanisha mwana wa Ahadi wa Adamu, na Mwana wa Ahadi wa Abraham na mwana wa Ahadi wa Daudi, huyu kwa vyovyote vile angetokea katika mti wa uzao wa Adamu, mti wa uzao wa Ibrahimu na mti wa uzao wa Daudi. Kwa hiyo Yesu alipokuwa akijita Mwana wa Adamu alikuwa anamanisha mwana wa Ahadi wa Adamu ambaye Mungu alikuwa amemkusudia kwa ukombozi, hii ni moja ya sababu ya kujiita mwana wa Adamu, na ni mwana wa adamu ambaye atateseka angalia neno KUPONDA KISIGINO na kupitia maumivu haya ya kupondwa kisigino yeye atakomesha mateso kwa kumaliza uadui kati yetu na shetani angalia neno KUPONDA KICHWA.  Yesu alitumia jina Mwana wa Adamu mara nyingi sana akitaka akili za watu zifunguke na kumwangalia mtoto wa Adamu aliyeahidiwa unaona!

 

Sababu nyingine kubwa ya Msingi ya Yesu kujiita mwana wa Adamu ilikuwa ni maalumu sana akijilinganisha na Mwana wa Adamu aliyeuawa na Ndugu yake, Mwana huyu wa Adamu alikuwa mwenye haki, hakuwa na kosa lolote lakini aliuawa tu kwa sababu alipata kibali kwa Mungu, mwana huyu wa Adamu ni Habili, ambaye aliuawa na kaka yake Kaini,  kwa msingi huo mara kwa mara Yesu alipojiita mwana wa Adamu alikuwa maalumu anajidhihirisha kuwa Yeye ndiye yule Mwenye haki aliyeuawa katika mikono ya watu wabaya, Mwana huyu wa Adamu alimuuma sana Adamu, hasa damu yake ilipomwagika hii ndio picha halisi ambayo wanatheolojia wengi hawajawahi kuizungumzia, lakini Roho Mtakatifu alinifundisha kuwa Yesu anapojiita mwana wa Adamu kwa hakika alikuwa akimaanisha MTOTO WA ADAMU MWENYE HAKI ALIYEUAWA kwa mikono ya ndugu yake na wakati huo huo msisitizo ukiwa katika kuuawa kwake ambako kimsingi kunafanana na kuuawa kwa Habili,  tumeona maswala kadhaa kumuhusu Habili katika maandiko

 

Mtoto huyu wa Adamu alikuwa Mchungaji wa wanyama – Mwanzo 4:2 “Akaongeza akamzaa ndugu yake, Habili. Habili alikuwa mchunga kondoo, na Kaini alikuwa mkulima ardhi.”      

 

Mtoto huyu wa Adamu alikubaliwa na Mungu kutokana na Sadaka yake - Mwanzo 4:4 “Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. BWANA akamtakabali Habili na sadaka yake;”

 

Mtoto huyu wa Adamu alisalitiwa na kuuawa na ndugu yake - Mwanzo 4:8-10 “Kaini akamwambia Habili nduguye, [Twende uwandani]Ikawa walipokuwapo uwandani, Kaini akamwinukia Habili nduguye,akamwua. BWANA akamwambia Kaini, Yuko wapi Habili ndugu yako? Akasema, Sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu? Akasema, Umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi.”

 

Mtoto huyu wa Adamu alikuwa mwenye haki - Mathayo 23:32-36 “Kijazeni basi kipimo cha baba zenu. Enyi nyoka, wana wa majoka, mtaikimbiaje hukumu ya jehanum? Kwa sababu hiyo, angalieni, mimi natuma kwenu manabii na wenye hekima na waandishi; na wengine wao ninyi mtawaua na kuwasulibisha, na wengine wao mtawapiga katika masinagogi yenu, na kuwafukuza mji kwa mji; hivyo ije juu yenu damu yote ya haki iliyomwagika juu ya nchi, tangu damu ya Habili, yule mwenye haki, hata damu ya Zakaria bin Barakia, mliyemwua kati ya patakatifu na madhabahu. Amin, nawaambieni, Mambo hayo yote yatakuja juu ya kizazi hiki.”

 

Mtoto huyu wa Adamu Damu yake ilidai haki - Waebrania 12:24 “na Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili.”

 

Mtoto huyu wa Adamu alikuwa tumaini la ukombozi wa Wazazi wake - Mwanzo 4:25-26 “Adamu akamjua mke wake tena; akazaa mwana mwanamume, akamwita jina lake Sethi; maana alisema, MUNGU AMENIWEKEA UZAO MWINGINE MAHALI PA HABILI; kwa sababu Kaini alimwua. Sethi naye akazaa mwana; akamwita jina lake Enoshi. Hapo ndipo watu walipoanza kuliitia Jina la BWANA.”

 

Mtoto huyu wa Adamu alifanya matendo yake kwa Imani - Waebrania 11:4 “Kwa imani Habili alimtolea Mungu dhabihu iliyo bora kuliko Kaini; kwa hiyo alishuhudiwa kuwa ana haki; Mungu akazishuhudia sadaka zake, na kwa hiyo, ijapokuwa amekufa, angali akinena.”

 

Jambo hili Muhimu sana linalomuhusu Mwana huyu wa kipekee wa Adamu lina umuhimu mkubwa sana ukiunganisha na matukio yaliyomkuta Bwana wetu Yesu Kristo, Habili alichunga Kondoo, Yesu ndiye Mchungaji mwema, Habili alitoa sadaka iliyokubaliwa na Mungu, Na Yesu mjumbe wa Agano jipya aliyetoa damu inenayo mema kuliko ile ya Habili, Kuuawa kwake kulileta mtoto wa matumaini ambaye baada yake watu walianza kuliitia jina la bwana, ni baada ya kifo cha Yesu Kristo wanadamu wanapata nafasi ya kumfikia Mungu na kumuabudu pasipo hofu, Habili alikuwa mwenye haki, akauawa na ndugu yake, Na Yesu hakuwa na hatia akauawa na ndugu zake kwa hiyo kwa mujibu wa maelekezo niliyopewa mimi kama mkuu wa wajenzi, Mungu alinielekeza niieleze dunia leo, jambo ambalo wanazuoni na wanatheolojia huwa hawalielezei, au hawakuwa wamefunuliwa ya kuwa Yesu anapojiita mwana wa Adamu ni ukweli ulio wazi kuwa katika ubongo wake hakuna na wazo la mtu yule katika Daniel, wala wazo la Mtu yule katika Isaya, wala wazo la kutwaa mwili, wala hakuwa na wazo lingine zaidi ya wazo la mtoto wa Adamu aliyeuawa na ndugu yake akijitaja kama Yeye ambaye atauawa na Nduguze kwaajili ya ukombozi wa ulimwengu!

 

Wanatheolojia wengi wanamtumia Habil kama alama kivuli au unabii kuhusu Kristo na wanakubali kuwa kama Habili alivyouawa na ndugu yake na sababu kubwa ikiwa ni kwa sababu Habili alikuwa mwenye haki, kadhalika Kristo naye aliuawa na Ndugu zake wayahudi akiwa hana hatia, Mungu alimkabili Kaini akihoji Yuko wapi ndugu yako angalia

 

Mwanzo 4:10-11BWANA akamwambia Kaini, Yuko wapi Habili ndugu yako? Akasema, Sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?Akasema, Umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi.”

 

Damu ya habili ililia kwaajili ya kutaka kisasi au haki, lakini Damu yake Yesu inalia kwaajili ya rehema na msamaha na wokovu, Waebrania 12:24 “na Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili.”

 

Waefeso 1:6-7 “Na usifiwe utukufu wa neema yake, ambayo ametuneemesha katika huyo Mpendwa. Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake.”

 

Kwa msingi huo utakubaliana nami kuwa kama Yesu alivyokuwa akisisitiza ni kwa mauti ya namna gani atauawa na katika dhana hiyo hiyo Yesu alikuwa akijiita Mwana wa Adamu, ni kama Yesu alikuwa akitaka makutano waelewe kuwa YEYE NDIYE HABILI WA PILI, na kama vile kifo hakikuweza kunyamazisha uhai wa Habili, kifo vilevile kimeshindwa kunyamazisha uhai wa Yesu Kristo. Nasisistiza tena na tena Yesu alipokuwa akijiita mwana wa Adamu alikuwa akimuwaza Habili akilini mwaka na kile ambacho wakuu wa makuhani wangemfanyia na kazi ya ukombozi ambayo angeikamilisha kwamkifo chake, aidha masikitiko na maneno ya Adamu alipomzaa Sethi aliposema MUNGU AMENIWEKEA UZAO MWINGINE MAHALI PA HABILI katika mtazamo finyu mtoto huyo ni SETHI na katika mtazamo mpana mtoto huyo ni YESU KRISTO, mtoto wa tumaini la Adamu lililopotea.

 

                       

 

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

 

Mkuuu wa wajenzi mwenye Hekima

Hakuna maoni: