Jumapili, 26 Mei 2024

Katika mlima wa Bwana itapatikana!


Mwanzo 22:13-14 “Ibrahimu akainua macho yake, akaangalia, na tazama, kondoo mume yuko nyuma yake, amenaswa pembe zake katika kichaka. Basi Ibrahimu akaenda akamtwaa huyo kondoo, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe. Ibrahimu akapaita mahali hapo Yehova-yire, kama watu wasemavyo hata leo, Katika mlima wa BWANA itapatikana.”




Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu na kujikumbusha tena na tena ya kuwa Mungu wetu ni mwaminifu na anajishughulisha sana na maisha yetu katika namna ya kushangaza sana kiasi ambacho akili zetu haziwezi kuelewa wakati mwingine, jinsi Mungu alivyo mwema katika maisha yetu, Lakini ni ukweli ulio wazi kuwa Mungu anajishughulisha sana na mambo yetu, na yeye hutupatia mahitaji yetu ya kimwili na kiroho, zaidi ya yote ni Mwalimu mzuri sana wa neno lake kivitendo. Mungu anazo njia elfu nyingi za kututunza watu wake ambazo wala hatuzijui, Endapo tu tutaamua kujiachilia kwa Mungu kwa Imani bila shaka, utamuona Mungu kama Yehova Yire katika maisha yako na hutatikisika.

1Petro 5:6-7 “Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake; huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.”

Wengi wetu tuliookolewa wakati tunapopita majaribuni, huwa tunajawa na mashaka na kuanza kuumiza vichwa kuwa mambo yatakuwaje na tunashindwa kwa namna Fulani kumpa Mungu nafasi ya kutuhudumia kwa sababu tu ya mashaka yetu, ukweli ni kuwa tukishindwa kumwachia Mungu fadhaa zetu na tukajaribu kuzibeba wenyewe tutajikuta tunashindwa na tunazimia roho na tunaweza kukosa Amani ile ambayo Mungu ameikusudia kwetu

Leo tutachukua muda kujifunza kwa kina na mapana na marefu na kumwangalia Mungu wetu kama Jehovah Yire katika somo hili Katika mlima wa Bwana itapatikana! Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia mambo ya msingi yafuatayo:-


·         Ibrahimu katika kipimo cha juu kabisa cha Imani

·         Katika mlima wa Bwana itapatikana

·         Jinsi na namna bwana atakavyokupatia


Ibrahimu katika kipimo cha juu kabisa cha Imani

Moja ya eneo ambalo linathibitisha ukuaji wa Imani ya Ibrahimu ni mara baada ya kushinda kipimo hiki cha juu kabisa cha Imani, Mwanzo 22:1-3 “Ikawa baada ya mambo hayo Mungu alimjaribu Ibrahimu, akamwambia, Ee Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa. Akasema, Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia. Ibrahimu akaondoka alfajiri, akatandika punda wake, akachukua vijana wawili pamoja naye, na Isaka mwanawe, akachanja kuni kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa, akaondoka, akaenda mpaka mahali alipoambiwa na Mungu.”

Mungu alikuwa amemjaribu Ibrahimu kwa kiwango cha juu kabisa, tena katika namna ya kushangaza sana ambayo iko kinyume na akili za kawaida za kibinadamu, na tabia na upendo wa Mungu, na zaidi ya yote kama mzazi wa Isaka, lakini katika namna ya kushangaza sana Ibrahimu alikuwa tayari kumtii Mungu katika kipimo hiki akiwa na imani kali sana, kimsingi tunaweza kusema kuwa Ibrahimu aliwahi kupimwa na Mungu katika mazingira makubwa matatu

1.       Kuondoka katika nchi yake mwenyewe na kwenda asikojua  - hii ilitokea wakati Mungu aliposema na Ibrahimu kwa mara ya kwanza kabisa kuwa aondoke katika nchi yake na nchi ya baba zake na watu wake aende katika inchi atakayoonyeeshwa na kimsingi inchi hiyo pia alikuwa hajaijua na Mungu alikuwa hajamwambia kuwa ni wapi ona

 

Mwanzo 12:1-4 “BWANA akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha; nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka; nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa. Basi Abramu akaenda, kama BWANA alivyomwamuru; Lutu akaenda pamoja naye. Naye Abramu alikuwa mtu wa miaka sabini na mitano alipotoka Harani.”

 

Waebrania 11:8-9 “Kwa imani Ibrahimu alipoitwa aliitika, atoke aende mahali pale atakapopapata kuwa urithi; akatoka asijue aendako. Kwa imani alikaa ugenini katika ile nchi ya ahadi, kama katika nchi isiyo yake, akikaa katika hema pamoja na Isaka na Yakobo, warithi pamoja naye wa ahadi ile ile.”                

 

Katika kipimo hiki Ibrahimu alifanikiwa kwani alitii na kuondoka kwenda katika inchi aliyoahidiwa na Mungu ambayo kimsingi ilikuwa inchi ya mkanaani na Mungu alimthibitishia kuwa atampa inchi hiyo yeye na uzao wake

 

Mwanzo 17:1-9. “Abramu alipokuwa mtu wa miaka tisini na kenda, BWANA akamtokea Abramu, akamwambia, Mimi ni Mungu Mwenyezi, uende mbele yangu, ukawe mkamilifu. Nami nitafanya agano langu kati ya mimi na wewe, nami nitakuzidisha sana sana. Abramu akaanguka kifudifudi. Mungu akamwambia, akasema, Mimi, agano langu nimefanya nawe, nawe utakuwa baba wa mataifa mengi, wala jina lako hutaitwa tena Abramu, lakini jina lako litakuwa Ibrahimu, kwani nimekuweka uwe baba wa mataifa mengi. Nitakufanya uwe na uzao mwingi sana, nami nitakufanya kuwa mataifa, na wafalme watatoka kwako. Agano langu nitalifanya imara kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, na vizazi vyao, kuwa agano la milele, kwamba nitakuwa Mungu kwako na kwa uzao wako baada yako. Nami nitakupa wewe na uzao wako baada yako nchi hii unayoikaa ugeni, nchi yote ya Kanaani, kuwa milki ya milele; nami nitakuwa Mungu wao. Mungu akamwambia Ibrahimu, Nawe ulishike agano langu, wewe na uzao wako kwa vizazi vyao baada yako.”

 

2.       Jaribu la kuwa na subira -  Mungu alimuahidi Ibrahimu kuwa atampa uzao kupitia Sara mke wake wakati ahadi inatolewa Ibrahimu alikuwa na miaka 75 bila shaka Sara alikuwa na miaka 65 kwa sababu Ibrahimu na Sara walikuwa na tofauti ya miaka 10, Jaribu hili la kuwa na subira kwa kweli liliwashinda, hata na sisi tunashindwa mara nyingi sana katika eneo la kuwa na subira  wapi Mungu alimuahidi Ibrahimu mtoto ona

 

Mwanzo 18:10-13Akamwambia, Hakika nitakurudia wakati huu huu mwakani, na tazama, Sara mkeo atapata mwana wa kiume. Sara akasikia mlangoni pa hema iliyokuwapo nyuma yake. Basi Ibrahimu na Sara walikuwa wazee, na umri wao mkubwa, na Sara alikuwa amekoma katika desturi ya wanawake. Kwa hiyo Sara akacheka moyoni mwake, akisema, Niwapo mkongwe, nitapata furaha, na bwana wangu mzee? BWANA akamwambia Ibrahimu, Mbona Sara amecheka akisema, Mimi kweli nitazaa mwana, nami ni mzee?

 

Katika mtihani huu hata hivyo Sara na Ibrahimu walikosa uvumilivu, kutimia kwa ahadi hii ya Mungu kuligharimu miaka karibu 25 hivi kwa hiyo hapo katikati mambo yalikuwa tofauti na Sara alikata tamaa na Ibrahimu alikubaliana na kukata tamaa huko na wakajitafutia mtoto, kwa njia za kibinadamu na kitamaduni.

 

Mwanzo 16:1-4 “Basi Sarai mkewe Abramu hakumzalia mwana, naye alikuwa na mjakazi, Mmisri, jina lake Hajiri. Sarai akamwambia Abramu, Basi sasa, BWANA amenifunga tumbo nisizae, umwingilie mjakazi wangu labda nitapata uzao kwa yeye. Abramu akaisikiliza sauti ya Sarai. Sarai mkewe Abramu akamtwaa Hajiri Mmisri mjakazi wake, baada ya kukaa Abramu katika nchi ya Kanaani miaka kumi, akampa Abramu mumewe, awe mkewe. Basi akamwingilia Hajiri, naye akapata mimba. Naye alipoona ya kwamba amepata mimba, bibi yake alikuwa duni machoni pake.”

 

Pamoja na Sara na Ibrahimu kushindwa jaribu hili, utaweza kuona kwa kuwa Mungu ndiye aliyekuwa ameahidi, Mungu ni mwaminifu hata kama watu hawaamini yeye hubaki wa kuaminiwa 2Timotheo 2:12-13 “Kama tukistahimili, tutamiliki pamoja naye; Kama tukimkana yeye, yeye naye atatukana sisi; Kama sisi hatuamini, yeye hudumu wa kuaminiwa. Kwa maana hawezi kujikana mwenyewe.”

 

Mungu yeye aliitimiza ahadi yake na Sara na Ibrahimu walipata mtoto kama alivyosema Bwana, muda haukuwa kitu kwa Mungu lakini Muda ulisumbua wanadamu,  na unaendelea kuwasumbua wanadamu hata sasa, kwa kawaida ni ngumu kusubiri,  na kusubiri huwasumbua wanadamu

 

Mwanzo 21:1-5 BWANA akamjia Sara kama alivyonena, na BWANA akamfanyia kama alivyosema. Sara akapata mimba akamzalia Ibrahimu mwana wa kiume katika uzee wake, kwa muhula alioambiwa na Mungu. Ibrahimu akamwita jina lake Isaka, yule mwana aliyezaliwa, ambaye Sara alimzalia. Ibrahimu akamtahiri Isaka mwanawe, alipokuwa mwenye siku nane, kama Mungu alivyomwamuru. Naye Ibrahimu alikuwa mtu wa miaka mia, alipozaliwa mwana wake Isaka.”             

 

3.       Jaribu la kumtoa Isaka kama sadaka ya kuteketezwa – jaribu hili ndilo lilikuwa kipimo cha juu zaidi kwa Ibrahimu, lakini habari njema ni kuwa Ibrahimu sasa alikuwa amekuwa kiimani, sasa alijua ya kuwa Mungu akisema kitu amesema na hakuna ubabaishaji kwake, kwa hiyo Mungu aliposema naye kuhusu swala la kumtoa Isaka Imani ya Ibrahimu ilikuwa kubwa sana kwani licha ya kuwa mtihani huu ulikuwa mgumu sana kibinadamu lakini kwaajili ya uelewa wake, upendo wake na imani yake kwa Mungu. Ibrahimu alikuwa amefikia ngazi ya juu zaidi ya Imani ya kusema kuwa sasa yuko tayari kutii, huenda kushindwa kwake katika kusubiri kwa jaribu la pili kulikuwa kumemkomaza kuwa hataki tena kumkwaza Mungu kwa agizo lolote hivyo jamaa alitii ona:-

 

Mwanzo 22:1-3 “Ikawa baada ya mambo hayo Mungu alimjaribu Ibrahimu, akamwambia, Ee Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa. Akasema, Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia. Ibrahimu akaondoka alfajiri, akatandika punda wake, akachukua vijana wawili pamoja naye, na Isaka mwanawe, akachanja kuni kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa, akaondoka, akaenda mpaka mahali alipoambiwa na Mungu.”

 

Tukio la utii wa Ibrahimu mahali hapa lilimpa Ibrahimu kuwa mtu mwenye heshima zaidi miongoni mwa watu ambao wamewahi kupata kumuamini Mungu, Mungu aliapa kumbariki Abrahamu kwa sababu alikuwa amekuwa kiimani, kwani alionyesha kuwa anamwamini Mungu sio tu kwa kutii agizo hilo lakini Abrahamu aliamini ya kuwa huenda hata baada ya kufanya hivyo Mungu atamfufua mwanae Isaka kutoka kwa wafu.

 

Waebrania 11:17-19 “Kwa imani Ibrahimu alipojaribiwa, akamtoa Isaka awe dhabihu; na yeye aliyezipokea hizo ahadi alikuwa akimtoa mwanawe, mzaliwa pekee; naam, yeye aliyeambiwa, Katika Isaka uzao wako utaitwa, akihesabu ya kuwa Mungu aweza kumfufua hata kutoka kuzimu; akampata tena toka huko kwa mfano.”

 

Katika kuamini na kutii agizo hili au jaribio hili la tatu kuna matukio kadhaa ya kiimani yaliyoambatana na tukio hili, tukio hili lilileta Baraka kubwa sana kwa Ibrahimu, lakini pia lilileta Baraka kubwa sana kwa ulimwengu, Ibrahimu kama nabii, na mwanae Isaka kama nabii kimsingi walitabiri ujio wa Yesu Kristo, kinabii Ibrahimu akisimama kama Mungu na Isaka akisimama kama mwana wa Mungu (Yesu Kristo) na mlima ule Moria ukisimama kama Golgotha na kuni zile zikisimama kama msalaba, ambapo Isaka anabeba kuni zile ambazo angeenda kutolewa dhabihu juu yake ni picha ya Yesu Kristo akiwa amebeba msalaba wake ambapo alikwenda kusulubiwa juu ya msalaba ule kwaajili ya ulimwengu mzima, Pamoja na somo hilo zuri jambo lingine la msingi tunalojifunza hapa ni neno lile Katika mlima wa Bwana itapatikana nini hiyo hilo linatuleta katika kutafakari kipengele cha pili.

 

Katika mlima wa Bwana itapatikana!

 

Ibrahimu na Isaka wakiwa njiani kuna maswala ya Msingi ambayo yanatufundisha na kutufunulia tabia ya Mungu tunayemuabudu kuwa ni Mungu wa namna gani, kwanza inaonekana wazi kuwa tabia ya Ibrahimu kumuabudu Mungu lilikuwa ni jambo la kawaida na huenda alikuwa amemfundisha Isaka mara kadhaa namna na jinsi anavyoendesha ibada zake, kwa hiyo Isaka katika ujana wake alikuwa amekwisha kuelewa jinsi Mungu anavyopokea dhabihu na namna dhabihu ya kuteketezwa inavyotekelezwa, Kimsingi kuwa na moto, na kuni na kisu pekee na kuelekea katika eneo la kuabudu havikuwa na msingi kama hakuna mwana kondoo, Kwa hiyo Isaka katika akili zake alifikiri kuwa safari hii baba yake atakuwa amesahahu au amepuuzia jambo la Muhimu katika ibada hiyo ambayo kimsingi ni mwana kondoo na kukaa kimya kungeweza kuwafanya waende mbali zaidi huku akiwa au wakiwa hawana kondoo wa sadaka hivyo Isaka akauliza

 

Mwanzo 22:5-8 “Ibrahimu akawaambia vijana wake, Kaeni ninyi hapa pamoja na punda, na mimi na kijana tutakwenda kule, TUKAABUDU, NA KUWARUDIA TENA. Basi Ibrahimu akazitwaa kuni za hiyo sadaka, akamtwika Isaka mwanawe; akatwaa moto na kisu mkononi mwake, wakaenda wote wawili pamoja. Isaka akasema na Ibrahimu baba yake, akinena, Babangu! Naye akasema, Mimi hapa, mwanangu. Akasema, Tazama! Moto upo, na kuni zipo, lakini yuko wapi mwana-kondoo kwa sadaka ya kuteketezwa? Ibrahimu akasema, MUNGU ATAJIPATIA MWANA-KONDOO KWA HIYO SADAKA, mwanangu. Basi wakaendelea wote wawili pamoja.”

 

Kimsingi maneno haya ya Ibrahimu yenyewe yalikuwa yamejaa Imani kubwa na unabii mkubwa na wa ajabu, Ibrahimu alikuwa amewabakiza vijana wakae na punda na kuwapa maelekezo kuwa yeye na kijana yaani Isaka watakwenda kuabudu na kisha KUWARUDIA TENA, kwa hiyo Ibrahimu alikua na uhakika kuwa atarudi na Isaka kama anavyokwenda naye, lakini jambo la pili swali la Isaka kwa baba yake kuwa moto upo, na kuni zipo lakini mwana-kondoo kwa sadaka ya kutekeketezwa yuko wapi? Ibrahimu anamjibu Isaka kuwa MUNGU ATAJIPATIA  neno hili kwa kiebrania linasomeka kama “elohiym raah” au Yehoha Yire maana yake kwa kingereza God will Provide  au Kiswahili Mungu atajipatia au katika mlima wa bwana itapatikana, kwa hiyo Isaka anapouliza sadaka iko wapi Ibrahimu anajibu katika mlima wa Bwana itapatikana  neno hili lilikuwa na maana gani?

 

Maana kubwa na ya msingi ni kuwa Mungu mwenyewe ataleta mwana kondoo sahihi kwa sadaka ya dhambi itakayowakomboa wanadamu wote, Mungu alitimiza yeye mwenyewe kile ambacho alikuwa amemuagiza Ibrahimu akifanye, kwa hiyo ni kweli Mungu aliwapa mwana kondoo aliyekuwa amenasa pembe zake katika kichaka cha miiba ikiwa ni picha ya Kristo aliyevishwa taaji ya miiba wakati anasulubiwa msalabani pale Golgotha , kauli ya Ibrahim ilitimizwa na Mungu kwa wakati ule kwa kuwapa kondoo halisi, lakini kinabii kwa Mungu kumtoa mwanakondoo atakayechukua dhambi za ulimwengu yaani Yesu Kristo

 

Mwanzo 22:9-14 “Wakafika mahali pale alipoambiwa na Mungu, Ibrahimu akajenga madhabahu huko, akaziweka tayari kuni, kisha akamfunga Isaka mwanawe, akamweka juu ya madhabahu, juu ya zile kuni. Ibrahimu akanyosha mkono wake, akakitwaa kisu ili amchinje mwanawe. Ndipo malaika wa BWANA akamwita kutoka mbinguni, akasema, Ibrahimu! Ibrahimu! Naye akasema,Mimi hapa. Akasema, Usimnyoshee kijana mkono wako, wala usimtendee neno; kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee. Ibrahimu akainua macho yake, akaangalia, na tazama, kondoo mume yuko nyuma yake, amenaswa pembe zake katika kichaka. Basi Ibrahimu akaenda akamtwaa huyo kondoo, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe. Ibrahimu akapaita mahali hapo Yehova-yire, kama watu wasemavyo hata leo, Katika mlima wa BWANA itapatikana.”

 

Yohana 1:29-32 “Siku ya pili yake amwona Yesu anakuja kwake, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu! Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Yuaja mtu nyuma yangu, ambaye amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu. Wala mimi sikumjua; lakini kusudi adhihirishwe kwa Israeli ndiyo maana mimi nalikuja nikibatiza kwa maji. Tena Yohana akashuhudia akisema, Nimemwona Roho akishuka kama hua kutoka mbinguni; naye akakaa juu yake.”

 

Kwa hiyo kimsingi, Ibrahimu alikuwa ametabiri ya kuwa Mungu atatimiza mahitaji yetu yote ya ukombozi wa mwanadamu na kutupatia wokovu, Ibrahimu alikuwa ameonyesha wazi kuwa kutakuwa na ukomo kwa sadaka za kutetekezwa pale Mungu atakapokuja kumtoa mwana wake wa pekee ambaye ndiye Yesu aliyekufa msalabani na kutuletea wokovu.

 

Jambo lingine tunalijifunza kutoka katika neno Yehova Yire yaani katika mlima wa Bwana itapatikana ni kuwa Mungu anajihusisha na mahitaji yetu sio ya kiroho tu bali na ya mwilini, Yehova yire maana yake Mungu atatoa, kila wakati tunapokuwa na upungufu wa aina yoyote katika mahitaji yetu ya mwilini ni lazima kwetu kujishusha na kumuachia Mungu na kumtazama Mungu kwa Imani kuwa atajishughulisha na mahitaji yetu, tunapokuwa tumepungukiwa na kitu Mungu wetu alituahidi ya kuwa hatatupungukia wala hatatuacha, Mungu atatupima Imani yetu kwa kutupitisha jangwani, atatupima Imani yetu tunapokuwa hatuna kazi, atatupima Imani yetu tunapokuwa hatuna chakula, hatuna fedha za kulipa bili ya umeme,  au ya maji, au kodi ya nyumba, au nauli ya dala dala, na wakati mwingine hata sadaka ya kumtolea yeye, au tunadaiwa kila kona jiachilie katika Mungu mwamini Mungu ya kuwa atashughulika na mahitaji yako kwa sababu yeye ni Yehova yire na katika mlima wake itapatikana! Ikiwa tuna mahitaji yoyote ya kimwili na kiroho, tunahitaji uwepo wake, tunahitaji neema yake au huruma zake yeye yupo na tunapomwangalia yeye atatupatia hata baada ya kupitia njia ya mateso, hofu na mashaka yakuwa itajuwaje Yeye atatupa uwepo wake na nguvu zake zitadhihirika na sisi tutakuwa katika Imani kwa msaada wa Mungu wetu Haleluyaa!                          

Jinsi na namna Bwana atakavyokupatia

Inawezeakana unakutana na somo hili ukiwa huelewi kuwa utatoka vipi katika hali unayoipitia, hujui itakuwaje, huna wa kukutia moyo, kutokana na magumu unayokutana nayo, huna fedha, huna namna ya kujitibu, kihisia hakuko vema, umejawa na mashaka na wasiwasi, majaribu yamekuzunguka kila kona, ni kama umepoteza tumaini, unahangaika, hakuna anayekujali, kuna mambo chungu nzima yanasumbua kichwa chako, hujui kesho itakuwaje, ada ya watoto shule itakuwa vipi, wazazi wanaokutegemea utawatunza vipi, ndugu zako uliokuwa unawasaidia, utawasaidiaje, mbingu ni kama zimekuwa chuma na ardhi ni kama imekuwa shaba, shambani mambo yamekataa, miradi imegoma, mzunguko wa fedha ni kama hauko, biashara haziendi, unawaza hivi itapatikana? Ndoa itapatikana? Kazi itapatikana? Uamsho kanisani kwangu utapatikana? Mtoto atapatikana? Mavazi yatapatikana ?, washirika katika huduma yangu watapatikana? Sadaka katika wakati huu mgumu itapatikana?  Endapo unazungukwa na maswali mengi sana yanayofanana na hayo somo hili haliko mikononi mwako kwa bahati Mbaya Roho Mtakatifu alinitaka niliandae somo hili na aliniambia nilimalize mara moja, nilikuwa na masomo mengine naendelea nayo, lakini niliamuriwa niayaache nishughulike na hili kwaajili yako wewe unayesoma somo hili Bwana anakuambia leo katika mlima wa Bwana itapatikana na unaweza kuniuliza swali itapatikanaje? Kumbuka Ibrahimu hakuwa na mahali aliponukuu ahadi ya Mungu au neno la Mungu ya kuwa Mungu ni Yehova Yire wala hakuwa na mahali pameandikwa katika mlima wa bwana itapatikana lakini Isaka alipouliza, Ibrahimu alijibu moja kwa moja kama vile vile Mungu alivyomfanyia baadaye nasema katika mlima wa bwana itapatikana, itapatikanaje sisi tunazo ahadi za Mungu nyingi sana zinazoonyesha kuwa Mungu anashughulika na mahitaji yetu

a.       Anashughulika na mahitaji yetu ya mwilini – Mungu aliyetuumba anatujua sisi ni viumbe wake na alipotuumba aliandaa kila kitu kwaajili yetu, anawajibika kutulisha kama anavyolisha wanyama na ndege wa angani kwa hiyo Mungu wetu hashindwi kujitokeza katika mahitaji yetu yote na katika chakula

Wafilipi 4:19 “Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu.”

Luka 12:240-26 “Watafakarini kunguru, ya kwamba hawapandi wala hawavuni; hawana ghala wala uchaga, na Mungu huwalisha. Bora ninyi mara nyingi kuliko ndege! Na yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja? Basi, ikiwa hamwezi hata neno lililo dogo, kwa nini kujisumbua kwa ajili ya yale mengine?

Zaburi 145:14-16 “Bwana huwategemeza wote waangukao, Huwainua wote walioinama chini.Macho ya watu wote yakuelekea Wewe, Nawe huwapa chakula chao wakati wake. Waufumbua mkono wako, Wakishibisha kila kilicho hai matakwa yake.”

Zaburi 37:25 “Nalikuwa kijana nami sasa ni mzee, Lakini sijamwona mwenye haki ameachwa Wala mzao wake akiomba chakula.”

b.      Mungu atakupa pumziko – Yesu/Mungu ameahidi kutupa pumziko, najua unahangaika sana roho yako inatanga tanga, hata wale waliokutimua wanataka kujua itakuwaje, wanatamani kujua unaishije, wanataka kuona ukihangaika, wanatamani kuona ukienda kuwaomba na kuwakopa, au ukihangaika, moyo wako ni kama una hofu hivi lakini weka tumaini lako kwa Yesu nawe utapata Pumziko.

 

Mathayo 11:28-29 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;”

 

Zaburi 23:1-6 “Bwana ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu. Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, Kando ya maji ya utulivu huniongoza. Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami, Gongo lako na fimbo yako vyanifariji.Waandaa meza mbele yangu, Machoni pa watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, Na kikombe changu kinafurika. Hakika wema na fadhili zitanifuata Siku zote za maisha yangu; Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele.”

 

c.       Mungu atakupa muongozo - Ni kazi ya Mungu kutuongoza na kutusafishia njia kwaajili ya kusudi lake, wakati mwingine unapokuwa na mashaka kuhusu muelekeo unawaza itapatikana kweli? Kuna muelekeo kweli yuko anayetoa muelekeo na atakuongoza kwenye maji ya utulivu, kwa nini kwa sababu anatoa muongozo, watu wengine hawawezi kujua njia yetu kwa sababu wao sio Mungu, wanadamu wakiijua njia yako wanaweza kuiharibu lakini Mungu ndiye mwenye mwenendo na yeye ndiye njia.

 

Mithali 3:5-6 “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako.”

 

Mithali 20:24 “Mwenendo wa mtu watoka kwa Bwana; Basi, awezaje mtu kuelewa na njia yake?

 

Zaburi 37:5-6 “Umkabidhi Bwana njia yako, Pia umtumaini, naye atafanya. Ataitokeza haki yako kama nuru, Na hukumu yako kama adhuhuri

 

d.      Mungu atatuoa neema – Iko neema maalumu ambayo Mungu atatupa kwaajili ya kila aina ya mapito unayoyapitia, neema ya Mungu itatuisaidia, itatusaidia kuwasamehe waliotukosea, na kusahau yote, itatusaidia kufurahi katika mazingira ambayo tulitakiwa tuwe tunalia, itatusaidia kuwapa kipaumbele wenzetu katika ndoa, itatusaidia kuzitunza familia zetu, neema itarahisisha maisha na kutupa nguvu ya kusonga mbele katika namna ya kushangaza sana, neema ya Mungu hainunuliwi, neema ya Mungu haipatikani kwa kujipendekeza, neema ya Mungu inatolewa Bure na kutufaa wakati wa mahitaji, Yeye mwenyewe anatoa, Mungu mwenyewe atatupa neema ya kuitusaidia wakati wa mahitaji yetu!

 

Waebrania 4:15-6. “Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi. Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.”

 

2Wakorintho 9:8 “Na Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema;”

 

Shetani na maajenti wake na maadui wanaotutakia mabaya hawajui kuwa iko neema na rehema za kutusaidia wakati wa mahitaji yetu, Mungu hujalia neema hiyo, Paulo alipokuwa na uhitaji wa kile alichokiita mwiba katika maisha yake Mungu alimjibu kuwa neema inatosha, maana yake Mungu akitupa neema yake tunawezeshwa kustahimili yale yanayotusibu kwa Amani bila kukosana na Mungu wetu wala kuwaudhi watu omba neema ya Mungu siku zote katika maisha yako na utakuwa na Amani kwani neema yake itakubeba.

 

e.      Mungu atatupa njia ya kutokea – Ni Isaka aliyekuwa amefungwa mikono yake, ni Isaka aliyekuwa katika hatari ya kuchomwa kisu na baba yake, wakati anasumbuka yuko wapi mwana kondoo, ghafla anashangaa kumbe yeye ndiye anayefanywa kondoo siku ile? Najua umefanywa kondoo wa kafara mara kadhaa katika maisha yako, watu waliona wakutoe wewe, ili wapate nafuu, waliona ufukuzwe wewe, waliona wakusingizie wewe, waliona wakuharibie wewe lakini kama alivyosema Ibrahimu Katika mlima wa Mungu itapatikana maana yake Mungu atajipatia mwana kondoo, kwa kila jaribu unalolipitia bwana ataweka na mlango wa kutokea.

 

Mwanzo 22:9-13 “Wakafika mahali pale alipoambiwa na Mungu, Ibrahimu akajenga madhabahu huko, akaziweka tayari kuni, kisha akamfunga Isaka mwanawe, akamweka juu ya madhabahu, juu ya zile kuni. Ibrahimu akanyosha mkono wake, akakitwaa kisu ili amchinje mwanawe. Ndipo malaika wa BWANA akamwita kutoka mbinguni, akasema, Ibrahimu! Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa. Akasema, Usimnyoshee kijana mkono wako, wala usimtendee neno; kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee. Ibrahimu akainua macho yake, akaangalia, na tazama, kondoo mume yuko nyuma yake, amenaswa pembe zake katika kichaka. Basi Ibrahimu akaenda akamtwaa huyo kondoo, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe.”

 

1Wakorintho 10:13Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili.”

 

Mungu atatupatia njia ya kutoka au kulishinda jaribu linalotukumba, neema ya Mungu ilivyo njema tuna neno lake, tuna Roho wake tukisimama karibu naye na kuomba msaada wake nakuhakikishia tutaona njia mbadala.

 

f.        Mungu ataleta msaada wakati tunaumizwa au tunakaribia kuumizwa – wakati wote Mungu wetu hatakubali uonevu, na tunapoumizwa na yeyote yule hata awe mtu wa Mungu, hiyo haimaanishi kuwa Mungu hatashughulika na sisi, Yeye ni msaada uonekanao tele wakati wa mateso, wakati maumivu yanapokuwa magumu kubeba kumbuka tumkimbilie Mungu yeye sio Mungu aliye mbali, wakati Ibrahimu anakaribia kumuumiza Isaka Mungu alimtuma malaika wake mbingu ziliingilia kati.

 

Zaburi 46:1-3 “Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso.Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari. Maji yake yajapovuma na kuumuka, Ijapopepesuka milima kwa kiburi chake.”

 

Zaburi 34:17-19 “Walilia, naye Bwana akasikia, Akawaponya na taabu zao zote. Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo, Na waliopondeka roho huwaokoa. Mateso ya mwenye haki ni mengi, Lakini Bwana humponya nayo yote.”

 

Mwanzo 16:6-11. “Naye Abramu akamwambia Sarai, Tazama, mjakazi wako yu mkononi mwako, mtendee lililo jema machoni pako. Sarai akamtesa, naye akakimbia kutoka mbele yake. Malaika wa BWANA akamwona kwenye chemchemi ya maji katika jangwa, chemchemi iliyoko katika njia ya kuendea Shuri. Akamwambia, Hajiri, wewe mjakazi wa Sarai, unatoka wapi, nawe unakwenda wapi? Akanena, Nakimbia mimi kutoka mbele ya bibi yangu Sarai. Malaika wa BWANA akamwambia, Rudi kwa bibi yako, ukanyenyekee chini ya mikono yake. Malaika wa BWANA akamwambia, Hakika nitauzidisha uzao wako, wala hautahesabika kwa jinsi utakavyokuwa mwingi. Malaika wa BWANA akamwambia, Tazama! Wewe una mimba, utazaa mwana wa kiume, nawe utamwita jina lake Ishmaeli, maana BWANA amesikia kilio cha mateso yako.”        

 

g.       Mungu atakupa Amani – unaonaje katika jaribu lile la Ibrahimu kama angemuua mwanae? Hata kama Mungu angemfufua katika wafu, uhusiano wa mtoto na baba yake ungekuwa mashakani, kila mmoja angepoteza Amani, lakini njia ya Mungu katika mlima wake ilikuwa ya kupendeza sana walirudi kwa Amani,  Mungu hutupoa Amani katika mazingira yoyote yale, ataitunza mioyo yetu na akili zetu zisiumizwe vibaya, anatuleta katika Amani, anatoa Amani,

 

Wafilipi 4:6-7 “Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.”       

 

Warumi 5:1 “Basi tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na mwe na amani kwa Mungu, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa yeye tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo mnasimama ndani yake; na kufurahi katika tumaini la utukufu wa Mungu. Wala si hivyo tu, ila na mfurahi katika dhiki pia; mkijua ya kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta saburi; na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo; na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini; ”

 

h.      Mungu atakuokoa – unaweza kusema mbona nimeshaokoka lakini neno wokovu katika lugha ya kiyunani wanatumie neno Sōtēria ambalo lina maana pana zaidi ya kusamehewa dhambi au kuzaliwa mara ya pili, Soteria ni kuwekwa huru, kuokolewa hatarini, kulindwa na hatari, kwa hiyo wakati unapitia changamoto na majaribu ya aina mbalimbali kumbuka pia kuwa Mungu atakuokoa, kama alivyomuokoa Isaka au alivyomfufua Yesu baada ya kusulubiwa Msalabani akamuokoa na mauti basi Mungu atakuokoa na wewe katika mapito yako  na hatari zako zote na maumivu yako yote.

 

Zaburi 61:1-3 “Ee Mungu, ukisikie kilio changu, Uyasikilize maombi yangu. Toka mwisho wa nchi nitakulilia nikizimia moyo, Uniongoze juu ya mwamba nisioweza kuupanda. Kwa maana ulikuwa kimbilio langu, Ngome yenye nguvu adui asinipate.”

 

Zaburi 27:1-3 “Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, Nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani? Watenda mabaya waliponikaribia, Wanile nyama yangu, Watesi wangu na adui zangu, Walijikwaa wakaanguka. Jeshi lijapojipanga kupigana nami, Moyo wangu hautaogopa. Vita vijaponitokea, Hata hapo nitatumaini.”

Unaweza kuona Mungu ametuahidi katika neno lake kukutana na mahitaji yetu yote, wakati tunapopungukiwa anatukumbusha tu kuwa tumuamini yeye kwani Yeye kama YEHOVA YIRE  “God will provide” maana yake atakutana na mahitaji yetu na katika mlima wake itapatikana, Mungu atatoa msaada na atatupa njia na namna ya kujikwamua kutoka katika pito lako, haijalishi unapitia pito la namna gani,  fahamu tu ya kuwa Mungu amekwisha kutupa njia ya kufanya wakati wa mahitaji yetu ya kimiwli na kiroho, tunaweza kuwa na amani na utulivu tukijua ya kuwa KATIKA MLIMA WA BWANA ITAPATIKANA.

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!

Maoni 2 :

Bila jina alisema ...

Nampa sifa Mungu aliyekutumia kutupa chakula hiki,pili,nikupongeze kwa utii wako ktk kufikisha ujumbe huu. Binafsi nimepokea kwa nafasi yangu. Mungu akutunze.

Mkuu wa Wajenzi Mwenye Hekima alisema ...

Asante sana kwa mrejesho huu wa maoni yako, Naamini Mungu alikuwa na kusudi kubwa kwa watu wake kupitia somo hili, Neema ya Mungu itufunike sote kwaajili ya utukufu wake katika jina la Yesu, Amen