Matendo 10:38 “habari za Yesu wa Nazareti,
jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huko
na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana
Mungu alikuwa pamoja naye”
Utangulizi:
Leo ni siku ya Pentecost:
Pentecost ni siku ambayo wakristo duniani wanaadhimisha na kukumbuka siku ya
kushuka maalumu duniani kwa ROHO
MTAKATIFU na kuanza kufanya kazi
akiwa na mitume na wanafunzi wengine wa Yesu Kristo, tukio hilo maalumu
limeelezwa katika kitabu cha Matendo
Matendo 2:1-4 “Hata ilipotimia siku ya
Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi
kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa
wameketi. Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia
kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha
nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.”
Sikukuu ya Pentecost
iliadhimishwa siku ya 50 baada ya sikukuu ya Pasaka, Na neno hilo Pentecost limetokana
na neno la asili ya kigiriki Pentecost
ambalo maana yake ni 50, hata hivyo sikukuu ya Pentekoste ambayo huadhimishwa
siku 50 baada ya pasaka au jumapili saba baada ya pasaka kwa wayahudi sikukuu
hii huitwa SHAVUOT ambayo kimsingi ilikuwa sikukuu ya mavuno kwa
Wayahudi, Hata hivyo katika siku hiyo Mungu aliitumia kumuachilia Roho wake Mtakatifu
kuchukua nafasi na kuleta nguvu kwa wanafunzi wa Yesu ili waweze kuwa mashahidi
wake na kuihubiri injili ya utukufu wa Mungu duniani kwa gharama yoyote. Siku
hii huadhimishwa na njia mbalimbali na kwa hutuba mbalimbali, wengine wakiliita
juma la Roho Mtakatifu, na kadhalika, Hata hivyo kwa upande wangu Roho
Mtakatifu alinitaka niikumbushe jamii kuwa Roho Mtakatifu vile vile yuko
kwaajili ya kushughulika na uonevu wa kila aina duniani kupitia kanisa lake, maana
yake ni kuwa Roho Mtakatifu anapokuja juu ya watumishi wake na kuwapaka mafuta
ni Dhahiri kuwa anawataka watumishi wake wakashughulikie uonevu na kuwaweka
huru watu wake kutoka katika migandamizo ya aina mbalimbali kama vile
alivyoshuka juu ya Masihi.
Luka 4:17-19. “Akapewa chuo cha nabii
Isaya, akakifungua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa, Roho wa Bwana yu juu
yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma
kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha
huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.”
Kwa msingi huo leo tutachukua
muda kujifunza somo hili muhimu ROHO WA
BWANA NA NGUVU ZA UONEVU! na tutajifunza somo hili muhimu kwa kuzingatia
vipengele kadhaa vifuatavyo:-
·
Maana ya
neno uonevu
·
Jinsi Mungu anavyochukizwa na uonevu
·
Roho wa Bwana na nguvu za uonevu
Maana ya neno uonevu.
Matendo 10:38 “habari za Yesu wa Nazareti,
jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huko
na huko, akitenda kazi njema na KUPONYA WOTE WALIOONEWA na Ibilisi; kwa maana
Mungu alikuwa pamoja naye”
Ni muhimu kufahamu kuwa katika
Biblia ya kiingereza neno na KUPONYA
WOTE WALIOONEWA linasomeka and HEALING ALL THAT WERE OPPRESSED neno hilo walioonewa ambalo kwa
kiingereza oppressed katika maandiko
ya kiyunani linasomeka kama katadunasteuō
ambalo
kwa tafasiri ya kiingereza ni exericise
Dominion against, kwa Kiswahili kutawala kwa mabavu, au kuonea kwa nguvu,
kutawala kikatili, au Dhuluma. Ukatili huo unaweza kuhusisha kuchukua kitu
kwa nguvu, kutumikishwa kwa ujira mdogo, kutawaliwa kimabavu, kukandamizwa,
kudhulumiwa, kuteswa, kufanyishwa kazi kupita kawaida au zaidi ya muda wa
kawaida, kuwekwa katika hali ya kukosa maamuzi yako mwenyewe, kuwekwa chini ya
utawala wa taifa jingine, na kadhalika na kwa sababu hiyo mtu anayeonewa
anajisikia uonyonge, anaugua au kulia au kuomboleza, au kukata tamaa moyoni, au
kulalamika huku mtu huyo au watu hao wakiwa hawana msaada wa kujitoa katika
uonevu huo. Isipokuwa kwa msaada token je yake
Kwa hiyo mojawapo ya kazi za Roho
Mtakatifu ni pamoja na kuharibu nguvu za uonevu, kwa hiyo Mungu anapotaka kushughulika
na uonevu wakati wowote, lazima atamtumia mtu na kumpaka mafuta mtu huyo ili
aweze kushughulikia uonevuo huo, na ndio
maana Leo au katika sikukuu ya Pentekoste ya Mwaka huu tunataka kumwangalia
Roho Mtakatifu katika picha kukomesha uonevu!
Luka 4:17-19. “Akapewa chuo cha nabii
Isaya, akakifungua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa, Roho wa Bwana yu juu
yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma
kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, KUWAACHA
HURU WALIOSETWA, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.” Unaweza
kuona katika kifungu hiki pia
kiingereza cha ESV kinasomeka “to set liberty those who are oppressed”
Kwa hiyo bado tunapata picha kuwa
kusudi kuu la Roho Mtakatifu kuwapa nguvu watumishi wake kwa kuwapaka mafuta
kusudi kubwa ni kukomesha uonevu, Dunia imejawa na uonevu wa kila aina kutoka
kwa shetani na maajenti wake, na magonjwa ni sehemu ya uonevu huo, maendeleo ya
kisayansi na teknolojia hayatoshi peke yake kumuweka huru mwanadamu kutoka
katika uonevu huo, aidha nguvu za kipepo kila wakati zinawasukuma wanadamu
kufanya yale wasiyopenda kuyafanya hasa kuyafanya mapenzi ya Mungu, ili kwa njia hiyo shetani apate kibali cha
kuendelea kuwaonea watu na kuwakandamiza, ni makusudi basi Pentekoste hii
tukajikumbusha sio tu kule kujazwa na Roho Mtakatifu na nguvu zake na kufurahia
kunena kwa lugha lakini wakati huu, tukubali nguvu za Roho Mtakatifu
zituelekeze katika matumizi ya kushughulika na nguvu za uonevu, maana yake nini
kuelekeza nguvu zetu zote katika kufunguliwa kwa aina binadamu ambao wanaonewa
na ibilisi, hii ikienda sambaba na kazi ya kuihubiri injili.
Jinsi Mungu anavyochukizwa na uonevu
Neno la Mungu linatudhihirishia
kuwa Mungu anachukizwa sana na uonevu wa kila aina duniani, wakati Israel
wanateswa kule Misri na wakawa wanakandamizwa katika utumwa mzito kiasi cha
kulia Machozi, Mungu aliguswa na kuamua kushuka ili ashughulike na uonevu
uliokuwa unaendelea wamisri wakiwaonea wana wa Israel
Kutoka 3:7-9 “BWANA akasema, Hakika
nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa
sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao; nami nimeshuka ili
niwaokoe na mikono ya Wamisri, niwapandishe kutoka nchi ile, hata nchi njema,
kisha pana; nchi ijaayo maziwa na asali; hata mahali pa Mkanaani, na Mhiti, na
Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi. Basi, tazama, kilio cha wana wa
Israeli kimenifikilia; tena nimeyaona hayo mateso ambayo Wamisri wanawatesa.”
Kumbukumbu 26:6-9 “Wamisri wakatuonea,
wakatutesa, wakatutumikisha utumwa mzito. Tukamlilia Bwana, Mungu wa baba zetu;
Bwana akasikia sauti yetu, akaona na taabu yetu, na kazi yetu, na kuonewa
kwetu. Bwana akatutoa kutoka Misri kwa mkono wa nguvu, na kwa mkono
ulionyoshwa, na kwa utisho mwingi, na kwa ishara, na kwa maajabu; naye
ametuingiza mahali hapa, na kutupa nchi hii, nchi ijaayo maziwa na asali.”
Aidha kwa sababu Mungu
alichukizwa na uonevu waliotendewa wana wa Israel kule Misri, aliwaonya waache
kuonea watu hata wageni akiwakumbusha kuwa na wao walikuwa wageni katika inchi
ya Misri, Neno hili sio kwaajili ya Israel pekee leo, lakini linamuhusu kila
mmoja wetu kwamba kupitia kitabu hiki cha Musa (Torati) tunawekewa msingi wa
kutokuwaonea watu wengine na kutujulisha kuwa Mungu anachukizwa na uonevu na
wakati mwingine ataingilia kati kuhakikisha kuwa anawatoa watu wake kutoka
katika mateso na uonevu.
Kutoka 22:21-24 “Usimwonee mgeni, wala
kumtendea jeuri; kwa kuwa ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri. Usimtese
mjane ye yote aliyefiwa na mumewe, wala mtoto yatima. Ukiwatesa watu hao katika
neno lo lote, nao wakanililia mimi, hakika yangu nitasikia kilio chao, na
hasira yangu itawaka moto, nami nitawaua ninyi kwa upanga; na wake wenu
watakuwa wajane, na watoto wenu mayatima.”
Kutoka 23:9 “Usimwonee mgeni; maana, ninyi
mwajua moyo wa mgeni ulivyo, kwa kuwa ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri.”
Waamuzi 10:11-12 “Naye Bwana akawaambia
wana wa Israeli, Je! Sikuwaokoa ninyi na hao Wamisri, na Waamori, na wana wa
Amoni, na Wafilisti? Hao Wasidoni nao, na Waamaleki, na Wamaoni, waliwaonea,
nanyi mlinililia, nami niliwaokoa na mikono yao.”
Tumeona namna na jinsi ambavyo
Mungu anachukizwa na uonevu, uonevu katika mazingira mbalimbali na kila eneo,
iwe dhuluma, kuonea masikini, kunyanyasa wanyonge, kuwaonea wajane na yatima,
na kuwaonea wageni, na kadhalika haya yote Mungu ameayaamrisha katika neno lake
kuwa anachukizwa nayo, anachukizwa na ukoloni, anachukizwa na unyonyaji, anachukizwa
na biashara ya utumwa, na mtu mwenye nguvu kumuonea mnyonge na hata taifa moja
kulionea taifa lingine, Israel walipoonewa na wamisri, waamori, wana wa Amoni na
hata wafilisti na mataifa mengine Mungu alichukizwa na kuingilia kati kukomesha
uonevu huo, lakini sio hivyo tu Mungu vile vile anachukizwa na uonevu unaofanywa
na shetani na mapepo yake, na zaidi sana anachukizwa na uonevu wa magonjwa na
kadhalika sasa ni jinsi gani Mungu anajihusisha na kukomesha uonevu? Neno la Mungu linatuonyesha wazi kuwa kila
wakati Mungu alipotaka kukomesha uonevu aliliacha swala hilo Kwa Mungu Roho
Mtakatifu, na ndipo unapoweza kuona Roho wa Mungu akitoa nguvu ya kukomesha
uonevu. Roho Mtakatifu alishusha nguvu zake na kuchochea wivu kwa watumishi
wake na kuwataharakisha ili kuwakomboa watu wake, hii ni ishara ya wazi kuwa
Mungu hawezi kuvumilia dhuluma na uonevu.
Yeremiah 21:12 “Ee nyumba ya Daudi, Bwana
asema hivi, Hukumuni hukumu ya haki asubuhi, mkawaponye waliotekwa nyara na
mkono wake aliyewadhulumu, ghadhabu yangu isije ikatoka kama moto, ikaunguza,
asiweze mtu ye yote kuuzima, kwa sababu ya uovu wa matendo yenu.”
Roho wa Bwana na Nguvu ya
uonevu.
Kama jinsi ambavyo tumejifunza
tangu mwanzo ya kuwa Mungu anachukizwa na uonevu, na watu wake wanapougua na
kulia kwaajili ya uonevu wa aina yoyote Mungu alikuwa tayari kuwainua
wasaidizi, au watumishi wake au waamuzi ambao aliwapaka mafuta yaani aliwapa
nguvu za Roho wake Mtakatifu kwa kusudi la kuwaokoa na adui zao waliowaonea,
Mungu alifanya hivyo kila wakati, na kitabu cha waamuzi ni mojawapo ya mfano
mzuri wa utendaji wa Mungu dhidi ya uonevu
Waamuzi 2:18. “Na wakati Bwana
alipowainulia waamuzi, ndipo Bwana alikuwa pamoja na mwamuzi huyo, akawaokoa na
mikono ya adui zao siku zote za mwamuzi huyo; maana Bwana alighairi kwa ajili
ya kuugua kwao kwa sababu ya watu wale waliowaonea na kuwasumbua.”
Waamuzi walipoinuliwa na Mungu
waliweza kuwaokoa wana wa Israel kutoka katika mikono ya adui zao na kuwasababishia
Amani na utulivu, lakini waamuzi hao hawakuenda kwa nguvu zao wenyewe bali
wakati wote walipakwa mafuta na Roho Mtakatifu na kupewa nguvu ili kukomesha
nguvu ya uonevu, hata kama wakati mwingine uonevu huo ulisababishwa na makossa na
dhambi ya Israel wenyewe, lakini kila walipomlilia alinuka kuwasaidia
-
Wakati wa uonevu wa Kushanrishathaimu mfalme wa Mesopotamia aliwaonea Israel na kuwakandamiza katika
utumwa mzito na Israel wakawa watumwa wake kwa miaka nane mpaka walipolia na
kuugua mbele za Mungu, Na Mungu aliwainulia Mwamuzi aliyeitwa Othiniel ambaye
hakwenda vitani hivi hivi bali alijiwa na Roho wa Bwana ona:-
Waamuzi 3:7-11 “Wana
wa Israeli walifanya yaliyo maovu mbele za macho ya Bwana, nao wakamsahau
Bwana, Mungu wao, nao wakawatumikia Mabaali na Maashtorethi. Kwa hiyo hasira za
Bwana ziliwaka juu ya Israeli, naye akawauza na kuwatia mikononi mwa
Kushan-rishathaimu mfalme wa Mesopotamia; na wana wa Israeli wakamtumikia huyo
Kushan-rishathaimu muda wa miaka minane. Kisha wana wa Israeli walipomlingana
Bwana, Bwana akawainulia wana wa Israeli mwokozi, aliyewaokoa, yaani, Othnieli
mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa Kalebu. Roho ya Bwana ikamjilia juu yake, naye
akawa mwamuzi wa Israeli; akatoka kwenenda vitani, naye Bwana akamtia huyo
Kushan-rishathaimu, mfalme wa Mesopotamia, mkononi mwake; na mkono wake
ukamshinda Kushan-rishathaimu. Nayo nchi ikawa na amani muda wa miaka arobaini.
Kisha Othnieli, mwana wa Kenazi, akafa.”
-
Tunasoma tena namna na jinsi Israel walivyofanya
uovu na kutoa nafasi ya kuonewa tena walionewa sana na wamidiani na amaleki,
walikuwa hata wakilima wakati wa mavuno chakula kilichukuliwa, mifugo
ilichukuliwa hawakuwa na amani kiasi cha kuamua kuishi kwenye mashimo kwa
ujumla walifanyiwa mambo mabaya neno la Mungu linasema walitwezwa sana ! yaani
walionewa mno au walionewa kupita kiasi
Waamuzi 6:1-6 “Kisha
wana wa Israeli walifanya yaliyo maovu mbele za macho ya Bwana; Bwana akawatia
mikononi mwa Midiani muda wa miaka saba Mkono wa Midiani ulikuwa na nguvu juu
ya Israeli; tena kwa sababu ya Midiani wana wa Israeli walijifanyia hayo
mashimo yaliyo milimani, na hayo mapango, na hizo ngome. Basi ikawa, hapo
Israeli walipokuwa wamepanda mashamba, Wamidiani wakakwea, na Waamaleki, na hao
wana wa mashariki; wakakwea juu yao; wakapanga marago juu yao, na kuyaharibu
hayo maongeo ya nchi, hata ufikapo Gaza, wala hawakuacha katika Israeli riziki
ziwazo zote; kondoo, wala ng'ombe, wala punda. Kwa maana walikwea na ng'ombe
zao na hema zao, wakaja mfano wa nzige kwa wingi; wao na ngamia zao pia
walikuwa hawana hesabu; nao waliingia katika hiyo nchi ili kuiharibu. Israeli
walitwezwa sana kwa sababu ya Wamidiani; nao wana wa Israeli wakamlilia Bwana.”
Wamidiani
walifanya uonevu juu ya wana wa Israel kiasi cha kusikitisha sana mpaka wana wa
Israel walipomlilia Bwana ndipo Bwana alimpomuinua Gideoni na maandiko
yanaeleza ya kuwa Gideoni alijiliwa na Roho wa Bwana juu yake ambaye alimsaidia
kupanga vita na kuleta ushindi kwa askari wachache.
Waamuzi 6:33-34 “Wakati
huo Wamidiani na Waamaleki, na hao wana wa mashariki walikutana pamoja;
wakavuka na kupanga hema zao katika bonde la Yezreeli. Lakini roho ya Bwana ikaja
juu yake Gideoni; naye akapiga tarumbeta; na Abiezeri walikutanika na kumfuata.”
-
Wana wa Amoni waliwasumbua sana Israel waliwapiga
na kuwatawala kiasi ambacho wazee wa mji waliamua kwenda kumuomba Yeftha ili aje
awasaidie dhidi ya uonevu na taabu waliyokumbana nayo wakati huo kutoka kwa
wana wa Amoni angalia
Waamuzi 11:5-7 “Ikatukia,
hapo wana wa Amoni walipopigana na Israeli, wazee wa Gileadi wakaenda kumtwaa
huyo Yeftha katika ile nchi ya Tobu; wakamwambia Yeftha, Njoo wewe uwe kichwa
chetu, ili tupate kupigana na wana wa Amoni. Yeftha akawaambia wazee wa
Gileadi, Je! Ninyi hamkunichukia mimi na kunifukuza nitoke katika nyumba ya
baba yangu? Basi kwani kunijilia hivi sasa wakati mlio katika taabu? ”
Yeftha aliwezaje
kupambana na wana wa Amoni? Maandiko yanaeleza ya kuwa Roho wa Bwana alikuja
juu yake na ni Mungu aliyemwenzesha Yeftha, kushindana na mfalme wa wana wa
Amani na kuwashinda
Waamuzi 11:29-33 “Ndipo
roho ya Bwana ikamjilia juu yake Yeftha, naye akapita katika Gileadi na Manase,
akapita na katika Mispa ya Gileadi, na kutoka hapo Mispa ya Gileadi akapita
kuwaendea wana wa Amoni.Naye Yeftha akamwekea Bwana nadhiri, akasema, Kwamba
wewe utawatia wana wa Amoni mkononi mwangu kweli, ndipo itakuwa ya kwamba, kile
kitakachotoka katika milango ya nyumba yangu kunilaki, hapo nitakaporudi na
amani kutoka kwa hao wana wa Amoni, kitu hicho kitakuwa ni cha Bwana, nami
nitakisongeza kiwe sadaka ya kuteketezwa. Basi Yeftha akavuka kuwaendea wana wa
Amoni ili kupigana nao; naye Bwana akawaua mkononi mwake. Akawapiga kutoka
Aroeri hata kufikilia Minithi, miji ishirini, na mpaka Abel-keramimu, akawapiga
kwa machinjo makuu mno. Basi hivyo wana wa Amoni walishindwa mbele ya wana wa
Israeli.”
-
Wafilisti wakati wote wa maisha ya Samsoni
walikuwa waonevu dhidi ya Israel, lakini Mungu alimuinua Samsoni kama mwamuzi
ili kuwakomesha wafilisti ni namna gani uonevu huo ulikomesha ilikuwa kupitia
Roho Mtakatifu ambaye alimshughulisha Samsoni kwa nguvu angalia;-
Waamuzi 15:14-16 “Alipofika
Lehi, Wafilisti wakapiga kelele walipokutana naye; ndipo roho ya Bwana ikamjia
kwa nguvu, na zile kamba zilizokuwa juu ya mikono yake zikawa kama kitani
iliyoteketezwa kwa moto, na vile vifungo vyake vikaanguka mikononi mwake. Naye
akaona mfupa mbichi wa taya ya punda, akautwaa, akapiga watu elfu kwa mfupa
huo; Samsoni akasema, Kwa taya ya punda chungu juu ya chungu, Kwa taya ya punda
nimepiga watu elfu.”
Hitimisho:
Katika vifungu vyote hapo juu
somo kubwa tunalojifunza ni kuwa hakuna mahali unaweza kutatua changamoto za
uonevu wa aina yoyote ile bila Roho wa Bwana, Katika juma hili la Pentekoste
wengi wa wahubiri watafundisha na kukazia kuhusu ujazo wa Roho Mtakatifu,
watafundisha umuhimu wa nguvu za Roho Mtakatifu, wataombea watu wajazwe Roho
Mtakatifu, watafundisha umuhimu wa kunena kwa Lugha, watafundisha kuhusu
ubatizo wa Roho Mtakatifu, watafundisha kunena kwa lugha kama ishara ya ujazo
wa roho Mtakatifu, watafundisha mpaka karama za Roho, Watafundisha namna na
jinsi Roho wa Mungu anavyosaidia katika kuomba, kutia nguvu, kutupa ujasiri na
kadhalika na kadhalika hayo yote ni sawa na ni ya muhimu lakini Roho Mtakatifu
ni kwaajili ya nini, ni kwaajili ya kukomesha uonevu, Roho Mtakatifu alipokuwa
juu ya masihi Yaani Bwana Yesu tunaona wakati wote alishughulika na walioonewa,
Hata wafalme walipotawala Mungu
aliwapaka mafuta ili wakomeshe uonevu dhidi ya watu wake, kanisa katika wakati
huu halina budi kurudi kwenye msingi huu, tunamuhitaji Roho Mtakatifu na nguvu
zake ili tuwasaidie ndugu zetu kwa kuwatoa katika uonevu wa aina mbalimbali,
uonevu wa dhambi, uonevu wa ibilisi, uonevu wa magonjwa, na ana nyingine zote
za uonevu!
Luka 4:18-19 “Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta
kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa
kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka
wa Bwana uliokubaliwa.”
Matendo 10:38 “habari za Yesu wa Nazareti,
jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huko
na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana
Mungu alikuwa pamoja naye”
Kwa hiyo Roho Mtakatifu na nguvu
zake ni kwaajili ya kuwaokoa wote walioonewa na ibilisi, ni nguvu kwaajili ya
kufungua watu, ni nguvu za kuwapa watu ufahamu, kuwafanya vipofu kuona, ni
nguvu za kuwaacha huru waliotekwa, na waliosetwa yaani waliogandamizwa na nguvu
za giza, ni nguvu za kuutanganza mwaka
wa Bwana uliokubaliwa yaani ni wakati wa kuwaweka huru watu kutoka katika
vifungo mbalimbali, Mungu wetu kupitia Roho wake Mtakatifu ataachlia karama na
vipawa vikubwa na kuwezesha watu kufanya kazi yake kwa uhodari na kwa hekima na
maarifa na kwa kutenda kazi iliyo njema
ya kuwasaidia walioonewa
Na. Rev. Innocent Mkombozi Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni