Wafilipi 2:9-11 “Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina
lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya
mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa
YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba.”
Utangulizi:
Ni majira ambayo leo Wakristo
wote nchini wanaungana na wakristo wenzao ulimwengu kusheherekea sikukuu ya
kuzaliwa kwa masihi yaani “Chrismas”,
Ujio wa Masihi “Yesu Kristo” una
maana pana sana kwa mustakabali wa maisha ya mwanadamu, kuja kwa Yesu Kristo
duniani ni zawadi kubwa sana kwani ujio wake unaambatana na faida kubwa sana.
Isaya alitabiri kuwa ni zawadi ya mtoto wa kiume ambaye ndani yake kuna msaada
mkubwa sana wa uungu ambao una faida kubwa sana kwa maisha ya mwadamu.
Isaya 9:6-7 “Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto
mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa jina Lake,
Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani. Maongeo
ya enzi yake na amani Hayatakuwa na mwisho kamwe, Katika kiti cha enzi cha
Daudi na ufalme wake; Kuuthibitisha na kuutegemeza Kwa hukumu na kwa haki,
Tangu sasa na hata milele. Wivu wa Bwana wa majeshi ndio utakaotenda hayo.”
Moja ya zawadi kubwa
inayoambatana na ujio wa Masihi ni pamoja na kukirimiwa jina lile lipitalo
majina yote, jina ambalo lina faida kubwa sana katika maisha ya mwanadamu, na
hili ndilo ambalo tutalijadili katika siku hii ya leo, ili kujikumbusha Baraka
kubwa ambayo Mungu amewapa wanadamu kupitia Bwana Yesu lakini zaidi sana pia
kupitia jina lake Matendo 2:21 “Na itakuwa kila
atakayeliitia jina la Bwana ataokolewa.”
Warumi 10:11-13 “Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika. Kwa
maana hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote,
mwenye utajiri kwa wote wamwitao; kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana
ataokoka.”
Jina la Yesu lina umuhimu
kwaajili ya wokovu wetu, katika mazingira yote yanayohitaji msaada wa kiungu,
jina hili lina nguvu, lina uwezo wa kubadilisha maisha ya watu kwa vizazi
vyote, lina siri ya ajabu, lina uwezo wa kuvunja minyororo ya dhambi na
kutufungulia malango ya mbinguni, jina hili linatufunulia mamlaka kubwa ya kiungu
na kutuonyesha upendo mkubwa wa Mungu kwa wanadamu na kwa sababu hiyo katika
msimu huu wa sikukuu ya kuzaliwa kwa masihi sisi tutachukua muda kuangalia
umuhimu wa jina hili la Yesu, tutajifunza somo hili Amekirimiwa jina lile
lipitalo kila jina kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Umuhimu
wa jina katika neno la Mungu.
·
Siri
kubwa katika jina la Yesu.
·
Amekirimiwa
jina lile lipitalo kila jina.
Umuhimu wa jina katika neno la Mungu.
Ni muhimu kufahamu kuwa kwa
mujibu wa tamaduni za kibiblia, Majina hayakuwa yanatolewa kama jina tu, Majina
yalikuwa ni tangazo linaloendana na tabia na mwenendo wa muhusika, majina
yalikuwa ni picha halisi ya kinabii yenye kufunua kusudi la Mtu huyo kupewa
jina, aidha majina pia yalikuwa yanatabiri kilele cha maisha ya mtu husika na
wakati mwingine jina la mtu lilibadilishwa kwa kusudi la kubadilisha muelekeo
wa maisha ya mtu huyo kutoka katika lile kusudi la kwanza la kupewa jina hilo,
kwa mfano Mungu alipomuita Abrahamu, ambaye alikuwa anaitwa Abram alibadilisha
jina lake hilo kuwa Abrahamu, Abram ikiwa na maana ya baba aliyeinuliwa, au
mwana wa mfalme, na Abraham ikiwa na maana ya Baba wa Mataifa, au baba wa
wafalme wengi, kwa hiyo Mungu alibadili jina la mwana wa mfalme, kuwa baba wa
wafalme, Mungu alimpa jina linaloonyesha kuwa mwana mfalme huyu atakuwa ni baba
wa wafalme wengi sana maarufu Duniani, Hali kadhalika Mungu alibadili jina la
Sarai kuwa Sara.
Mwanzo 17:1-6 “Abramu alipokuwa mtu wa miaka tisini na kenda, BWANA
akamtokea Abramu, akamwambia, Mimi ni Mungu Mwenyezi, uende mbele yangu, ukawe
mkamilifu. Nami nitafanya agano langu kati ya mimi na wewe, nami nitakuzidisha
sana sana. Abramu akaanguka kifudifudi. Mungu akamwambia, akasema, Mimi, agano
langu nimefanya nawe, nawe utakuwa baba wa mataifa mengi, wala jina lako hutaitwa
tena Abramu, lakini jina lako litakuwa Ibrahimu, kwani nimekuweka uwe baba wa
mataifa mengi. Nitakufanya uwe na uzao mwingi sana, nami nitakufanya kuwa
mataifa, na wafalme watatoka kwako.”
Mwanzo 17:15-16 “Mungu akamwambia Ibrahimu, Sarai mkeo, hutamwita jina lake
Sarai, kwa kuwa jina lake litakuwa Sara.Nami nitambariki, na tena nitakupa
mwana kwake, naam, nitambariki, naye atakuwa mama wa mataifa, na wafalme wa
kabila za watu watatoka kwake.”
Mungu alibadilisha jina la Abramu
kuwa Abrahamu kwa sababu Mungu alikusudia kubadilisha mustakabali wa maisha ya
Abrahamu na kumfanya kubwa Baraka kubwa kwa dunia ili kwamba kuputia yeye
mataifa yote yaweze kubarikiwa, na kama mtu atakuwa kinyume na Abrahamu
angeweza kumlaani naye angelaaniwa, kwa hiyo unaweza kuona jinsi maisha ya
Abrahamu yalivyogeuzwa na Mungu kuwa maisha ambayo yanaweza kumgusa kila mtu
duniani
Mwanzo 12:1-3 “BWANA akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na
jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha; nami
nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe
uwe baraka; nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na
katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa.”
Unaweza kuona, katika mpango huo
huo wa kuleta Baraka kwa Dunia nzima Mungu alilazimika kubadili jina la Yakobo
mjukuu wa Abrahamu kuwa Israel, ili kubadilisha mustakabali wa maisha ya Yakobo
na kumbadilisha kuwa kitu kingine
Mwanzo 32:26-28 “Akasema, Niache, niende, maana kunapambazuka. Akasema,
Sikuachi, usiponibariki. Akamwuliza, Jina lako n'nani? Akasema, Yakobo.
Akamwambia, Jina lako hutaitwa tena Yakobo, ila Israeli, maana umeshindana na
Mungu, na watu, nawe umeshinda.”
Kwa msingi huo utakubaliana nami
kuwa ni ukweli usiopingika kimaandiko kuwa majina yalihusika kwa sehemu kubwa
kuhusisha uweza wa Mtu tabia na mustakabali wa maisha yajayo, kwa hiyo kila
mkristo anapaswa kukumbuka jambo hili kwamba tuwape watoto wetu majina mazuri
kwaajili ya mustakabali mwema wa maisha yao ya baadaye na kamwe tusiruhusu
wakawa na majina yenye kuwakilisha uchungu, au machungu ya maisha, hasa kama
watoto hao hawahusiki na hilo walilolipitia wazazi, kwa mfano wakati Benjamin anazaliwa mama yake akiwa
katika hali ya kufa alimpa jina Benon
akiwakilisha mwana wa uchungu wake, lakini Yakobo alilibadilisha jina hilo mara
moja jina likimaanisha mwana wa mkono
wake wa kuume ona:-
Mwanzo 35;16-18 “Wakasafiri kutoka Betheli, hata ukabaki mwendo wa kitambo
tu kufika Efrathi, Raheli akashikwa na utungu wa kuzaa, na utungu wake ulikuwa
mzito. Ikawa alipokuwa anashikwa sana na utungu, mzalisha akamwambia, Usiogope,
maana sasa utamzaa mwanamume mwingine. Ikawa hapo katika kutoa roho yake, maana
alikufa, akamwita jina lake Benoni, lakini babaye alimwita Benyamini.”
Katika hali kama hiyo majina ya
Mungu katika maandiko yanafunua asili, tabia na uhusiano ulioko kati ya Mungu
na wanadamu, Mfano mtu alipofadhiliwa na Mungu alimwita Mungu wa fadhili zangu
Yehovah Yire, au mtu alipohakikishiwa Amani na Mungu alimuita Yehovah Shalom
akikubali Amani ya Mungu, majina hayo sio tu yanamfunua Mungu bali yanatukaribisha
kwake yakituonyesha kuwa Mungu anaweza kujitokeza kwetu pia sawasawa na
mahitaji yetu, sasa jina la Yesu linafunua ufunuo mkamilifu wa Mungu kwa
mahitaji yetu yote wanadamu kutokea upande wowote wa kiroho, nafsi, na mwili na
kutufundisha au kutufunulia ukamilifu wote wa Mungu na kusudi lake kwa wanadamu.
Siri kubwa katika jina la Yesu.
Sasa tunapokuja kuangalia kuhusu
jina la Yesu, utaweza kuona kuwa jina hili lilitangulia kutolewa kama zawadi
kwa wanadamu wakati wa maandalizi ya kuzaliwa kwake yeye mwenyewe, jina hili
lilikuja kama habari njema kwa Yusufu kuwajulisha watu wote Duniani kuwa mtoto
huyu mwanaume ambaye tumepewa kama zawadi ukiacha shughuli zote za ukombozi na
mafundisho yake yote jina lake tu ni msaada tosha kwa wanadamu na jina hili
lilikuja vilevile wakati wa kuzaliwa kwake, kwa hiyo mojawapo ya zawadi kubwa
kabisa katika siku za kuzaliwa kwa Masihi ni pamoja na jina lake ambalo ni jina
lipitalo majina yote.
Mathayo 1:20-25 “Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa Bwana
alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua
Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye atazaa
mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake
na dhambi zao. Hayo yote yamekuwa, ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa
ujumbe wa nabii akisema, Tazama, bikira atachukua mimba, Naye atazaa mwana; Nao
watamwita jina lake Imanueli; Yaani, Mungu pamoja nasi. Naye Yusufu alipoamka
katika usingizi, alifanya kama malaika wa Bwana alivyomwagiza; akamchukua
mkewe; asimjue kamwe hata alipomzaa mwanawe; akamwita jina lake YESU.”
Jina Yesu kwaasili limetokana na
jina “JESUS” la kiingereza ambalo
lina mzizi mkuu kutoka katika lugha ya kilatini, na kwa kiyunani, “IESOUS” ambalo asili yake ni jina la
kiibrania “yehōshua”
YEHOSHUA au JOSHUA ambalo maana yake ni “MUNGU
MWOKOZI” jina la Yesu lina maana pana katika kiibrania zinazojumuisha
Yeshua – yaani Mwokozi
Yoshua – yaani muunganiko wa maneno makuu mawili
·
Yah –
ambalo ni kifupi cha neno la kiibrania ambalo lilikuwa katika mfumo wa herufi
zisizo na silabii yaani Tetragrammaton
zijulikanazo kama YHWH au YAHWEH
·
Yasha
– ambalo maana yake wokovu au ukombozi Kwa hiyo jina la Yesu maana yake Yohova ni mwokozi, kwa hiyo unapolitaja jina hili unaita mamlaka
yote ya kiungu kwaajili ya kuleta msaada wa kiungu kokote uliko iwe ni
mbinguni, duniani au kuzimu jina hili lina nguvu na mamlaka kubwa ya kusababisha
ukombozi katika eneo husika, Mungu mwenyewe anashuka katika historia ya
mwanadamu na kuukomboa uumbaji wake
Kwa hiyo jina la Yesu, linatimiza
uhitaji mzima wa ukombozi wa mwanadamu ulioahidiwa katika agano la kale, kama
Yoshua aliwaingiza wana wa Israel katika inchi ya mkanaani basi Yesu
anawaingiza wanadamu wote duniani wamwaminio katika pumziko la uzima wa milele,
kwa hiyo jina hili sio tu linawaokoa wanadamu na dhambi zao, bali pia na
madhara ya dhambi, magonjwa na utumwa wa kila namna ambao wanadamu
wanatumikishwa na zaidi ya yote kumkomboa mwanadamu na mauti ya milele, jina
hili ni zaidi ya kazi za ukombozi, ni jina linaloachilia mamlaka ya kimbingu
kushuka na kushughulika na mahitaji ya wanadamu duniani.
Luka 2:9-11 “Na katika nchi ile ile walikuwako wachungaji wakikaa
makondeni na kulinda kundi lao kwa zamu usiku.Malaika wa Bwana akawatokea
ghafula, utukufu wa Bwana ukawang'aria pande zote, wakaingiwa na hofu kuu.
Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha
kuu itakayokuwa kwa watu wote; maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa
ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana.”
Jina la Yesu haliondoi majina
majina ya Mungu yaliyotumiwa wakati wa agano la kale lakini linayatimiza,
wakati wa agano la kale Mungu alijifunua kidogo kidogo kwa vipande vipande
kupitia jina lake mfano Yehova Rapha ilimaanisha, wokovu katika uponyaji, na
Yehova Nisi ilimaanisha wokovu katika vita hivi vilikuwa ni vipande vipande vya
ukombozi ambapo Mungu alijifunua kwa sehemu tu kulingana na uhitaji wa mtu kwa
wakati huo, kwa hiyo ufunuo kuhusu jina la Mungu ulikuwa ni kwa sehemu, sivyo
ilivyo katika jina la Yesu, hili linafunua wokovu kamili, ni kifurushi kamili
chenye kujitosheleza katika nyanja zote, kama muumba, asili yake, wajibu wake
kwa viumbe wake, na kadhalika kwa hiyo Yesu ni ufunuo kamili wa Mungu.
Waebrania 1:1-4 “Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii
kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi
katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya
ulimwengu. Yeye kwa kuwa ni mng'ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake,
akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi,
aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu; amefanyika bora kupita malaika, kwa
kadiri jina alilolirithi lilivyo tukufu kuliko lao.”
Isaya 45:22-23 “Niangalieni mimi, mkaokolewe, enyi ncha zote za dunia;
maana mimi ni Mungu; hapana mwingine.Kwa nafsi yangu nimeapa, neno hili
limetoka kinywani mwangu katika haki, wala halitarudi, ya kwamba mbele zangu
kila goti litapigwa, kila ulimi utaapa.”
Wafilipi 2:9-11 “Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina
lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya
mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa
YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba.”
Kwa msingi huo kila unabii katika
Mungu uliotabiriwa katika agano la kale umekuja kutimizwa katika agano jipya
kupitia jina la Yesu na kwa sababu hiyo tena hatuna jina lingine litupasalo
sisi kuokolewa kwalo isipokuwa jina la Yesu tu,
Matendo 4:10-12 “jueni ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya kuwa kwa jina
la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha, na Mungu akamfufua
katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu. Yeye ndiye
jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu la
pembeni.Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina
jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.”
Amekirimiwa jina lile lipitalo kila jina
Wafilipi 2:9-11 “Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, AKAMKIRIMIA JINA
LILE LIPITALO KILA JINA; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya
mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa
YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba.”
Yesu Kristo sasa ni jina lipitalo majina yote kwa vitu
vyote vya mbinguni na vya duniani na kuzimu neno LIPITALO katika kiyunani linatumika neno HUPER kimatamshi Hoo-per,
huupa ambalo tafasiri yake kwa kiingereza ni Beyond across, Superior to more than, above, very chiefest, Exceeding,
highly more than, very highly, jina lililo juu zaidi ya kawaida, Bora
kupita yote, liko juu, la juu zaidi, limepitiliza kuliko kawaida, liko juu mno,
Kwa hiyo nguvu iliyokuwa ikifunuliwa kupitia jina Yehova au Yahweh sasa inakaa
katika Yesu kwa ukamilifu wake wote, bila kupuuzia majina ya agano la kale
kuhusu Mungu, jina la Yesu sasa linabeba ufunuo mkamilifu wa mamlaka ya kiungu
na wokovu wa mwanadamu kwahiyo ni kusema ukitoa pepo kwa jina la YEHOVA halitatoka lakini ukitoa kwa
jina la Yesu litaondoka, jina hili hata shetani analijua, matumizi sahihi ya
jina hili huwakilisha Serikali, ufalme, dola, mamlaka na utawala na hivyo Pepo wakilisikia lazima wakimbie. Ni
Mungu mwenyewe ambaye amempa Yesu jina hili na ametaka alitambulishe kwa
wanadamu kwaajili ya kuwasaidia
Yohana 17:11-12 “Wala mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo
ulimwenguni, nami naja kwako. Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde
hawa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo. Nilipokuwapo pamoja nao, mimi
naliwalinda kwa jina lako ulilonipa, nikawatunza; wala hapana mmojawapo wao
aliyepotea, ila yule mwana wa upotevu, ili andiko litimie.”
Jina la Yesu likitumika katika
matamshi yoyote yawe ya Kiswahili, kiebrania, au kiyunani na kingereza nguvu
yake inabakia vilevile halichuji endapo tu utamaanisha Yesu huyu wa Nazareth tunayehubiri
habari zake jina hili lina nguvu, lina mamlaka, uwezo wa kuokoa na kufanya
mambo makubwa unapoliitia maana yake unaiita serikali ya mbinguni kutoa msaada
katika eneo husika
Jina hili linaokoa - Matendo 2:21 “Na itakuwa kila atakayeliitia jina
la Bwana ataokolewa.”
Jina hili kanisa limeamriwa kuliamini – 1Yohana 3:23 “Na hii ndiyo
amri yake, kwamba tuliamini jina la Mwana wake Yesu Kristo, na kupendana sisi
kwa sisi, kama alivyotupa amri.”
Jina hili lina mamlaka ya kuamuru lolote - Marko 16:17-18 “Na ishara hizi
zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha
mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa;
wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.”
Jina hili huitiwa na makanisa yote ya kweli – 1Wakorintho 1:2 “Na hii ndiyo
amri yake, kwamba tuliamini jina la Mwana wake Yesu Kristo, na kupendana sisi
kwa sisi, kama alivyotupa amri.”
Jina hili lilitumiwa na mitume kuponya na kufanya miujiza mbalimbali.
Matendo 3:6, “Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini
nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama
uende.”
Matendo 4:10 “jueni ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya kuwa kwa jina
la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha, na Mungu akamfufua
katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu.”
Jina hili mitume na kanisa la kwanza walilitumia katika kuhubiri
Matendo 8:12 “Lakini walipomwamini Filipo, akizihubiri habari njema za
ufalme wa Mungu, na jina lake Yesu Kristo, wakabatizwa, wanaume na wanawake.”
Matendo 9:27-29 “Lakini Barnaba akamtwaa, akampeleka kwa mitume, akawaeleza
jinsi alivyomwona Bwana njiani, na ya kwamba alisema naye, na jinsi
alivyohubiri kwa ushujaa katika Dameski kwa jina la Yesu. Naye akawa pamoja nao
katika Yerusalemu akiingia na kutoka. Akahubiri kwa jina la Bwana kwa ushujaa,
akinena na kuhojiana na Wayahudi wa Kiyunani. Nao wakajaribu kumwua.”
Jina hili ni ulinzi na kimbilio – Mithali 18:10 “Jina la Bwana
ni ngome imara; Mwenye haki huikimbilia, akawa salama.”
Jina hili lilitumiwa na mitume kufukuza pepo wabaya.
Matendo 16:18 “Akafanya hayo siku nyingi. Lakini Paulo akasikitika,
akageuka akamwambia yule pepo, Nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu.
Akamtoka saa ile ile.”
Jina hili lilaleta Amani – Yohana 16:23-24 “Tena hsiku ile hamtaniuliza neno lo
lote. Amin, amin, nawaambia, Mkimwomba Baba neno lo lote atawapa kwa jina
langu.Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu; ombeni, nanyi mtapata; furaha
yenu iwe timilifu.”
Jina hili ni kibali cha kujibiwa maombi – Yohana 14:13-15 “Nanyi mkiomba
lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana.
Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.”
Jina hili Mitume walikuwa tayari hata kulifia
Matendo 15:25-26 “sisi tumeona vema, hali tumepatana kwa moyo mmoja,
kuwachagua watu na kuwapeleka kwenu pamoja na wapendwa wetu Barnaba na Paulo,
watu waliohatirisha maisha yao kwa ajili ya jina la Bwana wetu Yesu Kristo.”
Matendo 21:12-13 “Basi
tuliposikia haya, sisi na watu wa mahali pale, tukamsihi asipande kwenda
Yerusalemu.Ndipo Paulo alipojibu, Mnafanya nini, kulia na kunivunja moyo? Kwa
maana mimi, licha ya kufungwa, ni tayari hata kuuawa katika Yerusalemu kwa
ajili ya jina lake Bwana Yesu.”
Jina hili linavuta uwepo wa Mungu – Mathayo 18:19-20 “Tena nawaambia,
ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lo lote
watakaloliomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni.Kwa kuwa walipo wawili
watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao.”
Kwa hiyo watu wa Mungu tuna
wajibu wa kulitumia jina la Yesu katika jambo lolote, najua yako mafundisho
mengi duniani hata yale yanayofundisha watu kutumia damu ya Yesu na kuinyunyiza
kwa Imani, maandiko yameelekeza katika changamoto yoyote ile tutumie jina la
Yesu, Shetani asikudanganye kutumia kingine tumia jina la Yesu moja kwa moja,
maandiko yametuagiza kulitumia katika maombi, kulitumia kwaajili ya uponyaji,
kulitumia katika vita vya kiroho, na kulitumia katika kuabudu, tumeagizwa ya
kuwa lolote tulifanyalo kwa neno au kwa tendo tulifanye kwa jina la Yesu,
tunapoliitia jina hili utendaji wa serikali ya mbinguni unahamia pale jina hili
linapotajwa na kutimiliza matakwa yetu kwa utukufu wa Mungu, wajibu wetu ni
kulitumia jina la Yesu kwa Imani, kwa heshima, kwa kulitumainia na kulitegemea,
kwa kulitangaza kwa ujasiri, na kuishi sawasawa na heshima ya jina hilo, kwani
jina hili ndio ufunuo mkamilifu wa upendo na wokovu wa mwanadamu kutoka kwa
Mungu, jina hili lilifichwa nyakati za agano la kale na kufunuliwa kwetu wa
kizazi hiki katika wakati huu wa neema hivyo ni zawadi ya kipekee ambayo hatuna
budi kuitumia kwa mustakabali wa maisha yetu, unapoadhimisha kuzaliwa kwa Yesu
Kristo basi kumbuka tumepewa jina kuu kuliko yote! Na ingawa amekirimiwa jina
hili, kimsingi tumekarimiwa sisi kwa matumizi yake, kwa changamoto zozote zile
unazokutana nazo katika maisha liitie jina la Yesu na utayafurahia maisha, omba
kwa jina la Yesu, kemea kwa jina la Yesu, Amini
na ishi kwa kulitegemea jina la
Yesu.
Wakolosai 3:16-17. “Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima
yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku
mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu. Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa
tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye.”
Maadui wa Yesu Kristo akiwepo
shetani wakati wote hawatataka kulisikia jina hili likitumika na wakati wote
watalikataa kama wanavyomkataa, Yesu Kristo mwenyewe, Shetani anatamani sana
kama ikiwezekana jina hili lisiwepo au litumike lingine kwa sababu anaijua
nguvu iliyomo katika jina hili. Nakusihi sana wakati huu tunapoadhimisha
kuzaliwa kwa Yesu Kristo kumbuka kuwa Mungu ametukirimia sio zawadi tu ya
maisha yake ya ukombozi kwa wanadamu lakini ametukirimia pia jina hili zuri
ambalo tunaweza kulitumia kwa mustakabali wa maisha yetu. Lakini hata manabii
wa uongo watalitumia jina hili kwa kusudi la kuwadanganya wateule hivyo hatuna
budi kuwa makini, si kila anayelitumia atakuwa ni mtu mzuri au mtu sahihi.
Mathayo 7:21 “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika
ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.”
Matendo 4:18 “Wakawaita,
wakawaamuru wasiseme kabisa wala kufundisha kwa jina la Yesu.”
Matendo 5:40-42 “Wakakubali maneno yake; nao walipowaita mitume, wakawapiga, wakawaamuru wasinene kwa jina lake Yesu; kisha wakawaacha waende zao. Nao wakatoka katika ile baraza, wakifurahi kwa sababu wamehesabiwa kuwa wamestahili kuaibishwa kwa ajili ya Jina hilo.Na kila siku, ndani ya hekalu na nyumbani mwao, hawakuacha kufundisha na kuhubiri habari njema za Yesu kwamba ni Kristo.”
Na. Rev. Mkombozi Samuel Kamote
Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni