Luka 1:31-35 “Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina
lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana
Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo
hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho. Mariamu akamwambia malaika,
Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu
atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa
sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu.”
Utangulizi
Ni muhimu kufahamu kuwa Neno la
Mungu katika agano jipya limeonyesha wazi namna na jinsi Roho Mtakatifu
akihusika kwa kiwango kikubwa sana katika mpango mzima wa kuzaliwa kwa Yesu
Kristo, jambo ambalo linatupa kutafakari sana na kupata ufahamu kuwa huwezi
kutenganisha habari nzima inayohusiana na kuzaliwa kwa Yesu Kristo na utendaji
wa Roho Mtakatifu, Kuzaliwa kwa Yesu Kristo ni mojawapo ya muujiza mkubwa sana
ambao unapita akili ya kawaida na utendaji mzima wa ufahamu wa kibinadamu, na
Ndio maana hata kitendo cha Mariamu kuwa mjamzito bila tukio la mwanaume
kuhusika Malaika alifafanua wazi kuwa ingewezekana kwa uweza wa Roho Mtakatifu,
hii maana yake ni kuwa kulikuwa na utendaji wa kiungu uliokuwa unahusika moja
kwa moja katika kumleta masihi Duniani. kwa hiyo tunaposheherekea wakati wa
kuzaliwa kwa masihi tusimsahau ROHO MTAKATIFU.
Mathayo 1:18-21 “Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama yake
alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba KWA
UWEZA WA ROHO MTAKATIFU. Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki,
asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri. Basi alipokuwa akifikiri hayo,
tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa
Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni KWA UWEZA WA ROHO
MTAKATIFU. Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye
atakayewaokoa watu wake na dhambi zao.”
Hii maana yake ni nini? mpango
mzima wa ukombozi wa Mwanadamu ni muujiza ambao umeratibiwa na Roho Mtakatifu
kwa muujiza mkubwa sana. Roho Mtakatifu ni wa muhimu mno na anahusika kwa namna
ya kipekee katika kazi ya ukombozi wa mwanadamu kwa sababu hata kuzaliwa kwa
Mkombozi mwenyewe tunamuona Roho wa Mungu akihusika katika muujiza huu mkubwa
wa kuunganisha kazi za uungu na ukombozi wa Mwanadamu, kwa muujiza mkubwa wa
Mungu kufanyika mwanadamu, au mwana wa Mungu kuwa mwana wa mwanadamu ili kuleta
ukombozi wa mwanadamu, ikiwa ni hivyo basi ni muhimu kufahamu kuwa tunaweza
kufurahia wakati huu wa msimu wa kuzaliwa kwa Masihi kwa kukubali pia utendaji
mzima wa Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu ni sehemu ya Utatu wa Mungu, na kwa
sababu hiyo, tnaposhangilia kuzaliwa kwa Yesu ambaye ni mkombozi wa ulimwengu
tunakumbushwa kuwa Utatuwa Mungu yaani Baba na Roho Mtakatifu ulihusika katika
mpango wa kumleta Mungu mwana duniani, Tutajifunza somo hili zuri kwa kuzingatia
vipengele vikuu vitatu vifuatavyo:-
·
Roho Mtakatifu na maandalizi ya kuzaliwa kwa
Masihi
·
Roho Mtakatifu na maisha na huduma ya masihi
·
Roho Mtakatifu na maisha yetu mimi na wewe
Roho Mtakatifu na maandalizi ya kuzaliwa kwa Masihi
Roho Mtakatifu anaonekana
kuhusika na ujio mzima wa masihi na maandalizi yake, Kumbuka nabii Yoeli
alitabiri kuwa siku za mwisho Mungu angemuachilia Roho wake Mtakatifu kwa wote
wenye mwili, kwa hiyo siku za mwisho zinaanzia katika msimu wote wa kuzaliwa
kwa Masihi na mpaka atakapokuja mara ya pili katika utawala wake wa miaka 1000
duniani, yaani millennium ambako umwagiko huo utakuwa katika ukamilifu wake au
utakuwa katika kilele chake.
Yoeli 2:28-29 “Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina roho
yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, waume kwa wake, watatabiri, wazee
wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono; tena juu ya watumishi wenu,
wanaume kwa wanawake, katika siku zile, nitamimina roho yangu.”
Roho Mtakatifu alihusika vipi katika maandalizi mazima ya kuzaliwa kwa
masihi?
-
Alihusika katika muujiza mzima wa kutungwa kwa
mimba katika tumbo la Mariamu kwa hiyo
tendo zima la Mariamu kupokea ujauzito liliratibiwa kwa uweza wa Roho Mtakatifu
Luka 1:35 “Malaika akajibu akamwambia, Roho
Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama
kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa
Mungu.”
-
Alihusika Katika kumjaza nguvu akiwa tumboni
Mtangulizi wa Masihi yaani Yohana Mbatizaji
Luka 1:13-16 “Lakini yule malaika akamwambia, Usiogope, Zakaria, maana dua yako
imesikiwa, na mkeo Elisabeti atakuzalia mtoto mwanamume, na jina lake utamwita
Yohana. Nawe utakuwa na furaha na shangwe, na watu wengi watakufurahia kuzaliwa
kwake. Kwa sababu atakuwa mkuu mbele za Bwana; hatakunywa divai wala kileo;
naye atajazwa Roho Mtakatifu hata tangu tumboni mwa mamaye. Na wengi katika
Waisraeli atawarejeza kwa Bwana Mungu wao.”
-
Alihusika katika kuwaongoza watu waliokuwa
wakimsubiria na kuona ahadi ya Mungu ikitimizwa katika maisha yao Luka 2:26-30 “Naye alikuwa ameonywa na Roho
Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa Bwana. Basi akaja
hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili
wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, yeye mwenyewe alimpokea mikononi
mwake, akamshukuru Mungu, akisema, Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, Kwa
amani, kama ulivyosema; Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako”
-
Athari za utendaji wa Roho Mtakatifu katika
kuzaliwa kwa masihi kunasababisha azaliwe mtu ambaye uungu unakaa ndani yake na
kwa sababu hiyo nguvu ya dhambi isingelimuweza, kwa sababu huyu aliyezaliwa
angekuwa ni mwana wa Mungu na hii ingeweza kumtofautisha na mwanadamu wa
kawaida ambaye asili yake ni Adamu, ambaye asili yake ni udongo, wakati Yesu
Kristo asili yake ni ya mbinguni.
1Wakorintho 15:47-48 “Mtu wa kwanza
atoka katika nchi, ni wa udongo. Mtu wa pili atoka mbinguni. Kama alivyo yeye
wa udongo, ndivyo walivyo walio wa udongo; na kama alivyo yeye wa mbinguni,
ndivyo walivyo walio wa mbinguni.”
Yohana 3:31 “Yeye ajaye kutoka juu, huyo yu juu
ya yote. Yeye aliye wa dunia, asili yake ni ya dunia, naye anena mambo ya
duniani. Yeye ajaye kutoka mbinguni yu juu ya yote.”
Kitendo cha Yesu
Kristo kuzaliwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kimemfanya kuwa mwanadamu mwenye
asili ya mbinguni na kwa sababu hiyo dhambi haingelimuweza na kupitia maisha
yake ya ushindi dhidi ya dhambi angeweza kuwa msaada kwa wanadamu wote, Na kwa
kufanywa mwenye dhambi ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu kupitia yeye hivyo
haya yasingeliwezekana kama sio kazi za Roho Mtakatifu.
2Wakorintho 5:21 “Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa
dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye.”
Roho Mtakatifu na maisha na huduma ya Masihi
Roho Mtakatifu anaonekana katika
maisha na huduma ya Yesu Kristo kuanzia ubatizo wake mpaka kupaa kwake Mbinguni
pamoja na ahadi aliyoitoa ya ujio rasmi wa Roho Mtakatifu juu ya wanafunzi wake
na sisi sote tuaminio.
-
Wakati
Yesu anabatizwa Roho wa Mungu alishuka juu yake – Mathayo
3:16-17 “Naye
Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu
zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake; na
tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu,
ninayependezwa naye.”
Hii ilikuwa ni
alama ya kupakwa mafuta kwa mtu huyu aliyezaliwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu
sasa anaanza kutumikia kusudi la baba yake, na baba anampaka mafuta kwa Roho
wake Mtakatifu ili sasa aweze kuwa kuhani, nabii na mfalme kwaajili ya
kuwakomboa wanadamu, uwezo wake wa kufundisha, kuhudumia watu, kufanya miujiza
na kila kitu alikifanya kwa uwezo wa Roho Mtakatifu huku maisha yake
yakiongozwa na Roho, kwa hiyo
a.
Aliongozwa
na Roho Mtakatifu – Marko 1:12-13 “Mara Roho
akamtoa aende nyikani. Akawako huko jangwani siku arobaini, hali akijaribiwa na
Shetani; naye alikuwa pamoja na wanyama wa mwitu, na malaika walikuwa
wakimhudumia.”
b. Alifanya
huduma zote za kuwafungua watu kama matokeo ya Roho Mtakatifu kuwa juu yake – Luka 4:18-19 “Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa
maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia
wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru
waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.”
Matendo 10:38 “habari za Yesu
wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye
akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na
Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye.”
c. Alitoa Pepo kwa Chanda cha Mungu yaani kwa
uwezo wa Roho Mtakatifu – Luka 11:20
“Lakini,
ikiwa mimi natoa pepo kwa kidole cha Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha
kuwajilia.”
Mathayo 12:28 “Lakini mimi
nikitoa pepo kwa Roho wa Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia.”
d. Nguvu wakati wa kusulubiwa – Roho
Mtakatifu aliyehusika katika kuzaliwa kwa Kristo, kubatizwa na kumuongoza na
kumtumia katika huduma zake duniani alimtia nguvu vilevile katika huduma yake
ya kuukabili Msalaba kwaajili ya ukombozi wetu, alikwenda Msalabani kwa upako
ule ule uliomuwezesha kufanya huduma nyingine, Roho alimpa ujasiri, upendo na
uvumilivu kwaajili ya ukombozi wa mwanadamu ili kuyatimiza mapenzi ya Mungu,
bila uweza wa Roho Mtakatifu uwezo wa kuvumilia mauti ya msalaba ambayo kwa
asili ilikuwa ni mauti mbaya na ya aibu isingeliwezekana au kuwa jambo jepesi.
Luka 22:41-43 “Mwenyewe
akajitenga nao kama kiasi cha kutupa jiwe, akapiga magoti akaomba, akisema, Ee
Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi
yangu, bali yako yatendeke. Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu.”
Waebrania
9:13-14 “Kwa
maana, ikiwa damu ya mbuzi na mafahali na majivu ya ndama ya ng'ombe
waliyonyunyiziwa wenye uchafu hutakasa hata kuusafisha mwili; basi si zaidi
damu yake Kristo, ambaye kwamba kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa
Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu,
mpate kumwabudu Mungu aliye hai?”
e. Wakati wa kufufuka kwake - Roho Mtakatifu anatumika pia kama muhusika
mkuu wakati wa kuurejesha uhai wa Yesu Kristo, yaani swala zima la kufufuka kwa
Yesu Kristo maandiko yanasema Roho Mtakatifu alihusika katika kumfufua Yesu
Kristo
Warumi 1:3-4 “yaani, habari
za Mwanawe, aliyezaliwa katika ukoo wa Daudi kwa jinsi ya mwili, na
kudhihirishwa kwa uweza kuwa Mwana wa Mungu, kwa jinsi ya roho ya utakatifu,
kwa ufufuo wa wafu, Yesu Kristo Bwana wetu;”
Warumi 8:11 “Lakini, ikiwa
Roho yake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua
Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa
Roho wake anayekaa ndani yenu.”
Roho Mtakatifu na maisha yetu mimi na wewe
Maisha yako wewe na mimi hayawezi
kuwa na ukamilifu bila kazi za Roho Mtakatifu kufanyika ndani yetu, Kristo
alisema sisi hatuwezi kufanya neno lolote pasipo yeye hii ni Dhahiri kuwa kama
Yesu Kristo Mwana wa Mungu alimtegemea Roho Mtakatifu katika maisha yake yote
na utumishi wake na uvumilivu wake na kila kitu, ni Dhahiri kuwa, maisha yetu
Bila Roho Mtakatifu na kazi zake katika maisha yetu itatufanya tuwe watu wasio
na faida maana imeandikwa wala si kwa uweza wala kwa nguvu Bali kwa uweza wa
Roho Mtakatifu yeye ndiye anayetupa
uwezo wa kufanya jambo lolote kwaajili ya Mungu.
Zekaria 4:6 “Akajibu
akaniambia, akisema, Hili ndilo neno la Bwana kwa Zerubabeli, kusema, Si kwa
uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema Bwana wa majeshi.”
Yohana 16:7-11 “Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi
niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi
nikienda zangu, nitampeleka kwenu. Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha
ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu. Kwa habari ya dhambi, kwa
sababu hawaniamini mimi; kwa habari ya haki, kwa sababu mimi naenda zangu kwa
Baba, wala hamnioni tena;kwa habari ya hukumu, kwa sababu yule mkuu wa
ulimwengu huu amekwisha kuhukumiwa.”
Roho Mtakatifu ni msaada ulio karibu katika maisha yetu – Yohana 14:26
“Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye
Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote
niliyowaambia.”
Roho Mtakatifu ni Msaada katika maombi – Warumi 8:26-27 “Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa
maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa
kuugua kusikoweza kutamkwa. Na yeye aichunguzaye mioyo aijua nia ya Roho
ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu.”
Roho Mtakatifu hututia nguvu – Matendo 1:4-8 “Hata
alipokuwa amekutana nao aliwaagiza wasitoke Yerusalemu, bali waingoje ahadi ya
Baba, ambayo mlisikia habari zake kwangu; ya kwamba Yohana alibatiza kwa maji,
bali ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu baada ya siku hizi chache. Basi
walipokutanika, wakamwuliza, wakisema, Je! Bwana, wakati huu ndipo
unapowarudishia Israeli ufalme? Akawaambia, Si kazi yenu kujua nyakati wala
majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe.Lakini mtapokea nguvu,
akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika
Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.”
Roho Mtakatifu hutupa karama za Rohoni – 1Wakorintho 12:4 “Basi pana
tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule.”
Tunaweza kufaidika na maswala
yote ya kiroho endapo tu Roho Mtakatifu atakuwa pamoja nasi atatusaidia katika
ujuzi, hekima, maarifa na kutuwezesha kutenda mambo kwa uhodari tukiwa na Roho
Mtakatifu. Najua wakati huu wa msimu wa sikukuu kuna maswala mengi sana na mada
nyingi zitazungumzwa lakini mimi niliongozwa kuwakumbusha watu wote kuwa
kuzaliwa kwa masihi nyuma yake uko uratibu mzima wa Roho wa Mungu na kwa sababu
hiyo ni vema tukashughulika na Kusheherekea sikukuu hii huku tukijikumbusha
kuwa ni kazi zipi Roho wa Mungu anazifanya ndani mwetu je kuna uhai katika
maisha yetu? Kuna uhai katika kanisa la Mungu? Iwapo tunataka kufurahia msimu
wa sikukuu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo kwa furaha ya kweli kutoka mbinguni
furaha hiyo itakamilishwa ndani yetu endapo tutaitumia nafasi hii kutafakari na
kutubu, na kumuomba Mungu asituondolee Roho wake Mtakatifu, sikukuu ya kuzaliwa
kwa masihi itakuwa tamu kama wanadamu watajiandaa kuzaliwa kwa Roho na kijazwa
kwa Roho Mtakatifu.
Na. Rev Innocent Mkombozi Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni