Jumapili, 29 Desemba 2024

Wale waliokwenda katika giza wameona nuru kuu!


Isaya 9:1-2 “Lakini yeye aliyekuwa katika dhiki hatakosa changamko. Hapo kwanza aliiingiza nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali katika hali ya kudharauliwa, lakini zamani za mwisho ameifanya kuwa tukufu, karibu na njia ya bahari; ng'ambo ya Yordani, Galilaya ya mataifa. Watu wale waliokwenda katika giza Wameona nuru kuu; Wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, Nuru imewaangaza.”




Utangulizi:

Moja ya habari za kinabii za kutia moyo na kuleta tumaini kwa jamii ni pamoja na ujio wa Masihi, Yesu Kristo Mwana wa Mungu aliye hai ambaye angeleta Nuru kwa watu waliokuwa gizani, na kuwaangazia tumaini watu waliokaa katika inchi ya uvuli wa mauti, Kimsingi giza pamoja na uvuli wa mauti ni hatia, hukumu, ni kupoteza tumaini, ni kuishi mbali na Mungu, ni kukosa muelekeo, pamoja na mateso yanayoambatana na kukata tamaa ambavyo vinawasumbua wanadamu kila iitwapo leo, kuzaliwa kwa Yesu Kristo kungekuwa ni sehemu muhimu ya kutimia kwa unabii huu ambao kimsingi ni habari njema zenye kuleta tumaini la Rehema kuu za Mungu kwa watu wote, kimsingi Kristo Yesu alipokuja Duniani alijitangaza rasmi kuwa yeye ni Nuru ya ulimwengu.

Yohana 8:12 “Basi Yesu akawaambia tena akasema, Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.”

Nuru ni ishara ya wema wa Mungu kwa wanadamu, na giza ni ishara ya uovu uonevu na utendaji wa ibilisi, Maisha ya Bwana wetu Yesu Kristo ni Nuru inayong’aa gizani, ambayo imekuja ulimwenguni kwa kusudi la kuwapa tumaini na kuwaondoa hofu wale wote waliokuwa wanakabiliwa na giza la uovu na uvuli wa Mauti. Wakati Yesu anazaliwa kimsingi watu walikuwa wamechoka sana, walikuwa wamekata tamaa, ukiacha ukoloni mzito  wa Warumi uliokuwa ukiwatawala kiserikali, maisha yao yalijawa na mateso, kukata tamaa na kufunikwa na giza la kiroho, miaka mingi karibu 400 ilikuwa imepita kukiwa na ukimya bila ya kuweko kwa nabii wala neno la Mungu la Dhahiri kwaajili yao, tumaini lilikuwa limebaki moja tu, kusubiri kutimizwa kwa unabii wa kuhusu kuja kwa Masihi, kiu yao hii inaonekana wazi hata Yohana alipokuwa ameanza kuhubiri ubatizo wake wa toba Maswali mengi yalielekea katika  kiu na hamu na shauku ya kumtamani Masihi ili aweze kukomesha mateso yao.

Yohana 1:20-23 “Naye alikiri, wala hakukana; alikiri kwamba, Mimi siye Kristo. Wakamwuliza, Ni nini basi? U Eliya wewe? Akasema, Mimi siye. Wewe u nabii yule? Akajibu, La. Basi wakamwambia, U nani? Tuwape majibu wale waliotupeleka. Wanenaje juu ya nafsi yako? Akasema, Mimi ni sauti ya mtu aliaye nyikani, Inyosheni njia ya Bwana! Kama vile alivyonena nabii Isaya.”              

Kwa nini kulikuwa na maswali mengi sana kwa Yohana Mbatizaji, kwa sababu watu walikuwa wamechoka sana na sasa walikuwa wakimtazamia Masihi aje kuwakomboa na kuwatoa katika maisha yaliyogubikwa na giza nene, tunapoadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristo, neno la Mungu linatukumbusha kuwa hatupaswi tena kuishi maisha ya mashaka, ya kukata tamaa, ya kutokuwa na matumaini, maisha ya machozi, na kuweko gizani, kwa sababu Nuru imekuja ulimwenguni, kimsingi sio Israel pekee waliokuwa wakimtarajia masihi lakini mataifa yote duniani ujio wa masihi ungekuwa ni habari njema za kuleta matumaini makubwa sana na kuondoa hofu.

Luka 2:8-14 “Na katika nchi ile ile walikuwako wachungaji wakikaa makondeni na kulinda kundi lao kwa zamu usiku.Malaika wa Bwana akawatokea ghafula, utukufu wa Bwana ukawang'aria pande zote, wakaingiwa na hofu kuu.Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana.Na hii ndiyo ishara kwenu; mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelala katika hori ya kulia ng'ombe. Mara walikuwapo pamoja na huyo malaika, wingi wa jeshi la mbinguni, wakimsifu Mungu, na kusema, Atukuzwe Mungu juu mbinguni, Na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.”                 

Tutajifunza somo hili Wale waliokwenda katika giza wameona nuru kuu. Kwa kuzingatia vipengele viwili muhimu vifuatavyo:-

 

·         Maana ya kwenda katika giza na kukaa katika nchi ya uvuli wa mauti

·         Wale waliokwenda katika giza wameona Nuru kuu!

 

Maana ya kwenda katika giza na kukaa katika nchi ya uvuli wa mauti

Neno kwenda katika giza, katika lugha ya kiebrania linatumika neno “chรดshek” kwa kiingereza “destruction” kwa Kiswahili kukaa katika “uharibifu” au kukaa katika uovu, Kabla ya ujio wa Yesu Kristo watu waliishi katika giza kubwa la kiroho, watu walikuwa hawana mwelekeo na hawaijui njia kwa sababu hiyo giza lilitawala na ukiwa ulikuwa juu ya nchi, Nguvu za wakuu wa giza ndizo zilizokuwa zinatawala ulimwengu, matendo ya giza yalikuwa yanatawala ulimwengu, Giza lilitawala kabla ya Nuru ya injili kuwazukia watu hivyo watu walikuwa wanaenenda gizani, watu walikuwa hawawezi wala hawana njia ya kurejesha uhusiano wao na Mungu ambao uliharibika tangu anguko la wazazi wetu Adam na Eva, Ni ujio wa Yesu Kristo ndio ulioleta Nuru ulimwenguni.

-          Yohana 4:4-10 “Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu. Nayo nuru yang'aa gizani, wala giza halikuiweza. Palitokea mtu, ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana. Huyo alikuja kwa ushuhuda, ili aishuhudie ile nuru, wote wapate kuamini kwa yeye. Huyo hakuwa ile nuru, bali alikuja ili aishuhudie ile nuru. Kulikuwako Nuru halisi, amtiaye nuru kila mtu, akija katika ulimwengu. Alikuwako ulimwenguni, hata kwa yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua

 

-          Wakolosai 1:12-14 “mkimshukuru Baba, aliyewastahilisha kupokea sehemu ya urithi wa watakatifu katika nuru. Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi;”

 

-          1Yohana 1:5-7 “Na hii ndiyo habari tuliyoisikia kwake, na kuihubiri kwenu, ya kwamba Mungu ni nuru, wala giza lo lote hamna ndani yake.Tukisema ya kwamba twashirikiana naye, tena tukienenda gizani, twasema uongo, wala hatuifanyi iliyo kweli; bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.”

 

-          Mika 7:7-8 “Lakini mimi, nitamtazamia Bwana; nitamngojea Mungu wa wokovu wangu; Mungu wangu atanisikia. Usifurahi juu yangu, Ee adui yangu; niangukapo, nitasimama tena; nikaapo gizani, Bwana atakuwa nuru kwangu.”                  

 

-          Zaburi 88:3-12 “Maana nafsi yangu imeshiba taabu, Na uhai wangu umekaribia kuzimu. Nimehesabiwa pamoja nao washukao shimoni; Nimekuwa kama mtu asiye na msaada. Miongoni mwao waliokufa nimetupwa, Kama waliouawa walalao makaburini. Hao ambao Wewe huwakumbuki tena, Wametengwa mbali na mkono wako. Mimi umenilaza katika shimo la chini, Katika mahali penye giza vilindini. Ghadhabu yako imenilemea, Umenitesa kwa mawimbi yako yote. Wanijuao umewatenga nami; Umenifanya kuwa chukizo kwao; Nimefungwa wala siwezi kutoka. Jicho langu limefifia kwa ajili ya mateso Bwana, nimekuita kila siku; Nimekunyoshea Wewe mikono yangu. Wafu je! Utawafanyia miujiza? Au waliofariki watasimama na kukuhimidi? Fadhili zako zitasimuliwa kaburini? Au uaminifu wako katika uharibifu? Miujiza yako itajulikana gizani? Au haki yako katika nchi ya usahaulifu?

 

Unapozisoma aya kadhaa za kibiblia hapo juu utaweza kugundua kuwa Giza ni baya sana na giza lina uhusiano wa karibu sana na mauti, giza humfanya mtu asiwe na msaada, giza ni sawa na mtu aliyetupwa miongoni mwa watu waliokufa, giza ni kukosa tumaini la kimwili na kiroho, giza ni kama kuwa shimoni, giza linakufanya usipambanue kati ya kifo na uhai, giza linamfanya mtu apoteze kibali, giza linamfanya mtu awe chukizo, giza linamfanya mtu asifurahie maisha kwa hiyo giza ni njia ya uovu, giza ni uharibifu, giza ni kuwa chini ya ukoloni wa kiroho, wa kimwili, wa kisiasa, wa kiuchumi, giza humfanya mwanadamu aishi kwa mashaka na kwa kubahatisha, mtu aliye gizani haoni mbele yake kukoje zaidi ya kuona giza, maisha ya dhambi, na ukosefu mkubwa wa kimaadili ni kutembea katika giza, giza pia linawakilisha hukumu, giza linawakilisha hofu na msahaka, giza ni bumbuwazi, giza kuchanganyikiwa na kutokuona.

Kutoka 10:21-23 “BWANA akamwambia Musa, Nyosha mkono wako kuelekea mbinguni, kuwe giza juu ya nchi ya Misri, watu wapapase-papase gizani. Basi Musa akaunyosha mkono wake kuelekea mbinguni; kukawa na giza nene katika nchi yote ya Misri muda wa siku tatu; hawakupata kuonana mtu na mwenziwe, wala hakuondoka mtu mahali alipokuwa muda wa siku tatu; lakini wana wa Israeli wote walikuwa na mwanga makaoni mwao.”

Sio hivyo tu Giza liliwakilisha hali ya mauti, au uvuli wa mauti “sheol” Msiba, kaburi au kuzimu yaani mwanadamu kupita katika msongo mkubwa wa mawazo wa kutokujua nini cha kufanya sawa tu na mtu aliyekuzimu, Katika Israel pia yalikuweko mapango ya kutisha ambapo watu waliokuwa wakichunga wanyama wakati mwingine walipenya katika mapango hayo ya kutisha kwa kusudi la kutokea katika eneo la kuwapa malisho wanyama wao ambayo pia waliyaita uvuli wa mauti, mapito mazito na huzuni unazozipitia ambazo hujui zitaisha lini ni giza, lakini ukiwa na Yesu ambaye ni Nuru ya ulimwengu utapita ukiwa salama kama mwandishi wa zaburi alivyoimba:-

Zaburi 23:4 “Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami, Gongo lako na fimbo yako vyanifariji.”

Kwa hiyo hali zote hizo zilikuwa zinaashiria kuwa mtu aliyepoteza uhusiano na Mungu na hana namna wala hajui njia ya kuurejesha ni sawa tu na mtu anayepita katika giza, na kuenenda katika uvuli wa mauti, Ujio wa Yesu Kristo kwakweli ulikuwa unaleta nuru kwa wale waliokuwa katika giza, wote waliokuwa wanapita katika mashaka na wote waliopoteza uhusiano wao na Mungu wangeweza kupata tumaini kwa upya kupitia ujio wa Yesu Kristo mwokozi na msaidizi wetu mkuu.               

Wale waliokwenda katika giza wameona nuru kuu!

Ujio wa Yesu Kristo ulikuwa ni wenye kuleta matumaini makubwa sana kwa wanadamu, kile alichokisema nabii Isaya miaka karibu na zaidi ya 700 kabla ya kuzaliwa kwa Kristo, ukweli ni kuwa alipozaliwa Yesu Kristo Nuru halisi ilikuwa imeingia sio tu Israel wala sio tu katika nchi za Zabuloni na Naftali na wala sio tu katika Galilaya lakini pia kwa ulimwengu mzima

Mathayo 4:13-16 “akatoka Nazareti, akaja akakaa Kapernaumu, mji ulioko pwani, mipakani mwa Zabuloni na Naftali; ili litimie neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali, Njia ya bahari, ng'ambo ya Yordani, Galilaya ya mataifa,Watu wale waliokaa katika giza Wameona mwanga mkuu, Nao waliokaa katika nchi na uvuli wa mauti Mwanga umewazukia.”

Luka 1:78-79 “Kwa njia ya rehema za Mungu wetu, Ambazo kwa hizo mwangaza utokao juu umetufikia, Kuwaangaza wakaao katika giza na uvuli wa mauti, Na kuiongoza miguu yetu kwenye njia ya amani.”

Ujio wa Yesu Kristo duniani unamuondoa kila amwaminiye yeye katika kuenenda gizani na kukabiliana na kutembea katika uvuli wa mauti bila kuogopa, Yesu Kristo mwenyewe alijitangaza kuwa yeye ndiye nuru ya ulimwengu na kuwa kila atakayemfuata yeye atakuwa na nuru na uzima wa milele, maisha yako hayatakuwa gizani tena.

Yohana 8:12 “Basi Yesu akawaambia tena akasema, Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.”

Kila mwanadamu anayeumwa na kuugua, kila mwanadamu asiye na kazi, kila mwanadamu aliyekata tamaa, kila mwanadamu mwenye misiba, kila mwanadamu anayeumizwa na hatia ya dhambi, kila mwanadamu anayejisikia upweke kwa sababu ametengwa mbali na Mungu, kila mwanadamua ambaye mahusiano yake yako katika vita, kila mwanadamu ambaye hana furaha mahali pa kazi, kila mwanadamu ambaye haabudu katika roho na kweli, kila mwanadamu ambaye hana utulivu wa nafsi, mwili na roho, kila mwanadamu ambaye yuko katika machafuko, kila mwanadamu ambaye dini yake haimpi tumaini la kweli, wala mungu wake hajishughulishi na mahitaji yake, kila aliye na huzuni, misiba na changamoto za aina mbali mbali na kila anaeyeelemewa na mizigo ya namna mbalimbali huyo yumo gizani, Habari njema ni kuwa Yesu Kristo ndiye nuru ya ulimwengu, yeye anaweza kuyaleta na kuyajenga matumaini ya kweli ya mwanadamu na kuondoa hali zote za kuvunjika moyo na kukata tamaa, yeye ndiye Nuru halisi, sio ile nuru ambayo watu waliandama mwezi na kuushangilia unapotoka gizani, huitaji tena kuandama mwezi na kuushangilia sasa nuru halisi ni Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai, hivyo katika majira haya ya kukumbuka siku ya kuzaliwa kwa masihi lazima tuwatangazie ya kuwa Nuru imekuja ulimwenguni na ni wakati sasa wa kuifuata nuru  

Wakolosai 2:16-17 “Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo.”

Ujio wa Yesu Kristo unatupa tumaini na kurejesha uhai – Ukimuamini Yesu Kristo yeye ataitupilia mbali hofu, atakuweka huru mbali na hatia ya dhambi, atakurudishia matumaini yaliyopotea na safari yako ya kupita katika uvuli wa mauti na badala yake nawe nuru kuu itakuzukia hutakuwa gizani tena.

Yohana 12:46 “Mimi nimekuja ili niwe nuru ya ulimwengu, ili kila mtu aniaminiye mimi asikae gizani.”

Ujio wa Yesu Kristo na kazi ile aliyokuja kuikamilisha imetuwezesha kuwa na mamlaka dhidi ya giza, giza sasa halituwezi kwa sababu nuru ina nguvu kuliko giza nasi tunayo mamlaka ya kuyakemea matendo yote ya giza.

Yohana 1:4-5 “Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu. Nayo nuru yang'aa gizani, wala giza halikuiweza.”

Waefeso 5:11-14. “Wala msishirikiane na matendo yasiyozaa ya giza, bali myakemee; kwa kuwa yanayotendeka kwao kwa siri, ni aibu hata kuyanena. Lakini yote yaliyokemewa hudhihirishwa na nuru maana kila kilichodhihirika ni nuru. Hivyo husema, Amka, wewe usinziaye, Ufufuke katika wafu, Na Kristo atakuangaza.”

Ujio wa Yesu Kristo kama nuru unatuhakikishia wema wa Mungu katika maisha yetu kuwa hatutakuja kuwa watumwa wa hofu, nuru ni njema, nuru ni kweli, nuru ni usalama, nuru ni maisha, nuru ni uwepo wa Mungu, Bwana akiwa nuru yako maana yake ni wokovu wako na nguvu zako na hakuna jeshi linaloweza kujipanga kupigana nawe na hata wakipigana nawe hutaogopa.

Zaburi 27:1-3 “Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, Nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani? Watenda mabaya waliponikaribia, Wanile nyama yangu, Watesi wangu na adui zangu, Walijikwaa wakaanguka. Jeshi lijapojipanga kupigana nami, Moyo wangu hautaogopa. Vita vijaponitokea, Hata hapo nitatumaini.”

Ujio wa Yesu Kristo kama Nuru unatukumbusha kuifanya kazi yake wakati nuru hiyo inawaka, kila mtu aliyeokolewa amepewa wajibu wa kuisambaza nuru ulimwenguni, kuamka na kuitangaza injili na kuwafanya mataifa yote kuwa wanafunzi agizo la kimaandiko linamtaka kila mmoja kufanya kazi na kuinuka na kuangaza nuru kila mahali kusiko na tumaini.

Yohana 9:4-5 “Imetupasa kuzifanya kazi zake yeye aliyenipeleka maadamu ni mchana, usiku waja asipoweza mtu kufanya kazi.Muda nilipo ulimwenguni, mimi ni nuru ya ulimwengu.”

Isaya 60:1-3 “Ondoka, uangaze; kwa kuwa nuru yako imekuja, Na utukufu wa Bwana umekuzukia. Maana, tazama, giza litaifunika dunia, Na giza kuu litazifunika kabila za watu; Bali Bwana atakuzukia wewe, Na utukufu wake utaonekana juu yako. Na mataifa wataijilia nuru yako, Na wafalme kuujia mwanga wa kuzuka kwako.”

Nuru inatukumbusha kuishi maisha matakatifu, kila mtu aliyeokolewa anapaswa kuwa mfano wa kuigwa na kuwaonyesha wengine njia, hatuwezi kuwa na madai kuwa tunamfuata Yesu kisha tukajificha, hatuwezi kuwa na madai ya kuwa tunamfuata Yesu kisha tukaishi kinyume naye Yesu alikuwa mtakatifu, kuishi maisha matakatifu ni agizo la kibiblia, hatuwezi kuacha kulihubiri na kulikazia, wala hatuwezi kuishi maisha ya dhambi kwa kisingizio cha neema, Nuru yake Yesu Kristo ni neema ya kutuwezesha kuishi maisha matakatifu chini ya msaada wake kwa hiyo matendo yetu mema yanapaswa kuiangazia dunia ili kila mmoja aweze kuona na kumtukuza baba wa Mbinguni, kwa sababu hiyo hatuna budi kutembea kama watoto wa nuru kwa kuishi maisha matakatifu.

Mathayo 5:14-16 “Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima. Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani.Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.”

Waefeso 5:8-9 “Kwa maana zamani ninyi mlikuwa giza, bali sasa mmekuwa nuru katika Bwana; enendeni kama watoto wa nuru, kwa kuwa tunda la nuru ni katika wema wote na haki na kweli;”

Nuru inatukumbusha kuhusu Nguvu za Mungu, za uumbaji na utendaji, wakati nguvu za uonevu zikiitwa nguvu za giza, Nguvu za Mungu ni nguvu za Nuru, wakati wowote kunapokuwa na giza ukiweka mwanga giza hutoweka haraka na kukimbia, kunapokosekana utaratibu na kuwepo kwa machafuko Nuru ikija utaratibu unakaa mahali pake na giza lote linakimbia, andiko linasema Nuru hung’aa gizani wala giza halikuiweza, Wakati huu tunapoadhimisha ujio wa Yesu Kristo Duniani na kushangilia kuzaliwa kwake, tujue ya kuwa ujio wake umekuwa na faida kubwa sana katika maisha yetu, Nguvu za giza hazituwezi tena, sisi tumehamishwa kabisa na kuokolea kabisa katika nguvu za giza na kutuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa mwana wa pendo lake, kwa hiyo nguvu zozote za uonevu wa kishateni hazituwezi, wala giza halikuiweza nuru, tuyakemee matendo yote yasiyozaa ya giza, tuiitie nuru wakati wote tunapokuwa na mashaka, au vita Bwana akiwa nuru yetu kamwe hatupaswi kuogopa, kwa kuwa sisi sasa ni miongoni mwa watu waliokaa katika giza na nuru imetuzukia, ni miongoni mwa watu waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti na nuru imetuangazia.

Wakolosai 1:13-14 “Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi;”

Yohana 1:4-5 “Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu. Nayo nuru yang'aa gizani, wala giza halikuiweza.”

1Yohana 3:8 “atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.”

 

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Hakuna maoni: