2Petro 2:14-16 “wenye macho yajaayo uzinzi, watu wasiokoma kutenda dhambi,
wenye kuhadaa roho zisizo imara, wenye mioyo iliyozoezwa kutamani, wana wa
laana; wakiiacha njia iliyonyoka, wakapotea, wakiifuata njia ya Balaamu, mwana
wa Beori, aliyependa ujira wa udhalimu; lakini alikaripiwa kwa uhalifu wake
mwenyewe; punda, asiyeweza kusema, akinena kwa sauti ya kibinadamu, aliuzuia
wazimu wa nabii yule.”
Utangulizi:
Nyakati hizi tulizo nazo ni
nyakati za mwisho, tunaishi dakika za mwishoni sana katika dakika za kinabii,
na maandiko yametueleza wazi kuwa nyakati hizi za mwisho ni nyakati za hatari,
hasa kwa sababu ya uwepo wa mafundisho ya uongo na uwepo wa manabii wengi wa
uongo pamoja na uwepo wa mafundisho ya mashetani na roho zidanganyazo, kwa hiyo
kila Mkristo anapaswa kulikumbuka hili na kuchukua tahadhari kujihami na uongo
wao:-
1Timotheo 4:1-3 “Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine
watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya
mashetani; kwa unafiki wa watu wasemao uongo, wakichomwa moto dhamiri zao
wenyewe; wakiwazuia watu wasioe, na kuwaamuru wajiepushe na vyakula, ambavyo
Mungu aliviumba vipokewe kwa shukrani na walio na imani wenye kuijua hiyo kweli.”
Mathayo24:11-14 “Na manabii wengi wa uongo watatokea, na kudanganya wengi.
Na kwa sababu ya kuongezeka maasi, upendo wa wengi utapoa. Lakini mwenye
kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka.Tena habari njema ya ufalme
itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo
ule mwisho utakapokuja.”
Katika nyakati hizi za mwisho ni
muhimu kwa kanisa yaani kila mtu aliyeokolewa kuwa makini na kuchukua tahadhari
juu ya utendaji wa shetani, hususani kwa kutuingizia mafundisho ambayo kusudi
lake ni kututoa katika kweli na usafi wa kiroho ili tuweze kuishi mbali na
uadilifu wa kiungu, aina hiyo na njia kama tutaifuata basi tutakuwa tumeifuata njia
ya Balaamu, ambaye yeye ni mfano wa manabii wa uongo na walimu wa uongo, leo
tutachukua muda kujifunza kwa kina na mapana na marefu juu ya somo hili lenye
kichwa “Kuifuata njia ya Balaamu”
ili kujiepusha na namna ya kifuata njia ya udanganyifu.Tutajifunza somo hili
kuifuata njia ya Balaam kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Ufahamu
kuhusu Balaamu.
·
Kuifuata
njia ya Balaamu.
·
Onyo la
kutokuifuata njia ya Balaamu.
Maandiko matakatifu yanatuonya vikali
kuacha kuifuata njia ya Balaamu kwa msisitizo mkubwa sana na kwa lugha kali ya maonyo Petro akionya kuwa kuifuata njia hiyo
ni kuacha njia iliyonyooka na kufuata udhalimu, Yuda akitoa onyo kali na
akiliita kosa la Balaamu aliyependa ujira wa udhalimu na Yesu mwenyewe katika
kitabu cha ufunuo akionyesha kuchukizwa na mafundisho ambayo yanatia watu
ukwazo na kuwaongoza katika maisha yasiyo na uadilifu wa Kristo, maonyo haya
makali yanatufanya leo tujadili na kutafakari tena huyu Balaamu ni nani na
alifanya nini hata kumuudhi Mungu na tahadhari ambayo kanisa linapaswa kuchukua
ili kujilinda na mafundisho ya uongo!
2Petro 2:15 “wakiiacha njia iliyonyoka, wakapotea, wakiifuata njia ya
Balaamu, mwana wa Beori, aliyependa ujira wa udhalimu;”
Yuda 1:11 “Ole wao! Kwa sababu walikwenda katika njia ya Kaini, na
kulifuata kosa la Balaamu pasipo kujizuia, kwa ajili ya ujira, nao wameangamia
katika maasi ya Kora.”
Ufunuo 2:14 “Lakini ninayo maneno machache juu yako, kwa kuwa unao huko
watu washikao mafundisho ya Balaamu, yeye aliyemfundisha Balaki atie ukwazo
mbele ya Waisraeli, kwamba wavile vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na
kuzini.”
Jina Balaamu linajitokeza kwa mara
ya kwanza katika maandiko mara baada ya wana wa Israel kuvuka bahari ya Shamu
na kuanza kuikabili inchi ya mkanaani wakiwa chini ya Musa, Katika wakati huu Israel
walikuwa wengi sana na tayari walianza kuogopwa na mataifa yaliyokuwa yakiishi
ng’ambo ya Yordani likiwemo taifa la wana wa Moabu, ambalo mtawala wake aliitwa
Balaki, akiwa na hofu kubwa sana ya kuwaogopa Israel Mfalme huyu aliamua kwenda
kumuita mtu mwenye uwezo wa nguvu za giza kuwalaani au kuwaroga Israel ili
ikiwezekana wasiweze kumvamia na kumshinda, mtu huyu aliitwa Balaamu, jina Balaamu kwa kiebrania
linasomeka kama “Bā’lam”
au “Bil’ām” ambalo kwa kiingereza ni “Devourer” a person of thing that eats,
consumes, or destroys something greedily, ravenously or voraciously yaani
kwa Kiswahili mtu mwenye kitu
kinachokula, kinachoteketeza, au kuharibu kitu fulani kwa uroho, mwenye uchu,
au mwenye tamaa, kwa hiyo mtu huyu Balaamu ambaye jina lake linafanana sana
na tabia zake alialikwa na Mfalme wa Moabu akiwa pamoja na muungano wa wazee wa
Midian kuja kuilaani na kuiroga Israel. Balaamu amekuwa ni mfano wa manabii na
walimu wa uwongo katika nyakati zote kanisa likiwepo duniani.
Hesabu 22:1-6 “Kisha wana wa Israeli wakasafiri na kupanga katika nchi
tambarare za Moabu ng'ambo ya pili ya Yordani karibu ya Yeriko. Na Balaki mwana
wa Sipori akaona mambo yote ambayo Israeli wamewatendea Waamori. Moabu
akawaogopa hao watu sana, kwa kuwa walikuwa wengi; Moabu akafadhaika kwa sababu
ya wana wa Israeli. Moabu akawaambia wazee wa Midiani, Sasa jeshi hili la watu
litaramba vitu vyote vinavyotuzunguka, kama vile ng'ombe arambavyo majani ya
mashamba. Na Balaki, mwana wa Sipori, alikuwa mfalme wa Moabu zamani zile. Basi
akatuma wajumbe kwa Balaamu mwana wa Beori, hata Pethori, ulio kando ya Mto,
mpaka nchi ya wana wa watu wake, kwenda kumwita, akisema, Tazama, kuna watu
waliotoka Misri; tazama, wanaufunika uso wa nchi, tena wanakaa kunikabili mimi.
Basi, njoo wewe, nakusihi unilaanie watu hawa; maana wana nguvu kunishinda
mimi. Labda nitawaweza, tupate kuwapiga, niwafukuze watoke katika nchi yangu,
kwa maana najua ya kuwa yeye umbarikiye hubarikiwa, na yeye umlaaniye hulaaniwa.”
Balaamu hatajwi kokote kuwa alikuwa
nabii, isipokuwa na Petro ambaye amemtaja kama nabii mwenye wazimu lakini tunaweza
kusema kuwa alikuwa ni mchawi au nabii wa uongo, alikuwa ni mchawi mwenye uwezo
wa kubariki au kulaani, hata hivyo Mungu aliweza kuingilia kati mara kadhaa na kusema naye, na
hata Roho wa Mungu aliingilia mfumo wa maneno yake ili aweze kubariki Israel
badala ya kuwalaani, na hivyo mtu huyu mwenye utata mwingi alijikuta akitoa
nabii nyingi za Baraka na za kweli kwa Israel na ukiwapo ujio wa Daudi na
Masihi, Bwana wetu Yesu.
Hesabu 24:1-4 “Basi Balaamu alipoona ya kuwa ilimpendeza Bwana kuwabariki
Israeli, hakwenda, kama hapo kwanza, ili kutafuta uchawi, bali alielekeza uso
wake jangwani. Balaamu akainua macho yake akawaona Israeli wamekaa kabila
kabila; roho ya Mungu ikamjia. Akatunga mithali yake, akasema, Balaamu mwana wa
Beori asema, Yule mtu aliyefumbwa macho asema; Asema, yeye asikiaye maneno ya
Mungu, Yeye aonaye maono ya Mwenyezi, Akianguka kifudifudi, amefumbuliwa macho;”
Balaamu alikuwa anamjua Mungu wa
kweli au wa Israel wazi wazi, hata baada ya Roho wa Mungu kuingilia mfumo wake,
inaonekana tu kuwa mtu huyu alikuwa amezingirwa na kuharibiwa na mazingira ya
dunia, tamaa, na ubinafsi ambao ulimfanya ashindwe kutii mapenzi ya Mungu mara
kadhaa, kiasi ambacho alitamani kumuendea Balaki, Hata hivyo baada ya
kubembelezwa kwa mali nyingi na heshima kubwa na akakaidi katazo la Mungu la
kwenda kuwalaani Israel jambo lililopelekea malaika wa Bwana kuingilia kati na
punda wake kugomea kwenda na hata kusema naye
Hesabu 22:7-35 “Wazee wa Moabu, na wazee wa Midiani, wakaenda, wakichukua
ujira wa uganga mikononi mwao; wakamfikilia Balaamu, wakamwambia maneno ya
Balaki. Akawaambia, Kaeni hapa usiku huu, nami nitawaletea jawabu kama Bwana
atakavyoniambia; wakuu wa Moabu wakakaa na Balaamu. Mungu akamjia Balaamu,
akasema, Ni watu gani hawa ulio nao pamoja nawe? Balaamu akamwambia Mungu,
Balaki mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, amewatuma kwangu, akisema, Tazama,
kuna watu waliotoka Misri, wanaufunika uso wa nchi; basi njoo unilaanie watu
hawa; labda nitaweza kupigana nao, na kuwafukuza. Mungu akamwambia Balaamu,
Usiende pamoja nao; wala usiwalaani watu hawa, maana wamebarikiwa. Balaamu
akaondoka asubuhi akawaambia wakuu wa Balaki, Enendeni zenu hata nchi yenu; kwa
maana Bwana amekataa kunipa ruhusa niende pamoja nanyi. Wakuu wakaondoka
wakaenda kwa Balaki, wakasema, Balaamu, anakataa kuja pamoja nasi. Basi Balaki
akatuma wakuu mara ya pili, wengi zaidi, wenye cheo wakubwa kuliko wale wa
kwanza. Wakamfikilia Balaamu, wakamwambia, Balaki mwana wa Sipori asema hivi,
Nakusihi, neno lo lote lisikuzuie usinijie; maana nitakufanyizia heshima nyingi
sana, na neno lo lote utakaloniomba nitalitenda; basi njoo, nakusihi, unilaanie
watu hawa. Balaamu akajibu akawaambia watumishi wa Balaki, Kama Balaki angenipa
nyumba yake imejaa fedha na dhahabu, siwezi kupita mpaka wa neno la Bwana,
Mungu wangu, kulipunguza au kuliongeza. Basi sasa nawasihi, kaeni hapa tena
usiku huu, nipate kujua Bwana atakaloniambia zaidi. Mungu akamjia Balaamu
usiku, akamwambia, Kwa kuwa watu hawa wamekuja kukuita, enenda pamoja nao;
lakini neno lile nitakalokuambia ndilo utakalolitenda, basi. Balaamu akaondoka
asubuhi, akatandika punda wake, akaenda pamoja na wakuu wa Moabu. Hasira ya
Mungu ikawaka kwa sababu alikwenda; malaika wa Bwana akajiweka njiani, ili
kumpinga. Basi alikuwa amepanda punda wake, na watumishi wake wawili walikuwa
pamoja naye. Na yule punda akamwona malaika wa Bwana amesimama njiani, na
upanga wake mkononi mwake amekwisha kuufuta; punda akageuka upande ili kuiacha
njia, akaingia shambani. Balaamu akampiga punda ili kumrejeza njiani. Kisha
malaika wa Bwana akasimama mahali penye bonde, katikati ya mashamba ya
mizabibu, tena penye kitalu upande huu na kitalu upande huu.Yule punda akamwona
malaika wa Bwana, akajisonga ukutani, akamseta Balaamu mguu wake, basi akampiga
mara ya pili. Malaika wa Bwana akaendelea mbele akasimama mahali pembamba sana,
hapakuwa na nafasi ya kugeukia mkono wa kuume, wala mkono wa kushoto. Yule
punda akamwona malaika wa Bwana, akajilaza chini ya Balaamu; hasira yake
Balaamu ikawaka, akampiga punda kwa fimbo yake. Bwana akakifunua kinywa cha
yule punda, naye akamwambia Balaamu, Nimekutenda nini, hata ukanipiga mara tatu
hizi? Balaamu akamwambia punda; Kwa sababu umenidhihaki; laiti ningekuwa na
upanga mkononi mwangu ningekuua sasa hivi. Yule punda akamwambia Balaamu, Je!
Mimi si punda wako, nawe umenipanda maisha yako yote hata leo? Nimezoea
kukutenda hayo? Akasema, La! Ndipo Bwana akafunua macho ya Balaamu akamwona
malaika wa Bwana amesimama njiani, ana upanga mkononi mwake, umekwisha kufutwa
naye akainama kichwa, akaanguka kifudifudi. Malaika wa Bwana akamwambia, Mbona
umempiga punda wako mara tatu hizi? Tazama mimi nimekuja ili kukupinga, kwa
sababu njia yako imepotoka mbele zangu, punda akaniona, akageuka upande mbele
zangu mara tatu hizi; kama asingejiepusha nami, bila shaka ningalikuua wewe,
nikamwacha yeye hai.Balaamu akamwambia malaika wa Bwana, Nimefanya dhambi;
maana sikujua ya kuwa wewe umesimama njiani ili kunipinga; basi sasa, ikiwa
umechukizwa, nitarudi tena. Malaika wa Bwana akamwambia Balaamu Enenda pamoja
na watu hawa, lakini neno lile nitakalokuambia, ndilo utakalosema. Basi Balaamu
akaenda pamoja na wakuu wa Balaki.”
Mchawi huyu mtata hata hivyo
aliruhusiwa kibishi na malaika wa Bwana lakini alilazimishwa kuwa atasema yale
tu Mungu atakayoweka katika kinywa chake na sio maneno yake wala makusudio yake
kwa hiyo agizo la Mungu kwake ilikuwa ni kubariki wana wa Israel na sio
kuwalaani au kuroga. Kama ilivyokusudiwa na mfalme wa wamoabu.
Kuifuata njia ya Balaamu.
Historia inaonyesha ya kuwa
Balaamu alipaswa kutamka yale tu ambayo Mungu alikuwa amemwamuru kutamka, wote
tunajua mapenzi ya Mungu kwa wanadamu, ya kuwa tangu zamani Mungu ametaka
watumishi wake watamke kile tu ambacho Mungu amekikusudia na hata neno lake
Mungu anataka litendewe haki katika tafasiri zake, Mungu ametamani watu wote
wamtii, watu wote wasikie neno lake kama lilivyo bila kuongeza au kupunguza, na
watumishi waiseme kweli yake na ni ukweli ulio wazi kuwa Mungu anachukizwa sana
na manabii na walimu wa uongo ona:-
Hesabu 22:20 “Mungu akamjia Balaamu usiku, akamwambia, Kwa kuwa watu hawa
wamekuja kukuita, enenda pamoja nao; lakini neno lile nitakalokuambia ndilo
utakalolitenda, basi.”
Yeremia23:25-29 “Nimesikia waliyoyasema manabii wanaotabiri uongo kwa jina
langu, wakisema, Nimeota ndoto; nimeota ndoto. Je! Mambo hayo yatakuwa katika
mioyo ya manabii wanaotabiri uongo hata lini, manabii hao wenye udanganyifu
katika mioyo yao wenyewe? Wanaodhania ya kuwa watawasahaulisha watu wangu jina
langu kwa ndoto zao, wanazomhadithia kila mtu jirani yake, kama vile baba zao
walivyolisahau jina langu, kwa ajili ya Baali. Nabii aliye na ndoto, na aseme
ndoto yake; na yeye aliye na neno langu, na aseme neno langu kwa uaminifu. Makapi
ni kitu gani kuliko ngano? Asema Bwana. Je! Neno langu si kama moto? Asema
Bwana; na kama nyundo ivunjayo mawe vipande vipande? ”
Kumbukumbu 4:1-2 “Na sasa, Ee Israeli, zisikilizeni amri na hukumu
niwafundishazo, ili mzitende; mpate kuishi na kuingia na kuimiliki nchi awapayo
Bwana, Mungu wa baba zenu. Msiliongeze neno niwaamurulo wala msilipunguze,
mpate kuzishika amri za Bwana, Mungu wenu, niwaamuruzo.”
Ufunuo 22:18-19 “Namshuhudia kila mtu ayasikiaye maneno ya unabii wa kitabu
hiki, Mtu ye yote akiyaongeza, Mungu atamwongezea hayo mapigo yaliyoandikwa
katika kitabu hiki. Na mtu ye yote akiondoa lo lote katika maneno ya unabii wa
kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima, na katika
ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.”
Neno la Mungu linakazia kuwa iko
haja ya kusema kile ambacho ni mapenzi ya Mungu na kwa dhamiri iliyo njema, na
Mungu alimuamuru Balaamu kufanya hivyo na kwa sehemu alifanya hivyo, Lakini
hata hivyo kwa sababu ya tamaa ya fedha na heshima na ujira mkubwa aliokuwa
ameandaliwa tunanaarifiwa katika maandiko kuwa baadaye Balaamu alishauri njia itakayoleta
madhara kwa wana wa Israel, na hili ndilo jambo walifanyalo manabii na walimu
wa uongo.
Hesabu 31:15-16 “Musa akawauliza, Je! Mmewaponya wanawake wote hai? Tazama,
hawa ndio waliowakosesha wana wa Israeli, kwa shauri la Balaamu, wamfanyie
Bwana dhambi katika hilo jambo la Peori, na kwa hivyo pigo lilikuwa katika
mkutano wa Bwana.”
Ni ushauri gani aliutoa Balaamu,
inaonekana kuwa baada ya kushindwa kuwalaani Israel na kuwaroga kwa sababu ya
karipio la Bwana, Balaamu aliamua kutoa ushauri wa kuwawekea kwazo wana wa
Israel, ambao walikuwa wamepiga kambi Shitimu, wanawake wa Moabu waliandaa
ibada za Baal Peor na waisrael hasa wanaume walialikwa au kushawishiwa katika
ibada hizo na waliruhusiwa kuingiliana na wanawake wanaohudumu katika madhabau
za baali,Yaani walizini kiwmili na kiroho, Jambo hili lilimuudhi Mungu na kumpa
hasira na kushusha mapigo kwa watu wake Israel kwa maelekezo ya Musa, kwa kuwa
ibada hizo za kipagani zilihusisha miungu ya uzazi matukio ya ngono ni sehemu
ya ibada hizo na hivyo Israel
yakawakuta, katika tukio hilo watu wapatao elfu 24 walikufa kwa pigo.
Hesabu 25:1-9 “Basi Israeli akakaa Shitimu, kisha watu wakaanza kuzini
pamoja na wanawake wa Moabu; kwa kuwa waliwaalika hao watu waende sadakani,
sadaka walizowachinjia miungu yao; watu wakala chakula, wakaisujudu hiyo miungu
yao. Ikawa Israeli kujiungamanisha na Baal-peori; hasira za Bwana zikawaka juu
ya Israeli.Kisha Bwana akamwambia Musa, Watwae wakuu wote wa hao watu,
ukamtungikie Bwana watu hao mbele ya jua, ili kwamba hizo hasira kali za Bwana
ziwaondokee Israeli. Basi Musa akawaambia waamuzi wa Israeli, Waueni kila mtu
watu wake waliojiungamanisha na Baal-peori. Na tazama, mtu mmoja miongoni mwa
wana wa Israeli akaja na kuwaletea nduguze mwanamke Mmidiani mbele ya macho ya
Musa, na mbele ya macho ya mkutano wote wa wana wa Israeli, hapo walipokuwa
walia mbele ya mlango wa hema ya kukutania. Naye Finehasi mwana wa Eleazari,
mwana wa Haruni kuhani, alipoona jambo hilo, akaondoka hapo katikati ya
mkutano, akashika fumo mkononi mwake; akamwandama huyo mtu wa Israeli na
kuingia ndani ya hema nyuma yake, naye akawachoma wote wawili kwa fumo lake,
yule mume wa Israeli na huyo mwanamke kati ya tumbo lake. Basi pigo likazuiwa
kwao wana wa Israeli. Nao waliokufa kwa hilo pigo walikuwa watu elfu ishirini
na nne hesabu yao.”
Kwa hiyo inaonekana wazi kuwa
Balaamu, aliposhindwa kuwalaani Israel na kuwaroga, alitoa ushauri, alitoa
ushauri huo ili kuwakosanisha watu wa Mungu kwa Mungu mwenyewe na kusababisha
madhara makubwa kwa Israel, Balaamu alifanya haya kwa sababu ya tamaa na kutaka
kumfurahisha Balaki ambaye alimuahidi mali nyingi sana, na kwa sababu hiyo
Balaamu anaingia katika rekodi ya watu waliowakosesha watu wa Mungu, na katika
nyakati za agano jipya manabii na walimu wote wa uongo na watu wote
wanaopotosha watu na kuharibu uadilifu wetu kwa Mungu nao wanaitwa watu
walioifuata njia ya Balaamu mwana wa Beori, wako watu ambao kwa makusudi kabisa
au kwa sababu ya tamaa zao wako tayari kuichuja injili kwa sababu kadhaa kama
Balaamu, aidha kwaajili ya mapato ya udhalimu na pia kama watumishi wa shetani,
Kanisa la kwanza lilipambana kufa na kupona
na walimu wa uongo.Tabia kadhaa za Balaamu hapa zinaweza kuwasaidia watu
wa Mungu kuwatambua wale wanaokwenda katika njia ya Balaamu ona:-
1.
Balaamu alikuwa na tamaa na aliamua kuchakachua
- Nyakati za leo, Mitume wa uongo, manabii wa uongo, wainjilisti wa uongo,
wachungaji wa uongo, na walimu wa uongo, na washirika wa uongo wako tayari
kulichakachua neno la Mungu na uadilifu wa kiroho kwa sababu ya faida za
mwilini, wanaingia katika jaribu hilo kwa sababu ya tamaa za mwili na mali na
utukufu wa wanadamu, wanafundisha watu na kuwaingizia tamaa za vitu vya mwilini
zaidi kuliko vya rohoni, sisemi kuwa vitu vya mwilini havina maana, lakini
wanasahu kutoa kipaumbele kwa ufalme wa Mungu na kwaajili ya tamaa na mapato ya
aibu wamechuja viwango vya injili na hawakemei dhambi, wala kuwaongoza watu
katika mafundisho sahihi na ya kweli. Walimu wa uwongo hujipa mamlaka kubwa
kana kwamba wao wako juu ya maandiko na kuwapa watu uhuru usiotokana na Mungu,
matokeo yake watu hawataishi maisha matakatifu na watajikuta wanarudi nyuma na
kuishi maisha yasiyo na uadilifu kama anavyofafanua Petro:-
2Petro 2:15-21 “wakiiacha njia iliyonyoka,
wakapotea, wakiifuata njia ya Balaamu, mwana wa Beori, aliyependa ujira wa
udhalimu; lakini alikaripiwa kwa uhalifu wake mwenyewe; punda, asiyeweza
kusema, akinena kwa sauti ya kibinadamu, aliuzuia wazimu wa nabii yule. Hawa ni
visima visivyo na maji, na mawingu yachukuliwayo na tufani, ambao weusi wa giza
ni akiba waliyowekewa. Maana wakinena maneno makuu mno ya kiburi, kwa tamaa za
mwili na kwa ufisadi huwahadaa watu walioanza kuwakimbia wale wanaoenenda
katika udanganyifu; wakiwaahidia uhuru, nao wenyewe ni watumwa wa uharibifu,
maana mtu akishindwa na mtu huwa mtumwa wa mtu yule.Kwa maana wale waliokwisha
kuyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua Bwana na Mwokozi Yesu Kristo, kama
wakinaswa tena na kushindwa, hali yao ya mwisho imekuwa mbaya kuliko ile ya
kwanza.Maana ingekuwa heri kwao kama wasingaliijua njia ya haki, kuliko kuijua,
kisha kuiacha ile amri takatifu waliyopewa.”
2.
Balaamu aliwashawishi watu wazini – Baada ya
kushindwa kuwalaani na kuwaroga waisrael alitoa ushauri kwamba wanawake wa
Moabu wawashawishi wanaume wa Israel ili wazini na kuabudu miungu, hii
inatufundisha kuwa wako watu nyakati za leo badala ya kuwaongoza watu katika
kutenda mema wanaichakachua injili na kuwaongoza watu vibaya maandiko
yanatuonya kuwa kuifuata njia ya Balaamu ni pamoja na kuwashawishi watu kwenda
kinyume na uadilifu, mfano mtu anawezaje kuacha kuikemea dhambi? Leo hii yako
makanisa hayakemei dhambi, wala hayaongozi watu katika toba, wala kuishi maisha
ya haki, na wala hawahubiri utakatifu na zaidi ya yote zinaa, uasherati,
utapeli na uongo, choyo, chuki, wivu, na mafarakano imekuwa ni moja ya maswala
au matunda yanayoonekana wazi kwa kanisa kinyume na uadilifu wa Mafundisho ya
Yesu Kristo na mitume, aidha watu hawawakemei wale wanaofundisha mafundisho ya
uongo. Leo hii uponyaji unanunuliwa kwa viwango vya kifedha na linaonekana kama
jambo la kawaida tu.
Mathayo 7:15-20 “Jihadharini na manabii wa uongo,
watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu
wakali. Mtawatambua kwa matunda yao. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au
tini katika mibaruti? Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti
mwovu huzaa matunda mabaya. Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti
mwovu kuzaa matunda mazuri. Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa
motoni. Ndiposa kwa matunda yao mtawatambua”
3.
Balaamu alikuwa mchawi – Pamoja na kuwa
Mungu alimtumia kusema na kutoa unabii, lakini huyu Balaamu alikuwa mchawi,
maandiko yanasema alikwenda kutafuta uchawi na pia wazee wa midian walimpa
ujira wa uganga, tukio la kutoa ushauri uliokuwa kinyume na mapenzi ya Mungu
unathibitisha wazi kuwa alikuwa nabii wa uongo wala hakusimama katika kweli,
swali kubwa la kujiuliza mtu anawezaje kuwa wa kiroho na wakati huo huo akatoa
ushauri unaoongoza katika kutenda dhambi? Unabii wa kweli na miujiza ya kweli
sio kipimo cha uadilifu wala uthibitisho kuwa Mungu yuko na mtu huyo,
tutawatambua kwa matunda yao.
Hesabu 24:1 “Basi Balaamu alipoona ya kuwa
ilimpendeza Bwana kuwabariki Israeli, hakwenda, kama hapo kwanza, ili kutafuta
uchawi, bali alielekeza uso wake jangwani.”
Hesabu 22:7 “Wazee wa Moabu, na wazee wa Midiani,
wakaenda, wakichukua ujira wa uganga mikononi mwao; wakamfikilia Balaamu,
wakamwambia maneno ya Balaki.”
Mathayo 7:21-23 “Si kila mtu aniambiaye, Bwana,
Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya
Baba yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana,
hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako
kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe;
ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.”
4.
Balaamu aliweka ukwazo - Ufunuo 2:14 “Lakini ninayo maneno machache juu yako, kwa kuwa unao huko
watu washikao mafundisho ya Balaamu, yeye aliyemfundisha Balaki atie ukwazo
mbele ya Waisraeli, kwamba wavile vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na
kuzini.”
Neno kuweka
ukwazo linalotumika hapo katika lugha ya kiyunani ni “Skandalon” ambalo kwa kingereza limetumika neno
“Stumbling-block” ambayo maana yake ni kuandaa au kutengeneza mazingira ya
kusababisha ugumu, au kumuingiza mtu katika mtego, kuhakikisha kuwa mtu
anaingia pagumu, au kusababisha mtu ajikwae, kwa hiyo walimu wa uongo au watu
wanaoifuata njia ya Balaamu, mojawapo ya kazi yao ni kutengeneza mazingira
yatakayowafanya watu wa Mungu au kanisa wajikute wapo pagumu, waingie mtegoni,
Skandalon ni kikwazo, ni kupotosha na kumuondoa mtu katika njia kwa kusudi la
kupoteza,ni kumuangusha mtu kutoka katika imani sahihi, Kristo Yesu alikwisha
kuonya juu ya changamoto hii ya kukosesha na kutangaza adhabu kali kwa mtu
atakayewakosesha watu wa Mungu, ukweli ni kuwa kunaweza kuwepo watu
watakaotenda dhambi katika kanisa na wakatubu na kupona, lakini kanisa
halipaswi kuvumialia watu wanaoleta mafundisho ya uongo na kuwaingiza watu
katika dhambi, au kuwatoa katika Imani ya kweli au kuwaacha wachukuliane na
dunia, ikiwa itakuwa hivyo hiyo ni njia ya Balaamu. Yesu Kristo pamoja na
mitume wake walikuwa wakali sana lilipokuja swala la kuwapotosha watu kutoka
katika njia ya kweli au injili ya kweli, dhambi inaweza kusameheka kirahisi kwa
sababu ni tatizo ndani ya mtu, lakini mafundisho ya uwongo hayawezi kusameheka
kwa urahisi kwa sababu yataongoza wengi katika uharibifu.
Mathayo 18:6 “bali atakayemkosesha mmojawapo wa
wadogo hawa waniaminio, yamfaa afungiwe shingoni jiwe kubwa la kusagia, na
kutoswa katika kilindi cha bahari.”
Wagalatia 1:8-9 “Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa
mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na
alaaniwe.Kama tulivyotangulia kusema, na sasa, nasema tena, mtu awaye yote
akiwahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe.”
5.
Balaamu
alikuwa na moyo wa kikatili - Balaamu
ni mfano wa watu ambao wanataka mambo yao yaende tu, na kuwatumikisha watu
wengine kwa nguvu lakini kwa kusudi la mafanikio yake bila kuwajali wale
anaowatumikisha, Balaamu hatajali kuwa wewe unakabiliwa na nini lakini
atakulazimisha ufanikishe jambo lake hata kama umemtumikia yeye kwa muda wa
kutosha na kwa uaminifu, moyo wa ukatili wa Balaamu unaonekana pale alipompiga
punda wake mpaka punda huyo akapewa uwezo wa kuzungumza akionyesha kuwa alikuwa
akiyaokoa maisha yake, Balaamu hakutaka hata kumshukuru Punda wake tofauti na
malaika wa Bwana ambaye alionyesha kujali kazi ya punda ya kuokoa maisha ya
Bwana wake, walimu wengi wa uongo ni makatili, huwatesa na kuwatumikisha watu
kwa kisingizo cha kumtumikia Mungu, watataka wewe ujitoe ukiwa na umasikini
wako lakini wao wanatajirika kila iitwapo leo, je watu huchuma zabibu katika
miiba? Aliwahi kuhoji Bwana Yesu, Mungu hajakuokoa uwe mtumwa wa mtu amekuokoa
uwe mtumishi wa Mungu na sisi tuhudumiane kwa upendo kila mmoja akimuhesabu
mwenzi wake kuwa bora kuliko nafsi yake
Hesabu 22:20-33 “Mungu akamjia Balaamu usiku,
akamwambia, Kwa kuwa watu hawa wamekuja kukuita, enenda pamoja nao; lakini neno
lile nitakalokuambia ndilo utakalolitenda, basi. Balaamu akaondoka asubuhi,
akatandika punda wake, akaenda pamoja na wakuu wa Moabu.Hasira ya Mungu ikawaka
kwa sababu alikwenda; malaika wa Bwana akajiweka njiani, ili kumpinga. Basi
alikuwa amepanda punda wake, na watumishi wake wawili walikuwa pamoja naye. Na
yule punda akamwona malaika wa Bwana amesimama njiani, na upanga wake mkononi
mwake amekwisha kuufuta; punda akageuka upande ili kuiacha njia, akaingia
shambani. Balaamu akampiga punda ili kumrejeza njiani. Kisha malaika wa Bwana
akasimama mahali penye bonde, katikati ya mashamba ya mizabibu, tena penye
kitalu upande huu na kitalu upande huu. Yule punda akamwona malaika wa Bwana,
akajisonga ukutani, akamseta Balaamu mguu wake, basi akampiga mara ya pili.
Malaika wa Bwana akaendelea mbele akasimama mahali pembamba sana, hapakuwa na
nafasi ya kugeukia mkono wa kuume, wala mkono wa kushoto. Yule punda akamwona
malaika wa Bwana, akajilaza chini ya Balaamu; hasira yake Balaamu ikawaka,
akampiga punda kwa fimbo yake. Bwana akakifunua kinywa cha yule punda, naye
akamwambia Balaamu, Nimekutenda nini, hata ukanipiga mara tatu hizi? Balaamu
akamwambia punda; Kwa sababu umenidhihaki; laiti ningekuwa na upanga mkononi
mwangu ningekuua sasa hivi. Yule punda akamwambia Balaamu, Je! Mimi si punda
wako, nawe umenipanda maisha yako yote hata leo? Nimezoea kukutenda hayo?
Akasema, La!nNdipo Bwana akafunua macho ya Balaamu akamwona malaika wa Bwana
amesimama njiani, ana upanga mkononi mwake, umekwisha kufutwa naye akainama
kichwa, akaanguka kifudifudi. Malaika wa Bwana akamwambia, Mbona umempiga punda
wako mara tatu hizi? Tazama mimi nimekuja ili kukupinga, kwa sababu njia yako
imepotoka mbele zangu, punda akaniona, akageuka upande mbele zangu mara tatu
hizi; kama asingejiepusha nami, bila shaka ningalikuua wewe, nikamwacha yeye
hai.”
Onyo la kutokuifuata njia ya Balaamu
Habari za Balaamu zinatufundisha
na kutuonya kuwa ni lazima wakristo wawe makini wao wenyewe kuyapima mafundisho
yaliyojaa ulimwengini katika nyakati za leo, sio kila mtu anaihubiri kweli, na
sio kila mtu ni salama, Yesu Kristo alichukizwa na mafundisho ya Balaamu ambayo
yalikuweko nyakati za kanisa la kwanza na kimsingi leo pia yapo ulimwenguni
hata kama hayaitwi kwa jina lake Balaamu, tamaa zao ziko katika kipato na
utajiri wa dunia hii, na hiki ndicho wanachijivunia na kukihubiri wala hakuna
mkazo wa kutafuta kwanza ufalme wa Mungu na haki yake, Balaamu alianza vizuri
lakini alishindwa mwishoni kwa sababu tamaa ilimzidi, na moyo wake ukadanganyika
kwa malipo na mapato ya aibu, ya aibu kwa sababu yalipatikana kinyume na
mapenzi ya Mungu au kinyume na njia zake
Ufunuo 2:14-16 “Lakini ninayo maneno machache juu yako, kwa kuwa unao huko
watu washikao mafundisho ya Balaamu, yeye aliyemfundisha Balaki atie ukwazo
mbele ya Waisraeli, kwamba wavile vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na
kuzini. Vivyo hivyo wewe nawe unao watu wayashikao mafundisho ya Wanikolai vile
vile.Basi tubu; na usipotubu, naja kwako upesi, nami nitafanya vita juu yao kwa
huo upanga wa kinywa changu.”
Maandiko yanatuonya kuwa wala
tusifuatishe namna ya dunia hii Warumi
12:2 “Wala
msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate
kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.”
Uko umuhimu mkubwa wa kuishi
maisha matakatifu, maisha ya haki na ya uaminifu kwa Mungu, Mafundisho yoyote
au mahubiri yoyote yanayotanguliza mahitaji ya kifedha kuliko kushughulika na
utakatifu na haki na uaminifu wa Mungu yanaweza kuwa yanaelekea katika njia ya
Balaamu, huu ni wakati ambao kanisa linapaswa kukemea kwa nguvu zote na
kuwaonya watu wawe makini na ukengeufu ambao sasa umeenea kila mahali duniani,
Sehemu yoyote ambayo hakuna upendo, kumejaa ubinafsi, na kujilimbikizia mali,
dhambi haikemewi, wenye dhambi hawasaidiwi, wanaibishwa, hawarejeshwi kwa Yesu,
watu wanafukuzwa, watumishi hawana mzigo na mshirika wala hawawafuatilii, wenye
fedha peke ndio wanaoheshimiwa, wachanga kiroho wanapewa vyeo, matajiri
wanapewa vyeo, kuna ugomvi na mafarakano ya kila namna, migogoro haiishi, watu
hawasameheani, hizo zote ni dalili za kutokuwepo kwa Mafundisho sahihi na kuwepo
kwa mafundisho ya Balaamu, Kanisa ni lazima kujitafakari na kujilinda. Na
kukazia kuwa Mungu ni Mtakatifu, na ametuitia utakatifu, ni lazima tufundishe
kwa mkazo huo na inawezekana kabisa watu wa Mungu kuishi maisha matakatifu,
ikiwa Ayubu aliweza kuishi kwa uadilifu wewe na mimi hatuwezi kushindwa kuishi
maisha ya uadilifu. Maandiko yanaonyesha kuwa inawezekana
1Petro 1:14-16 “Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza
za ujinga wenu; bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni
watakatifu katika mwenendo wenu wote;kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu
kwa kuwa mimi ni mtakatifu.”
Waebrania 12:14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo
utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;”
2Timotheo 4:1-4 “Nakuagiza mbele za Mungu, na mbele za Kristo Yesu,
atakayewahukumu walio hai na waliokufa; kwa kufunuliwa kwake na kwa ufalme wake;
lihubiri neno, uwe tayari, wakati ukufaao na wakati usiokufaa, karipia, kemea,
na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho. Maana utakuja wakati
watakapoyakataa mafundisho yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe
watajipatia waalimu makundi makundi, kwa kuwa wana masikio ya utafiti; nao
watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za uongo.”
Mwisho
Mungu atawahukumu walimu wa uongo
kama alivyomuhukumu Balaamu, Biblia inatuelezea kuwa hatimaye Balaamu aliuawa
na wana wa Israel wakikumbuka kuwa aliwakosesha katika tukio la Baal Peor Hivyo
waisrael waaminifu walihakikisha kuwa sio uwongo wake tu unafutwa lakini hata
na yeye nabii wa uongo anaondoka ili kukomesha mafundisho yasiyo sahihi, pamoja
na wale waliomuunga mkono, Kanisa ikiwa liko tunaloliamini kuwa ni sahihi
tulisimamie na ikiwa kuna kitu hakiko sahihi tumuombe Mungu na kutumia silaha
za kiroho kukiondoa, endapo utabaini kuwa fundisho Fulani sio sahihi usikae
kimya badala yake kwa upole na hekima rekebisha kwa mafundisho yaliyo sahihi,
wala usimshambulie mtu, lakini shambulia fundisho lisilo sahihi, na utawezaje
kujua fundisho lililo sahihi fika katika ibada za mafundisho kwa kusudi la
kuijua kweli, na ukitaka kujua watu wanaopenda mafundisho tembelea ibada za katikati
za mafundisho ndio utawajua wakristo wa kweli wanaotaka kujifunza na kukua
kiroho ili waweze kuwa msaada kwa wengine na kizazi kijacho.
Kumbukumbu 23:3-5 “Mwamoni wala Mmoabi wasiingie katika mkutano wa Bwana; wala
hata kizazi cha kumi mtu wao asiingie katika mkutano wa Bwana milele; kwa
sababu hapo mlipotoka Misri hawakuwalaki na chakula wala maji njiani; na kwa
kuwa walimwajiri juu yako Balaamu mwana wa Beori kutoka Pethori iliyo
Mesopotamia, aje akuapize. Lakini Bwana, Mungu wako, hakukubali kumsikiza huyo
Balaamu; Bwana, Mungu wako, aliyageuza yale maapizo kuwa ni baraka, kwa vile
alivyokupenda Bwana, Mungu wako.”
Yoshua 13:22 “Balaamu naye, huyo mwana wa Beori, huyo mchawi, wana wa
Israeli walimwua kwa upanga kati ya hao wengine waliowaua.”
Na. Rev Mkombozi Samuel Kamote
Maoni 2 :
Hongera sana mtumishi. Hakika ujumbe ni mzuri sana. Mungu aendelee kukulinda ili tuzidi kupata maarifa .
Asante sana Mtu wa Mungu Kwa kunitia moyo, endelea kuniombea neema Niko tayari kuendelea kutumiwa kama chombo Kwa ajili ya mwili wa Kristo
Chapisha Maoni