Jumatano, 29 Januari 2025

Kama umande wa Hermoni!


Zaburi 133:1-3 “Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa umoja. Ni kama mafuta mazuri kichwani, Yashukayo ndevuni, ndevu za Haruni, Yashukayo mpaka upindo wa mavazi yake. Kama umande wa Hermoni ushukao milimani pa Sayuni. Maana ndiko Bwana alikoamuru baraka, Naam, uzima hata milele.”



Utangulizi:


Moja ya siri kubwa sana ya mafanikio ya kiroho na Baraka nyingi sana katika jamii yoyote ile, iwe Taifa, Kanisa, Familia, Ndoa, taasisi, na kadhalika yote yenye kujumuisha na kuwakutanisha watu Pamoja, umoja ni mojawapo ya nyenzo muhimu sana ya kusababisha Baraka nyingi. 


Mtumishi wa Mungu Daudi alilijua hili na akalizungumzia katika Zaburi ya 133, na kutuonyesha kuwa umoja unaleta upako, umoja unaleta Baraka, umoja unaleta uzima, tena hata uzima wa milele, Kimsingi Roho Mtakatifu hawezi kutenda kazi mahali ambapo kuna utengano, ubaguzi, upendeleo, ubinafsi, mafarakano na kukosekana kwa umoja, kwa kulijua hili Hata Bwana wetu Yesu Kristo aliwaombea wanafunzi wake yaani ikiwa ni pamoja na wewe na mimi kuwa tuwe na umoja 


Yohana 17:11-12. “Wala mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo.Nilipokuwapo pamoja nao, mimi naliwalinda kwa jina lako ulilonipa, nikawatunza; wala hapana mmojawapo wao aliyepotea, ila yule mwana wa upotevu, ili andiko litimie.” 


Mpango wangu leo sio kuzungumzia kuhusu umoja, lakini Bwana amenituma kuzunguzia faida za umoja, au matokeo yanayoletwa na Umoja, Daudi anaona wema unaotokana na watu kukaa kwa umoja na anaelezea matokeo yake, au faida zake na anatoa mifano miwili, mmoja ni Mafuta mazuri kutoka kichwani, na pili umande wa Hermoni unaoshukia Sayuni, kimsingi Daudi anazungumzia Upako na Umande ambao ni matokeo ya Baraka za Roho Mtakatifu. Na kubwa zaidi nitazungumzia hili la “Kama umande wa Hermoni” tutajifunza somo hili kama umande wa Hermoni kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-


Umuhimu wa umande.

Kama umande wa Hermoni.

Jinsi ya kufunikwa na umande.



Umuhimu wa umande.

Ni muhimu kufahamu kuwa umande katika lugha ya kiebrania unaitwa “ţal” kwa kiingereza unaitwa “dew” umande una umuhimu mkubwa sana katika nchi sawasawa tu na mvua ilivyo na umuhimu, wale wanaoishi katika inchi zenye mfumo wa kuweko kwa umande watakuwa wanafahamu jinsi umande ulivyo wa muhimu, inchi ikikosa mvua hakuna tofauti na inchi ikikosa umande, Wayahudi walikuwa na uelewa mkubwa sana kuhusu umuhimu wa umande, ukweli ni kuwa kunyimwa mvua pamoja na umande ilikuwa ni hukumu kubwa sana ni janga


1Wafalme 17:1 “Basi Eliya Mtishbi, wa wageni wa Gileadi, akamwambia Ahabu, Kama Bwana, Mungu wa Israeli, aishivyo, ambaye ninasimama mbele zake, hakutakuwa na UMANDE wala mvua miaka hii, ila kwa neno langu.”


Umande katika historia ya Israel uliwakilisha uwepo wa Mungu, umande ulikuwa na umuhimu mkubwa sana kama ilivyo mvua, ulikuwa na manufaa makubwa sana kwao, umande uliifanya nchi iwe na utulivu na kupoa kutoka katika joto la jangwa, ulileta utulivu kwa wanadamu, umande huifanya nchi iwe na hali joto lenye kupendeza sana, umande unaifanya ardhi iwe tayari kupokea mbegu njema na kustawi, umande kuondoka ilikuwa sawa tu na uwepo wa Mungu kuondoka, Mungu alikuwa amewathibitishia Israel kuwa atakuwa pamoja nao kama umande, umande unapokuwepo kila kitu kinastawi na umande unapokauka hali huwa mbaya 


Hosea 14:4-6 “Mimi nitawaponya kurudi nyuma kwao; nitawapenda kwa ukunjufu wa moyo; kwa maana hasira yangu imemwacha. NITAKUWA KAMA UMANDE kwa Israeli; naye atachanua maua kama nyinyoro, na kuieneza mizizi yake kama Lebanoni. Matawi yake yatatandaa, na uzuri wake utakuwa kama uzuri wa mzeituni, na harufu yake kama Lebanoni.”


Israel walipokuwa jangwani wote tunakumbuka jinsi Mungu alivyowalisha kwa mana, lakini wote tunakumbuka kuwa mana ilishuka pamoja na umande, na umande ulikuwa ukiondoka basi muda wa kuokota mana ungeondoka na umande, na jua lingechukua nafasi yake na hivyo kusingeliweko na mana tena, kwa hiyo ujio wa Mana wakati wote uliambatana na umande 


Kutoka 16:13-15 “Ikawa wakati wa jioni, kware wakakaribia, wakakifunikiza kituo; na wakati wa asubuhi umande ulikuwa juu ya nchi pande zote za kituo. NA ULIPOINUKA ULE UMANDE uliokuwa juu ya nchi, kumbe! Juu ya uso wa bara kitu kidogo kilichoviringana, kidogo kama sakitu juu ya nchi. Wana wa Israeli walipokiona, wakaambiana, Nini hiki? Maana hawakujua ni kitu gani. Musa akawaambia, Ndio mkate ambao BWANA amewapa ninyi, mle.”


Hesabu 11:7-9 “Na hiyo mana ilikuwa mfano wa chembe za mtama na kuonekana kwake kulikuwa kama kuonekana kwake bedola. Watu wakazunguka-zunguka na kuikusanya, kisha wakaisaga kwa mawe ya kusagia, au kuitwanga katika vinu, kisha wakaitokosa nyunguni, na kuandaa mikate; na tamu yake ilikuwa kama tamu ya mafuta mapya. UMANDE ULIPOYAANGUKIA MARAGO WAKATI WA USIKU, HIYO MANA ILIANGUKA PAMOJA NAO.”


Wana wa Israel walifahamu umuhimu wa umande, Umande ulikuja na mana, na ni umande ulioifanya mana isichafuke japo iliangukia juu ya nchi, lakini nchi haikuweza kuichafua mana kwa sababu ilikuja na UMANDE, Endapo wote tunakubaliana kuwa Mana ni mkate kutoka mbinguni na unamwakilisha Yesu, basi vile vile utakubaliana nami kuwa Umande unawakilisha uwepo wa Roho Mtakatifu, Hakuna Baraka kubwa kwa kanisa kama kuwa na Roho Mtakatifu, yeye analeta wakati wa kuburudishwa na kuondoa kila aina ya hali ya ukavu wa kiroho, katika kanisa na kutuletea uamsho na wakati mzuri wa kufanya naye kazi, bila kupigwa na jua, sasa kwa mujibu wa Daudi kama watu wanataka kuburudishwa na kufurahia Baraka za Mungu siri imejificha katika wema wa kukaa kwa umoja, na hii ndio kanuni muhimu ya kanisa kuwa na uamsho, na zaidi ya yote kama ulijifunza kuwa katika alama za Roho Mtakatifu ni pamoja na njiwa, moto, maji, mafuta, wingu, kisima, mito ya maji, na upepo, leo nakuongezea na UMANDE. 


Kama umande wa Hermoni.


Zaburi 133:1-3 “Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa umoja. Ni kama mafuta mazuri kichwani, Yashukayo ndevuni, ndevu za Haruni, Yashukayo mpaka upindo wa mavazi yake. KAMA UMANDE WA HERMONI ushukao milimani pa Sayuni. Maana ndiko Bwana alikoamuru baraka, Naam, uzima hata milele.”


Kwa nini kama umande wa Hermoni? Mlima Mlima Hermoni ni Moja ya safu za milima yenye urefu wa maili 30, na upana wa maili 15 urefu wake kwenda juu ni futi zaidi ya 9000 kutoka usawa wa bahari, safu hii ya milima imefunikwa na theluji kama unavyoweza kuona pichani, Milima hii iko kaskazini mashariki mwa Israel katika mpaka wa Syria na Lebanon Mlima huu una utajiri mkubwa sana wa kusababisha mvua, lakini pia una chemichemi za maji na zaidi ya yote ni chanzo kikuu cha mto Yordani, lakini mlima huu pia husababisha umande katika Sayuni au Israel kwa hiyo Daudi anauona mlima huu kama chanzo cha Baraka kubwa sana kwa Israel, Daudi anaona kuwa watu wakikaa kwa umoja Mungu huachilia Baraka zake na ustawi sawa na mlima huu unavyotumiwa na Mungu kuwa chanzo kikubwa cha mafanikio ya kilimo kwa Israel, Ni katika mlima huu pia ndiko inakohisiwa kuwa Yesu alipanda na wanafunzi wake na kugeuka sura yake MLIMA MREFU FARAGHANI


Mathayo 17:1-8 “Na baada ya siku sita Yesu akawatwaa Petro, na Yakobo, na Yohana nduguye, akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani; akageuka sura yake mbele yao; uso wake ukang'aa kama jua, mavazi yake yakawa meupe kama nuru. Na tazama, wakatokewa na Musa na Eliya, wakizungumza naye. Petro akajibu akamwambia Yesu, Bwana, ni vizuri sisi kuwapo hapa; ukitaka, nitafanya hapa vibanda vitatu, kimoja chako wewe, na kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya. Alipokuwa katika kusema, tazama, wingu jeupe likawatia uvuli; na tazama, sauti ikatoka katika lile wingu, ikasema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye. Na wale wanafunzi waliposikia, walianguka kifulifuli, wakaogopa sana.”


2Petro 1:16-18 “Maana hatukufuata hadithi zilizotungwa kwa werevu, tulipowajulisha ninyi nguvu zake Bwana wetu Yesu Kristo na kuja kwake; bali tulikuwa tumeuona wenyewe ukuu wake. Maana alipata kwa Mungu Baba heshima na utukufu, hapo alipoletewa sauti iliyotoka katika utukufu mkuu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye. Na sauti hiyo sisi tuliisikia ikitoka mbinguni tulipokuwa pamoja naye katika mlima ule mtakatifu.” 


Kwa ujumla Ustawi mzima wa Israel unategemea sana mlima wa Hermoni, na ndio maana Daudi anasema huko ndiko Mungu alikoziamuru Baraka, na kwanini anasema hivyo kwa sababu umande pia katika Israel unaungamanishwa na baraka, hakuna mahali popote pale katika Biblia mtu alibarikiwa kisha neno UMANDE lisitajwe, wakati wote wazee katika Biblia walipotamka baraka walimtamkia mtu kuwa na UMANDE kama neema na baraka kubwa sana kutoka mbinguni kwa hiyo kutamkiwa ya UMANDE katika maisha ya mwanadamu ni ishara ya Baraka ona:-


Mwanzo 27:27-29 “Akakaribia akambusu. Naye akasikia harufu ya mavazi yake, akambariki akasema, Tazama, harufu ya mwanangu Ni kama harufu ya shamba alilolibariki BWANA. MUNGU NA AKUPE YA UMANDE WA MBINGU, Na ya manono ya nchi, Na wingi wa nafaka na mvinyo. Mataifa na wakutumikie Na makabila wakusujudie, Uwe bwana wa ndugu zako, Na wana wa mama yako na wakusujudie. Atakayekulaani alaaniwe, Na atakayekubariki abarikiwe.” 


Mwanzo 27:39 “Esau akamwambia babaye, Una mbaraka mmoja tu, babangu? Unibariki mimi, mimi nami, Ee babangu. Esau akapaza sauti yake, akalia. Isaka, baba yake, akajibu, akamwambia, Angalia, penye manono ya nchi patakuwa makao yako, NA PENYE UMANDE WA MBINGU UNAOTOKA JUU.”


Kumbukumbu 33:13-15 “Na Yusufu akamnena, Nchi yake na ibarikiwe na Bwana; Kwa vitu vya thamani vya mbinguni, KWA HUO UMANDE, Na kwa kilindi kilalacho chini, Na kwa vitu vilivyo bora vya matunda ya jua, Na kwa vitu vilivyo bora vya maongeo ya miezi, Na kwa vitu viteule vya milima ya kale, Na kwa vitu vilivyo bora vya vilima vya milele,”


Mika 5:7-9 “Na hayo mabaki ya Yakobo yatakuwa kati ya kabila nyingi MFANO WA UMANDE UTOKAO KWA BWANA, mfano wa manyunyu katika manyasi; yasiyomngojea mtu, wala kuwakawilia wanadamu.Na hayo mabaki ya Yakobo yatakuwa kati ya mataifa, kati ya kabila nyingi, mfano wa simba kati ya wanyama wa msituni, kama mwana-simba kati ya makundi ya kondoo, ambaye, akiwa anapita katikati, hukanyaga-kanyaga na kurarua-rarua, wala hakuna wa kuokoa.Mkono wako na uinuliwe juu ya adui zako, na adui zako wote wakauliwe mbali.” 


Ayubu 29:19-20 “Shina langu limeenea hata kufika majini, NA UMANDE hukaa usiku kucha katika matawi yangu; Utukufu wangu utakuwa mpya kwangu, Na uta wangu hurejezwa upya mkononi mwangu.”


Unaona? Kwa hiyo Umande ni alama ya Baraka, umande ni alama ya ustawi, umande ni alama ya kuburudishwa, umande ni alama ya Roho Mtakatifu na matunda yake, Baraka hizi tunaweza kuziona kwa sharti la kukaa pamoja na kwa umoja, hatuwezi kukaa pamoja na kwa umoja kama hakuna msamaha, kama hakuna umoja, kama hakuna upendo, kama hakuna amani, kama hakuna furaha, kama hakuna kiasi, kama hakuna adabu, kama hakuna uvumilivu, kama hakuna kutokuhesabu mabaya, kama hakuna kuchukuliana, kama hakuna kujaliana, kama hakuna kula pamoja, kama hakuna ushirikiano, kama kuna ubinafsi, kama kuna mimi kwanza, kama kuna kujiona bora, kama kuna kusengenyana, kama kuna kuchafuana, kama kuna kuchokana, kama hakuna fadhili, kama kuna husuda, kama kuna kujivuna, kama kuna kiburi, kama kuna uchungu, kama kuna udhalimu, kama hakuna ukweli, kama kuna fitina, kama kuna majungu, kama kuna wivu, kama kuna uadui, kama kuna uzushi, kama kuna husuda, kama kuna kurogana na kuharibiana, kama kuna mashindano, Mungu hataweza kuamuru Baraka zake kuja kwetu kama hatuna ukomavu wa kutosha na kufikia hatua ya kuchukuliana unataka Baraka za Mungu zije kwako kumbuka, unataka Mungu aziamuru Baraka kumbuka kumbuka, katika Taifa, katika Kanisa, katika ndoa, katika taasisi, katika mashirika, katika kampuni, katika biashara, kote tutaziona Baraka za Mungu ikiwa tu tutakaa kwa umoja, Mungu ataachilia upako wake kwa kila kiungo katika mwili wa Kristo na ataachilia Baraka zake kama umande wa Hermoni katika maisha yetu yote   


Jinsi ya kufunikwa na umande.


Mtafute Mungu kwanza – Kama hauna uhusiano mzuri na Mungu hakikisha kuwa unautafuta kwanza uso wake, unatafuta kuwa na uhusiano mzuri na Mungu, yeye ndiye chanzo cha Baraka zote yaani UMANDE endapo utautafuta uso wake hakuna kitu ambacho Mungu atakunyima kwa sababu Mungu amekusudia kumbariki kila mmoja 


Mathayo 6:31-33 “Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.”


Mwabudu yeye – Ulimwengu wa roho unaachilia vitu kwa ibada ukimuabudu shetani atakupa heshima, mali na utajiri wa dunia lakini nafsi yako itaangamia, lakini ukimtumikia Mungu na kumtii hiyo ndiyo ibada ataziachilia Baraka zake na zitakupata 


Mathayo 4:8-10 “Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mlima mrefu mno, akamwonyesha milki zote za ulimwengu, na fahari yake, akamwambia, Haya yote nitakupa, ukianguka kunisujudia. Ndipo Yesu alipomwambia, Nenda zako, Shetani; kwa maana imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake.”


Kumbukumbu 28:1-8 “Itakuwa utakaposikia sauti ya Bwana, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo Bwana, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani; na baraka hizi zote zitakujilia na kukupata usikiapo sauti ya Bwana, Mungu wako. Utabarikiwa mjini, utabarikiwa na mashambani. Utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, na uzao wa wanyama wako wa mifugo, maongeo ya ng'ombe wako, na wadogo wa kondoo zako. Litabarikiwa kapu lako, na chombo chako cha kukandia unga. Utabarikiwa uingiapo, utabarikiwa na utokapo. Bwana atawafanya adui zako wainukao juu yako kupigwa mbele yako; watakutokea kwa njia moja, lakini watakimbia mbele yako kwa njia saba. Bwana ataiamuru baraka ije juu yako katika ghala zako, na mambo yote utakayotia mkono wako; naye atakubarikia katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako.”  


Kuwa na Amani na watu wote – Uhusiano wetu hauwezi kuwa kamili kama tutakuwa na madai kuwa tunampenda Mungu huku hatuwajali wengine, huna Amani na watu wengine maana yake hakuna umoja, Mungu hawezi kuachilia Baraka zake kwa watu wenye mafarakano, ndio maana moja ya silaha kubwa anayoitumia shetani katika kanisa, taifa, familia, taasisi na kdhalika ni pamoja na kuondoa umoja. Kwa kuvuruga Amani.


Waebrania 12:14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;”


Acha kuwa mwilini - Acha ukristo wa mwilini, jikaze, onyesha ukomavu, jionyeshe kuwa mwanaume, onyesha kukua, uwe na uwezo wa kusamehe na kuachilia, wewe kila siku una yale yale tu, fungua moyo wako kubali kukua kiroho, usiweke mtu moyoni, usimchafue nduguyo, kuwa na amani na watu wote maana yake hata wale waliokukosea, wakati mwingine usisubiri waje kukuomba msamaha wewe achilia au nenda kaombe Amani usijifungie kwenye gereza la kukosa mafanikio utajichelewesha

 

1Wafalme 2:1-3 “Basi siku ya kufa kwake Daudi ikakaribia, akamwusia Sulemani mwanawe, akasema, Mimi naenda njia ya ulimwengu wote; basi uwe hodari, ujionyeshe kuwa mwanamume; uyashike mausia ya Bwana, Mungu wako, uende katika njia zake, uzishike sheria zake, na amri zake, na hukumu zake, na shuhuda zake, sawasawa na ilivyoandikwa katika torati ya Musa, upate kufanikiwa katika kila ufanyalo, na kila utazamako;”


1Wakorintho 3:1-3 “Lakini, ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama na watu wenye tabia ya rohoni, bali kama na watu wenye tabia ya mwilini, kama na watoto wachanga katika Kristo.Naliwanywesha maziwa sikuwalisha chakula; kwa kuwa mlikuwa hamjakiweza. Naam, hata sasa hamkiwezi,kwa maana hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya mwilini. Maana, ikiwa kwenu kuna husuda na fitina, je! Si watu wa tabia ya mwilini ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu?  

  

Acha uchoyo uwe mtoaji – Neno la Mungu limesema ni heri kutoa kuliko kupokea, wewe hutoi, umekuwa mchoyo kila kitu kizuri unajilimbikizia na kutaka kiwe chako, unataka Baraka za Mungu ili iweje? Ili uringishie watu? Ili uwakanyage watu kichwani? Ili uwe na mamalaka juu ya watu? Mungu amekusudia kutubariki ili tuwe baraka Kwa wengine.


Matendo 20:33-35 “Sikutamani fedha wala dhahabu, wala mavazi ya mtu. Ninyi wenyewe mnajua ya kuwa mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami.Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea.” 


Tumejifunza kuwa UMANDE unawakilisha Baraka za Mungu na baraka hizi za Mungu ni pamoja na uwepo wake na upako wa Roho Mtakatifu, lakini ili tuweze kufunikwa na baraka hizo ni lazima tuyatende mambo yale yote ambayo katika jamii yanatufanya tuwe na umoja na amani na kuacha yale yote yanayotufarakanisha tukiwa na umoja katika jambo lolote lile tutafanikiwa, kwa umri wangu huu nimeona taasisi zikifa, zikiharibika, na kudumaa kwa sababu tu watu walitanguliza maslahi yao mbele na wakaacha kuwajali wengine na wakavuruga umoja na kuondoa Amani na matokeo yake ikawa ni ukiwa, Mungu anapoona ya kuwa hatumjali yeye wala hatutendeani kwa hisani basi, atamtuma nabii wake ambaye atatangaza kuwa hapatakuwa na mvua wala umande………  


Na. Mchungaji Innocent Kamote


Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Hakuna maoni: