Jumatano, 22 Januari 2025

Mungu ajibuye kwa Moto!


1Wafalme 18:20-24 “Basi, Ahabu akapeleka watu kwa wana wa Israeli wote, akawakusanya manabii pamoja katika mlima wa Karmeli. Naye Eliya akawakaribia watu wote, akanena, Mtasita-sita katikati ya mawazo mawili hata lini? Bwana akiwa ndiye Mungu, mfuateni; bali ikiwa Baali ni Mungu, haya! Mfuateni yeye. Wale watu hawakumjibu neno. Ndipo Eliya akawaambia watu, Mimi nimesalia, mimi peke yangu, nabii wa Bwana; lakini manabii wa Baali ni watu mia nne na hamsini. Kwa hiyo na watutolee ng'ombe wawili; wao na wajichagulie ng'ombe mmoja, wamkate-kate na kumweka juu ya kuni, wasitie moto chini; nami nitamtengeza huyo ng'ombe wa pili, na kumweka juu ya kuni, wala sitatia moto chini. Nanyi ombeni kwa jina la mungu wenu, nami nitaomba kwa jina la Bwana; na Mungu yule ajibuye kwa moto, na awe ndiye Mungu. Watu wote wakajibu wakasema, Maneno haya ni mazuri.



Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa mojawapo ya njia ya kupambana na manabii wa uongo, sio tu kuwajibu kwa mafundisho peke yake, lakini ni pamoja na ishara na miujiza inayoambatana na utendaji wa Roho Mtakatifu, katika maisha ya watumishi na Kanisa kwa ujumla. Wakati mwingine ili Mungu wa kweli apate kujulikana ni lazima ishara mashuhuri zifanyike, ili watu wapate kuamini kuwa Mungu ni mwenye nguvu, Ishara na miujiza ni ya Muhimu sana katika kuthibitisha uweza na nguvu za Mungu.

Kutoka 7:10-12 “Basi Musa na Haruni wakaingia kwa Farao, wakafanya vivyo kama BWANA alivyowaambia; Haruni akaibwaga fimbo yake chini mbele ya Farao, mbele ya watumishi wake, ikawa nyoka. Ndipo Farao naye akawaita wenye akili na wachawi; na hao waganga wa Misri wakafanya vivyo kwa uganga wao. Wakabwaga chini kila mtu fimbo yake, nazo zikawa nyoka; lakini fimbo ya Haruni ikazimeza fimbo zao.”

Mungu amewapa watumishi wake Ishara na miujiza kwa uweza wa Roho wake Mtakatifu kwaajili ya kusaidia watu lakini wakati mwingine kama ishara kwa wasioamini wapate kuamini na kuondoka katika hali ya mashaka na kusita sita, Wakati wa Nabii Eliya jamii kubwa ya wana wa Israel walikuwa wamepoteza njia sahihi ya kumuabudu Mungu na wengi walikuwa wamegeukia miungu mingine wakiabudu miungu ya kikanaani akiwemo Baali, kwa hiyo ulifikia wakati wakaanza kuchanganya ibada za Mungu wa kweli na ibada za Baali, kimsingi walikuwa ni watu wenye kusitasita katika mawazo mawili. Eliya akilielewa hili huku moyoni mwake akiwa na agizo la kuirejesha mioyo ya wana wa Israel katika ibada ya Mungu wa kweli yeye alitoa wazo, ambalo liliungwa mkono na manabii wa Baali na watu wote kwamba ufikie wakati sasa Mungu yule atakayejibu kwa Moto huyo awe ndiye Mungu wa kufuatwa na kuabudiwa. Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-


Mtasita-sita katikati ya mawazo mawili hata lini?

Mungu yule ajibuye kwa moto

Mwisho wa Manabii wa uongo


Mtasita-sita katikati ya mawazo mawili hata lini?

Moja ya mambo ambayo yanamuudhi sana Mungu ni pamoja na kuwa na mtu au watu wenye kusitasita, Mungu anavutiwa sana na mtu au watu wanaofanya maamuzi, Mara kwa mara Mungu kupitia watumishi wake kadhaa amewahi kuwapa changamoto wanadamu kufanya maamuzi ya kuchagua, kila siku katika maisha yetu tunaweza au tumepewa kuchagua, unaweza kuchagua uzima au mauti, unaweza kuchagua laana au baraka, unaweza kuchagua Mungu au miungu, unaweza kuchagua kuwa moto au baridi, Kuchagua upande mmoja ndio njia sahihi, na kusisita katika mawazo mawili sio sahihi na ni jambo ambalo linamchukiza sana Mungu na kumnyima furaha.

Kumbukumbu 30:15-16. “Angalia, nimekuwekea leo mbele yako uzima na mema, na mauti na mabaya; kwa hivi nikuagizavyo leo kumpenda Bwana, Mungu wako, kuenenda katika njia zake, na kushika maagizo yake, na amri zake, na hukumu zake, upate kuwa hai na kuongezeka; Bwana, Mungu wako, apate kukubarikia katika nchi uingiayo kuimiliki.”

Kumbukumbu 11:26-28 “Angalieni, nawawekea mbele yenu hivi leo baraka na laana;baraka ni hapo mtakapoyasikiza maagizo ya Bwana, Mungu wenu, niwaagizayo leo; na laana ni hapo msiposikiza maagizo ya Bwana, Mungu wenu, mkikengeuka katika njia niwaagizayo leo, kwa kuandama miungu mingine msiyoijua.”

Yoshua 24:14-15 “Basi sasa mcheni Bwana, mkamtumikie kwa unyofu wa moyo na kwa kweli; na kuiweka mbali miungu ambayo baba zenu waliitumikia ng'ambo ya Mto, na huko Misri; mkamtumikie yeye Bwana.Nanyi kama mkiona ni vibaya kumtumikia Bwana, chagueni hivi leo mtakayemtumikia; kwamba ni miungu ile ambayo baba zenu waliitumikia ng'ambo ya Mto, au kwamba ni miungu ya wale Waamori ambao mnakaa katika nchi yao; lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia Bwana.” 

Ufunuo 3:15-16 “Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto. Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.” 

Waebrania 10:38 “Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani; Naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye.

Maisha yetu ni uchaguzi, Maandiko yanashauri tumchague Mungu lakini tusibaki katikati, kumchagua Mungu ni Baraka kubwa sana na kuacha kumchagua Mungu ni laana, Mungu hapandezwi wala havutiwi na watu wanaositasita, wala havutiwi na watu vuguvugu, Mungu anataka tuwe moto na tumchague yeye kumchagua yeye ni kuchagua mafanikio, tatizo lililoko leo halina tofauti na tatizo lililokuweko wakati wa Eliya, jamii ya watu katika Israel walikuwa wanasitasita, walikuwa vugu vugu, walikuwa wakichanganya ibada ya Mungu mwenyezi na miungu ya Kanaani ya Baali, Eliya alitokea kama nabii aliyesalia peke yake na wengi walikuwa wakimuabudu Baali, akaamua kuweka changamoto ya kitaifa, kuanzia na mfalme kwamba watu wote wafanye uamuzi na Mungu halisi wa kweli ajulikane kuwa Mungu ili afuatwe, Eliya alikuja sio tu na swali lakini alikuja na suluhu ya changamoto iliyokuwa inawakabili watu, Eliya alisema

 “manabii wa Baali ni watu mia nne na hamsini. Kwa hiyo na watutolee ng'ombe wawili; wao na wajichagulie ng'ombe mmoja, wamkate-kate na kumweka juu ya kuni, wasitie moto chini; nami nitamtengeza huyo ng'ombe wa pili, na kumweka juu ya kuni, wala sitatia moto chini” 

katika mjadala huu na hoja hii Eliya aliwapa changamoto kuwa moto utoke kwa Mungu, kama manabii wa baali wana mungu kwa kweli basi sadaka yao itatiwa moto na Baali na kama Mungu anayewakilishwa na Eliya ni wa kweli basi sadaka yake itatiwa moto na Mungu mwenyezi na wazo hilo lilikuwa jema na lilikubalika ili kuumaliza utata.

1Wafalme 18:20-24 “Basi, Ahabu akapeleka watu kwa wana wa Israeli wote, akawakusanya manabii pamoja katika mlima wa Karmeli. Naye Eliya akawakaribia watu wote, akanena, Mtasita-sita katikati ya mawazo mawili hata lini? Bwana akiwa ndiye Mungu, mfuateni; bali ikiwa Baali ni Mungu, haya! Mfuateni yeye. Wale watu hawakumjibu neno. Ndipo Eliya akawaambia watu, Mimi nimesalia, mimi peke yangu, nabii wa Bwana; lakini manabii wa Baali ni watu mia nne na hamsini. Kwa hiyo na watutolee ng'ombe wawili; wao na wajichagulie ng'ombe mmoja, wamkate-kate na kumweka juu ya kuni, wasitie moto chini; nami nitamtengeza huyo ng'ombe wa pili, na kumweka juu ya kuni, wala sitatia moto chini. Nanyi ombeni kwa jina la mungu wenu, nami nitaomba kwa jina la Bwana; na Mungu yule ajibuye kwa moto, na awe ndiye Mungu. Watu wote wakajibu wakasema, Maneno haya ni mazuri.

Mungu yule ajibuye kwa moto

Eliya alikuwa anajua kwamba ili kumaliza utata kuna umuhimu wa kufanya ishara mashuhuri, Na muujiza huu ambao ulifanyika kando ya mlima Karmel ulikuwa ni wa muhimu sana na umeweka alama ya kipekee katika historia ya Israel, kutokana na umashuhuri wake, Karmel kwa kiebrania (ho Kármelos maana yake ni bustani ya matunda hata hivyo kutokana na ishara kubwa na muujiza uliofanyioka hapo watu wengi sana hupaita mahali hapo Mlima wa Moto) Ishara mashuhuri inapofanyika huwanyima maadui uwezo wa kujibu hoja na kukosa mashiko ya kile wanachokisimamia, Ishara mashuhuri ni lile tukio ambalo Mungu hulifanya na macho ya watu wote wakishuhudia kwa macho ya nyama yaani sio kwa kutilia shaka, Mfano Yesu alipomfufua Lazaro, ambaye alikuwa amezikwa siku nne na taarifa zake zilijulikana sana, au mfano wa Mlemavu ambaye Petro na Yohana walimsaidia kwenye mlango mzuri ambaye alikuwa anajulikana na jamii nzima kuwa anaomba omba, watu wale ambao dunia inawajua, mji unajua, nchi inajua na taifa linajua na maadui wa Mungu hawawezi kuikana ishara hiyo hiyo huitwa ishara mashuhuri, hiki ndicho ambacho Eliya alikuwa amekikusudia kifanyike ili dunia yote na taifa zima liweze kukubali na kuamini ya kwamba Adonai ndiye Mungu wa kweli ilikuwa ni lazia lifanyike tukio ambalo sio la kawaida.

Matendo 4:15-16 “Wakawaamuru kutoka katika baraza, wakafanya shauri wao kwa wao, wakisema, Tuwafanyie nini watu hawa? Maana ni dhahiri kwa watu wote wakaao Yerusalemu ya kwamba ishara mashuhuri imefanywa nao, wala hatuwezi kuikana.” 

Jamii nzima ilikubaliana na tukio hilo na manabii wa Baali walikuwa wakwanza kuomba nadhani ilikuwa asubuhi kuanzia mida ya saa tatu mpaka jioni kwenye saa tisa, na kisha saa tisa Eliya alichukua nafasi naye na kuomba na hivi ndivyo mambo yalivyokuwa:-

1Wafalme 18:25-39 “Eliya akawaambia manabii wa Baali, Jichagulieni ng'ombe mmoja, mkamtengeze kwanza; maana ninyi ndio wengi; mkaliitie jina la mungu wenu, wala msitie moto chini. Wakamtwaa yule ng'ombe waliyepewa, wakamtengeza, wakaliitia jina la Baali tangu asubuhi hata adhuhuri, wakisema, Ee Baali, utusikie. Lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu. Nao wakaruka-ruka juu ya madhabahu waliyoifanya. Ikawa, wakati wa adhuhuri, Eliya akawafanyia dhihaka, akasema, Mwiteni kwa sauti kuu; maana ni mungu huyo; labda anazungumza, au ana shughuli, au anasafiri, au labda amelala, sharti aamshwe. Wakapiga kelele, wakajikata-kata kwa visu na vyembe kama ilivyo desturi yao, hata damu ikawachuruzika. Ikawa, wakati wa adhuhuri ulipopita, walitabiri hata wakati wa kutoa dhabihu ya jioni; lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu, wala aliyeangalia. Kisha Eliya akawaambia watu wote, Nikaribieni mimi. Watu wote wakamkaribia. Akaitengeneza madhabahu ya Bwana iliyovunjika. Eliya akatwaa mawe kumi na mawili, kwa hesabu ya kabila za wana wa Yakobo, aliyejiliwa na neno la Bwana na kuambiwa, Jina lako litakuwa Israeli. Naye akaijenga madhabahu kwa mawe hayo katika jina la Bwana; akafanya mfereji, kama wa vipimo viwili vya mbegu, ukiizunguka madhabahu. Kisha akazipanga zile kuni, akamkata yule ng'ombe vipande vipande, akaviweka juu ya kuni. Akasema, Jazeni mapipa manne maji, mkayamwage juu ya sadaka ya kuteketezwa, na juu ya kuni. Akasema, Fanyeni mara ya pili. Wakafanya mara ya pili. Akasema, Fanyeni mara ya tatu. Wakafanya mara ya tatu. Yale maji yakaizunguka madhabahu; akaujaza mfereji maji. Ikawa, wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, Eliya nabii akakaribia, akasema, Ee Bwana, Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Israeli, na ijulikane leo ya kuwa wewe ndiwe Mungu katika Israeli, na ya kuwa mimi ni mtumishi wako, na ya kuwa nimefanya mambo haya yote kwa neno lako. Unisikie, Ee Bwana, unisikie, ili watu hawa wajue ya kuwa wewe, Bwana, ndiwe Mungu, na ya kuwa wewe umewageuza moyo wakurudie. Ndipo moto wa Bwana ukashuka, ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na kuni, na mawe, na mavumbi, ukayaramba yale maji yaliyokuwamo katika mfereji. Na watu wote walipoona, wakaanguka kifudifudi; wakasema, Bwana ndiye Mungu, Bwana ndiye Mungu.”

Unaona? Eliya hakufanya mambo haya kwa nafsi yake tu alikuwa amepokea maelekezo kutoka kwa Bwana anasema na yakuwa nimefanya haya kwa neno lako, alikuwa ameutafuta uso wa Mungu kwa kiwango cha kutosha ili Mungu aweze kuthibitika na sio Mungu tu na nabii wa kweli aweze kuthibitika, Mungu anapojibu kwa Moto utendaji wake huonekana kwa Dhahiri na hiki ndicho kilichotokea watu wote walijua kuwa Mungu wa Ibrahimu, na Isaka na Yakobo kuwa ni Mungu wa kweli, na hapo ndipo Eliya na watu wote walipokuwa na nguvu dhidi ya manabii wa uongo, kanisa la Mungu leo tutaweza kuwashinda manabii wa uongo ikiwa tu miujiza yetu, itazidi yao, Imani yetu itazidi yao, makusanyiko yetu yatazidi yao, watu wenye changamoto mbalimbali duniani watatujia na kuhitaji msaada kutoka kwetu, hakuna siasa kwa Mungu, Mungu wa kweli atadhihirika na mashaka ya watu yataondoka ikiwa tu tutakuwa na uwezo wa kujibu changamoto zinazowakabili watu, hatuwezi kamwe kumtanganza Mungu kwa ujasiri endapo Mungu wetu hawezi kuwasaidia watu hata ugonjwa wa mafua tu, Umefika wakati tumtafute Bwana, tumtake Bwana na nguvu zake ili Mungu wetu aweze kudhihirika wazi wazi kwa wale wasioamini na wale wanaotupinga hivi ndivyo Eliya alivyoibuka mbabe mbele ya wale waliokuwa wanampinga yaani Mungu wake kuonyesha uwezo wa kujibu kwa moto na hii ndio tofauti ya Mungu aliye hai na mungu aliyekufa.

Mwisho wa Manabii wa uongo

Jambo kubwa la msingi lililotokea ni kuwa manabii wa uongo walipoteza washirika wao kwani watu wote baada ya tukio hilo walimrudia Mungu, Walitambua kuwa Mungu wa Ibrahimu, na Isaka na Yakobo, Mungu wa Eliya ni Mungu wa kweli na walitubu wakitambua ya kuwa wamefanya dhambi kwa kuabudu miungu mingine 

1Wafalme 18:39 “Na watu wote walipoona, wakaanguka kifudifudi; wakasema, Bwana ndiye Mungu, Bwana ndiye Mungu.

Ni lazima watu wote duniani wamjue Mungu wa kweli, zimekuweko falsafa nyingi duniani na dini nyingi lakini watu wengi hawamjui Mungu wa kweli, sisi kama Eliya Leo hatuna budi kuitangazia jamii kuwa Yesu Kristo ndiye njia na kweli na uzima, Yeye ni ishara mashuri kwani amefufuka yu hai na ameketi mkono wa kuume wa Mungu baba Mwenyezi, watu wote wanapaswa kutambua hilo na kuacha mashaka na kusita sita wote wanapaswa kumchagua Mungu aliye hai na wa kweli kwa hiyo ni muhimu kwetu kufanya uamuzi leo, na kumkubali Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yetu, watu wote wanapaswa kujua kuwa duniani kuna watu wengi wanaabudu, wengine mpaka wanajikata kata na kujitoa dhabihu, lakini hii haimaanishi kuwa jitihada zao za kidini na kiimani walizonazo kwamba zinaweza kuwaokoa au kana kwamba wako sahihi, wakati umefika na saa ipo ambayo waabuduo halisi watamuabudu Mungu katika Roho na kweli, na wakati huo ni sasa, ni lazima jamii itambue kuwa kubudu kusiko sahihi kuna matokeo yasiyo sahihi na moja ya matukio hayo ni kutupwa katika ziwa liwakalo Moto, Mungu sio tu awawahukumu manabii wa uongo lakini pia ataihukumu miungu kwa sababu imeiba utukufu wake kwa muda mrefu na kwa miaka Mingi,  na kuwapotosha wanadamu. Jamii ya watu wa wakati wa Eliya walirudisha utukufu kwa Mungu wakisema Bwana ndiye Mungu, Bwana ndiye Mungu, Navutiwa na maneno hayo ninapoyasoma katika Biblia ya kingereza iitwayo Complete Jewish Bible “CJB” inasoma hivi 

When all people saw it, they fell on their faces and said, ADONAI is God! ADONAI is God."

Watu walisujudu na kukubali kuwa Mungu ndiye Bwana Mungu ndiye Bwana, watu walirudisha utii kwa Mungu na huo ndio ukawa mwisho wa manabii wa uongo, hatuwezi kuwaua leo manabii wa uwongo, lakini nyakati za agano la kale watu makafiri waliuawa hivyo Eliya aliamuru manabii wa baali wakamatwe na wakachinjwa, sisi namna yetu ya kuwachinja ni kumuhubiri Mungu wa kweli na kufanya miujiza na ishara za kweli kwa jina la Yesu Kristo, kwa kusudi la kurejesha mioyo ya watu kwa Mungu wa kweli na kumpa yeye heshima na utukufu, huku wakitambua kuwa Yesu ndiye njia na kweli na uzima!

1Wafalme 18:40 “Eliya akawaambia, Wakamateni hao manabii wa Baali, asiokoke hata mmoja. Wakawakamata; na Eliya akawachukua mpaka kijito cha Kishoni, akawaua huko.

Hitimisho 

Kumbuka kumtumikia Mungu wa kweli, kumbuka kumuabudu Mungu wa kweli na ondoka katika kusita sita, acha kupeleka ibada mahali kusiko sahihi, je umewahi kujiuliza kama unaabudu Mungu wa kweli? Kama uko kwenye Imani sahihi au la? Amua leo kabla ya hukumu 

Mwenye haki ataishi kwa Imani akisitasita Roho yangu haina furaha naye asema Bwana

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.  

Hakuna maoni: