Yoel 2:25-27 “Nami nitawarudishia hiyo miaka iliyoliwa na nzige, na parare, na madumadu, na tunutu, jeshi langu kubwa nililotuma kati yenu. Nanyi mtakula chakula tele na kushiba, na kulihimidi jina la Bwana, Mungu wenu, aliyewatendea mambo ya ajabu; na watu wangu hawatatahayari kamwe. Nanyi mtajua ya kuwa mimi ni katikati ya Israeli, na ya kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu, wala hakuna mwingine; na watu wangu hawatatahayari kamwe.”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa wakati mwingine katika maisha ya mwanadamu duniani huwa kunakuwa na maafa yanayojitokeza katika nyanja mbalimbali za mifumo ya kimaisha, maafa hayo yanaweza kuwa ya kiroho, kisiasa, kiuchumi na kimwili. Aidha aina hizi za maafa sio ngeni kwa ulimwengu na kwa watu wa Mungu likiwemo taifa la Israel, Wana wa Israel walikuwa na ufahamu wa kina kuhusiana na aina hizi za maafa zilizokuwa zimewakuta na kuwapata katika taifa lao, na hivyo walikuwa na ujuzi wa kutafasiri na kuelewa kwa kina kile ambacho manabii walikizungumza kwa uwazi au kwa mafumbo na hii iliwasaidia kutambua mpango na makusudi ya Mungu katika maisha yao sawa na Maneno ya manabii. Nabii Yoeli alikuwa moja ya manabii walioweza kuainisha wazi na kuijulisha jamii yake kwa habari ya maafa hayo au majanga lakini sio hivyo tu njia ya kuondoa majanga hayo na namna ambavyo Mungu angeyakomesha maafa hayo na kuwapa miaka ya neema au ya urejesho
Yoeli 1:2-4 “Sikieni haya, enyi wazee; Sikilizeni, enyi wenyeji wote wa nchi. Je! Mambo haya yamekuwako katika siku zenu, Au katika siku za baba zenu? Waarifuni watoto wenu habari yake, Watoto wenu wakawaambie watoto wao, Na watoto wao wakakiambie kizazi kingine. Yaliyosazwa na tunutu yameliwa na nzige; na yaliyosazwa na nzige yameliwa na parare; na yaliyosazwa na parare yameliwa na madumadu.”
Unaona hapo nabii alitangaza maafa ya kiroho, kisiasa na kiuchumi kwa wana wa Israel na kisha baadaye aliwapa njia ya namna ya kufanya ili kurejesha neema ya Mungu katika maisha yao na kisha alitangaza kurejeshwa kwa miaka hiyo ya hasara, ujumbe huu leo uko wazi kwaajili ya ulimwengu, Israel, Kanisa, taifa, jamii, familia na kila mtu mmoja mmoja kwa nafasi yake na maisha yake kwa hiyo ni muhimu kuzingatia kile ambacho Mungu anataka kusema nasi leo jambo litakaloutaufanya mwaka mpya huu na miaka mingine kwako kuwa mwaka wa neema kuliko majira na nyakati ulizozipitia katika maisha yako, kwa sababu hiyo Leo tutajifunza somo hili “Kurejeshwa kwa miaka ya hasara” kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
• Kutangazwa kwa miaka ya hasara.
• Namna ya kuondoa miaka ya hasara.
• Kurejeshwa kwa miaka ya hasara.
Kutangazwa kwa miaka ya hasara
Nabii Yoel alipokea ujumbe wake kama neno la Mungu kwa utawala wa Yuda lakini pia ukiuhusu ulimwengu wote, Yoeli alikuwa na makusudi makubwa matatu tu, kutangaza hukumu ya Mungu inayokuja kwa utawala wa Yuda, kuwaita watu pamoja ili waweze kumrudia Mungu kwa toba na kutangaza neema ya Mungu Kwa watu wake wanapokubali kujinyenyekeza, anapotangaza ujumbe wake nabii huyu hususani katika eneo la kwanza lakutangaza hukumu ya Mungu, kimsingi nabii anazungumza kuwa hukumu hii ya Mungu kwa watu wake itahusu, maswala yote muhimu ya mwanadamu, kiroho, kisiasa na kiuchumi, kuwa endapo watu wake Mungu wangeendelea katika mfumo wa maisha ya kutokujali kuhusu Mungu, Mungu angeinua taifa lenye nguvu, au mataifa adui yenye nguvu yatakayoishambulia Yuda na kuleta maafa katika taifa lao, hali ya kiroho ya Taifa, kanisa, familia na mtu mmoja mmoja ina mchango mkubwa sana katika kuamua mustakabali wa kisiasa na kiuchumi katika maisha ya taifa, kanisa na mtu awayeyote yule.
Yoeli 1:2-4 “Sikieni haya, enyi wazee; Sikilizeni, enyi wenyeji wote wa nchi. Je! Mambo haya yamekuwako katika siku zenu, Au katika siku za baba zenu? Waarifuni watoto wenu habari yake, Watoto wenu wakawaambie watoto wao, Na watoto wao wakakiambie kizazi kingine. Yaliyosazwa na tunutu yameliwa na nzige; na yaliyosazwa na nzige yameliwa na parare; na yaliyosazwa na parare yameliwa na madumadu.”
Tangazo la nabii Yoeli limewasumbuwa watafasiri wengi wa Biblia hususani katika pigo la tunutu, nzige, parare na madumadu, hii ni kwa sababu nabii alitumia mfano wa wadudu waharibifu wa mazao kuzungumzia uharibifu wa kisiasa, kiuchumi na kiroho kwa watu wa taifa lake, Yuda. Israel kama ilivyo hapa Afrika huwa tunafahamu kuwa ziko nyakati ambapo, katika secta za kilimo hutokea wadudu waharibifu wa mazao ambao kimsingi husababisha hasara kubwa sana na hata kuleta njaa na uharibifu mkubwa wa mazao ya chakula, wadudu hao Kwa kawaida huvamia kama jeshi, na wanajulikana kama tunutu, nzige, parare na madumadu, kwa hiyo Yoeli anawatumia wadudu hawa kutangaza miaka ya hasara kiroho, kisiasa na kiuchumi. Kimsingi Yoel hazungumzii wadudu halisi bali anazungumzia Mataifa mabaya ambayo yataivamia Israel na mataifa hayo yatakuwa yameruhusiwa na Mungu kuwaumiza na kuwaletea hali ngumu kwa sababu ya dhambi zao, Yoeli anatumia uzoefu wa wadudu waharibifu wa mazao kuwakilisha uharibifu wa taifa, kisiasa, kiuchumi na ambako kumesababishwa na hali yao ya kiroho.
Muda wa hasara ungeweza kuhusisha uharibifu katika maeneo kadhaa, kiuchumi, kisiasa, na kiroho muda huo hapa umeitwa miaka, lakini ni nyakati na majira ambayo Mungu amekusudia upite ko sio lazima iwe miaka:-
Kiuchumi – Watu walioishi siku nyingi na wale watakaoishi siku nyingi yaani wenye uzoefu ambao nabii anawataja kama wazee watakuwa wanafahamu maafa ya kiuchumi yanayosababishwa na wadudu waharibifu kama tunutu, nzige, parare na madumadu, Yoeli aliwadhihirishia wazee yaani wenye uzoefu kufikiri na kutafakari kuwa hali kama hiyo kama umewahi kwako katika nyakati zao, wajitafakari kwani hali ambayo ingewakuta hata wazee, na wenyeji wa nchi wasingeliweza kuamini kwani lilikuwa ni pigo la kiuchumi la kihistoria ambalo halijawahi kutokea katika maisha yao
Yoeli 1:2-4 “Sikieni haya, enyi wazee; Sikilizeni, enyi wenyeji wote wa nchi. Je! Mambo haya yamekuwako katika siku zenu, Au katika siku za baba zenu? Waarifuni watoto wenu habari yake, Watoto wenu wakawaambie watoto wao, Na watoto wao wakakiambie kizazi kingine. Yaliyosazwa na tunutu yameliwa na nzige; na yaliyosazwa na nzige yameliwa na parare; na yaliyosazwa na parare yameliwa na madumadu.”
Tunutu hawa ni jamii ya panzi/nzige wakiwa katika hatua ya kuwa kama buu au kiwavi, hapa kwetu wanaitwa viwavi jeshi kwa kawaida hawa ni waharibifu sana viwavi wanapovamia shamba kwa muda mfupi huwa wanashambulia Matunda au maua ambayo yanaelekea kuzaa matunda na hivyo kusababisha tunda lisizaliwe au kama tunda limezaliwa lioze kwa hiyo wadudu hawa huharibu MATUNDA ya mimea yaliyozaliwa au yanayotaka kuzaliwa
Nzige hawa ni jamii ya panzi ambao huruka kwa makundi makubwa sana yenye kutisha nao pia kama viwavi jeshi huweza kushambulia MAJANI ya mazao na kusababisha uharibifu mkubwa wa mazao, na kuleta njaa na kuathiri uchumi wa watu
Parare ni jamii ya panzi ambao nao kimsingi huweza kushambualia MATAWI na vijiti na kuvitafuna na kuozesha kabisa, kama mmea unaweza kushambuliwa na nzige na kisha wasije hawa parare mmea unaweza kupata nguvu na kustawi tena lakini wakija parare wao hula kabisa matawi na kuacha miti ikiwa imesalia kama kijiti kilichosimama, kikavu na kuharibu kabisa ustawi wa mmea na kusababisha majanga ya njaa
Madumadu wao huja kumalizia MTI wenyewe na kuutafuna mpaka kubakiza shina tu, lakini kama haitoshi Madumadu huwa wanaharufu mbaya kama utawakanyaga na kuwauwa wao ni wakubwa zaidi na ni wanye kutia kinyaa kabisa sehemu nyingine panzi hawa jamii ya madumadu huitwa panzia kunuka kwa hiyo endapo Mungu angeruhusu wadudu hao kuivamia inchi ukweli ni kuwa hali ya uchumi wanchi au taifa au kanisa au mtu mmoja mmoja ingwakuwa iko katika hali ngumu wao humalizia kabisa mmea na kuua
Kisiasa – Yoeli aliendelea kuweka wazi kuwa hukumu ya Mungu kwa watu wa Mungu isingelikuwa ya kiuchumi pekee, bali ingelihusu pia hali ya kisiasa ambayo ingewatesa Israel kwa ukoloni tofauti na ule waliowahi kuusikia huko Misri, Mungu angeleta hukumu ya kisiasa ambako Israel na Yuda wangekwenda utumwani na kuwa chini ya tawala kubwa za dunia za nyakati hizo Falme hizo zingeinuka kutoka kaskazini mwa Yuda na kusababisha maafa sawa tu na wadudu waharibifu wanavyoweza kushambulia mti au mazao, mataifa hayo yanatajwa kama mataifa nyenye nguvu na wenye jeshi kubwa na wakali na wangeharibu watu wa Mungu na kuwachukua na kuwapeleka utumwani na wangeondoa kabisa ustawi wa kiroho na kimwili na kiuchumi wa taifa la Mungu na wangejaribu kuwatawanya kabisa Wayahudi ona
Yoeli 1:6-7 “Maana taifa limepanda juu ya nchi yangu, Lenye nguvu, tena halina hesabu; Meno yake ni kama meno ya simba, Naye ana magego ya simba mkubwa. Ameuharibu mzabibu wangu; ameuvunja mtini wangu; ameyaambua magamba yake kabisa; ameuangusha chini; matawi yake yamefanywa kuwa meupe.”
Tunutu – Wangewakilisha utawala wa Ashuru na Babeli (900-600BC) Israel wangepoteza utawala wa kisiasa chini ya dola kubwa ya Ashuru na Yuda wangepoteza utawala wa kisiasa chini ya utawala wa Babeli, Amani na utulivu pamoja na furaha ya Israel au watu wa Mungu ingeweza kutoweshwa kabisa na mataifa hayo yenye nguvu
Yoel 1:10-12 “Shamba limeharibika, nchi inaomboleza; maana nafaka imeharibika, divai mpya imekauka, mafuta yamepunguka. Tahayarini, enyi wakulima; Pigeni yowe, enyi watunzaji wa mizabibu; Kwa ajili ya ngano na shayiri, Maana mavuno ya mashamba yamepotea. Mzabibu umesinyaa, mtini nao umevia; Nao mkomamanga na mtende na mtofaa; Naam, miti yote ya mashamba imekauka; Maana furaha imekauka katika wanadamu.”
Nzige – Wangewakilisha utawala uliofuata baada ya kuanguka kwa utawala wa Babeli ambao ni Waamedi na Waajemi (550-331BC) kimsingi hawa nao wangeendeleza uharibifu ule ule ulioanzishwa na tunutu, wao wangeendelea kula majani na magamba ya mti na kuuacha mti huu ukiwa uchi na chini ya aibu, kubwa sana na hatari ya kifo cha mti husika.
Parare –Wangewakilisha utawala wa Wayunani/Wagiriki (800-146 BC) wao wangesababisha ukimya kabisa kwa wana wa Israel na wangeweza kubalisha kabisa mtazamo wao na kuwaingizia elimu na falsafa na mitazamo mipya kutokana na Maendeleo ya kielimu waliyokuwa nayo wayunani, Parare walikula kabisa matawi na kuufanya mti usionekane tena wala kujulikana kuwa ni mti wa namna gani na mti ungepoteza sura yake
Madumadu – wanawakilisha utawala wa kisiasa wa Warumi, (31 BC-476 AD) Israel wote wangekuwa chini ya utumwa na kutiwa unajisi na watu hawa, ambao wangemsulubisha hata masihi, na kuiharibu kabisa Yerusalem na kuwaondoa kabisa wayahudi na kuwatawanya Dunia nzima wasiwepo katika nchi ya Yuda kabisa kwa hiyo sio tu kuwa Matunda ya mti yangeliwa, au majani ya mti yangeliwa au matawi na maganda yake yangeliwa lakini mti ungeliwa kabisa na kuozeshwa na kuharibiwa mpaka shinani Warumi ndio waliowaondoa Israel na kuwatawanya wayahudi wengi duniani na kuwahamisha Israel kabisa lakini pia walimsulubisha Masihi
Kiroho – uharibifu ambao ulifanywa na mataifa haya sio tu ulihusu uchumi na siasa lakini vile vile ulihusu swala zima la kiroho, uchumi unapoguswa na siasa inapoguswa hali ya kiroho haiwezi kuwa salama kwa hiyo Yoeli anaonyesha kuwa hata Imani iliguswa katika maafa hayo aliyoyatabiri, Inawezekana wakati mwingine sio mara zote hali ya kiroho ikiwa mbovu ikasababisha hali ya uchumi na siasa pia kuwa mbovu, au hali ya uchumi na siasa ikiwa mbovu, wito wa kuweka sawa ya maswala kiroho yanaweza kurejesha uponyaji wa kitaifa, kisisasa na kiuchumi, Yoeli anaonyesha kuwa mapigo hayo pia yaliunganishwa na hali ya kiroho.
Yoeli 1: 13-14 “Jikazeni mkaomboleze, enyi makuhani; Pigeni yowe, enyi wahudumu wa madhabahu; Njoni mlale usiku kucha katika magunia, Enyi wahudumu wa Mungu wangu; Kwa kuwa sadaka ya unga na sadaka ya kinywaji Zimezuiwa katika nyumba ya Mungu wenu.Takaseni saumu, iteni kusanyiko la dini, Wazee na wakusanye wenyeji wote wa nchi; Waende nyumbani kwa Bwana, Mungu wenu, Na kumlilia Bwana,”
Tunutu – Wanasahambulia “TUNDA LA ROHO” au matunda ya kiroho, ile hali njema ya watu wa Mungu kuwa na upendo, furaha, Amani, uvumilivu. Utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi katika jamii sasa imetoweka imeliwa na tunutu, Yoeli analiona taifa na kanisa kuwa limepoteza haki, limepoteza ile hali ya kuwa na sifa ya watu wacha Mungu, dhuluma kila mahali, kiburi na majivuno, unibafsi na choyo, chuki na mafarakano, uchawi na uadui ndio ambao unachukua nafasi sasa na kuondoa upendo wa kwanza, sio hivyo tu kunaupungufu mkubwa wa matendo ya ajabu, miujiza na uponyaji pamoja na utendaji wa karama za Roho Mtakatifu, kanisa limeachwa jeupee na maombi ya dhati na kuugua hayapo.
Yoeli 1:7 “Maana taifa limepanda juu ya nchi yangu, Lenye nguvu, tena halina hesabu; Meno yake ni kama meno ya simba, Naye ana magego ya simba mkubwa.”
Ufunuo 2:4-5 “Lakini nina neno juu yako, ya kwamba umeuacha upendo wako wa kwanza.Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu.”
Nzige – Inawakilisha kutoweka kwa “NENO LA MUNGU”, Hapa hakuna unabii na hali ya neno la Mungu limekuwa adimu, zaidi ya yote kuchakachuliwa kwa Neno na tafasiri zake halali, kila mmoja anatafasiri neno anavyojisikia na unabii unafifia, ni manabii wachache sana labda Daniel tu walioweza kusema chochote walipokuwa utumwani Babeli, lakini wakati wa utawala wa Uajemi na uamedi, hakukuwa tena na nabii na ukimya ukatawala kwa muda mrefu, katika maafa ya kiroho yanayoweza kuwakumba watu wa Mungu ni pamoja na kutokuwepo kwa unabii ambao kimsingi unatoa mwelekeo wa watu wa Mungu na kuwatia moyo, aidha kama hakuna wahudumu halali wa neno la Mungu wanaowasaidia watu wa Mungu kujua NENO, jamii ya watu wa Mungu inaathirika na kuwa kama imevuliwa nguo, Neno la Mungu ndilo linalochochea utendaji wa Roho Mtakatifu. Kwa hiyo wakati neno la Bwana linapokuwa adimu, Roho wa Mungu hutulia na hivyo kuzimishwa.
Mwanzo 1:2 “Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji.”
1Samuel 3:1 “Basi, mtoto Samweli akamtumikia Bwana mbele ya Eli. Na neno la Bwana lilikuwa adimu siku zile; hapakuwa na mafunuo dhahiri.”
Yoeli 1:16-17 “Je! Chakula hakikukatiliwa mbali mbele ya macho yetu? Naam, furaha na kicheko mbali na nyumba ya Mungu wetu? Mbegu zinaoza chini ya udongo wake; ghala zimeachwa ukiwa; mabanda yamevunjika; kwa maana nafaka imekauka.”
Parare – wenyewe wanahusika na kupotea kwa UTAKATIFU Parare wanahusika na uharibifu na wakati huu wanaharibu kabisa matawi na maganda ya mti, wanaharibu muonekano halisi wa mti, hii inaashiria kuondoka kwa hofu ya Mungu, watu kuacha kuishi kwa uadilifu na mwenendo wa njia za Mungu, watu hawawezi tena kuushinda ulimwengu, wala hakuna tena mahubiri yanayozungumia au kuelekeza watu kuishi maisha matakatifu, wala watumishi wa Mungu wanaokemea dhambi kwa viwango vya juu, hakuna tena mtu na nayeweza kukaza kama na kuhubiri Utakatifu kama walivyofanya mitume ona
1Petro 1:15-16 “bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.”
2Timotheo 2:19 “Lakini msingi wa Mungu ulio imara umesimama, wenye muhuri hii, Bwana awajua walio wake. Na tena, Kila alitajaye jina la Bwana na auache uovu.”
Waebrania 12:14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;”
Madumadu – Mti umeliwa mpaka shinani na unaoza hii ni hali ya kutoweka kwa matumaini na ni wakati ambapo imani imekwisha na ni kipindi cha GIZA/KUFA KIROHO – kila kitu kimekufa na limebaki jina tu, uko uwezekano wa taifa, au kanisa au mtu fulani mmoja mmoja kubakia na jina tu lakini hali ya kiroho inakuwa imekufa kabisa mmea hauna matunda, hauna majani, na matawi yameliwa na shina lake linabaki limeoza, katika hali kama hiyo hakuna matunda ya kiroho, Neno la Mungu limechakachuliwa, hakuna msisitizo wa kujaa nguvu za Roho Mtakatifu, hakuna mkazo wa utakatifu na uchafu unabaki katika kanisa, kuchukulina na dunia, hakuna haki, upendeleo unachukua nafasi, majungu masengenyi na Kila aina ya ubaya na hata kuuana na kurogana mwili mwili mwili unakuwa katika nafasi ya kiroho, hakuna imani. Watu wamepoteza umakini wa kimaadili na wameleweshwa katika anasa na upatikanaji wa mali za duniani
Yoel 1:5 “Levukeni, enyi walevi, mkalie; Pigeni yowe, ninyi nyote mnywao divai; Kwa sababu ya divai mpya; Maana umekatiliwa mbali na vinywa vyenu.”
Ufunuo 3:1 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Sardi andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye na hizo Roho saba za Mungu, na zile nyota saba. Nayajua matendo yako, ya kuwa una jina la kuwa hai, nawe umekufa.”
Luka 18:8 “Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani?”
Kwa hiyo tunaweza kuona jinsi nabii Yoeli alivyokuwa akiionya jamii dhidi ya ujio wa miaka ya hasara, Mungu alikuwa amempa neno la maonyo na kuwaonya watu wake dhidi ya uharibifu na maafa ya kiuchumi, kisiasa na kiroho, huu ni ujumbe kwa ulimwengu mzima kwa kila taifa na kanisa na mtu mmoja mmoja, wakati wote kila taifa litakapopuuzia maswala ya Mungu ni lazima ijulikane wazi kuwa Mungu ataondoa mkono wake na kumruhusu yule alaye aweze kuharibu kila kitu, Ustawi wa taifa lolote na kanisa familia na mtu mmoja mmoja unategemeana na namna tunavyompa Mungu heshima katika kila eneo, kama tutaruhusu ufisadi, mmomonyoko wa uadilifu rushwa na dhuluma kila mahali, tujue wazi kabisa Mungu ataiondoa heshima yake katika kanisa au taifa Mithali 14:34 “Haki huinua taifa; Bali dhambi ni aibu ya watu wo wote.” Hata hivyo ikiwa hali kama hizo zimelikuta taifa, au kanisa au mtu binafsi bado liko tumaini kwa kuwa Mungu ni mwingi wa rehema na si mwepesi wa hasira ni Mungu ambaye hatatulipa sawasawa na makosa yetu yeye kama Baba anavyowahurumia watoto wake ndivyo Anavyowahurumia wale wamchao naye anatoa njia ya kufanya ili kuondoa miaka ya hasara au kwa lugha nyingine muda wa hasara, hilo linatupa neema ya kutafakari kipengele cha pili.
Namna ya kuondoa miaka ya hasara
Ni ukweli ulio wazi kuwa licha ya nabii Yoeli kutoa maonyo kwa watu wa Mungu juu ya kupatwa na mambo mabaya au juu ya taifa kupitia miaka ya hasara nabii Yoeli anatoa wito wa kutubu ili Mungu aweze kuleta uamsho, na ufufuo na urejesho kwa miaka iliyoliwa na tunutu, nzige, parare, na madumadu, wakati wowote tunapotaka kuona Mungu akiliponya kanisa, taifa au watu wake katika Nyanja zote za kisiasa, kiuchumi na kiroho, ni silaha za kiroho pekee ndizo zinazoweza kuleta uponyaji wa mazingira yote makubwa na silaha hiyo ni unyenyekevu na toba ya kweli na hiki ndicho anachokisema Yoeli
Yoeli 1:13-14 “Jikazeni mkaomboleze, enyi makuhani; Pigeni yowe, enyi wahudumu wa madhabahu; Njoni mlale usiku kucha katika magunia, Enyi wahudumu wa Mungu wangu; Kwa kuwa sadaka ya unga na sadaka ya kinywaji Zimezuiwa katika nyumba ya Mungu wenu. Takaseni saumu, iteni kusanyiko la dini, Wazee na wakusanye wenyeji wote wa nchi; Waende nyumbani kwa Bwana, Mungu wenu, Na kumlilia Bwana,”
Yoeli 2:12-17 “Lakini hata sasa, asema Bwana, nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa kuombolea; rarueni mioyo yenu, wala si mavazi yenu, mkamrudie Bwana, Mungu wenu; kwa maana yeye ndiye mwenye neema, amejaa huruma; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, naye hughairi mabaya. N'nani ajuaye kwamba hatarudi na kugeuka, na kutuachia baraka nyuma yake, naam, sadaka ya unga, na sadaka ya kinywaji, kwa Bwana, Mungu wenu? Pigeni tarumbeta katika Sayuni, Takaseni saumu, kusanyeni kusanyiko kuu; Kusanyeni watu, litakaseni kusanyiko, Kusanyeni wazee, kusanyeni watoto, Na hao wanyonyao maziwa; Bwana arusi na atoke chumbani mwake, Na bibi arusi katika hema yake. Hao makuhani, wahudumu wa Bwana, na walie Kati ya patakatifu na madhabahu, Na waseme, Uwaachilie watu wako, Ee Bwana, Wala usiutoe urithi wako upate aibu, Hata mataifa watawale juu yao; Kwani waseme kati ya watu, Yuko wapi Mungu wao?”
Wakati wowote hali inapokuwa mbaya katika jambo lolote nabii anatoa wito kwa watu wa Mungu kutubu kwa kumlilia Mungu, na kumuomba Mungu kwa kufunga na kuomba, na hata kukesha usiku na mchana, wito huu unatolewa kwa watu wote kuanzia kwa makuhani yaani watumishi wa Mungu mpaka watu wengine wote, Nabii anaonyesha kuwa hii ndio namna ya kiroho ambayo Mungu alikuwa amemuagiza kuwa watu wafanye hivyo, akiwakumbusha kuwa Mungu ni wa neema na rehema na kuwa amejaa huruma wala sio mwepesi wa hasira, na kuwa yeye hughairi mabaya, hii ndio njia iliyotumiwa na mataifa yote hata ya kipagani katika kujiokoa na hasira za Mungu pale zilipotangazwa
Yona 3:4-10 “Yona akaanza kuuingia mji mwendo wa siku moja, akapaza sauti yake, akasema, Baada ya siku arobaini Ninawi utaangamizwa. Basi watu wa Ninawi wakamsadiki Mungu; wakatangaza kufunga, wakajivika nguo za magunia, tangu yeye aliye mkubwa hata aliye mdogo. Habari ikamfikia mfalme wa Ninawi, naye akaondoka katika kiti chake cha enzi, akavua vazi lake, akajivika nguo za magunia, na kuketi katika majivu.Naye akapiga mbiu, akatangaza habari katika mji wa Ninawi, kwa amri ya mfalme na wakuu wake; kusema, Mwanadamu asionje kitu, wala mnyama wala makundi ya ng'ombe, wala makundi ya kondoo; wasile, wala wasinywe maji; bali na wafunikwe nguo za magunia, mwanadamu na mnyama pia, nao wakamlilie Mungu kwa nguvu, naam, na wageuke, kila mtu akaache njia yake mbaya, na udhalimu ulio mikononi mwake. Ni nani ajuaye kwamba Mungu hatageuka na kughairi, na kuiacha hasira yake kali, ili msiangamizwe? Mungu akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi Mungu akalighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende.”
Biblia imejaa mifano na maandiko ya kutosha yanayoonyesha kuwa kila wakati Mungu alipotaka kuadhibu au hata alipoadhibu toba ilileta mabadiliko makubwa, Bwana yuko tayari kughairi kila aina ya uovu alioukusudia au kuuruhusu endapo tu tutaitikia kwa toba kile ambacho neno la Mungu limetuagiza kukifanya hii ni kwa mtu mmoja mmoja, kwa taifa na kwa kanisa pia na watu wowote wanaotaka kuona mkono wa Mungu wa rehema ukiwa juu yao, ikiwa unaona wazi kuwa unapita katika miaka/muda iliyoliwa na tunutu, nzige, parare na madumadu basi changamkia agizo la toba na acha maovu yako nawe utaona uamsho mkubwa, mapinduzi makubwa ya kiuchumi, kisiasa na kiroho na mvua ya Baraka itanyesha juu yako.,
Unabii. Kuhusu 2025 na kuendelea!
Wakati Mungu ananipa ujumbe huu alitaka niseme wazi na mataifa ya Malawi na Kenya na Tanzania, alitaka pia niseme na ulimwengu na mtu mmoja mmoja lakini zaidi sana Malawi na Kenya, huku Tanzania ikijifunza kutoka katika unabii huo, “Mungu ameniambia kwa habari ya Malawi na Kenya, Kwamba siku za karibuni aliinua viongozi wacha Mungu katika mataifa hayo, yaani marais ambao wanamjua Mungu na wameokoka, lakini amenimeambia pamoja na hayo nchi hizo zinahali mbaya ya maporomoko makubwa ya kiroho, na kwa sababu hiyo uharibifu mkubwa unazipata nchi hizo, watapata majanga ya kawaida ya asili na njaa na mporomoko mkubwa ya kiuchumi na vurugu za hapa na pale, lakini sababu kubwa ni kuwakumbusha maraisi hao kuirudisha nchi ya Malawi na Kenya katika kilele, cha uchaji wa Mungu, hizi ni nchi ambazo Mungu alizikusudia ziwe nchi za kiinjilisti na kimisheni, lakini zimeacha wajibu huo na hivyo wanapaswa kutubu na wakifanya hivyo kutakuwa shwari Malawi na Kenya, Malawi Umisheni, Kenya Uinjilisti Kwa Tanzania Mungu amekuchagua kuwa Mwalimu wa neno la Mungu na mafundisho sahihi, lakini Mungu anaionya Tanzania kuwa nayo imeanza kuruhusu mafundisho potofu kuenea na injili imechakachuliwa katika taifa hili, Mungu anaionya Tanzania na kanisa la Tanzania kusimama imara katika kusimamia kweli ya Mungu vinginevyo iko hukumu nzito italijia taifa hili, lakini wakitubu na kila mtu akiisimamia kweli na kuacha kuichuja injili Tanzania itakuwa mfano wa kuigwa Afrika, aidha matukio ya kidunia yatakayojitokeza katika miaka hii kuanzia 2025, kutakuwa na uamsho mkubwa sana wa kasi katika Israel, katika jamii ya wayahudi, kiu ya kuwa taifa kubwa itaongezeka na kiu ya kulijenga Hekalu itawajia kwa nguvu, Israel itaendelea kuwa na nguvu kubwa sana na hakutakuwa na mtu wa kuwanyamazisha katika kile wanachotaka kukifanya Duniani, kutakuwa na maendeleo makubwa sana kwa Taifa la Saud Arabia, Jordan na Misri, lakini taifa la Iran litafifia sana kwa nguvu zake, kutakuwa na utulivu mkubwa sana katika taifa la Syria na watu wake watatulia na kujali katika kujijenga wenyewe kiuchumi na kimaendeleo na hawatatamani vita tena milele, viongozi wengi wa dunia wenye asili ya kidikteta wataangushwa madarakani, kutakuweko na viongozi wengi wenye kupigiwa kura za kutokuwa na Imani nao na wengi kuondolewa madarakani kwa kura za kibunge na maandamano ya wananchi, kutakuwa na uamsho mkubwa sana katika nchi ya Msumbiji, watanzania na wakenya wengi watahubiri Msumbiji na kuwa na makanisa makubwa sana, miujiza mingi na wahubiri wakubwa sana watapatikana Msumbiji na watu wengi watakuwa wakisafiri kwenda Msumbiji kwaajili ya maombi na maombezi, Aidha kutakuwa na watu wenye misimamo mikali wengi sana katika Imani ambao watakuwa na uelewa wa kumcha Mungu kwa viwango vya juu bila unafiki na watakuwa na wivu wa bwana hawa watainuka kwa wingi hususani Tanzania, aidha Muhubiri wa kimataifa aitwaye Bushiri huko Malawi, atang’ara sana na kuwa tegemeo la watu wengi, Mungu atamtumia kwa viwango vikubwa sana na ninaambiwa atakuwa ni mtu mwenye upendo mwingi sana mimi simjui na simfuatilii sana, lakini Mungu atamtumia katika kilele chake” Mwisho
Kurejeshwa kwa miaka ya hasara
Yoeli sio tu kuwa alitangaza hukumu ya Mungu, lakini alionyesha njia ya kumrejea Mungu na kama hayo hayatoshi Yoeli anaonyesha na kutabiri kurejeshwa kwa hali ya kiroho na Baraka za Mungu ambazo kimsingi asili yake ni rohoni akionyesha kuwa Mungu atawahurumia watu wake na kusikia wivu kwaajili yao na kwa sababu hiyo atawajibu watu wake na kuwaponya kiroho, kimwili na kisiasa
Kiuchumi - Yoel 2:18-19 “Hapo ndipo Bwana alipoona wivu kwa ajili ya nchi yake, akawahurumia watu wake. Bwana akajibu, akawaambia watu wake; Tazameni, nitawaletea nafaka, na divai, na mafuta, nanyi mtashiba kwa vitu hivyo; wala sitawafanya tena kuwa aibu kati ya mataifa;”
Kisiasa – Yoel 2:20-22 “lakini jeshi lililotoka kaskazini nitaliondolea mbali nanyi, nami nitalifukuza mpaka nchi ya ukame na ukiwa; sehemu yake iliyo mbele itaingia katika bahari ya mashariki, na sehemu yake iliyo nyuma itaingia katika bahari ya magharibi; na uvundo wake utapanda juu, na harufu yake mbaya itapanda juu, kwa sababu ametenda mambo makubwa.Ee nchi, usiogope; furahi na kushangilia; kwa kuwa Bwana ametenda mambo makuu.Msiogope, enyi wanyama wa kondeni; maana malisho ya jangwani yanatoa miche, na huo mti unazaa matunda yake, mtini na mzabibu inatoa nguvu zake.”
Kiroho – Yoel 2:23-27 “Furahini, basi, enyi wana wa Sayuni, mkamfurahie Bwana, Mungu wenu; kwa kuwa yeye huwapa ninyi mvua ya masika, kwa kipimo cha haki, naye huwanyeshea mvua, mvua ya masika, na mvua ya vuli, kama kwanza. Na sakafu za kupepetea zitajaa ngano, na mashinikizo yatafurika kwa divai na mafuta.Nami nitawarudishia hiyo miaka iliyoliwa na nzige, na parare, na madumadu, na tunutu, jeshi langu kubwa nililotuma kati yenu.Nanyi mtakula chakula tele na kushiba, na kulihimidi jina la Bwana, Mungu wenu, aliyewatendea mambo ya ajabu; na watu wangu hawatatahayari kamwe.Nanyi mtajua ya kuwa mimi ni katikati ya Israeli, na ya kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu, wala hakuna mwingine; na watu wangu hawatatahayari kamwe.”
Hatimaye – Yoel 2:28-29 “Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, waume kwa wake, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono; tena juu ya watumishi wenu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile, nitamimina roho yangu.”
Hatimaye Mungu ataleta uamsho mkubwa sana na kurejesha tena matunda ya roho, karama za Roho Mtakatifu na utendaji mkubwa wa Mungu, kila eneo la ustawi wa maisha ya mwanadamu litaimarika hii itatokea kwa taifa, itatokea kwa kanisa na ustawi wa mtu mmoja mmoja kwa kadiri anavyojitoa kwa Mungu na hiki ndio bwana anachotaka kukiona kama tutatudumu katika utakatifufu na imani na kuishi katika uweza na nguvu za Roho Mtakatifu basi tegemea Ustawi huu, tukidumu katika unyenyekevu na uaminifu na kuwa mbali na ukaidi hakuna mtu atakaye tahayarika, Mungu atatuhurumia, na Roho wa Mungu atamwagwa kwa wingi na karama na madhihirisho yataachiwa katika kanisa na watu watakiri wazi kuwa Mungu yu katikati yenu.
Wishes Happy new year to you All, love you
Na. Rev. Mkombozi Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni