Mathayo 2:13-15 “Na hao walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize. Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda zake Misri; akakaa huko hata alipokufa Herode; ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii, akisema, Kutoka Misri nalimwita mwanangu.”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa Taifa la Misri ni moja ya mataifa muhimu sana katika historia nzima ya ukombozi wa mwanadamu na Israel, Taifa la Misri limetumiwa na Mungu katika maandiko kutufundisha maswala makuu kadhaa muhimu na penginepo unaweza kuongezea na mengine, lakini Misri ni alama ya Usalama kwa watu wa Mungu, Lakini Misri pia inasimama kama alama ya utumwa na mateso kwa watu wa Mungu na pia, Misri inasimama kama alama uhamisho kwa watu wa Mungu, na sehemu ya alama ya ukatili kwa watoto wa Mungu, Kwa hiyo Misri ni moja ya taifa ambalo Mungu amelitumia kama Ishara ya ukombozi na katika kutupa somo watu wake, Hakuna sababu ya kuichukia Misri kama vile ni sehemu mbaya na badala yake tunaweza kuipenda Misri kama sehemu muhimu ya ardhi iliyotumiwa na Mungu kutufundisha maswala kadhaa muhimu katika maisha.
Mwanzo 12:10 “Basi kulikuwa njaa katika nchi ile; Abramu akashuka Misri, akae huko kwa muda maana njaa ilikuwa nzito katika nchi.”
Tunaona kuwa wakati ambapo kulikuwa na njaa katika nchi ya Kanaani, Ibrahimu alishuka Misri kwa muda kwaajili ya kupisha njaa kali na nzito iliyokuwa imejitokeza Kanaani, kwa hiyo Misri hapa inaonekana kuwa ni eneo salama kwa Abramu na watu wake kwaajili ya Usalama wao, sio tu wakati wa Ibrahimu, lakini hata wakati wa Yakobo njaa kubwa ilipotokea wana wa Israel sio tu walishuka kununua nafaka Misri lakini kupitia Yusufu walishuka na kukaa Misri katika eneo la Gosheni wao pamoja na mifugo yao kwa kusudi la kupisha njaa kali iliyoikumba dunia ya wakati ule
Mwanzo 47:27-30 “Israeli akakaa katika nchi ya Misri, katika nchi ya Gosheni. Wakapata mali humo, wakaongezeka na kuzidi sana.Yakobo akaishi katika nchi ya Misri miaka kumi na saba, basi siku za miaka ya maisha yake Yakobo ilikuwa miaka mia moja na arobaini na saba. Siku za kufa kwake Israeli zikakaribia; akamwita mwanawe Yusufu, akamwambia, Kama nimeona kibali machoni pako, weka mkono wako chini ya paja langu, ukanifanyie rehema na kweli; nakusihi usinizike katika Misri. Lakini nitakapolala pamoja na baba zangu, unichukue toka Misri, unizike katika kaburi lao. Akasema, Nitafanya kama ulivyosema.”
Kwa hiyo tunajifunza hapo kuwa Misri ilifanyika mahali salama kwaajili ya Ibrahimu, na baadaye Yakobo na wana wa Israel kabla ya utawala uliokuja baadaye na kuwageuza Israel kuwa watumwa, na sasa katika namna ya kushangaza tunaiona Misri sasa ikiwa alama ya Usalama kwa Yusufu na Mariamu na mtoto Yesu pale alipokuwa anawindwa na Herode kwa kusudi la kutaka kumwangamiza
Mathayo 2:13-15 “Na hao walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize. Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda zake Misri; akakaa huko hata alipokufa Herode; ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii, akisema, Kutoka Misri nalimwita mwanangu.”
Kwa hiyo Misri ni sehemu salama, ni alama ya usalama, lakini vile vile Misri ni alama ya utumwa na ukatili, Misri vile vile ni alama ya uhamishoni, Misri haikuwa nchi ya ahadi, lakini ilikuwa ni sehemu Muhimu sana kwa Usalama wa Israel, uhifadhi wao, maendeleo yao, uimara wao na Ustawi wao, kwa hiyo Misri ina historia kubwa sana katika fundisho la ukombozi wa mwanadamu na wana wa Israel, na zaidi sasa kwa Usalama wa Yesu Kristo aliye mwokozi wa ulimwengu.
Leo tutachukua Muda kiasi kujifunza juu ya somo hili muhimu katika msimu unaoelekea sikukuu za kuzaliwa kwa Mwokozi, kwa kutafakari ujumbe huu wenye kichwa Kutoka Misri Nalimwita Mwanangu na tutajifunza somo hili kutoka Misri nalimwita Mwanangu kwa kuzingatia vipengele viwili tu vifuatavyo:-
Kutimizwa kwa neno lililonenwa na Bwana
Kutoka Misri Nalimwita mwanangu
Kutimizwa kwa neno lililonenwa na Bwana.
Mathayo 2:13-15 “Na hao walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize. Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda zake Misri; akakaa huko hata alipokufa Herode; ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii, akisema, Kutoka Misri nalimwita mwanangu.”
Kitendo cha Malaika wa Bwana kumtokea Yusufu katika ndoto na kumuelekeza kumchukua mtoto na Mariamu mama yake kisha waelekee Misri, ni swala linalozingatia Usalama wa Yesu kule Misri, kwa sababu kulikuwa na hatari ya kutaka kuuawa kwa mtoto huyu kutoka kwa mfalme Herode, na Baada ya kifo cha Herode Bwana alimtokea Tena Yusufu na kumtaka arejee Israel, lakini katika mtazamo wa Matayo yeye analiona tukio hili ni kutimizwa kwa unabii wa mjumbe wa Bwana yaani nabii Hosea aliyesema haya katika
Hosea 11:1 “Israeli alipokuwa mtoto, nalikuwa nikimpenda, nikamwita mwanangu atoke Misri.”
Kimsingi Nabii Hosea anaonyesha jinsi Mungu alivyoipenda Israel na kuwaita kuja katika nchi ya Mkanaani, Mathayo anamuona nabii Hosea kuwa anazungumza kihistoria na kinabii, kihistoria nabii Hosea anazungumzia tukio la Mungu kuwaokoa wana wa Israel watoke uhamishoni, watoke katika nchi ya makimbilio na kuwarejeza katika nchi ya ahadi, Mungu alifanya hivyo kwa upendo wake, kwa watu wake akiwa amewabariki na kuwaimarisha kijeshi na kisayansi na kuwafunza sheria na taratibu zake, Israel ni watoto wa Mungu ni watoto wake aliowachagua nimzaliwa wake wa kwanza
Kutoka 4:22 -23 “Nawe umwambie Farao, BWANA asema hivi, Israeli ni mwanangu mimi, mzaliwa wa kwanza wangu; nami nimekuambia, Mpe mwanangu ruhusa aende, ili apate kunitumikia, nawe umekataa kumpa ruhusa aende; angalia basi, mimi nitamwua mwanao, mzaliwa wa kwanza wako.”
Lakini kinabii Mathayo anauona ujumbe wa Hosea kuwa unamzungumzia Yesu Kristo, nikamwita mwanangu atoke Misri, Mathayo anamuona Yesu kuwa ndiye Israel Halisi na kuwa wengine wote ni kama wamekuwa Israel mwitu, hii ni kwa sababu Israel walipopandishwa katika nchi ya ahadi Mungu alitarajia wangemtii yeye na kuacha kuabudu miungu mingine lakini hata hivyo mwanzoni walishindwa na ni Yesu Peke yake aliyeweza kutii maagizo yote ya Mungu na kuitimiza Sheria Yote hivyo Mathayo anakubaliana na maandiko kuwa Yesu ndiye Israel halisi na ndiye mzabibu wa kweli
Yeremia 2:21 “Nami nalikuwa nimekupanda, mzabibu mwema sana, mbegu nzuri kabisa; umegeukaje, basi, kuwa mche usiofaa wa mzabibu-mwitu machoni pangu? ”
Yohana 15:1-2 “Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa.”
kwa msingi huo maneno haya kutoka Misri nalimwita mwanangu katika mtazamo wa kinabii Mathayo anauona kuwa unabii huu unatimizwa kwa Yesu Kristo, Lakini pia ni wito kwa watoto wote wa Mungu kuondoka katika inchi isiyo sahihi na mahali pasipo sahihi, na kujiweka wakfu kwaajili ya kumtumikia Mungu aliye hai.Mungu hafurahii hata kidogo uwepo ugenini, ukimbizini, na utumwani
Kutoka Misri nalimwita mwanangu.
Tumejifunza katika utangulizi ya kuwa Misri inawakilisha maswala mbalimbali ikiwa ni pamoja na utumwa na ukatili, Japo Mungu pia aliitumia Misri kuwaneemaesha Israel na kumtunza Musa na Yusufu na Ibrahimu na Yesu, Hata hivyo Kimsingi ujumbe huu wa kutoka misri nalimwita mwanangu haukuwa tu unamuhusu Israel na Yesu pekee, lakini ni ujumbe wa Mungu leo kwa watu wake wote walioko uhamishoni, Mungu anakuita utoke katika hali yoyote ya mashaka, wasiwasi, kupoteza tumaini na kuishi kama mkimbizi, Mungu anataka urudi katika uhalisia wako Misri haikuwa nchi halisi ya Israel wala haikuwa nchi halisi ya Yesu, ilikuwa ni sehemu tu ya kujihifadhi, sasa Mungu anakuita katika eneo lako la asili, Eneo ambalo amekusudia kukupumzisha, eneo ambalo amekusudia kukupa raha, eneo ambalo amekusudia kukutumia eneo ambalo amekusudia kukupa utulivu, Eneo ambako ameandaaa ustawi wako na makazi yako ya kudumu!, hapo ulipo uko kwenye nchi ya utumwa, uko uhamishoni, uko unatumikishwa, uko na mizigo, uko ukimbizini,huko huwezi kumuabudu Mungu kwa uhuru, na sasa Bwana kwa kinywa cha nabii anakuita wewe ni mtoto wake halisi na hauko mahali halisi alikokuweka anataka akutoe huko, kutoka Misri nalimwita mwanangu! Mungu hatakubali uendelee kuweko uhamishoni, Mungu hawezi kukubali mtoto wake aendelee kuwepo Misri ni lazima atakuita kutoka huko, Hosea analiona tukio hilo kana kwamba Mungu aliwaita wana wa Israel watoke Misri na Mathayo analiona tukio hilo kuwa Mungu alimuita Yesu kutoka Misri nami naliona tukio hilo kuwa Mungu anakuita wewe Katika nafasi aliyokukusudia kwayo. Kwa sababu
Kutoka Misri ni kujitenga kwaajili ya Mungu ili umuabudu na kumtumikia yeye na sio Farao, Mungu anajua ya kuwa huwezi kumuabudu Mungu kwa uhusu na Amani ukiwa Misri, Farao atataka uendelee kuwako Misri ili utumie muda mwingi kumtumikia yeye kuliko Mungu wako, au umuabudu Mungu pamoja na machukizo ya dhambi za ulimwengu
Kutoka 8:25-26. “Farao akawaita Musa na Haruni akawaambia, Endeni mkamtolee Mungu wenu dhabihu ndani ya nchi hii. Musa akasema, Haitupasi kufanya hivyo; kwa kuwa tutamchinjia sadaka BWANA, Mungu wetu, na hayo machukizo ya Wamisri; je! Tutachinja sadaka ya hayo machukizo ya Wamisri mbele ya macho yao, wasitupige kwa mawe? ”
Farao hatatamani uende mbali na Misri kwa sababu hataki uzame sana katika uhusiano wako na Mungu anatamani uwe vuguvugu, anatamani uishi maisha mchanganyiko, hataki uwe mbali na changamoto zake za kitumwa na ukawe huru kwa Mungu na ndio maana Mungu anatoa wito utoke Misri, na kuja katika inchi sahihi ambako utasitawi, kiroho, kimwili na nasfi yako kuburudika
Kutoka 8:27-28 “La, tutakwenda safari ya siku tatu jangwani, tumchinjie dhabihu BWANA, Mungu wetu, kama atakavyotuagiza. Farao akasema, Mimi nitawapa ruhusa mwende, ili mmchinjie dhabihu BWANA, Mungu wenu, jangwani; lakini hamtakwenda mbali sana; haya niombeeni.”
Misri itatamani wanaume tu waende, lakini wanawake na watoto wabaki, Mungu anataka wote wanaume na familia zao wote wamjue Mungu, ukiwa Misri farao atatamani wanaume tu ndio wamuabudu Mungu wao peke yako bila kujali familia zetu, Musa hakukubali alisema tutakwenda kumuabudu Mungu na kila kitu tulicho nacho na hakutasalia hata ukwato
Kutoka 10:9-11 “Musa akamjibu, Tutakwenda na vijana wetu na wazee wetu, na wana wetu, na binti zetu, tutakwenda na kondoo zetu na ng'ombe zetu; kwa kuwa inatupasa kumfanyia BWANA sikukuu. Lakini akawaambia, Ehe, BWANA na awe pamoja nanyi, kama nitakavyowapa ruhusa kwenda zenu pamoja na watoto wenu; angalieni, kwa kuwa pana uovu huko mbele yenu. Sivyo; endeni ninyi mlio watu wazima, mkamtumikie BWANA; kwa kuwa ndilo jambo mtakalo. Nao walifukuzwa usoni pa Farao.”
Misri itatamani uondoke mikono mitupu, usiwe na mali, Misri ianataka mali zote zibaki, mapato yako yote na kila kitru ukipendacho kibaki kwaajili ya uchumi wa Misri na haitataka uende na kitu kwa Mungu wala kutumia mapato yako na mali zako kwa utukufu wa Mungu na ndio Maana Mungu anakuita utoke Misri ili kila alichikubariki na kukupa kitumike kwaajili ya utukufu wa Mungu
Kutoka 10:24-26 “Farao akamwita Musa, na kumwambia, Haya, nendeni, mkamtumikie BWANA; kondoo zenu na ng'ombe zenu tu na waachwe; watoto wenu nao na waende pamoja nanyi. Musa akasema, Ni lazima utupe mikononi mwetu na wanyama wa dhabihu na wa sadaka za kuteketezwa, ili tupate kumchinjia BWANA Mungu wetu dhabihu. Makundi yetu pia watakwenda pamoja nasi; hautasalia nyuma hata ukwato mmoja; kwa maana inampasa kutwaa katika hao tupate kumtumikia BWANA, Mungu wetu; nasi hatujui, hata tutakapofika huko, ni kitu gani ambacho kwa hicho inatupasa kumtumikia BWANA.”
Kimsingi Mungu aliwaita watu wake watoke Misri ili wamuabudu yeye kwa uhuru na pasipo hofu, wamtumikie yeye na sio kuwa chini ya nira mbili, yaani sio kuwa chini ya utumwa wa dunia na utumishi wa Mungu, kuitwa kuja kutoka Misri ni kutengwa kwaajili ya utumishi ambao Mungu ameukusudia, ni kutengwa kwaajili ya kazi yake, ni kurejeshwa katika eneo sahihi, umuabudu yeye peke yake
Na. Rev. Mkombozi Samuel Kamote
Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni