Jumanne, 7 Januari 2025

Msimwite Mtu Baba Duniani!


Mathayo 23:8-10 “Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu. Wala msimwite mtu baba duniani; maana Baba yenu ni mmoja, aliye wa mbinguni. Wala msiitwe viongozi; maana kiongozi wenu ni mmoja, naye ndiye Kristo.




Utangulizi:

Moja ya maonyo aliyoyatoa Yesu Kristo Kiongozi mkuu wa wokovu wetu kwa wanafunzi wake ni pamoja na kuacha kutafuta heshima kutoka kwa wanadamu na au kuwapa wanadamu heshima isiyostahili, Yesu aliwakumbusha wanafunzi wake kuwa wao ni ndugu, yaani kaka na dada katika Bwana, kwa hivyo wakristo ni familia moja ya Mungu, na Mungu pekee ndiye baba yetu,  lakini zaidi ya yote aliwaonya wasimuite mtu rabi wala baba duniani wala kiongozi, kwa kuwa baba yetu ni mmoja aliye wa mbinguni na Mwalimu wetu ni mmoja ndiye Yesu na wala tusiitwe viongozi, kwa hiyo kamwe hatupaswi kutafuta heshima, wala kumpa mtu heshima ambayo hastahili na badala yake kuhakikisha tunawatumikia watu,  na kuwa heshima na utukufu ni mali ya Mungu Baba yetu.

Marko 10:42-45 “Yesu akawaita, akawaambia, Mwajua ya kuwa wale wanaohesabiwa kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu, na mtu anayetaka kuwa wa kwanza wenu, atakuwa mtumwa wa wote. Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.”

Mafundisho ya Yesu Kristo ni tofauti sana na mafundisho ya ulimwengu huu, watu wa ulimwengu huu wanatafuta kutambulika, wanatafuta umaarufu na heshima kubwa na kutawala, na kutumikisha au kutumikiwa,lakini Kristo anasisitiza unyenyekevu, kujishusha na kuwatumikia watu, na wale wanaojinyenyekeza wawapo duniani watainuliwa katika ufalme wa Mungu, Leo tutachukua muda sasa kujifunza kwa kina na mapana na marefu somo hili zuri lenye na lenye mabishano makubwa sana lenye kichwa“Msimwite mtu Baba duniani” kwa kuzingatia vipengele viwili vifuatavyo:-


Asili na matumizi ya neno Baba.

Msimwite Mtu Baba Duniani!. 


Asili na matumizi ya neno Baba.

Ni muhimu kufahamu kuwa itakuwa ni vigumu sana kuelewa kwanini Yesu anawaonya wanafunzi wake wasimwite mtu Baba hapa duniani, kama hatutaelewa kuwa katika Biblia yaani neno la Mungu jina hilo baba lilikuwa lina maana gani, na lilikuwa linatumikaje hususani katika tamaduni za kiebrania, ni muhimu kufahamu kuwa:- 

Neno baba katika lugha ya asili ya Kiebrania linatumika kama neno “Abh” “abea” au “av” na katika Kiyunani ni “Patēr” kwa kiingereza “Father” na katika lugha ya kiaram ni “Abba” ambalo maana yake ni mtu anayeaanzisha jambo ambalo anafikiri kuwa ni sahihi na anahakikisha linaendelea kuwepo, Baba ni mmiliki, Baba ni Mwanzilishi, Baba ni Mlinzi, Mzazi wa kiume, Baba ni mwenye mamlaka ya uzima au kifo, Baba ni muheshimiwa. (Upholder, the owner, Founder, Protector, A male ancestor, Respect). Katika maandiko yaani nyakati za agano la kale na agano jipya pia Neno baba lilipotumika liligusa maeneo hayo muhimu katika maneno hayo niliyoyataja hapo juu. Lakini neno la kiaramu “Abba” linahusika na uhusiano wa ndani zaidi wa kifamilia sawa na neno “Papa” au “Daddy” Hebu sasa tuchukue muda wa kutosha kuangalia jinsi neno Baba lilivyokuwa likitumika katika maandiko:-

Mzazi au mlezi wa kiume  “Abh”– Jina baba au neno baba katika tamaduni za kiebrania na warumi lilikuwa lina uhusiano wa moja kwa moja na Mzazi mwanaume ambaye ana uhusiano wa damu au uhusiano wa kibailojia wa moja kwa moja na wahusika kama ni watoto wa kiume au wa kike, kwa hiyo matumizi ya neno baba yalimaanisha moja kwa moja baba mzazi, mwanaume ambaye anahusika kukuzaa kibaiolojia kama mzazi wa damu, na hata babu yako na babu yake baba yako nao waliweza kuunganishwa katika kundi hilo kumaanisha baba zako yaani watu ambao ni sababu ya wewe kuwepo duniani, ni waanzilishi wa asili yako ya kimwili duniani, ni sababu ya wewe kuweko kwako duniani, ni damu yako, hawa Mungu anawatambua na ameamuru waheshimiwe na kuna Baraka za kufanya hivyo ikiwa ni pamoja na kupewa siku nyingi za kuishi na heri duniani, Kimsingi hawa ukiwaita baba hakuna shida na Yesu hakukataza tukio la aina hii kwa sababu hii ni kawaida na mzazi au mlezi wa familia yako anastahili heshima hii, kwa hiyo hakuna dhambi wala kosa kumuita mzazi wako baba hii ni heshima yake na ni agizo la Mungu katika maandiko kuwa wazazi wetu wanastahili kuheshimiwa. Kwa hiyo matumizi baba kwa mtu aliyekuzaa au kukulea hayana shida katika katazo la Yesu Kristo.


Kutoka 20:12 “Waheshimu baba yako na mama yako; siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na BWANA, Mungu wako.” (Neno linalotumika hapo ni âb au av)


Matendo 7:32 “Mimi ni Mungu wa baba zako, Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Musa akatetemeka, asithubutu kutazama.” (Neno linalotumika hapa ni Patēr au Patriachs)


1Wafalme 11:42-43 “Na siku alizotawala Sulemani katika Yerusalemu juu ya Israeli wote zilikuwa miaka arobaini. Naye Sulemani akalala na baba zake, akazikwa katika mji wa Daudi baba yake; na Rehoboamu mwanawe akatawala mahali pake.” (Neno linalotumika hapa ni âb au av)


Mababa hawa wa duniani wana mamlaka nyingi, ikiwa ni pamoja na kukuzaa, kukulea, kukupa elimu, kukupa chakula, kukutoa uoe au uolewe, kukulinda, kukuongoza, kukutia moyo, kukuelimisha, kukufundisha, pamoja na kukurithisha, Baba wa waabudu miungu zamani  walikuwa na mamlaka ya kuwatoa watoto wao kafara kwa miungu hivyo kuonyesha kuwa baba wa kibaiolojia pia alikuwa ana mamlaka ya uhai wako na kifo chako, Sawa tu na Ibrahimu alivyotaka kumtoa Isaka, au Yeftha alivyomtoa binti yake, hii ni mamlaka nzito sana aliyo nayo baba, Baba hawa wanaweza kukuonya, kukukemea, kukudekeza, kukuadhibu, kukufundisha hekima, kukurithisha Imani, kushughulika na mahitaji yako kukuhurumia  na hata kuwa rafiki na kadhalika. hawa ni baba wa miili yetu. Ni mababa wa kibaiolojia hawa wana haki ya kuitwa Baba. Kuitwa baba ni heshima yao maalumu na wala sio ya kuitafuta wamepewa na Mungu, kwa hiyo baba hawa huitwa baba wa miili yetu, na Mungu ni baba wa roho zetu. Unaweza kuona:-


Waebrania 12:7-9 “Ni kwa ajili ya kurudiwa mwastahimili; Mungu awatendea kama wana; maana ni mwana yupi asiyerudiwa na babaye? Basi kama mkiwa hamna kurudiwa, ambako ni fungu la wote, ndipo mmekuwa wana wa haramu ninyi, wala si wana wa halali. Na pamoja na hayo tulikuwa na baba zetu wa mwili walioturudi, nasi tukawastahi; basi si afadhali sana kujitia chini ya Baba wa roho zetu na kuishi? ” 


Zaburi 103:13 “Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake, Ndivyo Bwana anavyowahurumia wamchao.


Kwa hiyo maana ya kwanza ya neno baba ni mzazi wa kiume aliyekuzaa au aliyekulea na kuku-kuza, baba ambaye mna asili ya damu na hata yule anayeweza kukuasili ili uwe mwanaye na kadhalika na wale waliohusika katika malezi yako baba mlezi hii ni kawaida. Na hao wanastahili kuitwa baba lakini ni baba wa miili yetu na kwa habari za kiroho, Mungu ndiye baba yetu, anaitwa Baba wa roho zetu unaweza kuona!.


Mwanzilishi – Jina au neno baba pia katika maandiko linatumika kumuelezea mwanzilishi au aliyeweka msingi wa jambo Fulani, aidha kiulimwengu, au kitaifa, au kiimani, au kitabia au kifalsafa au kuweka miongozo, kwa hiyo waanzilishi wa kitu fulani au jambo Fulani au hata waanzilishi wa taifa, katika maandiko waliitwa baba wa hicho alichokianzisha yaani mgunduzi, au mwanzilishi au  sababu au chanzo cha hiyo tabia au jambo, mwanzilishi au mgunduzi wa jambo fulani linaweza kuwa jema au baya hapa duniani  huyo naye katika maandiko aliitwa baba mfano:-


ImaniWarumi 4:11-12. “Naye aliipokea dalili hii ya kutahiriwa, muhuri ya ile haki ya imani aliyokuwa nayo kabla hajatahiriwa; apate kuwa BABA YAO WOTE WAAMINIO, ijapokuwa hawakutahiriwa, ili na wao pia wahesabiwe haki; tena awe baba ya kutahiriwa, kwa wale ambao si waliotahiriwa tu, bali pia wanazifuata nyayo za imani yake baba yetu Ibrahimu aliyokuwa nayo kabla hajatahiriwa.


Ibrahimu anaitwa baba wa Imani, kwa sababu ndiye mtu wa kwanza kuwasiliana na Mungu aliye hai baada ya miaka mingi sana tangu nyakati za Nuhu, na hivyo kuwa sababu ya watu wengi kumwamini Mungu na kumjua Mungu aliye hai na imani kubwa duniani zikiwemo ya kiyahudi, kikristo na nyinginezo ambazo mzizi wake ni nabii Ibrahimu zinakubali na zinamtambua Ibrahimu kama baba wa Imani yaani mwanzilishi wa Imani yetu kwa Mungu na ndiye mgunduzi wa uhusiano na Mungu wa kweli duniani.


Uongo na dhambiYohana 8:44 “Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo.”


Hapa shetani anatajwa kama baba wa uongo, na mwanzilishi wa uongo duniani, ambaye hakuna kweli ndani yake yeye ni mwongo na baba wa huo, yaani shetani ndiye asili au mwanzilishi wa uongo, kwa hiyo neno baba hapa linatumika kuonyesha chanzo, asili au mwanzilishi, mwanzilishi wa uongo ni baba wa huo uongo.

 

Mgunduzi, au mwanzilishi (Meyased) – Mwanzo 4:20-22 “Ada akamzaa Yabali; huyo ndiye baba yao wakaao katika hema na kufuga wanyama. Na jina la nduguye aliitwa Yubali; huyo ndiye baba yao wapigao kinubi na filimbi. Sila naye akamzaa Tubal-kaini, mfua kila chombo cha kukatia, cha shaba na cha chuma; na umbu lake Tubal-kaini alikuwa Naama.” 


Hapa Yabali anatajwa kama asili au mwanzilishi wa kukaa katika mahema na kufuga wanyama, na Yubali ni mwanzilishi wa wapiga muziki yaani kinubi na filimbi, na Tubal-Kaini yeye ni mwanzilishi au mgunduzi wa vyombo vya kukatia vya chuma na shaba au mgunduzi wa silaha 


Aidha katika hali ya isiyokuwa ya kawaida Marekani walimuita George Washington na Abraham Lincoln kama Baba labda kwa sababu ya Washington kuwa mwanzilishi wa taifa hilo, na Lincoln kuwa mtu muhimu katika kujinga Marekani iliyotulia, India walimuita Mahatma Ghand, na Tanzania Mwalimu Nyerere kuwa baba wa mataifa yao, heshima hii kamwe hawajawahi kujipa wala kujiita wenyewe, lakini watu waliwaita hivyo kwa sababu labda ni waanzilishi wa mataifa yao, hatupati kuungwa mkono moja kwa moja kutoka katika maandiko kama wanaweza kufaa kuitwa hivyo kama waanzilishi.  


Uhusiano wa karibu na kihisia – katika tamaduni za kiebrania pia kama mtu alikuwa na uhusiano wa karibu sana na wewe wa kawaida na wa kihisia, waliweza pia kutumia neno baba, watu hawa sio tu walikuwa na uhusiano wa kihisia bali pia uhusiano wa uaminifu ambao unahusisha kujitoa na kushika ahadi na mwenye kumtunza mtu kwa ndani sana Neno la kiebrania linalotumika hapo ni “Masculine” maneno mengine yanayotumika kuelezea aina hii ya uhusiano wa kibaba ni Khesed – anayekutunza, Ahav - anayekupenda, Kesher – zaidi ya rafiki, Kirvah mnayetofautiana kiumri na Yada – unayemjua au unayemuingilia kimwili, hii hutumiwa sana na wanawake kuwaita waume zao baba, Paulo mtume alikuwa na uhusiano wa karibu na kanisa la Korintho na uhusiano wa kihisia kwa hiyo alitumia neno baba hapa kama mtu anayejali na kulilinda kanisa kwaajili ya mafundisho sahihi, na alimuita Timotheo mwanaye katika picha ya uhusiano kama huo, ukaribu na ufahamu wa kile anachiokifundisha zaidi.


1Wakorintho 4:15-17 “Kwa kuwa ijapokuwa mna waalimu kumi elfu katika Kristo, walakini hamna baba wengi. Maana mimi ndimi niliyewazaa katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili. Basi, nawasihi mnifuate mimi. Kwa sababu hii nimemtuma Timotheo kwenu, aliye mwanangu mpendwa, mwaminifu katika Bwana, atakayewakumbusha njia zangu zilizo katika Kristo, kama vile nifundishavyo kila mahali katika kila kanisa.”


Paulo mtume alikuwa ndiye mwanzilishi wa kanisa la Korintho na aliwazaa watoto wa kiroho kupitia injili, na aliruhusu walimu wengine kutoka sehemu mbalimbali kufundisha katika kanisa la Korintho, lakini kutokana na uchungu aliokuwa nao na kutokana na kuwepo kwa walimu wa uongo aliwasihi wao kumfuata yeye kama anavyomfuata Kristo, na ama kumfuata Timotheo ambaye ni mwanae mwaminifu katika bwana, hii ilikuwa lugha ya kisamiati yenye lengo la kutaka kuweka wazi kwa wakorintho namna na jinsi wanavyotakiwa kupokea mafundisho kwa walimu wote lakini wakisheshimu mafundisho ya Msingi ya mwanzilishi wa kanisa hilo na kijana wake, lakini kielelezo ikiwa ni kama wanavyomfuata Kristo, hapa hapakua na agizo endelevu la Paulo kuitwa Baba, hivyo hajapingana Bwana.


Kwa hiyo neno kla kiebrania pia meyased linafaa kutumika hapa kama mwanzilishi, mwanzilishi wa kanisa la Korintho, kwa kiyunani megiasménos, yaani kuwazaa kwa njia ya nguvu za Mungu (injili) wao kuwa kanisa. Na katika uhusiano wa Paulo na Timotheo, Paulo alimuita Timotheo mwanae kwa sababu ya umri, malezi na namna alivyoshughulika na kijana huyu kwa uhusiano wa ndani sana hata kutahiriwa kwa Timotheo ona 


Matendo 16:1-3 “Basi akafika Derbe na Listra, na hapo palikuwa na mwanafunzi mmoja jina lake Timotheo, mwana wa mwanamke Myahudi aliyeamini; lakini babaye alikuwa Myunani. Mtu huyo alishuhudiwa vema na ndugu waliokaa Listra na Ikonio. Paulo akamtaka huyo afuatane naye, akamtwaa akamtahiri kwa ajili ya Wayahudi waliokuwako pande zile; kwa maana wote walijua ya kuwa babaye ni Myunani.” 


Paulo mtume alikuwa na uhusiano wa karibu na Timotheo, na hivyo alimuita mwanangu, hii ilikuwa ni katika kudumisha uhusiano waliokuwa nao binafsi “TEKNON” katika mandiko ya kiyunani uhusiano wa baba na mwanae, hii ilikuwa katika uhalisia wa huduma zao na sio kuwa Paulo alitafuta heshima au kuliagiza kanisa kumuite yeye Baba, wakati wote Paulo alijiita Mtumwa wa Yesu Kristo “Doulos” akimaanisha kuwa yeye ni mtumwa wa Yesu Kristo na sio baba kumbuka hilo, alijitoa maisha yake kutumikia na wala sio kutumikiwa kwa hiyo matumizi na ubaba hapa hayakumaanisha mitume waitwe baba.


Katika mahusiano hayo ya kiumri pia utaweza kumuonya mtume Yohana nadhani kwa sababu ya umri au utu uzima aliokuwanao yeye naye alikuwa akitumia lugha ya kuwaita washirika watoto, hii ni kwa sababu ya umri ona 


1Yohana 2:1 “Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki, naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote.”


Biblia ya kiingereza ya “Complete Jewish Bible” inatumia neno “Wanangu” yenyewe inasema hivi “My Children, Iam writing you these things so that you won’t sin. But if anyone does sin, we heve Yeshua the Messiah, the Tzaddik, who pleads our cause with the Father”


Muumba au kiini Adonai (Lord or Master) – Waefeso 1:17 “Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye;”


Ayubu 38:28-29 “Je! Mvua ina baba? Au ni nani aliyeyazaa matone ya umande? Barafu ilitoka katika tumbo la nani? Na sakitu ya mbinguni ni nani aliyeizaa?


Neno baba pia linatumika kama neno Lord yaani Bwana mkubwa, na Master yaani Mwalimu au kwa kiibrania Adonai hii ikiwa na maana ya Bwana wa Mabwana, au Bwana wa viumbe vyote kwa hiyo huyu ni chanzo cha uhai wa kimwili na kiroho na hivyo neno Adonai bila shaka lina sifa ya kutumiwa kwa Mungu peke yake

Kiongozi wa kiroho au nabii – Nyakati za agano la kale kiongozi wa kiroho kama nabii aliitwa baba pia hii ni kabla ya katazo la Yesu Kristo wakati wa agano jipya, lakini waitaji walilia hivyo kutoka moyoni si kwa agizo la manabii kama ilivyo leo, lakini hii pia ilitokana na uhusiano wa karibu na kihisia, wakati mwingine sio wachungaji na watumishi wa Mungu wanaojiita baba na ndio maana agizo la Yesu Kristo linasisitiza “Msimwite mtu baba duniani”, hii maana yake nini inawahusu sana waitaji, manabii hata hivyo walikuwa wanyenyekevu na hawakuchukulia kuitwa baba kama heshima ya kuidai, lakini watu wa Mungu wenyewe kwa hiyari waliwaita baba, sasa tunalo katazo kutoka kwa Yesu Kristo Msimwite mtu baba duniani. 


2Wafalme 2:11-13 “Ikawa, walipokuwa wakiendelea mbele na kuongea, tazama! Kukatokea gari la moto, na farasi wa moto, likawatenga wale wawili; naye Eliya akapanda mbinguni kwa upepo wa kisulisuli. Naye Elisha akaona, akalia, Baba yangu, baba yangu, gari la Israeli na wapanda farasi wake! Asimwone tena kabisa; akashika mavazi yake mwenyewe, akayararua vipande viwili. Kisha akaliokota lile vazi la Eliya lililomwangukia, akarudi, akasimama katika ukingo wa Yordani.”


2Wafalme 13:14 “Basi Elisha alikuwa ameshikwa na ugonjwa wake uliomwua; naye Yehoashi mfalme wa Israeli akatelemka amtazame, akamlilia mbele yake, akasema, Baba yangu! Baba yangu! Gari la Israeli na wapanda farasi wake! ” 


Kuitwa baba kama tamaduni au mapokeo  -  Aidha Kanisa Catholic, Othodoxy, Anglican na Lutherran huwaita viongozi wao wa kidini Babakwa mujibu wa tamaduni zao au mapokeo yao, na madai yao makubwa ni ushirikiano au uhusiano wa karibu ulioko kati ya washirika na makuhani wa makanisa hayo wito huu ulipata nguvu katika karne za kati maarufu kama Middle Ages wakati wa utambuzi wa viongozi wa kiroho, kama makuhani Mapadre walipopewa heshima hii ya kuitwa baba na maaskofu wakiitwa Papa, watetezi wa hoja hii, ya kuwaita viongozi wa kiroho baba, wanamadai kuwa hata baadhi ya mitume waliitwa hivyo baba mfano


Yohana 2:1 “Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki,”


1Timotheo 1:18 “Mwanangu Timotheo, nakukabidhi agizo hilo liwe akiba, kwa ajili ya maneno ya unabii yaliyotangulia juu yako, ili katika hayo uvipige vile vita vizuri;”


1Petro 5:12-13 “Kwa mkono wa Silwano, ndugu mwaminifu kama nionavyo, nimewaandikia kwa maneno machache, kuonya na kushuhudia ya kuwa hii ndiyo neema ya kweli ya Mungu. Simameni imara katika hiyo. Mwenzenu mteule hapa Babeli awasalimu, na Marko mwanangu.” 


Makanisa mengi leo ukiacha Catholic na Othodoxy wameanza kuwa na kusimika wanawake kuwa makasisi, Anglican na lutheran sasa siku hizi wana wachungaji wengi wanawake na makanisa mengi ya kipentekoste pia yamekuwa yakisimika makasisi wanawake, wachungaji wanawake n ahata kuwaruhusu kuhudumu na kuchunga makanisa wao wanaitwaje sasa katika heshima hii, tuwaite Mama, au tuwaite baba?  Utamaduni na mapokeo hapa yanasemaje Jibu la swali hilo unaweza kubaki nalo kichwani? 


Msimwite Mtu Baba Duniani! 

Yesu aliposema katika Mathayo 23:9 “Wala msimwite mtu baba duniani; maana Baba yenu ni mmoja, aliye wa mbinguni.” Alikuwa anazungumza moja kwa moja kwa wanafunzi wake na kinyume na waandishi yaani walimu waliobobea katika torati pamoja na mafarisayo yaani viongozi wa dini na baraza la Sanhedrin, kimsingi watu hawa walikuwa na tabia ya kujitukuza sana na kutafuta kuheshimiwa sana na watu wote, kuheshimiwa sio kubaya ni sehemu ya maagizo ya maandiko lakini walipenda sana kuheshimiwa na kutafuta umaarufu na heshima hiyo kwa nguvu na kimazingira, Baraza la wazee wakipenda kuitwa baba na waandishi wakipenda kuitwa Rabbi, kimsingi ndani yao hakukuwa na tabia ya unyenyekevu lakini walijawa na tamaa ya kutafuta heshima na waliitengenezea mazingira ya kuipata, mtu alikuwa asipowaita baba hawaridhiki na wanaweza kumuona kama anadharau, mioyoni mwao walijisikia heshima kubwa sana kuitwa baba, Rabbi na Viongozi na vichwa vilivimba, na Kimsingi Yesu alikuwa akiwaona mpaka nia ya ndani moyoni mwao na tabia zao

Marko 12:38-40 “Akawaambia katika mafundisho yake, Jihadharini na waandishi, wapendao kutembea wamevaa mavazi marefu, na kusalimiwa masokoni, na kuketi mbele katika masinagogi, na viti vya mbele katika karamu; ambao hula nyumba za wajane, na kwa unafiki husali sala ndefu; hawa watapata hukumu iliyo kubwa.”

Matendo 7:1-3 “Kuhani Mkuu akasema, Je! Mambo hayo ndivyo yalivyo? Naye akasema, Ndugu zangu na baba zangu, sikilizeni: Mungu wa utukufu alimtokea baba yetu Ibrahimu, alipokuwa katika Mesopotamia, kabla hajakaa Harani, akamwambia, Toka katika nchi yako na katika jamaa zako, ukaende hata nchi nitakayokuonyesha.”

Mafarisayo na Waandishi walipenda kuitwa Rabbi na Baba, na kila aina ya heshima ya hadharani ambako kimsingi wangeweza kuheshimika, walijifikiria wenyewe kuwa ni watu wa kuheshimika na ni walimu wakubwa na ndio maana Yesu alitumia nafasi hii kuwafundisha wanafunzi wake kuwa kinyume na tabia isiyo ya mfano ya kutafuta heshima, kama walivyo wao mafarisayo na sio hivyo tu aliwakataza wanafunzi wake kutokumuita mtu awaye yote Baba au Rabi,  Alisisitiza kuwa wakristo Mwalimu wao ni mmoja tu Bwana Yesu na baba yao ni Mmoja tu Baba wa mbinguni, tofauti na hilo wakristo wote ni ndugu, kaka na dada katika Bwana na wote ni familia ya Mungu. Baba yetu wa Kiroho ni Mungu peke yake tulipofanyika kuwa wana wa Mungu baada ya kumpokea Yesu kama Bwana na mwokozi wa maisha yetu, tulifanyika wana wa Mungu kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kwa hiyo kuzaliwa kwetu kwa upya ni matokeo ya kazi ya Roho Mtakatifu na wala sio ya mwanadamu yeyote yule.

Tangu kuokolewa kwetu sisi sote tumekuwa wanafunzi wa Yesu na kila siku tunajifunza, Mwalimu wetu mkuu ni Yesu Kristo na Roho Mtakatifu kwa hiyo sisi sio Rabbis, wala mafundisho yetu asili yake sio sisi bali ni Yesu Kristo mwenyewe na Roho Mtakatifu. Kumbuka neno lile naye alitoa wengine hii maana yake yeye ndiye asili ya watumishi

Waefeso 4:11-13 “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo;”

Kristo Yesu ndiye anayetoa huduma ya kitume, kinabii, kiinjilisti, kichungaji na kialimu, wote hawa wanaongozwa na Roho Mtakatifu chanzo cha mafundisho yao ni Kristo mwenyewe na Roho Mtakatifu, kila aina ya mafundisho ya neno la Mungu asili yake ni Roho Mtakatifu yeye ndiye asili ya mafundisho yetu, Yesu alisema atakapokuja Roho wa Kweli atatufundisha na kwa sababu hiyo katika kanisa Roho wa Mungu amekuwa akitumia watu kufundisha kweli zake na kuyafunua maandiko.

Yohana 14:26 “Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.” 

Kristo anatufundisha kuwa badala ya kutafuta heshima miongoni mwa wanadamu sisi tunapaswa kuwa watumishi wa watu, unyenyekevu ni sehemu muhimu sana inayoweza kumfanya Mungu Roho Mtakatifu kuendelea kuleta mafundisho kwetu na kutufunulia jumbe zake kwaajili ya mwili wa Kristo, sisi au mimi na wewe sio chanzo cha mafundisho hayo bali Yesu mwenyewe, Mafarisayo na waandishi walijiweka katika nafasi ya kujifikiri kuwa wao ndo chanzo cha mafundisho na kuwa mafunuo ya kweli yanatoka kwao na wao ndio wenye mamlaka ya kuamuru mtu afundishe, wasipo kuidhinisha watahakikisha haukubaliki, hivyo wakakutana na fundisho hili zito kutoka kwa Yesu Kristo. Ni kwa nini hasa Yesu alitoa fundisho hili ambalo ni kama siku za karibuni kanisa linajisahau na kuanza tena kuwaita viongozi wa kiroho baba? Mimi niiteni Mchungaji tu inanitosha kwa nini Yesu alikataza? Hapa ziko sababu:-

Kumpa Mungu heshima anayoistahili – Yesu alikuwa anataka kukazia ukweli kwamba Baba wa mbinguni ndiye baba wa kweli wa watu wote waliomuamini Bwana Yesu na kumpokea kama Bwana na mwokozi wao, Hakuna mtu mwingine anayeweza kuichukua nafasi hiyo au hata kujipa nafasi hii, Yaani ya kumuita mtu mwingine baba katika maswala ya kiroho, Heshima ya baba wa kiroho ni heshima ya Mungu baba peke yake, ikiwa mtumishi wa Mungu awaye yote atajiita baba au watu wanamuita baba anajiweka katika hatari ya kuichukua heshima ya Mungu baba au utukufu wake, kwa hiyo ni lazima tuwaelimishe watu wasituite mtu baba. 


Malaki 1:6 “Mwana humheshimu baba yake, na mtumishi humcha bwana wake; basi, kama mimi ni baba yenu, heshima yangu iko wapi? Na kama mimi ni bwana wenu, kicho changu ki wapi? Bwana wa majeshi awauliza ninyi, enyi makuhani, mnaolidharau jina langu. Nanyi mwasema, Tumelidharau jina lako kwa jinsi gani? ” 


Isaya 42:6-8 “Mimi, Bwana, nimekuita katika haki, nami nitakushika mkono, na kukulinda, na kukutoa uwe agano la watu, na nuru ya mataifa; kuyafunua macho ya vipofu, kuwatoa gerezani waliofungwa, kuwatoa wale walioketi gizani katika nyumba ya kufungwa. Mimi ni Bwana; ndilo jina langu; na utukufu wangu sitampa mwingine, wala sitawapa sanamu sifa zangu.”


Yesu anatoa tahadhari kwa kusisitiza kwamba baba wa mbinguni ndiye baba wa kweli na halisi wa watu waliookolewa au walioamini, na kwamba hakuna mtu mwingine anayeweza kuichukua nafasi hiyo, kwa hiyo unapomuita mtu mwingine baba katika maana ya heshima ya kiroho, maana yake unampa mtu heshima ambayo inamstahili Mungu pekee, Mwenyewe ana hoji kama mimi ni Baba yenu heshima yangu iko wapi? 


Kuzuia mamlaka makubwa juu ya watu – Kwaasili Mungu alipomuumba mwanadamu alikusudia wanadamu kutawala viumbe vyote, lakini sio watu kuwatawala watu, Waandishi na mafarisayo walikuwa wamejenga mfumo wa kidini ambao ulikuwa unawapa mwanya wa wao kuwa na mamlaka kubwa juu ya maisha ya watu ni wao ndio walikuwa wanaamua hata nani aishi na nani auawe, inapofikia hatua ya mwanadamu kujipa mamlaka mpaka ya kuamua ni nani atakula au nani atakaa na njaa, nani atamuoa nani, na nani ataolewa na nani?  Mungu huwa anachukizwa na hali hiyo, Mwanadamu sio mtawala wa mwanadamu mwenzake lakini ni msimamizi tu, na ndio maana mitume hawakuwahi kutengeneza mifumo ya kiutawala bali mifumo ya kimaongozi, hakuna aliyekuwa mkubwa miongoni mwa wanafunzi Yesu., Mungu ni Mungu wa utaratibu na mifumo ya kisimamizi haina shida kwake lakini kumbuka hata wazee waliochaguliwa kumsaidia Musa katika uongozi, hawajawahi kuitwa baba, wala mitume hawajawahi popote pale kujiita baba na walipotumia neno baba au mwanangu au watoto wangu wadogo, hawakutumia maneno hayo katika mtazamo wa ubora bali katika mtazamo wa uhusiano.Musa ni nabii mkubwa sana aliyekuwa na uhusiano mkubwa na wa karibu na Mungu lakini hatuoni kokote katika maandiko akiitwa baba. Badala yake yeye alimuita Mungu baba.


Mwanzo 1:28-31 “Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi. Mungu akasema, Tazama, nimewapa kila mche utoao mbegu, ulio juu ya uso wa nchi yote pia, na kila mti, ambao matunda yake yana mbegu; vitakuwa ndivyo chakula chenu; na chakula cha kila mnyama wa nchi, na cha kila ndege wa angani, na cha kila kitu kitambaacho juu ya nchi, chenye uhai; majani yote ya miche, ndiyo chakula chenu; ikawa hivyo. Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya sita.”


Kumbukumbu 32:6 “Je! Mnamlipa Bwana hivi, Enyi watu wapumbavu na ujinga? Je! Yeye siye baba yako aliyekununua? Amekufanya, na kukuweka imara.”


Matendo 12:20-23 “Naye Herode alikuwa amewakasirikia sana watu wa Tiro na Sidoni; wakamwendea kwa nia moja, na wakiisha kufanya urafiki na Blasto, mwenye kukitunza chumba cha mfalme cha kulalia, wakataka amani; kwa maana nchi yao ilipata riziki kwa nchi ya mfalme. Basi siku moja iliyoazimiwa, Herode akajivika mavazi ya kifalme, akaketi katika kiti cha enzi, akatoa hotuba mbele yao. Watu wakapiga kelele, wakisema, Ni sauti ya Mungu, si sauti ya mwanadamu. Mara malaika wa Bwana akampiga, kwa sababu hakumpa Mungu utukufu; akaliwa na chango, akatokwa na roho.”


Herode alifikia hatua ya kuamua mtu wa kufa na mtu wa kuachiwa huru, alifikia hatua ya kuamua nani akae na njaa na nani anufaike na Mungu alimsubiria hapo baada ya kuwafunga mitume na kumuua Yakobo na kutaka kumuua Petro na kutawala watu wa Tiro na Sidoni kwa kuamua kuwanyima chakula maana wanaishi kwa mkono wake, Mungu alichukizwa na hatua hii, wakristo lazima tufikie ngazi ya kujihadhari sana kuwa na mamlaka juu ya watu, sisi ni viongozi tu wa kiroho, ni wasimamizi tu, hatuna mamlaka juu ya maisha ya watu, Mungu ametuweka kama watumishi ili tuwahudumie watu wa Mungu, na hili halimaanishi watu wa Mungu waache kuwaheshimu viongozi wa kiroho, hapana lakini sisi hatupaswi kutukuzwa, wala kujitukuza.


Kujifunza njia ya unyenyekevu – Katika tukio hili pia Bwana Yesu alikuwa akifundisha kuhusu umuhimu wa unyenyekevu, kuwakataza wanafunzi wake kuitwa baba au rabi au kiongozi alikuwa akiwaelekeza kinyume na mafarisayo na masadukayo na waandishi ya kuwa katika njia ya ufalme wa Mungu hakuna nafasi yoyote ya kujivuna na kujiona au kufikiri ya kuwa tuko juu kuliko wengine, Mungu kumuita mtu katika huduma ya  kitume, kinabii, kiinjilisti, kichungaji, na ualimu aliweka ndani mwetu huduma, na nyakati za leo uko utaratibu mzuri wa kimaongozi katika kanisa kama mtu ni Askofu mkuu ita tu Askofu mkuu, kama ni askofu wa jimbo ita tu askofu wa jimbo, kama ni mwangalizi ita tu mwangalizi, kama ni mchungaji ita tu mchungaji, ni mtume ita tu mtume, ni nabii ita tu nabii, na mwinjilisti ita tu mwinjilisti na mchungaji ita tu mchungaji, ni Mwalimu ita tu Mwalimu, ni padre ita tu padre, ni kuhani itatu tu kuhani, ni paroko ita tu paroko usimuite mtu baba, Hakuna  mahali popote katika maandiko ya agano jipya ambapo wakristo walimuita mtu baba, huduma hizo zenyewe ni heshima tosha maana zimetoka kwa Mungu, usianze na baba askofu, baba mchungaji, baba paroko, unaanza kujiingiza katika anga lingine wakati dhambi iliyomuangusha shetani ikiwa ni kiburi, sifa zilizomuinua Yesu Kristo na kumfanya awe na jina kuu kuliko yote ilikuwa ni tabia ya unyenyekevu. 


Ezekiel 28:11-17 “Ulikuwa ndani ya Adeni, bustani ya Mungu; kila jiwe la thamani lilikuwa kifuniko chako, akiki, na yakuti manjano, na almasi, na zabarajadi, na shohamu, na yaspi, na yakuti samawi, na zumaridi, na baharamani, na dhahabu; kazi ya matari yako na filimbi zako ilikuwa ndani yako; katika siku ya kuumbwa kwako zilitengenezwa tayari. Wewe ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye; nami nalikuweka hata ukawa juu ya mlima mtakatifu wa Mungu, umetembea huko na huko kati ya mawe ya moto. Ulikuwa mkamilifu katika njia zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata uovu ulipoonekana ndani yako. Kwa wingi wa uchuuzi wako watu walikujaza udhalimu ndani yako, nawe umetenda dhambi; kwa sababu hiyo nimekutoa kwa nguvu katika mlima wa Mungu, kama kitu kilicho najisi; nami nimekuangamiza, Ewe kerubi ufunikaye, utoke katika mawe hayo ya moto. Moyo wako uliinuka kwa sababu ya uzuri wako; umeiharibu hekima yako kwa sababu ya mwangaza wako; nimekutupa chini, nimekulaza mbele ya wafalme, wapate kukutazama.”


Wafilipi 2:5-11“Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba.”


Yesu hakumaanisha kuwa tusiwaite baba zetu wa kutuzaa kuwa baba, maandiko yanaposema tuwahehimu wazazi moja wapo ya sehemu ya heshima hiyo ni kuwaita kwa majina yao mzazi wa kiume baba na mzazi wa kike mama na tunapaswa kuwaheshimu. Wala Yesu hajafundisha kuwa tuache kuwaheshimu viongozi wetu wa kidini na kiimani na wa kiserikali tunapaswa kuwaheshimu sawasawa na madaraka ambayo Mungu amewapa na kuwanyenyekea 


1Timotheo 5:17 “Wazee watawalao vema na wahesabiwe kustahili heshima maradufu; hasa wao wajitaabishao kwa kuhutubu na kufundisha.”


Neno watawalao katika lugha ya kiyunani linalotumika hapo ni “Proistēmi” maana yake kwa kiingereza ni to preside – to be in a position of authority in a meeting or gathering, na neno lingine ni rule – governing au conducting a procedure, kwa Kiswahili kutawala kunakotajwa hapo ni mtu mwenye mamlaka ya kuongoza mkutano au kanisa, au kuendesha utaratibu, kwa msingi huo maandiko hayazungumzii kudhibiti “control” na watumishi wa Mungu wameonywa kuacha tabia ya kujifanya mabwana (Boss) katika mitaa yao


1Petro 5:1-3 “Nawasihi wazee walio kwenu, mimi niliye mzee, mwenzi wao, na shahidi wa mateso ya Kristo, na mshirika wa utukufu utakaofunuliwa baadaye; lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo. WALA SI KAMA WAJIFANYAO MABWANA JUU YA MITAA YAO, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile kundi. 


Petro anaeleza Mungu anavyotaka watu waongozwe si kama tujifanyao mabwana juu ya mitaa bali vielelezo kwa kundi, neno hilo mabwana maana yake “Boss” ambao lina tafasiri mbaya sana, na tunapoitwa baba ni kama tunaelekea huko, uongozi wa kikristo unatupa tahadhari sana kujilinda na kujihami kiasi cha kutokuangukia katika lawama na mtego wa ibilisi, mtego wa ibilisi ni kiburi na majivuno na hukumu ya ibilisi ni anguko linalotokana na kiburi na majivuno au kujiinua na hivyo kutupiliwa mbali nje ya neema ya Mungu


1Timotheo 3:6-7 “Wala asiwe mtu aliyeongoka karibu, asije akajivuna akaanguka katika hukumu ya Ibilisi. Tena imempasa kushuhudiwa mema na watu walio nje; ili asianguke katika lawama na mtego wa Ibilisi.”


Njia iliyo bora wakati wote ni kujifunza unyenyekevu kutoka moyoni na kuwa na tahadhari, shetani anaweza kuwatumia washirika wetu kutuingiza katika mtego wa ibilisi kwani wakati mwingine ni wao ndio wanaotuita baba hivyo hatuna budi kulikataa hilo na kuwafundisha kwamba ukiniita tu Mchungaji hiyo imetosha ni heshima kubwa na kuwa kuniita baba ni kunipalia makaa, tunaye baba mmoja baba wa roho zetu, Mungu.


Kujilinda na kujiweka katika nafasi ya Mungu – Mafarisayo na waandishi walijikweza mno kiasi cha kujiweka katika ngazi ya kutumikiwa na sio kuwatumikia watu, kujiinua sana kungewaweka katika hatari ya kujiweka katika nafasi ya Mungu, Bwana Yesu alikuwa anataka kututahadharisa na hilo, aidha Yesu alikuwa akionyesha tofauti ya mafundisho yake na yale ya ulimwengu huu, watu wa ulimwengu huu wanatafuta kujikweza na mwisho wa siku watahukumiwa na kutupwa chini, lakini wale wanaotubu na kunyenyekea watainuliwa 


Mathayo 18:1-4 “Saa ile wanafunzi wakamwendea Yesu wakisema, Ni nani basi aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni? Akaita mtoto mmoja, akamweka katikati yao, akasema, Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. Basi, ye yote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni.”


Marko 9:35 “Akaketi chini, akawaita wale Thenashara akawaambia, Mtu atakaye kuwa wa kwanza atakuwa wa mwisho kuliko wote, na mtumishi wa wote.


1Petro 5:5-6 “Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema.Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake;” 

Neno la Mungu linawataka wanafunzi wote wa Yesu kujivika unyenyekevu, na unyenyekevu wa kweli sio maigizo ni unyenyekevu kutoka ndani, kila mtu ajione na kujifunza kuwa hastahili mbele za Mungu na kuwa mtumwa wa wengine, mtu mnyenyekevu anatambua ya kuwa anayafanya yote kwa neema ya Mungu, unyenyekevu sio tabia rahisi kama tunavyodhani sababu kubwa ni kuwa kinyume cha unyenyekevu ni majivuno na kiburi jambo ambalo ndio dhambi ya ndani zaidi ya mwanadamu, ambayo shetani aliwaingizia wanadamu. 


Mwanzo 3:4-5 “Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi MTAKUWA KAMA MUNGU, mkijua mema na mabaya.” 


Shetani alitamani kuwa kama Mungu na ni aina hii ya wazo aliingiza kwa wanadamu na wakamkosea Mungu, kwa msingi huo ni lazima tuchukue tahadhari kuwa neno lolote, cheo chochote na nafasi yoyote ile ambayo anayestahili ni Mungu sisi ni lazima tujifunze kuwa mbali nayo, na sasa kwa bahati isiyo njema katazo hili la wanadamu kuitwa baba limetolewa na Yesu mwenyewe, je unataka kuabudiwa? Jilinde tujilinde na namna yoyote ile ya kutaka kuchukua nafasi ya Mungu, Yesu alihakikisha wakati wote nafasi ya ubaba inakwenda kwa anayestahili na ukichunguza katika maandiko Yesu ndiye anayeongoza kwa kutumia neno baba kuliko mtu awaye yote, Yesu amemtaja Mungu kwa kutumia neno baba mara zaidi ya 165 katika injili pekee mkazo huu sio wa kijinga, wala wa kupuuziwa wakati katika maandiko mengine ya kiyahudi ikiwepo agano la kale watu wamemtaja Mungu kama baba mara 15 tu, hii sio kwa sababu tu Yesu alikuwa mwana wa Mungu, bali kwa sababu Yesu alitaka uhusiano wa wanafunzi wake kwa Mungu uwe hivyo na kuwa mwenye sifa ya kuitwa baba ni Mungu peke yake.


Mathayo 23:8-12 “Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu.Wala msimwite mtu baba duniani; maana Baba yenu ni mmoja, aliye wa mbinguni. Wala msiitwe viongozi; maana kiongozi wenu ni mmoja, naye ndiye Kristo. Naye aliye mkubwa wenu atakuwa mtumishi wenu.Na ye yote atakayejikweza, atadhiliwa; na ye yote atakayejidhili, atakwezwa


Yohana 14:6-11 “Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi. Kama mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba; tangu sasa mnamjua, tena mmemwona. Filipo akamwambia, Bwana, utuonyeshe Baba, yatutosha.Yesu akamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuonyeshe Baba? Husadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu? Hayo maneno niwaambiayo mimi siyasemi kwa shauri langu; lakini Baba akaaye ndani yangu huzifanya kazi zake. Mnisadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu; la! Hamsadiki hivyo, sadikini kwa sababu ya kazi zenyewe.”


Wakati wote Yesu alihakikisha anamtambua baba yake na alimuita baba katika maeneo mengi sana, leo hii ukitaja baba basi lazima ufafanue ni yupi anazungumzwa, yaani yuko mwanadamu fulani tu mwenye madhaifu kibao anajiita baba, Mungu na atusaidie, ikiwa watu wanatuita hivyo tunaweza kuwafundisha na tunaweza kuwakataza na kuwafunulia maandiko ili wasituingize mtegoni, nao pia wasiingie mtegoni.


Matendo 14:8-15 “Na huko Listra palikuwa na mtu mmoja, dhaifu wa miguu, kiwete tangu tumboni mwa mamaye, ambaye hajaenda kabisa. Mtu huyo alimsikia Paulo alipokuwa akinena; ambaye akamkazia macho na kuona ya kuwa ana imani ya kuponywa, akasema kwa sauti kuu, Simama kwa miguu yako sawasawa. Akasimama upesi akaenda. Na makutano walipoona aliyoyafanya Paulo wakapaza sauti zao, wakisema kwa Kilikaonia, Miungu wametushukia kwa mifano ya wanadamu. Wakamwita Barnaba, Zeu, na Paulo, Herme, kwa sababu ndiye aliyekuwa mnenaji. Kuhani wa Zeu ambaye hekalu lake lilikuwa mbele ya mji, akaleta ng'ombe na taji za maua hata malangoni, akitaka kutoa dhabihu pamoja na makutano. Walakini mitume Barnaba na Paulo, walipopata habari, wakararua nguo zao, wakaenda mbio wakaingia katika makutano, wakipiga kelele, wakisema, Akina bwana, mbona mnafanya haya? Sisi nasi tu wanadamu hali moja na ninyi; twawahubiri habari njema, ili mgeuke na kuyaacha mambo haya ya ubatili na kumwelekea Mungu aliye hai, aliyeumba mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo;”


Roho Mtakatifu hutuelekeza wa kumuita baba – Ni muhimu kufahamu kuwa watu wote waliompokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yao na kuamini katika kazi aliyoifanya pale msalabani wanapewa neema ya kufanyika watoto wa Mungu, watu hawa wanazaliwa kwa mapenzi ya Mungu na sio ya mtu au mwili kwa sababu hiyo ni wana wa Mungu, kwa hiyo Mungu Roho Mtakatifu huwaelekeza watoto wake nani wa kumuita baba ona  


Yohana 1:12-13 “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu.”


Sio hivyo tu Biblia inatufundisha kuwa Roho Mtakatifu huweka mzigo ndani yetu kumuita Mungu baba kwa sababu yeye ndiye aliyewazaa kiroho kwa mapenzi yake na anatujulisha kuwa Mungu ndiye baba yetu na ya kuwa uhusiano wa karibu sana tulio nao watu tuliookolewa na Mungu ni uhusiano wa baba na mwana wake


Wagalatia 4:4-7 “Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana. Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, Aba, yaani, Baba. Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu.”


Warumi 8:14-15 “Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu. Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba.”


Warumi 8:15-16 “Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye.”


Abba”  ni neno linalotumika katika kiyunani kuonyesha uhusiano wa ndani zaidi wa mtu na baba yake ni neno lililolotumiwa na watoto wadogo kuita baba zao waliowazaa, Roho Mtakatifu tunapookoka anaweka hiyo hali ndani yetu tuliookolewa kuelekeza neno baba kwa Mungu wetu aliyetuumba na kutuokoa, kuonyesha uhusiano wa ndani tulio nae kama watoto wake, sasa basi ikiwa Roho Mtakatifu hutuelekeza sisi kumuita Mungu baba yetu, swali ni nani anayetuelekeza kumuita mtu wa kawaida ambaye ni kiongozi wa kiroho nani anatuelekeza kumuita baba? Usinijibu swali hilo! Ubaba wote wa mbinguni na duniani unaelekezwa wapi?


Waefeso 3:14-15 “Kwa hiyo nampigia Baba magoti, ambaye kwa jina lake ubaba wote wa mbinguni na wa duniani unaitwa,”


Kristo alikazia sana kutuelekeza kwa baba – Kama ilivyo kwa Roho wa Mungu kutufundisha na kutuelekeza wa kumuita baba, ni ukweli ulio wazi kuwa katika maandiko Yesu Kristo katika maisha na mafundisho yake alikazia sana sana sana neno baba akilielekeza kwa Mungu baba, kulikuwa na sababu maalumu sana za Yesu kulikazia hili, na ziko sababu maalumu za Roho Mtakatifu kutufundisha kumuita Mungu kama baba yetu, Kama Yesu ni kiongozi mkuu wa wokovu wetu na kama kweli tunafuata nyayo zake utaweza kuona akikazia katika maeneo mbalimbali katika maandiko akikazia kuhusu ubaba wa Mungu wetu.


Mathayo 11:25-27 “Wakati ule Yesu akajibu, akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga. Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyopendeza mbele zako. Akasema, Nimekabidhiwa vyote na baba yangu; wala hakuna amjuaye Mwana, ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba, ila Mwana, na ye yote ambaye Mwana apenda kumfunulia.”


Marko 14:35-36 “Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akiomba ya kuwa, ikiwezekana, saa hiyo imwepuke.Akasema, Aba, Baba, yote yawezekana kwako; uniondolee kikombe hiki; walakini, si kama nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe.”


Luka 23:34 “Yesu akasema, Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo. Wakagawa mavazi yake, wakipiga kura.”


Yohana 14:6-10 “Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi. Kama mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba; tangu sasa mnamjua, tena mmemwona. Filipo akamwambia, Bwana, utuonyeshe Baba, yatutosha. Yesu akamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuonyeshe Baba? Husadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu? Hayo maneno niwaambiayo mimi siyasemi kwa shauri langu; lakini Baba akaaye ndani yangu huzifanya kazi zake.”


Yohana 17:1-5 “Maneno hayo aliyasema Yesu; akainua macho yake kuelekea mbinguni, akasema, Baba, saa imekwisha kufika. Mtukuze Mwanao, ili Mwana wako naye akutukuze wewe; kama vile ulivyompa mamlaka juu ya wote wenye mwili, ili kwamba wote uliompa awape uzima wa milele.Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma. Mimi nimekutukuza duniani, hali nimeimaliza kazi ile uliyonipa niifanye. Na sasa, Baba, unitukuze mimi pamoja nawe, kwa utukufu ule niliokuwa nao pamoja nawe kabla ya ulimwengu kuwako.”


Yohana 17:21-26 “Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma. Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja. Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi.Baba, hao ulionipa nataka wawe pamoja nami po pote nilipo, wapate na kuutazama utukufu wangu ulionipa; kwa maana ulinipenda kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu. Baba mwenye haki, ulimwengu haukukujua; lakini mimi nalikujua, na hao wamejua ya kuwa ndiwe uliyenituma. Nami naliwajulisha jina lako, tena nitawajulisha hilo; ili pendo lile ulilonipenda mimi liwe ndani yao, nami niwe ndani yao.”


Mitume walielekeza watu kwa baba – Unapoangalia katika nyaraka zote za maelekezo na mafundisho ya mitume utaweza kuona wakilitii agizo la Yesu Kristo kwa kumtaja Mungu kama Baba, kwa hiyo ni wazi kuwa mamlaka ya ubaba ilipelekwa kwa usahihi kwa Mungu baba mwenyewe na wala sio kwa wanadamu, Wazo la ubaba wa Mungu halikuwa na Msingi sana katika agano la kale , lakini limekuwa ni jambo la msingi sana katika nyakati za gano jipya, huku Yesu akilitilia mkazo sana kuonyesha ni mapenzi ya Mungu, Baba aitwe baba, kwa hiyo utaweza kuona mitume waliukazia ubaba huu kuliko tunavyofikiri kumbuka kuwa mitume walikuwa makini sana, Yesu alifanya hivyo ili sisi tushike hili na kulitumia, labda limesahaulika lakini huu ndio wakati sahihi sasa wa kulikumbusha kanisa msituite baba, tunaye baba mmoja tu ndiye Mungu muumba.


1Wakorintho 8:6 “lakini kwetu sisi Mungu ni mmoja tu, aliye Baba, ambaye vitu vyote vimetoka kwake, nasi tunaishi kwake; yuko na Bwana mmoja Yesu Kristo, ambaye kwake vitu vyote vimekuwapo, na sisi kwa yeye huyo.”


1Wakorintho 1:3 “Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo.”


Wagalatia 4:6 “Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, Aba, yaani, Baba.”


Warumi 1:7 “kwa wote walioko Rumi, wapendwao na Mungu, walioitwa kuwa watakatifu. Neema na iwe kwenu na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo.”


Waefeso 5:19-21 “mkisemezana kwa zaburi na tenzi na nyimbo za rohoni, huku mkiimba na kumshangilia Bwana mioyoni mwenu; na kumshukuru Mungu Baba sikuzote kwa mambo yote, katika jina lake Bwana wetu Yesu Kristo; hali mnanyenyekeana katika kicho cha Kristo.”


Wakolosai 1:2 “kwa ndugu watakatifu, waaminifu katika Kristo, walioko Kolosai. Neema na iwe kwenu, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu.”


2Yohana 1:9 “Kila apitaye cheo, wala asidumu katika mafundisho ya Kristo, yeye hana Mungu. Yeye adumuye katika mafundisho hayo, huyo ana Baba na Mwana pia.”


1Yohana 2:1 “Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki,“


1Yohana 4:14 “Na sisi tumeona na kushuhudia ya kuwa Baba amemtuma Mwana kuwa Mwokozi wa ulimwengu.


Yakobo 1:17 “Kila kutoa kuliko kwema, na kila kitolewacho kilicho kamili, hutoka juu, hushuka kwa Baba wa mianga; kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeuka-geuka.”


1Wathesalonike 1:1-2 “Paulo, na Silwano, na Timotheo, kwa kanisa la Wathesalonike, lililo katika Mungu Baba, na katika Bwana Yesu Kristo. Neema na iwe kwenu na amani. Twamshukuru Mungu siku zote kwa ajili yenu nyote, tukiwataja katika maombi yetu.” 


Hitimisho


Msimwite mtu baba Duniani. Ni agizo la Bwana Yesu lililo la muhimu sana, Yesu alitaka kila mkristo aelewe  kuwa uhusiano wetu na Mungu ni wa karibu zaidi, Mungu ni Baba yetu na heshima yake kubwa ni ubaba wake ambao kimsingi heshima hii haipaswi kutolewa kwa mwingine kirahisi, kwa msingi huo katika maisha yetu ya kiroho tunaye baba mmoja tu ndiye Mungu. Nanyi msalipo semeni, Baba yetu uliye mbinguni ona:-


Mathayo 6:9-12 “Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje, Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.Utupe leo riziki yetu.Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu. Na usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu. [Kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele. Amina.]


Yesu alitaka watu wote waelewe kuwa Mungu pekee ndiye baba naye alikuja kutupa kielelezo tukifuate wengine wote wanaobaki ni watumishi wa Mungu kwaajili ya maisha yetu ya kiroho, ni wasimamizi tu, hawana mamlaka ya kutawala wanadamu, wana mamlaka ya kusimamia, heshima ya u baba ni ya Mungu pekee, Waandishi na mafarisayo walikuwa wamejenga mfumo ambao kwa bahati mbaya sana miaka ya hivi karibuni unarudi kwa kasi, mifumo inayowaruhusu wao kuwa na mamlaka makubwa juu ya watu, Yesu alitaka watu wasiwategemee viongozi wa kidini, Yesu alikataa mfumo huo na kuwakumbusha watu kuwa wanapaswa kumtegemea Mungu pekee. Aidha Yesu alitaka watu wawe wanyenyekevu na kuacha kujipa majina makubwa kwani kwa makusudi ya kupata heshima, uhusiano wetu na viongozi wa kidini na wao ni watu hauwezi kuwa uhusiano wa karibu kama uhusiano wetu na Mungu Baba, Hivyo ni Mungu pekee ndiye baba yetu, najua kuna watu wanaweza kuchukizwa na fundisho hili, lakini ni ukweli ulio wazi hatuwezi kuwa na akili au hekima kumzidi Yesu Kristo, kama Yesu amekataza wewe una nini? Endelea kujiita baba lakini yatakayokukuta mie simo, kazi yangu ni kukufunulia kweli za neno la Mungu na ni juu yako kuelewa, kutii au kuasi kukubali au kubisha. Lakini ukweli uko wazi kuwa washirika wengi sana nyakati za leo wanatuita baba, kila mahali ninakoenda nikijitambulisha kama mchungaji watu wanaita baba, ukweli sijawahi kuwakataza lakini moyoni ninapata taabu sana kwanini wakristo wanaacha kuniita mchungaji wananiita baba? Au kwa nini waniite baba mchungaji wakati nadhani ukiniita mchungaji tu inatosha, Ni ukweli ulio wazi kuwa mimi najua kuwa hawakuwa wamejifunza neno na agizo la Yesu na kulifikiri kwa kina lakini ilivyo ni kwamba hata Yesu hatumuiti baba, iweje Yesu aje akute mimi naitwa baba jina ambalo yeye hajawahi kulitumia wala Roho Mtakatifu hajawahi kutuongoza tumuite Yesu baba, wala mitume hawajafundisha wakristo kumuita mtu baba, wala biblia haijaelekeza kumuita mtu baba, alafu hapa kuna mtu mwanadamu tunamuita baba? Yesu Kristo mpaka dakika ya mwisho akiwa anapaa bado alikuwa akimtaja Mungu baba kama baba ona hii


Matendo 1:4-8 “Hata alipokuwa amekutana nao aliwaagiza wasitoke Yerusalemu, bali waingoje ahadi ya Baba, ambayo mlisikia habari zake kwangu; ya kwamba Yohana alibatiza kwa maji, bali ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu baada ya siku hizi chache. Basi walipokutanika, wakamwuliza, wakisema, Je! Bwana, wakati huu ndipo unapowarudishia Israeli ufalme? Akawaambia, Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe. Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.”


Kwa hiyo sasa itakuwaje? Kanisa hatuna budi kutubu, na kuacha mara moja kuwaita watumishi wa Mungu wowote wale Baba, watumishi wa Mungu ni lazima tukatae kuitwa baba, na ni muhimu kuwafundisha watu wote duniani kuacha mara moja kutuita baba, hivi hujawahi kujiuliza ni kwanini Mashehe na mamufti na viongozi wakubwa wa dini kama ya kiislamu hawawaiti viongozi wao wa dini baba?  na sasa wengine tumeenda mbali sana mpaka tuna BABA MTAKATIFU. Hii ni kufuru kubwa sana narudia tena hii ni kufuru kubwa sana narudia mara ya tatu hii ni kufuru kubwa sana, Shetani kuna mahali anataka kutupeleka taratibu bila sisi kujielewa, ile ile tabia yake ya kutaka kuwa kama Mungu anaipanda kwetu na kutuingizia bila kujua mwisho majina yote ya Mungu yatakuwa ndio ya wanadamu ni lazima tuwe makini na hili ndilo Mungu alinituma niweze kuwaonya watu, angalia kwa mujibu wa Yesu Kristo BABA MTAKATIFU ni nani? Ona:- 


Yohana 17:11-12. “Wala mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako. BABA MTAKATIFU, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo. Nilipokuwapo pamoja nao, mimi naliwalinda kwa jina lako ulilonipa, nikawatunza; wala hapana mmojawapo wao aliyepotea, ila yule mwana wa upotevu, ili andiko litimie.”


Makanisa yanayoongoza kwa kuita wachungaji na makuhani wao baba ni pamoja na Catholics, Orthodox, Anglican na Lutheran kwa bahati mbaya siku hizi hata watu waliookoka wameanza kuwaita wachungaji baba, Hata Haruni alikuwa ni kuhani mkuu lakini Wayahudi hawakumuita baba, kule kuchaguliwa tu na Mungu umtumikie ni heshima kubwa sana na inatosha. 


Lakini ni kwanini Catholics, Orthodox, Anglican na Lutheran huwaina makuhani wao na viongozi wao wa dini Baba? Akijibu swali hili Padre Colin Wen ambaye ni kuhani wa kikatoliki yeye alijibu hivi!


“Sio vibaya kabisa kumuita mtu mwingine baba sawa na katazo la Kristo katika Mathayo 23:9 yeye alisema kuwa mstari huu, unaweza kuwa umetafasiriwa vibaya kwa kuzingatia muktadha wa kile alichokuwa anakisema Bwana Yesu, Yesu hapa alikuwa anakemea tabia ya waandishi namafarisayo ambao waliweka mkazo wa kutafuta heshima hata kuliko utumishi wao kwa Mungu, Padre Colin Wen anaendelea kueleza kuwa ni kweli tuna baba mmoja tu wa mbinguni lakini makuhani wa kidini na wengine wanaoitwa baba wanatumia jina hili kwa sababu wanahusika katika ubaba huo kupitia utumishi wao,  na hivyo sio vibaya wakiitwa baba, wao sio baba kimamlaka lakini wanamuwakilisha baba mbinguni, kama jinsi ambavyo wao sio baba wa kimwili, aliongeza kuwa hata kuwaita baba viongozi wa kiroho maaskofu na makunani sio kitu ambacho kimeibuka siku za karibuni  kwani hata Paulo mwenyewe anasema 


1Wakorintho 4:14-15 “Siyaandiki hayo ili kuwatahayarisha; bali kuwaonya kama watoto niwapendao. Kwa kuwa ijapokuwa mna waalimu kumi elfu katika Kristo, walakini hamna baba wengi. Maana mimi ndimi niliyewazaa katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili.”


Kwa maelezo hayo anasema Paulo alijiona kuwa anafiti kabisa kujiita baba na akaeleza kuwa katika maandiko Petro, Paulo na Yohana wote waliwaona waamini wao kama watoto katika mtazamo wa kuwaona wao kuwa ni familia yao na kuwa uhusiano waliokuwa nao ulikuwa ni kama uhusiano wa baba na mwana anasema Petro alimuita Marko mwanangu , na Yohana akiwaita wakristo wanae


1Petro 5:12-13 “Kwa mkono wa Silwano, ndugu mwaminifu kama nionavyo, nimewaandikia kwa maneno machache, kuonya na kushuhudia ya kuwa hii ndiyo neema ya kweli ya Mungu. Simameni imara katika hiyo. Mwenzenu mteule hapa Babeli awasalimu, na Marko mwanangu.”


1Yohana 2:1-2 “Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki, naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote.” 


Anaeleza kuwa tabia hii iliendelea kuwa tabia ya kanisa kwa nyakati zote za maisha ya kanisa na akaeleza ndio maana Askofu mkuu wa kanisa Catholic anatumia jina Papa kama ilivyo kwa kiongozi wa kanisa la Coptic la huko Misri tangu enzi na enzi, Je hoja hizi zinajitosheleza? Kujenga fundisho? Kuwa watumishi wa Mungu wanaushiriki ubaba katika huduma na kwa sababu hiyo kuitwa kwao baba sio tatizo? Padre Colin Wen anaona kuwa japo wao sio baba wa kibailojia, lakini wanashiriki ubaba kila siku katika huduma kuanzia ubatizo na sakramenti nyinginezo na anaeleza kuwa kila siku katika huduma yake anashiriki ubaba huo na anauona na anasema anapoitwa baba inamkubusha kuwa yeye ni nani”. Mwisho wakumnukuu.


Kwa mtazamo wangu mimi naona Padre Colin Wen hoja zake hazina mashiko, kitendo cha kuchaguliwa tu na Mungu kuwa kuhani au Padre tayari kwa Mungu ni heshima kubwa sana, wangeridhika tu kuitwa Padre, au kuhani, au kasisi, na siew engine Mchungaji inatosha lakini nionavyo mimi kuna mstari mwembamba sana kati ya katazo la Yesu Kristo na utetezi wa kuitwa baba tunaoutaka na mtazamo mpana wa kibiblia, Petro kumuita Marko mwanangu, au Paulo kumuita Timotheo mwanangu, au Yohana kuwaita wakristo wanae, inaweza kuwa sio tatizo kwanza kwa sababu ya ukaribu mkubwa wa kimahusiano walio nao Petro na Marko na hali kadhalika Paulo na Timotheo, kama nilivyotangulia kufafanua hapo juu kwenye jinsi na namna neno baba lilivyoelezewa maana zake, lakini pia Umri wao ukilinganisha na washirika waliokuwepo wakati huo mfano Yohana alikuwa mzee sana ukilinganisha na washirika waliokuwako wakati huo kwa umri wake kutumia neno mwanangu haikuwa kitu cha kushangaza. Paulo na Timotheo walikuwa na ukaribu kiasi ambacho Timotheo alitahiriwa nadhani chini ya mamlaka ya Paulo na kama sio Paulo mwenyewe, wao walikuwa na uhusiano wa karibu na kihisia. 


Matendo 16:1-3 “Basi akafika Derbe na Listra, na hapo palikuwa na mwanafunzi mmoja jina lake Timotheo, mwana wa mwanamke Myahudi aliyeamini; lakini babaye alikuwa Myunani. Mtu huyo alishuhudiwa vema na ndugu waliokaa Listra na Ikonio. Paulo akamtaka huyo afuatane naye, akamtwaa akamtahiri kwa ajili ya Wayahudi waliokuwako pande zile; kwa maana wote walijua ya kuwa babaye ni Myunani.”


Kwa hiyo unaweza kuona uhusiano wa Paulo na Timotheo ulikuwa wa ndani kiasi ambacho Timotheo kuitwa mwanangu na Paulo halikuwa jambo la kushangaza, sina Muda sana wa kuzungumzia Marko Kwa Petro, Lakini wote tunajua jinsi ambavyo Petro alifahamiana na Marko tangu akiwa kijana mdogo katika jengo lililokuwako Yerusalem siku ya Pentekoste, na historia ya kanisa inaonyesha uhusiano huo, aidha ukubwa wa umri wa Yohana ambaye aliishi siku nyingi kuwaita wanae washirika pia sio jambo la kushangaza, na zaidi ya yote katazo la Kristo msimuite mtu baba, lilikuwa kwa wanafunzi wa Yesu tusimuite mtu baba duniani, sisi sasa ndio wanafunzi wa Yesu na swala hilo linatuhusu, lakini hatujakatazwa kumuita mtu mwanangu. Katazo linawahusu watu wasituite baba, tunaweza kujenga hoja za kimaandiko na Roho Mtakatifu Mwalimu mkuu anaweza kutufafanulia kama ni haki kuitwa baba katika uhusiano wa kiroho! Kwa sababu Baba ndiye Mwanzilishi wa Maisha yetu sifa ya Ubaba ni sifa ya Mungu peke yake na sio sisi, makasisi wa kikatoliki waitwe Padre, maksaisi wa kiprotestant na waitwe wachungaji, na majina mengineyo lakini hata hivyo swala la kuitwa baba katika uhusiano wa Kiroho linatuweka katika wakati mgumu ambao hakuna hoja ya kimaandiko ya kututetea.



Na Rev. Innocent Samuel Kamote


Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Hakuna maoni: