Kumbukumbu 33:24-27 “Na Asheri akamnena, Na
abarikiwe Asheri kwa watoto; Na akubaliwe katika nduguze, Na achovye mguu wake
katika mafuta. Makomeo yako yatakuwa ya chuma na shaba; Na kadiri ya siku zako
ndivyo zitakavyokuwa nguvu zako. Hapana aliyefanana na Mungu, Ee Yeshuruni,
Ajaye amepanda juu ya mbingu ili akusaidie. Na juu ya mawingu katika utukufu
wake. Mungu wa milele ndiye makazi yako, Na mikono ya milele i chini yako. Na
mbele yako amemsukumia mbali adui; Akasema, Angamiza.”
Utangulizi:
Moja ya tahadhari inayotolewa kwa
wahubiri wa neno la Mungu ni pamoja na kuhakikisha kuwa tunalitumia neno la
Mungu kwa halali, Neno la Mungu linatahadharisha kuwa walimu wa neno la Mungu
watapata hukumu iliyokubwa zaidi, kwa sababu hiyo ni muhimu kwa kila mtafasiri
wa neno la Mungu kulitafasiri kwa halali neno la kweli ili watu wa Mungu
wasipotoshwe na kujikuta wakipotezwa kwa kutokuwa na maarifa ya kuifahamu kweli
ya neno la Mungu, na kanuni zake za kulitafasiri! Neno la Mungu likitafasiriwa
kwa usahihi linaleta mwelekeo sahihi kwa watu wa Mungu. Tafasiri sahihi na
njema kwa neno la Mungu huwajengea watu makuzi sahihi ya kiroho, kuikulia Imani
sahihi na kujenga uhusiano imara na Mungu na kujiepusha na matumizi mabaya ya
maandiko yatakayopelekea kuzuka kwa Imani potofu au Imani za kizushi na
kuwafanya wadamu wasitimize kusudi sahihi la Mungu katika maisha yao!
2Timotheo 2:14-15 “Uwakumbushe mambo hayo,
ukiwaonya machoni pa Mungu, wasiwe na mashindano ya maneno, ambayo hayana
faida, bali huwaharibu wasikiao. Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na
Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la
kweli.”
Yakobo 3:1-2 “Ndugu zangu, msiwe waalimu
wengi, mkijua ya kuwa mtapata hukumu kubwa zaidi. Maana twajikwaa sisi sote pia
katika mambo mengi. Mtu asiyejikwaa katika kunena, huyo ni mtu mkamilifu,
awezaye kuuzuia na mwili wake wote kama kwa lijamu.”
Kwa msingi huo basi leo nataka
tuchukue muda kujifunza kwa kina na mapana na marefu tafasiri ya Maana ya kuchovya mguu wako katika Mafuta!
Ili kwamba kila mwanafunzi wa Yesu Kristo aweze kuwa na ufahamu wa kutosha na uliosahihi kuhusu fundisho linaloendelea
mitaani ambapo kumekuwako na watumishi wa Mungu wanaowakanyagisha watu mafuta
wakifikiri kuwa kwa kufanya hivyo wanaweza kusababisha mabadiliko ya maisha ya
watu kiroho, kiuchumi na kimwili jambo ambalo sio sahihi, na wakristo wengi sana wasomi kwa wasio wasomi
lakini wasio na ujuzi kuhusu neno la Mungu wameshawishika kukanyaga mafuta
halisi kwa kutumia tafasiri isiyo halisi ya neno la Mungu, tutajifunza somo
hili Maana ya kuchovya mguu wako katika
Mafuta! Kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuafuatayo:-
·
Umuhimu
wa kuzingatia kanuni za kutafasiri maandiko.
·
Tafasiri
halisi ya Maana ya kuchovya mguu wako katika Mafuta!
·
Jinsi ya
kuchovya mguu wako katika Mafuta!
Umuhimu wa kuzingatia kanuni za kutafasiri maandiko.
Moja ya changamoto kubwa
inayolikumba kanisa la Mungu katika nyakati za leo ni pamoja na kuweko kwa
kundi kubwa la mashambulizi ya mafundisho ya uongo ambayo yamekuwa mwiba na
usumbufu mkubwa katika kanisa la Mungu kwa miaka mingi, unaweza ukalichukulia
swala hili kuwa ni swala la kawaida, lakini ni ukweli usioweza kupingika kuwa
Mungu hafurahii watu wanaojitafasiria neno lake kama wapendavyo, Biblia ni
kitabu cha Heshima kubwa sana ni neno la Mungu na kwa sababu hiyo haipendezi
hata kidogo kila mtu tu akijitafasiria maandiko kama apendavyo kamwe huo sio
mpango wa Mungu, Roho Mtakatifu ndiye mwandishi mkuu wa Biblia na bila shaka
hangeweza kufurahia watu wajitafasirie neno lake kama watakavyo tu kwa mapenzi
yao wenyewe!
2Petro 1:19-21 “Nasi tuna lile neno la
unabii lililo imara zaidi, ambalo, mkiliangalia, kama taa ing'aayo mahali penye
giza, mwafanya vyema, mpaka kutakapopambazuka, na nyota ya asubuhi kuzuka
mioyoni mwenu. Mkijua neno hili kwanza, ya kwamba hakuna unabii katika maandiko
upatao kufasiriwa kama apendavyo mtu fulani tu. Maana unabii haukuletwa po pote
kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu,
wakiongozwa na Roho Mtakatifu.”
Mungu anachukizwa sana pale watu
wanaposema kile ambacho yeye hajawahi kukisema, nakumbuka niliwahi kuwa na Muhasibu
ambaye alikuwa akiandika jina langu katika namna ambayo mimi mwenyewe sikuwahi
kuitwa hivyo, Mimi naitwa INNOCENT
SAMUEL KAMOTE Lakini muhasibu wangu yeye alikuwa akiandika jina langu INNOCENT SAMWELI KAMMTTE nililalamika mara kadhaa kuwa Jina langu
unavyoliandika sivyo linavyopaswa kuwa lakini hata hivyo hakujali na aliendelea
kuliandika jina langu katika namna hiyo hiyo aliyokuwa anataka yeye, mimi sio
mwepesi wa hasira lakini hata hivyo nilianza kumtafasiri vibaya muhasibu huyu
aliyekazania kuliandika jina langu katika namna anayoitaka yeye hata pamoja na
kumuonyesha vitambulisho vyangu vilivyo na jina sahihi,yeye aliendelea
kuliandika jina langu katika namna hiyo hiyo aliyoikubali yeye na hakukubali
masahihisho, kimsingi nilianza kumchukia na kumuona kama mtu mwenye nia ovu kwa
maslahi yangu kwani nafahamu kuwa dosari katika jina la mtu hasa ikiachwa hivyo
katika documents muhimu linaweza kuwa na athari kubwa sana baadaye
utakapohitajika kuthibitisha uhalisi wa mtu anayetajwa hapo na ukweli kuhusu
jina lako, sio hivyo tu nilianza kuingia shaka kuhusu elimu yake na aidha akili
zake, kwa hiyo sikuwa namfurahia tena, na alipoteza umuhimu wake kwangu, katika
maumivu kama hayo ni ukweli ulio wazi kuwa Mungu anachukizwa sana watu
wanapomnukuu vibaya tofauti na maana aliyokuwa anaikusudia kwenye neno lake,
Mungu anataka neno lake lisemwe kwa uaminifu na kama mtu hataki aache, Mungu
hataki kusingiziwa kwamba amesema kitu ambacho yeye hakukisema, iwe ni kwa
misingi ya ndoto wala mafunuo anataka atendewe haki katika tafasiri halali kwa
neno lake ili watu wake wasipotoshwe ona
Yeremia 23:25-32.“Nimesikia waliyoyasema
manabii wanaotabiri uongo kwa jina langu, wakisema, Nimeota ndoto; nimeota
ndoto. Je! Mambo hayo yatakuwa katika mioyo ya manabii wanaotabiri uongo hata
lini, manabii hao wenye udanganyifu katika mioyo yao wenyewe? Wanaodhania ya
kuwa watawasahaulisha watu wangu jina langu kwa ndoto zao, wanazomhadithia kila
mtu jirani yake, kama vile baba zao walivyolisahau jina langu, kwa ajili ya
Baali. Nabii aliye na ndoto, na aseme ndoto yake; na yeye aliye na neno langu,
na aseme neno langu kwa uaminifu. Makapi ni kitu gani kuliko ngano? Asema
Bwana. Je! Neno langu si kama moto? Asema Bwana; na kama nyundo ivunjayo mawe
vipande vipande? Basi kwa sababu hiyo mimi ni juu ya manabii hao, asema Bwana,
wanaompokonya kila mtu jirani yake maneno yangu. Tazama, mimi ni juu ya
manabii, asema Bwana, wanaotumia ndimi zao na kusema, Yeye asema, Tazama, mimi
ni juu ya hao wanaotabiri ndoto za uongo, asema Bwana, na kuzisema, na
kuwakosesha watu wangu kwa uongo wao, na kwa majivuno yao ya upuzi, lakini mimi
sikuwatuma, wala sikuwapa amri; wala hawatawafaidia watu hawa hata kidogo,
asema Bwana.”
Kwa msingi huo hatuwezi
kulichezea neno la Mungu na kuruhusu litafasiriwe vyo vyote vile kama watu
wanavyotaka, ziko kanuni zinazoongoza tafasiri halali kwa neno la Mungu, katika
karne ya 20 wa NAZI wa Ujerumani
waliona kuwa kuna uhalali wa kuwaangamiza wayahudi na kuwaua kwa sababu
walitumia andiko la Mathayo 27:24-25
vibaya:-
Mathayo 27:24-25 “Basi Pilato alipoona ya
kuwa hafai lo lote, bali ghasia inazidi tu, akatwaa maji, akanawa mikono yake
mbele ya mkutano, akasema, Mimi sina hatia katika damu ya mtu huyu mwenye haki;
yaangalieni haya ninyi wenyewe. Watu wote wakajibu wakasema, Damu yake na iwe
juu yetu, na juu ya watoto wetu.”
Tafasiri yoyote mbaya ya
kimaandiko inaweza kuleta matokeo mabaya yasiyokusudiwa katika jamii wala
yasiyo sawa na mapenzi ya Mungu, kama kila mwanadamu anapenda kunukuliwa vizuri
basi Mungu anapenda kunukuliwa vizuri zaidi. Katika mtindo kama huo Madaktari
wanafahamu athari zinazoweza kutokea endapo mtu atazidishiwa dozi au kupewa
dozi chini ya kiwango wakati wa kumtibu mgonjwa kufanya hivyo kunaweza
kusababisha madhara ya usugu wa dawa au kumuumiza mgonjwa, kadhalika neno la
Mungu linaagizwa litafasiriwe kwa halali na sio kwa maslahi ya mtu na mafunuo
yake au ndoto zake, sio kila mtu ana sifa ya kuwa mtafasiri wa maandiko, na sio
kila mtu anaweza kuelewa neno la Mungu bila msaada wa mtu mwingine, na wako
watu Mungu amewaweka ili waifanye kazi hiyo ya kuelewesha wengine neno la Mungu
ili malengo yake yaweze kufikiwa. Kwa hiyo usipuguze wala kuongeza neno.
Matendo 8:29-35 “Roho akamwambia Filipo,
Sogea karibu na gari hili, ukashikamane nalo. Basi Filipo akaenda mbio,
akamsikia anasoma chuo cha nabii Isaya; akanena, Je! Yamekuelea haya unayosoma?
Akasema, Nitawezaje kuelewa, mtu asiponiongoza? Akamsihi Filipo apande na kuketi
pamoja naye. Na fungu la Maandiko alilokuwa akilisoma ni hili, Aliongozwa
kwenda machinjoni kama kondoo, Na kama vile mwana-kondoo alivyo kimya mbele
yake amkataye manyoya, Vivyo hivyo yeye naye hafunui kinywa chake. Katika
kujidhili kwake hukumu yake iliondolewa. Ni nani atakayeeleza kizazi chake? Kwa
maana uzima wake umeondolewa katika nchi. Yule towashi akamjibu Filipo,
akasema, Nakuomba, nabii huyu; asema maneno haya kwa habari ya nani; ni habari
zake mwenyewe au za mtu mwingine? Filipo akafunua kinywa chake, naye, akianza
kwa andiko lilo hilo, akamhubiri habari njema za Yesu.”
Kumbukumbu 4:1-2 “Na sasa, Ee Israeli,
zisikilizeni amri na hukumu niwafundishazo, ili mzitende; mpate kuishi na
kuingia na kuimiliki nchi awapayo Bwana, Mungu wa baba zenu. Msiliongeze neno
niwaamurulo wala msilipunguze, mpate kuzishika amri za Bwana, Mungu wenu,
niwaamuruzo.”
Wakati mwingine ili mtu aelewe
neno la Mungu anahitaji kuongozwa na wale ambao Mungu ameweka neema maaalumu ya
kuwa wakufunzi wa neno la Mungu, kumbuka sisi ni wanafunzi wa Yesu na tunapaswa
kujifunza kila iitwapo leo, tukiwa na moyo wa unyenyekevu na kuweka kiburi
pembeni Mungu anaweza kutufundisha njia yake kwa usahihi zaidi.
Matendo 18:24-28 “Basi Myahudi mmoja, jina
lake Apolo, mzalia wa Iskanderia, mtu wa elimu, akafika Efeso; naye alikuwa
hodari katika maandiko. Mtu huyo alikuwa amefundishwa njia ya Bwana; na kwa
kuwa roho yake ilikuwa ikimwaka, alianza kunena na kufundisha kwa usahihi
habari za Yesu; naye alijua ubatizo wa Yohana tu. Akaanza kunena kwa ujasiri
katika sinagogi; hata Prisila na Akila walipomsikia wakamchukua kwao,
wakamweleza njia ya Bwana kwa usahihi zaidi. Na alipotaka kuvuka bahari aende
mpaka Akaya, ndugu wakamhimiza, wakawaandikia wale wanafunzi wamkaribishe, naye
alipofika akawasaidia sana wale waliokwisha kuamini kwa neema ya Mungu. Kwa
maana aliwashinda Wayahudi kabisa kabisa mbele ya watu wote, akionyesha kwa
maneno ya maandiko ya kuwa Yesu ni Kristo.”
Kwa hiyo wakristo tunakubaliana
kuwa mtu anaweza kusoma neno la Mungu na asielewe bila uongozi, na pia mtu
anaweza kuwa muhubiri lakini asihubiri kwa usahihi kama hajafundishwa vizuri na
tunakubaliana kuwa maandiko yana kanuni zake katika kulitafasiri neno la Mungu
ili yamkini liweze kutendewa haki katika tafasiri zake na kutumika kwa halali
jambo ambalo linamfurahisha Mungu pia, tusiruhusu kitabu chetu kitakatifu
kikatafasiriwa kama apendavyo mtu tu kwa mapenzi yake mwenyewe bali sawa na
kanuni za kiungwana na kiungu sawasawa na mapenzi ya Mungu. Kwa sababu hiyo ziko kanuni rahisi kumi
zinazoongoza watu wa Mungu katika kutafasiri maandiko na ingawa hatutakuwa na
muda wa kuzifafanua sana kwa undani lakini zinaweza kukupa mwanga wa namna ya
kusimamia tafasiri njema na sahihi ya maandiko:-
1. Lazima
mtafasiri wa maandiko awe na Kanuni ya
utii (The Principle of Obidience) – hii ni kanuni ya dhamiri njema,
mtafasiri wa maandiko lazima ahakikishe kuwa ana moyo wenye dhamiri njema na
kuwa mpango wake ni kumtii Mungu, na
kumtumikia kwa dhati, Kila mwanadamu mwenye utii kwa mapenzi ya Mungu na mwenye
dhamiri njema Mungu humsaidia muelekeo wake wa moyo kuwa na uweza wa kuifahamu
kweli na hata akikosea kwa sababu alikuwa na dhamiri safi rehema za Mungu huwa
juu yake, kwa sababu Mungu akiiangalia nia yake anaona kuwa ni mtu mwenye
mapenzi mema, Mungu hawezi kuwa radhi na mtu anayekusudia mabaya wakati
wanapotaka kulitafasiri neno la Mungu, hata hivyo utii na dhamiri njema
havitoshi peke yake vinaweza kutosha kwa Mungu anayechunguza mioyo lakini
havitoshi kwetu kwa sababu tutajuaje kuwa ulikuwa na dhamiri njema iwapo
fundisho lako limesababisha upotofu miongoni mwa jamii? Kwa hiyo kanuni ya utii
inaweza kukuweka salama kwa Mungu tu lakini haikuachi salama kwetu sisi
tuliosomea utaalamu wa kutafasiri maandiko haikuweki salama kwa sababu neno la Mungu linasema Moyo una
ugonjwa wa kufisha
Yeremia 17:9-10 “Moyo
huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye
kuujua? Mimi, Bwana, nauchunguza moyo, navijaribu viuno, hata kumpa kila mtu
kiasi cha njia zake, kiasi cha matunda ya matendo yake.”
Kwa hiyo
wakristo wana haki ya kuyachunguza maandiko ili waone kama kile kinachohubiriwa
na kusemwa ni kitu sahihi ama hapana! Hapo haijalishi anayehubiri ni nani na
ana mamlaka gani lazima tumpime katika maandiko ili tuone yale anayotupa ndio
mapenzi ya Mungu hasa, kinyume cha hapo tutakuwa tumekosa uungwana, watu wa
Beroya hawakuwahi kujali kuwa Paulo ana mafunuo gani laiki waliyachunguza
maandiko wajionee wenyewe kama mambio ndivyo yalivyo, usiamini katika moyo wa
mtu.
Matendo 17:10-11 “Mara
hao ndugu wakawapeleka Paulo na Sila usiku hata Beroya. Nao walipofika huko
wakaingia katika sinagogi la Wayahudi. Watu hawa walikuwa waungwana kuliko wale
wa Thesalonike, kwa kuwa walilipokea lile neno kwa uelekevu wa moyo,
wakayachunguza maandiko kila siku, waone kwamba mambo hayo ndivyo yalivyo.”
2. Lazima
mtafasiri wa neno la Mungu awe na uelewa kuhusu Kanuni ya uvuvio (The Principle
of Inspiration) – hii ni kanuni inayomsaidia kujua kuwa kila andiko lenye
pumzi ya Mungu linafaa kwa mafundisho, kwa hiyo tunaweza kuwafundisha watu neno
la Mungu kwa njia nyepesi tu na kama tuna mapenzi mema tutawaelekeza watu wake
katika mapenzi yake kwa kutumia neno la Mungu kwa sababu lijna pumzi ya Mungu
2Timotheo 3:16-17 “Kila
andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa
yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe
kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.”
Kanuni hii
haitoshi ingawa kuna ukweli kuwa kila andiko lenye pumzi ya Mungu linafaa kwa
mafundisho, lakini maandiko yanahitaji ulinganifu wa kina na ndio maana shetani
pia alipoona Yesu anatumia maandiko naye akayatumia lakini si kwa nia nzuri kwa
hiyo uko ulinganifu maalumu unaohitajika katika kujua andiko fulani
linatumikaje na kwa wakati gani
Mathayo 4:5-7 “Kisha
Ibilisi akamchukua mpaka mji mtakatifu, akamweka juu ya kinara cha
hekalu,akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini; kwa maana
imeandikwa, Atakuagizia malaika zake; Na mikononi mwao watakuchukua; Usije
ukajikwaa mguu wako katika jiwe.Yesu akamwambia, Tena imeandikwa, Usimjaribu
Bwana Mungu wako.”
3. Lazima
mtafasiri wa Maandiko pia awe na uelewa kuhusu Historia na mazingira ya andiko
(Mukhtadha) (Principle of Historical
Context) – hapa mtafasiri anapaswa kujifunza historia ya Mazingira yanayozunguka
andiko husika mfano historia ya mji wa Korintho, lugha zao, wakati ambapo neno
linaandikwa, tamaduni zao, jamii yao na kadhalika , sio hivyo tu lazima
mtafasiri aelewe kitu kilichoandikwa au kusemwa pamoja na maneno yote na maana
zake zinazozunguka andiko husika, mazingira yaliyopelekea kutamkwa kwa maneno
hayo huo ndio muktadha, tafasiri hii
inakulazima uwe msomi ili uweze kujua lugha za wakati ule, tamaduni za wakati
ule, jamii ya wakati ule, na jinsi tunavyoweza kulitumia andiko hilo kwa sasa,
lazima uwe na kamusi au ujuzi wa lugha za asili kwaajili ya kupata maana sahihi
iliyokusudiwa na mwandishi
4. Lazima
mtafasiri aweze pia kufanya uchunguzi wa kimaandiko yaani “ajue yaliyomo” lugha zilizotumika misamiati iliyotumika na maana ya
maneno yanayotumika,- (Principle of
content) mfano lugha hiyo ni ya namna gani, maneno yake yana maana gani
anaweza pia kwenda kwenye lugha za asili kama kiebrania, kiaramu, kiyunani na
kilatini ili kupata matumizi ya lugha halisi ya wakati ule na jinsi inavyoweza
kutumika katika wakati wa sasa, lazima uchunguze kuwa lugha hiyo ni ya
kimafumbo au ya kawaida inaweza kutafasiriwa kama kawaida au inaweza kuwa
fumbo? Na madhara gani yanaweza kujitokeza, ni lazima uwe na ujuzi kuhusu
kitabu unachotaka kukitafasiri kama ni cha kinabii, kimashairi, kihistoria,
sheria, nyaraka, au injili na msemaji alikuwa akizungumza na jamii ya watu wa
aina gani, kwa wakati gani, kwa tamaduni gani na inaweza kutuhusu vipi sisi
katika nyakati za leo, Lazima uwe na ujuzi kuhusu stori nzima, somo zima, wazo
zima, mpangilio mzima, mtiririko mzima na nia nzima ya mwandishi na yote
yaliyomo kabla na baada ya andiko husika.
5. Lazima
mtafasiri pia wakati mwingine achukue “lugha
rahisi” tu iliyoko kama ilivyo bila kutumia utaalamu kutafasiri japo kwa
kufanya hivyo mtafasiri anaweza anaweza kujikuta yuko katika wakati mgumu kwa
sababu sio kila lugha iliyotumika inaweza kuwa na maana hizo, ziko lugha za
mficho, za kimashairi, za kimafumbo, za kinabii, na kadhalika (The
principle of simplicity) ziko Lugha au maana katika biblia ambazo
hazihitaji tafasiri yoyote kwa hiyo ukizichukulia kama zilivyo bila kutafasiri
unakuwa salama, huitaji kuyafanya mambo kuwa magumu, lakini yako maandiko
ambayo yanahitaji kutokuchukuliwa kirahisi au kama yalivyo mfano:-
-
Jicho
lako likikukosesha ling’oe – Mathayo 18:8-9 “Basi
mkono wako au mguu wako ukikukosesha, ukate ukautupe mbali nawe; ni afadhali
kuingia katika uzima hali umepungukiwa na mkono au mguu, kuliko kuwa na mikono
miwili au miguu miwili, na kutupwa katika moto wa milele. Na jicho lako
likikukosesha, ling'oe, ukalitupe mbali nawe; ni afadhali kuingia katika uzima
una chongo, kuliko kuwa na macho mawili, na kutupwa katika jehanum ya moto.”
-
Je unaweza kulichukua andiko hilo hapo juu na
kulitafasiri kama lilivyo? Je andiko hilo ni la kawaida au ni la kimafumbo? Sasa
ukichukulia kila kitu kama kilivyoandikwa hutaweza kupata tafasiri sahihi ya
andiko hilo hali kadhalika neno na “Na achovye
mguu wake katika mafuta”. Haliwezi
kuchukuliwa katika maana yake nyepesi au rahisi kama ilivyo hiyo ilikuwa lugha
inayohitaji ufafanuzi, ukiichukulia kama ilivyo wajinga watakanyaga mafuta
6. Lazima
mtafasiri pia ajifunze kufanya ulinganifu wa kimaandiko (The Principle of Harmonisation) yaani ili uweze kufanya fundisho
kutoka katika andiko basi andiko hilo liwe na mashahidi wawili au watatu, ni
lazima ufanye ulinganifu wa fundisho unalotaka kulitengeneza kutoka katika
ushahidi wa maandiko mengine (Combination
of scriptures references) Biblia imekaa katika mfumo unaotegemeana sana kwa
sababu hiyo huwezi kuchomoa uzi mmoja wa nguo kisha ukadai kuwa hii ni nguo,
nguo kamili ni mfungamano wa nyuzi nyingi zinazoifanya nguo kuwa nguo kwa hiyo
mzani wako wa ulinganifu wa maandiko utakusaidia kuwa na fundisho sahihi na hupaswi kusingizia kila kitu kuwa
kimetokana na ufunuo wa kiungu
Isaya 28:9-10 “Atamfundisha
nani maarifa? Atamfahamisha nani habari hii? Je! Ni wale walioachishwa maziwa,
walioondolewa matitini? Kwa maana ni amri juu ya amri, amri juu ya amri; kanuni
juu ya kanuni, kanuni juu ya kanuni; huku kidogo na huku kidogo.”
2Wakorintho 13:1 “Hii
ndiyo mara ya tatu ya mimi kuja kwenu. Kwa vinywa vya mashahidi wawili au
watatu kila neno litathibitishwa.”
Kumbukumbu 19:15 “Shahidi mmoja asimwinukie mtu awaye yote
kumshuhudia kwa uovu wo wote, wala kwa dhambi yo yote, katika makosa akosayo yo
yote; jambo na lithibitishwe kwa vinywa vya mashahidi wawili, au watatu.”
7. Lazima
uwe na utaalamu wa kutosha kuhusu ulinganifu wa maswala ya agano la kale na
agano jipya, (The Principles of Covenants)
uwe na ufahamu kuwa ni mafundisho gani hasa yaliweza kuwahusu watu wa agano la
kale na kwa wakati gani na wale wa agano
jipya, sheria zipi zilifaa kwa wakati ule na zipi hazifai kwa wakati huu na ni
yapi mapenzi ya Mungu hasa kwa wakati wetu
Matendo 17:30-31 “Basi,
zamani zile za ujinga Mungu alijifanya kama hazioni; bali sasa anawaagiza watu
wote wa kila mahali watubu. Kwa maana ameweka siku atakayowahukumu walimwengu
kwa haki, kwa mtu yule aliyemchagua; naye amewapa watu wote uthabiti wa mambo
haya kwa kumfufua katika wafu.”
8. Lazima
uwe na utaalamu wa kujua ni mambo gani hasa yametimizwa katika ufalme wa Mungu
na yale ambayo bado hayajatimizwa, Kanuni
za ufalme wa Mungu (The Principle of
the Kingdom) yako maswala kadhaa katika maswala yahusuyo ufalme wa Mungu
ambayo yametimizwa na ambayo bado, kwa hiyo mtaalamu wa neno la Mungu anapaswa
kuwa na uelewa huo.
9. Lazima
mtaalamu wa kutafasiri maandiko awe na ujuzi wa kina na wa kutosha kuhusu
kutafasiri mifano ya ufalme wa Mungu (The
Principle of Parables) mifano ya ufalme wa Mungu ina kanuni zake na
taratibu zake na inabeba maana moja kubwa iliyokusudiwa na hivyo huwezi
kuitafasiri kama unayefanya uchambuzi
10. Lazima
mtaalamu wa neno la Mungu awe na ujuzi wa kina kuhusu maswala ya unabii, (The Principle
of Prophecy) ajue kuwa ni unabii gani umeshatimizwa na upi ambao bado
haujatimizwa ili kujua ni namna gani anaweza kuyaweka sawa maswala ya kinabii
asikosee au kwenda kinyume na zile kanuni za kimungu na ile tabia za unabii
kujirudia kwa mfumo za zaidi ya mara moja.
Hizo hapo juu ni kanuni kumi
muhimu zinazomuongoza mtafasiri wa maandiko kulitafasiri neno la Mungu kwa
halali, sina muda mkubwa sana wa kuzielezea hapa kwa kina lakini zinapatikana katika somo maalumu
la kitheolojia linalohusika na namna na jinsi ya kuyatafasiri maandiko kwa
halali somo hilo kitaalamu katika vyo vya Biblia linaitwa the “Principles of Biblical
interpretations” au “Hermaneutics” the sientifical study of the methodological
principles of interpretation of the Bible kwa Kiswahili hizo ni sayansi za
ufundi na njia au kanuni za kimatumizi katiika kutafasiri maandiko au
Biblia, kwa hiyo watumishi wa Mungu
wanaokuwa wameitwa na Mungu na kukubali kwenda katika vyuo vya Biblia
hufundishwa masomo hayo kwa kusudi au lengo la kupunguza changamoto za
kutafasiri vibaya maandiko, Uchungaji hausomewi, lakini yeye aliyeitwa anapaswa
kuupeleka witio wake katika vyuo vya Biblia kwa walimu kwa kusudi la kuunoa
wito wako ili uyatumie maandiko kwa halali au kwa mujibu wa kanuni kwa hiyo mtu
anyezingatia kanuni hizo sasa anakuwa katika nafasi nzuri sasa ya kulitendea
haki neno la Mungu kwa kuitafasiri Biblia katika njia iliyo njema, hairuhusiwi
kutengeneza maana yako ya kibiblia kisha ukalisingizia andiko, to guide in “EISOGESIS” na badala yake unatakiwa kutafuta maana
iliyokusudiwa na mwandishi na kuiweka wazi kwa jamii unayoifundisha to guide out “EXEGESIS” wale
wanaotafuta maana iliyokusudiwa na mwandishi kwa wakati wake kisha wakatafuta
namna ya kuitumia maana ile kwa wakati huu wa sasa wako salama kabisa katika
kulitafasiri neno la Mungu kwa usahihi, kwa hiyo tafasiri ya maandiko ni
sayansi na sio swala la kukurupuka tu!
Sasa baada ya kujenga msingi huo
wa ufahamu nataka twende moja kwa moja tukaaangalie sasa tafasiri ya kimaandiko
kuhusu “Tafasiri halisi ya Maana ya
kuchovya mguu wako katika Mafuta!” je andiko hili lilimaanisha nini kwa
wakati wa Musa na linaweza kutafasiriwa vipi na linaweza kutendewa kazi katika
mazingira yapi? Katika wakati wetu
wa leo?
Tafasiri halisi ya Maana ya kuchovya mguu wako katika Mafuta!
Ni muhimu kwanza kufahamu kuwa
andiko la msingi linatoka katika
Kumbukumbu 33:24-25 “Na Asheri akamnena, Na
abarikiwe Asheri kwa watoto; Na akubaliwe katika nduguze, Na achovye mguu wake
katika mafuta. Makomeo yako yatakuwa ya chuma na shaba; Na kadiri ya siku zako
ndivyo zitakavyokuwa nguvu zako.”
Andiko hili kwa asili linatokana
na lugha ya kiebrania kwa sababu ndio lugha ya asili iliyotumika kuandikia
agano la kale tofauti na agano jipya ambalo kimsingi liliandikwa kwa lugha ya
kiyunani sasa basi katika lugha ya kiebrania andiko hilo linasomeka namna hii:-
Âshềr âmar âshềr bârak bền râtsâh âch ţâbal regel
shemen “24 âshềr âmar âshềr
bârak bền
râtsâh
âch ţâbal
regel shemen” kwa kiingereza ingetakiwa kusomeka Of Asher he said May Asher be most blessed of sons, may he be favorite
among his brothers and bathe his feet in oil
KJV inasomeka hivi “And
Asher he said, Let Asher be blessed with children; let him be acceptable to
brethren, and let him dip his foot in oil”
SUV inasomeka hivi “Na Asheri akamnena, Na abarikiwe Asheri kwa watoto; Na
akubaliwe katika nduguze, Na achovye mguu wake katika mafuta.”
Kwa asili andiko hili limetokana
na Musa nabii ambaye alikuwa akitamka Baraka za aina mbalimbali kwa makabila 12
ya Israel sawa tu na jinsi Yakobo baba yao alivyowatabiria watoto wake kuhusu
maswala yatakayowapata siku za mwisho kwa hiyo haya yalikuwa ni maneno ya
kinabii kutoka kwa Musa akiongezea yale
yaliyotoka kwa Yakobo ona
Mwanzo 49:1-2 “Yakobo akawaita wanawe,
akasema, Kusanyikeni, ili niwaambie yatakayowapata siku za mwisho. Kusanyikeni,
msikie, enyi wana wa Yakobo, Msikilizeni Israeli, baba yenu.”
Mwanzo 49:20 “Asheri, chakula chake
kitakuwa kinono, Naye atatoa tunu za kifalme.” Kimsingi Musa alikuwa
akijazilizia Baraka zilizokuwa zimetamkwa na Baba yao Israel kwa kabisa zote 12
za wana wa Israel lakini linapokuja swala la kabila la Asheri inaonekana wazi
kuwa Musa pamoja na Yakobo walikuwa wanalizungumzia kabila hili kama kabila ambalo
Bwana angelibariki sana kwa hiyo maneno “Thy feet in the oil or and let him dip
his foot in Oil” au kwa Kiswahili “Na achovye mguu wake katika mafuta” yana maana
ya kinabii inayoashiria kuwa kabila la Asheri katika Israel ni kabila ambayo
imetamkiwa kutembea katika utajiri mkubwa sana kwa chakula na tunu au madini hiyo lugha inayotumika hapo ni lugha ya
kinabii au pia inaweza kuitwa (figurative
language) au figurative expression,
yaani lugha ya mficho au lugha ya kimafumbo inayoashiria kuwa Asheri litakuwa
ni kabila litakalokanyaga mafanikio makubwa sana, Asheri watakuwa una utajiri
mkubwa wa mafuta ya mzeituni.
Nyakati za agano la kale mtu
aliyekuwa anamiliki mafuta hasa yaliyotokana na mzeituni, alikuwa ni mtu ambaye
anaweza kutengeneza fedha nyingi sana na kuwa vizuri kiuchumi, kwa nyakati
zile, kwa hiyo lugha kubwa ya mafanikio na utajiri pia ililinganishwa na wingi
wa mafuta ya mizeituni ambao mtu aliweza kuwa nao kama mtu angekuwa na mafuta
ya kutosha angeweza kuyamudu maisha yake na kuondokana kabisa na madeni au
kupoteza mali na rasilimali alizokuwa nazo, kuchovya mguu katika mafuta
kulimaanisha ni kuwa juu ya Baraka zilizopitiliza, kabila la Asheri
wanabarikiwa kuwa kabila lenye mafanikio na utajiri unaomwagika, pia mbaraka
huu uliashiria kuwa mipaka ya kabila la Asheri itakuwa ni mipaka inayozingirwa
na utajiri wa ardhi yenye rutuba na yenye kustawi mizeituni kwa wingi jambo
ambalo litawapa utajiri wa mafuta. Kwa hiyo kuchovya mguu wake katika mafuta
kunamaanisha kutembea katika mafanikio na maisha ya starehe, mafuta yalikuwa ni
ishaya ya mafanikio makubwa nyakati za zamani kwa ichi za mashariki ya kati,
ukibarikiwa kuwa uchovye mguu wako katika mafuta maana yake Mungu akufanikishe
kwa njia rahisi na isiyo ya taabu.
2Wafalme 4:1-7 “Basi, mwanamke mmoja
miongoni mwa wake za wana wa manabii alimlilia Elisha, akasema, Mtumishi wako
mume wangu amekufa; nawe unajua ya kuwa mtumishi wako alikuwa mcha Bwana; na
aliyemwia amekuja ili ajitwalie wana wangu wawili kuwa watumwa. Elisha akamwambia,
Nikufanyie nini? Niambie; una kitu gani nyumbani? Akasema, Mimi mjakazi wako
sina kitu nyumbani, ila chupa ya mafuta. Akasema, Nenda, ukatake vyombo huko
nje kwa jirani zako wote, vyombo vitupu; wala usitake vichache. Kisha uingie
ndani, ukajifungie mlango wewe na wanao, ukavimiminie mafuta vyombo vile vyote;
navyo vilivyojaa ukavitenge. Basi akamwacha, akajifungia mlango yeye na wanawe;
hao wakamletea vile vyombo, na yeye akamimina.Ikawa, vilipokwisha kujaa vile
vyombo, akamwambia mwanawe, Niletee tena chombo. Akamwambia, Hakuna tena
chombo. Mafuta yakakoma.Ndipo akaja akamwambia yule mtu wa Mungu. Naye akasema,
Enenda ukayauze mafuta haya, uilipe deni yako; nayo yaliyosalia uyatumie wewe
na watoto wako.”
Mtu alipokuwa amebarikiwa sana
nyakati za agano la kale mafanikio yalionekana ni kama kukanyaga siagi au
kumiminiwa mito ya mafuta, wakati huo ulikuwa unaitwa wakati wa ustawi mkubwa
sana mfano Ayubu alipokuwa amebarikiwa sana kabla ya mapito yake alizikumbuka
nyakati zake za Baraka kubwa na kuzitaja kama nyakati za kukanyaga siagi au
kuoshwa hatua zako kwa siagi ona
Ayubu 29:4-6 “Kama nilivyokuwa katika siku
zangu za kukomaa, Hapo siri ya Mungu ilipokuwa hemani mwangu; Wakati Mwenyezi
alipokuwa akali pamoja nami, Nao watoto wangu walipokuwa wakinizunguka; Wakati
hatua zangu zilipokuwa zikioshwa kwa siagi, Nalo jabali liliponimiminia mito ya
mafuta!”
Kwa hiyo katika andiko la msingi
ni muhimu kila mwanafunzi wa maandiko akawa na uelewa kuwa hakuna mahali
maaandiko yameagiza au kutoa amri au agizo la kukanyaga mafuta, andiko hili ni
sehemu kamili ya maneno ya Baraka ya Musa kwa kabila kadhaa za Israel kabla ya
kufa kwake, Musa alikuwa akifanya hivyo kama kiongozi wa kiroho kama ilivyokuwa
kwa Israel au Yakobo ambaye ilipofika saa yake ya mwisho pia aliwaita watoto
wake na kuwatamkia Baraka kwa hiyo
maneno na “Na achovye mguu wake katika mafuta”
yana uhusiano na Baraka ya moja kwa
moja kwa kabila la Asheri na ni lugha ya
kinabii inayohusiana na mafanikio yao utajiri mkubwa ambao Mungu amewapa Kabila
la Asheri, kabila hili lilibarikiwa sana kimwili, na kiroho na kwa maelezo ya
marabi wa kiyahudi ni kuwa kabila hili pia lilikuwa na wanawake wazuri na
waliokuwa na adabu na wala hawana maringo, kabila hili lilibarikiwa kwa
utajiri, mafanikio na ongezeko kubwa lakini pia walibarikiwa kama watu ambao
hawapigiki kirahisi vitani na watakuwa
na ulinzi wa uhakika “Makomeo yako yatakuwa ya chuma na shaba“ Asheri litakuwa ni kabila la watu wenye
mafanikio makubwa sana na wingi wa mafuta unaashiria utajiri mkubwa sana wa
Ardhi yenye kuzalisha mizeituni kwa wingi bna ambay ingewabeba kiuchumi.
Mafuta ya mzeituni nyakati za Biblia
ilikuwa ni bidhaa adimu na ya thamani sana, mafuta yalitumika kwa kupikia,
kuwashia taa, kutibu, kujipaka na kwa sababu mbali mbali kwa hiyo kabila hili
kuwabarikiwa kiasi cha kukanyaga mafuta kulimaanisha wingi wa utajiri wa bidhaa
hii adimu waliyokuwa nayo, kukanyaga mafuta au zabibu pia kulikuwa na maana ya
kuendesha mtambo wa kukamulia Mafuta au zabibu kwaajili ya mvinyo, Mashine ya
kutengenezea Zabibu au Mafuta ya mzeituni ilitengenezwa kwa mawe makubwa mawili
ambapo jiwe moja kubwa lilikaa chini na jiwe moya lilikuwa juu na lile la juu
lingesukumwa ili kusaga zaituni zilizovunwa na kuoshwa vizuri kisha zilikamuliwa
katika mashinde (Shinikizo) na hivyo kuendesha mashine ya kukamua mafuta au
Zabibu kwaajli ya juisi ya zabibu pia kuliitwa kukanyaka shinikizo
Isaya 63:1-2. “Ni nani huyu atokaye Edomu,
Mwenye mavazi ya kutiwa damu kutoka Bosra? Huyu aliye na nguo za fahari,
Anayekwenda katika ukuu wa uweza wake? Kwani mavazi yako kuwa mekundu, Na nguo
zako kama za mtu akanyagaye zabibu? Nalikanyaga shinikizoni peke yangu; Wala
katika watu hakuwapo mtu pamoja nami; Naam, naliwakanyaga kwa hasira yangu,
Naliwaponda kwa ghadhabu yangu; Na mavazi yangu yametiwa madoa kwa damu yao,
Nami nimezichafua nguo zangu zote.”
Unaona kukanyaga Zabibu hapo
maana yake ni kusaga zabibu kwaajili ya kupata juisi ya zabibu, na kukanyaga
mafuta ya zeituni ni kukanyaga shinikio (Mashine za kizamani) za kukamulia
mafuta ua mizabizu, kwa hiyi utaweza kuona kama Mungu alikuwa anamaaisha
kuchovya mguu katika mafuta ni tukio halisi basi kukanyaka Zabibu nalo
lingekuwa ni tukio halisi unaelewa?
Kwa hiyo Kabila la Asheri
linatamkiwa na Musa kuwa kabila lenye wingi wa mafanikio na utajijiri wa mafuta
ya zeituni na watu wasiopigika kirahisi, kabila la Asehri walikuwa na sifa
njema sana nyakati za biblia kimwili na kiroho maana walitabiriwa kukubalika
pia na kupata kibali kwa ndugu zao wakati Yesu alipokuwa anazaliwa mwanamke
mmoja mcha Mungu aliyekuwa wa kiroho sana mwenye umri mkubwa sana na tabia
njema na uvumilivu alijitokeza pia kutoa unabii kumuhusu Yesu Kristo mwanamke
huyu maarufu alitokea kabila la Asheri ona
Luka 2:36-38 “Palikuwa na nabii mke, jina
lake Ana, binti Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa miaka mingi,
alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake. Naye ni mjane wa
miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana
kwa kufunga na kuomba. Huyu alitokea saa ile ile akamshukuru Mungu, na wote
waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea habari zake.”
Kwa sababu hiyo ni muhimu
wakristo wakawa na uelewa kuwa hakuna agizo la kibiblia la aina yoyote lile linaloamuru
wanadamu wakanyage mafuta, hii ilikuwa ni lugha ya kinabii ya kumtakia mtu
mafanikio hata kama utakuwa ulikanyaga mafuta mahali na ukaona mafanikio fulani
kumbuka tu kuwa Mungu aliweza kukuhurumia tena alikuhurumia kwa sababu ya
ujinga wako na kwa kufilisika kwako kimawazo na kwa tafasiri mbovu za kibiblia,
na kwa sababu ya jina lake ambalo lilitajwa huko lakini, andiko hilo halina
uhusiano wowote na kukanyaga mafuta kunakofanywa na watumishi kadhaa leo. Maandiko hayajakakataza mtu kupakwa mafuta
miguuni baada ya kunawa au kuoga, lakini hilo sio agizo la kibiblia kwamba
tukanyage mafuta, Nayaweka haya hadharani kwa sababu nimeagizwa kuihubiri
kweli, nimeagizwa kuwafungua watu akili ili watoke gizani na kumgeukia Yesu
Kristo mzima mzima sawa sawa na mapenzi yake nimeagizwa kuweka kweli ya Mungu
kwa uwazi kwa kusudu la kuleta uelewa ulio wazi ili watu waifahamu kweli na
kweli iwaweke huru maandiko yanaonyesha wazi kuwa wakati wa Yoshua alipopiga
kura ya kugawa ardhi watu wa kabila la Asheri walipata inchi yenye utajiri
mkubwa wa madini pamoja na ustawi wa miti ya mizeituni na chakula cha kutosha,
kwa hiyo unabii kuhusu kubarikiwa kwa kabila hilo la Asheri ulitimizwa!
Yoshua 19:24-31 “Kisha kura ya tano
ilitokea kwa ajili ya kabila ya wana wa Asheri kwa kuandama jamaa zao. Na mpaka
wao ulikuwa ni Helkathi, na Hali, na Beteni, na Akishafu; na Alameleki, na
Amadi, na Mishali; nao ukafikilia hata Karmeli upande wa magharibi, tena
ulifikilia hata Shihor-libnathi; kisha ukazunguka kuelekea maawio ya jua mpaka
Beth-dagoni, nao ukafikilia hata Zabuloni, tena mpaka bonde la Iftaeli upande
wa kaskazini hata Bethemeki na Neyeli; kisha ukatokea hata Kabuli upande wa
kushoto; na Ebroni, na Rehobu, na Hamoni, na Kana, hata kufikilia Sidoni mkuu; kisha
mpaka ulizunguka kuelekea Rama, na mji wa Tiro ulio na boma; kisha mpaka
ulizunguka kuelekea Hosa; na matokeo yake yalikuwa baharini katika nchi ya
Akzibu; na Uma pia, na Afeka, na Rehobu; miji ishirini na miwili, pamoja na
vijiji vyake.Huu ndio urithi wa kabila ya wana wa Asheri kwa kuandama jamaa
zao; miji hii pamoja na vijiji vyake.”
Tafasiri ya Kabila la Asheri
kuchovya mguu wao katika mafuta inaweza kutafasiriwa leo kama kutembea katika
Baraka za Mungu, kubarikiwa na kupata kibali kiroho, kiuchumi na wingi wa mafanikio,
kufurahia neema ya Mungu na kuwa na mapito yasiyo na taabu na masumbufu, lakini
kamwe andiko hilo haliwezi kutafasiriwa kama lisemavyo moja kwa moja kwa
kufanya hivyo ni kufanya mambo ya kijinga kwani mnakanyaga chakula, kukanyaga
chakula kunaleta laana kubwa sana kwa
hiyo Mwandishi au Musa hakuagiza watu wakanyage chakula au wakanyage mafuta
mwandishi hajawahi kukusudia hivyo! Msipoelewa maneno ya Mungu mtakanyagishwa
mpaka ugali, Bwana ampe neema kila mmoja kutembea katika Baraka za Mungu kama
kabila ya Asheri katika jina la Yesu Kristo amen!
Jamani swala la kuchovya mguu
katika mafuta tafasiri yake sio kukanyaka mafuta halisi, hii ni lugha ya
kimafumbo yenye maana kuwa kabila la Asheri watafanikiwa sana kwa utajiri
mwingi utakaopatikana kwao naomba ieleweke kwa njia hiyo!
Naomba niseme kwa kiingereza hapa
labda nitaeleweka pia
My brothers and Sisters the
phrase is not a literal instruction to dip feet in oil, but rather a metaphor
for the tribe of Asher’s Prosperity and abundance of resouces available to them
I beg to be understood in that way!
Jinsi ya kuchovya mguu wako katika Mafuta!
Kuchovya mguu wako katika mafuta
maana yake ni kutembea katika Baraka za Mungu, matokeo ya kutembea katika
Baraka za Mungu sio tukio linalokuja kama kufumba na kufumbua bali ni mchakato
unaotokana na mtindo wa maisha ya kila siku, unaoendana na utii kwa Mungu.
Badala ya kuwakanyagisha watu chakula watumishi wa Mungu wawafundishe watu
jinsi ya kutembea katika Baraka za Mungu na kutembea katika Baraka za Mungu
kuna kanuni zake.
Wakati Musa au Yakobo anawabariki
kabla la Asheri kumbuka kuwa alikuwa amewasoma mtindo wao wa maisha tabia na
mwenendo wao kwa Bwana, Imani yao, ushirika wao na kujitoa kwao katika maisha
ya kila siku na safari ya kila siku ya maisha yao kwa hiyo Yakobo alipofikia
mwisho aliwatabiria Asheri na Musa naye alipokuwa anafikia mwisho aliwatabiria
Asheri Baraka nyingi sana kwa hiyo mtu awaye yote anayetaka Baraka za Mungu
atapaswa kukanyaga katika kanuni za Mungu kwa kufanya yafuatayo katika maisha yake
ya siku zote:-
1.
Ishi
maisha ya utii kwa neno la Mungu – Baraka za Mungu huja kwetu pale
tunapotii, huenda Musa alikuwa amewaangalia sana wana wa Asheri na kubaini kuwa
walikuwa watii katika sheria za Mungu na sheria ya Mungu ilikuwa na ahadi
kwamba kama mtu ataisikiliza sauti ya Bwana Mungu wake na kuyatunza maagizo
yake basi Mungu angeamuru Baraka zije juu ya mtu huyu au kabila hiyo, utii wetu
kwa Mungu katika mambo yote hata madogo madogo utawapelekea watu kufurahia
matunda ya utii huo.
Kumbukumbu 28:1-2 “Itakuwa
utakaposikia sauti ya Bwana, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo
yake yote nikuagizayo leo, ndipo Bwana, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya
mataifa yote ya duniani; na baraka hizi zote zitakujilia na kukupata usikiapo
sauti ya Bwana, Mungu wako.”
Isaya 1:19-20 “Kama
mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi; bali kama mkikataa na kuasi
mtaangamizwa kwa upanga; maana kinywa cha Bwana kimenena haya.”
2.
Ishi
maisha ya Imani – Mwamini na
kumtegemea Mungu, hakuna namna iwayo yote mtu anaweza kuishi kwa imani bila
kutii na kutegemea, tunaelezwa kuwa Mungu alimuahidi Ibrahimu Baraka lakini ili
Baraka hizo ziweze kumjilia Ibrahimu yeye alimuamini Mungu na kutii na
ikahesabiwa kwake kuna na haki, hakuna namna yoyote ile ambayo tunaweza
kumpendeza Mungu pasipo Imani
Mwanzo 12:1-4 “BWANA
akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba
yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha; nami nitakufanya wewe kuwa taifa
kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka; nami nitawabariki
wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia
watabarikiwa. Basi Abramu akaenda, kama BWANA alivyomwamuru; Lutu akaenda
pamoja naye. Naye Abramu alikuwa mtu wa miaka sabini na mitano alipotoka Harani.”
Waebrania 11:6 “Lakini
pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima
aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.”
Yeremia 17:5-8 “Bwana
asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa
kinga yake Na moyoni mwake amemwacha Bwana. Maana atakuwa kama fukara nyikani,
Hataona yatakapotokea mema; Bali atakaa jangwani palipo ukame, Katika nchi ya
chumvi isiyokaliwa na watu. Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana, Ambaye
Bwana ni Tumaini Lake. Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji, Uenezao
mizizi yake karibu na mto; Hautaona hofu wakati wa hari ujapo, Bali jani lake
litakuwa bichi; Wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, Wala hautaacha
kuzaa matunda.”
3.
Ishi
maisha ya utoaji – hakikisha kuwa unatoa kwa ukarimu na sio kwa sheria
maandiko yanaonyesha kuwa Mungu huwabariki watu wake wote wanaotoa kwa moyo wa
upendo na kwa ukarimu unapokuwa na moyo wa kuwasaidia wengine Mungu huamuru
Baraka zake zikujie.
Matendo 20:34-35 “Ninyi
wenyewe mnajua ya kuwa mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale
waliokuwa pamoja nami. Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi
hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi
alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea.”
Luka 6:38 “Wapeni
watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa
hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile
kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa.”
Hitimisho:
Kutembea katika Baraka za Mungu
ni matokeo ya maisha endelevu yenye kudumisha uhusiano wako na Mungu, kumpenda
Mungu kwa moyo wako wote, kumtii na kumtumikia huku ukiendelea kumuamini, Mungu
sio mchoyo kwani yeye amekusudia kumbariki kila mtu na yuko tayari kumimina
Baraka zake katika maisha yako ili hatimaye wewe nawe uchovye mguu wako katika
mafuta yaani utembee katika Baraka za Mungu, wakristo ni lazima wakumbuke kuwa
hakuna njia ya mkato, lakini iko njia ya mchakato, usikubali kudanganywa hata
kama watu wanayatumia maandiko, kama kukanyaka mafuta ingekuwa ni njia halisi
ya kibiblia ya kufunguliwa na kupata Baraka za Mungu wengi tungekanyaga mafuta
hayo, lakini je tangu umenza kukanyaga mafuta halisi kuna badiliko lolote la
kiroho, kiafya au kiuchumi? Watumishi wa Mungu tuamke na kutembea katika nuru
kwani saa ya kutoka gizani imekwisha kuwadia asomaye na afahamu!, iwapo
kukanyaga mafuta lingekuwa agizo halisi la kimaandiko, mitume wa Bwana
wangefanya hivyo, na Yesu angeagiza hivyo, na ingekuwa rahisi tu tungekanyaga
mafuta na kupata mafanikio lakini hakuna njia ya mkato kwa Mungu kanyaga njia
halisi za mapenzi yake na utafanikiwa, kama bado hujamwamini Yesu tafuta kwanza
ufaome wake na haki yake na mengine yote mtazidishiwa jiulize je ni wapi Yesu ameagiza katika agano jipya?
Tuchovye mguu katika mafuta? Je Yesu
alipowaosha wanafunzi wake miguu alikuwa akimaanisha na sisi tuoshane miguu? La
hasha alikuwa akijibu swali la wanafunzi wake ni yupi aliye mkubwa na akajibu
kwa vitendo ni yule atumikaye au anayewahudumia wengine, hebu tulitendee haki
neno la Mungu na tusikubali kudanganyika kila tunachofundishwa duniani tuhoji
na tujiulize kikoje katika maandiko na je ndivyo kilivyo? Imekuwaje wakristo wa
kipindi hiki ambao ni wasomi na maarifa nyameongezeka wanadanganyika kwa njia
rahisi? Do you think that to think critical is sin? Je unafikiri kwamba
kufikiri kwa kuhoji au kujiuliza ni dhambi? Amka kuanzia sasa na jaribu kila
fundisho au roho uone kama ndivyo ilivyo, Mafundisho huwa yana roho nyuma yake
Yohana 6:63 “Roho ndiyo itiayo uzima, mwili
haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima.”
1Yohana 4:1-4 “Wapenzi, msiiamini kila
roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii
wa uongo wengi wametokea duniani. Katika hili mwamjua Roho wa Mungu; kila roho
ikiriyo kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili yatokana na Mungu. Na kila roho
isiyomkiri Yesu haitokani na Mungu. Na hii ndiyo roho ya mpinga Kristo ambayo
mmesikia kwamba yaja; na sasa imekwisha kuwako duniani. Ninyi, watoto wadogo,
mwatokana na Mungu nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu
kuliko yeye aliye katika dunia.”
Na. Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!
Maoni 1 :
Ameen Pastor Asante kwa Kutufungua akili...! Mungu akubariki
Chapisha Maoni