Ijumaa, 2 Mei 2025

Nafasi ya wafanya kazi wa ndani katika nyumba za wachungaji!


2Wafalme 5:1-5 “Basi Naamani, jemadari wa jeshi la mfalme wa Shamu, alikuwa mtu mkubwa mbele ya bwana wake, na mwenye kuheshimiwa, kwa sababu kwa mkono wake Bwana alikuwa amewapa Washami kushinda; tena alikuwa mtu hodari wa vita; lakini alikuwa mwenye ukoma. Na Washami walikuwa wametoka vikosi, wakachukua mfungwa mmoja kijana mwanamke kutoka nchi ya Israeli; naye akamhudumia mkewe Naamani. Akamwambia bibi yake, Laiti bwana wangu angekuwa pamoja na yule nabii aliyeko Samaria! Maana angemponya ukoma wake.” 



  

Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kwamba mojawapo ya nafasi ya Muhimu sana katika utumishi wa Mungu ni pamoja na kupata nafasi ya kuwa mfanyakazi wa ndani katika nyumba ya Mchungaji au mtumishi awaye yote wa Mungu, hii ni nafasi ya kipekee sio tu ya kupata neema ya kuwahudumia watumishi wa Mungu lakini pia ya kupitia kujifunza kwa namna ya kipekee na kushuhudia maisha ya utumishi wa watu wa Mungu na kujiletea baraka  na heshima kutoka kwa Mungu, hii ni kwa sababu neno la Mungu limesema yeye amuhudumiaye nabii kwa kuwa ni nabii atapata thawabu ya nabii.


Mathayo 10:40-42 “Awapokeaye ninyi, anipokea mimi; naye anipokeaye mimi, ampokea yeye aliyenituma. Ampokeaye nabii kwa kuwa ni nabii, atapata thawabu ya nabii; naye ampokeaye mwenye haki kwa kuwa ni mwenye haki, atapata thawabu ya mwenye haki. Na mtu awaye yote atakayemnywesha mmojawapo wa wadogo hawa ngaa kikombe cha maji ya baridi, kwa kuwa ni mwanafunzi, amin, nawaambia, haitampotea kamwe thawabu yake.”


Wafanyakazi wa ndani katika nyumba za watumishi wa Mungu wanahitaji maelekezo maalumu ili waweze kutambua wajibu wao na baraka ambazo Mungu amezikusudia kwao, wasipoelekezwa vema wanaweza kutumika kinyume na mapenzi ya Mungu na kusababisha changamoto kubwa za kihuduma kwa mtu wa Mungu na hata na kanisa lake kwa ujumla na huduma ya Mchungaji na mama Mchungaji, Ni lazima watumishi wa ndani katika nyumba za wachungaji watambue kuwa kazi yao ni huduma kamili na ni ibada kamili mbele za Mungu na kwa sababu hiyo wanapaswa kuifanya kwa moyo na ni nafasi ya kipekee sana na kwa sababu hiyo hawapaswi kuichukulia kama nafasi isiyo ya heshima, wao wanaweza kuyatumia mazingira ya kiroho yapatikanayo katika nyumba ya mtumishi wa Mungu kama njia ya Baraka kubwa katika maisha yao.


Kwa msingi huo leo tutachukua Muda kujifunza maswala ya msingi ambayo wafanyakazi wa ndani katika nyumba za watumishi wa Mungu wanaweza kuyaishi ili waweze kuwa Baraka katika mwili wa Kristo na kwa kanisa la Mungu bila kusababisha madhara katika nyumba za watumishi wa Mungu na huduma walizoaminiwa na Mungu katika maisha yao. Huduma ya kichungaji inapaswa kulindwa na kwa sababu hiyi mtenda kazi wa ndani ni moja ya walinzi wa huduma ya kichungaji, ni walinzi wa madhabahu iliyo hai yaani moyo na maisha ya Mchungaji.

1.       Watumishi wa ndani katika nyumba ya mchungaji ni watenda kazi pamoja na mtumishi wa Mungu.

 

Inapotokea kuwa kwa njia yoyote ile umepata nafasi ya kuishi katika nyumba ya Mchungaji au nabii, Mtume na kadhalika kwaajili ya kazi za ndani ni lazima utambue kuwa wewe ni mtumishi wa Mungu katika nafasi uliyo nayo, kwa sababu umepata neema ya kumtumikia Mungu pamoja na mtumishi wake na familia yake, na kwa sababu hiyo kazi yako sio kazi ya kawaida bali ni ibada mbele za Mungu na Mungu atakubariki endapo utaifanya kazi hiyo kwa uaminifu na uchaji wa Mungu, kwa hiyo fanya kazi hiyo kama sehemu ya utumishi wako kwa Mungu na kamwe acha kujifikiri kuwa u mtumwa au mjakazi.

 

Wakolosai 3:23-24 “Ninyi watumwa, watiini hao ambao kwa mwili ni bwana zenu, katika mambo yote, si kwa utumwa wa macho, kama wajipendekezao kwa wanadamu, bali kwa unyofu wa moyo, mkimcha Bwana. Lo lote mfanyalo, lifanyeni kwa moyo, kama kwa Bwana, wala si kwa wanadamu,mkijua ya kuwa mtapokea kwa Bwana ujira wa urithi. Mnamtumikia Bwana Kristo.”    

 

Nimeishi na wasichana wa kazi wengi katika maisha yangu na wengi wa wale waliokaa na mimi vizuri Mungu aliwabariki na waliolewa na sasa wana nyumba zao na wanaishi maisha mazuri na yenye utulivu, nay a kuvutia sana, vijana  wengi waliamini kuwa mambinti hao wako salama  na wote waliooa kutoka katika nyumba za wachungaji hawakuwahi kujutia hii ni moja ya Baraka kubwa, wakati mwingine kutokana na kuishi katika utumishi wa Mtumishi wa Mungu, Mungu amewafanya wafanyakazi katika nyumba za watu wa Mungu kuja kuwa na huduma ya kitumishi vile vile na wengi wameinuliwa kutoka kuwa watumishi wa ndani na hata kuwa mama wachungaji, mama maaskofu na kadhalika  

 

Roho ya utumishi wa Mungu imewahi kuwakalia wale waliokuwa watumishi wa watumishi wa Mungu, hii ni kwa sababu watumishi wa waliokuwa watumishi wa Mungu wanajua mapito na mateso yote ambayo Bwana zao waliyapitia kwa hiyo haishangazi kuona Mungu akijitwalia viongozi kutoka wale waliokuwa wakifanya kazi kama za utumwa tu, kimsingi wakati mwingine huwezi kuwa mtumishi wa Mungu kabla ya kuwa mtumishi wa mwanadamu.

 

Kutoka 3:1-4 “Basi huyo Musa alikuwa akilichunga kundi la Yethro mkwewe, kuhani wa Midiani; akaliongoza kundi nyuma ya jangwa, akafika mpaka mlima wa Mungu, hata Horebu. Malaika wa BWANA akamtokea, katika mwali wa moto uliotoka katikati ya kijiti; akatazama, na kumbe! Kile kijiti kiliwaka moto, nacho kijiti hakikuteketea. Musa akasema, Nitageuka sasa, niyaone maono haya makubwa, na sababu kijiti hiki hakiteketei. BWANA alipoona ya kuwa amegeuka ili atazame, Mungu akamwita kutoka katikati ya kile kijiti, akasema, Musa! Musa! Akasema, Mimi hapa.”  

 

Hesabu 11:28-29 “Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Musa tangu ujana wake, akajibu akasema, Ee bwana wangu Musa, uwakataze. Musa akamwambia, Je! Umekuwa na wivu kwa ajili yangu; ingekuwa heri kama watu wote wa Bwana wangekuwa manabii na kama Bwana angewatia roho yake.”

 

Yoshua 1:1-3 “Ikawa baada ya kufa kwake Musa, mtumishi wa Bwana, Bwana akamwambia Yoshua, mwana wa Nuni, mtumishi wa Musa, akasema, Musa mtumishi wangu amekufa; haya basi, ondoka, vuka mto huu wa Yordani; wewe na watu hawa wote, mkaende hata nchi niwapayo wana wa Israeli.Kila mahali zitakapopakanyaga nyayo za miguu yenu, nimewapa ninyi, kama nilivyomwapia Musa.”

 

Ni jambo la kushangaza kuwa Musa alikuwa akifanya kazi ya kulichunga kund la Yethro mkwewe ambaye alikuwa kuhani wa Midian, Lakini Mungu alimuita Musa akiwa katika hali ya kumtumikia mkwewe na kufanya kazi hiyo ambayo kimtazamo ilionekana ni kama kazi ya chini sana, Yoshua alikuwa mtumishi wa Musa na baadaye Musa alipokufa Yoshua ndiye aliyekuwa kiongozi mkubwa aliyewaingiza Israel katika inchi ya mkanaani  hii inaweza isiwe kanuni lakini inatufunza Mungu anajali utumishi wako dhidi ya watumishi wake.               

 

2.       Watumishi wa ndani katika nyumba ya mchungaji ni lazima wajifunze kuwaheshimu wachungaji na familia zao.

 

Kila anayefanya kazi katiia nyumba ya mtumishi wa Mungu ni lazima awe na uelewa kuwa watumishi hao wa Mungu wanahitaji kuheshimiwa sana wao pamoja na familia zao, Mchungaji au nabii au mtume ni mtu aliyeitwa na Mungu na ni mtu anayestahili heshima yeye pamoja  na mkewe pia na watoto wao, kwa sababu hiyo kila anayefanya kazi ndani ya nyumba za watumishi wa Mungu anapaswa kujiheshimu, ni marufuku kuutumia udhaifu wa mke wa Mchungaji kama nafasi ya kutaka kumvunjia Heshima mama Mchungaji na au mchungaji, Moja ya mgogoro mkubwa uliompata Sara na Hajiri hata kufikia ngazi ya kuanza kutesana ni pamoja na Hajiri kuanza kumdharau Bibi yake.

 

Mwanzo 16:6-9 “Naye Abramu akamwambia Sarai, Tazama, mjakazi wako yu mkononi mwako, mtendee lililo jema machoni pako. Sarai akamtesa, naye akakimbia kutoka mbele yake. Malaika wa BWANA akamwona kwenye chemchemi ya maji katika jangwa, chemchemi iliyoko katika njia ya kuendea Shuri. Akamwambia, Hajiri, wewe mjakazi wa Sarai, unatoka wapi, nawe unakwenda wapi? Akanena, Nakimbia mimi kutoka mbele ya bibi yangu Sarai. Malaika wa BWANA akamwambia, Rudi kwa bibi yako, ukanyenyekee chini ya mikono yake.”

 

Wafanyakazi wa ndani watapaswa kuishi na mke wa mchungaji vizuri na kujiepusha na migogoro isiyo na msingi, aidha wao ni waajiriwa wa mwanamke na kamwe halitakuwa jambo lenye kupendeza Mchungaji kujihusisha na malipo ya mshahara wa mfanyakazi, wafanyakazi wa ndani wanapaswa kuheshimu mamlaka ya kiroho ya kichungaji sawa tu na ilivyo Kanisani na nyumbani pia.

 

1Timotheo 5:17 “Wazee watawalao vema na wahesabiwe kustahili heshima maradufu; hasa wao wajitaabishao kwa kuhutubu na kufundisha.”

 

Aidha kila msichana wa kazi katika nyumba ya mtumishi wa Mungu anapaswa kuwa kielelezo kwa kuishi maisha matakatifu na yaliyo kielelezo kwani watu wanaitazamia nyumba ya mchungaji kuwa kielelezo, wako mambinti wengi katika nyumba za watumishi wa Mungu ambao wametia aibu kwa kuishi maisha yasiyokuwa na kielelezo na kwa sababu hiyo kusababisha maswali yasiyoyokuwa na majibu, wengine walipata ujauzito na wakarudhishwa makwao huku washirika wakibaki na maswali kwamba waliwezaje kufanya matukio ya aina hiyo ili hali wanaishi katika nyumba za watu wa Mungu, huku ni kufanya uchafuzi wa kimazingira na kuleta shaka juu ya usimamizi wa huduma ya kichungaji kwani Mchungaji na mama Mchungaji wana wajibu wa kuisimamia nyumba ya Mchungaji ili iwe kielelezo kwa waamini.

 

1Timotheo 3:4-5 “mwenye kuisimamia nyumba yake vema, ajuaye kutiisha watoto katika ustahivu; (yaani, mtu asiyejua kuisimamia nyumba yake mwenyewe, atalitunzaje Kanisa la Mungu?)

 

3.       Watumishi wa ndani katika nyumba ya mchungaji ni lazima wawe kielelezo katika Uadilifu, Nidhamu na kutunza siri za nyumbani

 

Ukiacha kuwa ni jukumu la kila mfanyakazi wa ndani katika nyumba ya Mchungaji kuishi maisha yaliyo kielelezo na ya uadilifu na nidhamu, pia kila msichana wa kazi katika nyumba za watumishi wa Mungu anapaswa kuwa mstari wa mbele katika kutunza siri za changamoto zinazojitokeza katika nyumba ya mtumishi wa Mungu, Nyumbani Mchungaji ni Baba, ni Mume  na ni kiongozi wa familia, lakini sio hivyo tu Nyumba ya mchungaji ina mapito mengi, wanaweza kulala na njaa, kufunga, kula vibaya yaani chakula kisicho na hadhi, kupungukiwa na kadhalika pia Mchungaji anao ndugu na jamaa ambao wanaweza kuwa hawajaokoka, hivyo watendakazi nyumbani kwa mchungaji hupita mapito hayo pamoja na familia ya Mchungaji na kwa sababu hiyo wakati mwingine usiri unahitajika kuhusiana na mapito hayo, Ni lazima mfanyakazi wa ndani katika nyumba ya mchungaji awe mwaminifu kwa kila linaloendelea nyumbani, hupaswi kulianika nje? Usieneze siri ya matatizo au mapito ya ndani ya nyumba ya mchungaji, hakikisha kuwa washirika wengine hawatengenezi nafasi ya udadisi ya kutaka kujua yanayoendelea katika nyumba ya mchungaji wewe endelea kuwa mwaminifu na kufanya kazi kwa heshima, usafi na kwa moyo acha kueneza fitina hususani kati ya nyumba ya mchungaji na washirika wake, waache waguswe wenyewe kuihudumia nyumba ya Mchungaji na usiwaeleze watu kabisa hata kama mmeshinda na njaa. Aidha kama kuna jambo watu wanajaribu kulidadisi kuhusu Mchungaji au mama Mchungaji waelekeze watu kuwaona wasemaji wa familia ya Mchungaji na wewe baki kama mtu usiyejua kinachoendelea!

 

Mithali 11:13 “Mwenye kitango akisingizia hufunua siri; Bali mwenye roho ya uaminifu husitiri mambo.”

 

Mithali 25:2 “Ni utukufu wa Mungu kuficha jambo; Bali ni utukufu wa mfalme kuchunguza jambo.”

 

Aidha ishi na watoto wa Mtumishi wa Mungu sawa na makusudi ambayo kwayo watoto hao wamezaliwa, wewe kama yaya wa watoto wa Mchungaji usijihusishe katika kuwapandikizia watoto wa Mchungaji uharibifu, lilikuwa ni jambo la kusikitisha kuwa Hajiri yeye alianza kumnyanyasa Isaka na akiwa na mwanae Ishmael walianza kutumiwa na shetani kumdhihaki Isaka na kumfanya mtoto yule wa ahadi asiyafurahie maisha nyumbani kwao jambo lililompelekea Sara kuamuru kutimuliwa kwa mjakazi na mwanae.

 

Mwanzo 21:8-12 “Mtoto akakua, akaachishwa kunyonya; Ibrahimu akafanya karamu kuu siku ile Isaka alipoachishwa kunyonya. Sara akamwona yule mwana wa Hajiri Mmisri, ambaye alimzalia Ibrahimu, anafanya dhihaka. Kwa hiyo akamwambia Ibrahimu, Mfukuze mjakazi huyu na mwanawe, maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka. Na neno hilo lilikuwa baya sana machoni pa Ibrahimu, kwa ajili ya mwanawe. Mungu akamwambia Ibrahimu, Neno hili lisiwe baya machoni pako, kwa ajili ya huyo mwana, na huyo mjakazi wako. Kila akuambialo Sara, sikiza sauti yake, kwa maana katika Isaka uzao wako utaitwa.”

 

Aidha uzembe uliowahi kufanya na yaya wa Yonathan mwana wa Sauli kwa kijana wake Methiboehseth ulisababisha ulemavu usio wa lazima kwa mtoto wa Mtumishi wa Mungu Yonathan, kwa hiyo hata yaya katika nyumba za watumishi wa Mungu anapaswa kuwa mtu mwangalifu kwa familia ya Mchungaji, watoto wke mkewe na nduguze na kuchukua tahadhari za kutokuwasababishia matatizo au changamoto watumishi wa Mungu zikiwemo changamoto za kiafya!

 

2Samuel 4:4 “Naye Yonathani, mwana wa Sauli alikuwa na mwana aliyekuwa na kilema cha miguu. Alikuwa amepata miaka mitano, habari za Sauli na Yonathani zilipofika Yezreeli, na yaya wake akamchukua akakimbia ikawa, alipokimbia kwa haraka, huyo mtoto akaanguka, akawa kilema. Na jina lake aliitwa Mefiboshethi.”       

 

4.       Watumishi wa ndani katika nyumba ya mchungaji ni lazima waishi kwa kutumia fursa za kiroho zinazopatikana katika nyumba ya mtumishi

 

Kuishi na watumishi wa Mungu kwa uzuri ubora na uaminifu kunaleta Baraka kubwa sana kutokana na utendaji wako uliotukuka wewe unaweza kufanikisha watumishi wa Mungu kuhudhuria ibada kwa wakati huku wakiwa wameshiba, kuwapikia chakula bora, kuitumia nafasi ya kufunga kwao na kuomba kukua kiroho, kuhudhuria ibada pamoja nao na kujifunza maisha ya utumishi, kwa ujumla ni Baraka kubwa sana kuwatumikia watumishi wa Mungu wale waliotumika kwa uaminifu walipata Baraka na wale walioshindwa kuwa waaminifu walipata madhara kwa sababu hiyo wewe itumie nafasi ya kuishi kwa mchungaji kwa nia njema, usikubali kuwaacha watumishi wa Mungu kwa sababu zozote zile hata wanapopitia changamoto wewe ni lazima uwe mtu wa kwanza kusimama nao

 

2Wafalme 2:9-15 “Hata ikawa, walipokwisha kuvuka, Eliya akamwambia Elisha, Omba kwangu lo lote utakalo nikutendee, kabla sijaondolewa kwako. Elisha akasema, Nakuomba, sehemu maradufu ya roho yako na iwe juu yangu. Akasema, Umeomba neno gumu; lakini, ukiniona nitakapoondolewa kwako, utalipata; la hukuniona, hulipati. Ikawa, walipokuwa wakiendelea mbele na kuongea, tazama! Kukatokea gari la moto, na farasi wa moto, likawatenga wale wawili; naye Eliya akapanda mbinguni kwa upepo wa kisulisuli. Naye Elisha akaona, akalia, Baba yangu, baba yangu, gari la Israeli na wapanda farasi wake! Asimwone tena kabisa; akashika mavazi yake mwenyewe, akayararua vipande viwili. Kisha akaliokota lile vazi la Eliya lililomwangukia, akarudi, akasimama katika ukingo wa Yordani. Akalitwaa lile vazi la Eliya lililomwangukia, akayapiga maji, akasema, Yuko wapi Bwana, Mungu wa Eliya? Naye alipoyapiga maji, yakagawanyika huku na huku, Elisha akavuka.Na hao wana wa manabii, waliokuwako Yeriko wakimkabili, walipomwona, walisema, Roho ya Eliya inakaa juu ya Elisha. Wakaja kuonana naye, wakainama kifudifudi mbele yake.”

 

Elisha alikuwa ni mtumishi binafsi wa Eliya, alitumika kwa uaminifu mpaka dakika ya mwisho, jambo hili lilimletea Baraka kubwa sana wakati wa kuagana ulipofika kwa kweli Eliya alikuwa amekusudia kumbariki Elisha na Elisha aliomba sehemu maradufu ya roho ya Eliya imkalie juu yake na kwa kweli Mungu alifanya hivyo na wote waliokuwa wakimtambua Elisha kama mtumishi wa Eliya walimuinamia mpaka nchi wakijua kuwa Roho ya Eliya inakaa juu ya Elisha

 

Wakati Elisha akiwa anafaidika na utumishi wake mambo yalikuwa kinyume kwa Gehazi ambaye aliweka maslahi yake mbele na kutokufuata maelekezo ya Bwana wake na kwa sababu hiyo aliambulia kuwa na ukoma siku zote za maisha yake

 

2Wafalme 5:20-27 “Lakini Gehazi, mtumishi wa Elisha mtu wa Mungu, akasema, Tazama, bwana wangu amemwachilia huyo Naamani Mshami, asivipokee mikononi mwake vile vitu alivyovileta; kama Bwana aishivyo, mimi nitamfuata mbio, nipokee kitu kwake. Basi Gehazi akamfuata Naamani. Naye Naamani, alipoona mtu apigaye mbio anakuja nyuma yake, alishuka garini amlaki, akasema, Je! Ni amani? Akasema, Amani. Bwana wangu amenituma, kusema, Tazama, sasa hivi wamenijia kutoka milimani mwa Efraimu vijana wawili wa wana na manabii; uwape, nakuomba, talanta ya fedha, na mavazi mawili. Naamani akasema, Uwe radhi, ukatwae talanta mbili. Akamshurutisha, akafunga talanta mbili za fedha ndani ya mifuko miwili, na mavazi mawili, akawatwika watumishi wake wawili; nao wakayachukua mbele yake. Naye alipofika kilimani, alivitwaa mikononi mwao, akaviweka nyumbani; akawaacha wale watu kuondoka, nao wakaenda zao. Lakini yeye akaingia, akasimama mbele ya bwana wake. Elisha akamwambia, Watoka wapi, Gehazi? Akanena, Mtumwa wako hakuenda mahali. Akamwambia, Je! Moyo wangu haukuenda na wewe, hapo alipogeuka yule mtu katika gari ili akulaki? Je! Huu ndio wakati wa kupokea fedha, na kupokea mavazi, na mashamba ya mizeituni, na mizabibu, na kondoo, na ng'ombe, na watumwa, na wajakazi? Basi ukoma wa Naamani utakushika wewe, na wazao wako hata milele. Naye akatoka usoni pake mwenye ukoma kama theluji.”

 

Kutokuitumia fursa ya kiroho ya kuishi na watumishi wa Mungu kunaweza kutuletea laana na wazao wetu, lakini tukiwa na akili na kujua mapenzi ya Mungu neema ya Mungu itatuinua na watumishi hao wa Mungu watatuachia Baraka kubwa sana katika maisha yetu, kama ukiitambua siri ya kuishi na watumishi wa Mungu na ukajua Baraka zinazopatikana kwa kweli utasema kama Daudi kuwa siku moja katika nyua zako ni bora kuliko siku 1000, kuitumikia nyumba ya mtumishi wa Mungu ni kuitumikia madhabahu ya Bwana

 

Zaburi 84:10 “Hakika siku moja katika nyua zako Ni bora kuliko siku elfu. Ningependa kuwa bawabu nyumbani mwa Mungu wangu, Kuliko kukaa katika hema za uovu.”

 

5.       Watumishi wa ndani katika nyumba ya mchungaji ni lazima waitumie nafasi ya kuishi kwa maombi na neno la Mungu

 

Kupata nafasi ya kuishi katika nyumba ya mtumishi wa Mungu kusikufanye wewe kubweteka na kuishi maisha ya kiburi na majivuno, badala yake lazima uitumie nafasi hiyo kwa kuishi kwa maombi huku ukiwa mtu uliyejaa neno la Mungu, lazima mtu anayeishi katika nyumba ya mchungaji awe msikilizaji na mtendaji mzuri wa neno la Mungu, huku ukiwa kielelezo cha maisha ya kiroho, kushiriki ibada na mafundisho na hata kuandika notes, watu wanaokaa kwa mchungaji hawachukuliwi kuwa watu wa kawaida kwa hiyo ni lazima uwe kielelezo.

 

Kutoka 33:11 “Naye BWANA akasema na Musa uso kwa uso, kama vile mtu asemavyo na rafiki yake. Kisha akageuka akarejea hata maragoni; bali mtumishi wake Yoshua, mwana wa Nuni, naye ni kijana, hakutoka mle hemani.”

 

Mathayo 4:4 “Naye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.”

 

6.       Watumishi wa ndani katika nyumba ya mchungaji ni lazima kuitumia nafasi ya kuishi kwa Mchungaji kama sehemu ya huduma na Upendo kwa wengine.

 

Kufanya kazi katika nyumba ya Mchungaji kunahitaji hekima, uvumilivu na upendo kwa wengine lakini zaidi sana kwa Mchungaji, wachungaji wakati  mwingine hukosa nafasi ya Mapumziko mfanyakazi katika nyumba ya Mchungaji anapaswa kuwa na hekima sio kila wakati utamwamsha mchungaji au kuwakaribisha wageni katika nyumba yake, utawahoji wageni kwa hekima na upendo iwapo wana ahadi ya kukutana na Mchungaji nyumbani kwake au ofisini, Afya ya Mchungaji ni lazima ilindwe kwa gharama yoyote, muda wake binafsi na Mungu, muda wake wa kujiandaa kwaajili ya neno la Mungu, utulivu wake kula kwake na mapumziko yake kwa hiyo ni wajibu wa mfanyakazi katika nyumba ya Mchungaji ni kusimamamia ratiba za mtumishi wa Mungu badala ya kumwamsha kila anapokuja mtu yoyote na hata matapeli tu kwa hiyo tunaaswa kuwa na huduma na moyo wa upendo lakini tukiyanusuru na kuyalinda maisha ya mtumishi wa Mungu yasiiingiliwe kama mtu atakavyo

 

Wagalatia 5:13-14 “Maana ninyi, ndugu, mliitwa mpate uhuru; lakini uhuru wenu usiwe sababu ya kuufuata mwili, bali tumikianeni kwa upendo. Maana torati yote imetimilika katika neno moja, nalo ni hili, Umpende jirani yako kama nafsi yako.”

 

7.       Watumishi wa ndani katika nyumba ya mchungaji ni lazima wafanyike Baraka katika nyumba ya Mchungaji.     

 

Katika mstari wa msingi wa somo hili nimenukuu habari za binti mmoja kijakazi katika nyumba ya Naamani ambaye alichukuliwa mateka huko Syria, lakini binti huyu aligeuka Baraka kubwa kwa sababu kupitia yeye na imani yake Bwana wake aliponywa ukoma wake, mfanyakazi huyu alichukuliwa mateka kutoka Israel lakini jambo la kushangaza hajawahi kuweka kinyongo chochote alikubali maisha ya ujakazi na utumwa huku akiwa mwaminifu kwa Bwana wake huku akimtakia afya njema na mafanikio zaidi, Naaman tunaelezwa kuwa alikuwa mzuri sana kwani jina Naaman maana yake ni mzuri lakini alipougua ukoma hali yake iliharibika na sasa kijakazi huyu anamtakia bibi yake na bwana wake furaha ya kweli kwa kujali afya ya Naamani

 

2Wafalme 5:1-5 “Basi Naamani, jemadari wa jeshi la mfalme wa Shamu, alikuwa mtu mkubwa mbele ya bwana wake, na mwenye kuheshimiwa, kwa sababu kwa mkono wake Bwana alikuwa amewapa Washami kushinda; tena alikuwa mtu hodari wa vita; lakini alikuwa mwenye ukoma. Na Washami walikuwa wametoka vikosi, wakachukua mfungwa mmoja kijana mwanamke kutoka nchi ya Israeli; naye akamhudumia mkewe Naamani. Akamwambia bibi yake, Laiti bwana wangu angekuwa pamoja na yule nabii aliyeko Samaria! Maana angemponya ukoma wake.”

 

Kila mfanyakazi katika nyumba ya mtumishi wa Mungu anapaswa kuwa sababu ya Baraka na uponyaji wa nyumba ya mtumishi badala ya kutumika kama ajenti wa shetani na kusababisha maafa na anguko la mtumishi wa Mungu au huduma yake, aidha kuwa na moyo wa shukurani na subira kuacha tamaa, wivu na kutokuyatenda majukumu yako ipaswavyo, binti yule wa kiyahudi alikuwa mwaminifu na mwenye moyo wa kweli kwani licha ya kuwa alikuwa amechukuliwa mateka lakini alikuwa ni mtu aliyethamini utumishi wa Naamani na kutamani kama angeponywa ukoma wake, alikuwa na imani kubwa kwani haijawahi kusikika kokote kuwa mtu amewahi kuponywa ukoma wake lakini yeye alimuamini Elisha na kusaidiki kuwa bwana wake anaweza kupata msaada Endapo angekutana na mtu wa Mungu na ikawa hivyo kwani Naamani aliponywa na sio mwili wake tu na alimuamini Mungu wa Israel hata ushindi wake ulitokana na Mungu wa Israel

 

8.       Watumishi wa ndani katika nyumba ya mchungaji ni lazima wavae kwa kujisitiri

 

Kama mtumishi wa Mungu ndani ya nyumba ya mchungaji hakikisha kuwa unavaa kwa heshima na kujisitiri, haiwezekani unakaa katika nyumba ya Mtu wa Mungu kisha ukawa unavaa mavazi ya kikahaba na kutumika kama chombo cha ibilisi kwaajili ya kumaliza huduma ya kichungaji swala hilo halitaleta Baraka kwako na kwa mwili wa Kristo, acha kujifikiri mwenyewe na starehe zako na baadala yake fikiri kuhusu faida za mwili wa Kristo na ufalme wa Mungu.

               

1Timotheo 2:9-10 “Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani; bali kwa matendo mema, kama iwapasavyo wanawake wanaoukiri uchaji wa Mungu.”

 

Mithali 7:10-18 “Na tazama, mwanamke akamkuta, Ana mavazi ya kikahaba, mwerevu wa moyo; Ana kelele, na ukaidi; Miguu yake haikai nyumbani mwake. Mara yu katika njia kuu, mara viwanjani, Naye huotea kwenye pembe za kila njia. Basi akamshika, akambusu, Akamwambia kwa uso usio na haya, Kwangu ziko sadaka za amani; Leo hivi nimeziondoa nadhiri zangu; Ndiyo maana nikatoka nikulaki, Nikutafute uso wako kwa bidii, nami nimekuona. Nimetandika kitanda changu, magodoro mazuri, Kwa matandiko ya Kimisri yenye mistari. Nimetia kitanda changu manukato, Manemane na udi na mdalasini. Haya, na tushibe upendo hata asubuhi, Tujifurahishe nafsi zetu kwa mahaba.”

 

9.       Watumishi wa ndani katika nyumba ya mchungaji wasijaribu kuwa mrithi wa mama Mchungaji

 

Hakuna sheria inayokataza Mchungaji kumuoa binti wake wa kazi endapo itatokea Mungu ametaka iwe hivyo, hata hivyo litakuwa ni jambo lenye kuchukiza na kuleta utata mkubwa sana endapo itatokea unaolewa na Mchyhungaji baada ya mama Mchungaji, maandiko yanaonyesha kuwa ni chukizo kwa mjakazi kumrithi bibi yake, Muombe Mungu akupe mumeo na usijihusishe na maisha ya Mchungaji wale mke wake hata kama uliyasoma  madhaifu yake, watmishi wa Mungu tafadhali Mungu akupe hekima usilitupia jicho lako kwa binti wa kazi yeye na awe kama moja ya mabinti zako tu nyumbani, Mwandishi wa kitabu cha Mithali alionyesha kuwa kuoa housegirl ni jambo lisilovumilika na linaweza kutetemesha nchi

 

Mithali 30:21-23 “Kwa ajili ya mambo matatu nchi hutetemeka, Naam, kwa ajili ya manne haiwezi kuvumilia. Mtumwa apatapo kuwa mfalme; Mpumbavu ashibapo chakula; Mwanamke mwenye kuchukiza aolewapo; Na mjakazi aliye mrithi wa bibi yake.”

 

10.   Watumishi wa ndani katika nyumba ya mchungaji Wanaweza kumjua Mchungaji vema zaidi kuliko watu wengine wote

 

Watumishi wa ndani katika nyumba ya Mchungaji wanauwezo wa kumjua Mchungaji na mahitaji yake vema zaidi kuliko watu wengine, Nyakati za kanisa la kwanza wakati Mchungaji Yakobo na Petro walipokuwa wamekamatwa, na Yakobo akauawa na Herode ni ukweli uliokuwa wazi kuwa kanisa lilimuomba Mungu kwa bidii sana lakini hata hivyo hawakuwa na Imani kuwa Mungu angefanya muujiza, Hata hivyo Mungu alimtuma malaika akamfungua Petro Gerezani na hata alipokuwa akigonga mlango mtu aliyetambua kuwa Petro anagonga mlango alikuwa ni Roda mfanyakazi wa ndani katika nyumba ya Mariamu mama yake Yohana, binti huyu kwa furaha aliacha kufungua mlango na kuwapasha wote kuwa Petro anagonga mlango, hata hivyo kila mmoja katika kanisa walifikiria kuwa binti huyo ana wazimu ni kichaa, hayuko sawasawa,  lakini ni ukweli ulio wazi yeye ndiye aliyekuwa sahihi kuliko watu wote, moyo wake upendo na Imani yake kwa Mungu ilimfanya kuwa na mtazamo tofauti na watu wengine wote yeye alimjua Petro vizuri na hata sauti yake na alipogonga pia alikuwa anajua namna Petro anavyogonga mlango wa nyumba

 

Matendo 12:11-16 “Hata Petro alipopata fahamu akasema, Sasa nimejua yakini ya kuwa Bwana amempeleka malaika wake na kunitoa katika mkono wa Herode na katika kutazamia kote kwa taifa la Wayahudi. Na alipokuwa akifikiri haya akafika nyumbani kwa Mariamu, mamaye Yohana, ambaye jina lake la pili ni Marko; na watu wengi walikuwa wamekutana humo wakiomba. Naye alipobisha kilango cha lango, kijakazi, jina lake Roda, akaja kusikiliza. Alipoitambua sauti ya Petro, hakukifungua lango, kwa ajili ya furaha, bali alipiga mbio, akaingia ndani akawaambia kwamba Petro anasimama mbele ya lango. Wakamwambia, Una wazimu. Lakini yeye akakaza sana, akasema ya kwamba ndivyo hivyo. Wakanena, Ni malaika wake. Petro akafuliza kugonga, hata walipokwisha kumfungulia wakamwona, wakastaajabu.”

 

Hii inatukumbusha na kutufundisha kuwa watumishi wa ndani katika nyumba ya Mchungaji wanaweza kuwa na ufahamu mkubwa na wa kina kumuhusu mtumishi wa Mungu nahata kumjua Mungu na utendaji wake kuliko mtu mwingine yeyote na Mungu amewapa wao neema ya kutambua mwenendo na uhitaji wa Mchungaji wakati mwingine kuliko wengine katika kanisa, na tunakumbushwa hapa kuwa hatupaswi kuwafikiria kuwa ni wenye wazimu hata kidogo, na kuwapuuzia au kuipuuzia mitazamo yao ya kiroho

 

11.   Watumishi wa ndani katika nyumba ya mchungaji ni lazima wawe waaaminifu kwa mama Mchungaji

 

Ruthu ni mfano wa kuigwa kwa uaminifu wake aliokuwa nao kwa Mkwewe, alisimama na mkwewe katika mazingira yaliyokuwa magumu sana na kujionyesha kuwa mwaminifu hata kwa gharama yoyote, Yeye alikuwa ni Mmoabu na hakukuwa na kitu cha kupoteza endapo angemuacha Naomi lakini alisimama na mkwewe katika mazingira magumu sana ambo lililomletea sifa za kipekee na faraja kubwa sana hapo baadaye, simama na mama Mchungaji katikamhali zote iwe njema au mbaya usikubali kumuacha mama Mchungaji isipokuwa kama utaolewa na kuwa na majukumu yako mengine yanayokulazimu

 

Ruthu 1:16-18 “Naye Ruthu akasema, Usinisihi nikuache, Nirejee nisifuatane nawe; Maana wewe uendako nitakwenda, Na wewe ukaapo nitakaa. Watu wako watakuwa watu wangu, Na Mungu wako atakuwa Mungu wangu; Pale utakapokufa nitakufa nami, Na papo hapo nitazikwa; Bwana anitende vivyo na kuzidi, Ila kufa tu kutatutenga wewe nami.Basi alipomwona kuwa amekaza nia yake kufuatana naye, aliacha kusema naye.”       

 

Ufunuo 2:10 “Usiogope mambo yatakayokupata; tazama, huyo Ibilisi atawatupa baadhi yenu gerezani ili mjaribiwe, nanyi mtakuwa na dhiki siku kumi. Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima.”  
           

Hitimisho:

Wafanyakazi wa ndani hasa katika nyumba za watumishi wa Mungu wameitwa kuwa mabalozi wa Baraka za Mungu, kwa Imani yao, mwenendo na tabia zao, kamwe hatuwatarajii wao kuwa sababu ya kusambaratika kwa huduma za wachungaji au kusababisha kero na ugomvi katika nyumba ya Mchungaji, haipendezi wao kuwa sababu ya dharau, na uchonganishi kati ya huduma ya Mchungaji na washirika wake, somo hili linatoa mwanga tu wa namna na jinsi iwapaswavyo kuishi kwaajili ya Mungu na wala si kwaajili yao, aidha na kuwaonyea ili kwamba waache kutumika kama chombo cha shetani na badala yake waweze kutumika kuiinua huduma ya kichungaji na kuiweka kwenye heshima inayostahili, ni imani yangu kuwa kama unafanya kazi katika nyumba za watumishi wa Mungu hutakata tamaa na kujidharau na kujifikiri kuwa huna maana nataka nikutie moyo ili ujue ya kuwa Mungu anakuzingatia sana anajua umuhimu wako katika kuitumikia familia ya mtumishi wake!


Wengi wa waliofanya kazi katika nyumba za watumishi wa Mungu kamwe Mungu hakuwahi kuwapuuzia kwani wengine alijifunua kwao na kuwabariki na wengine walimuona Mungu hata pale walipopita katiia changamoto ngumu Mungu aliwatokea


Wakati Sara alipomtendea vibaya Hajiri malaika wa Bwana hawakumuacha Hajiri na badala yake walimuelekeza njia sahihi ya kufanya na kuyalinda maisha yake na ya mtoto wake, Mungu hajawahi kuwadharau wajakazi na kuwaona kama watu wasio na maana na badala yake aliwahusisha katika Baraka zake alizozikudsudia sawa na nyumba za watumishi wake  


Mwanzo 16:6-11 “Naye Abramu akamwambia Sarai, Tazama, mjakazi wako yu mkononi mwako, mtendee lililo jema machoni pako. Sarai akamtesa, naye akakimbia kutoka mbele yake. Malaika wa BWANA akamwona kwenye chemchemi ya maji katika jangwa, chemchemi iliyoko katika njia ya kuendea Shuri. Akamwambia, Hajiri, wewe mjakazi wa Sarai, unatoka wapi, nawe unakwenda wapi? Akanena, Nakimbia mimi kutoka mbele ya bibi yangu Sarai. Malaika wa BWANA akamwambia, Rudi kwa bibi yako, ukanyenyekee chini ya mikono yake. Malaika wa BWANA akamwambia, Hakika nitauzidisha uzao wako, wala hautahesabika kwa jinsi utakavyokuwa mwingi.Malaika wa BWANA akamwambia, Tazama! Wewe una mimba, utazaa mwana wa kiume, nawe utamwita jina lake Ishmaeli, maana BWANA amesikia kilio cha mateso yako.”


1Timotheo 4:12 “Mtu awaye yote asiudharau ujana wako, bali uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi.”

               

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

 Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Maoni 1 :

Bila jina alisema ...

AMEEN Pastor, somo zuri Mungu akubariki