Alhamisi, 15 Mei 2025

Nguvu ya maombi!


Isaya 38:1-6 “Siku hizo Hezekia aliugua, akawa katika hatari ya kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amozi, akaenda kwa mfalme, akamwambia, Bwana asema hivi, Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona. Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Bwana, akasema, Ee Bwana, kumbuka haya, nakusihi, kwamba nimekwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana. Ikawa, neno la Bwana likamjia Isaya, kusema, Enenda ukamwambie Hezekia, Bwana, Mungu wa Daudi, baba yako, asema hivi, Mimi nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama, nitaziongeza siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano. Nami nitakuokoa wewe, na mji huu, na mkono wa mfalme wa Ashuru, nami nitaulinda mji huu.”



Utangulizi:

Mojawapo ya njia ya kutuletea neema kubwa sana kutoka kwa Mungu ni pamoja na njia ya maombi, wote tutakuwa tunafahamu jinsi maombi yalivyo na nguvu kubwa sana, yana nguvu ya kuteremsha rehema na neema kutoka kwa Mungu hata wakati tunapopitia changamoto za aina mbalimbali katika maisha yetu, maombi yana uwezo wa kumfanya mwanamke aliye tasa kuwa na watoto wengi, maombi yana uwezo wa kusababisha adui kupigwa na ushindi kupatikana, maombi  yana uwezo wa kufungua utendaji wa miujiza na kuchochewa kwa karama, maombi yana uwezo wa kubatilisha hukumu ya kifo na kurejesha uhai, maombi yana uwezo wa kugeuza kesi, maombi yanauwezo wa kubatilisha kile Mungu amesema. Maombi yana uwezo wa kufungua magereza za kimwili na kiroho, Mungu ametupa maombi kama njia ya kufanya kazi na yeye na kumruhusu kufanya kazi duniani. Maombi yana nguvu isiyoweza kuelezeka katika changamoto yoyote unayokutana nayo duniani wewe tumia maombi.

Mathayo 7:7-11 “Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. Au kuna mtu yupi kwenu, ambaye, mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe? Au akiomba samaki, atampa nyoka? Basi ikiwa ninyi, mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao?

Sisi ndio wenye maamuzi ya mwisho ya kuamua Mungu atafanya nini duniani kwa kutumia maombi, Hapa duniani sio eneo la utawala wa Mungu, ni eneo ambalo Mungu amewapa wanadamu kutawala, yeye utawala wake uko mbinguni, huko mapenzi yake yote hutimizwa kwa ukamilifu, lakini sivyo ilivyo duniani, ili kumpa Mungu kibali cha kufanya mambo duniani ni lazima tuombe, tunapoomba tunamruhusu Mungu kufanya yanayotakiwa yafanyike duniani kama yanavyofanyika mbinguni.

Zaburi 123:1-3 “Nimekuinulia macho yangu, Wewe uketiye mbinguni. Kama vile macho ya watumishi Kwa mkono wa bwana zao Kama macho ya mjakazi Kwa mkono wa bibi yake; Hivyo macho yetu humwelekea Bwana, Mungu wetu, Hata atakapoturehemu.”

Mwanzo 1:26-28 “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi. Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba. Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi.”

Kupitia maombi tunaweza kumfungulia Mungu njia ya kututendea mambo makubwa na magumu tusiyoyajua, maombi yana uwezo mkubwa sana wa kubadilisha mambo na utendaji wa Mungu kutoka katika maisha ya mtu binafsi mpaka maswala ya kitaifa na ulimwengu kwa ujumla, tunapoomba tunamruhusu Mungu kuinguilia kati na kufanya jambo kwaajili yetu hapa duniani, tunaruhusu utawala wa kimbingu kuleta msaada wa haraka duniani.

-          Maombi yanaweza kumfanya tasa kuwa na watoto - Hana aliyekuwa mwanamke tasa, alipitia machungu na mateso na mashutumu kutoka kwa mke mwenzake, alinyanyasika hata pamoja na kupendwa sana na mumewe, lakini Penina mara kwa mara alimchokoza na kumkumbusha hali yake ya kukosa mtoto jambo ambalo lilimsikitisha sana na kumfanya kutembea kwa huzuni, Hana hata hivyo alifahamu kuwa njia pekee inayoweza kubadilisha hali yake ni maombi, hivyo alimimina maombi yake mbele za Mungu na hatimaye Mungu alisikia na kubadilisha hali yake aliyokuwa nayo, kutoka hali ya utasa kuwa mama wa watoto wengi.

 

1Samuel 1:1-6 “Palikuwa na mtu mmoja wa Rama, Msufi, wa nchi ya milima milima ya Efraimu, jina lake akiitwa Elkana, mwana wa Yerohamu, mwana wa Elihu, mwana wa Tohu, mwana wa Sufu, Mwefraimu naye alikuwa na wake wawili; jina lake mmoja akiitwa Hana, na jina lake wa pili aliitwa Penina; naye huyo Penina alikuwa na watoto, lakini Hana hakuwa na watoto. Na mtu huyo alikuwa akikwea kutoka mjini kwake mwaka kwa mwaka, ili kuabudu, na kumtolea Bwana wa majeshi dhabihu katika Shilo. Na wale wana wawili wa Eli, Hofni na Finehasi, makuhani wa Bwana, walikuwako huko. Hata siku ile ilipofika Elkana alipotoa dhabihu, kumpa mkewe Penina sehemu, akawapa na watoto wake wote, waume kwa wake, sehemu zao; lakini Hana humpa sehemu mara mbili; maana alimpenda Hana, ingawa Bwana alikuwa amemfunga tumbo. Ila mwenzake humchokoza sana, hata kumsikitisha, kwa sababu Bwana alikuwa amemfunga tumbo.”

 

1Samuel 1:10-20 “Naye huyo mwanamke alikuwa na uchungu rohoni mwake, akamwomba Bwana akalia sana. Akaweka nadhiri, akasema, Ee Bwana wa majeshi, ikiwa wewe utaliangalia teso la mjakazi wako, na kunikumbuka, wala usinisahau mimi mjakazi wako, na kunipa mimi mjakazi wako mtoto mume, ndipo mimi nitakapompa Bwana huyo mtoto siku zote za maisha yake, wala wembe hautamfikilia kichwani kamwe. Ikawa, hapo alipodumu kuomba mbele za Bwana, Eli akamwangalia kinywa chake. Basi Hana alikuwa akinena moyoni mwake; midomo yake tu ilionekana kama anena, sauti yake isisikiwe; kwa hiyo huyo Eli alimdhania kuwa amelewa. Ndipo Eli akamwambia, Je! Utakuwa mlevi hata lini? Achilia mbali divai yako. Hana akajibu, akasema, Hasha! Bwana wangu, mimi ni mwanamke mwenye roho ya huzuni, mimi sikunywa divai wala kileo, ila nimeimimina roho yangu mbele za Bwana. Usimdhanie mjakazi wako kuwa ni mwanamke asiyefaa kitu; kwa kuwa katika wingi wa kuugua kwangu na kusikitika kwangu ndivyo nilivyonena hata sasa. Ndipo Eli akajibu, akasema, Enenda kwa amani; na Mungu wa Israeli akujalie haja yako uliyomwomba. Naye akasema, Mjakazi wako na aone kibali machoni pako. Basi huyo mwanamke akaenda zake, naye akala chakula, wala uso wake haukukunjamana tena. Wakaondoka asubuhi na mapema, wakasali mbele za Bwana, kisha wakarejea na kufika nyumbani kwao huko Rama; Elkana akamjua mkewe Hana; naye Bwana akamkumbuka. Ikawa, wakati ulipowadia, Hana akachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; akamwita jina lake Samweli, akisema, Kwa kuwa nimemwomba kwa Bwana.”

 

Tunajifunza hapa kuwa maombi yana uwezo wa kubadilisha aibu kuwa heshima, yana uwezo wa kufumba vinywa vya maadui zetu, yana uwezo wa kunyamazisha wanaotubeza, yana uwezo wa kuifanya biashara yako kufanikiwa, mashamba kuzaa, mifugo yako kuongezeka, maisha yako kujawa na mafanikio, Huduma yako kutendeka kwa kiwango na kanisa lako linaloonekana kama tasa likawa kanisa lenye watu wengi, tunaweza kubadilisha hali yoyote inayotukabili iwe ni chungu kuwa furaha, Hana hakukubali kubakia vile alivyo lakini kwa kupitia maombi alibadilisha mwelekeo wa maisha yake na kurejesha heshima yake kama mwanamke kamili kwa njia ya maombi, Maombi yanaweza kubadilisha hatima yako na jina lako.

 

-          Maombi yanaweza kutuletea ushindi vitani - Maandiko yanaonyesha kuwa watu waliookolewa wako vitani, Paulo anasema kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama maana yake hatuna adui wa kimwili sisi, wala hatuwezi kumuhesabu mwanadamu awaye yote kuwa ni adui yetu, lakini adui zetu wako rohoni, ni mamlaka, ni falme ni wakuu wa giza na majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho, hao tunaweza kushughulika nao kwa njia ya kuomba peke yake, maombi yatatupa ushindi dhidi ya nguvu za giza popote.  

 

Waefeso 6:10-18 “Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama. Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani, na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani; zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu; kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;”

 

Ushindi wetu hauwezi kupatikana kwa nguvu za mwili na akili za kibinadamu na ujanja ujanja ushindi wetu utapatikana kwa kumualika Mungu katika vita zetu kupitia maombi, wakati Musa alipokuwa jangwani wanaikabili Kanaani njiani waameleki walitokea na wakapigana na Israel neno la Mungu linatuambia kuwa Musa na Haruni na Huri walipanda mlimani  na huko Musa alinyoosha mikono yake kwa Mungu na Yoshua  na Israel walipata ushindi, Musa akishusha mikono Israel wanashindwa, watumishi wa Mungu ili tuweze kuwa na ushindi tusikubali kushusha mikono yetu, tuendelee kumuinulia Mungu mikono yetu na ushindi utakuwa upande wetu kwa Dhahiri hapo tunajifunza nguvu ya maombi, kwamba tunaweza kupata ushindi.

 

Kutoka 17:10-13 “Basi Yoshua akafanya kama Musa alivyomwambia, akapigana na Amaleki; na Musa na Haruni na Huri wakapanda juu ya kile kilima. Ikawa, Musa alipouinua mkono wake, Israeli walishinda; na alipoushusha mkono wake, Amaleki walishinda. Lakini mikono ya Musa ilikuwa mizito; basi wakatwaa jiwe, wakaliweka chini yake akalikalia. Haruni na Huri wakaitegemeza mikono yake, mmoja upande huu na mmoja upande huu; mikono yake ikathibitika hata jua lilipokuchwa. Yoshua akawaangamiza Amaleki na watu wake kwa ukali wa upanga.”

 

-          Maombi yanaongeza nguvu wakati wa upinzani – Nyakati za kanisa la kwanza Mitume walipoanza kuhubiri injili na kufanya miujiza, walikutana na upinzani, walikamatwa, waliwekwa gerezani, waliadhibiwa na walitishwa na walikatazwa wasizungumze lolote kwa jina la Yesu, kanisa lilipopata taarifa walijua ni namna gani wanaweza kuendelea na injili, walijua dawa ni kuomba na walipoomba mahali pale walipokuweko pakatikiswa wakajaa nguvu  za Roho Mtakatifu na kazi ya Mungu ikaendelea na neno la Mungu linaenea.

 

Matendo 4:21-31 “Nao walipokwisha kuwatisha tena wakawafungua, wasione njia ya kuwaadhibu, kwa sababu ya watu; kwa kuwa watu wote walikuwa wakimtukuza Mungu kwa hayo yaliyotendeka; maana umri wake yule mtu aliyefanyiwa ishara hii ya kuponya ulipita miaka arobaini. Hata walipofunguliwa, wakaenda kwa watu wao, wakawapasha habari ya mambo yote waliyoambiwa na wakuu wa makuhani na wazee. Nao waliposikia, wakampazia Mungu sauti zao kwa moyo mmoja, wakisema, Mola, wewe ndiwe Mungu, ndiwe uliyefanya mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo; nawe ulinena kwa Roho Mtakatifu kwa kinywa cha babaetu Daudi, mtumishi wako, Mbona mataifa wamefanya ghasia, Na makabila wametafakari ubatili? Wafalme wa dunia wamejipanga, Na wakuu wamefanya shauri pamoja Juu ya Bwana na juu ya Kristo wake. Maana ni kweli, Herode na Pontio Pilato pamoja na Mataifa na watu wa Israeli, walikusanyika katika mji huu juu ya Mtumishi wako mtakatifu Yesu, uliyemtia mafuta, ili wafanye yote ambayo mkono wako na mashauri yako yamekusudia tangu zamani yatokee. Basi sasa, Bwana, yaangalie matisho yao; ukawajalie watumwa wako kunena neno lako kwa ujasiri wote, ukinyosha mkono wako kuponya; ishara na maajabu vifanyike kwa jina la Mtumishi wako mtakatifu Yesu. Hata walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri.”

 

-          Maombi yanaweza kubadilisha mpango mbaya wa Serikali na wafalme – Mfalme Herode alikuwa na mpango wa kuwaangamiza viongozi wa kanisa, na alimkamata Yakobo na kumuua na alipoona imewapendeza wayahudi akamkamata na Petro ili naye amuuue vile vile, maandiko yanatueleza kuwa Kanisa lilimuomba Mungu kwa bidii kwaajili ya Petro aliyekuwa amefungwa na Mungu alijibu maombi kwa kumtuma malaika wake aliyemtokea Petro gerezani na kumfungua, hakuna mlango wowote mgumu utakaofungiwa au mnyororo wowote wa adui unaoweza kushindana na nguvu ya maombi, maombi yana nguvu dhidi ya wafalme, Maombi yana nguvu dhidi ya serikali, na yana nguvu dhidi ya magereza yoyote.

 

Matendo 12:5-11 “Basi Petro akalindwa gerezani, nalo kanisa likamwomba Mungu kwa juhudi kwa ajili yake. Hata wakati Herode alipotaka kumtoa, usiku ule ule Petro alikuwa analala katikati ya askari wawili, amefungwa minyororo miwili; walinzi mbele ya mlango wakailinda gereza. Mara malaika wa Bwana akasimama karibu naye, nuru ikamulika mle chumbani, akampiga Petro ubavuni, akamwamsha, akisema, Ondoka upesi. Minyororo yake ikamwanguka mikononi. Malaika akamwambia, Jifunge, kavae viatu vyako. Akafanya hivyo. Kisha akamwambia, Jivike nguo yako, ukanifuate. Akatoka nje, akamfuata; wala hakujua ya kuwa ni kweli yaliyofanywa na malaika; bali alidhani kwamba anaona maono. Na walipopita lindo la kwanza na la pili, wakaja hata mlango wa chuma wa kuingilia mjini, ukawafungukia wenyewe. Wakatoka nje, wakapita katika njia moja; mara malaika akamwacha. Hata Petro alipopata fahamu akasema, Sasa nimejua yakini ya kuwa Bwana amempeleka malaika wake na kunitoa katika mkono wa Herode na katika kutazamia kote kwa taifa la Wayahudi.”

 

-          Maombi yanaweza kufungua milango ya gereza – Paulo na Sila waliokuwa wakiihubiri injili walipata matokeo makubwa sana na watu wengi waliokolewa lakini baada ya kijakazi mmoja kutolewa pepo wa uaguzi bwana zake walikasirika na kuwafanyia ghasia kubwa sana na hivyo mitume waliwekwa gerezani, na kufungwa katika mikatale, tunaelezwa kuwa watu hawa waliimba na kumuomba Mungu usiku wa manane na mara walipofanya hayo tunaelezwa kuwa kila kifungo cha magereza kiliachia sio wao tu na wafungwa wote na matokeo makubwa ni kuwa hata mkuu wa gereza aliokolewa na familia yake yote, tunajifunza kuwa hakuna kifungo chochote kiwe cha kimwili, cha kiroho, cha gereza cha waganga wa kienyeji cha wachawi kinachoweza kusimama mbele ya maombi, hakuna mtu yeyote awe askari awe mfungwa ambaye maombi hayana nguvu za kumgusa, kuna nguvu ya ajabu katika kuomba kwa sababu hiyo kanisa tusipuuzie kuomba kwa kila jambo tuombe, omba kila unapokutana na changamoto yoyote ile omba omba omba!  

 

Matendo 16:25-31 “Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. Ghafula pakawa tetemeko kuu la nchi, hata misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, vifungo vya wote vikalegezwa. Yule mlinzi wa gereza akaamka, naye alipoona ya kuwa milango ya gereza imefunguka, alifuta upanga, akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wamekimbia. Ila Paulo akapaza sauti yake kwa nguvu, akisema, Usijidhuru, kwa maana sisi sote tupo hapa. Akataka taa ziletwe, akarukia ndani, akitetemeka kwa hofu, akawaangukia Paulo na Sila; kisha akawaleta nje akasema, Bwana zangu, yanipasa nifanye nini nipate kuokoka? Wakamwambia, Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako.”

 

-          Maombo yanaweza kubadilisha mpango wa maangamizo – Mungu mwenyewe alikuwa amemtuma Yona kwamba aende Ninawi na kuuonya mji ule na kuutangazia kuwa baada ya siku 40 ataungamiza, watu wa Ninawi na mfalme wao walipoambiwa kuhusu mpango huo walimgeukia Mungu wakafunga na kuomba na kumshawishi Mungu kubadili hukumu na Mungu akaghairi maangamizi aliyokuwa ameyakusudia, maombi ya toba yanaweza kubadilisha hukumu ya Mungu ya kitaifa na ya mtu mmoja mmoja na kusababisha neema na rehema za Mungu ziweze kumwagika kwetu.

 

Yona 3:4 -10 “Yona akaanza kuuingia mji mwendo wa siku moja, akapaza sauti yake, akasema, Baada ya siku arobaini Ninawi utaangamizwa. Basi watu wa Ninawi wakamsadiki Mungu; wakatangaza kufunga, wakajivika nguo za magunia, tangu yeye aliye mkubwa hata aliye mdogo. Habari ikamfikia mfalme wa Ninawi, naye akaondoka katika kiti chake cha enzi, akavua vazi lake, akajivika nguo za magunia, na kuketi katika majivu. Naye akapiga mbiu, akatangaza habari katika mji wa Ninawi, kwa amri ya mfalme na wakuu wake; kusema, Mwanadamu asionje kitu, wala mnyama wala makundi ya ng'ombe, wala makundi ya kondoo; wasile, wala wasinywe maji; bali na wafunikwe nguo za magunia, mwanadamu na mnyama pia, nao wakamlilie Mungu kwa nguvu, naam, na wageuke, kila mtu akaache njia yake mbaya, na udhalimu ulio mikononi mwake. Ni nani ajuaye kwamba Mungu hatageuka na kughairi, na kuiacha hasira yake kali, ili msiangamizwe? Mungu akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi Mungu akalighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende.”

 

-          Maombi yana uwezo wa kubatilisha tangazo la kifo – Katika kifungu chetu cha msingi cha somo hili tunamuona nabii Isaya akitangaza mauti kwa Mfalme Hezekia, tangazo hilo nabii Isaya alikuwa amepewa na Mungu, lakini Hezekia alilipuuzia tangazo hilo na kugeukia ukutani aliomba kwa bidii na kwa kulia machozi na kumkumbusha Mungu matendo yake ya rehema hata alipokuwa akiomba katikati ya kuomba kwake Mungu alisema na nabii Isaya kwamba amemuongezea Hezekia miaka 15 ya kuishi kwake, kumbe kupitia maombi tunaweza kukata rufaa kwa Mungu kwaajili ya tangazo lolote la hukumu hata kama tangazo hilo au tamko hilo limetoka kwa Bwana mwenyewe! Tunaweza kumsihi Mungu kwa rehema zake na akafanya kwa maombi

 

Isaya 38:1-6 “Siku hizo Hezekia aliugua, akawa katika hatari ya kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amozi, akaenda kwa mfalme, akamwambia, Bwana asema hivi, Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona. Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Bwana, akasema, Ee Bwana, kumbuka haya, nakusihi, kwamba nimekwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana. Ikawa, neno la Bwana likamjia Isaya, kusema, Enenda ukamwambie Hezekia, Bwana, Mungu wa Daudi, baba yako, asema hivi, Mimi nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama, nitaziongeza siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano. Nami nitakuokoa wewe, na mji huu, na mkono wa mfalme wa Ashuru, nami nitaulinda mji huu.”

 

Hitimisho.

 

Tunajifunza hapo kuwa hakuna jambo lolote lililo gumu lisiloweza kubadilishwa kwa maombi, kama watumishi wa Mungu waliotutangulia waliweza kubatilisha maswala kadhaa wa kadhaa katika maisha yao na huduma zao kupitia kuomba sisi nasi leo tunaweza kuliitia jina la Bwana Mungu wetu asiye badilika ambaye ni yeye yule jana leo na hata milele na tukashuhudia matokeo makubwa katika maisha yetu kwa sababu hiyo tusiache kuomba tudumu katika maombi siku zote za maisha yetu

 

Wakolosai 4:2-3 “Dumuni sana katika kuomba, mkikesha katika kuomba huku na shukrani; mkituombea na sisi pia, kwamba Mungu atufungulie mlango kwa lile neno lake, tuinene siri ya Kristo, ambayo kwa ajili yake nimefungwa

 

Karibu na wewe, Mungu wangu, Karibu zaidi Bwana wangu……

 

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

 

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Maoni 1 :

Bila jina alisema ...

Ameen Pastor