Jumatano, 28 Mei 2025

Mleteni huku kwangu!


Mathayo 17:14-21 “Nao walipoufikia mkutano, mtu mmoja akamjia, akampigia magoti, akisema, Bwana, umrehemu mwanangu, kwa kuwa ana kifafa, na kuteswa vibaya; maana mara nyingi huanguka motoni, na mara nyingi majini. Nikamleta kwa wanafunzi wako, wasiweze kumponya. Yesu akajibu, akasema, Enyi kizazi kisichoamini, kilichopotoka, nitakaa pamoja nanyi hata lini? Nitachukuliana nanyi hata lini? Mleteni huku kwangu. Yesu akamkemea pepo, naye akamtoka; yule kijana akapona tangu saa ile. Kisha wale wanafunzi wakamwendea Yesu kwa faragha wakasema Mbona sisi hatukuweza kumtoa? Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu. [Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.]




Utangulizi:

Katika kifungu chetu cha msingi wa maandiko leo, tunakutana na kisa chenye kushangaza sana ambapo wanafunzi wa Yesu walishindwa kumsaidia kijana aliyekuwa anateswa na pepo wa kifafa, Baba wa kijana alileta mashitaka hayo kwa Yesu kwamba kijana wake amekuwa akisumbuliwa na pepo hao wa kifafa ambao wakati mwingine wamemtupa kijana wake katika maji na katika moto, na alipomleta kwa wanafunzi wake wao walishindwa kumtoa, Ndipo Yesu kwa uchungu mkubwa alitoa agizo lenye uzito “Mleteni huku Kwangu” agizo hili sio agizo la kawaida ni mamlaka ya kiroho yenye maana pana kwa kila mtu anayetafuta msaada wa kweli.

Mleteni Kwangu!

Ni muhimu kufahamu kuwa ni swala la kawaida kwamba kila mwanadamu anapopatwa na shida au changamoto zozote zile zikiwepo changamoto za kiafya huwa anatafuta msaada, na wakati mwingine wanadamu huwa na tabia ya kupeana taarifa wapi pa kwenda ili changamoto zako ziweze kutatuliwa, Baba wa kijana huyu anaonekana wazi kukosa Amani kwaajili ya afya ya mtoto wake ambaye alikuwa anasumbuliwa na Pepo wa kifafa, na huenda alihangaika sehemu nyingi sana kwaajili ya kujaribu kutatua hali ya kiafya iliyokuwa ikimkabili kijana wake, hatimaye huenda alisikia habari za Yesu, lakini wakati huu Yesu alikuwa mlimani pamoja na Petro na Yakobo na Yohana wanafunzi wengine walibaki, Mzee huyu aliwakabidhi wanafunzi wa Yesu changamoto za mwanae na wanafunzi walishindwa kushughulika nayo, Yesu alipofika baba wa kijana alitoa taarifa kwa Yesu na ndipo Yesu alipotoa amri “Mleteni huku kwangu

Kwanini aletwe kwa Yesu?

Watu wengi sana wanapopatwa na changamoto za namna mbalimbali kwa kawaida huwa hawampi Yesu nafasi ya Kwanza, na badala yake huanza kutumia akili zao za kawaida na za kibinadamu katika kutatua changamoto zinazowakabili na Yesu huwa anapewa nafasi ya mwisho, hii sio tu kwa wanadamu wa siku za leo, bali hata wakati Bwana Yesu alipokuwa duniani bado wako watu waliokuwa na changamoto mbalimbali walianza kupeleka changamoto zao kwa matabibu mbalimbali na kuingia gharama kubwa

Marko 5:25-29 “Na mwanamke mmoja mwenye kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, na kuteswa mengi kwa mikono ya matabibu wengi, amegharimiwa vitu vyote alivyo navyo, kusimfae hata kidogo, bali hali yake ilizidi kuwa mbaya aliposikia habari za Yesu, alipita katika mkutano kwa nyuma, akaligusa vazi lake;maana alisema, Nikiyagusa mavazi yake tu, nitapona. Mara chemchemi ya damu yake ikakauka, naye akafahamu mwilini mwake kwamba amepona msiba ule

Inawezekana umekuwa ukipitia changamoto za aina mbalimbali kama mwanadamu katika maisha yako ya kawaida, ni desturi na jambo la kawaida sana wanadamu kuomba ushauri kwa wanadamu wenzao na kuelezewa kuwa wajaribu hiki au kile, nenda hospitali hii au ile kamuone mwanasaikolojia huyu au yule, kamuone daktari huyu au yule, nenda kwa mganga huyu au yule, changamoto yako hii yuko mama mmoja huyo ni kiboko, changamoto yako hii inangekuwa kule Sumbawanga ingeshughulikiwa, tatizo lako hili lingekuwa kule Kwamsisi ni jambo dogo tu, changamoto yako hii ingekuwa kule Lamu - Mombasa sharifu angekusomea, hili tatizo lingepelekwa kule Korogwe kwa Semangube lingekuwa kama chai tu, hii kitu kuna wazee kule Kigombe Muheza inaisha na kadhalika na kadhalik wanadamu wanaweza kukupa ushauri wa kupeleka matatizo yako huku na kule na ukasumbuka sana kwaajili ya kutafuta uzima, na ikakugharimu sana, Mzee huyu ambaye alihangaika vile vile kwaajili ya kijana wake alipeleka changamoto yake huku na kule hospitali za kawaida zilishindwa, hospitali za rufaa zilishindwa na sasa akawaona wanafunzi wa Yesu ambao nao vile vile walishindwa!

·         Wanafunzi wa Yesu walishindwa – Bado walikuwa wanajifunza, Yesu alikuwa amewapa amri na mamlaka juu ya pepo, lakini walikosa namna na jinsi ya kuachilia nguvu za Mungu na kuitumia mamlaka hiyo kutoa Pepo, hii ni kwa sababu waliogopa, walishindwa kuamini na pia walikosa maisha ya kufunga na kuomba na hivyo mamlaka yao ilikuwa chini, Yesu aliwajulisha kuwa Pepo wana mamlaka za kijeshi na Pepo wa kifafa (aina hii) wana daraja la juu katika mamlaka za kipepo za kuwatesa wanadamu na kuwa wanaweza kutolewa kwa maisha ya kufunga na kuomba

 

Luka 10:17-19. “Ndipo wale sabini waliporudi kwa furaha, wakisema, Bwana, hata pepo wanatutii kwa jina lako. Akawaambia, Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme. Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru.”

 

Mathayo 17:17-21 “Yesu akajibu, akasema, Enyi kizazi kisichoamini, kilichopotoka, nitakaa pamoja nanyi hata lini? Nitachukuliana nanyi hata lini? Mleteni huku kwangu. Yesu akamkemea pepo, naye akamtoka; yule kijana akapona tangu saa ile. Kisha wale wanafunzi wakamwendea Yesu kwa faragha wakasema Mbona sisi hatukuweza kumtoa? Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu. [Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.]

 

Maisha duni ya kufunga na kuomba, pamoja na upungufu wa Imani ya wanafunzi wa Yesu ilikuwa ni sababu ya kushindwa kwao kuwaamuru pepo hawa wa kifafa kumuachia kijana na kumuweka huru Yesu aliwajulisha baadae tatizo lililokuwako, kwa hiyo walishindwa kumsaidia, na mzazi aliwashitaki kwa Yesu.

 

·         Wanafunzi wa Yesu walikuwa wanadamu – watu wengi sana wanapokuwa na changamoto za aina mbalimbali katika maisha katika akili zao kichwani kwanza huanza kuwafikiri wanadamu, wanafikiria mtu atakayewapa muunganiko “connection” mtu wa kuwaunganishia, wanaelekeza mawazo yao na kuwategemea wanadamu na kama ilivyo ada Mungu anakuwa chagua la mwisho

 

Yeremia 17:5-8 “Bwana asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha Bwana. Maana atakuwa kama fukara nyikani, Hataona yatakapotokea mema; Bali atakaa jangwani palipo ukame, Katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu. Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana, Ambaye Bwana ni tumaini lake. Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji, Uenezao mizizi yake karibu na mto; Hautaona hofu wakati wa hari ujapo, Bali jani lake litakuwa bichi; Wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, Wala hautaacha kuzaa matunda.”

 

·         Yesu ndiye suluhisho – Ziko shida ambazo madaktari wa kawaida hawawezi kushughulika nazo, ziko changamoto ambazo wanadamu hawawezi, ziko changamoto ambazo huwezi kuzidhibiti kwa mifumo ya kidini na kiserikali wala kwa uzoefu wako na maarifa yako bila kumkaribia Yesu Mwenyewe!

 

Yeye peke yake ndiye mwenye mamlaka yote mbinguni na duniani, hata wenye mamlaka na waliopewa mamlaka wanahitaji kumtegemea Yesu kila wakati, Yesu anapoagiza mleteni huku kwangu alikuwa anatualika wote kwamba changamoto yoyote kubwa au ndogo inayokukabili yeye anaweza kushughulika nayo, yeye ndiye mwenye mamlaka yote, jina lake lina kibali kila mahali, yeye ni mwisho wa matatizo zote, na kuwa kwake hakuna jambo lisilowezekana, hakuna linaloshindikana kwake, kila kitu ambacho kimeshindikana kipelekwe kwa Yesu, peleka watoto walioshindikana, peleka mke aliyeshindikana, peleka mume aliyeshindikana, peleka magonja na shida na changamoto zote zilizoshindikana kwa sababu Yesu sio wa kawaida !

 

Mathayo 28:18 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.”

 

Ufunuo 1:8 “Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, asema Bwana Mungu, aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi.”

 

Wafilipi 2:9-11 “Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba.”

 

Hakuna mafanikio ya kweli unayoweza kuyapata nje ya Yesu Kristo, yeye ndiye mwenye mamlaka yote, yeye ndiye mwanzo na mwisho Alfa na Omega, yeye kwa jina lake kila kitu kitapiga goti kiwe cha kuzimu, duniani au mbinguni, kila kitu kimetiishwa chini yake, mapepo yametiishwa chini yake magonjwa yametiishwa chini yake roho wote wachafu, falme mamlaka wakuu wa giza na majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho yametiishwa chini yake, hakuna shida ambayo yeye hawezi kuitatua, maarifa yako yanaweza kushindwa wagaganga wako wanaweza kushindwa, washauri wako wanaweza kukwama, dini yako inaweza kukwama, wanasaikolojia wako wanaweza kushindwa kukukwamua Lakini Yesu anasema na kutoa mwaliko leo Mleteni huku kwangu, Yako mambo katika maisha yako huwezi kuyashughulikia, unahangaika kwa sababu hujawahi kujaribu kwa Yesu, sikiliza mwito wa Mwana wa Mungu yeye anasema Mleteni huku kwangu, ni mke aliyeshindikana kwa ukorofi, mleteni huku kwangu, ni mtoto aliyeshindikana kwa ukorofi mleteni huku kwangu, ni mume aliyetekwa na makahaba mleteni huku kwangu, ni mlevi aliyepindukia kila mtu amemkataa mleteni huku kwangu, ni huduma yako haieleweki, mleteni huku Kwangu, ni magonjwa madakatari wameshindwa mleteni huku kwangu, ni mwenye nyumba mkorofi mleteni huku kwangu, ni bosi mwenye gubu mleteni huku kwangu, ni shida ya aina yoyote imekushika kooni Yesu anatoa mwaliko mleteni huku kwangu  Yesu habadiliki uwezo wake wa kutoa msaada bado uko pale pale yeye ni yeye yule jana leo na hata milele na hakuna jambo lililo gumu la kumshinda yeye.Hebu twende mbele za Bwana na kupeleka mahitaji yetu yote yaliyoshindikana kwake yeye ni mwema atatusaidia.

 

Waebrania 13:8 “Yesu Kristo ni yeye yule, jana na leo na hata milele.” Luka 1:37 “kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu.”

 

Fanya uamuzi leo, wa kumkabidhi Yesu lolote linalokusibu na lolote libnalokusumbua katika maisha yako

 

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Hakuna maoni: