Jumanne, 20 Mei 2025

Yeye peke yake akanyagaye mawimbi ya bahari!


Ayubu 9:8-12 “Ambaye peke yake ni mwenye kuzitandika mbingu, Na kuyakanyaga mawimbi ya bahari. Yeye afanyaye hizo nyota za Dubu, na Orioni, na hicho Kilimia, Na makundi ya nyota ya kusini.Atendaye mambo makuu yasiyotafutikana; Naam, mambo ya ajabu yasiyohesabika. Tazama, yuaenenda karibu nami, nisimwone; Tena yuapita kwenda mbele, nisimtambue. Tazama, yuakamata, ni nani awezaye kumzuia? Ni nani awezaye kumwuliza, Wafanya nini?



Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa muujiza wa Bwana Yesu kutembea juu ya mawimbi ya bahari ya Galilaya haukuwa muujiza wa kawaida kama wengi tunavyodhani, muujiza huu wa aina yake kati ya miujiza mingi aliyoifanya Bwana Yesu huu umerokodiwa na injili tatu zisizo fanana kwa kusudi maalumu


Mathayo 14:22-33 “Mara akawalazimisha wanafunzi wake wapande chomboni na kutangulia mbele yake kwenda ng'ambo, wakati yeye alipokuwa akiwaaga mkutano.Naye alipokwisha kuwaaga makutano, alipanda mlimani faraghani, kwenda kuomba. Na kulipokuwa jioni, alikuwako huko peke yake. Na kile chombo kimekwisha kufika katikati ya bahari, kinataabika sana na mawimbi; maana upepo ulikuwa wa mbisho. Hata wakati wa zamu ya nne ya usiku Yesu akawaendea, akienda kwa miguu juu ya bahari. Wanafunzi walipomwona akienda juu ya bahari, wakafadhaika, wakisema, Ni kivuli; wakapiga yowe kwa hofu. Mara Yesu alinena, akawaambia, Jipeni moyo ni mimi; msiogope. Petro akamjibu, akasema, Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji. Akasema, Njoo. Petro akashuka chomboni, akaenda kwa miguu juu ya maji, ili kumwendea Yesu. Lakini alipouona upepo, akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe, akisema, Bwana, niokoe. Mara Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka? Nao walipopanda chomboni, upepo ulikoma. Nao waliokuwamo ndani ya chombo wakamsujudia, wakisema, Hakika wewe u Mwana wa Mungu.”


Marko 6:45-52 “Mara akawalazimisha wanafunzi wake wapande mashuani, watangulie kwenda ng'ambo hata Bethsaida, wakati yeye alipokuwa akiwaaga mkutano. Hata alipokwisha kuagana nao akaenda zake mlimani kuomba. Na kulipokuwa jioni mashua ilikuwa katikati ya bahari, na yeye yu peke yake katika nchi kavu. Akawaona wakitaabika kwa kuvuta makasia, kwa maana upepo ulikuwa wa mbisho; hata ilipopata kama zamu ya nne ya usiku akawaendea, akitembea juu ya bahari; akataka kuwapita. Nao walipomwona anatembea juu ya bahari, walidhani ya kuwa ni kivuli, wakapiga yowe, kwa kuwa wote walimwona, wakafadhaika. Mara akasema nao, akawaambia, Changamkeni; ni mimi, msiogope. Akapanda mle chomboni walimo; upepo ukakoma; wakashangaa sana mioyoni mwao; kwa maana hawakufahamu habari za ile mikate, lakini mioyo yao ilikuwa mizito.”


Yohana 6:16-21 “Hata ilipokuwa jioni wanafunzi wake wakatelemka baharini wakapanda chomboni, wakaanza kuivuka bahari kwenda Kapernaumu. Nako kumekwisha kuwa giza, wala Yesu hajawafikia. Na bahari ikaanza kuchafuka kwa kuvuma upepo mkuu. Basi wakavuta makasia kadiri ya maili tatu nne, wakamwona Yesu anakwenda juu ya bahari na kukikaribia chombo; wakaogopa.Naye akawaambia, Ni mimi, msiogope. Basi wakataka kumpokea chomboni; na mara hiyo chombo kikaifikilia nchi waliyokuwa wakiiendea.”


Muujiza huu wa Yesu Kutembea juu ya mawimbi ya bahari kimsingi ulikuwa ni muujiza maalumu wa kujifunua kwa wanafunzi wake mamlaka kubwa aliyokuwa nayo Yesu dhidi ya majanga ya asili na uweza wake wa kiungu, na ndio maana muujiza huu haukufanyika mbele ya watu wote isipokuwa wanafunzi wake peke yao kimsingi muujiza huu ulikuwa unamfunua Yesu kwa wanafunzi wake kwamba yeye ana upekee wa aina yake!


1.       Uwezo wake wa kiungu – Wanafunzi wake wote waliorekodi muujiza huu hawakuacha kutaja neno “NI MIMI” Msiogope, Yesu Kristo alitumia mara kadhaa neno NI MIMI au mimi ndimi moja kwa moja akijifunua kwa mamlaka na uweza wa kiungu sawa na mwokozi aliyemtokea Musa tayari kwa wokovu wa wana wa Israel kutoka utumwani kule Misri neno NI MIMI lilitumiwa na Mungu kujitambulisha yeye ni  nani wakati Musa alipopata wasi wasi kuhusu wovovu wa wana wa Israel mbele za Farao.


Kutoka 3:13-15 “Musa akamwambia Mungu, Tazama, nitakapofika kwa wana wa Israeli, na kuwaambia, Mungu wa baba zenu amenituma kwenu; nao wakaniuliza, Jina lake n'nani? Niwaambie nini? Mungu akamwambia Musa, MIMI NIKO AMBAYE NIKO; akasema, Ndivyo utakavyowaambia wana wa Israeli; MIMI NIKO amenituma kwenu. Tena Mungu akamwambia Musa, Waambie wana wa Israeli maneno haya, BWANA, Mungu wa baba zenu, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amenituma kwenu; hili ndilo jina langu hata milele, nalo ni kumbukumbu langu hata vizazi vyote.”

 

Kwa kujitambulisha hivyo kwa wanafunzi wake Yesu ni sawa tu na anarudia namna Mungu alivyojitambulisha kwa Musa MIMI NDIMI, NI MIMI “I AM WHO I AM” jina hilo tafasiri yake ndio YHWH au Yahweh ambalo maana yake ni Mungu mwenye kujitosheleza na wa milele ni mwokozi kwa hiyo Yesu aliposema NI MIMI msiogope alikuwa anafunua mamlaka yake kamili ya uungu kwa wanafunzi wake

 

Kuna nguvu kubwa ya kupita kawaida nguvu ya uungu yenye uwezo zaidi ya wanadamu wa kawaida Yesu alipojitambulisha NI MIMI au MIMI NDIMI mwanafunzi wa Yesu Yohana katika injili yake anaonyesha jinsi majeshi ya wakamataji, yaani kikosi kilichotumwa kumkamata Yesu kilivyopata misuko suko mkubwa wakati Yesu alipojitambulisha kwao kwa usemi huo

 

Yohana 18:4-6 “Basi Yesu, hali akijua yote yatakayompata, akatokea, akawaambia, Ni nani mnayemtafuta? Wao wakamjibu, Ni Yesu Mnazareti. Yesu akawaambia, Ni mimi. Yuda naye aliyemsaliti alikuwa amesimama pamoja nao. Basi alipowaambia, Ni mimi, walirudi nyuma, wakaanguka chini.”

 

2.       Uweza wake juu ya maswala ya asili – Kristo Yesu alijifunua kupitia muujiza huu kuwa yeye anazo nguvu juu ya uumbaji na maswala yote ya asili, (Power over nature) kila janga la asili iwe ni matetemeko, iwe ni radi, iwe ni dhuruba, uwe ni upepo au bahari iliyochafuka Yesu ana uweza juu ya majanga ya asili, anauwezo wa kufanya yale yasiyowezekana kibinadamu ama yale yasiyofikirika injili zinaelezea kuwa mara Yesu alipopanda chomboni upepo na dhruruba vilikoma.

 

Mathayo 14:32-33 “Nao walipopanda chomboni, upepo ulikoma. Nao waliokuwamo ndani ya chombo wakamsujudia, wakisema, Hakika wewe u Mwana wa Mungu.”

 

Marko 6:49-51 “Nao walipomwona anatembea juu ya bahari, walidhani ya kuwa ni kivuli, wakapiga yowe, kwa kuwa wote walimwona, wakafadhaika. Mara akasema nao, akawaambia, Changamkeni; ni mimi, msiogope. Akapanda mle chomboni walimo; upepo ukakoma; wakashangaa sana mioyoni mwao;”

 

3.       Kutimiza unabii na kufunua uungu wake – Ayubu aliwahi kutabiri miaka 2,000 kabla ya Yesu kuwa ni Mungu peke yake mwenye kuzitandaza mbingu na kukanyaga mawimbi ya bahari, kwa hiyo kimsingi Yesu Kristo alikuwa anaufanya muujiza huu na maalumu alikuwa akitimiza unabii huu, kitabu cha Ayubu kiliandikwa yapata miaka 1000 kabla ya Yesu  na Yesu aliishi mnamo karne ya kwanza na kwa sababu hiyo kutoka Ayubu mpaka kuzaliwa kwa Yesu Kristo ilikuwa ni zaidi ya miaka 2,000. wanafunzi wa Yesu na watu wengine bila shaka walikuwa wamewahi kuyasoma maneno ya Ayubu na hivyo Kristo alipofanya muujiza huu walishangazwa sana na kujiuliza kuwa huyu ni mtu wa namna gani? Hata Pepo na bahari zamtii?

 

Mathayo 8:26-27 “Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga, enyi wa imani haba? Mara akaondoka, akazikemea pepo na bahari; kukawa shwari kuu. Wale watu wakamaka wakisema, Huyu ni mtu wa namna gani hata pepo na bahari zamtii?                 

 

Ayubu 9:8-12 “Ambaye peke yake ni mwenye kuzitandika mbingu, Na kuyakanyaga mawimbi ya bahari. Yeye afanyaye hizo nyota za Dubu, na Orioni, na hicho Kilimia, Na makundi ya nyota ya kusini. Atendaye mambo makuu yasiyotafutikana; Naam, mambo ya ajabu yasiyohesabika. Tazama, yuaenenda karibu nami, nisimwone; Tena yuapita kwenda mbele, nisimtambue.Tazama, yuakamata, ni nani awezaye kumzuia? Ni nani awezaye kumwuliza, Wafanya nini?

 

Andiko hilo linafunua kuwa ni Mungu peke yake azitandaye mbingu na kukanyaga mawimbi ya bahari, kwa hiyo ni Dhahiri na ni wazi kuwa kitendo cha Yesu Kristo kutembea juu ya maji kwa kuyakanyaga mawimbi ya bahari alikuwa akiutimiza unabii huu, kwa hiyo muujiza unatufunulia ya kuwa Yesu hakuwa wa kawaida tu bali alikuwa na mamlaka ya uungu ndani yake, Bahari ilimtii, kanuni za kisayansi zilivunjika na Yesu alitembea juu ya maji, alikemea upepo na bahari na zikamtii.


Mambo ya Msingi ya kujifunza:

Kwanini Kristo anajifunua hivi kwa wanafunzi wake na kwa watu wote leo? Yesu hajifunui hivi kwa faida yake tu kwamba awe na sifa za uungu, Yesu anajifunua hivi kwetu leo ili kwamba wote tupate kumuamini kuwa yeye yuko pamoja nasi katika aina yoyote ya dhuruba, unapomuamini Yesu kwa kumfanya kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako kumbuka muujiza huu haukuwa wa watu wote huu ulikuwa ni maalumu kwa wanafunzi wake ni muujiza maalumu kwa wale wanaomuamini yeye  kwa hiyo kwanza tunafunuliwa ya kuwa hatuko peke yetu, Wakati wanafunzi walipokuwa wakisumbuliwa na dhuruba na kujifikiri ya kuwa wako peke yao Yesu Kristo aliwatokea na kuingilia kati masumbufu yao, mashaka yao na wasiwasi wao, Leo tunajifunza ya kuwa muumba ulimwengu, mwenye nguvu juu ya majanga yote ya asili yeye ambaye Peke yake anaweza kukanyaga mawimbi ya bahari yuko pamoja nasi na atatutokea na atatuliza dhoruba zote zinazotukabili katika maisha yetu katika namna iliyo nyepesi sana na ya kushangaza, kwa hiyo hatuwezi kuogopa linapotokea janga la aina yoyote yeye ni kimbilio letu na nguvu zetu ona:-

Zaburi 46:1-3 “Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso. Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari. Maji yake yajapovuma na kuumuka, Ijapopepesuka milima kwa kiburi chake.”

Tunajifunza kuwa tunapaswa kumwangalia yeye kwa imani bila kuona shaka, Petro alipomtambua Yesu aliyekuwa anatembea juu ya dhuruba na kuomba atembee juu ya dhuruba Bwana alimpa kibali na aliweza, lakini pale alipoona shaka na kuanza kuangalia dhuruba mara alianza kuzama, tunajikumbusha au kukumbushwa kuwa wakati wa changamoto zozote za maisha ni lazima tuendelee kumtazama Yesu, Ni lazima tumwamini na kutambua ya kuwa yeye peke yake anaweza kutusaidia na kuwa tunapoliitia jina lake atatushika mkono

Waebrania 12:2- “tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu. Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu.”

Waebrania 10:38-39 “Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani; Naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye.Lakini sisi hatumo miongoni mwao wasitao na kupotea, bali tumo miongoni mwa hao walio na imani ya kutuokoa roho zetu.”

Tunapomtazama Yesu ni muhimu kufahamu kuwa hakuna kuzimia na hakuna kuchoka wala kukata tamaa au kuingia mashaka, tunajifunza uweza mkubwa na mamlaka kubwa ya Yesu Kristo ili kwamba tupate kuamini na tukiisha kumwamini hakuna mtu awaye yote atakayetahayarika, Kama  Bwana wetu Yesu Kristo aliweza kupita sehemu hatarishi na akavuka salama tunajifunza kuwa sisi nasi tukimwangalia yeye tutapita sehemu hatarishi pamoja naye na tutavuka salama, maji na radi na vilindi vya bahari na dhuruba za kila namna vyote vina muogopa Mungu na kwa sababu hiyo hakuna jaribu liltakaloweza kusimama mbele yako lisishughulikiwe kwa jina la Yesu Kristo aliye hai.

Zaburi 77:16-20 “Ee Mungu, yale maji yalikuona, Yale maji yalikuona, yakaogopa. Vilindi vya maji navyo vikatetemeka, Mawingu yakamwaga maji. Mbingu nazo zikatoa sauti, Mishale yako nayo ikatapakaa. Sauti ya radi yako ikawa katika kisulisuli; Umeme uliuangaza ulimwengu. Nchi ilitetemeka na kutikisika; Njia yako ilikuwa katika bahari. Na mapito yako yalikuwa katika maji makuu; Hatua zako hazikujulikana. Uliwaongoza watu wako kama kundi, Kwa mkono wa Musa na Haruni.”

Hitimisho!

Leo nakutangazia kuwa  haijalishi unapitia changamoto ya aina gani, dhuruba ya aina gani, upepo wa aina gani, haijalishi madaktari wamekuambia nini, haijalishi kuwa una rufaa mkononi kwenda hospitali kubwa, haijalishi mapigo yako ya moyo yako juu au chini, haijalishi umevamiwa na virusi vya korona, au ukimwi, haijalishi vipimo vikubwa vimekuja na matokeo magumu kiasi gani, haijalishi una maadui waliojipanga kwa kiwango cha kukutishia, haijalishi unaogopa nini,  haijalishi una madeni ya kausha damu, na mikopo umiza, haijalishi wamekodi mganga gani akuroge, haijalishi kuna vikao gani vya majungu vimekukalia, haijalishi fitina na majungu, na mizengwe unayowekewa nakutangazia ya kuwa yuko yeye akanyagaye mawimbi, kila aina ya wimbi katika maisha yako litakanyagwa na kutulia tuli katika jina la Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai, usiogope, usione shaka, usitikisike, usisitesite, usitetemeke, usikate tamaa, usilie, usiogope na kuwaza itakuwaje nakutangazia ya kuwa yuko akanyagae mawimbi ya bahari kila wimbi linalopita katika maisha yako Yesu atalikanyaga na litatulia kimya kwake yeye aliyezifanya mbingu na nchi katika jina la Yesu. 

“Kumbuka ni Yeye peke yake akanyagaye mawimbi ya bahari! Wokovu una yeye Mungu wetu!”

Tufani inapovuma

sana moyoni mwangu!

Huona pa kujificha 

Mkononi mwa Mungu.

 

Hunificha, hinificha, Adui hatanipata, Hunificha, hunificha mkononi mwake

 

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Hakuna maoni: