1Samuel 17:32-36 “Daudi akamwambia Sauli,
Asizimie moyo mtu ye yote kwa ajili ya huyu; mimi mtumishi wako nitakwenda
kupigana na Mfilisti huyu. Sauli akamwambia Daudi, Huwezi wewe kumwendea
Mfilisti huyu upigane naye; maana wewe u kijana tu; na huyu ni mtu wa vita
tangu ujana wake. Daudi akamwambia Sauli, Mtumishi wako alikuwa akichunga
kondoo za baba yake, na alipokuwa akija simba, au dubu, akamkamata mwana-kondoo
wa lile kundi, mimi hutoka nikamfuata, nikampiga, nikampokonya kinywani mwake;
na akinirukia, humshika ndevu zake, nikampiga, nikamwua. Mtumishi wako alimwua
simba na dubu pia; na huyu Mfilisti asiyetahiriwa atakuwa kama mmoja wao, kwa
sababu amewatukana majeshi ya Mungu aliye hai.”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa katika
maisha haya mara nyingi mimi na wewe kama wanadamu huwa tunakutana na
changamoto mbali mbali ambazo nyinginezo zinaweza kutuvunja moyo na kutukatisha
tamaa, sio hivyo tu pia zinaweza kutuogopesha na kutufanya tupoteze kujiamini
au hata kuamini kuwa Mungu anaweza kutusaidia tena, Katika Israel wakati fulani
waliwahi kukutana na hali kama hii unayoipitia wewe, walikuwa katika vita na
wafilisti, na katika jeshi la wafilisti alijitokeza mtu mmoja mkubwa sana
mwenye nguvu na mwenye kutisha ambaye alizungumza maneno ya propaganda za
kivita na kuwatia hofu sana wana wa Israel kiasi ambacho jeshi lote la Israel
wakiongozwa na Sauli mfalme wao waliogopa na kuzimia moyo, Neno “Asizimie” katika Lugha ya kiebrania
linasomeka kama “Nรขphal” ambalo kwa kiingereza ni “fall” limetumika hivyo mara 318 likimaanisha kuanguka, au kupoteza
matumaini, au kushuka chini kutoka katika hali yake ya awali, kwa Kiswahili
kuvunjika moyo yaani asivunjike moyo mtu awaye yote unapokutana na changamoto.
1Samuel 17:1-11 “Wakati huo Wafilisti
walikusanya majeshi yao kwa vita, nao wakakusanyika huko Soko, ulio mji wa
Yuda, wakatua kati ya Soko na Azeka, katika Efes-damimu. Naye Sauli na watu wa
Israeli wakakusanyika, wakatua katika bonde la Ela, nao wakapanga vita juu ya
hao Wafilisti. Wafilisti wakasimama juu ya mlima upande huu, na Waisraeli
wakasimama juu ya mlima upande huu, napo palikuwa na hilo bonde katikati. Ndipo
akatoka shujaa katika kambi ya Wafilisti, aliyeitwa Goliathi, wa Gathi, ambaye
urefu wake ulikuwa mikono sita na shibiri moja. Alikuwa na chapeo ya shaba
kichwani, tena amevaa darii ya shaba; na uzani wake ile darii ya shaba ulikuwa
shekeli elfu tano za shaba. Tena amevaa mabamba ya shaba miguuni mwake, naye
alikuwa na mkuki wa shaba kati ya mabega; yake. Na mti wa fumo lake ulikuwa
kama mti wa mfumaji; na kichwa cha mkuki wake kilikuwa shekeli mia sita za
chuma uzito wake; na mtu aliyemchukulia ngao yake akamtangulia. Naye akasimama,
akawapigia kelele majeshi ya Israeli akawaambia, Mbona mmetoka kupanga vita?
Je! Mimi si Mfilisti, na ninyi si watumishi wa Sauli? Jichagulieni mtu,
akanishukie mimi. Kama akiweza kupigana nami na kuniua, sisi tutakuwa watumwa
wenu; nami nikimshinda yeye na kumwua, ninyi mtakuwa watumwa wetu, na
kututumikia. Yule Mfilisti akasema, Nayatukana leo majeshi ya Israeli; nipeni
mtu tupigane. Basi Sauli na Israeli wote waliposikia maneno hayo ya Mfilisti,
wakafadhaika na kuogopa sana.”
Kutokana na maneno ya shujaa huyo
wa wafilisti mwenye kutisha sana Israel waliogopa na kuzimia moyo, ni jambo la
kawaida wakati mwingine kwamba linapotokea jambo la kutisha kutokana na
propaganda za kishetani huwa tunasahau uweza wa Mungu na ukuu wake na kuitazama
ile changamoto huku tukijiuliza kama tunaweza kutokaje katika changamoto hiyo,
unajiuliza nitatoboa kweli au safari hii ndio nafariki, nitatokaje katika
ugonjwa huu, nawezaje kukabiliana na deni hili kubwa namna hii, aibu
inakaribia, nawezaje kutoka katika matatizo haya na kwa sababu ya utisho wa
hali inayotuzunguka ni rahisi kwetu kuvunjika moyo au kuzimia moyo, Kijana
mdogo sana katika Israel Daudi alisimama kwa ujasiri na kuwatia moyo taifa zima
ya kuwa asizimie moyo mtu! Kwani yeye atapambana na hali inayowakabili kwa jina
la Mungu wa Israel!. Leo kila changamoto unayokabiliana nayo, kila ukuta
unaosimama kama kikwazo katika maisha yako, kila mlima na jaribu, na mateso, na
ugonjwa na majini na mapepo na nguvu za giza zinazosimama kama changamoto
katika maisha yako ambazo zimekufanya ukazimia moyo kwa jina la Yesu Kristo
mwana wa Mungu aliye hai tunakwenda kukabiliana nazo na kuzisambaratisha kabisa
haleluyaa Asizimie moyo mtu!.Tutajifunza somo hili Asizimie Moyo mtu kwa
kuzuingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Sababu za
watu kuzimia moyo!
·
Asizimie
moyo mtu!
·
Kwanini
asizimiye moyo mtu!
Sababu za watu kuzimia moyo!
Ni ukweli uliokuwa wazi kuwa
Israel kama ilivyo kwa watu wengine walikuwa wamevunjika moyo na kuzimia kabisa
kwa woga, mazingira waliokuwa wanakabiliana nayo, yalikuwa ni magumu na yenye
kuogopesha sana, propaganda za kivita zilikuwa zimewatia hofu na kuwachosha,
Goliath alikuwa akijitokeza kila siku asubuhi na jioni kwa siku 40 akiwatukana
na kuwatisha sana, jambo lilolopelekea jeshi zima na mashujaa wakubwa wakiwepo
kaka zake Daudi na mfalme Sauli kutishika na kufadhaika sana, Goliathi
aliyatukana majeshi ya Israel waziwazi, hadharani kila mtu akishuhudia!
1Samuel 17:10-16 “Yule Mfilisti akasema,
Nayatukana leo majeshi ya Israeli; nipeni mtu tupigane. Basi Sauli na Israeli
wote waliposikia maneno hayo ya Mfilisti, wakafadhaika na kuogopa sana. Basi
Daudi alikuwa mwana wa yule Mwefrathi, wa Bethlehemu ya Yuda, aliyeitwa jina
lake Yese; naye huyo alikuwa na wana wanane; na yeye mwenyewe alikuwa mzee siku
za Sauli, na mkongwe miongoni mwa watu. Nao wale wana watatu wa Yese waliokuwa
wakubwa walikuwa wamefuatana na Sauli kwenda vitani, na majina ya hao wanawe
watatu waliokwenda vitani ni haya, mzaliwa wa kwanza Eliabu, na wa pili wake
Abinadabu, na wa tatu Shama. Naye huyo Daudi alikuwa mdogo wa wote; na hao
watatu waliokuwa wakubwa wakafuatana na Sauli. Basi Daudi alikuwa akienda kwa
Sauli na kurudi ili awalishe kondoo za baba yake huko Bethlehemu. Naye yule
Mfilisti hukaribia asubuhi na jioni, akajitokeza siku arobaini.”
Sisi nasi katika maisha yetu tunaweza
kufadhaika na kutishika na hata kuvunjika moyo kutokana na uhalisia wa changamoto,
ni ukweli uliokuwa wazi kuwa Golitahi lilikuwa jitu kubwa lenye nguvu na uzoefu
wa kivita, na jeshi lote la Israel lilimuogopa, yako mambo ambayo yakikupata
wewe mwenyewe na hata wataalamu wanaweza kukubaliana kuwa ni jambo zito na
kubwa, ikiwa una ukimwi, ikiwa una sukari, ikiwa umepatwa na kiharusi, ikiwa
una kansa ya damu, ikiwa una changamoto ya ini, kansa, figo, changamoto za
mfumo wa fahamu, umeme katika mwili, moyo na kadhalika ni magonjwa ya kutisha
ambayo hata wataalamu wa afya wenyewe wanayaogopa na una historia yake namna na
jinsi yalivyoua watu mbalimbali kwenye jamii yako, familia yako na hata
majirani, changamoto za mikopo umiza, madeni ya aibu, kufilisika, hasara za
namna mbalimbali, kutapeliwa fedha nyingi, kuporomoka kwa biashara, hali mbaya
ya kiuchumi, kutokujitosheleza kwa mahitaji mbalimbali na umasikini wa kutisha
vinaweza kuwa sababu ya kuzimia moyo, Sio hivyo tu maneno unayoyasikia kutoka
upande wa upinzani au wa adui yako na wakati mwingine wanaweza hata kusema
kuhusu Mungu wako kwamba tuone kama Mungu wake anaweza kumsaidia hivyo vyote
vinaweza kukufanya ukazimia moyo, wakati unapokuwa katika changamoto kali na
ngumu sana maneno ya adui zako yanaweza kukuumiza sana, na hata maneno ya wale
watu usiowatarajia, kama wapendwa wenzetu, Yesu alipokuwa msalabani adui zale
walisema pia kuhusu Mungu kwamba amemtegemea Mungu na amwokoe sasa Msalabani
nasi tutamwamini maneno ya kuumiza!
Mathayo 27:40-43. “Ewe mwenye kulivunja
hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe nafsi yako; ukiwa ndiwe Mwana wa
Mungu, shuka msalabani.Kadhalika na wale wakuu wa makuhani wakamdhihaki pamoja
na waandishi na wazee, wakisema, Aliokoa wengine, hawezi kujiokoa mwenyewe. Yeye
ni mfalme wa Israeli; na ashuke sasa msalabani, nasi tutamwamini. Amemtegemea
Mungu; na amwokoe sasa, kama anamtaka; kwa maana alisema, Mimi ni Mwana wa
Mungu.”
Hatupaswi kamwe kukosa imani na
kuvunjika moyo au kuzimia moyo wala kuyatazama mazingira na badala yake
tunapaswa kumwangalia Mungu ambaye ni mkubwa kuliko changamoto yako, Daudi kamwe
hakukubali kuwa na aibu ya kitaifa na wala hakukubali Mungu wake adhalilike na
ndugu zake waaibike, akiwa amejaaa Imani, uzoefu, ujuzi kuhusu Mungu na ujasiri
mkubwa ambao wengi walikuwa wameupoteza yeye alisema atapambana na hali hiyo na
kwa sababu hiyo asizimie moyo mtu, usizimie moyo kwaajili ya ugonjwa wako,
usizimie moyo kwaajili ya adui zako, usizimie moyo kwaajili ya umasikini wako,
usizimie moyo kwaajili ya changamoto na matatizo ya kifamilia, haijalishi adui
anatisha kwa kiwango gani sisi tutamjia kwa jina la Bwana Mungu wa Israel aliye
hai.
Asizimie moyo mtu!
Wakati kila mtu akiwa ameingiwa
na hofu fadhaa na kukata tamaa au kuzimia Moyo, Daudi alikuwa na mtazamo
tofauti na wengine Yeye alikuwa amejifunza kuwa Mungu ni mkubwa kuliko
changamoto ya aina yoyote ile, alikuwa amejifunza na kupata uzoefu na shuhuda
namna na jinsi Mungu alivyompa ushindi dhidi ya
wanyama wakali wenye nguvu kuliko binadamu wanyama kama Dubu, Simba na
kadhalika alitambua kuwa Mungu alikuwa pamoja naye hata alipokuwa akiwachunga
kondoo wa baba yake na kwa sababu hiyo Golitahi kwake lilikuwa ni jambo dogo
sana wala sio la kufadhaisha mtu na hivyo aliwapa tumani watu wote pamoja na
mfalme Asizimie moyo mtu!
1Samuel 17:34-37 “Daudi akamwambia Sauli,
Mtumishi wako alikuwa akichunga kondoo za baba yake, na alipokuwa akija simba,
au dubu, akamkamata mwana-kondoo wa lile kundi, mimi hutoka nikamfuata,
nikampiga, nikampokonya kinywani mwake; na akinirukia, humshika ndevu zake,
nikampiga, nikamwua. Mtumishi wako alimwua simba na dubu pia; na huyu Mfilisti
asiyetahiriwa atakuwa kama mmoja wao, kwa sababu amewatukana majeshi ya Mungu
aliye hai. Daudi akasema, Bwana aliyeniokoa na makucha ya simba, na makucha ya
dubu, ataniokoa na mkono wa Mfilisti huyu. Sauli akamwambia Daudi, Enenda, na
Bwana atakuwa pamoja nawe.”
Daudi aliamini kuwa sio kwa nguvu
za kibinadamu atamkabili Goliath lakini ni kwa nguvu za Mungu na kwa msaada wa
Mungu, alikumbuka shuhuda za ukuu wa Mungu na matendo yake na uaminifu wake,
alitambua jinsi jina la Mungu linavyopaswa kutakaswa na kutukuzwa na alijua ya
kuwa kwa jina hilo hakuna kinachoweza kusimama, alifahamu ya kuwa Mungu hawezi
kutukanwa wala kudhalilishwa na jeuri na kiburi cha kibinadamu na kisha
akakubali, Daudi alitambua kuwa kutukanwa kwa majeshi ya Mungu aliye hai ni
kutukanwa kwa Mungu kwa hiyo alitaka kuitetea heshima ya Mungu, Daudi alitambua
kuwa ushindi wake ni ushindi wa kitaifa na sio wa mtu mmoja na kuwa kushindwa
kwa Goliathi ni kushindwa kwa wafilisti wote, Ni ukweli uliowazi katika ulimwengu
wa roho vita ya Daudi na Goliati ilikuwa inawakilisha vita ya Yesu Kristo na
Shetani, yule atakayeshindwa atakuwa mtumwa wa yule atakayeshindwa na watu wake
na yule atakayeshinda atatawala yeye na watu wake kila mtu aliyeokoka ni
mshindi kupitia ushindi wa Yesu Kristo, wakati Goliathi akiwa na kofia ya chuma
na mabamba ya chuma kila mahali Daudi yeye hakuwa na kizuizi chochote na
alikuwa na silaha laini yaani manati-kombeo na mawe matano tu laini
1Samuel 17:45-47.”Ndipo Daudi akamwambia
yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi
ninakujia wewe kwa jina la Bwana wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli
uliowatukana. Siku hii ya leo Bwana atakuua mkononi mwangu, nami nitakupiga, na
kukuondolea kichwa chako, nami leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi
mizoga ya majeshi ya Wafilisti, ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko Mungu
katika Israeli. Nao jamii ya watu wote pia wajue ya kwamba Bwana haokoi kwa
upanga wala kwa mkuki; maana vita ni vya Bwana, naye atawatia ninyi mikononi
mwetu.”
Wakati Goliathi alikuwa akitema
propaganda tu na vitisho kwa kujiamini kwa kiburi na majivuno, Daudi alikuwa
akizitamka shuhuda za Mungu na ukweli wa neno lake Mungu na uweza wake, ni ukweli
ulio wazi kuwa siku ile Daudi alimpiga Goliathi na kwa kutumia upanga wa
Goliathi mwenyewe alikata kichwa chake, tukio hili liliwapa nguvu Israel na
waliwakimbiza wafilisti na kuwachinja kama walivyotaka na kujikusanyia nyara:-
1Samuel 17:48-52 “Ikawa, hapo Mfilisti
alipojiinua, akaenda akamkaribia Daudi, ndipo Daudi naye akapiga mbio,
akalikimbilia jeshi ili akutane na yule Mfilisti. Daudi akatia mkono wake
mfukoni, akatwaa humo jiwe moja, akalitupa kwa kombeo lake, akampiga Mfilisti
katika kipaji cha uso; jiwe hilo likamwingilia kipajini, akaanguka chini
kifudifudi. Hivyo Daudi akamshinda yule Mfilisti kwa kombeo na jiwe, akampiga
Mfilisti, akamwua; walakini Daudi hakuwa na upanga mkononi mwake. Ndipo Daudi
akapiga mbio, akasimama juu ya Mfilisti, akautwaa upanga wake, akaufuta alani
mwake, akamwua, akamkata kichwa kwa upanga huo. Nao Wafilisti walipoona ya kuwa
shujaa wao amekufa, wakakimbia. Nao watu wa Israeli na wa Yuda wakainuka, na
kupiga kelele, nao wakawafuata Wafilisti mpaka ufikapo Gathi, na mpaka malango
ya Ekroni. Nao majeruhi wa Wafilisti wakaanguka kando ya njia iendayo Shaarimu,
mpaka Gathi, na mpaka Ekroni.”
Kwanini asizimiye moyo mtu!
Daudi alikuwa na ufahamu kuwa
ushindi wake hautokani na yeye mwenyewe bali ushindi wake unatokana na Mungu,
sisi nasi hatuna budi kufahamu kwamba ushindi wetu unapatikana kupitia Yesu Kristo
ambaye alishinda kifo na mauti, ushindi wowote tulio nao na tutakaokuwa nao ni
ushindi unaotokana na ushindi wake Kristo Yesu mwana wa Daudi.
1Wakorintho 15:57 “Lakini Mungu na
ashukuriwe atupaye kushinda kwa Bwana wetu Yesu Kristo.”
Maandiko yanatukumbusha tu kuwa
hakuna changamoto kubwa kuliko Mungu wetu, kila mtu aliyeokolewa na
anayemtegemea Mungu anapaswa kumtegemea Mungu na kumfanya kuwa ngao yake na
kinga yake, tunapaswa kuwa na ujasiri na kuacha kupoteza matumaini, hatupaswi
kamwe kuzimia moyo kama tumemfanya Bwana kuwa ngao yetu, hatupaswi kulia wala
kufadhaika maana Mungu ndiye wokovu wetu, na ngome yetu na hakuna wa
kutukaribia wala kutudhuru vyovyote vile!
Zaburi 27:1-3 “Bwana ni nuru yangu na
wokovu wangu, Nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani?
Watenda mabaya waliponikaribia, Wanile nyama yangu, Watesi wangu na adui zangu,
Walijikwaa wakaanguka. Jeshi lijapojipanga kupigana nami, Moyo wangu
hautaogopa. Vita vijaponitokea, Hata hapo nitatumaini.”
Maandiko yanatukumbusha kuwa
Mungu hutumia mambo manyonge sana, wakati ambapo Goliath anaonekana kuwa na
silaha bora, mkuki mkubwa na uzoefu mkubwa vitani, huku mwili wake umezingirwa
na mambamba ya shaba Daudi alikuwa ni kijana mdogo, mzuri macho mekundu lakini
alijikinga kwa jina la Mungu na kumfanya Mungu kuwa tumaini lake, hii
inatukumbusha kuwa Mungu anaweza kutumia chochote na kumtumia mtu yeyote bila
kujali hali yake, historia yake na muonekano wake wa nje, unyonge wake au
kupuuzwa kwake, Mungu hutumia vilivyodharaulika!
1Wakorintho 1:26-29 “Maana, ndugu zangu,
angalieni mwito wenu, ya kwamba si wengi wenye hekima ya mwilini, si wengi
wenye nguvu, si wengi wenye cheo walioitwa; bali Mungu aliyachagua mambo
mapumbavu ya dunia awaaibishe wenye hekima; tena Mungu alivichagua vitu dhaifu
vya dunia ili aviaibishe vyenye nguvu; tena Mungu alivichagua vitu vinyonge vya
dunia na vilivyodharauliwa, naam, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile
vilivyoko; mwenye mwili awaye yote asije akajisifu mbele za Mungu.”
Maandiko yanatukumbusha kuwa
Mungu ni mwaminifu na kuwa tunapokabiliana na changamoto za aina yoyote katika
maisha yetu na tukumbuke namna na jinsi alivyotusaidia katika mambo mengine kumbuka
matendo yake ya kale na hii itamuimarisha kila mmoja wetu kujua kuwa Mungu yule
yule asiyebadilika aliyewasaidia baba zetu katika vita zao atajitokeza tena kwa
namna nyingine kutusaidia
Zaburi 77:11-14 “Nitayakumbuka matendo ya
Bwana; Naam, nitayakumbuka maajabu yako ya kale. Pia nitaitafakari kazi yako
yote; Nitaziwaza habari za matendo yako. Ee Mungu, njia yako i katika
utakatifu; Ni nani aliye mungu mkuu kama Mungu? Wewe ndiwe Mungu ufanyaye
maajabu; Uliudhihirisha uweza wako kati ya mataifa.”
Ee Bwana usimuache msomaji wangu,
na msikilizaji wangu na kila mtu duniani anayekutegemea wewe, usimwache
akazimia moyo wakati wa taabu yake lakini umpe moyo wa ujasiri kama Daudi na
nutupe ushindi katika vita zetu za maisha katika jina la Yesu Kristo amen!
Na. Rev Innocent Samuel Kamote.
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!