Yoshua 6:22-25. “Naye Yoshua akawaambia
wale wanaume wawili walioipeleleza nchi, Ingieni katika nyumba ya yule kahaba,
mkamtoe huyo mwanamke mwenyewe na vitu vyote alivyo navyo, kama mlivyomwapia.
Basi wale vijana wapelelezi wakaingia, wakamtoa Rahabu, na baba yake, na mama
yake, na ndugu zake, na vitu vyote walivyokuwa navyo, wakawatoa na jamaa zake
wote pia; wakawaweka nje ya matuo ya Israeli. Kisha wakauteketeza mji kwa moto,
na vitu vyote vilivyokuwa ndani yake; bali fedha, na dhahabu, na vyombo vya
shaba, na vya chuma, wakavitia katika hazina ya nyumba ya Bwana. Lakini Yoshua
akamhifadhi Rahabu, yule kahaba, na watu wa nyumba ya baba yake, na vitu vyote
alivyokuwa navyo; naye akakaa kati ya Israeli hata leo; kwa sababu aliwaficha
wale wajumbe aliowatuma Yoshua ili kuupeleleza mji wa Yeriko.”
Utangulizi:
Hakuna mtu mbaya sana, wala
hakuna mtu aliye mbali sana kiasi cha Rehema za Mungu kushindwa kumfikia na
kuokolewa, Haijalishi mtu ametoka wapi na amefanya nini, Mpango wa Mungu uko
pale pale kwamba yeye alikuja duniani kuwaokoa wenye dhambi na kwa sababu hiyo
hashindwi kumbadilisha yeyote na kumtumia katika mpango wake mkuu, kimsingi
Yesu Kristo ambaye ndiye mwokozi, hakuja duniani kuwaita watu wema bali alikuja
kuwaita wenye dhambi na kuokoa wale waliopotea.
Luka 5:30-32 “Ikawa Mafarisayo na waandishi
wao kuwanung'unikia wanafunzi wake, wakisema, Mbona mnakula na kunywa pamoja na
watoza ushuru na wenye dhambi? Yesu akajibu akawaambia, Wenye afya hawana haja
na tabibu, isipokuwa walio hawawezi. Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye
dhambi, wapate kutubu.”
Luka 19:9-10 “Yesu akamwambia, Leo wokovu
umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu.Kwa kuwa Mwana
wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.”
Katika maandiko tunauona moyo wa
Mungu, jinsi usivyokuwa na ubaguzi wala mipaka katika kuokoa, Mungu alimuingiza
Rahabu yule kahaba katika mpango wake wa ukombozi kwa sababu ya Imani yake
kwake, Yeye alimuamini Mungu na kuokolewa, licha ya kuwa na historia mbaya ya
maisha ya nyuma, tunajifunza kuwa Mungu anaweza kumuokoa yeyote bila kujali
historia ya maisha yake ya nyuma, kama alivyomuokoa Rahabu, Leo tutachukua muda
basi kujifunza kwa habari ya Rahabu na kujifunza namna na jinsi ambavyo Mungu
anaweza kukuokoa na wewe na kukuingiza katika mpango wake na makusudi yake ya
ukombozi bila kujali unatokea wapi.
Tutajifunza ujumbe huu Rahabu
yule kahaba kwa kuzingatia mambo ya muhimu yafuatayo!
·
Rahabu
alikuwa mtu wa namna gani?
·
Mambo
yaliyopelekea maisha ya Rahabu kubadilika
·
Kujifunza
kutoka kwa Rahabu yule kahaba
Rahabu alikuwa mtu wa namna gani?
Kwa mujibu wa maandiko Rahabu
aliyeishi mwaka wa 1481 Kabla ya
Kristo alikuwa ni mwanamke kahaba wa kabila za kikanaani aliyeishi katika jiji
la Yeriko, lililokuwako katika inchi ya ahadi, moja ya sifa kubwa
inayomtambulisha Rahabu ilikuwa ni pamoja na kazi yake ya ukahaba, Neno Kahaba
katika maandiko ya kiebrania linasomeka kama “Zânâh”
Neno hilo kwa kiingereza ni Harlot
au hookers au zona yaani Prostitute ambalo
tafasiri yake ni mtu anayejishughulisha na kuuza mwili wake ili kujipatia
fedha, au mtu anayetoa huduma ya tendo la ngono kwa kusudi la kujipatia fedha,
Kwa hiyo Rahabu alikuwa ni mtu anayefanya biashara hiyo, sio hivyo tu, Rahabu
pia alikuwa anamiliki nyumba ya wageni au nyumba ya kufanyia mapenzi maarufu
kama danguro, kwa hiyo ilikuwa rahisi kwa wageni wa kila aina kufikia nyumbani
mwake au kwenye nyumba yake ya wageni
Yoshua 2:1-3 “Yoshua, mwana wa Nuni,
akawatuma watu wawili kutoka Shitimu kwa siri, ili kupeleleza, akawaambia,
Enendeni mkaitazame nchi hii, na Yeriko. Wakaenda wakafika nyumbani kwa kahaba
mmoja jina lake aliitwa Rahabu, wakalala huko. Mfalme wa Yeriko akaambiwa,
kusema, Tazama, watu wawili wa wana wa Israeli wameingia humu leo usiku, ili
kuipeleleza nchi. Mfalme wa Yeriko akatuma watu kwa Rahabu, akasema, Watoe watu
wale waliokuja kwako, walioingia ndani ya nyumba yako, maana wamekuja ili
kuipeleleza nchi.”
Utafiti wa hivi karibuni
unaonyesha kuwa duniani kuna watu wapatao milioni 42 ambao wanajihusisha na
biashara ya ukahaba na wengi wao ni wanawake, Ukahaba ni swala lililo kinyume
na sheria katika inchi nyingi na linahesabika kama uhalifu, lakini hata hivyo
biashara hii inashamiri hata katika maeneo ambayo ni vigumu sana kuamini kuwa
yanaweza kuwa na ukahaba, mfano katika nchi ya Jordan ni rahisi kuona waziwazi
wanawake wa kiarabu wakijiuza kwa watalii, katika mpango mkakati wa kuhubiri
injili, Kanisa halina budi kuwa na Programu maalumu ya kujaribu kusaidia na
kuwafikia makahaba au watu wanaojihusisha na biashara hii kwa injili, kwani
wengine wamelazimika kuwa hivyo kutokana na kushindwa kuvumilia changamoto
mbalimbali za kimaisha, Mungu alimuhurumia Kahaba huyu na kumuokoa na kumsamehe
kabisa na kuolewa katika ukoo wa Yuda na hivyo kuingia katika mstari wa
wanawake maarufu wanaotajwa katika ukoo wa Masihi
Mathayo 1:1-5 “Kitabu cha ukoo wa Yesu
Kristo, mwana wa Daudi, mwana wa Ibrahimu. Ibrahimu alimzaa Isaka; Isaka
akamzaa Yakobo; Yakobo akamzaa Yuda na ndugu zake; Yuda akamzaa Peresi na Zera kwa Tamari;
Peresi akamzaa Esromu; Esromu akamzaa Aramu; Aramu akamzaa Aminadabu; Aminadabu
akamzaa Nashoni; Nashoni akamzaa Salmoni; Salmoni akamzaa Boazi kwa Rahabu;
Boazi akamzaa Obedi kwa Ruthu; Obedi akamzaa Yese; Yese akamzaa mfalme Daudi.
Daudi akamzaa Sulemani kwa yule mke wa Uria;”
Mambo yaliyopelekea maisha ya Rahabu kubadilika
Pamoja na changamoto aliyokuwa
anakabiliana nayo Rahabu katika maisha yake kama kahaba, Kahaba huyu alikuwa na
ufahamu mkubwa au ufahamu mpana jina lake Rahabu katika kiebrania linasomeka
kama “Rāhāb” au “Rahav” ambalo maana yake
mwenye ufahamu mpana au mwenye ufahamu mkubwa, kwa hiyo ni wazi kuwa Rahabu
alikuwa ni mwanamke mwenye uelewa mkubwa sana na ufahamu mpana,upana wa ujuzi
wake ulihifadhi siri nyingi sana na taarifa kubwa kama bahari. Rahabu alikuwa
ni mtu mwenye taarifa nyingi tena zilizo sahihi, kwa hiyo mwanamke huyu
vilevile alikuwa “informer” alikuwa ni
mtu mwenye uwezo mkubwa wa kudukuu taarifa na ndio maana hata mfalme wa inchi
alijua kuwa anaweza kupata taarifa sahihi za wapelekezi walioingia nchini mwake.
Yoshua 2:2-5 “Mfalme wa Yeriko akaambiwa,
kusema, Tazama, watu wawili wa wana wa Israeli wameingia humu leo usiku, ili
kuipeleleza nchi. Mfalme wa Yeriko akatuma watu kwa Rahabu, akasema, Watoe watu
wale waliokuja kwako, walioingia ndani ya nyumba yako, maana wamekuja ili
kuipeleleza nchi. Yule mwanamke akawatwaa wale watu wawili, akawaficha, akasema,
Naam, wale watu walikuja kwangu, lakini sikujua walikotoka; ikawa kama wakati
wa kufungwa lango la mji, kulipokuwa giza, watu wale wakatoka, wala sijui
walikokwenda; wafuateni upesi, maana mtawapata.”
Kutokana na uwezo wake mkubwa wa
kupata taarifa kahaba huyu alikuwa na taarifa zote za Wana wa Israel na matendo
yote ya Mungu wao na alitambua kila kitu kuhusu Wayahudi na Mungu wao Tangu
siku walipotoka Misri hivyo alikuwa na taarifa sahihi kuhusu Mungu huyu wa
kweli na kuamini
a.
Alimwamini
Mungu wa Israel - Yoshua 2:9-11 “ akawaambia wale wanaume, Mimi najua ya kuwa Bwana amewapa
ninyi nchi hii, na ya kuwa hofu imetuangukia mbele yenu, na ya kuwa wenyeji
wote wa nchi wanayeyuka mbele yenu. Maana tumesikia jinsi Bwana alivyoyakausha
maji ya bahari ya Shamu mbele yenu, hapo mlipotoka Misri, tena mambo hayo
mliyowatendea wafalme wawili wa Waamori waliokuwa huko ng'ambo ya Yordani,
yaani, Sihoni na Ogu, mliowaangamiza kabisa. Na mara tuliposikia hayo mioyo
yetu iliyeyuka, wala haukusalia ujasiri wo wote katika mtu awaye yote, kwa
sababu yenu; kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, yeye ndiye Mungu, katika mbingu juu na
katika nchi chini.”
b.
Alitaka
Agano la ukombozi – Licha ya kuwa na taarifa nyingi na sahihi na pana
kuhusu Waisrael na kuhusu Mungu wao, Rahabu pia alijua ni namna gani anaweza
kuyaokoa maisha yake na familia yake, alitambua namna anavyoweza kujiepusha na
maangamizi kwa sababu hiyo alifahamu namna na jinsi anavyoweza kujiweka salama
kwa kuingia katika agano na Mungu wa Israel na watu wake kwa sababu hiyo
aliwaomba wapelelezi wamuhakikishie wokovu wake na nyumba yote ya baba yake
Yosua 2:12-14 “Basi
sasa, nawasihi, niapieni kwa Bwana, kwa kuwa nimewatendea ihisani, ya kwamba
ninyi nanyi mtaitendea ihisani nyumba ya baba yangu; tena nipeni alama ya uaminifu;
ya kwamba mtawaponya hai baba yangu na mama yangu, na ndugu zangu wanaume na
wanawake, na vitu vyote walivyo navyo, na kutuokoa roho zetu na kufa. Wale
wanaume wakamwambia, Uhai wetu badala ya uhai wenu, ikiwa hamwitangazi habari
ya shughuli yetu hii; kisha itakuwa, wakati Bwana atakapotupa nchi hii,
tutakutendea kwa ihisani na uaminifu.”
c.
Alionyesha
Imani na matendo – Licha ya kumuamini Mungu wa Israel Rahabu aliwatendea
mema wapelelezi wale kwa kuwaficha na
kuwaelekeza njia ya kutorokea aliwalinda na hakutaka kuwatoa kwa watu wanchi
yake ili wauawe au kukamatwa, aliwatendea mema watu wa Mungu
Yoshua 2:15-16 “Ndipo
akawashusha kwa kamba dirishani, maana nyumba yake ilikuwa katika ukuta wa mji;
naye alikaa ukutani. Akawaambia, Enendeni zenu mlimani, wale wanaowafuatia
wasije wakawapata; mkajifiche huko siku tatu hata wao wanaowafuatia
watakaporudi; kisha enendeni zenu.”
Yakobo 2:25 “Vivyo
hivyo na Rahabu, yule kahaba naye, je! Hakuhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo,
hapo alipowakaribisha wajumbe, akawatoa nje kwa njia nyingine? Maana kama vile
mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa.”
Kujifunza kutoka kwa Rahabu yule kahaba
Ni wazi kuwa mtu huyu hakuwa
myahudi wala hakuwa mwenye metendo mema alikuwa kahaba, lakini Mungu alimuokoa
kwa sababu alimuamini Mungu, Yesu Kristo amekuja duniani sio kwaajili ya watu
Fulani maalumu, Mungu yuko tayari kumuokoa mtu yeyote wa kabila lolote na wa
historia yoyote maadamu tu mtu huyo atamuamini Mungu aliye hai na kazi yake ya
ukombozi kupitia mwanae mpendwa Yesu Kristo
Yohana 3:16 -18 “Kwa maana jinsi hii Mungu
aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye
asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni
ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye
hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la
Mwana pekee wa Mungu.”
Awaye yote akimuamini Yesu
Kristo, ataokolewa bila kujali kuwa anatokea katika historia gani, wala Mungu
haangalii makosa yetu ya zamani na badala yake anatazama moyo uliobadilika
kumuelekea yeye, Mungu alimuinua Kahaba Rahabu na kumpeleka juu sana hata kuwa
sehemu ya ukoo wa Yesu Kristo, wakati mwingine kuonelewa kwako sana na ibilisi
kunadhihirisha wivu mkubwa sana alio nao kwako endapo Mungu angekutana na wewe
Wokovu na haki ya Mungu sio vitu
vinavyopatikana kwa jitihada na matendo ya kibinadamu, bali Imani katika Mungu
na neema anayoitoa yeye, neema hii inaweza kwenda kwa yeyote yule bila kujali
historia yake.
Waefeso 2:8-9. “Kwa maana mmeokolewa kwa
neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha
Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu.”
No one is too special to meet the
Grace of God, Hakuna mtu ambaye yeye anaweza kudai kuwa ni maalumu sana mpaka
aweze kupokea neema ya Mungu, ni Imani yako kwake tu ndiyo inayoweza kumgusa na
akabadilisha maisha yako, huna lolote unaloweza kulifanya ukampendeza yeye,
zaidi ya kuamini. Usihuzunike kwa sababu labda umewahi kupitia historia mbaya
zaidi ya maisha yasiyofaa ambayo labda unaweza kudhania kuwa kwajili ya hayo
hustahili kuhurumiwa na Mungu, lakini nakutangazia kuwa haijalishi umepitia
maisha mabaya kiasi gani, Rahabu ni ishara ya kuwa hata wewe unaweza kupokelewa
na Mungu na historia ya maisha yako ikabadilika, ukamtangaza Kristo.
2Wakorintho 5:17 “Hata imekuwa, mtu akiwa
ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.”
Yeriko ulipoharibiwa Rahabu
pamoja na familia yake na nyumba ya baba yake waliokolewa wote kwa sababu ya
Imani na agano lile aliloapiwa na Wapelelezi katika inchi ya Kanaani, Mungu
alikuwa mwaminifu kwa ahadi zake, na watu wake walikuwa wamejifunza kusimamia
viapo vyao kwani Yoshua alikumbuka kuwa yuko mtu ambaye hastahili kuangamizwa
kwa sababu amemuamini Mungu wa Israel na ana agano na Mungu wa Yakobo!
Yoshua 6:22-25 “Naye Yoshua akawaambia wale
wanaume wawili walioipeleleza nchi, Ingieni katika nyumba ya yule kahaba,
mkamtoe huyo mwanamke mwenyewe na vitu vyote alivyo navyo, kama mlivyomwapia.
Basi wale vijana wapelelezi wakaingia, wakamtoa Rahabu, na baba yake, na mama
yake, na ndugu zake, na vitu vyote walivyokuwa navyo, wakawatoa na jamaa zake
wote pia; wakawaweka nje ya matuo ya Israeli. Kisha wakauteketeza mji kwa moto,
na vitu vyote vilivyokuwa ndani yake; bali fedha, na dhahabu, na vyombo vya
shaba, na vya chuma, wakavitia katika hazina ya nyumba ya Bwana. Lakini Yoshua
akamhifadhi Rahabu, yule kahaba, na watu wa nyumba ya baba yake, na vitu vyote
alivyokuwa navyo; naye akakaa kati ya Israeli hata leo; kwa sababu aliwaficha
wale wajumbe aliowatuma Yoshua ili kuupeleleza mji wa Yeriko.”
Wokovu ni zawadi ya Mungu kwa
watu wote, Mungu hana upendeleo, hatupaswi kujivunia wokovu na kujifikiri kuwa
sisi ni watu maalumu sana kuliko wengine, Mungu ni Mungu wa wote wenye mwili
anaweza kumuokoa yeyote na anaweza kumuinua yeyote ana anaweza kumtumia yeyote,
wapelelezi hawakuweza kabisa kumdharau Rahabu kwa sababu ya ukahaba wake na
maisha yake yaliyopita badala yake walimuheshimu na kumsikiliza, na walifuata
maelekezo yake. Mungu alimhamisha Rahabu kutoka katika maisha ya dhambi kwenda
katika historia ya ukombozi wa mwanadamu, ni kupitia rehema za Mungu, na neema
yake yeye anaweza kuwafikiwa watu wote na wa jinsia zote na imani zote duniani,
hupaswi kujikinai na kujifikiri kuwa wewe ni mtu asiyefaa, badala yake mtazame
yule tu awezaye kuokoa, haki yetu haihesabiwi na wanadamu, haki yetu
inahesabiwa na Mungu na hakuna mwanadamu yeyote mwenye mamlaka ya kutushitaki
Zaburi 130:3-4 “Bwana, kama Wewe ungehesabu
maovu, Ee Bwana, nani angesimama? Lakini kwako kuna msamaha, Ili Wewe uogopwe.”
Warumi 8:33-34 “Ni nani atakayewashitaki
wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia
adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika
wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea.”
Na. Rev. Innocent Mkombozi bin Samuel bin Hamza bin Jumaa bin Athumani
bin Salim Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni