Jumapili, 5 Julai 2026

Kwa kuwa sasa Bwana ametufanyia nafasi!


Mwanzo 26:19-22 “Watumwa wa Isaka wakachimba katika lile bonde, wakapata kisima cha maji yanayobubujika. Wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema, Maji haya ni yetu. Ndipo akakiita jina la kile kisima Eseki, kwa sababu waligombana naye. Wakachimba kisima kingine, wakagombania na hicho tena. Akakiita jina lake Sitna. Akaondoka huko akachimba kisima kingine, wala hicho hawakukigombania. Akakiita jina lake Rehobothi, akasema, Kwa kuwa sasa BWANA ametufanyia nafasi, nasi tutazidi katika nchi.”




Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa mtu awaye yote anapokuwa amebarikiwa na Mungu, au kama Mungu yuko pamoja na yeye anaweza kupitia vipingamizi vya aina mbalimbali katika maisha, watu wa Mungu wakati mwingine watapitia chuki zisizokuwa za kawaida, kuonewa wivu, na wakati mwingine kupitia mapambano mengi, Maisha ya Isaka ni mojawapo ya mfano wa matukio kama hayo, baada ya kuwa Mungu amemfungulia milango ya Baraka na uhuru, kutoka katika kuandamwa na vita na chuki na wivu wa maisha kutoka kwa wafilisti, Waligombania na kumpokonya visima vyake viwili yaani maji ya Eseki na Stina, hatimaye alipata maji sehemu nyingine ambapo alipaita Rehoboth akitangaza kwa imani kuwa sasa Bwana amemfanyia nafasi!, kwani kisima hicho hakikugombaniwa tena.

Mwanzo 26:19-22 “Watumwa wa Isaka wakachimba katika lile bonde, wakapata kisima cha maji yanayobubujika. Wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema, Maji haya ni yetu. Ndipo akakiita jina la kile kisima Eseki, kwa sababu waligombana naye. Wakachimba kisima kingine, wakagombania na hicho tena. Akakiita jina lake Sitna. Akaondoka huko akachimba kisima kingine, wala hicho hawakukigombania. Akakiita jina lake Rehobothi, akasema, Kwa kuwa sasa BWANA ametufanyia nafasi, nasi tutazidi katika nchi.”

Leo tutachukua muda kujifunza na kutafakari kwa kina kuhusiana na maisha ya Isaka ambayo kimsingi yanatufundisha kuwa maisha ya watu wa Mungu na watu wa kawaida yana changamoto za aina mbalimbali lakini hata hivyo tunapoendelea kumtegemea Mungu hatimaye Mungu hutupa ahueni, tutajifunza somo hili Kwa kuwa sasa Bwana ametufanyia nafasi kwa kuzingatia vipengele muhimu vitatu vifuatayo:-

·         Maana ya maneno Bwana ametufanyia nafasi

·         Maisha ya changamoto za mtu wa Mungu

·         Kwa kuwa sasa Bwana ametufanyia nafasi


Maana ya maneno Bwana ametufanyia nafasi.

Maneno Kwa kuwa Bwana ametufanyia nafasi  kwa Kiebrania “Rehoboth” yalitamkwa na Isaka yakimaanisha majira ya Mungu ya kuwapa watu wake mpenyo, pumziko la kiroho, nafasi ya kukua, nafasi ya kuongezeka, nafasi ya kuwa na Amani, nafasi ya kutokuweko katika migogoro, nafasi ya kustawi pasipokuwa na upinzani, nafasi ya thamani na utulivu, kwa hiyo neno “Rehoboth” au “Rechovoth” la Kiebrania lina maana ya Nafasi kubwa, eneo la kukua na kupanuka, uhuru wa kutenda bila upinzani, nafasi ya kustawi, na nafasi ya kuwa nje ya vikwazo, hali hii haisababishwi na akili za kibinadamu bali inasababishwa na Mungu anapoingilia kati na kundoa shinikizo na msongamano wa changamoto ili kutoa utulivu kwa watu wake, huu ni mchakato wa kuondoka katika mashinikizo kadhaa ya maisha yanayopelekea kuifikia ndoto ya utulivu unaohitajika kibinadamu.

Mungu alimpa nafasi Rehoboth Yusufu baada ya mapito ya muda mrefu katika maisha kwa kusudi la kufikia hatima yake - Mwanzo 41:38-41 “Farao akawaambia watumwa wake, Tupate wapi mtu kama huyu, mwenye roho ya Mungu ndani yake? Farao akamwambia Yusufu, Kwa kuwa Mungu amekufahamisha hayo yote, hapana mwenye akili na hekima kama wewe. Basi wewe utakuwa juu ya nyumba yangu, na kwa neno lako watu wangu watatawaliwa. Katika kiti cha enzi tu nitakuwa mkuu kuliko wewe. Farao akamwambia Yusufu, Tazama, nimekuweka juu ya nchi yote ya Misri.”

Mungu alimpa nafasi Daudi nafasi ya kutoka katika hali duni ya kuchunga kondoo na kudharaulika katika familia mpaka kuwa mfalme katika Israel – 1Samuel 16:11-13 “Kisha Samweli akamwambia Yese, Watoto wako wote wapo hapa? Naye akasema, Amesalia mdogo wao, na tazama, anawachunga kondoo. Basi Samweli akamwambia Yese, Tuma watu, wamlete; kwa sababu hatutaketi hata atakapokuja huku. Basi akatuma mtu, naye akamleta kwao. Naye alikuwa mwekundu, mwenye macho mazuri, na umbo lake lilikuwa la kupendeza. Bwana akasema, Ondoka, umtie mafuta; maana huyu ndiye.Ndipo Samweli akaitwaa pembe yenye mafuta, akamtia mafuta kati ya ndugu zake; na roho ya Bwana ikamjilia Daudi kwa nguvu tangu siku ile. Basi Samweli akaondoka, akaenda zake Rama.”

Mungu anapokufanyia nafasi au kukuletea “Rehoboth” anakuweka katika mahali ambapo adui zako hawawezi kuzuia maendeleo na ustawi wako, Milango iliyokuwa imefungwa au iliyokuwa inakutana na upinzani huanza kufunguka na kupata upenyo, Milango ya Baraka huanza kutiririka kwa urahisi, miguu yako inawekwa mahali palipoinuka na hakuna taabu tena ya kupita katika mabonde

Zaburi 31:7-8 “Na nishangilie, nizifurahie fadhili zako, Kwa kuwa umeyaona mateso yangu. Umeijua nafsi yangu taabuni, Wala hukunitia mikononi mwa adui; Miguu yangu umeisimamisha panapo nafasi.”

Maisha ya changamoto za mtu wa Mungu

Kabla Isaka hajapata utulivu wa maisha “Rehoboth” alipitia changamoto nyingi sana ambazo wakati mwingine hata watu wengine wa Mungu wanapitia, hii inamaanisha kuwa changamoto ni sehemu ya kawaida ya maisha ya mwanadamu lakini hata hivyo tukimtegemea Mungu atajitokeza hatimaye na kutupatia nafasi

·         Isaka alipoteza mama yake mpendwa Sara -  Jambo hili liliumiza sana maisha yake kama wote tunavyofahamu unapoondokewa na wazazi, moyo unauma sana na unagubikwa na upweke mkubwa  hata hivyo ujio wa Rebeka katika maisha ya Isaka ulimpa unafuu katika changamoto hiyo

 

Mwanzo 24:67 “Isaka akamwingiza Rebeka katika hema ya mama yake, Sara, akamtwaa Rebeka, akawa mkewe, akampenda; Isaka akafarijika kwa ajili ya kufa kwa mamake.”

 

·         Isaka alipitia kipindi cha kukosa mtoto miaka 20 – Baada ya Rebeka kuwa faraja kwa muda sasa wanakutana na changamoto nyingine katika maisha na sasa wanakosa mtoto kwa muda wa miaka 20, Isaka alimuoa Rebeka akiwa na miaka 40 na alikuja kupata watoto Esau na Yakobo akiwa na miaka 60, hiki ni kipindi cha kupimwa imani na uvumilivu, na ni mpaka Isaka alipomuomba Mungu ndipo Mungu alipojibu maombi na watoto mapacha wakapatikana

 

Mwanzo 25:19-28 “Na hivi ndivyo vizazi vya Isaka, mwana wa Ibrahimu. Ibrahimu alimzaa Isaka. Isaka akawa mwenye miaka arobaini alipomtwaa Rebeka binti Bethueli, Mshami, wa Padan-aramu, ndugu wa Labani, Mshami, kuwa mke wake. Isaka akamwomba BWANA kwa ajili ya mke wake, maana alikuwa tasa. Naye BWANA akamwitikia, na Rebeka mkewe akachukua mimba. Watoto wakashindana tumboni mwake. Naye akasema, Ikiwa ni hivi, kuishi kwanifaa nini? Akaenda kumwuliza BWANA. BWANA akamwambia, Mataifa mawili yamo tumboni mwako, Na kabila mbili za watu watafarakana tangu tumboni mwako. Kabila moja litakuwa hodari kuliko la pili, Na mkubwa atamtumikia mdogo. Siku zake za kuzaa zilipotimia, tazama! Mapacha walikuwamo tumboni mwake. Wa kwanza akatoka, naye alikuwa mwekundu mwili wote kama vazi la nywele. Wakamwita jina lake Esau. Baadaye ndugu yake akatoka, na mkono wake unamshika Esau kisigino. Akaitwa jina lake Yakobo. Isaka alikuwa mwenye miaka sitini mkewe alipowazaa. Watoto wakakua, Esau alikuwa mtu ajuaye kuwinda wanyama, mtu wa nyikani, na Yakobo alikuwa mtu mtulivu, mwenye kukaa hemani. Basi Isaka akampenda Esau, kwa sababu alikula mawindo yake, na Rebeka akampenda Yakobo.”

 

·         Isaka alikabiliwa na njaa kubwa katika inchi – Akiwa katika nchi ya ahadi Isaka anakumbwa na njaa kali sana, njaa kama ya siku za baba yake Abrahamu ambayo ilimpelekea Abrahamu kukimbilia Misri hata hivyo kwa neema ya Mungu, Mungu alisema na Isaka asishuke kwenda Misri kama ilivyokuwa kwa baba yake, Mungu aliamua kumbariki pale pale  mahali ambapo wengine walikuwa hawana matumaini.

 

Mwanzo 26:1-5 “Ikawa njaa katika nchi hiyo, mbali na njaa ile ya kwanza iliyokuwa siku za Ibrahimu. Isaka akamwendea Abimeleki, mfalme wa Wafilisti, huko Gerari. BWANA akamtokea, akasema, Usishuke kwenda Misri, kaa katika nchi nitakayokuambia. Kaa ugenini katika nchi hiyo, nami nitakuwa pamoja nawe, na kukubariki, maana nitakupa wewe na uzao wako nchi hizi zote. Nami nitakifanya imara kiapo nilichomwapia Ibrahimu baba yako. Nitazidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, nami nitawapa uzao wako nchi hizi zote, na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia. Kwa sababu Ibrahimu alisikia sauti yangu, akayahifadhi maagizo yangu, na amri zangu, na hukumu zangu, na sheria zangu.”

 

·         Isaka alikabiliwa na kuonewa wivu (Husuda) na wafilisti – Mungu alimbariki sana Isaka baada ya kubaki katika inchi ya Mkanaani, Mungu alikuwa amemuwezesha Isaka kuchimba visima vya baba yake Ibrahimu na kumsaidia kwa kutumia maji yanayobubujika kufanya kilimo cha umwagiliaji na kujipatia mazao na kuwanywesha mifugo hivyo kukawa na mafanikio makubwa sana hata wakati wa njaa Isaka alipanda kipimo cha mbegu na kuvuna mara mia, hivyo mtu huyu akawa mkuu mno na hapo ndipo Wafilisti wakamuonea wivu, kumbe kadiri Mungu anavyokubariki sana na kukuinua juu ndivyo Baraka zako zinavyoambatana na upinzani kutoka kwa watu wenye wivu wenye uchungu

 

Mwanzo 26:12-14 “Isaka akapanda mbegu katika nchi ile, akapata mwaka ule vipimo mia kwa kimoja, BWANA akambariki. Na mtu huyu akawa mkuu, akazidi kusitawi, hata akawa mkuu sana. Akawa na mali ya kondoo, na mali ya ng'ombe, na watumwa wengi. Hao Wafilisti wakamhusudu.”

 

·         Isaka alipambana na jaribu la kufukiwa kwa visima vyake – Bila shaka wafilisti walibaini kuwa utajiri wa Isaka na mafanikio makubwa aliyokuwa nayo ni uwepo wa Mungu na vile vile visima alivyokuwa amechimba na vikawa vinabubujisha maji, Wafilisti waliamua kuvifukia  visima  vyote ambavyo kimsingi vilikuwa vya baba yake yaani Abrahamu, Wafilisti walivifukia, wakati wote shetani atataka kufukia kila chanzo cha Baraka kwa watu wa Mungu ili usitoke

 

Mwanzo 26:15-21 “Na vile visima vyote walivyochimba watumwa wa baba yake, siku za Ibrahimu babaye, Wafilisti walikuwa wamevifukia, wakavijaza kifusi. Abimeleki akamwambia Isaka, Utoke kwetu, maana wewe una nguvu sana kuliko sisi. Basi Isaka akatoka huko akapiga kambi katika bonde la Gerari, akakaa huko.Isaka akarudi akavichimbua vile visima vya maji walivyovichimba siku za Ibrahimu babaye; maana wale Wafilisti walikuwa wamevifukia baada ya kufa kwake Ibrahimu; naye akaviita majina kufuata majina alivyoviita babaye.Watumwa wa Isaka wakachimba katika lile bonde, wakapata kisima cha maji yanayobubujika. Wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema, Maji haya ni yetu. Ndipo akakiita jina la kile kisima Eseki, kwa sababu waligombana naye. Wakachimba kisima kingine, wakagombania na hicho tena. Akakiita jina lake Sitna.”

 

·         Isaka alifukuzwa kwa sababu ua ukuu wake -  Isaka alibarikiwa sana na kuwa mtu mkubwa sana, uwepo wa Mungu ulikuwa pamoja naye, upako na karama zilikaa juu yake, hakuwa mtu wa vita alikuwa mtu wa utulivu na mtu wa Amani lakini hata hivyo adui zake walishindwa kumstahimili na hivyo waliamua kumfukuza, ziko nyakati ambazo unaweza kukataliwa bila sababu au unaweza kutengenezewa zengwe ili usiwepo katika maeneo hayo na sababu kubwa watu wanadhani ukuu wako unatokana na hapo ulipo, lakini sio hivyo tu watu wema wakati mwingine hukataliwa na hata kuuawa kwa sababu ya wema wao

 

Mwanzo 26:13-16 “Na mtu huyu akawa mkuu, akazidi kusitawi, hata akawa mkuu sana. Akawa na mali ya kondoo, na mali ya ng'ombe, na watumwa wengi. Hao Wafilisti wakamhusudu. Na vile visima vyote walivyochimba watumwa wa baba yake, siku za Ibrahimu babaye, Wafilisti walikuwa wamevifukia, wakavijaza kifusi. Abimeleki akamwambia Isaka, Utoke kwetu, maana wewe una nguvu sana kuliko sisi.”

 

·         Isaka alinyimwa nafasi – Mgogoro wa visima pamoja na kufukuzwa katika nchi ya Wafilisti wakati wote ilikuwa inalenga kumnyima Isaka ustawi, adui alikuwa anawekwa vikwazo ili kumnyima Isaka fursa ya utulivu na mafanikio, waligombea kisima cha kwanza akakiita Eseki maana yake UGOMVI, walifukia kisima cha pili na kukigombea akakiita Sitna maana yake UADUI kwa hiyo utaona Isaka anakabiliwa na ugomvi, uadui, upinzani, chuki na husuda, lakini kwa jinsi alivyokuwa muungwana na mwororo, hakugombana na mtu, tunajifunza ya kuwa tunaweza kushinda vita vingi kwa kuwa waungwana na kwa kutumia hekima kuliko kushindana na kujiingiza kwenye migogoro, kutokana na utulivu huu hatimaye Mungu aliamua kumpa utulivu halisi na hapa ndipo Bwana alipompa Nafasi, Rehoboth

 

Mwanzo 26:17-22 “Basi Isaka akatoka huko akapiga kambi katika bonde la Gerari, akakaa huko. Isaka akarudi akavichimbua vile visima vya maji walivyovichimba siku za Ibrahimu babaye; maana wale Wafilisti walikuwa wamevifukia baada ya kufa kwake Ibrahimu; naye akaviita majina kufuata majina alivyoviita babaye. Watumwa wa Isaka wakachimba katika lile bonde, wakapata kisima cha maji yanayobubujika. Wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema, Maji haya ni yetu. Ndipo akakiita jina la kile kisima Eseki, kwa sababu waligombana naye. Wakachimba kisima kingine, wakagombania na hicho tena. Akakiita jina lake Sitna. Akaondoka huko akachimba kisima kingine, wala hicho hawakukigombania. Akakiita jina lake Rehobothi, akasema, Kwa kuwa sasa BWANA ametufanyia nafasi, nasi tutazidi katika nchi.”            

Kwa kuwa sasa Bwana ametufanyia nafasi

Mpenzi maisha ya Isaka  yanamkumbusha kila mmoja wetu kuwa changamoto unazozipitia ni za kawaida, kila mtu wa Mungu anaweza kupitia changamoto za iana mbalimbali katika maisha, Yesu alisema ulimwenguni mnayo dhiki, kwa sababu hiyo dhiki kama hizi ni za kawaida kwa watu wa Mungu, hata hivyo tunapoendelea kuwa na subira na kumtegemea Mungu hatimaye Mungu atatufanyia nafasi REHOBOTH Isaka kwa kweli hakuzitegemea akili zake mwenyewe, tunaweza kukiri kuwa kweli alikuwa na taaluma ya kuchimba visima lakini taaluma hiyo ingeweza kuigizwa na wengine au kusambazwa lakini hii ilikuwa ni ishara ya kuwa Mungu alikuwa pamoja naye, ukiri wake na kauli yake haikuwa kuwa sasa tumetoboa na badala yake alikiri kuwa ni Mungu ndiye aliyewafanyia  nafasi. Isaka aliendelea kubarikiwa mpaka adui zake walikuja kujipendekeza na kufanya Amani naye huku wakitambua kuwa hakika alikuwa na Mungu

Mwanzo 26:22-29 “Akaondoka huko akachimba kisima kingine, wala hicho hawakukigombania. Akakiita jina lake Rehobothi, akasema, Kwa kuwa sasa BWANA ametufanyia nafasi, nasi tutazidi katika nchi. Akapanda kutoka hapo mpaka Beer-sheba. BWANA akamtokea usiku uleule, akasema, Mimi ni Mungu wa Ibrahimu baba yako, usiogope, maana mimi ni pamoja nawe, nami nitakubarikia, na kuzidisha uzao wako kwa ajili ya Ibrahimu mtumishi wangu. Akajenga madhabahu huko, akaliitia jina la BWANA. Akapiga hema yake huko, na watumwa wa Isaka wakachimba kisima huko. Ndipo Abimeleki akamwendea kutoka Gerari, pamoja na Ahuzathi rafiki yake, na Fikoli, jemadari wa jeshi lake. Isaka akawauliza, Mbona mwanijia, nanyi mmenichukia, mkanifukuza kwenu?Wakasema, Hakika tuliona ya kwamba BWANA alikuwa pamoja nawe; nasi tukasema, Na tuapiane, sisi na wewe, na kufanya mapatano nawe ya kuwa hutatutenda mabaya, iwapo sisi hatukukugusa wewe, wala hatukukutendea ila mema, tukakuacha uende zako kwa amani; nawe sasa u mbarikiwa wa BWANA.”

Mambo ya kujifunza kutokana na maisha ya Isaka hapo:-

1.       Mungu ndiye anayetengeneza nafasi – Isaka hakusema kwamba tumetoboa, au tumewapiga bao Wafilisti au hawatuwezi hapana, yeye alisema sasa Bwana ametufanyia nafasi na tutazidi kuongezeka alisema haya kutokana na amani kwamba sasa maadui waliogopa kumfuatilia, dhamiri zao ziliwashitaki kwamba wataendelea na dhuluma zao mpaka lini mafanikio ya kweli ni yale ambayo Bwana ndiye anayekupigania, adui zako wanatamani usiwepo lakini wewe unaendelea kustawi na sababu ya ustawi wako inagunduliwa wazi kuwa ni Mungu, Mungu akikuandalia mazingira inapendeza sana kuliko wewe mwenyewe ukijilazimishia mazingira ya mafanikio

 

Zaburi 127:1 “Bwana asipoijenga nyumba Waijengao wafanya kazi bure. Bwana asipoulinda mji Yeye aulindaye akesha bure.”          

 

2.       Mafanikio ya kweli yanahitaji uvumilivu – wako watu ambao wanatamaa ya mafanikio na wanadhani kuwa mafanikio yanakuja kwa kuamka tu asubuhi, au kwa kuyalazimisha, nimeona watu wengi sana hasa vijana wanataka kila kitu kitokee kwa haraka lakini ni muhimu kuwa wavumilivu na kuwa wenye subira kwa sababu Mungu sio dhalimu kwa wakati wake atafanya, Isaka alivumilia, dhihaka, utasa, huzuni, njaa, wivu, ugomvi, kufukuzwa, uadui, dhuluma na kadhalika, alikuwa na nguvu kubwa sana lakini hakuitumia kupigana na adui zake  na kisha Bwana mwenyewe alimfanyia nafasi, hatupaswi kujipigania, hatupawi kukata tamaa hata kama Eseki na Sitna zitatokea katika maisha yetu hatimaye REHOBOTH italetwa na Bwana  kila mtu wa Mungu ajifunze ya kuwa anahitaji uvumilivu Saburi na mambo hayatakuja kuwa wakati mwingine kwa haraka kama tunavyofikiri

 

3.       Mungu anapokufungulia mlango Rehoboth - anakutengenezea mazingira ya kuongezeka, anakufanya ukue, huduma yako itakua, familia yako itaongezeka, uchumi wako utakuwa, Kiroho utakuwa, ushawishi utaiongezeka  utaogopwa, utaabudu kwa Amani na usalama, utafutwa machozi, adui zako watakuja kupatana na wewe wao wenyewe, utafurahia ndoa yako, utamfurahia Bwana Mungu wako, utafurahia biashara zako, utafurahia mifugo na kilimo, utaongeza maarifa hekima na elimu, utatimiza makusudi ya Mungu utakuwa na shuhuda, utatumika  

 

Zaburi 4:1-5 “Ee Mungu wa haki yangu, uniitikie niitapo; Umenifanyizia nafasi wakati wa shida; Unifadhili na kuisikia sala yangu. Enyi wanadamu, hata lini utukufu wangu utafedheheka? Je! Mtapenda ubatili na kutafuta uongo? Bali jueni ya kuwa Bwana amejiteulia mtauwa; Bwana atasikia nimwitapo. Mwe na hofu wala msitende dhambi, Tafakarini vitandani mwenu na kutulia. Toeni dhabihu za haki, Na kumtumaini Bwana

Ndugu zangu wapenzi kaka zangu na dada zangu, haijalishi ni maisha ya namna gani unayapitia, tambua tu kuwa dunia haina huruma hata kidogo na maisha yako, ni lazima umuwekee Mungu tumaini lako, unapojikita katika kumtegemea Mungu na kujiepusha na migogoro kisha wewe kuwa sababu ya Amani Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka na Yakobo baba zetu hatatuacha dunia yote na kila mtu anayesikia shuhuda zako atajua wazi kuwa Bwana yuko pamoja nawe, Bwana atakupigania nawe utanyamaza kimya, adui zako watakuja kukusujudia, hiki ndicho kilichomtokea Isaka Bwana alikuwa pamoja naye mpaka adui zake walilitambua hilo na kufanya Amani naye, wewe hupigani mwenyewe yuko anayekupigania naye yu hai katika jina la Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai, Amen!

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Hakuna maoni: