Jumapili, 8 Novemba 2026

Kuondolewa kwa kinara cha Kanisa katika mahali pake!


Ufunuo 2:2-5 “Nayajua matendo yako, na taabu yako, na subira yako, na ya kuwa huwezi kuchukuliana na watu wabaya, tena umewajaribu wale wajiitao mitume, nao sio, ukawaona kuwa waongo; tena ulikuwa na subira na kuvumilia kwa ajili ya jina langu, wala hukuchoka. Lakini nina neno juu yako, ya kwamba umeuacha upendo wako wa kwanza. Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, NAMI NITAKIONDOA KINARA CHAKO KATIKA MAHALI PAKE, usipotubu.”




Utangulizi:

Mojawapo ya Kanisa ambalo lilikuwa na historia nzuri sana nyakati za Kanisa la kwanza pamoja na makanisa mengine lilikuwa ni Kanisa la Efeso, Kanisa hili lilikuwa ni kanisa la watu wenye bidii katika kazi ya Mungu, wavumilivu, waliokuwa na uwezo mkubwa wa kupima walimu (Mitume) wa uongo na kutokuchukuliana na watu wabaya, walikuwa na subira kwaajili ya Yesu Kristo na wala hawakuchoka, watu wa Efeso waliupokea wokovu kwa gharama kubwa na kwa upendo mkuu sana wakichoma vitabu vya uganga vya gharama kubwa sana kwa wakati huo vikikadiriwa kuwa na thamani ya vipande vya fedha 50,000. Sawa na shillingi za kitanzania zipatazo milioni 846 (845,908,525.00 TZS) katika tafasiri ya siku za leo. Kitendo kilichoonyesha toba ya kweli na upendo mkubwa kwa Yesu Kristo kwa hiyo lilikuwa ni kanisa lililojitoa kwa Mungu kwa moyo wote!

Matendo 19:18-20 “Na wengi wa wale walioamini wakaja wakaungama, wakidhihirisha matendo yao. Na watu wengi katika wale waliotumia mambo ya uganga wakakusanya vitabu vyao, wakavichoma moto mbele ya watu wote; wakafanya hesabu ya thamani yake, wakaona ya kwamba yapata fedha hamsini elfu. Hivyo ndivyo neno la Bwana lilivyozidi na kushinda kwa nguvu.”

Kitendo hiki kiliashiria upendo wa dhati kwa Mungu na kusababisha neno la Mungu kuenea kwa nguvu kubwa zaidi na imani hii iliheshimiwa na watu wengi kila mahali, kwani huu ulikuwa ni ushuda wa hadharani unaodhihirisha kuwa watu hawa waliamua kuwa kielelezo na nuru katika Asia, wakiacha ibada za sananu na miungu maarufu na kumgeukia Kristo. Hata hivyo pamoja na maswala kadhaa mema yaliyokuwako katika kanisa hili Yesu katika waraka wake kupitia kitabu cha Ufunuo analikemea kanisa hili kuwa limeuacha upendo wa Kwanza na kulitaka litubu lakini swala la kuogopesha zaidi ni kuwa Yesu analitahadharisha kanisa hili kuwa “nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu”, hili onyo linatupa kutafakari kwa kina sana nini maana ya kuondolewa kwa kinara cha kanisa katika mahali pake, kumbe basi kanisa linaweza kuwa na shughuli nyingi za kidini, wahubiri wengi, ibada nyingi, makongamano mengi, mipango mingi, na mafanikio mengi yanayoweza kuonekana kwa macho lakini tukapoteza kitu muhimu ambacho huenda Kristo anakitamani zaidi, tutajifunza somo hili Kuondolewa kwa kinara cha Kanisa katika mahali pake kwa kuzingatia vipengele muhimu vikuu vitatu vifuatavyo:-

·         Maana ya Kinara.

·         Kuondolewa kwa kinara cha Kanisa katika mahali pake.

·         Mambo ya kufanya ili kinara kisiondolewe.

Maana ya Kinara.

Ufunuo 2:4-5 “Lakini nina neno juu yako, ya kwamba umeuacha upendo wako wa kwanza. Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, nami NITAKIONDOA KINARA CHAKO katika mahali pake, usipotubu.”

Neno kinara linalotumika katika maandiko yetu ya msingi hapo katika lugha ya Kiyunani (Greek) linatumika neno “luchnia” ambalo kwa kiingereza ni “lampstand” kwa Kiswahili ni “kinara cha taa” Katika lugha ya Kiebrania kinara hicho kiliitwa “Menora” ambacho kimsingi kilitengenezwa kwa dhahabu yenye uzito wa Paund 75 kikiwa na umbile la mmea wa mlozi (Almond) huku kukiwa na matawi sita matatu upande huu na matatu upande huu na sehemu ya katikati hivyo kufanya kinara hicho kubeba taa saba, kifaa hiki kiliwekwa upande wa kusini mwa Hekalu katika eneo la patakatifu sehemu iliyokuwa ikihusisha makuhani katika kazi zao za kila siku ikikabiliana na meza ya mikate ya wonyesho kazi yake kubwa ilikuwa ni kuwapa makuhani mwanga wa kuendelea na shughuli zao za kiibada katika eneo hilo muhimu la Hekalu liitwalo patakatifu, kinara hiki taa zake ziliwaka kupitia mafuta ya mti wa mzeituni!

Kutoka 25:31-40 “Nawe fanya kinara cha taa cha dhahabu safi; hicho kinara na kifanywe cha kazi ya kufua, tako lake, na mti wake, vikombe vyake, na matovu yake, na maua yake, vyote vitakuwa vya kitu kimoja nacho; nacho kitakuwa na matawi sita yenye kutoka ubavuni mwake; matawi matatu ya kinara upande wake mmoja, na matawi matatu ya kinara upande wake wa pili vikombe vitatu vilivyofanywa mfano wa maua ya mlozi katika tawi moja; tovu na ua; na vikombe vitatu vilivyofanywa mfano wa maua ya mlozi katika tawi la pili, tovu na ua; vivyo hivyo hayo matawi yote sita yatokayo katika kile kinara; na katika hicho kinara vikombe vinne vilivyofanywa mfano wa maua ya mlozi, matovu yake, na maua yake; na tovu chini ya matawi mawili la kitu kimoja nacho, na tovu chini ya matawi mawili la kitu kimoja nacho, na tovu chini ya matawi mawili la kitu kimoja nacho, kwa hayo matawi sita yatokayo katika kile kinara. Matovu yake na matawi yake yatakuwa ya kitu kimoja nacho; kiwe chote pia kazi moja ya kufua, ya dhahabu safi. Nawe zifanye taa zake saba; nao wataziwasha hizo taa zake, zitoe nuru mbele yake. Na makoleo yake, na visahani vyake, vyote vitakuwa vya dhahabu safi. Kitafanywa cha talanta moja ya dhahabu safi, pamoja na vyombo hivi vyote. Nawe angalia ya kwamba uvifanye kama mfano wake, ulioonyeshwa mlimani.”

Kutoka 37:17-23 “Kisha akakifanya kile kinara cha taa cha dhahabu safi, akakifanya kile kinara cha taa cha kazi ya kufua, tako lake, na mti wake; vikombe vyake, na matovu yake, na maua yake, vyote vilikuwa vya kitu kimoja nacho, nacho kilikuwa na matawi sita yaliyotoka ubavuni mwake; matawi matatu ya kinara yalikuwa upande huu, na matawi matatu ya kinara yalikuwa upande huu; vikombe vitatu, vilivyofanywa mfano wa maua ya mlozi vilikuwa katika tawi moja, tovu na ua; na vikombe vitatu, vilivyofanywa mfano wa maua ya mlozi, katika tawi la pili, tovu na ua; yalikuwa ni vivyo hivyo yale matawi sita yaliyokuwa katika hicho kinara. Katika kinara mlikuwa na vikombe vinne, vilivyofanywa mfano wa maua ya mlozi, matovu yake na maua yake; kisha chini ya matawi mawili mlikuwa na tovu iliyokuwa ya kitu kimoja nacho, na chini ya matawi mawili mengine mlikuwa na tovu ya kitu kimoja nacho, tena chini ya matawi mawili hayo mengine mlikuwa na tovu ya kitu kimoja nacho; kwa ajili ya hayo matawi sita, yaliyotokana nacho. Hayo matovu yake na matawi yake yalikuwa ya kitu kimoja nacho; kinara hicho kizima chote pia ni kazi moja ya kufua ya dhahabu safi. Kisha akafanya taa zake saba, na makoleo yake, na visahani vyake, vya dhahabu safi.”

Zekaria 4:2-6 “Akaniuliza, Unaona nini? Nikasema, Nimeona, na tazama, kinara cha taa cha dhahabu tupu, nacho kina bakuli juu yake, na taa zake saba juu yake; tena iko mirija saba ya kuleta mafuta, kwa taa zote zilizo juu yake; na mizeituni miwili karibu yake, mmoja upande wa kuume walile bakuli, na mmoja upande wake wa kushoto. Nami nikajibu, nikamwambia yule malaika aliyesema nami, nikasema, Ee Bwana wangu, vitu hivi ni nini? Ndipo malaika aliyesema nami akajibu, akaniambia, Hujui vitu hivi ni nini? Nikasema, La, Bwana wangu. Akajibu akaniambia, akisema, Hili ndilo neno la Bwana kwa Zerubabeli, kusema, Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema Bwana wa majeshi.”

Kinara hiki kimsingi ambacho kilijulikana pia kama taa yenye vinara saba katika agano la kale ilikuwa inawakilisha Nuru ambayo ilikuwa inaondoa giza lote katika patakatifu ili kuwasaidia makuhani kufanya wajibu wao wa ibada za upatanisho kati ya watu na Mungu, aidha taa hii ilikuwa inawakilisha Ustawi na ukuaji wa maisha ya watu wa Mungu na ndio maana iliundwa ikifanana na mti wa mlozi, lakini pia ilikuwa ikiwakilisha kuchanua au kufufuka  zaidi ya yote  taa hii ilikuwa inawakilisha uwepo wa Roho Mtakatifu ambaye alikuwa akimiminika kila siku na kusababisha uhai na uwepo wa nuru katika maisha na ustawi wa watu wake, lakini katika maono ya Yohana taa hii ilikuwa inawakilisha makanisa saba yaliyokuwa katika Asia ndogo yakiwakilisha uwepo wa Mungu duniani, kanisa ni nuru ya ulimwengu ndio ujumbe mahususi uliokuwa unatolewa na kinara hiki na kama kikiondolewa maana yake kutakuwa na giza kuu!

Ufunuo 1:19-20 “Basi, uyaandike mambo hayo uliyoyaona, nayo yaliyopo, na yale yatakayokuwa baada ya hayo. Siri ya zile nyota saba ulizoziona katika mkono wangu wa kuume, na ya vile vinara saba vya dhahabu. Zile nyota saba ni malaika wa yale makanisa saba; na vile vinara saba ni makanisa saba.”

Kwa msingi huo tunapozungumzia maana ya kinara, tunazungumzia wajibu mzima wa kanisa, katika kuondoa giza duniani, katika kuifanya kazi ya ukuhani na upatanisho kwa watu na Mungu, kazi ya kanisa ni kusimamia ustawi wa jamii kimwili, na kiroho na kisaikolojia, ukuaji wa watu wa Mungu, uwepo wa Roho Mtakatifu na ustawi wa kiroho wa watu wa Mungu na uwezo au nguvu ya kanisa kuwaondoa watu katika giza na kuwaleta katika nuru, unaona?

Kuondolewa kwa kinara cha Kanisa katika mahali pake.

Katika waraka wake kwa Kanisa Yesu Kristo mwenyewe aliliandikia Barua Kanisa la Efeso kupitia Mtume Yohana katika kitabu cha ufunuo akiwa na uelewa kamili wa mambo yote mazuri yaliyokuwa yakifanywa na kanisa hilo, lakini vile vile alilionya kanisa hilo kuwa limeuacha upendo wa kwanza na kuwaonya kuwa endapo hawatatubu atakiondoa kinara cha kanisa hilo mahali pake, Kanisa hili lilikuwa na mambo mengi mazuri, na Yesu aliyatambua hayo yote lakini kulikuwa na onyo kali NITAKIONDOA KINARA CHAKO MAHALI PAKE kama usipotubu!

Ufunuo 2:1-6 “Kwa malaika wa kanisa lililoko Efeso andika; Haya ndiyo anenayo yeye azishikaye hizo nyota saba katika mkono wake wa kuume, yeye aendaye katikati ya vile vinara saba vya dhahabu. Nayajua matendo yako, na taabu yako, na subira yako, na ya kuwa huwezi kuchukuliana na watu wabaya, tena umewajaribu wale wajiitao mitume, nao sio, ukawaona kuwa waongo; tena ulikuwa na subira na kuvumilia kwa ajili ya jina langu, wala hukuchoka. Lakini nina neno juu yako, ya kwamba umeuacha upendo wako wa kwanza. Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu, Lakini unalo neno hili, kwamba wayachukia matendo ya Wanikolai, ambayo na mimi nayachukia.”

Mji wa Efeso ulikuwa ni mji mkubwa na wenye bandari, ujenzi na maendeleo makubwa sana katika Uturuki (Turkey) ya kale, mji huu kwa sasa umehifadhiwa kama mjawapo ya miji ya kale ambayo ni urithi wa dunia na shirika la kimataifa liitwalo UNESCO, mji huu uko magharibi ya Uturuki zamani Ugiriki, ulikuwa ni moja ya miji mikubwa ya kale na mji uliokuwa na Ukristo wenye nguvu wakati wa utawala wa Kirumi.

Kabla ya wokovu katika mji huu, ulikuwa ni mji uliogubikwa na ibada za sanamu, miungu ya kipagani, dini za kienyeji Aminism na Hekalu kubwa la mungu mke aliyejulikana kama Artemis, au Diana, Hekalu hilo kubwa lilivunja rekodi za kiujenzi na maajabu na kuingizwa katika rekodi ya maajabu saba ya kale ya dunia, Atemi alikuwa ni mungu wa maswala ya uzazi, kwa hiyo alikuwa ni mungu mke “goddess” na wafua vyuma wa Efeso waliyeyusha vyuma na kutengeneza sanamu ndogo ndogo za Artemis na kuziuza na kupata faida kubwa sana, Injili ilipoingia jamaa hawa walipata hasara kwani watu walimgeukia Mungu aliye hai na sananu zikakosa biashara, uganga na uchawi ukapoteza soko. Miji ikapunduliwa na mageuzi makubwa na mioyo ya watu kuacha ibada za miungu na kumgeukiza Yesu Kristo!

Matendo 19:33-38 “Wakamtoa Iskanda katika mkutano, Wayahudi wakimweka mbele ya watu. Iskanda akawapungia mkono, akitaka kujitetea mbele ya wale watu. Lakini walipotambua ya kuwa yeye ni Myahudi, wakapiga kelele wote pia kwa sauti moja kwa muda wa kama saa mbili, wakisema, Artemi wa Waefeso ni mkuu. Na karani wa mji alipokwisha kuwatuliza watu, akasema, Enyi wanaume wa Efeso, ni mtu gani asiyejua ya kuwa mji wa Efeso ni mtunzaji wa hekalu la Artemi, aliye mkuu, na wa kitu kile kilichoanguka kutoka mbinguni? Basi kwa kuwa mambo haya hayawezi kukanushwa, imewapasa kutulia; msifanye neno la haraka haraka. Kwa maana mmewaleta watu hawa, wasioiba vitu vya hekalu wala kumtukana mungu mke wetu. Basi ikiwa Demetrio na mafundi walio pamoja naye wana neno juu ya mtu, baraza ziko, na maliwali wako; na washitakiane.”

Kanisa katika mji wa Efeso lilianzishwa na Paulo katika safari yake ya tatu ya kitume na watu wengi waliokolewa na kumpokea Yesu huku wakidhihirisha matendo yao kwa kuchoma vitabu vyao vya uganga (uchawi) na kukubali mabadiliko.

Matendo 19:18-20 “Na wengi wa wale walioamini wakaja wakaungama, wakidhihirisha matendo yao. Na watu wengi katika wale waliotumia mambo ya uganga wakakusanya vitabu vyao, wakavichoma moto mbele ya watu wote; wakafanya hesabu ya thamani yake, wakaona ya kwamba yapata fedha hamsini elfu. Hivyo ndivyo neno la Bwana lilivyozidi na kushinda kwa nguvu.”

Paulo mtume alikaa Efeso kwa karibu miaka mitatu akiifanya kazi kubwa sana ya kuwafundisha na kuwaimarisha na kuwaonya kuwa utakuja wakati ambapo mbwa mwitu wakali wataingia na hawatakuwa na huruma dhidi ya Kanisa!

Matendo 20:28-31. “Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe. Najua mimi ya kuwa baada ya kuondoka kwangu mbwa-mwitu wakali wataingia kwenu, wasilihurumie kundi; tena katika ninyi wenyewe watainuka watu wakisema mapotovu, wawavute hao wanafunzi wawaandamie wao. Kwa hiyo kesheni, mkikumbuka ya kwamba miaka mitatu, usiku na mchana, sikuacha kumwonya kila mtu kwa machozi.”

Baadaye Kanisa hili alilisimamia Timotheo ili kukemea mafundisho potofu yaliyoletwa na baadhi ya waamini tofauti na injili halisi iliyokuwa imehubiriwa na kufundishwa na Paulo Mtume Hivyo Timotheo alitumwa kwa kusudi la kulichunga na kulitunza Kanisa hilo zuri la Efeso. Kwa hiyo unaweza kupata picha kuwa lilikuwa, Kanisa imara kiimani

 

1Timotheo.1:1-3. “Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu na Kristo Yesu, taraja letu; kwa Timotheo, mwanangu hasa katika imani. Neema na iwe kwako, na rehema, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Bwana wetu. Kama vile nilivyokusihi ukae Efeso, nilipokuwa nikisafiri kwenda Makedonia, ili uwakataze wengine wasifundishe elimu nyingine;”

 

Kwa ujumla lilikuwa ni Kanisa zuri, Yesu analisifia kuwa walikuwa na bidii, walikuwa wavumilivu, hawakuvumilia uovu, walikemea dhambi, walikuwa na uwezo wa kuwajaribu wao waliojiita kuwa mitume kwa hiyo kulikuwa na uwezo mkubwa wa kupambanua mafundisho ya kweli na potofu, hawakuchukuliana na mafundisho ya Wanikolao ambao waliamini kuwa Mwanamke ni kwaajili ya jamii na sio mali  ya mtu binafsi “Woman is For social not Personal” Pia Wanikolai walifundisha kuwa mtu anaweza kuwa ameokoka lakini akashiriki maswala na maisha yote ya kipagani na hata ibada za miungu bila shida, walifundisha kuwa zinaa na uasherati hauathiri maswala ya kiroho, Yesu alionyesha kuchukizwa na fundisho hilo lisilozingatia usafi na Kanisa la Efeso pia walilikataa fundisho hilo,

 

Ufunuo 2:14-16 “Lakini ninayo maneno machache juu yako, kwa kuwa unao huko watu washikao mafundisho ya Balaamu, yeye aliyemfundisha Balaki atie ukwazo mbele ya Waisraeli, kwamba wavile vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na kuzini. Vivyo hivyo wewe nawe unao watu wayashikao mafundisho ya Wanikolai vile vile. Basi tubu; na usipotubu, naja kwako upesi, nami nitafanya vita juu yao kwa huo upanga wa kinywa changu.”

 

Efeso lilikuwa ni Kanisa lenye subira hawakuchoka katika kusubiri kurudi kwa Kristo huku wakijiandaa na kuwa tayari, kwa hiyo lilikuwa ni Kanisa lililoonyesha kumpenda Mungu sana huku wakisubiria kurudi kwa Yesu  

 

Historia ya Kanisa inaonyesha kuwa baadae Mtume Yohana aliishi katika mji huu na ndiko alikoandika injili yake ijulikanayo kama injili ya Yohana na aliishi na Mariamu mama yake Yesu maili chache kiasi na ambako ndiko kulikuwa makazi yake ya mwisho.              

 

Waefeso waliipokea Injili kwa nguvu kubwa na kwa upendo mkubwa sana, waliihubiri injili kwa watu wote, walihakikisha kuwa watu wote wanaokolewa, walijitoa katika maombi, walijitoa katika mafundisho, walikuwa wakarimu na watu waliosaidiana na kupitia wao ushuhuda wa Kristo ulienea sana Efeso ulikuwa nuru ya Asia ndogo kwa wakati ule na kwa kweli ushuhuda wao ulikuwa wa msingi na wa muhimu ni Kanisa la Kwanza kutajwa na Yesu katika waraka wake.

 

Yesu analionya Kanisa hili kuwa walikuwa wameuacha upendo wa Kwanza, maana yake ile nguvu ya upendo wa ndani (zeal) waliyokuwa wameanza nayo, kule kujitoa na ule upendo na bidii waliyokuwa nayo katika kumpenda Yesu ilikuwa imetoweka na wameanza kupoa maswala mengi sasa yalianza kufanyika kama mazoea na taratibu za kawaida na wala haikuwa kutoka moyoni, mambo yalikuwa yanaendeshwa kitaasisi tu na katika hali ya kawaida ya taratibu za kawaida. Kanisa hili lilianzishwa kati ya mwaka 53-56 Baada ya Kristo na waraka wa Yesu kutoka kitabu cha Ufunuo uliandikwa kati ya mwaka wa 95-96 Baada ya Kristo kwa hiyo ni kati ya miaka 40-43 tayari kanisa hili lilianza kupoteza ladha yake na kile walichokuwa wamekipokea mimi sijui kanisa lako lina miaka mingapi? Unaweza kuchungulia historia ya kanisa lako na ukapata picha kuwa je ule moto, ile nuru, ule uwepo, ile kiu na ule uwakilishi na ule ushawishi wa kanisa hapa duniani kama kinara bado unaendelea kuwepo? Si kanisa lako tu je wewe mwenyewe na mimi pia tuna muda gani katika wokovu na katika huduma ulikuwaje miaka kadhaa iliyopita na sasa ukoje? Muulize jirani yako hapo KINARA bado kipo? Au kimeondolewa? Ni jambo la kusikitisha kuwa eneo hili la Efeso leo sasa hakuna Ukristo ni eneo linalotawaliwa na Uislamu katika nchi ya Uturuki, kila mahali imekuwa misikiti, mpaka kwenye viwanja vya ndege, Waturuki wa leo hawa tunaweza kusema ni wajukuu wa waliokuwa wakristo zamani! tukipoa, tukiuacha upendo wa kwanza tukibaki na desturi za kawaida tu za kidini nataka nikuhakikishie kuwa Yesu atatuacha gizani, ataondoa mafuta, ataondoa ukuaji, ataondoa ukomavu, ataondoa Baraka zake kwa kanisa na giza kubwa litaingia, lakini sio hivyo tu atainua wengine watakaojali, kwa sababu yeye kusudi lake ni lazima litimie, Yesu alikuwa hatanii alikuwa akitoa maonyo halisi ambayo yanaweza kulihusu kanisa la leo, chuja kweli, acha kukemea dhambi, acha desturi za kawaida ziendelee katika kanisa, kinara kitaondolewa na tutapoteza ushawishi katika jamii na dini za uongo zitachukua nafasi, Kanisa ni lazima tujitathimini kila mmoja wetu ajitathimini na kuchukua hatua kwani kama tusipotubu kinara kitaondolewa mahali pake, ujumbe huu wa toba ni kwa kanisa la kila mahali na ni ujumbe kwa kila mtu, Kanisa likiacha kuwaambia watu ukweli, Mungu atatuacha na atatafuta njia nyingine mbadala na kusudi lake litaendelea nimeshuhudia kwa macho yangu Mungu akiyaacha baadhi ya makanisa  na Mungu akiwaacha wachungaji kwa sababu watu hawataki mabadiliko na wanataka kung’angami mapokeo yao, Yesu anajua ni wapi alipokutoa na anajua ni njia gani unapaswa kutembea nayo na anajua wapi tumepungua ni wakati wa toba kwa kila mmoja kila mahali ambapo tumepungua tunapaswa kufanya marekebisho haraka, liko wapi leo kanisa la Ulaya, liko wapi leo Kanisa la Marekani?, iko wapi leo Ufaransa nchi iliyokuwa na ushawishi mkubwa kutokana na misimamo ya Kikristo, Yesu ni mkali sana linapokuja swala la Kanisa lake ni lazima tusimame imara!

 

Ufunuo 2:2-5 “Nayajua matendo yako, na taabu yako, na subira yako, na ya kuwa huwezi kuchukuliana na watu wabaya, tena umewajaribu wale wajiitao mitume, nao sio, ukawaona kuwa waongo; tena ulikuwa na subira na kuvumilia kwa ajili ya jina langu, wala hukuchoka. Lakini nina neno juu yako, ya kwamba umeuacha upendo wako wa kwanza. Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu.”

Hatupaswi kuvumilia mafundisho ya uongo, hatupaswi kupoa, hatupaswi kuacha kuitetea imani, hatupaswi kuvumilia uasherati, hatupaswi kuwa na jina la uhai huku tumekufa, hatupaswi kujivunia dhehebu letu na kuacha kujivunia Yesu Kristo, hatupaswi kuliozea neno, hatupaswi kulipua lipua ibada wala maandalizi yake, hatupaswi kuwa vuguvugu, hatupaswi kujidhani ya kuwa sisi ni matajiri na kuacha kumtegemea Mungu kumbe kiroho ni masikini, hatupaswi kuacha upendo wa Kwanza maonyo haya yote ambayo Yesu alilionya Kanisa yanaweza kusababisha kinara kiondolewe kama hatutazingatia; Bwana atupe neema kinara kisiondolewe mahali pake katika jina la Yesu Kristo!

Mambo ya kufanya ili kinara kisiondolewe.

Kimsingi Yesu hakuwa anazungumza na Kanisa la Efeso pekee, onyo kwa kanisa la Efeso na mengineyo ni kwa kila mmoja wetu na ni ujumbe kwaajili ya kizazi chetu kwa hiyo kila mmoja wetu hana budi kujiuliza kama anavyompenda Kristo leo ndio namna ile ile alivyokuwa anampenda zamani, je unahuzunika kiasi gani leo watu wanapopotea bila wokovu, je unahuzunika kiasi gani leo watu wanaporudi nyuma, je unawapa vyeo watu kwa sababu ya hali ya kiroho au kwa sababu ya fedha, je tunaishi maisha matakatifu leo au tumepoa, je huduma zetu zinatokana na upendo au kwaajili ya kulinda maslahi yetu, Je Kristo anapendezwa na maisha yetu na Kanisa letu? Tunajivunia Kristo au historia yetu? Tunajivunia majengo huku tumempoteza Kristo? Tunajivunia idadi huku tumeacha upendo wa kwanza, tuna shughuli nyingi kuliko kuutafuta uwepo wa Mungu; Mungu hajafunga mlango, analitaka kanisa ligeuke na kutubu lirudie matendo yake ya Kwanza vinginevyo kinara kitaondolewa ni jambo la kusikitisha kama tutakuwa na Historia nzuri mbele ya wanadamu lakini Kristo akapoteza nafasi yake katika mioyo yetu, Kanisa lisipimwe tu kwa ukubwa wa idadi ya watu lakini lipimwe kwa ukuaji wa upendo wa Mungu na kiu ya watu kuishi maisha matakatifu, ukomavu wa kiroho na kuzaa matunda ya roho, Kanisa lisipimwe kwa mafanikio ya vitu vya nje tu japo tunavihitaji, lakini lipimwe kwa nuru inayowaangazia wasio na matumaini, kanisa lisipimwe kwa wingi wa shughuli lakini lipimwe kwa wingi wa wale wanaoketi miguuni pa Yesu na kumsikiliza na kuyatendea Kazi yote aliyotuagiza. Tukifanya hayo na kuyazingatia Kinara cha kanisa letu hakitaondolewa mahali pake na tutaendelea kuwa Nuru ya ulimwengu! 

Ufunuo 2:1-6 “Kwa malaika wa kanisa lililoko Efeso andika; Haya ndiyo anenayo yeye azishikaye hizo nyota saba katika mkono wake wa kuume, yeye aendaye katikati ya vile vinara saba vya dhahabu. Nayajua matendo yako, na taabu yako, na subira yako, na ya kuwa huwezi kuchukuliana na watu wabaya, tena umewajaribu wale wajiitao mitume, nao sio, ukawaona kuwa waongo; tena ulikuwa na subira na kuvumilia kwa ajili ya jina langu, wala hukuchoka. Lakini nina neno juu yako, ya kwamba umeuacha upendo wako wa kwanza. Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu, Lakini unalo neno hili, kwamba wayachukia matendo ya Wanikolai, ambayo na mimi nayachukia.”

 

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Hakuna maoni: