Alhamisi, 28 Januari 2016

Mwanadamu ni nini hata Umkumbuke?



Ujumbe: Mwanadamu ni nini hata Umkumbuke?
(“What is Man that You Are Mindful of Him?”).
“Waebrania 2:5-8”Zaburi 8:3-4”

Ni muhimu kwetu kwa kila mmoja wetu kujiuliza, kuwa katika akili zetu ni nani tunampa kipaumbele kikuu kila siku? Tunaweza kuhisi kuwa wengi wa wale tunaowapa kipaumbele kwanza wanaweza kuwa ni wana familia zetu, wapenzi na marafiki na labda Mungu!
Au kama kuna mtu mwingine uneyeweza kumpa kipaumbele zaidi anaweza kuwa mtu unayemchukia, adui yako anayekusumbua na kukunyima raha, Kwa kawaida tunapenda kufikiri vile vyenye umuhimu katika maisha yetu na vile visivyona umuhimu au mguso tunaweza kuvipuuzia na kuvitupa kando.  Ni uwazi ulioje kuwa kuweko kwa Mungu kumekuwa ni kama dhana inayofikiriwa kuwa ni ya kusadikika tu, wengi wetu kwa ndani sana tunaweza kufikiri kuwa Mungu hayuko na hajishughulishi na chochote kuhusu wanadamu na hususani tunapopitia nyakati ngumu tunafikiri kama Mungu yupo kweli angelitazama hili bila kushughulika nalo?
Wagiriki wengi walikuwa hawaamini katika Mungu na hivyo walikuwa na miungu mingi dhana kuhusu Mungu haikuwa halisi katika maisha yao na hivyo waliabudu miungu mingi ili kutafuta msaada na kutafuta kuwezeshwa na miungu hiyo baadhi ya miungu yao ni kama hii

1.      Aphrodite alikuwa Mungu wa Mapenzi
2.      Apollo alikuwa Mungu wa Music na Uponyaji
3.      Ares alikuwa Mungu wa Vita
4.      Athena alikuwa Mungu mke bikira na mungu wa Hekima
5.      Hermes alikuwa Mungu wa Ujumbe
Pamoja na miungu kadhaa wa kadhaa

Biblia inatufundisha kwamba Mungu tunayemuabudu yeye ni wa tofauti kabisa ni Mungu anayemjali mwanadamu na kujishughulisha naye bila kujali hali yake, kwamba ni msomi au mjinga ni masikini aua tajiri, mweusi au mweupe ni wahali ya juu au ya chini, ni mwanamke au mwanamume, ni mtakatifu au ni mwenye dhambi, Mungu anapendezwa na Mwanadamu sana, Watakatifu waliotutangulia waliona upendo huu wa Mungu kwa ndani sana akijishughulisha na wanadamu kwa namna ya kupita kawaida Katika tafakari zake mfalme Daudi alifikiri hivi? Na kujiuliza maswala haya hasa baada ya kugundua namna Mungu anavyomjali Mwanadamu

Waebrania 2: 5-8 “Maana hakuuweka chini ya malaika ulimwengu ule ujao tunaounena, ila mtu mmoja ameshuhudia hivi mahali fulani, akisema, 6. Mwanadamu ni nini hata umkumbuke, Ama mwana wa binadamu, hata umwangalie? 7. Umemfanya mdogo punde kuliko malaika, Umemvika taji ya utukufu na heshima, Umemtawaza juu ya kazi za mikono yako;  8. Umeweka vitu vyote chini ya nyayo zake. Kwa maana katika kuweka vitu vyote chini yake hakusaza kitu kisichowekwa chini yake. Lakini sasa bado hatujaona vitu vyote kutiwa chini yake.”

Katika Mistari hiyo hapo juu kuna maswala Matatu Muhimu ambayo Mungu anamfanyia mwanadamu kuonyesha namna alivyomthamini “Hata umkumbuke” “Hata Umwangalie” “Umemtawaza juu ya kazi za mikono yako” haya yanadhihirisha uthamani na upendo mkuu wa Mungu wetu kwetu.
           
1.      Mungu humkumbuka Mwanadamu “Mindful of Him”.
Biblia inaushahidi mwingi unaodhihirisha kuwa sisi ni wa thamani machoni pa Mungu na kuwa Mungu anatuwazia sisi kama kipaumbele chake hata kama sisi hatumjali  na kumuheshimu yeye alituumba kwa  mfano wake alitupenda mno Zaburi 8:3 Isaya 43:4. Biblia inathibitisha kuwa Mungu hajatuacha wala hatatusahau, anatuhurumia na kuwa ametuchora katika vitanga vya mikono yake Isaya 49:15-16 Kama ilivyongumu kwa Mama kumsahau mtoto wake anyonyaye ndivyo ilivyo na kwa Mungu wetu.Ndugu yangu Mungu hajakusahau Mungu hajakutupa Umejaa katika wazo la Mungu.

2.      Mungu humwangalia Mwanadamu “Care of Him”
Licha ya Mungu kujawa na binadamu katika akili zake ni muhimu pia kufahamu kuwa Mungu anakuangalia!, anajali Mungu anapokuangalia anajisikia kukufanyia mambo makubwa sana anaguswa na maumivu yako na huzuni ulizonazo na anajali Luka 7:11-16 Hataweza kukuachia hata umezwe na huzuni na jaribu kuliko uwezo wako ataingilia kati na kuleta faraja Kama alivyo mfanyia mjane huyu katika Luka na watu wakakiri kuwa Mungu amewaangalia watu wake tunaye Mungu ambaye huangalia.

3.      Umemtawaza juu ya kazi zako “ You put everything under his feet”
Mungu ameweka kila kitu chini ya miguu yetu, ametupa kutawala, ametiisha hata malaika hutuhudumia mwanadamu ametukuzwa na Mungu kwa kiwango kikubwa cha kifalme Luke 10:18-19 Mungu ametiisha kila kitu chini yetu hatupaswi kuogopa, tunapaswa kuelewa jinsi Mungu anavyotujali, anavyotukumbuka na anavyotuangalia  na uwezo aliotupa, Mungu anapendezwa na wanadamu kuliko hata malaika, waoa wanatajwa kama roho wanaotumwa kuwahudumia wale watakaourithi wokovu Waebrania 1:13-14. Kama ikiwa Mungu anatujali kwa kiwango hiki………

Swali la Kumalizia ni kuwa wewe je unampa Mungu kipaumbele? Umamuheshimu, Unamuogopa au unamvunjia Heshima?
Mwandishi wa zaburi alikaa chini akatafakari na kugundua kuwa mwanadamu ni sehemu ndogo  sana ya uumbaji wa Mungu, ndogo mmno lakini akajiuliza swala kwa vipi Muumba anatoa nafasi kubwa kwa wanadamu? Daudi mwandishi wa zaburi hii alikuwa anaona kwa Mbali jinsi Kristo atakavyoacha enzi na utukufu na vyote na kuja kumkomboa mwanadamu kwa Damu yake ya Thamani jambo linalotudhihirishia Uthamani mkubwa sana alio nao mwanadamu, swali
Mwanadamu ni nani hata umkumbuke? Kamwe hatuwezi kutambua uthamani wetu kama Mungu sio Kipaumbele cha Maisha yetu Kadiri tunavyojifunza kuhusu Mungu ndivyo tunatambua uthamani wetu na kusudi la kuweko kwetu duniani.
Yeye aligharimika mno kwaajili yetu Yohana 3:16 Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda Ulimwengu” Biblia ya kiyunani ingesomeka hivi Katika namna isiyoweza kuelezeka Mungu aliipenda Dunia iliyojawa na uasi na udhalimu na desturi zenye kila aina ya machukizo “Cosmos” hata akamtoa mwanae wa Pekee, Maisha yetu yamegharimu Damu ya Yesu
“Wewe sio matokeo ya vile watu wanavyosema wewe ni matokeo ya vile Mungu anavyosema”
Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote.

LAWEZA NENO JEMA KUTOKA NAZARETHI ?


(CAN ANYTHING GOOD COME OUT OF NAZARETH?)

 Nazareth
 
ANDIKO LA MSINGI: Yohana 1:43-46. Biblia inasema hivi
“43. Siku ya pili yake alitaka kuondoka kwenda Galilaya, naye akamwona Filipo. Yesu akamwambia, Nifuate. 44. Naye Filipo alikuwa mtu wa Bethsaida, mwenyeji wa mji wa Andrea na Petro. 45. Filipo akamwona Nathanaeli, akamwambia, Tumemwona yeye aliyeandikiwa na Musa katika torati, na manabii, Yesu, mwana wa Yusufu, mtu wa Nazareti. 46. Nathanaeli akamwambia, Laweza neno jema kutoka Nazareti? Filipo akamwambia, Njoo uone.”

Ni muhimu kufahamu kuwa Nazareth ulikuwa ni mji mdogo uliokuwa kusini mwa jimbo la Galilaya (Lower Galilee), Mji huu ulikuwa ni moja ya miji iliyodharauliwa sana, kwa ujumla Israel ilikuwa na majimbo makuu Matatu, Yuda, Samaria na Galilaya, Yuda ndio eneo ambalo liliheshimika sana hususani kwa kuwa lilikuwa ni eneo lililotoa manabii na viongozi wakubwa na walioonyesha utii na uwezo wa kumuamini na kumtegemea Mungu, maeneo yaliyofuata kama Galilaya na Samaria hayakuwa maeneo yaliyopewa heshima wala kipaumbele kutokana na historia zake za kuongoza katika ibada za Sanamu, watu wasioshika dini  viongozi waovu na wasiomcha Mungu, hivyo Galilaya ilidharaulika na kuonekana kama miji isiyoweza kutoa neno Jema.

Aidha kwa habari ya Kumtazamia masihi ni wazi pia ilijulikana kuwa Masihi angekuja kutokea Uyahudi yaani Yuda katika mji wa Daudi Bethelehemu kwa vile nabii Mika alitabiri hivyo Mika 5:2 Biblia inasema “Bali wewe, Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele.” Marabi na wataalamu wote wa Maandiko na wajuzi na wanasheria wa kiyahudi wote walikuwa wanatambua wazi unabii huu na kukubali kuwa Masihi angetokea Bethelehemu Mathayo 2:1-6 Biblia inasema hivi:- “1. Yesu alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama, mamajusi wa mashariki walifika Yerusalemu, wakisema, 2. Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia. 3. Basi mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na Yerusalemu pia pamoja naye. 4. Akakusanya wakuu wa makuhani wote na waandishi wa watu, akatafuta habari kwao, Kristo azaliwa wapi? 5. Nao wakamwambia, Katika Bethlehemu ya Uyahudi; kwa maana ndivyo ilivyoandikwa na nabii, 6. Nawe Bethlehemu, katika nchi ya Yuda, Hu mdogo kamwe katika majumbe wa Yuda; Kwa kuwa kwako atatoka mtawala Atakayewachunga watu wangu Israeli.”

Unaweza kuona ni kwa sababu na msisitizo mkuu ilikuwa ngumu kwa Mwanafunzi kama Nathaeli kuamini kuwa Yeye aliyetabiriwa na Musa na manabii kama angeweza kutokea Nazareth
Kwa ujumla Nazareth ulikuwa ni mji usioheshimika na uliongoza kwa umasikini na mmomonyoko mkubwa wa uadilifu, watu wasiomcha Mungu waabudu sanamu na kimji hiki hakikuwahi kabisa kutajwa katika unabii wa agano la kale, mtu aliyetokea Nazareth alionekana sawa tu na mtu aliyetokea Mbagala, au Gongo la Mboto au manzese tofauti na Ostabey au sinza ni sawa na mtu akikuambia unatokea Kwatango, au kilosa au mbulizaga kule Pangani, au kwa msisi huko Handeni, au Nchebebwa huko Newala au Naluleo huko Liwale, Nazareth na Galilaya ilidharaulika ilikuwa mtu akikuita wewe ni mgalilaya au Mnazareth ilikuwa ni Lugha ya dharau ya hali ya juu Yohana 7: 40-42, 52. Biblia inaonyesha jinzi ambavyo maadui wa Yesu Kristo pia waliutumia mji huu.

Mathayo anajaribu kuonyesha kuwa uko unabii, ulioashiria kuwa Yesu ataitwa Mnazareth Mathayo 2:19-23 unabii huu kwa undani, unabii huu unatokana na Mathayo kuunganisha Isaya 11: 1 ambao kuna neno shina na Chipukizi neno hili kwa kiebrania husomeka kama “NETSER” kwa Kiingereza Shoot au Root yaani shina hili ndio asili ya Jina Nazareth.

Ni muhimu kufahamu kuwa katika somo hili tunajifunza kuwa Mungu huweza kuinua mtu kutoka katika Hali ya kudharaulika, ingawa kijiji cha Nazareth kilidharaulika lakini kilipoungwa na jina la Yesu kilipata umaarufu mkubwa sana, Yesu mwenyewe alikubali kuitwa Yesu wa Nazareth, Majini na Mapepo yakitajiwa Yesu wa Nazareth yanalia kwa nguvu mitume walipoombea waginjwa na kufanya miujiza mara kwa mara walilitumia jina la Yesu Kristo wa Nazareth hivyo Nazareth leo umekuwa ni mji maarufu

Awaye yote bila kujali umetokea ukoo gani, kabila gani, dini gani, jamii gani ukiunganishwa na Yesu Kristo historia yako inabadilishwa hata kama ulikuwa mnyonge kiasi gani utakuzwa na utatiwa nguvu na utatumiwa na Mungu kwa namna ya kipekee Nazareth leo ikitajwa kila mtu anajua ni moja ya miji ambayo Bwana Yesu alilelewa na kukulia
Mungu alitaka  Jina hili dhaifu na lililodharauliwa  liunganishwa na jina la Mwanae Mpendwa  na kufuta Historia mbaya ya Jimbo la Galilaya, Filipo alimwambia Nathanael njoo uone, Mtu akiunga na Yesu hwi wa kawaida Maisha yake yanabadilishwa na Historia yake inakuwa mbaya na adui zako wataisoma Namba.
Na Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima!
Rev. Innocent Kamote.

^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^

UJUMBE: KWENDA KATIKA NJIA YA KAINI



Neno la Mungu linatuonya na kututahadharisha kutokwenda katika njia ya Kaini Yuda 1:11 Biblia inasema Hivi “Ole wao! Kwa sababu walikwenda katika njia ya Kaini” Hapo sio mahali pa kupita hivihivi kwa sababu Yuda Ndugu yake Bwana analionya kanisa kutokwenda katika njia ya Kaini, Onyo hili kwa Yuda liliwahusu hasa walimu wa Uongo kwa nyakati zile, lakini tutakapokuwa tunaichunguza njia ya Kaini tutagundua Maonyo makuu kwa kila mtu. Bwana ampe neema kila mmoja wetu kutokuifuata njia hii ya Kaini kwa namna yoyote Katika Jina la Yesu.
 

Utangulizi
Kaini alikuwa ni Mtoto wa kwanza wa Adamu na Hawa Mwanzo 4:1, Jina lake kwa kiingereza ni “ACQURE” ambalo maana yake kwa kiingereza ni “To gain something by your own effort” yaani kupata kitu/vitu kwa juhudi zako mwenyewe! Biblia inatuonya kutokuifuata njia ya Kaini Kulikoni? Ni muhimu sasa tukifuatilia kwa makini sana alifanya nini ili yamkini tusijikute tukifuata mfano wake.

1.     Hakuabudu Katika njia ya Mungu
Ni muhimu kufahamu kuwa mapema sana Mungu alikuwa amewafundisha Adamu na Hawa namna wanavyoweza kumfikia Mungu na kumuabudu ni wazi kuwa pasipo damu ni vigumu kumfikia Mungu, Ni imani yangu kuwa Adamu na Hawa waliwafunza watoto wao namna ile ambayo Mungu aliwafundisha kumuabudu Mwanzo 3:21 Katika namna ya kusikitisha sana Kaini aliamua kumuabudu Mungu katika Iliyompendeza yeye mwenyewe! Mwanzo 4:3-5 Bwana aliikataa namna ya ibada aliyofanyiwa na Kaini, ni vema wanafunzi wa Biblia tukajikumbusha kwamba hatuwezi kumuabudu Mungu katika namna tunayojitakia Ibada ya kweli ni lazima izingatie maagizo na maelekezo ya Nneo la Mungu, ni lazima tujiulize namna tunavyoombea wagonjwa, tunavyotoa sadaka na kuzitumia na kujihoji  katika njia ya Mungu Kanisa la leo linasahau wajibu wa Kumuabudu Mungu katika njia iliyo sahii, kuabudu katika namna tunayojisikia wenyewe ni kufuata njia ya Kaini.
·         Nadabu na Abihu wana wa Haruni waliuawa na Mungu kwa kutokufuata utaratibu  ambao Mungu aliwaagiza Walawi 10:1-2
·         Mungu alimuazibu Uzza kwa kulishika na kusafirisha Sanduku la Agano kinyume na Agizo la Mungu 2Samuel 6:1-8
·         Mungu alimuadhibu Musa vikali kwa sababu ya kutokufuata maelekezo yake katika kuwapa maji Israel Hesabu 20:8-12, hii ilikuwa ni ibada ya maombezi kwaajili ya maji lakini kulikuwa na maelekezo, Mtaweka mikono juu ya wagonjwa nao watapata Afya na sio Miguu, wala kuwakanyaga watu leo hii ziko ibada za Maombezi ambazo wala Mungu hakuagiza, simuonei wivu mtu yoyote anayetumiwa na Mungu kwa Karama za uponyaji kwa sababu hata mie natumiwa, na ninapenda watu waponywe na wakati mwingine hata na mimi nahitaji kuombewa na wajenzi wenzangu Lakini kweli nikakanyagwe? Ndivyo Yesu alivyofanya? Ndivyo Yesu alivyoagiza? Musa hakuruhusiwa kuingia Kanaani, kwa sababu alifanya kwa namna anayotaka yeye hata ingawa maji yalitoka, yaani hata kama watu wanaponywa kwa jina lilelile lakini lazima tuhoji aina za ibada hizi za maombezi. Je ni maagizo ya Mungu? Muombezi anakupanda mgongoni kama msukule je ndivyo Yesu alivyoagiza, hatuwezi kukubali mbwembwe zisizo na kiasi kutawala ibada na kumtukanisha Mungu!
·         Mungu aliwaadhibu Anania na Safira kwa sababu hawakufuata maelekezo ya Mitume Matendo 5:1-10
Unaweza kuona sasa kwa nini Biblia inatuonya kutokuifuata njia ya Kaini? Ni wazi kuwa si kila aina ya ibada inakubalika kwa Mungu, lazima tufuate namna ile aliyotufundisha Kristo, Mtume Paul anawaonya wakolosai kutokufuata namna za ibada za kujitungia Wakolosai 2:23. Wakati umefika kwa kanisa kukataa namna za ibada ambazo zinatupotezea muda, Ibada yoyote ile ambayo haifuati maelekezo ya neno la Mungu ni bure Yesu alizikemea Ibada ambazo ni maagizo ya wanadamu Mathayo 15: 7-9, Mungu anatafuta watu watakao muabudu yeye katika Roho na kweli Yohana 4:23-24. Ndugu zangu ni lazima tuwe na tahadhari hasa katika nyakati hizi tulizo nazo wengi wameifuata njia ya Kaini sitaki kuhukumu Lakini kama mkuu wa wajenzi mwenye hekima nataka nikujenge katika neno utambue namna unavyoweza kumuabudu Mungu bila Madhara, Kaini alionyesha kutokumjali Bwana na kukosa Imani Waebrania 11:4 Mungu anachukizwa na namna ya ibada tulizojitungia
2.     Hakuamua kuishinda Dhambi
Njia nyingine ya Kaini ni kutokuamua kuishinda Dhambi, Mungu ametupa nguvu kubwa sana ya maauzi, tunaweza kutumia maamuzi yetu kutenda mema au kutenda mabaya Mwanzo 4:5-8. Mungu alimwambia Kaini ukitenda vema utapata kibali, usipotenda vema dhambi iko mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde. Mungu alimwambia Kaini hayo kwa sababu alijua kuwa uwezo huo uko ndani yake, watu nwengi sana wanapofanya Dhambi humsingizia shetani, huku ni kukataa kuwajibika nisikilize! Unawajibika kwa dhambi zako! Dhambi haitusukumi kuitenda mpaka tumeamua, na ndio maana unapofanya dhambi Mungu hamuhukumu Shetani anakuhukumu wewe, Kaini alimezwa na Dhambi na Badala ya kutubu aliongeza dhambi juu ya dhambi
·         Alikasirika - Mwanzo 4:5 Nafsi yake ilijawa na chuki dhidi ya Ndugu yake na dhidi ya Mungu, watu wengi hawajui kuwa Mungu anatuona mioyoni mwetu tunapokuwa tumejawa na chuki na kukasirika Mungu anaona, wengi wanafikiri kuwa Hasira sio dhambi, lakini ni dhambi, Kaini alishindwa kuonyesha Uvumilivu, huruma na wema na hata kuwa na moyo wa kusamehe, na  kwa ugumu wa Moyo dhambi hii ilimpelekea kuua, Musa alipata Hasara kwa sababu ya hasira na Ghadhabu Zaburi 106:32-33, Yeyote asiyeweza kuidhibiti nafsi yake katika Hasira yuko katika njia ya Kaini.
·         Alikuwa na wivu Mwanzo 4:4-5 Nafsi ya Kaini ilijawa na wivu, inakuwaje mtu usifurahie Mafanikio ya ndugu yako? Ndugu yako akibarikiwa ndio furaha yenu wote, Kaini hakufurahi kuona Habili anafanikiwa alitaka mazuri yawe yake mabaya yawe ya ndugu yake Mtu aliyeokoka vema hapaswi kuishi katika wivu (husuda) na chuki, jamani umeokoka inakuwaje unachuki? Unakuaje una wivu? Inakuaje una donge? Tito 3:3, kama una husuda hakuna sababu ya kujinyima pombe na zinaa kwa sababu njia ya watu hao ni moja tu Wagalatia 5:21 hakuna mtu mwenye husuda ataingia mbinguni, kama una wivu na husuda tubu kwa vile ninjia ya Kaini.
·         Alijawa na Chuki – Ni wazi kuwa Kaini hakuwa na Upendo kwani chuki ni kinyume cha upendo he hate his Brother!  Neno hate katika Dictionary ya Kiingereza linachambuliwa hivi
i.                    Animosity – strong feeling of Opposition Ni watu wasiotaka kukubali kuzidiwa ni wenye hisia kali ya kupinga hasa mafanikio ya kimwili na kiroho ya wengine
ii.                 Contempt – the feeling that something is without value Ni watu wenye hisia kudharau wengine na kuona hawana thamani tena
iii.               Disdain – The feeling that something is not good enough to deserve your respect or attention Hujawahi kuona watu wa aina hii hawakuoni kuwa ni mwema hata kidogo, hawakubali lolote jema ulifanyalo, wenye dharau, hawataki hata kukuona, lakini eti wanasema ni watu wa Mungu Chuki ni njia ya Kaini hakuna mtu mwenye kuifuata njia ya Kaini atakubaliwa na Mungu kama unachuki nab ado ukajiona salama unahitaji kujiangalia kwa upya 1Yohana 3: 11-12, 15. Kama unafikiri Chuki ni nyepesi soma 1Yohana 3:15 Biblia inasema hivi “ Kila amchukiaye Ndugu yake ni muuaji: nanyi mnajua ya kuwa kila muuaji hana uzima wa milele ukikaa ndani yake. Ndugu yangu leo tuna wauaji wengi kama Kaini tunaabudu nao makanisani, tunahudumu nao pamoja ni wauaji si kwa kukuchinja tu lakini wanaweza pia kukuua kwa kutumia maneno, wanakusema vibaya ili ikiwezekana ukose kibali kwa watu wanaokukubali huu ni uuaji nah ii ndio njia ya Kaini
·         Aliamua kuua – Mwanzo 4:8, Kwa asili uuaji wa kivitendo ni matokeo ya uuaji wa ndani yaani chuki, Biblia inasema Usiue Kaini aliamua kuua Katika mafundisho yake Yesu anaweka wazi kuwamauaji yanatoka Moyoni Marko 7:20-23
3.      Alijaribu kumdanganya Mungu
Mwanzo 4:9, Kaini ni kama hakuwa anahusika wala kujali wala kuwajibika kwa Maisha ya ndugu yake, Mungu alipomuuliza Yuko wapi ndugu yako alisema Sijui kwani mimi ni mlinzi wa Ndugu yangu? Mungu anatujua vema mpaka mioyoni mwetu kujaribu kumdanganya yeye ni kujidanganya wenyewe Waebrania 4:13 kila kiumbe kiko wazi mbele za Mungu, Hakuna mwanadamu ambaye hajapewa wajibu wa wanadamu wengine, hauwezi kwa namna yoyote ile kutokujali maisha ya wengine na ukajifanya unajali ya Mungu huko ni kujidanganya
i.                    Anania na Saphira hawakuweza kujificha mbele za Mungu
ii.                 Tunaweza kujikuta tukijidanganya wenyewe kwa kumdanganya Mungu kuwa
a.      Tukidai kuwa tunampenda Yeye huku tunawachukia ndugu zetu IYohana 4:20
b.     Kwa kutoa kidogo kuliko alivyotubariki
c.      Kwa madai kuwa tutafanya vizuri, tutatubu Lakini tunaishi katika njia zilezile za zamani
d.     Kuimba vizuri huku tunaishi maisha ya dhambi Waefeso 5: 19-21
Ni muhimu kukumbuka kuwa Mungu hadhihakiwi wala hadanganywi Wagalatia 6:7, waongo hawataweza kuepuka Hsira ya Mungu Ufunuo 21:8. Hii ni njia ya Kaini
4.     Aliachana na Uwepo (USO) wa Mungu Mwanzo 4:16
“So Cain went out from the Lord presence” Kaini aliona masiha ya kuongozwa na neno la Mungu na maelekezo yake yanamnyima uhuru, Hakukubali toba na badiliko la kweli katika maisha yake Mwanzo 4:7-8 lakini alijiombea tu asife na asitangetange hakusikiauchungu wala kutubia dhambi zake, Mungu alimuonyesha Huruma Mwanzo 4:15-16 lakini hata pamoja na wema wa Mungu, kwa vile ilikuwa afe, lakini Kaini aliondoka katika uwepo wa Mungu, Dhambi zote ikiwa ni pamoja na hizi za Kaini zinamtenga mwanadamu na uwepo wa Mungu Isaya 59:1-2 Kwa nini tuiruhusu dhambi iharibu uhusiano wetu na Mungu? Aliamua kuwa na Maisha yasiojali Mungu ili ajiongoze mwenyewe
Hitimisho:
Ni njia gani umechagua kuifuata? Hatuwezi kumdanganya Mungu, Hasira ni dhambi, wivu ni dhambi, chuki ni dhambi, kutokujali maisha ya wengineni dhambina ubinafsi, kuabudu katika namna tunayoitaka sisi ni dhambi, uadui ni dhambi na zote hizi ni njia za Kaini Je unachagua nini katika maisha yako? “Ee Mungu naomba unilinde na Mafundisho yangu mie mtumwa wako nishiishie kuwahubiri wengine mimi nikawa wa kukataliwa nisaidie nisiifuate njia ya Kaini nipe kuwa mkweli mbele zako na mbele za wanadamu naomba sana ee Mola wangu usiniache kuondoka katika uwepo wako, nisaidie niwarejeze na wengine katika njia zako asante kwa sababu fadhili zako ni za Milele naamini hujaniumba niwe chombo cha ghadhabu yako bali mfano wa Rehema zako na wokovu wako Amen”

Ndimi Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote.