Alhamisi, 28 Januari 2016

UJUMBE: KWENDA KATIKA NJIA YA KAINI



Neno la Mungu linatuonya na kututahadharisha kutokwenda katika njia ya Kaini Yuda 1:11 Biblia inasema Hivi “Ole wao! Kwa sababu walikwenda katika njia ya Kaini” Hapo sio mahali pa kupita hivihivi kwa sababu Yuda Ndugu yake Bwana analionya kanisa kutokwenda katika njia ya Kaini, Onyo hili kwa Yuda liliwahusu hasa walimu wa Uongo kwa nyakati zile, lakini tutakapokuwa tunaichunguza njia ya Kaini tutagundua Maonyo makuu kwa kila mtu. Bwana ampe neema kila mmoja wetu kutokuifuata njia hii ya Kaini kwa namna yoyote Katika Jina la Yesu.
 

Utangulizi
Kaini alikuwa ni Mtoto wa kwanza wa Adamu na Hawa Mwanzo 4:1, Jina lake kwa kiingereza ni “ACQURE” ambalo maana yake kwa kiingereza ni “To gain something by your own effort” yaani kupata kitu/vitu kwa juhudi zako mwenyewe! Biblia inatuonya kutokuifuata njia ya Kaini Kulikoni? Ni muhimu sasa tukifuatilia kwa makini sana alifanya nini ili yamkini tusijikute tukifuata mfano wake.

1.     Hakuabudu Katika njia ya Mungu
Ni muhimu kufahamu kuwa mapema sana Mungu alikuwa amewafundisha Adamu na Hawa namna wanavyoweza kumfikia Mungu na kumuabudu ni wazi kuwa pasipo damu ni vigumu kumfikia Mungu, Ni imani yangu kuwa Adamu na Hawa waliwafunza watoto wao namna ile ambayo Mungu aliwafundisha kumuabudu Mwanzo 3:21 Katika namna ya kusikitisha sana Kaini aliamua kumuabudu Mungu katika Iliyompendeza yeye mwenyewe! Mwanzo 4:3-5 Bwana aliikataa namna ya ibada aliyofanyiwa na Kaini, ni vema wanafunzi wa Biblia tukajikumbusha kwamba hatuwezi kumuabudu Mungu katika namna tunayojitakia Ibada ya kweli ni lazima izingatie maagizo na maelekezo ya Nneo la Mungu, ni lazima tujiulize namna tunavyoombea wagonjwa, tunavyotoa sadaka na kuzitumia na kujihoji  katika njia ya Mungu Kanisa la leo linasahau wajibu wa Kumuabudu Mungu katika njia iliyo sahii, kuabudu katika namna tunayojisikia wenyewe ni kufuata njia ya Kaini.
·         Nadabu na Abihu wana wa Haruni waliuawa na Mungu kwa kutokufuata utaratibu  ambao Mungu aliwaagiza Walawi 10:1-2
·         Mungu alimuazibu Uzza kwa kulishika na kusafirisha Sanduku la Agano kinyume na Agizo la Mungu 2Samuel 6:1-8
·         Mungu alimuadhibu Musa vikali kwa sababu ya kutokufuata maelekezo yake katika kuwapa maji Israel Hesabu 20:8-12, hii ilikuwa ni ibada ya maombezi kwaajili ya maji lakini kulikuwa na maelekezo, Mtaweka mikono juu ya wagonjwa nao watapata Afya na sio Miguu, wala kuwakanyaga watu leo hii ziko ibada za Maombezi ambazo wala Mungu hakuagiza, simuonei wivu mtu yoyote anayetumiwa na Mungu kwa Karama za uponyaji kwa sababu hata mie natumiwa, na ninapenda watu waponywe na wakati mwingine hata na mimi nahitaji kuombewa na wajenzi wenzangu Lakini kweli nikakanyagwe? Ndivyo Yesu alivyofanya? Ndivyo Yesu alivyoagiza? Musa hakuruhusiwa kuingia Kanaani, kwa sababu alifanya kwa namna anayotaka yeye hata ingawa maji yalitoka, yaani hata kama watu wanaponywa kwa jina lilelile lakini lazima tuhoji aina za ibada hizi za maombezi. Je ni maagizo ya Mungu? Muombezi anakupanda mgongoni kama msukule je ndivyo Yesu alivyoagiza, hatuwezi kukubali mbwembwe zisizo na kiasi kutawala ibada na kumtukanisha Mungu!
·         Mungu aliwaadhibu Anania na Safira kwa sababu hawakufuata maelekezo ya Mitume Matendo 5:1-10
Unaweza kuona sasa kwa nini Biblia inatuonya kutokuifuata njia ya Kaini? Ni wazi kuwa si kila aina ya ibada inakubalika kwa Mungu, lazima tufuate namna ile aliyotufundisha Kristo, Mtume Paul anawaonya wakolosai kutokufuata namna za ibada za kujitungia Wakolosai 2:23. Wakati umefika kwa kanisa kukataa namna za ibada ambazo zinatupotezea muda, Ibada yoyote ile ambayo haifuati maelekezo ya neno la Mungu ni bure Yesu alizikemea Ibada ambazo ni maagizo ya wanadamu Mathayo 15: 7-9, Mungu anatafuta watu watakao muabudu yeye katika Roho na kweli Yohana 4:23-24. Ndugu zangu ni lazima tuwe na tahadhari hasa katika nyakati hizi tulizo nazo wengi wameifuata njia ya Kaini sitaki kuhukumu Lakini kama mkuu wa wajenzi mwenye hekima nataka nikujenge katika neno utambue namna unavyoweza kumuabudu Mungu bila Madhara, Kaini alionyesha kutokumjali Bwana na kukosa Imani Waebrania 11:4 Mungu anachukizwa na namna ya ibada tulizojitungia
2.     Hakuamua kuishinda Dhambi
Njia nyingine ya Kaini ni kutokuamua kuishinda Dhambi, Mungu ametupa nguvu kubwa sana ya maauzi, tunaweza kutumia maamuzi yetu kutenda mema au kutenda mabaya Mwanzo 4:5-8. Mungu alimwambia Kaini ukitenda vema utapata kibali, usipotenda vema dhambi iko mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde. Mungu alimwambia Kaini hayo kwa sababu alijua kuwa uwezo huo uko ndani yake, watu nwengi sana wanapofanya Dhambi humsingizia shetani, huku ni kukataa kuwajibika nisikilize! Unawajibika kwa dhambi zako! Dhambi haitusukumi kuitenda mpaka tumeamua, na ndio maana unapofanya dhambi Mungu hamuhukumu Shetani anakuhukumu wewe, Kaini alimezwa na Dhambi na Badala ya kutubu aliongeza dhambi juu ya dhambi
·         Alikasirika - Mwanzo 4:5 Nafsi yake ilijawa na chuki dhidi ya Ndugu yake na dhidi ya Mungu, watu wengi hawajui kuwa Mungu anatuona mioyoni mwetu tunapokuwa tumejawa na chuki na kukasirika Mungu anaona, wengi wanafikiri kuwa Hasira sio dhambi, lakini ni dhambi, Kaini alishindwa kuonyesha Uvumilivu, huruma na wema na hata kuwa na moyo wa kusamehe, na  kwa ugumu wa Moyo dhambi hii ilimpelekea kuua, Musa alipata Hasara kwa sababu ya hasira na Ghadhabu Zaburi 106:32-33, Yeyote asiyeweza kuidhibiti nafsi yake katika Hasira yuko katika njia ya Kaini.
·         Alikuwa na wivu Mwanzo 4:4-5 Nafsi ya Kaini ilijawa na wivu, inakuwaje mtu usifurahie Mafanikio ya ndugu yako? Ndugu yako akibarikiwa ndio furaha yenu wote, Kaini hakufurahi kuona Habili anafanikiwa alitaka mazuri yawe yake mabaya yawe ya ndugu yake Mtu aliyeokoka vema hapaswi kuishi katika wivu (husuda) na chuki, jamani umeokoka inakuwaje unachuki? Unakuaje una wivu? Inakuaje una donge? Tito 3:3, kama una husuda hakuna sababu ya kujinyima pombe na zinaa kwa sababu njia ya watu hao ni moja tu Wagalatia 5:21 hakuna mtu mwenye husuda ataingia mbinguni, kama una wivu na husuda tubu kwa vile ninjia ya Kaini.
·         Alijawa na Chuki – Ni wazi kuwa Kaini hakuwa na Upendo kwani chuki ni kinyume cha upendo he hate his Brother!  Neno hate katika Dictionary ya Kiingereza linachambuliwa hivi
i.                    Animosity – strong feeling of Opposition Ni watu wasiotaka kukubali kuzidiwa ni wenye hisia kali ya kupinga hasa mafanikio ya kimwili na kiroho ya wengine
ii.                 Contempt – the feeling that something is without value Ni watu wenye hisia kudharau wengine na kuona hawana thamani tena
iii.               Disdain – The feeling that something is not good enough to deserve your respect or attention Hujawahi kuona watu wa aina hii hawakuoni kuwa ni mwema hata kidogo, hawakubali lolote jema ulifanyalo, wenye dharau, hawataki hata kukuona, lakini eti wanasema ni watu wa Mungu Chuki ni njia ya Kaini hakuna mtu mwenye kuifuata njia ya Kaini atakubaliwa na Mungu kama unachuki nab ado ukajiona salama unahitaji kujiangalia kwa upya 1Yohana 3: 11-12, 15. Kama unafikiri Chuki ni nyepesi soma 1Yohana 3:15 Biblia inasema hivi “ Kila amchukiaye Ndugu yake ni muuaji: nanyi mnajua ya kuwa kila muuaji hana uzima wa milele ukikaa ndani yake. Ndugu yangu leo tuna wauaji wengi kama Kaini tunaabudu nao makanisani, tunahudumu nao pamoja ni wauaji si kwa kukuchinja tu lakini wanaweza pia kukuua kwa kutumia maneno, wanakusema vibaya ili ikiwezekana ukose kibali kwa watu wanaokukubali huu ni uuaji nah ii ndio njia ya Kaini
·         Aliamua kuua – Mwanzo 4:8, Kwa asili uuaji wa kivitendo ni matokeo ya uuaji wa ndani yaani chuki, Biblia inasema Usiue Kaini aliamua kuua Katika mafundisho yake Yesu anaweka wazi kuwamauaji yanatoka Moyoni Marko 7:20-23
3.      Alijaribu kumdanganya Mungu
Mwanzo 4:9, Kaini ni kama hakuwa anahusika wala kujali wala kuwajibika kwa Maisha ya ndugu yake, Mungu alipomuuliza Yuko wapi ndugu yako alisema Sijui kwani mimi ni mlinzi wa Ndugu yangu? Mungu anatujua vema mpaka mioyoni mwetu kujaribu kumdanganya yeye ni kujidanganya wenyewe Waebrania 4:13 kila kiumbe kiko wazi mbele za Mungu, Hakuna mwanadamu ambaye hajapewa wajibu wa wanadamu wengine, hauwezi kwa namna yoyote ile kutokujali maisha ya wengine na ukajifanya unajali ya Mungu huko ni kujidanganya
i.                    Anania na Saphira hawakuweza kujificha mbele za Mungu
ii.                 Tunaweza kujikuta tukijidanganya wenyewe kwa kumdanganya Mungu kuwa
a.      Tukidai kuwa tunampenda Yeye huku tunawachukia ndugu zetu IYohana 4:20
b.     Kwa kutoa kidogo kuliko alivyotubariki
c.      Kwa madai kuwa tutafanya vizuri, tutatubu Lakini tunaishi katika njia zilezile za zamani
d.     Kuimba vizuri huku tunaishi maisha ya dhambi Waefeso 5: 19-21
Ni muhimu kukumbuka kuwa Mungu hadhihakiwi wala hadanganywi Wagalatia 6:7, waongo hawataweza kuepuka Hsira ya Mungu Ufunuo 21:8. Hii ni njia ya Kaini
4.     Aliachana na Uwepo (USO) wa Mungu Mwanzo 4:16
“So Cain went out from the Lord presence” Kaini aliona masiha ya kuongozwa na neno la Mungu na maelekezo yake yanamnyima uhuru, Hakukubali toba na badiliko la kweli katika maisha yake Mwanzo 4:7-8 lakini alijiombea tu asife na asitangetange hakusikiauchungu wala kutubia dhambi zake, Mungu alimuonyesha Huruma Mwanzo 4:15-16 lakini hata pamoja na wema wa Mungu, kwa vile ilikuwa afe, lakini Kaini aliondoka katika uwepo wa Mungu, Dhambi zote ikiwa ni pamoja na hizi za Kaini zinamtenga mwanadamu na uwepo wa Mungu Isaya 59:1-2 Kwa nini tuiruhusu dhambi iharibu uhusiano wetu na Mungu? Aliamua kuwa na Maisha yasiojali Mungu ili ajiongoze mwenyewe
Hitimisho:
Ni njia gani umechagua kuifuata? Hatuwezi kumdanganya Mungu, Hasira ni dhambi, wivu ni dhambi, chuki ni dhambi, kutokujali maisha ya wengineni dhambina ubinafsi, kuabudu katika namna tunayoitaka sisi ni dhambi, uadui ni dhambi na zote hizi ni njia za Kaini Je unachagua nini katika maisha yako? “Ee Mungu naomba unilinde na Mafundisho yangu mie mtumwa wako nishiishie kuwahubiri wengine mimi nikawa wa kukataliwa nisaidie nisiifuate njia ya Kaini nipe kuwa mkweli mbele zako na mbele za wanadamu naomba sana ee Mola wangu usiniache kuondoka katika uwepo wako, nisaidie niwarejeze na wengine katika njia zako asante kwa sababu fadhili zako ni za Milele naamini hujaniumba niwe chombo cha ghadhabu yako bali mfano wa Rehema zako na wokovu wako Amen”

Ndimi Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote.

Hakuna maoni: