Alhamisi, 28 Januari 2016

LAWEZA NENO JEMA KUTOKA NAZARETHI ?


(CAN ANYTHING GOOD COME OUT OF NAZARETH?)

 Nazareth
 
ANDIKO LA MSINGI: Yohana 1:43-46. Biblia inasema hivi
“43. Siku ya pili yake alitaka kuondoka kwenda Galilaya, naye akamwona Filipo. Yesu akamwambia, Nifuate. 44. Naye Filipo alikuwa mtu wa Bethsaida, mwenyeji wa mji wa Andrea na Petro. 45. Filipo akamwona Nathanaeli, akamwambia, Tumemwona yeye aliyeandikiwa na Musa katika torati, na manabii, Yesu, mwana wa Yusufu, mtu wa Nazareti. 46. Nathanaeli akamwambia, Laweza neno jema kutoka Nazareti? Filipo akamwambia, Njoo uone.”

Ni muhimu kufahamu kuwa Nazareth ulikuwa ni mji mdogo uliokuwa kusini mwa jimbo la Galilaya (Lower Galilee), Mji huu ulikuwa ni moja ya miji iliyodharauliwa sana, kwa ujumla Israel ilikuwa na majimbo makuu Matatu, Yuda, Samaria na Galilaya, Yuda ndio eneo ambalo liliheshimika sana hususani kwa kuwa lilikuwa ni eneo lililotoa manabii na viongozi wakubwa na walioonyesha utii na uwezo wa kumuamini na kumtegemea Mungu, maeneo yaliyofuata kama Galilaya na Samaria hayakuwa maeneo yaliyopewa heshima wala kipaumbele kutokana na historia zake za kuongoza katika ibada za Sanamu, watu wasioshika dini  viongozi waovu na wasiomcha Mungu, hivyo Galilaya ilidharaulika na kuonekana kama miji isiyoweza kutoa neno Jema.

Aidha kwa habari ya Kumtazamia masihi ni wazi pia ilijulikana kuwa Masihi angekuja kutokea Uyahudi yaani Yuda katika mji wa Daudi Bethelehemu kwa vile nabii Mika alitabiri hivyo Mika 5:2 Biblia inasema “Bali wewe, Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele.” Marabi na wataalamu wote wa Maandiko na wajuzi na wanasheria wa kiyahudi wote walikuwa wanatambua wazi unabii huu na kukubali kuwa Masihi angetokea Bethelehemu Mathayo 2:1-6 Biblia inasema hivi:- “1. Yesu alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama, mamajusi wa mashariki walifika Yerusalemu, wakisema, 2. Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia. 3. Basi mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na Yerusalemu pia pamoja naye. 4. Akakusanya wakuu wa makuhani wote na waandishi wa watu, akatafuta habari kwao, Kristo azaliwa wapi? 5. Nao wakamwambia, Katika Bethlehemu ya Uyahudi; kwa maana ndivyo ilivyoandikwa na nabii, 6. Nawe Bethlehemu, katika nchi ya Yuda, Hu mdogo kamwe katika majumbe wa Yuda; Kwa kuwa kwako atatoka mtawala Atakayewachunga watu wangu Israeli.”

Unaweza kuona ni kwa sababu na msisitizo mkuu ilikuwa ngumu kwa Mwanafunzi kama Nathaeli kuamini kuwa Yeye aliyetabiriwa na Musa na manabii kama angeweza kutokea Nazareth
Kwa ujumla Nazareth ulikuwa ni mji usioheshimika na uliongoza kwa umasikini na mmomonyoko mkubwa wa uadilifu, watu wasiomcha Mungu waabudu sanamu na kimji hiki hakikuwahi kabisa kutajwa katika unabii wa agano la kale, mtu aliyetokea Nazareth alionekana sawa tu na mtu aliyetokea Mbagala, au Gongo la Mboto au manzese tofauti na Ostabey au sinza ni sawa na mtu akikuambia unatokea Kwatango, au kilosa au mbulizaga kule Pangani, au kwa msisi huko Handeni, au Nchebebwa huko Newala au Naluleo huko Liwale, Nazareth na Galilaya ilidharaulika ilikuwa mtu akikuita wewe ni mgalilaya au Mnazareth ilikuwa ni Lugha ya dharau ya hali ya juu Yohana 7: 40-42, 52. Biblia inaonyesha jinzi ambavyo maadui wa Yesu Kristo pia waliutumia mji huu.

Mathayo anajaribu kuonyesha kuwa uko unabii, ulioashiria kuwa Yesu ataitwa Mnazareth Mathayo 2:19-23 unabii huu kwa undani, unabii huu unatokana na Mathayo kuunganisha Isaya 11: 1 ambao kuna neno shina na Chipukizi neno hili kwa kiebrania husomeka kama “NETSER” kwa Kiingereza Shoot au Root yaani shina hili ndio asili ya Jina Nazareth.

Ni muhimu kufahamu kuwa katika somo hili tunajifunza kuwa Mungu huweza kuinua mtu kutoka katika Hali ya kudharaulika, ingawa kijiji cha Nazareth kilidharaulika lakini kilipoungwa na jina la Yesu kilipata umaarufu mkubwa sana, Yesu mwenyewe alikubali kuitwa Yesu wa Nazareth, Majini na Mapepo yakitajiwa Yesu wa Nazareth yanalia kwa nguvu mitume walipoombea waginjwa na kufanya miujiza mara kwa mara walilitumia jina la Yesu Kristo wa Nazareth hivyo Nazareth leo umekuwa ni mji maarufu

Awaye yote bila kujali umetokea ukoo gani, kabila gani, dini gani, jamii gani ukiunganishwa na Yesu Kristo historia yako inabadilishwa hata kama ulikuwa mnyonge kiasi gani utakuzwa na utatiwa nguvu na utatumiwa na Mungu kwa namna ya kipekee Nazareth leo ikitajwa kila mtu anajua ni moja ya miji ambayo Bwana Yesu alilelewa na kukulia
Mungu alitaka  Jina hili dhaifu na lililodharauliwa  liunganishwa na jina la Mwanae Mpendwa  na kufuta Historia mbaya ya Jimbo la Galilaya, Filipo alimwambia Nathanael njoo uone, Mtu akiunga na Yesu hwi wa kawaida Maisha yake yanabadilishwa na Historia yake inakuwa mbaya na adui zako wataisoma Namba.
Na Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima!
Rev. Innocent Kamote.

^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^

Hakuna maoni: