Alhamisi, 4 Februari 2016

Kugeuka Nyuma na kuuacha Wokovu !



Mstari wa msingi Mwanzo 19;16-17 “ Akakawiakawia nao wale watu wakamshika mkono na mkono wa mkewe na mkono wa binti zake  wawili , kwa jinsi Bwana alivyomuhurumia , wakamtoa nje  ya mji ikawa walipomtoa nje mmoja alisema jiponye nafsi yako usitazame nyuma wala usisimame katika hilo bonde popote ujiponye nafsi mlimani usije ukapotea “

 Nguzo ya Chumvi

Wewe na mimi siku ile bwana alivyotuokoa Yesu alituhurumia  na kututoa na kutuweka nje ya mji  unaposoma Mwanzo 19;12-19, utaipata picha hii vizuri  kuokolewa ni kama Yesu ametutoa nje ya mji wa Sodoma na Gomora yaani sawa na dunia hii ya watu watendao maovu ambayo wakati wowote itaanguka katika hukumu ya Mungu Isaya 24;19-20, wakati wowote Mungu atauhukumu ulimwengu huu na kelele za ulevi na uasherati havitasikika tena  wakati walimwengu watakapohukumiwa motoni  lakini Lutu alionywa kuwa ajiokoe mwenyewe kwa kutokugeuka nyuma
Mtu awaye yote aliyeokoka anaonywa kuto kurudi nyuma Luka 9;62  Yesu akamwambia mtu aliyetia mkono wake kulima kisha akaangalia nyuma hafai kwa ufalme wa Mungu Biblia inatuonya kuwa tusigeuke nyuma baada ya kuwa tumeokolewa mkewe Lutu yeye baada ya wokovu mkuu aligeuka nyuma  kwa kuipenda dunia Mwanzo 19;26 na tunasoma kuwa akawa nguzo ya chumvi awaye yote ambaye ameokolewa kisha akaangalia nyuma na kukumbuka maisha ya anasa za dunia hii uasherati, uvutaji wa sigara na madawa ya kulevya kukumbuka sinema na dansi huyo anawezea kuharibiwa na ulimwengu huu na kupoteza wokovu mkuu kiasi hiki. 

 NINI MAANA YA KUGEUKA NYUMA 
·         Nikumsaliti bwana Yesu – mtu yeyote aliyeokolewa anapoamua kurudi nyuma hana tofauti na Yuda kwani anamsaliti Bwana Yesu  Luka 22;47-48
·         Kugeuka nyuma na kuacha wokovu ni kumkana Bwana Yesu na kudai kuwa hatumjui kama alivyofanya Petro Mathayo 26;71-72

·         Kugeuka nyuma na kuacha wokovu kunakufanya uwe nguzo ya chumvi Mwanzo 19;26  nchi yenye chumvi ni nchi iliyolaaniwa  hakuna kitu kinaweza kustawi katika inchi ya chumvi hata maji yake hayanyweki  wala kiumbe chochote hakiwezi kuishi Yeremia 17;5-6, Kumbukumbu 29;23 

·         Kurudi nyuma na kuacha wokovu ni kujionyesha kuwa wewe ni mkosaji mbele za Mungu  na wote wakaao mbinguni  Mwanzo 11;3-8  kuacha wokovu ni kuyajenga tena yale uliyoyabomoa  ni kujionyesha jinsi ulivyo mkosaji mbele za Mungu soma Wagalatia 2;18 siku ile ulipookoka mbingu ilishangilia kwaajili yako sasa unaporudi nyuma ni aibu kule mbinguni ni huzuni na kilio kikubwa na masikitiko na ibilisi na ufalme wake unashangilia kukupatawewe tena  huu ni ukosaji mkubwa mbele za Mungu na majeshi yake huko mbinguni.

·         Kugeuka na kuacha wokovu ni kumtukama Mungu Hesabu 15;30
·         Kugeuka nyuma na kuacha wokovu ni kumkanyaga mwana wa Mungu na kumfanyia jeuri Roho wa neema Waebrania 10;26-29
·         Kugeuka nyuma na kuacha wokovu  ni kumsulubisha mwana wa Mungu mara ya pili na kumfedhehi kwa dhahiri Waebrania 6;4-6
·         Kugeuka nyuma na kuacha wokovu kunakufanya uwe nchi inayoota magugu na miiba  soma Waebrania 6;7-8, Yohana 15;1 Kutoka 16;4, Hosea 10;12
·         Kugeuka nyuma na kuacha wokovu ni sawa na mbwa aliyerudia matapishi yake mwenyewe na nguruwe aliyeoshwa kurudi na kugaagaa matopeni 2Petro 2;20-22, Mithali 26;11 

TATIZO LA KURUDI NYUMA HUANZIA MOYONI
Mtu aliyeokoka anaporudi nyuma jambo hili huanzia moyoni Matendo 7;39  ziko dalili kadhaa zinazoweza kuonyesha kwamba mtu Fulani amegeuka nyuma na kuacha wokovu
Hatataka kulitii neno la Mungu tena, Hofu ya Mungu ndani yake inakuwa haiko, hafurahii mafundisho ya neno la Mungu na hufikia hatua ya kulikataa neno la Mungu na kukosoa kila aina ya mahubiri na hakuna cha kumgusa, atalizoea neno la Mungu na kuliona la kawaida, haoni umuhimu wa kukaa katika mafundisho, hufikia hatua ya kulidharau neno la Bwana Hesabu 15;31, Mithali 13;13  mtu wa aina hii anaitwa mtu aliyeshiba njia zake mwenyewe Mithali 14;14 ageukaye moyoni hushiba njia zake mwenyewe.

SABABU ZINAZOSABABISHA WATU WENGI KURUDI NYUMA
·         Kukosa viongozi wanaofundisha kweli ya neno la Mungu Kutoka 32;1 Waamuzi 2 18-19
·         Kuupenda ulimwengu huu wa sasa 2Timotheo 4;10 Mithali 24;1,23,17 Warumi 12;2 2Wafalme 17;15
·         Kukaa katika ushirika uliojaa maasi Mathayo 24;12
·         Kukosa mizizi na hivyo kuogopa dhiki na mateso Luka 8;13 Mathayo 13;20-21,Luka 12;4-5 inatupasa kufahamu kuwa imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi  Matendo 14;19-22
 kwa msingi huo basi inatupasa kuendelea kushikamana na wokovu  kama mwanzo wa uthabiti wetu Waebrania 3;14.

Uwezekano wa kukataliwa na Mungu !



Mstariwa Msingi 1wakoritho 9;27 “Bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha isiwe nikiisha kuwahubiri wengine mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa”

           Adam na Eva wakifukuzwa katika Bustani ya Eden (Neno Eden maana yake Uwepo wa Mungu)

Tunapokuwa tumeokolewa kwa kutubu dhambi zetu kwa kumaanisha kuziacha  na kuliitia jina la bwana  na damu yake ili itutakase  dhambi zetu tunakuwa tumealikwa katika harusi ya mwana kondoo Yesu Kristo na furaha ya baba yetu aliye mbinguni, hata hivyo ni makosa kufikiri kuwa kila mtu aliyeitwa na kuokolewa kuwa atakwenda mbinguni bila kujali kuwa anafanya nini . Yako mafundisho potofu yaitwayo “Eternal Security” yanayoeleza kwamba mtu akiisha kuokolewa ameokolewa (once saved forever saved ) basi hata afanye nini  yeye ni mtoto wa Mungu na ataingia mbinguni na hutumia maandiko yafuatayo  kufundisha uzushi huo Warumi 8;33, Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu?, Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki”Warumi 8;1”…..Hakuna hukumu ya adhabu juu ya hao walio katika Kristo Yesu” Yohana 10; 27-29 “….Nami nawapa uzima wa milele wala hawatapotea kamwe, wala hakuna mtu atakayewapokonya  katika mkono wangu” ni makusudi  ya somo hili basi kujifunza ili kuifahamu kweli juu ya jambo kama hilo ili tuwekwe huru mbali na mafundisho yaliyo potofu

Mfano wa safari ya wana wa Israel.
Safari hii ni kama mfano au kielelezo cha safari ya watu waliookolewa kuelekea mbinguni, kama vile wana wa Israel walivyookolewa kutoka Misri kuelekea kanaani, jambo la kushangaza ni kuwa  sio wana wa Israel wote waliotoka Misri kuelekea kanaani walifika. Neno la Mungu linatuonyesha kuwa wengi waliangamizwa Jangwani ili kuwa mfano kwetu 1Wakoritho 10;1-6.

Mfano wa Paulo Mtume .
Mtume Paulo ingawa alikuwa Muhubiri mkubwa wa injili na mwalimu wa Neno la Mungu mwenye wingi wa mafunuo na miujiza ya kupita kawaida iliyoambatana na huduma yake bado alikuwa anajua kuwa hajafika bado alijua kuwa anaweza kukataliwa ikiwa hata kishika kile alicho nacho mpaka mwisho 1Wakoritho 9;26-27 mtume Paulo hapa anasema hata mimi Mstari wa 26 ikiwa  Paulo angeweza kukataliwa baada ya kuitwa ni zaidi sana wewe na mimi.

Ulinganifu wa maandiko unaofundisha uwezekano wa kukataliwa baada ya kuitwa
Biblia imejaa maandiko mengi yanayotuthibitishia kuwa kuna uwezekano wa kukataliwa baada ya kuitwa, tunaona pia kumbe kuna uwezekano wa Mtu kufutwa katika kitabu cha uzima  maandiko haya ni pamoja  na
Kutoka 32;32-33, Yoshua 24;20, 1Nyakati 28;9,2Nyakati 15;2,Yeremia 18;10,Ezekiel 18;24 Ezekiel 33;12-13,Mathayo 5;13 ,10;22, Yohana 15;6,Warumi 11;22, 1Timotheo 1;19, Waebrania 3;12-14, 8;9 2Yohana 1;8, Ufunuo 22;18-19

Waitwao ni wengi bali wateule ni wachache Mathayo 22;14
Wateule ni wale ambao hata baada ya wokovu wanaendelea kumtii Mungu katika kila eneo la Neno lake, malaika walioendelea kumtii Mungu baada ya malaika mkuu Lucifer kuasi na ambaye sasa ni shetani  wanaitwa malaika wateule  soma 1Timotheo 5;21 Warumi 8;33 Biblia inaposema ni nani atakayewashitaki wateule inamaanisha wale ambao baada ya kuitwa wanaendelea  kuongozwa na kulitii Neno la Mungu hao hakuna atakayewashitaki  mtu anayempendezaa Mungu siku zote ni ngumu kupata jambo la kumshitaki kama ilivyokuwa kwa Bwana Yesu Yohana 8;29, kila mtu ambaye maisha yake yanaongozwa na neno la Mungu hawezi kuadhibiwa Warumi 8;1, Kristo Yesu ndiye neno la Mungu lenyewe Ufunuo 19;13 kila anayemfuata Yesu na kushika kielelezo chake  hataweza kuadhibiwa.

aidha ni muhimu kufahamu kuwa Biblia inaposema  kuwa wala hawatapotea kamwe wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu Yohana 10;28 ina maanisha nini kumbuka kuwa hakuna mtu aliyekuwa katika mikono ya Yesu kama Yuda Iskariote aliyekuwa mweka hazina  wake lakini amepotea yuko motoni  milele, pamoja na kutumiwa katika kuhubiri na kutoa pepo Yuda alipotea  ili mtu asipotee ni lazima aisikie sauti ya Yesu na pia kumfuata  maana yake ni kuwa lazima tuishi sawa na neno la Mungu  ili tusipotee Zabiri 119;9

Mambo sita ya msingi ya kuyaangalia ili tusiwe watu wa kukataliwa baada ya kuitwa
·         Maisha Yetu katika wokovu ni lazima yawe sawa na injili yuote na sio sawa na dhehebu fulani Warumi 2;16
·         Tusikubali kufarijiwa na kukataa kuonywa , kukaripiwa  na kukemewa kwa neno la Mungu  Ayubu 16;2, Isaya 30;20-21, Wafilipi 3;12-14
·         Penda mafundisho zaidi baada ya kuokoka kuliko mahubiri, mahubiri lengo lake ni kutuleta kwa Yesu na mafundisho ni kutupa maarifa ili kujua yatupasayo kujua kwani kuna aina mbili za dhambi (a). Kutenda yasiyotupasa 1Yohana 3;10 na (b). kutokutenda yanayotupasa kutenda Yakobo 4;17  bila mafundisho hatuwezi kufahamu yanayotupasa kutenda  mpaka tumedumu katika mafundisho Mambo ya Walawi 5;17
·         Tusikubali kuandamana na mkutano katika kutenda uovu,  neno mkutano maana yake ni watu wengi  hatupaswi kuridhika kufanya jambo eti kwa sababu watu fulani wengi wanafanya, wakati wa Nuhu watu wote ulimwengu mzima waliangamizwa na ni watu nane tu walioachwa hai  Luka 13; 22-23, Kutoka 23;2 tumwangalie Yesu tu na sio wanadamu Zaburi 37;37
·         Inatupasa kulifuata neno la Mungu bila kuchagua la kufuata Kumbukumbu 1; 35-36.
·         Kila unapogundua kuwa umamfanya Bwana dhambi inakupasa kutubu 1Yohana 2;1-2, kumbuka kumkana Bwana ni kujitafutia mauti Hesabu 15;30-31 tunahitaji kuvumilia hata mwisho ili kukamilisha wokovu wetu Mathayo 24;12-13. 

Jinsi ya Kuomba !



Mstari wa Msingi Luka 11;1 “Ikawa alipokuwa mahali Fulani akiomba , alipokwisha mmoja katika wanafunzi wake alimwambia Bwana tufundishe sisi kusali kama vile Yohana alivyowafundisha wanafunzi wake”
                                                       Maombi yana uhusiano mkubwa na Ukristo wetu

Mara tu baada ya mtu kuokoka  na kufanyika mtoto wa Mungu Yohana 1;12  inakuja shauku na hamu  kubwa ya mtu huyo kutaka kuwasiliana na Mungu aliye baba yake  wa Mbinguni. Mawasiliano hayo yanafanyika kwa njia ya maombi, Yesu kristo kiongozi mkuu wa wokovu wetu waebrania 2;10 alikuwa mwombaji mkuu, Alfajiri na mapema sana alikuwa anakwenda mahali pasipokuwa na watu  akawa anaomba Marko 1;35 Jioni pia alikuwa akifanya maombi Marko 6;46-47 wakati mwingine pia alikuwa akifanya maombi usiku kucha  Luka 6;12  Yesu alichukua muda mrefu wa kuomba mpaka akalia sana na machozi Waebrania 5;7 , hakukubali kutingwa sana na shughuli na kukosa muda wa kuomba, wakati mwingine hata katikati ya kilele cha shughuli zake  alikuwa akijiepusha  na kwenda mahali pasipokuwa na watu na kuomba Luka 5;15-16 wakati mwingine aliomba mpaka hari yake  au jasho lake likawa kama matone ya damu  yakidondoka katika inchi Luka 22;44 Mara nyingi aliwaambia wanafunzi wake waombe ili wasiingie majaribuni  halafu yeye akajitenga mbali kidogo nao na kuendelea kuomba , wanafunzi wake walipojaribu kuomba waliishiwa na maneno hata ikawa kwao vigumu kuomba hata kidogo Luka 22;39-41 Mathayo 26;40-41 na ndipo wanafunzi wake walipoona ni vema kumuomba awafundishe jinsi ya kuomba ni makusudi ya somo hili sasa kujifunza jinsi ya kuomba , Yesu kristo alikuwa muombaji na alikuwa ni kielelezo chetu Mtu awaye yote aliyeokoka hawezi kufika mbali katika wokovu wake kama  akiwa sio muombaji tutajifunza somo hili jinsi ya kuomba kwa kuzingatia vipengele vitano vifuatavyo
·         Mikao inayofaa kwa ajili ya maombi
·         Swala la kuomba kwa sauti kubwa
·         Swala la kuomba kwa kufumba macho au kufumbua macho
·         Umuhimu wa kuomba kwa jina la Yesu.
·         Matumizi ya sala ya Bwana katika Maombi
Mikao inayofaa kwa ajili ya maombi.
Wako watu wengi sana wanaofikiri kuwa wakati wote mtu anapotaka kumuomba Mungu ni lazima awe amepiga magoti, hii sio sahii kwani tunaweza kumuomba Mungu katika mikao tofauti tofauti  katika namna nyingine pia kutegemea na nafasi, Kupiga magoti ni jambo linalimfurahisha Mungu sana  wakati wa kuomba Isaya 45;23. Lakini hata hivyo kuna njia nyingi za kibiblia za jinsi ya kuomba zifuatazo ni baadhi ya njia zilizomo kwenye Biblia
a.       Kupiga magoti – Tunaona mifano katika Luka 22;41Yesu, Katika Daniel 6;10 Daniel, katika Zaburi 95;6 Daudi, katika Matendo ya mitume 7;60Stefano, katika Matendo 9;40Petro na katika  matendo 20;36,21;5 Paulo mtume na watu wengine.
b.      Kupiga magoti na kukunjua mikono kuelekea mbinguni – Mfalme Sulemani katika 1Wafalme 8;54, 2Nyakati 6;13, na pia Ezra kuhani katika Ezra 9;5.
c.       Kuinamisha kichwa  Mwanzo 24;26,Kutoka 4;31, 12;27 na 34;8
d.      Kuanguka kifulifuli uso kugusa Ardhi - Tunaona mfano wa Yesu Mathayo 26; 39. Yehoshafati 2Nyakati 20;18 Eliya 1wafalme 18;42,Yoshua katika Yoshua 5;14,Musa   na Haruni katika Hesabu 20;6
e.      Kusimama – Marko 11;25,Luka 18;11
f.        Kusimama na kukunjua mikono kuelekea mbinguni – 1Wafalme 8;22
Hizo zote hapo juu ni njia zinazo faa kwaajili ya kumuomba Mungu ni mazingira tu ndiyo yatakayoamua njia gani itumike, kwa mfano huwezi kupiga magoti ukiwa stendi ya mabasi au katika kanisa lisilo na sakafu Lakini kama mazingira ni mazuri na yanaruhusu kupiga magoti kufanya hivyo sio tatizo Daniel 6;10, wala sio busara kugusa uso chini mpaka utoke sugu ili watu wajue kuwa wewe ni muombaji maombi ya jinsi hii ni ya kinafiki Mathayo 6;1-5, Biblia inatufundisha kuwa mambo yote yatendeke kwa  uzuri na kwa utaratibu 1Koritho 14;40 kwa msingi huo inatupasa kuchagua  ni wapi na ipinjia ipi inafaa  na kuitumia kwa mfano ukiwa una usingizi ukapiga magoti ili kuomba ni rahisi kulala usingizi hapo njia sahii ni kusimama na kutembea huku unaomba itakusaidia kutokulala unaona.
Swala la kuomba kwa sauti kubwa
Kumekuwako na utata wa kitheolojia kuhusu kuomba kwa sauti kubwa ikifikiriwa kuwa kufanya hivyo ni kupayuka payuka kunakotajwa katika Mathayo 6;7-8 lakini tafasiri hiyo sio halali katika Biblia ya kiingereza King James Version ambayo ni tafasiri iliyo karibu na lugha za asili zilizoleta Biblia kwetu kiibrania na kiyunani Mathayo 6;7  husomeka hivi “But when ye pray use not vain repetitions as the heathen do” kwa msingi huo kupayuka payuka ni kurudia rudia maneno yale yale  kama kasuku  hii ilifanywa na mataifa kwa sababu hawajui kuomba  hawana maneno mengi ya kutosha kujieleza mbele za Mungu. Hivyo kuomba kwa kupaza sauti sio kupayuka Biblia imejaa mifano ya watu wengi ambao waliomba kwa kupaza sauti na hata kulia sana machozi kama alivyofanya Bwana Yesu Biblia inatoa ushauri wa kufanya hivyo
Waamuzi 2;4,21;21Samuel 30;3-4 Mithali 2;3-6 zaburi 77;1 Matendo 4;24  kuomba kimya kimya au kwa kupaza sauti kote ni sawa mbele za Mungu nako pia kunategemea na mzingira, kwa mfano sio busara kufanya hivyo kwenye nyumba ya kupanga  au mahakamani ukiwa kizimbani au wakati mumeo anayepinga wokovu akiwa chumbani anakusikia ukimuombea Niokoe na Mume huyu mkaidi anayepinga wokovu n.k. maswala kama hayo ungeweza kuyaomba kimyakimya Mathayo 7;6.
Swala la kuomba kwa kufumba macho au kufumbua macho.
Swala la kufumba macho au kufumbua ni swala linalohusiana na maswala ya kisaikolojia  kwa Mungu hakuna sharti Yeye huweza kuwasiliana na mwanadamu hata akiwa amelala usingizi kwa njia ya ndoto, na hii haina maana kuwa ukifumbua macho ndo kuna kitu utakiona  wakati mwingine mtu anaweza kuona maono akiwa amefumbua macho  na macho hutumika kuyaona maono hayo  lakini roho zetu huitwa zimezimia kwani tunakuwa hatuko katika hali ya kawaida  Matendo 10;9-12 wakati mwingine kufumbua macho kunaweza kusababisha kuingiza picha au mambo ambayo yatatutoa katika kuzingatia mwelekeo wetu kwa Mungu kwahiyo hili nalo ni swala la kisaikolojia na kimazingira kwa mfano kama unaendesha gari unaweza kuomba lakini sio kwa kufunika macho
Umuhimu wa kuomba kwa jina la Yesu.
Kuomba kibiblia ni kuomba kupitia jina la Yesu hili ni jambo la muhimu namna yoyote ya kutumia vitu vilivyochongwa au kutengenezwa kwa shaba, mbao, dhahabu , fedha n.k  na kuvisimamisha kati yetu na Mungu  na kuviangalia wakati wa kuomba na kuvitaja , kuvitumia, kuviangalia au kuvitafakari  na kufikiri kuwa vitafanikisha sala zetu hiyo ni ibada ya sanamu ambayo ni  machukizo makubwa mbele za Mungu Kutoka 20;4-5,1Yohana 5;21,1Wakoritho 10;14 Isaya 31;7, Sanamu yoyote au lozari na vitu vyote vya jinsi hiyo siyo sehemu ya maelekezo ya jinsi ya kuomba katika Biblia , Mungu ni Roho nao wamwabuduo au kumuomba wanapaswa kumuabudu katika roho na kweli na siyo kwa kutumia kitu chochote kinachoonekana Yohana 4;23-24, aidha ni muhimu kufahamu kuwa kuwaomba wafu pia ni chukizo kubwa mbele za Mungu Kumbukumbu 18;9-12, kuwaomba watakatifu ambao wamekwisha kufa kama Petro, Yohana, Paulo, Bikira Maria, Yusufu .n.k watuombee sio sahii kibiblia kila mmoja anapaswa kuomba mwenyewe na kuzungumza na Mungu kwa jina la Yesu na ukifanya hivyo anakusikia na kupokea dua zako,
Kila mtoto wa Mungu ana haki sawa kabisa na mwenziwe anapoomba  kila aombaye hupokea Yohana 16;24, Luka 11;9-11 Biblia inaonyesha kuwa ni wawili tu wanaotuombea  hao ni Yesu Kristo na Roho Matakatifu nao hufanya hivyo bila sisi kuwaomba watuombee 1Yohana 2;1 Warumi 8;26-27 Tukifanya jinsi neno la Mungu linavyotuongoza na kulitii ndipo tutakapofanikiwa katika njia zetu Zaburi 119;9, aidha ni muhimu kufahamu kuwa kuwaombea wafu pia siyo sahii Biblia inasema katika Waebrania  9;27 kuwa mtu amewekewa kufa mara moja tu na baada ya kifo ni hukumu, tunaweza kuomba kwa ajili ya wale walio hai ili waokolewe kabla hawajafa lakini inapotokea mtu amekufa hakuna kinachoweza kubadilika 1Yohana 5;14-16
Maombi yetu ili yaweze kuwa na mafanikio inatupasa kumuomba Mungu baba kwa kupitia jina la Yesu Yohana 16;23, sio maelekezo ya Biblia kumuomba Mungu kupitia Mariam  kwa mawazo potofu eti ukipitia kwa mama wa Mungu  ndio utajibiwa kwa sababu kina mama wana huruma  ni muhimu kufahamu Kua Maria kamwe sio mama wa Mungu Mungu hana mama wala Baba hana mwanzo wa siku zake wala mwisho wa siku zake  hali kadhalika kwa Yesu Kristo hivyo hivyo Waebrania 7;3 Yesu hakuanzia maisha yake tumboni mwa Mariamu  yeye alikuwepo hata kabla ya Ibrahimu hajazaliwa Yohana 8;58, Yesu ndiye aliyeufanya ulimwengu Waebrania 1;2 katika Yesu kila kitu kiliumbwa  Wakolosai 1;13-17 Yeye ndiye aliyemuumba Musa Waebrania 3;1-4 na pia ndiye aliyemuumba Maria  na watu wote, aliyeumbwa hawezi kuwa mama wa aliyemuumba Biblia inaonyesha kuwa Maria mwenyewe alihusika katika kumuomba Mungu  pamoja na wanafunzi wa Yesu Matendo 1;4,12-14 Bikira Maria kamwe hawezi kujiita mama wa Mungu kinyume chake alijiita mjakazi wa Bwana  yaani mtumwa wa kike wa Bwana Biblia inasema katika Luka 1;38 “Mariam akasema Tazama mimi ni mjakazi wa Bwana” 
Matumizi ya sala ya Bwana katika Maombi
Mathayo 6;9-13 Yesu Kristo alipowafundisha wanafunzi wake kuomba aliwaelekeza kuomba kwa misingi inayojulikana kama sala ya Bwana, kimsingi hakuwa anamaanisha waitamke kama ilivyo na kuimaliza kama kasuku kama watu wengi wanavyofikiri , Biblia inaposema katika Mathayo 6;9 “Basi ninyi salini hivi baba yetu uliye mbinguni……” Tafasiri ya kiingereza ya King James Version inasema “After this manner therefore pray Ye” tafasiri ya kiingereza ya LIVING BIBLE inasema Pray alon these lines” Katika Luka 11;2 kwa msingi huo kinachozungumzwa hapa ni kuwa sala ya bwana ni mafundisho ya msingi ya kutumia katika maombi, kilichozungumzwa ni kuomba kupitia misingi hii kila tunapotaka kuomba Luka 9;54 Mathayo 20;20-22 Kutamka sala ya bwana kama ilivyo ingeweza kuchukua dakika mbili tu na isingelikuwa suluhisho la kufundisha maombi ambao wao walikuwa wakitaka kujifunza kuomba kwa muda mwingi wa kutosha  kama alivyokuwa akiomba Bwana Yesu  vinginevyo Yesu hangeshangazwa na wanafunzi wake kulala usingizi ikiwa sala Yenyewe ingeweza kuchukua dakika chache. Mafundisho mengi aliyokuwa akiyatoa Bwana Yesu Mara nyingi yalikuwa yakihitaji ufafanuzi Mathayo 13;36, na pia mafundisho ambayo wanafunzi waliweza kuyaelewa leo yanahitaji ufafanuzi  Mathayo 13;51 Mengine ambayo yalikuwa magumu kueleweka kwa wanafunzi kwa mfano habari za kuteseka kufa na kufufuka sio tatizo kubwa kueleweka leo Marko 9;30-32, Luka 24;44-45 na ndio maana kanisa linahitaji waalimu ambao wanaweza kufunuliwa na Roho wa Mungu  Neno lake ili kulilisha kanisa 1Wakoritho 2;10.
JINSI YA KUOMBA KWA KUTUMIA SALA YA BWANA.
Baba yetu uliye mbinguni.Mathayo 6;9.
Tunapokuja kumuomba Mungu inatupasa kufahamu kuwa Yeye ni baba yetu, kama unaweza kuwasiliana na baba yako wa duniani  anayejishughulisha na  na mahitaji yetu na kuyajali  ni muhimu kufahamu kuwa Hatupaswi kumuomba Mungu tukidhani kuwa yuko mbali ni lazima tuweke mawazo yetu kuwa Mungu ni baba yetu na kuwa yuko karibu mno tunapomuomba Zaburi 145;18,Zaburi 119;151 103;13 Fahamu kuwa ni baba mwenye upendo mwenye uwezo anayejishughulisha  sana na mambo yetu 1Petro 5;6-7  hatupaswi kufikiri kuwa yeye hatujali Zaburi 37;28 Isaya 49;14-16,1Wakoritho 10;10. Aidha uhusiano wetu na Mungu lazima uwe wa baba na mwana maana yake kama hujazaliwa mara ya Pili huwezi kuwa na uhusiano wa aina hiyo.
Misingi Saba ya kufuata katika maombi yetu Kama alivyotufundisha Yesu Kristo
1.       Jina lako litukuzwe Mathayo 6;9.
Maombi yetu yanapaswa kuanza kwa kumtukuza Mungu na kumsifu si busara kuanza kumimina shida tulizo nazo  mtukuze Mungu kwa uweza wake na uumbaji mfano Zaburi 104;5-28, mtukuze kwa wingi wa Rehema na huruma zake Zaburi 103;8 na pia unaweza kumtukuza kwa matendo yake makuu aliyokutendea Zaburi 106
2.       Ufalme wako uje Mathayo 6;9 Baada ya kuokolewa ujue kuwa umetolewa katika ufalme wa giza  au utawala wa shetani  hivyo inakupasa kuwakumbuka wengine omba watu waokolewe katika taifa lako, ombea wale wasio na mafundisho na kuombea kazi ya Mungu ikiwa ni pamoja na Bwana wa mavuno kupeleka watenda kazi katika kazi yake Waebrania 12;14 Mathayo 9;37-38.1Wakoritho 10;24,Wafilipi 2;4 Warumi 15;1
3.       Mapenzi yako yatimizwe hapa duniani kama huko mbinguni Mathayo 6;10 mapenzi ya Mungu kutimizwa  ni watu kuishi sawa na Neno lake tumuombe Mungu kwaajili ya serikali na wanaotawala duniani 1Timotheo 2;1-4,Mithali 21;1 ombea lolote lililo kinyume  na mapenzi ya Mungu  lililotawala duniani mambo kama rushwa, vita, njaa uonevu, kuzuia Neno la Mungu, kuenea kwa uislamu n.k
4.       Utupe leo riziki Yetu  Mathayo 6;11 Ni mapenzi ya Mungu baba yetu kuwa kila mtoto wake apate riziki yake kila siku  kuna riziki za aina nyingi  Afya Marko 7;25-27, Yeremia 30;17, 33;6 Chakula nguo  nazo ni aina za riziki Zaburi 37;25,1Timotheo 6;8 zaburi 34;10 pia unaweza kuomba kwaajili ya mahitaji ya wengine  na mahitaji mengine
5.       Utusamehe Deni zetu kama sisi nasi tunavyowasamehe wadeni wetu Mathayo 6;12  Deni zinazozungumzwa hapa ni makosa au dhambi  Luka 11;4  katika maombi Mungu anatutazamia tuangalie mahali tulipomtenda dhambi kwa kuwaza kusema na kutenda  kwani dhambi ni kizuizi cha maombi  lakini wakati huohuo tunapaswa kuwasamehe wengine au kupatana na watu tuliokosana nao Luka 17;4 kwani kama hatujasamehe  dhambi zetu pia zinakuwa ngumu kusameheka Mathayo 6;14-15.
6.       Na usitutie majaribuni lakini utuokoe na Yule mwovu kwa kuwa ufalme ni wako na nguvu na utukufu hata milele Mathayo 6;13, ni muhimu kufahamu kuwa Mungu hamjaribu mtu Yakobo 1;13-14 lakini shetani hatuwazii mema watu wa Mungu na ndiye ambaye anazunguka huko na huko akitafuta mtu ammeze 1Petro 5;8  Kwa kuwa Mungu ni mwenye nguvu zote inatupasa kumuomba atuokoe na mipango ya shetani  Luka 10;18-19Mathayo 18;18,Daniel 10;11-13 Kemea mipango yote ya shetani juu ya watu wote na kanisa pia kazi ya Mungu  na namna yoyote ya kuwazuia watu wasilielekee Neno la Mungu.
7.       Amina Mathayo 6;13 Neno hili amina maana yake ni na iwe hivyo, baada ya maombi amini kuwa imekuwa sawasawa na kuomba kwako Marko 11;24 Hivyo mshukuru Mungu kwa imani kwamba umepokea uliyoyaomba 1Thesalonike 5;18 Endelea kuwa mtu wa maombi Yeremia 33;3 penda pia kuwa mwenye kushiriki siku za maombi kanisani ambako uatajifunza kutoka kwa watu wenye uzoefu mkubwa wa kuomba na kupata changamoto. Mithali 27;17.