je zaka ni halali katika
agano jipya?
Moja ya maswala
yanayosumbua sana wakristo katika nyakati hizi za leo ni pamoja na swala la
zaka! Zaka ni moja ya kongwa kubwa sana la sheria ambalo limewatesa Wakristo
wengi na watumishi wengi wa Mungu na hii inatokana na aidha kukaziwa sana kwa
kupita kawaida na wakristo wengi wamekuwa wakikataa kutii swala zima la utoaji
wa zaka. Kwa ujumla swala la utoaji lilitakiwa kuwa la furaha na Baraka lakini
kinyume chake huzuni imekuwa ikitawala na uchungu katika swala zima la utoaji na hasa zaka!
Zaka kikaangoni tafadhali wewe mwenyewe uhukumu!
Zaka ni sehemu ya sheria
Biblia inasema katika Walawi 27;30 “Tena zaka yote ya nchi
kama ni ya mbegu ya nchi au kama ni matunda ya nchi ni ya Bwana ni takatifu kwa
Bwana”
Malaki 3;9 inasema
“Ninyi mmelaaniwa kwa laana maana mnaniibia mimi naam taifa hili lote” Kumbe
kutokutoa zaka kwa mujibu wa sheria ni laana lakini Agano jipya linatuambia
Wagalatia 3;13 “ Kristo alitukomboa katika laana ya torati kwa kuwa alifanywa
laana kwaajili yetu maana imeandikwa amelaaniwa kila aangikwaye juu ya mti”
Je sisi tuko chini ya sheria ya agano la kale leo?
Jibu la swala hilo ni
ndio na sio. Agano la kale linahusiana na mitazamo miwili ya maisha ya kiyahudi
wao binafsi na taifa lao katika uhusiano wao na Mungu.Agano hilo la kale lina
kanuni za kiraia na za kidini na kimaadili zile za kiraia bado zinatumika hata
leo katika mifumo ya serikali mbalimbali. Lakini sheria zenye uhusiano na
maswala ya uhusiano wetu na Mungu katika agano la kale zimekomeshwa na
kubadilishwa Waebrania 7; 12 “Kwa
kuwa yanapotokea mabadiliko ya ukuhani, pia lazima yawepo mabadiliko ya
sheria”. Kwa sasa basi tuko chini ya sheria ya Kristo Galatia 6;2 ambayo ina chachu ya sheria za kimaadili ambazo mzizi
wake uko katika agano la kale.
Lakini sheria
za kidini za agano la kale yakiwemo maswala ya zaka, Tohara na maswala ya
kiibada ya kutawadha na sabato na kadhalika vimebatilishwa hata ingawa tunazo
baadhi ya sheria za maswala ya kiibada kama Ushirika wa meza ya Bwana na
ubatizo wa maji, lakini haya si ya lazima katika kutufanya tusiwe na mahusiano
maalumu na Mungu, Hayo ni ya muhimu katika kutimiza kila ambacho kristo
alikiagiza na kukitenda. Wakati katika agano la kale zaka na tohara na
mengineyo yalikuwa ni ya lazima ili uwe na uhusiano mzuri na Mungu, lakini kwa
habari ya wokovu ushirika na ubatizo haviwezi kutuzuia kuwa na Ushirika na
Mungu.
Ukweli kwamba
tuko huru kutoka katika sheria ya agano la kale ndio ufunuo ambao Paulo mtume
aliupokea na ndio alioupigania vikali, wazo hili lilikuwa gumu kukubalika hata
na kwa mitume wengine na ilikuwa ngumu kuelewana nalo Lakini ndio ufunuo
aliopewa na Bwana Yesu Kristo. Yesu alizungumza kuwa sheria imekamilishwa na
kuwa imekwisha kupita lakini hawakuwa na masikio ya kusikia.Kama tunajaribu
kuishika sheria leo tunauweka wokovu wetu katika hali yenye utata Wagalatia 5;4
Biblia inasema hivi “Mmetengwa na Kristo
ninyi Mtakao kuhesabiwa haki kwa sheria; Mmeanguka kutoka katika hali ya
Neema.” Kwa nini
1.
kwa
sababu hakuna mtu aliyeweza kuitimiza Sheria yote isipokuwa Yesu Kristo peke
yake
2.
Pili
kwa sababu ukivunja moja tu katika sheria utakuwa na hatia ya kuwa umeivunja
yote na unastahili kifo.
Kujaribu
kuishika sheria ni kujaribu kuendeleza haki yako mwenyewe. Kumpokea Yesu ni
kupokea haki yake na kutambua kuwa hatuwezi kuwa na wema wa kutosha sisi wenyewe
na kwa hiyo Mungu anataka tuache kujaribu, Mungu anataka kujaribu kutuzuia
kulitii agano la kale, Tunapokuwa tumempokea Yesu sheria yake inaandikwa katika mioyo yetu.
Wokovu wetu ni mara moja na endelevu, na kutembea kwetu kunajumuisha maendeleo
ya wokovu wetu na nafsi zetu kwa kuruhusu maisha katika roho kupiga hatua kila
wakati kutoka utukufu hata utukufu. Roho zetu zinakuwa mpya mara tu unapokuwa
umeokoka roho zetu zinakuwa kiumbe kipya mara moja na nafsi zetu zinahuishwa
siku hadi siku Neno la Mungu linakata pazia la nafsi na roho na kuruhusu
mabadiliko ya maisha kwa nguvu ya neno la Mungu ndani yetu na Roho wa Mungu
anatujulisha mara tunapokuwa tumeivunja sheria ya ndani. Sasa basi zaka,
kutahiriwa, kutawadha kwa namana ya kidini, kushika miandamo ya mwezi na
sabato, siku takatifu, na aina za vyakula, msishike msiguse msionje, ibada za
hekaluni, kuua kwa mawe, haya yote ni sehemu ya sheria za agano la kale unaweza
kuamua kuyashika YOTE au Kutokuyashika yote.Tafadhali ndugu msmaji wangu hebu
tafakari kwa kutumia Biblia yako na soma pamoja name maandiko kadhaa yafuatayo
katika hali ya kuomba kasha utaanza kuhisi uhuru mkubwa na utajiri mkubwa
uliomo katika Kristo na wokovu wetu.
Sheria
imetimizwa, kwa uwazi kabisa Biblia inasema mpaka wakati wa Yohana mbatizaji
Yesu alizaliwa chini ya sheria na ndio maana aliwaambia wayahudi kuifuata
sheria nah ii ilikuwa sahii mpaka baada ya kifo chake, Kuzikwa na kufufuka,
ninaamini kuwa Yesu alishika kila kitu kilichoamriwa na Torati na nina hakika
inamuuma sana kuona sisi nasi tukijaribu kuishika vilevile, Yeye alifanya hivyo
ili sisi tusiwe na haja. Aligongomelea utaratibu huo msalabani Wakolosai 2; 14
sasa tuko huru tuko huru tuko huru!.
Kama
tukidanganya leo tunaivunja sheria ya agano la kifalme na sio agano la kale
“Usishuhudie uongo” hii sio propaganda bali ni uwazi wa
kibiblia kabisa
·
Wagalatians 5:4.-
Mmetengwa na
Kristo ninyi Mtakao kuhesabiwa haki kwa sheria; Mmeanguka kutoka katika hali ya
Neema.
·
Mathayo 11:13 Kwa maana
manabiiwote na torati walitabiri mpaka wakati wa Yohana
·
Luka 16:16 Torati na
manabii vilikuwako mpaka wakati wa Yohana Tangu wakati huo habari njema ya
ufalme wa Mungu hutangazwa na kila mtu hujiingiza kwa nguvu.
·
Mathayo 22:37. Mpende
Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote na kwa akili zako
zote, mpende jirani yako kama nafsi yako, hizi mbili ndio sheria yote na
manabii.
·
Yohana 1:17 Sheria
ilikuja kwa mkono wa Musa neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo.
·
Yohana 7:23 Tohara ni ya
lazima kwaajili ya sheria ya Musa
·
Matendo 13:39 na kwa
Yeye kila amwaminiye huhesabiwa haki katika mambo yale yote asiyoweza
kuhesabiwa haki kwa torati ya Musa
·
Matendo 15:5-20 Je
waishike sheria si wanaokolewa kwa imani.
·
Matendo 18:13 Wakisema
mtu huyu huwavuta watu ili wamuabudu Mungu kinyume cha Sheria
·
Matendo
21:21Unawafundisha Wayahudi wote wakaao
katika mataifa kumwacha Musa
·
Warumi 3:19 Basi twajua ya kuwa mambo yote inenayo
torati huyanena kwa walio chini ya Torati
·
Romans 3:21 Lakini sasa
haki ya Mungu imedhihirika pasipo sheia inashuhudiwa na torati na manabii, ni
haki ya Mungu iliyo kwa njia ya Imani katika Kristo Yesu kwa wote waaminio.
·
Warumi 3:27 Kwa sheria
ya imani na sio ya Matendo.
·
Warumi 3:28 Mwanadamu
huhesabiwa haki kwa imani pasipo matendo ya sheria
·
Warumi 4:1-16 kuhesabiwa
haki ka njia ya imani.
·
Warumi 6:14 Kwa maana
dhambi haitawatawala ninyi kwa sababu Hatuko chini ya sheria bali chini ya
neema
·
Warumi 7:4 tumeifia
Torati
·
Warumi 7:6 Tumefunguliwa
katika sheria.
·
Warumi 8:3-4 Sheria
imekwisha kutimizwa
·
Warumi 10:4 Kristo ndiye
mwisho wa Sheria
·
Warumi 13:8, 10 Upendo
huitimiza Sheria.
·
1Wakorintho 9:20 Mimi
mwenyewe siko chini ya sheria.
·
Wagalatia 2:16
hatuhesabiwi haki kwa Matendo ya Sheria.
·
Wagalatia 2:21 ikiwa
haki Hupatikana kwa sheria Basi kristo alikufa bure
·
Wagalatia 3:2 Roho
hapokelewi kwa Sheria
·
Wagalatia 3:5 Je miujiza
inapatikana kwa sheria?
·
Wagalatia 3:10 Kwa maana
wale walio wa matendo ya sheria wako chini ya laana maana imeandikwwa
amelaaniwa kila mtu asiyedumu katika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha
torati ayafanye.
·
Wagalatia 3:11 Hakuna
mtu ahesabiwaye haki mbele za Mungu atika sheria.
·
Wagalatia 3:13 Kristo
alitukomboa katika laana ya torati
·
Wagalatia 3:17-29 si Kwa
sheria bali kwa imani twapokea mbaraka wa Ibrahim.
·
Wagalatia 5:3-4 mmetengwa
na Kristo ninyi mtakao kuhesabiwa haki kwa sheria.
·
Galatians 5:14 sheria
inatimizwa katika upendo
·
Galatians 5:18 lakini
mkiongozwa na Roho hamko chini ya sheria
·
Galatians 6:2 sheria ya
Kristo.
·
Wafilipi 3:9 haki
ipatikanayo kwa imani
·
1Timotheo 1;9 Sheria haimuhusu mtu wa haki bali waasi
·
Waebrania 7;12 Ukuhani
ukibadilika ni lazima na sheria ibadilike.
Waebrania 7:28 baada ya sheria Mwana
Waebrania 7:28 baada ya sheria Mwana
·
Waebrania 8:6 Tuko chini
ya Agano lililobora zaidi.
·
Waebrania 8:7 baada ya
lile la kwanza la pili.
·
Waebrania 8:13 Kwa kule kusema agano jipya amelifanya
lile la kwanza kuwa kuu kuu
·
Waebrania 9-10 Ukuhani
mpya na dhabihu moja inayodumu milele.
Kimsingi kanisa
lingefaidika sana kama kila mkristo angepeleka fedha na kwa makusudi ya
kutimiza agizo kuu. na angalau
kibinadamu fungu la kumi au zaka ingelikuwa jibu la swala hilo na hususani kama
ingekuwa inaishia katika hilo tu basi hali ya kanisa kifedha ingekuwa duni
zaidi. Fungu la kumi linazuia utoaji wa fedha zaidi kuliko tunavyofikiri kwa
sababu kama unaongozwa na sheria na sio Roho ungetoa au utatoa kiasi hicho tu
na hakuna hata mtu mmoja angetoa 20%, 30%, 40%. Ya mapato yake na nini
kinafanya hilo lisiwezekane ni dini na sheria na sio kusikia kunakotokana na
imani Wagalatia 3;2b. Jijaribuni wenyewe kwamba mmekuwa katika imani.
Je Zaka (Fungu la Kumi) ni sehemu ya Agano Jipya?
Kama ndio basi Mungu
aliamua kulificha hilo kwa Paulo Mtume na kwa waandishi wengine wa agano jipya,
kwani ukitaka kufundisha kuhusu zaka hata ukijaribu vipi hutaweza kuhalalisha
mpaka utumie agano la kale ili ufundishe kuhusu zaka, wengine watajitetea kuwa
zaka ilikuweko kabla ya sheria na ikawa sehemu ya sheria kwa msingi huo hata
sasa inapaswa kuweko? Ni sawa na jiulize kuhusu kutahiri je? Hakukuweko kabla
ya sheria? Mwanzo 17;24 na ikawa sehemu ya sheria je inapaswa leo
kutahiriwa?baadhi ya mitume katika agano jipya walijaribu kufanya hayo Matedno
15;5-11 wagalatia 2;11 Lakini Paulo hakufanya hayo hata moja
Kitabu cha waebrania
kinaonyesha kuwa Abraham alimpa zaka Melkizedeki lakini ni katika kifungu
hichohicho inapozungumzwa kuwa sheria ilibadilishwa Waebrania 7;12, waebrania
8;13 na 9;1.inazungumza kuwa agano la kwanza lilikuwa na kawaida zake za ibada
(regulations) na zaka ni sehemu ya taratibu hizo likaondolewa waebrania 10;9
yaani na zaka pia iliondolewa ili kustawisha agano la pili ambalo zaka si
sehemu ya agano hiliambalo huandikwa moyoni katika nia Waebrania 10;16 je Mungu ameandika zaka
katika moyo wako na nia yako au ni kongwa? Zaka haikuandikwa katika moyo wangu
wala nia yangu.
Hoja ya Melkizedeki
Baadhi wanasema kuwa
melkizedeki alikuwa ni Yesu Kristo, na kwa sababu hiyo kama Ibrahimu alitoa
zaka basi Kristo anapaswa kupokea zaka leo. Hii ni dhana tu isiyo na msingi wa
kimaandiko. Na tatizo kubwa ni kuwa Yesu sio Mtu na wala sio Melkizedeki Huduma
ya Kikuhani ya kwa mfano wa Melkizedeki Yesu Kristo si ya kidunia.
Melkizedeki alikuwa
Kuhani aliyembariki Ibrahimu katika mifumo mikuu miwili Kwa sheria alichukua
Zaka na kwa Neema walishiriki mkate na divai Mwanzo 14; 18 Yesu naye ni Kuhani
wa mifumo miwili Kanisa (Mataifa sasa) na mfumo wa Hekalu (mfumo wa ibada za
kiyahudi baada ya unyakuo) katika Yerusalem mpya Ufunuo 21;9-27.
Je Yesu alikuwa Melkizedeki?
Katika Mwanzo 14;17-23
tunaona Melkizedeki akijitokeza kwa mara ya kwanza na mfalme wa Sodoma
walikwenda kumlakikatika bonde la shawe Abrahamu alipokuwa ametoka kumpiga
mfalme Kedorlaoma na Melkizedeki mfalme wa salem akaleta mkate na divai naye
alikuwa kuhani wa Mungu aliye juu sana
akambariki na kusema Abrahamu na abarikiwe na Mungu aliye juu
sana, muumba wa mbingu na nchi na ahimidiwe Mungu aliye juu sana aliyewatia
adui zako mikononi mwako .Abrahamu akampa fungu la kumi la vitu vyote. Na
Mfalme wa Sodoma alimwambia Ibarahim nipe mimi hao watu na hizo mali uchukue
wewe, Abrahamu akamwambia nimeinua mkono wangu kwa Bwana Mungu aliye juu sana
Muumba wa mbing na nchi ya kuwa sitatwaa
uzi wala gidamu usije ukasema nimemtajirisha Abraham
Biblia inamtaja
Melkizedek kama Mfalme na kuhani na inaelezwa kuwa abrahamu alimpa zaka 10 ya
yote hii ilikua ni kivuli cha utoaji wa zaka na alipokea mkate na divai kivuli
cha ushirika wa meza ya Bwana . kwa ufupi Melkizedeki alifahamu kuwa anabariki
vyote Sheria na Neema kwa Ibrahimu.
Zaburi 110 ni Eneo
lingine linalomzungumzia Melkizedeki.
BWANA amwambia
Bwana
wangu:
“Keti mkono wangu wa kuume,
mpaka niwafanye adui zako kuwa
mahali pa
Kuweka miguu yako.’’
BWANA ataeneza fimbo yako ya
utawala
kutoka Sayuni,
Utatawala katikati ya adui zako.
Askari wako
watajitolea kwa moyo
Katika siku yako ya vita.
Ukiwa umevikwa fahari takatifu,
kutoka kwenye tumbo la
mapambazuko
Utapokea umande wa ujana wako.
BWANA ameapa,
naye hatabadilisha mawazo yake:
“Wewe ni kuhani milele,
kwa mfano wa Melekizedeki.’’
Bwana yuko mkono
wako wa kuume,
atawaseta wafalme siku
ya ghadhabu yake.
Atawahukumu
mataifa, akilundika mizoga
na kuwaseta watawala wa dunia
nzima.
Atakunywa maji katika kijito
kando ya njia, kwa hiyo atainua kichwa chake juu.
Unabii huu unatambulika kama Mungu baba
anamwambia Yesu kuwa atakuwa kuhani milele kwa mfano wa Melkizedek kwa ujumla
zaburi hii inatabiri matukio yatakayotukia baada ya Msalaba nah ii inamaanisha
kuwa ukuhani huo ungeanza baada ya kifo cha Msalaba na inaonekana kama
Waebrania 5;1 inasema Maana kila kuhani mkuu aliyetwaliwa katika wanadamu amewekwa
kwaajili ya wanadamu katika mambo yamuhusuyo Mungu ili atoe matoleo na dhabihu
kwaajili ya dhambi, Inaonekana maaandiko
haya yanayozungumzia ukuhani wa Kristo yanazungumza kuhusu kuhani aliyetwaliwa
katika wanadamu je ni wakati gani Mungu alifanyika mwanadamu? Mungu hakufanyika
mwanadamu wakati wa Ibrahimu, na mstari wa pili kuhani alitakiwa kuwa anayeujua
udhaifu wa wanadamu ili kuchukuliana nao sasa ni wakati gani Mungu alikuwa
katika hali hiyo bila shaka ni wakati Kristo alipozaliwa na Mariam
Waebrania 5;7 inasema “siku hizo za
mwili wake” na mstari wa 10 unasema sasa
anatajwa kama kuhani mkuu kwa mfano wa Melkizedeki kwa msingi huo ni wazi
kabisa kuwa Melkizedeki wa wakati wa siku za Ibrahimu hakuwa Kristo na
waebrania 7;1-28 inaangalia ulinganifu wa Melkizedeki na Yesu Kristo kweli wote
walikuwa makuhani lakini katika mitindo tofauti Waebrania 7;3 Je Melkizedeki
hakuwa na baba wala mwana? Hapana alikuwa na baba na mwana lakini Roho wa Mungu
aliruhusu kutokunukuliwa kwa uzao wake ili kuweka unabii unaohusiana na Kristo
ambaye ni Mungu Waebrania 7;3, Waebrania 7;4, Maandiko yanaonyesha kuwa
Melikizedeki alikuwa ni mwanadamu,waebrania 7;6.inazungumza kuwa uzao wa
Melkizedeki hautoki katika Ibrahimu, lakini wa Yesu unatoka katika Ibrahimu
Mathayo 1;1-17,waebrania 7;15 inazungumzia kuhani kwa mfano wa Melkizedeki kwa
mfano haimaanishi ni kufanana au ni sawa inamaanisha kama.Waebrania 7;22
inasema Yesu amekuwa maana yake siku zote yuko au amekuwa kuhani kwa mfano wa
Melkizedeki. Na ingawa kuna maswala yenye kufanana kati ya Yesu na Melkizedeki
biblia inaweka wazi kuwa ni watu wawili tofauti waebrania 8;4 Jambo
linalokubaliana na zaburi 110 uketi mkono wangu wa kuume linalomaanisha ni
huduma ya kikuhani ya Yesu Kristo Mbinguni.baada ya kuliweka hilo sawa sasa
turejee katika smo letu kuhusu zaka
Je
Yesu amesema nini kuhusu zaka?
Luka 11; 42 “Ole wenu Mafarisayo kwa
kuwa mnatoa zaka za mnnaa na mchicha na kila mboga na huku mwaacha mambo ya
adili na upendo wa Mungu iliwapasa kufanya hayo ya kwanza bila kuyaacha hayo ya
pili”.
Mathayo 23; 23-24 “Ole wenu waandishi na
Mafarisayo wanafiki kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na Bizari na jira lakini
mmeacha mambo makuu ya sheria yaani adili na rehema na imani hayo imewapa
kuyafanya wala yale mengine msiyaache Viongozi vipofu, wenye kuchuja mbu na
kumeza ngamia.”
Mathayo 5; 17-20 “Msidhani ya kuwa
nalikuja kuitangua torati au manabii la sikuja kutangua bali kutimiliza kwa
maana nawaambia, mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka yodi moja wala nukta moja
ya torati haitaondoka hata yote yatimie, basi mtu yeyote atakayevunja amri moja
kati ya hizi zilizo ndogo na kuwafundisha watu hivyo ataitwa mdogo kabisa
katika ufalme wa mbinguni, maana nawaambia ya kwamba haki yenu isipozidi hiyo
haki ya waandishi na Mafarisayo hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.
Mstari wa 17 unanifurahisha zaidi kwani
unatumia neno Torati na Manabii na Mstari wa 18 anatumia Torati, kuuelewa
mstari huu ni moja ya jambo la muhimu sana
na kuelewa muktadha wake katika mazingira aliyoyasemea sasa kwa
kuiangalia historia ya mwanadamu tunaona kuwa kutoka Adamu mpaka Abrahamu na
Musa ni miaka 2000 na kutoka Musa mpaka
Yohana Mbatizaji na Yesu iko miaka 2000, na kutoka kifo cha Yesu kuzikwa na
kufufuka mpaka sasa ni miaka 2000 vipindi hivi vikuu vitatu ni vya muhimu sana,
katika kushughulikia maswala ya Mungu anavyojishughulisha na mwanadamu kutoka
Abrahamu mpaka wakati wa Musa ni kipindi cha Mpito (miaka 430) kufikia wakati
wa sheria na manabii, Ibrahimu alikuwa mtu wa Muhimu sana kwani maisha yake yanazungumza
kuhusu maswala makuu mawili maisha yake yanazungumza kuhusu Wayahudi chini ya
sheria na Wakristo chini ya Neema kwa kuwa maisha ya Ibarahimu yana wazo la [kuhesabiwa haki kwa imani] na wazo la
sheria [Zaka na Tohara]
Sheria ilitolewa kwa wayahudi ni mfumo
wa kiyahudi Luka 16;16 ( torati na manabii vilikuwa ni mpaka wakati wa Yohana
mbatizaji) Biblia inasema ni mfumo uliotumika mpaka wakati wa Yohana sasa nini
kinafuata baada ya Yohana mbatizaji ni kipindi kingine cha mpito kutoka Yohana mbatizaji
mpaka wakati wa Mateso, kifo kuzikwa na kufufuka kwa Bwana Yesu Wagalatia 4;4-5
inasema Yesu alizaliwa chini ya sheria Yesu ndiye alikuwa funguo ya kipindi cha
mpito alifundisha agano la kale Mathayo 5;17-20, Luka 11;42, Mathayo 23;23-24
na alifundisha sheria ya kifalme yaani Agano jipyaMathayo 22;37 na Warumi 13;9
kwa hiyo anaposema usizini,usiue, usiibe, usishuhudie uongo usitamani n.k
anasema mpende jirani yako kama nafsi yako.
Baada ya ufufuo alipokuwa ameyatimiza
matakwa ya sheria kwa damu yake
tumeingia katika mfumo mpya na agano jipya na ukuhani mpya na (zaka ilikuwa ni
ya ukuhani wa walawi) sawa na maagizo ya sheria, sheria Torati ilikuja kwa
mkono wa Musa Lakini neema na kweli zimekuja kwa mkono wa Yesu Kristo Yohana
1;17, mfumo wa Musa ulikuwa ni torati yaani zaka, siguse, msishike, msionje,
kula aina Fulani ya wanyama wengine msile, n.k lakini mfumo mpya katika Kristo
unahitimishwa na warumi 6;14 Hatuko chini ya sheria yaani mfumo wa Musa bali
tuko chini ya neema, kwa msingi huo sisi tulio wa mfumo wa neema hatupaswi tena
kufuata mfumo wa agano la kale kama kutoa dhabihu za kuchinja wanyama,kuchoma
ubani, kukusanyika hekaluni kwa ibada za hekaluni na halikadhalika
kujishughulisha na zaka au kutahiriwa au kushika sabato “Kumbukumbu la torati
32;21”.
Sasa tunaporejea katika mstari wetu wa
18 wakati Yesu anaendelea kuzungumza alikazia kuitimiza sheria yaani ya (Musa)
na baadhi ya Unabii (Eliya) na hii nduio maana mstari wa 18 unajumuisha na
manabii ikiwa na maana baadhi ya unabii hautatimia mpaka wakati wa kuja kwake
mara ya pili, kwa wayahudi walifikiri kuwa wakati ule Kristo angeweza
kusimamisha ufalme na angetanguliwa na Eliya lakini wayahudi hawakujua kuwa
kuna nafasi iliyo wazi kutoka Kristo aliyeteseka Isaya 53 na Kristo Mtawala
Ufunuo 21;15-16 na kwa msingi huo kuna nafasi kati ya kuitimiza sheria (Musa)
na kuitimiza Manabii (Eliya) na naamini
kuwa utakuwa umeona wazi kabisa kuwa sheria imetimizwa.
Ni wazi kabisa wayahudi walielewa kuwa Mitume wanafundisha mafundisho
tofauti mapya na ambayo yanapingana na sheria Matendo 18; 13 Biblia inasema
hivi “wakisema mtu huyu huwavuta watu ili wamuabudu Mungu kinyume cha sheria”
Matendo 21; 21. “Nao wameambiwa habari zako ya kwamba unawafundisha Wayahudi
wote wakaao Katika Mataifa kumwacha Musa ukiwaambia wasiwatahiri watoto wao
wala wasizifuate desturi.” Yesu alizaliwa chini ya sheria lakini pia ndiye
mwisho wa sheria Warumi 10;4. Je sheria ni nini? Inapatikana wapi je ni kwenye
agano la kale? Baadhi hudhani ni vitabu vitano vya Musa, lakini huu ni mgawanyo
tu, Yesu ananukuu na kusema imeandikwa katika sheria katika Yohana 15;25
ananukuu Zaburi 35;19,69;4 na katika 1Wakoritho 14;21 walinukuu kutoka katika
sheria lakini ni Isaya 28;11 kwa msingi huo nafikiri kwamba Mungu anaiita
migawanyo yote hiyo kuwa ni sheria na kutoka Musa mpaka wakati wa Yohana
mbatizaji ilikuwa ni sheria (Musa) sheria na Manabii (Elia) inawakilisha
maswala ambayo yamekwisha kupita na sasa tuko chini ya agano jipya.
Ni ukweli kuwa ziko nabii ambazo bado
hazijatimizwa kazi ya Eliya haijakamilika, Lakini ya Musa tayari, kwa sababu
kuna mvunjiko mkubwa wa Mungu kujishughulisha na wayahudi kwa sasa unabii
unaonyesha atakapokuja tena atafanya kazi kimsingi na wayahudi tena Zekaria
2;12,8;23 Yesu aliposema Livunjeni Hekalu hili name katika siku tatu
nitalijenga(Siku moja ni sawa na miaka 100). hakuwa anamaanisha tu mwili wake
ambao ungefufuka siku ya tatu lakini pia alikuwa anazungumzia Hekalu halisi
yaani Mfumo wa tamaduni za Kiyahudi ambao angeujenga upya katika siku tatu
Mathayo 27;51”Na tazama pazia la Hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata
nchi ikatetemeka miamba ikapasuka” hii ina maana Yesu na Hekalu walikufa siku
moja wote walitoa roho, Hekalu litakapofufuka Mungu ataanza kufanya kazi na
wayahudi chini ya sheria na sheria ilitolewa kwa wayahudi na sio kwa Mataifa.
Ukweli kuwa Ibrahim hakuwa anatoa zaka
kama sheria alitoa zaka kama kivuli tu kama ilivyo kwa Yohana mbatizaji ni
kivuli cha Eliya. Kwa msingi huo hakuna ushahidi wa maandiko mengine
yanayoonyesha kuwa Melkizedeki alikuwa anakuja tena na tena kuchukua zaka kwani
hakukuwa na sheria wakati huo (Musa na Makuhani wa Lawi)
Je
tuko sawa kwa Mungu tukiifuata sheria Leo?
Je ni haki kuisimamia sheria na je
tumeamriwa kutoa zaka leo? Na je tusipoitoa hatuko sawa na Mungu Biblia inasema
katika Wagalatia 2;21 “Siibatili neema
ya Mungu maana ikiwa haki hupatikana kwa sheria basi Kristo alikufa Bure” haki
yetu inapatikana kwa kusikia kunakotokana na imani Wagalatia 3;2 “.....au kwa
kusikia kunakotokana na imani?”
Sheria ilikuwa ni Mwalimu ilitufundisha
kutoa zaka wagalatia 3;25 kwa kuwa sasa imani imekuja hatuhitaji tena Mwalimu,
wale walio chini wa sheria ni watumwa wa sheria Wagalatia 4;7 sisi sio watumwa
tena Warumi 9;31-32 kwa njia ya imani na sio matendo, Sheria ya zaka inaweka
pia deni kubwa sana la fedha Amosi 5;11 Kama hatulipi zaka tuko katika shida
sheria ina madai kadhaa ili uwe sahii kwa Yule unayempa nah ii itaharibi kabisa
asili yetu ya haki katika agano jipya
Amosi 5;7 na ndio maana aliye
chini ya sheria amelaaniwa Wagalatia 3;10
Kuiacha
sheria ni jambo Gumu kwa wapendwa wengi!
Maisha ya Abrahamu yana kitu cha
kutufundisha kuhusu sheria, Abrahamu alikuwa na watoto wawili Ishmael (Sheria)
na Isaka (Ahadi) Wagalatia 4;21-31,5;1-10, Mwana wa Ibrahimu aliyezaliwa
kupitia Hajiri ambaye alipatikana kwa mujibu wa sheria ya kimwili yaani sheria
na tamaduni za wakati huo, mwana wa Abrahamu ambaye alimpata kupitia Sara ni
Isaka mwana wa Ahadi. Siku moja Roho Mtakatifu alimwambia Abrahamu Kupitia Sara
Mfukuze mjakazi na mwanawe yaani (Agano la kale) na (zaka) Kisha Mungu Baba
alimwambia Abrahamu kukubali kumuondoa Ishamel milele au nje ya kambi yake
nafikiri unaweza kuhisi maumivu gani aliyoyapata Abrahamu unaweza kuona huenda
alijiuliza maswala kadhaa kwa Mungu je sitaweza kumtembelea hata mara moja kwa
wiki?(Sabato)Lakini Mungu akamwambia hapana, akauliza tena je siweszi kupeleka
hata kiasi Fulani cha fedha (Zaka) Bwana akamwambia hapana je naweza kumpelekea
baadhi ya vyakula au mlo maalumu (Sheria za vyakula) jibu ni hapana atakuwa
mwenyewe huko jangwani je siwezi kumlinda (Hukumu Ya kupiga mawe) hapana , je
siwezi kumtembelea katika siku kadhaa za sikukuu? (Kushika siku, miezi na
sikukuu za kiyahudi) Bado Mungu alisema hapana, je Mungu siwezi ku.... lakin
Mungu aliendelea kusema Hapana, hapana, hapana.
Sheria yaani (Ishmael yaani zaka) lazima
awekwe nje ya kambi Neema (Kanisa). Wakristo (Neema) wanaweza kujaribu kuishika
sheria (Ishmael/Waarabu) Lakini sheria (Ishael/Waarabu) wataiharibu Neema
(Isaka) Isaka (Neema) pekee anaruhusiwa kuishi ndani ya kambi, ishimael
haruhusiwi kwani anamdhihaki atamuua motto wa ahadi (Ahadi, Isaka, Neema).
Ukweli huu unabaki kuwa kweli jana leo na hata mlele.
Haijalishi inatuuma vipi kuhusu kuiacha
sheria lakini ni lazima itupwe nje ya kanisa hili ni kongwa lazima litupwe
jangwani, kama wachungaji najua tunajua umuhimu wa zaka katika kanisa na
mazingira yake na ni yenye faida kubwa sana kanisani, ni kweli kama daktari
anaweza kuona umuhimu wa Tohara kwa wanaume ina faida nyingi sana, kama
mtaalamu wa tiba mbadala anaweza kuona umuhimu wa kujihadhari na baadhi ya
vyakula katika kuimarisha afya zetu lakini inatupasa kuweka mbali haya yote
Tohara, Zaka,agano la kale na taratibu zake na kutii matakwa ya Mungu Hajiri na
Mwanaye ni lazima wawe nje ya kambi hakuna manungu’uniko hakuna kujiuliza
maswali.
Kanuni
za utoaji katika gano jipya
Ni muhimu kufahamu kuwa baada ya
kulivunja kongwa la sheria la zaka ni muhimu sasa kufahamu kanuni za utoaji
katika agano jipya inaonekana katika Wagalatia 6;6, inasema “mwanafunzi na
amshirikishe mkufunzi wake katika mema yote” andiko hili linafanana na ile kazi
ya zaka zaka ilikuwa kwaajili ya ukuhani wa kilawi, lakini hapa
tuafundishwa kuwashirikisha mema wale
wanaotufundisha neno la Mungu kwa maana ningine ni jukumu la wte wanaofundishwa
neno la Mungu kuwasaidia wale wanaowafundisha neno la Mungu kwa kuwapa vitu vya
kimwili 1Koritho 9;14, 1Timotheo 5;18 “Usimfunge ng’ombe kinywa apurapo
nafaka” na kila mtenda kazi anastahili
ujira wake naamini hili ndilo jibu la wale wanaojiuliza itakuaje? Tukiamini
kuwa agano la kale lilikuwa linatoa kivuli tu cha agano jipya swali linaweza
kuwa inakuwaje endapo tutaachana na zaka? Naamini unaondoka katika kongwa la
sheria sasa na kuifurahia neema ya Mungu na uhuru tulionao katika Kristo jambo
la msingi sasa ni kumsikiliza Roho wa Mungu anakusukuma nini moyoni unapaswa
kusaidia pale unapolishwa neno la Mungu kwa kanuni hii ya upendo na msukumo wa
moyo na kumpenda kwako Mungu.
Tunafundishwa pia kanuni ya kupanda na
kuvuna Wagalatia 6;7,2Wakoritho 9;6 upandaji huu unaendana na kuvuna lakini sio
deni kuwa ni lazima uvune, tunafundishwa kutoa kwa kadiri ya neema na moyo
2wakoritho 8;2-3 kwa msingi huo katika Agano jipya kutoa ni mpango au msukumo
wa moyoni na sio sheria, kutoa huko kwa moyo sio kule kwa manunguniko na
maumivu bali kwa ukarimu 2Koritho 9;7 ni kwa msukumo wa huruma waefeso 4;28
kuwagawia wahitaji, kuacha ubinafsi, 2Wakoritho 11;9, kwa nini Paulo
asifundishe kuhusu zaka?Paulo anazungumza kuhusu ujira 1Timotheo 5;18
anazungumza pia kuhusu zawadi na sio kupokea zaka na msaada na sio zaka au
mafungu wafilipi 4;15-19, ni kwa moyo 2Wakoritho 8;16, Mungu ameiandika
sheriaya agano jipya katika mioyo yetu kwa msingi huo viongozi wa kanisa
wanapaswa kumuamini Mungu kuwa wasshirika wao watamsikiliza Mungu katika mioyo
yao na siku zote njia ya mwanadamu ni pamoja na kutokuamini tunaweza kuhubiri
injili hata bila ujira 2wakoritho 11;7. Kama nitalipa zaka nitakuwa na la
kujisifia lakini katika Kristo ni kwa neema na Imani na sio kwa matendo si kwa
matedno mtu awaye yote asijisifu Efeso 2;8-9.
Zaka kwa kweli ni kodi ndani ya uhuru
wetu katika Kristo ni muhimu kwetu kuasi kodi hii na kudai uhuru wetu katika
Kristo, Mungu anataka kuweko na uhuru ambao utaruhusu utoaji wa imani na
wakimiujiza ambapo watu watatoa kwa ukarimu hata zaidi ya zaka imebainika hata
katika inchi ambazo wanalegeza kodi uchumi huimarika na wanapata sana kuliko
katika inchi zinazokazia, je unadhani kama kanisa litaachana na kutegemea zaka
kama mabaki ya sheria na wakaundishwa kutoa kwa moyo uchumi wa kanisa
utaongezeka? Jibu ni ndiyo 2Wakoritho 8;2 Biblia inasema “Maana walipokuwa
wakijaribiwa kwa dhiki nyingi, wingi wa furaha yao na umasikini wao ulikuwa
mwingi uliwaongezea utajiri wa ukarimuwao maana nawashuhudia kwamba kwa uwezo
wao na zaidi ya uwezo wao kwa hiyari yao wenyewe walitoa vitu vyao”unaona watu masikini
sana lakini walitoa zaidi ya kawaida huu ni utoaji wa kiimani na kimuujiza ni
wazi kuwa hata ufanye nini huwezi kupata ushahidi wa kimaandiko katika agano
jipya ili kupata mashahidi wawili au watatu na kufanya fundisho 2Wakoritho
13;1, Warumi 8;2 na tuifuate sheria ya Roho wa uzima.
Hebu jaribu kuwaza mpezni msomaji kuhusu
sheria za agano lake zilivyokuwa ngumu Hekalu la agano la kel na sheria zake
yaani pamoja na zaka zimekufa hekalu limekufa miaka 2000 iliyopita Mathayo
27;51 Warumi 7;2 hatuwezi tena kuendesha farasi aliyekufa sasa ni zaidi ya
miaka 2000 tangu hekalu na taratibu zake zilipozikwa kwa nii tuendelee kuabudu
kwa namna za kihekalu?Je inatupasa kutoa sadaka za kuteketezwa sasa? Je
inatupasa kutahiriwa sasa? Je ni sheria ngapi za agano la kale tunazifuata
katika mtindo huu mpya wa kuabudu? Ni nini makusudi ya kifo cha Kristo? Je
sadaka yake haitoshelezi? Efeso 2;15, Wakolosai 2;14-23
Fedha zinazolipwa zaka leo zinaweza
kulaaniwa
Waangalie wanandoa ambao wamekuwa
wakilipa zaka kwa miaka mingi leo makanisani je wamewahi kutoa asilimia
Ishirini ya mapato yao? Jibu ni la Binafsi naamini tunapaswa kutenda vema zaidi
ya wakati wa agano la kale, Zaka wanazotoa wengi ni katika mfumo ule wa agano
la kale katika mfumo huo 10% walawi 27;30 na ingine ni ile itolewayo kwa upendo
Warumi 13;8, wengi wameacha sheria iliyoko katika mioyo yaom wanafuata ile
iliyoandikwa katika mbaombili za mawe Warumi 14;23 na wanaacha kuitii sheria ya
kifalme yaani imani na upendo ambao ndio udongo mzuri. Kuna maandiko zaidi ya
39 katika agano la kale na agano jipya yanayozungumzia au kugusia zaka lakini
ni 7 tu kati ya hayo ni ya agano jipya esu alioyatimiza hayo yote 39 na hatuko
chini ya deni katika agano la kale usipolipa zaka ya shs 3;76 utadaiwa kulipa
shs 9 na tukiifuata hii kwa asilimia 99.9999 tutakuwa chini ya laana asilimia
100 je Mungu angetupenda tena? Si vema kuwatishia waamini katika agano jipya
kuwa watalaaniwa kwa kutokutoa zaka laana? Ndani ya agano jipya? Yesu alikufa
kwaajili gani sasa? Wale washikao sheria wamelaaniwa Wagalatia 1;6-8 na wale
wanaowahubiri watu injili nyingine ya kuambatana na sheria ndani ya Kristo
wamelaaniwa Warumi 4;15 “sheria ndiyo ifanyayo hasira Pasipokuwa na sheria
hapana kosa”
Utoaji
halisia
Kwa bahati mbaya unaweza kusoma kitabu
hiki na ukaamua kutokutoa au kupunguza swala la utoaji nitakuomba usome tena na
tena mada hii ili uweze kuielewa vema kwa moyo wako na sio kwa kichwa chako,
utahitaji kichwa chaki kiasi kwaajili ya kujifunza maarifa, unahitaji kutumia
akili kiasi kupiga hesabu wakati unataka kutoa zaka lakii pia utahitaji kupiga
hesabu pia wakati unataka kujaribu kuacha kutoa vyote vinahitaji kichwa na sio
moyo Yakobo 2;26 inasema hivi na mwili pasipo roho imekufa kwa hiyo imani
pasipo matendo pia imekufa kama akili zako zitakuwa sawa utaendelea kutoa zaka
kwa sababu uko chini ya sheria na utumwa na utavuna haba Hagai 1;6 mtu ambaye
sio mtoaji amejitenga na tabia ya uungu kabisa.
Wengi wa wachungaji wanaosoma
habari hii watakubaliana name kuwa ni asilimia chache sana ya washirika
wanaotoa Fungu la Kumi kwa ujumla inaweza kuwa chini ya asilimia tano ya
washirika ndio wanaotoa zaka aibu kwa kanisa hii ni kwa nini kwa sababu
hawalijui neno la Mungu Mungu aliupenda ulimwengu na akamtoa.......Yohana 3;16
lazima tuwe na tabia ya uungu moja ya tabia ya uungu ni pamoja na kutoa Waefeso
5;1-2,
“Kwa
hiyo, mfuateni Mungu kama watoto wapendwao, Mkiishi maisha ya upendo, kama vile
Kristo alivyotupenda sisi akajitoa kwa ajili yetu kuwa sadaka yenye harufu
nzuri na dhabihu kwa Mungu”.Luka
6;38 “Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa. Kipimo cha kujaa na kushindiliwa na
kusukwasukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa
kipimo kile kile mpimacho, ndicho mtakachopimiwa.”Matendo 20;35 “Ni heri kutoa
kuliko Kupokea” Biblia inaahadi nyingi sana kuhusu utoaji kadiri unavyojitoa
ndivyo unavyofungua mlango wa kupokea zaidi huu ni wakati wa mwisho Mungu
anakusudia kuleta uamsho mkubwa sana ambao unahitaji fedha kufanikisha kazi
yake ma inahitaji wakristo wakarimu nimalizie kwa kusema hivi katika agano
jipya zaka ni 100% kila kitu ni cha Mungu na hivyo tumkumbuke Mungu ka
kuisapoti kazi yake, usijifunge katika kifungo cha laana ya zaka ya agano la
kale bali ruhusu Mungu akuongoze ukitoa zaidi ni vema na ukiwa na kichache
usijihukumu.