Jumapili, 19 Julai 2026

SHULE YA HUDUMA!


Waefeso 4:11-12 “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe;”



Utangulizi

Shule ya huduma ni mafundisho maalumu ya kibiblia  yaliyoandaliwa  na Rev. Innocent Samuel Kamote kwa kusudi la kuwaadaa watu wa Mungu kuwa tayari kwaajili ya huduma za kichungaji ndani ya kanisa, huduma za kikanisa, na huduma zote za kiroho kupita mafundisho ya Biblia, mafundisho haya huandaliwa kwa programu maalumu zinazolingana na maono ya kanisa letu na mtindo ambao sisi tumechagua kumtumikia Mungu kwa huo, Ni muhimu kujikumbusha kuwa kusudi kubwa la Mungu kutuokoa sio kwaajili ya kuhudhuria ibada makanisani pekee bali kwaajili ya kumtumikia yeye, Mungu anachukizwa sana na wakristo waliodumaa kiroho ambao anawatarajia labda wangelikuwa walimu wa wengine lakini kwa kutokufahamu wao wamebaki kuwa wachanga kwa miaka mingi sasa.

Waebrania 5:11-14 “Ambaye tuna maneno mengi ya kunena katika habari zake; na ni shida kuyaeleza kwa kuwa mmekuwa wavivu wa kusikia. Kwa maana, iwapasapo kuwa waalimu, (maana wakati mwingi umepita), mnahitaji kufundishwa na mtu mafundisho ya kwanza ya maneno ya Mungu; nanyi mmekuwa mnahitaji maziwa wala si chakula kigumu. Kwa maana kila mtu atumiaye maziwa hajui sana neno la haki, kwa kuwa ni mtoto mchanga. Lakini chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa kupambanua mema na mabaya.”

Mungu anapotuokoa anataka tuimarike kwanza kiroho na kisha baada ya kuimarika atutumie sisi kuimarisha wengine, kwa hiyo Mungu hutukuza na kutukomaza kiroho, ili tuje tumtumikie na kuhakikisha kuwa kazi ya huduma inatendeka, kwa hiyo kila mtu aliyeokoka anapaswa kukua na kufikia ngazi ya kuwa mtenda kazi yaani watu wanaowahudumia wengine katika mwili wa Kristo, sio mpango wa Mungu wewe ubaki kama ulivyo kila mwaka!

Luka 22:31-32 “Akasema, Simoni, Simoni, tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano; lakini nimekuombea wewe ili imani yako isitindike; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako.”

Leo tunapochukua muda kuzama kwa kina na mapana na marefu katika kujifunza shule hii maalumu ya huduma, Mungu anataka kukuimarisha na kuleta ufahamu na ukomavu kwako ili wewe uweze kuwa msimamizi wa roho za watu ndani ya kanisa letu na kuwasaidia wengine, tutajifunza somo hili  shule ya huduma kwa kuzingatia vipengele vikuu muhimu vitatu vifuatayo:-


  • Sifa za mwanafunzi wa shule ya huduma.
  • Umuhimu wa kuwa na uzoefu katika huduma.
  • Mambo yatupasayo kufanya kama wahudumu katika kanisa.

 

Sifa za mwanafunzi wa shule ya huduma.

Nyakati za kanisa la kwanza walipochagua watenda kazi walikuwa makini sana kuzingatia sifa  za wale  waliowachagua walijua kuwa wale watakaochaguliwa au kuteuliwa kusaidia kazi mbalimbali wana sifa na vigezo vyenye kuwafaa sana na kuwa wanaaminika na ni wanyenyekevu na watii ambao kupitia wao wataisaidia kazi ya Mungu, na kuwasaidia watu wote walioamini kusimama imara katika Bwana na kuwafundisha wengine kuishika imani vile vile kama wao walivyofundishwa, tunaona kwa mfano Paulo Mtume alimchagua Timotheo mtu ambaye alikuwa anaheshimika sana katika Kanisa  kutokana na usafi wa Imani yake na sifa zake zilijulikana na watu wote wa makanisa yaliyokuwako Listra na Ikonio na baada ya kuongezeka kwake makanisa yakatiwa nguvu katika imani ona:-

Matendo 16:1-5 “Basi akafika Derbe na Listra, na hapo palikuwa na mwanafunzi mmoja jina lake Timotheo, mwana wa mwanamke Myahudi aliyeamini; lakini babaye alikuwa Myunani. Mtu huyo alishuhudiwa vema na ndugu waliokaa Listra na Ikonio.Paulo akamtaka huyo afuatane naye, akamtwaa akamtahiri kwa ajili ya Wayahudi waliokuwako pande zile; kwa maana wote walijua ya kuwa babaye ni Myunani. Basi walipokuwa wakipita kati ya miji ile, wakawapa zile amri zilizoamriwa na mitume na wazee walioko Yerusalemu, ili wazishike. Makanisa yakatiwa nguvu katika ile Imani, hesabu yao ikaongezeka kila siku.”

Ni imani yangu kuwa kila aliyechaguliwa/atakayechaguliwa kuingia katika shule hii ya huduma atakuwa mtii, atakuwa mnyenyekevu, atafuatilia kwa makini mafundisho yetu, na kujitahidi sana kuwa na sifa zinazohitajika sawa na maandiko ili aweze kutumika kwa uaminifu na kupitia wewe makanisa yetu yakatiwe nguvu na kuimarika lakini sio hivyo tu hesabu  ya watu wa makanisa yetu ikaongezeke kila iitwapo leo. Sasa basi mwanafunzi wa shule ya huduma anapaswa kuwa na sifa hizi kama neno la Mungu lisemavyo:-

  1. Kulishika neno la Mungu kama ulivyofundishwa – Mwanafunzi wa shule ya huduma anapaswa kuwa mtu anayeyaamini mafundisho yetu kuyakubali, kuyashahika na kuyafuata vile vile kama alivyofundishwa, mtu hawezi kuwa mwanafunzi wa mtu ambaye hayashiki mafundsho yake, mwanafunzi wetu ni lazima atusome, asome nia ya mitume wa kanisa kuwa wanataka nini wana maono gani na wanaelekea wapi, wanaamini nini, Misingi ya imani yetu ni ipi, kisha aanze kuishi sawa na kile alichojifunza kutoka kwetu na kukisimamia/tetea

 

Yohana 8:31-32 “Basi Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru.”

 

Yohana 14:23-24 “Yesu akajibu, akamwambia, Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake. Mtu asiyenipenda, yeye hayashiki maneno yangu; nalo neno mnalolisikia silo langu, ila ni lake Baba aliyenipeleka.”                                

 

Tito 1:7-9 “Maana imempasa askofu awe mtu asiyeshitakiwa neno, kwa kuwa ni wakili wa MUNGU; asiwe mtu wa kujipendeza nafsi yake, asiwe mwepesi wa hasira, asiwe mlevi wala mgomvi, asiwe mpenda mapato ya aibu. Bali awe mkaribishaji, mpenda wema, mwenye kiasi, mwenye haki, mtakatifu, mwenye kudhibiti nafsi yake; akilishika lile neno la imani vile vile kama alivyofundishwa, apate kuweza kuwaonya watu kwa mafundisho yenye uzima, na kuwashinda wenye kupinga.”

 

2Yohana 1:9-10 “Kila apitaye cheo, wala asidumu katika mafundisho ya Kristo, yeye hana Mungu. Yeye adumuye katika mafundisho hayo, huyo ana Baba na Mwana pia. Mtu akija kwenu, naye haleti mafundisho hayo, msimkaribishe nyumbani mwenu, wala msimpe salamu.”

 

Mwanafunzi wetu ni lazima awe yule anayeyashika mafundisho ya Kristo, awe mtu aliyeiva katika neno la Mungu, amejaa neno, analijua neno analipenda anamoyo wa kujifunza na mwenye sifa za kumpenda Yesu huyu anaweza kwenda na kile ambacho Kristo amekikusudia akilishika neno la imani vilevile kama alivyofundishwa!.

 

  1. Awe mwaminifu – Kila mwanafunzi ambaye amechaguliwa au kuteuliwa katika shule ya huduma anapaswa kujifunza kuwa mwaminifu, Imani yangu ni kuwa kila ambaye yuko katika darasa hili atakuwa mwaminifu, na kama hauna uaminifu utaomba Mungu sasa akupe kuwa mwaminifu, Mungu anakuleta katika darasa hili ili akukabidhi injili, na injili inapaswa kukabidhiwa kwa watu waaminifu ambao wana sifa ya kuikabidhi kwa wengine, uaminifu huu unaanzia katika kuhudhuria ibada, zote kufika katika mafundisho ya neno la Mungu, kuandika na kukua kiroho, na kuwa tayari  kuyapeleka hayo katika makanisa yetu yote na nje ya makanisa yetu ili kujenga umoja na afya ya  kiroho inayofanana vile vile sawa na ile aliyotuachia Kristo  na mitume wa Bwana

 

Matendo 2:41-42 “Nao waliolipokea neno lake wakabatizwa; na siku ile wakaongezeka watu wapata elfu tatu. Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali.”

 

2Timotheo 2:2 “Na mambo yale uliyoyasikia kwangu mbele ya mashahidi wengi, hayo uwakabidhi watu waaminifu watakaofaa kuwafundisha na wengine.”

 

1Wakorintho 4:1-2 “Mtu na atuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa Kristo, na mawakili wa siri za Mungu. Hapo tena inayohitajiwa katika mawakili, ndiyo mtu aonekane kuwa mwaminifu.”

 

Mathayo 24:45-47 “Ni nani basi yule mtumwa mwaminifu mwenye akili, ambaye bwana wake alimweka juu ya nyumba yake, awape watu chakula kwa wakati wake? Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta akifanya hivyo.  Amin, nawaambieni, atamweka juu ya vitu vyake vyote.”         

 

  1. Awe na unyenyekevu – Tunapoingia katika shule ya huduma kama hivi, tunaandaliwa kwa lengo, nia na makusudi ya kuwatumikia watu, watu ndio mtaji wetu mkubwa na sio vinginevyo, tunataka roho zao tuzipeleke kwa Kristo kwa ibada na  utumishi wake,  kwa hiyo ni lazima tujifunze unyenyekevu, hatuendi kuwa mabwana wakubwa tunakwenda kuwahudumia watu, Unyeyekevu unapaswa kuwa kama vazi letu iwe ni tabia yetu inayotutambulisha kila mahali, mavazi humtambulisha mtu, watumishi wa Kristo wanapaswa kutambulika kwa unyenyekevu wao kwa sababu ndivyo Bwana wetu Yesu alivyokua na sisi tu mawakili wake

 

Wakolosai 3:12-14 “Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi. Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu.”

 

Wafilipi 2:5-8 “Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.”

 

1Petro 5:2-5 “lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo. Wala si kama wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile kundi. Na Mchungaji mkuu atakapodhihirishwa, mtaipokea taji ya utukufu, ile isiyokauka. Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema.”

 

  1. Awe kielelezo – Katika shule ya huduma kila mwanafunzi anapaswa kudhamiria kuwa kielelezo chema katika Imani yetu na mafundisho yetu, Mungu anapoona kuwa sote tumedhamiria kuwa kielelezo kwa wale watakaoamini ataendelea kutuamini na kutuletea watu wengi zaidi, kwa sababu wanafunzi huigiza kila kitu kinachofanywa na walimu wao, wale tunaowahudumia wataigiza kila kitu kutoka kwetu hivyo neno la Mungu linasiistiza tuwe kielelezo yaani mfano wa kuigwa, wakristo wote watuigize sisi watuone ndio wa kuigizwa na sio wakrito pekee bali kila mahali katika jamii tuwe mfano bora wa kuigwa kwa tabia na mwenendo.

 

Neno kuwa kielelezo katika maandiko ya Kiyunani linatajwa kama neno “tupos” ambalo kwa kiingereza ni “a model for imitation” sawa na mfano wa kuigwa au kielelezo katika Imani, kila muhudumu anapaswa kuwa kielelezo katika usemi, mwenendo imani na usafi hakuna namna ya kukwepa jambo hili.

 

Tito 2:7-8 “katika mambo yote ukijionyesha wewe mwenyewe kuwa kielelezo cha matendo mema, na katika mafundisho yako ukionyesha usahihi na ustahivu, na maneno yenye uzima yasiyoweza kuhukumiwa makosa, ili yule mwenye kupinga atahayarike, kwa kuwa hana neno baya la kunena juu yetu.”

 

1Timotheo 4:12 “Mtu awaye yote asiudharau ujana wako, bali uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi.”

 

1Wathesalonike 1:4-7 “Kwa maana, ndugu mnaopendwa na Mungu, twajua uteule wenu; ya kwamba injili yetu haikuwafikia katika maneno tu, bali na katika nguvu, na katika Roho Mtakatifu, na uthibitifu mwingi; kama vile mnavyojua jinsi zilivyokuwa tabia zetu kwenu, kwa ajili yenu. Nanyi mkawa wafuasi wetu na wa Bwana, mkiisha kulipokea neno katika dhiki nyingi, pamoja na furaha ya Roho Mtakatifu. Hata mkawa kielelezo kwa watu wote waaminio katika Makedonia, na katika Akaya.”

 

  1. Nidhamu – Ni muhimu kufahamu kuwa kamwe huwezi kumtenganisha mwanafunzi na maswala ya nidhamu, wanafunzi wa Yesu ni lazima wawe na nidhamu, hii ni sawa na kujitia nidhamu, kuwa na kiasi, kujidhibiti, Neno nidhamu katika kiingereza linatamkwa “Discipline” ambalo kwaa asili linatokana na neno la Kilatini “Discipulus” ambalo maana yake ni “leaner” au “Student”  hii ndio maana ya mzizi wa neno “Disciples” yaani wanafunzi,  kwa msingi huo wanafunzi ni watu wanaojitawala, wanaojitia nidhamu, kama tunataka kumtumikia Mungu kwa kiwango kikubwa na kumpa Mungu nafasi ya kututumia lazima tujitie nidhamu, maisha matakatifu  yanahitaji nidhamu, maombi yanahitaji nidhamu, kujisomea neno kunahitaji nidhamu, kutunza upako kunahitaji nidhamu, kufunga kunahitaji nidhamu, kuabudu kunahitaji nidhamu.

 

1Wakorintho 9:24-27. “Je! Hamjui, ya kuwa wale washindanao kwa kupiga mbio, hupiga mbio wote, lakini apokeaye tuzo ni mmoja? Pigeni mbio namna hiyo, ili mpate. Na kila ashindanaye katika michezo hujizuia katika yote; basi hao hufanya hivyo kusudi wapokee taji iharibikayo; bali sisi tupokee taji isiyoharibika. Hata mimi napiga mbio vivyo hivyo, si kama asitaye; napigana ngumi vivyo hivyo, si kama apigaye hewa; bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa.”

               

  1. Upendo kwa watu – Kuna uhusino mkubwa sana kati ya kuhudumia watu na upendo, huduma zote zinazohusisha kuwahudumia watu zinahitaji uwe na upendo, na wala usiwe na ubinafsi, na unapaswa kuwa na huruma kwa watu, upendo huu sio wa hisia  wala wa kinafiki ni utendaji wa kivitendo unaohusisha kukutana na mahitaji ya wengine, kwa hiyo muda wetu, vipawa vyetu tunawekeza katika kuhakikisha tunawahudumia watu kwa huruma na upendo

 

Mathayo 9:35-38 “Naye Yesu alikuwa akizunguka katika miji yote na vijiji, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri habari njema ya ufalme, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. Na alipowaona makutano, aliwahurumia, kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasio na mchungaji. Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache. Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake.”

                               

Umuhimu wa kuwa na uzoefu katika huduma

Ni muhimu kufahamu kuwa nyakati za kanisa la kwanza walipotaka kuchagua mtu katika huduma mojawapo ya msingi waliouzingatia ulikuwa ni uzoefu katika huduma, jambo hili lilikubalika na jamii yote ya wanafunzi, kumtumikia Mungu na kutumikia watu linahesabiwa kama jambo la furaha katika Kristo na sio mzigo kwa sababu iliaminika kama njia ya kujiweka karibu na Mungu huku ukitimiza kazi hii njema ya kiungu

Matendo 1:21-26 “Basi katika watu waliofuatana nasi wakati wote Bwana Yesu alipokuwa akiingia na kutoka kwetu, kuanza tangu ubatizo wa Yohana, hata siku ile alipochukuliwa kwetu kwenda juu, inapasa mmoja wao awe shahidi wa kufufuka kwake pamoja nasi. Wakaweka wawili, Yusufu, aitwaye Barsaba, aliyekuwa na jina la pili Yusto, na Mathiya. Kisha wakaomba, wakasema, Wewe, Bwana, ujuaye mioyo ya watu wote, tuonyeshe ni nani uliyemchagua katika hawa wawili, ashike mahali katika huduma hii na utume huu, alioukosa Yuda, aende zake mahali pake mwenyewe. Wakawapigia kura; kura ikamwangukia Mathiya; naye akahesabiwa kuwa pamoja na mitume kumi na mmoja.”

Tunapozungumzia uzoefu hapa tunamaanisha mtu aliyekaa katika mafundisho ya Bwana Yesu kwa muda wa kutosha au aliyepitia shule zote muhimu zinazohusiana na utumishi huu tulioitiwa, kwa maana nyingine hapaswi kuwa mtu aliyeokoka hivi karibuni au aliyepandishwa kwa haraka haraka, kanisa la sasa lina watu wengi walioibuka kama uyoga, mtu alikuwa mganga wa kienyeji, mchawi, sheikh hata hajakaa sawa tayari kesho unasikia ni mhudumu

1Timotheo 3:6-7 “Wala asiwe mtu aliyeongoka karibu, asije akajivuna akaanguka katika hukumu ya Ibilisi. Tena imempasa kushuhudiwa mema na watu walio nje; ili asianguke katika lawama na mtego wa Ibilisi.”

Kanisa linalotaka uamsho mzito  na wa kudumu halina budi kwenda na msingi huu, ambapo neno la Mungu linaonya kuwa hatupaswi kumchagua mtu katika huduma ambaye bado ni mchanga, kumpaisha mtu kwa haraka kunaweza kutuletea madhara makubwa kutokana na kuwa mtu huyo anaweza asiwe na uzoefu wa ukomavu wa kiroho, kwa hiyo kumuinua mtu kwa haraka kunaweza kumletea kiburi na majivuno na anguko la haraka pia kama Shetani alivyoanguka kwa majivuno, kwa hiyo mwanafunzi anayeandaliwa kuwa mhudumu wa injili anapawa kuwa mtu mzima kiroho mtu aliyepitishwa na Mungu katika shule mbalimbali na sio kwa sababu ya kipawa chake  kuepusha hatari ya kuwa na majivuno kwa hiyo asiwe mtu mchanga au aliyeinuka haraka “Novice”  kwa Kiyunani “neophutos” maana yake kwa kingereza ni “Newly planted” yaani pandikizi jipya mtu ambaye hana ukomavu katika imani, kwa hiyo anaweza kuwa ameokoka hivi karibuni, au akawa mtu ambaye amedumaa kiroho, ndio maana siku hizi unaweza kuona mtu ni Askofu lakini ana bifu na mtu fulani, anabagua ana mtu ana uadui naye, ana uchungu, na ugomvi na kupoozesha kabisa sifa zinazomuonyesha kuwa ni mwanafunzi wa Yesu, makanisa mengi yamepoteza mwelekeo pale yalipowababaikia watu kwa sababu walikuwa Masheihk, au Wasomi, au wenye vyeo vikubwa na bila kupitia michakato kadhaa ya kiimani wakapaishwa kuwa viongozi wa kanisa na hii imechangia kuilifanya kanisa kupoa na kuwa na watu wenye kutumia akili zao zaidi kuliko hata kumsikiliza Mungu Roho Mtakatifu japo tunahitaji uwiano.

Onyo la kutokuweka viongozi wachanga katika kanisa linatolewa katika misingi mikuu minne ya tahadhari:-

  1. Kuanguka katika mtego wa ibilisi kuwa na kiburi
  2. Kuitia aibu kanisa kutokana na kukosa ukomavu na mizizi ya kiimani
  3. Kukosekana kwa msimamo katika mafundisho na kushindwa kuisimamia imani au kuitetea
  4. Kwamba bado anahitaji ukomavu katika wokovu,mafundisho na tabia, ukomavu wa hekima na busara

 

Matendo 6:3-4 “Basi ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili; na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno.”

Ukomavu wa kiroho ni mchakato unachukua muda, wokovu ni mara moja lakini kujengeka kiroho ni safari inayohitaji mchakato wa muda mpaka mtu akue afikie hatua ya kuweza kula chakula kigumu, wakati mtoto mchanga kiroho anahitaji maziwa na huduma ya kichungaji, mtoto mdogo anahitaji malezi na sio kubebeshwa mzigo, kuwabebesha watoto wachanga kiroho mzigo wa uongozi ni kutafuta kuwadhuru na kuwaharibu na pia kuliharibu kanisa, unaweza kuwafanya wawe na kiburi na majivuno, unaweza kusababisha imani yao ikaharibika, unaweza kuwafanya wakakata tamaa,angalau mtu awe amedumu katika Imani na mafundisho kwa muda usiopungua miaka mitatu kama alikuwa mwaminifu kuhuduhria ibada na mafundisho ya kanisa letu, anaijua imani yetu na anauwezo wa kuitetea.

Waebrania 5:14 “Lakini chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa kupambanua mema na mabaya.”

1Wakorintho 3:1-2 “Lakini, ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama na watu wenye tabia ya rohoni, bali kama na watu wenye tabia ya mwilini, kama na watoto wachanga katika Kristo. Naliwanywesha maziwa sikuwalisha chakula; kwa kuwa mlikuwa hamjakiweza. Naam, hata sasa hamkiwezi,”

1Timotheo 3:8-10 “Vivyo hivyo mashemasi na wawe wastahivu; si wenye kauli mbili, si watu wa kutumia mvinyo sana, si watu wanaotamani fedha ya aibu. Wakiishika siri ya imani katika dhamiri safi.Hawa pia na wajaribiwe kwanza; baadaye waitende kazi ya shemasi, wakiisha kuonekana kuwa hawana hatia.”

Mambo yatupasayo kufanya kama wahudumu katika kanisa.

Kila mwanafunzi wa shule ya huduma anapaswa kufahamu kuwa ameitwa kuutumikia mwili wa Kristo huu ni utu mishi mwema sana na wa hali ya juu na kama kila mmoja atakuwa mwaminifu Mungu atampa thawabu, kwa hiyo huduma hii iko kwaajili ya kufaidiana yaani kuujenga mwili wa Kristo na sio kushindana na uongozi, bali kusaidia.

1Wakorintho 12:4-7 “Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule. Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule. Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote. Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana.”

Neno kufaidiana katika maandiko ya kiyunani linatumika neno “Sumpherōambalo kwa kiingereza linatumika neno “Contribute” sawa na kuchangia kwa faida kama vile Paulo alivyosema mahali Fulani mmoja alipanda mwingine akatia maji bali mwenye kukuza ni Mungu, Mungu ametupa huduma na akili na vipawa mbalimbali ili viweze kuchangia katika kuujenga mwili wa Kristo ambao kimsingi hauwezi kujengwa na mtu mmoja kwa sababu hiyo tuhudumiane kwa Upendo.

Wagalatia 5:13 “Maana ninyi, ndugu, mliitwa mpate uhuru; lakini uhuru wenu usiwe sababu ya kuufuata mwili, bali tumikianeni kwa upendo.”

Kila mwanafunzi wa shule ya huduma anapaswa kufahamu kuwa ameitwa kwaajili ya kuwatia nguvu wengine, kufarijiana, kujengana na kunoana, kumbuka kuwa chuma hunoa chuma!

1Wathesalonike 5:9-11. “Kwa kuwa Mungu hakutuweka kwa hasira yake, bali tupate wokovu, kwa Bwana wetu Yesu Kristo; ambaye alikufa kwa ajili yetu, ili tuishi pamoja naye, kwamba twakesha au kwamba twalala. Basi, farijianeni na kujengana kila mtu na mwenzake, vile vile kama mnavyofanya.”

Kila mwanafunzi wa shule ya huduma anapaswa kufahamu kuwa anapaswa kusaidia huduma ya kichungaji, karama za huduma tulizo nazo ni huduma za masaidiano kwa hiyo katika kanisa tunawasaidia viongozi wetu katika kubeba maono, kulinda umoja na kusaidia kazi za kichungaji        

Warumi 12:4-8 “Kwa kuwa kama vile katika mwili mmoja tuna viungo vingi, wala viungo vyote havitendi kazi moja; Vivyo hivyo na sisi tulio wengi tu mwili mmoja katika Kristo, na viungo, kila mmoja kwa mwenzake. Basi kwa kuwa tuna karama zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema mliyopewa; ikiwa unabii, tutoe unabii kwa kadiri ya imani; ikiwa huduma, tuwemo katika huduma yetu; mwenye kufundisha, katika kufundisha kwake; mwenye kuonya, katika kuonya kwake; mwenye kukirimu, kwa moyo mweupe; mwenye kusimamia kwa bidii mwenye kurehemu, kwa furaha.”

 

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote.

 

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Hakuna maoni: