Jumanne, 14 Julai 2026

Nafsi yangu kwa nini kuinama?


Zaburi 42:5-6 “Nafsi yangu, kwa nini kuinama, Na kufadhaika ndani yangu? Umtumaini Mungu; Kwa maana nitakuja kumsifu, Aliye afya ya uso wangu, Na Mungu wangu. Nafsi yangu imeinama ndani yangu, kwa hiyo nitakukumbuka, Toka nchi ya Yordani, na Mahermoni, na toka kilima cha Mizari.”



Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa ziko nyakati katika maisha ya mwanadamu na hata watu wa Mungu ambapo tunapitia vipindi ambavyo nasfi zetu zinainama kwa sababu ya kuzidiwa na maumivu ya  kihisia na kiroho, kunakosababishwa na huzuni, kukata tamaa, kukosa utulivu, kuwa na mashaka kusongwa na mawazo, hofu, kutokujitosheleza. Misiba na kuwa mbali na nyumbani au kuwa  ugenini au uhamishoni, Watakatifu waliotutangulia wanaonyesha kuwa nao pia katika nyakati tofauti tofauti walipitia hali hizi za kuzidiwa na mgandamizo wa mawazo, kukosa tumaini, kuhisi kama Mungu yuko mbali nao na kuelemewa na changamoto za maisha na upweke na hivyo kusababisha nafsi zao kuinama. Kutokana na hali hizo wakati mwingine waliziuliza nafsi zao maswali makali kwanini nafsi yangu unainama ilihali Mungu yupo? Kwa nini kufadhaika? Wakati Mungu ni tumaini lako?  Ona;-

Zaburi 43:3-5 “Niletewe nuru yako na kweli yako ziniongoze, Zinifikishe kwenye mlima wako mtakatifu na hata maskani yako. Hivyo nitakwenda madhabahuni kwa Mungu, kwa Mungu aliye furaha yangu na shangwe yangu; Nitakusifu kwa kinubi, Ee MUNGU, Mungu wangu. Nafsi yangu, kwa nini kuinama, Na kufadhaika ndani yangu? Umtumaini Mungu; Kwa maana nitakuja kumsifu, Aliye afya ya uso wangu, Na Mungu wangu.”

Nafsi zetu zinaweza kuinama sio kwa sababu ya changamoto za maisha pekee lakini pia wakati mwingine ile hali ya maumivu ya kihisia, kiu ya kuhitaji uwepo wa Mungu, ukavu wa kiroho na ile tamaa ya kutaka uwepo wa Mungu uwe ndani yetu kwa wingi ili tuweze kuzishinda changamoto za nje kwa hiyo tunajifunza hapo kuwa tunaweza kuzihubiri nafsi zetu kuzikemea, kusema nazo na kuzitaka nafsi zetu zisivunjike moyo wala zisifadhaike na badala yake zimtegemee Mungu. tutajifunza somo hili Nafsi yangu kwa nini kuinama kwa kuzingatia vipengele vitatu muhimu vifuatavyo:-

·         Maana ya nafsi kuinama.

·         Sababu zinazopelekea nafsi zetu kuinama.

·         Nafsi yangu kwa nini kuinama?


Maana ya nafsi kuinama

Zaburi 42:5-6 “Nafsi yangu, kwa nini kuinama, Na kufadhaika ndani yangu? Umtumaini Mungu; Kwa maana nitakuja kumsifu, Aliye afya ya uso wangu, Na Mungu wangu. Nafsi yangu imeinama ndani yangu, kwa hiyo nitakukumbuka, Toka nchi ya Yordani, na Mahermoni, na toka kilima cha Mizari.”

Ni muhimu kufahamu kuwa neno nafsi iliyoinama katika lugha ya Kiebrania inasomeka kama “Shachach Nephesh” misamiati ambayo kwa Kiingereza inasomeka kama “downcast soul”, “discouraged soul”, “Depressed within me” au “overwhelmed soul” maana zake kwa Kiswahili ni nasfi iliyovunjika, nafsi iliyokata tamaa, au nafsi iliyolemewa na mawazo, nafsi iliyopoteza tumaini au nafsi iliyozidiwa na kuelemewa au nafsi inayopoteza nguvu na ujasiri, nasfi ya mtu ikiinama ni ukweli ulio wazi kuwa nguvu zote zinaisha na unapoteza kiu na shauku ya kufanya lolote, mtu mwenye nasfi iliyoinama anakuwa na changamoto ya kihisia kimwili na kiroho na wakati mwingine inachangiwa na kutoweka au kupotea kwa matarajio, kutokujibiwa maombi, mambo kutokuenda sawa na kuwa na hisia kana kwamba Mungu yuko mbali, upweke wa kiroho, na kadhalika, kwa ujumla mwandishi anaonyesha kuwa nafsi yake  imeinama kwa sababu ya kuwa mbali na uwepo wa Mungu, Yeye anaonekana kuwa mbali na nyumbani, na tena mbali na Nyumba ya Mungu iliyokuwako Yerusalem, Yeye yu katika chanzo cha mto Jordani katikati ya mlima Hermoni, mahali paitwapo Mizari mbali na Hekalu la Mungu wa Israel au ukuta ule wa kulia machozi mahali pa ibada.

Sababu zinazopelekea nafsi zetu kuinama.

Kiu na hisia za kuwa mbali na Mungu – Mwanadamu mwenye akili timamu anayempenda Mungu anapokuwa na hisia za kuwa mbali na Mungu au kukosa utoshelevu wa kiibada kwa kweli anakosa amani na kuhisi kupungukiwa, Mwandishi wa Zaburi hii nyakati za agano la kale  alikuwa mbali na nyumba ya Bwana alikuwa katika sehemu ya chanzo cha mto Jordani mahali unapoishia mlima Hermoni kaskazini mwa nchi ya Israel na kuanzia kilele cha Mizari,  akiwa huko safarini mbali na nyumba ya Mungu anahisi upweke na anaona kama Mungu amemuacha, nasfi yake inaumia, mambo hayaendi na ni kama maombi yanaonekana kutokujibiwa na anakata tamaa nafsi yake inainama kwa sababu ana kiu na hisia ya kuwa mbali na Mungu  kuna namna anakosa muunganiko na Mungu wake

Zaburi 42:8-11 “Mchana Bwana ataagiza fadhili zake, na usiku wimbo wake utakuwa nami, Naam, maombi kwa Mungu aliye uhai wangu. Nitamwambia Mungu, mwamba wangu, Kwa nini umenisahau? Kwa nini ninakwenda nikihuzunika, adui wakinionea? Watesi wangu hunitukana mithili ya kuniponda mifupa yangu, Pindi wanaponiambia mchana kutwa,Yuko wapi Mungu wako? Nafsi yangu, kwa nini kuinama, Na kufadhaika ndani yangu? Umtumaini Mungu; Kwa maana nitakuja kumsifu, Aliye afya ya uso wangu, Na Mungu wangu.”

Mazingira magumu ya maisha – Mwandishi akiwa mbali na nyumba ya Mungu iliyokuwako Yerusalem anazungukwa na changamoto za maisha na mazingira magumu, anaomba kwa kulia machozi, lakini ni kama hajibiwi, huku akishutumiwa na kuhojiwa yuko wapi Mungu wake, anaonewa, anatukanwa maumivu yanaingia mpaka kwenye mifupa yake, nafsi yake inajikuta inainama, Tunapozungukwa na shida za kifamilia, ugumu wa maisha, magonjwa na kukosa mahitaji muhimu na kila aina ya fadhaa haya yote yanaweza kuisababisha nafsi ya mwanadamu kuinama.

Zaburi 42:3-5 “Machozi yangu yamekuwa chakula changu mchana na usiku, Pindi wanaponiambia mchana kutwa, Yuko wapi Mungu wako. Nayakumbuka hayo nikiweka wazi nafsi yangu ndani yangu, Jinsi nilivyokuwa nikienda na mkutano, Na kuwaongoza nyumbani kwa Mungu, Kwa sauti ya furaha na kusifu, mkutano wa sikukuu. Nafsi yangu, kwa nini kuinama, Na kufadhaika ndani yangu? Umtumaini Mungu; Kwa maana nitakuja kumsifu, Aliye afya ya uso wangu, Na Mungu wangu.”

Shinikizo kutoka kwa watu – tunaishi katika dunia ambayo wakati mwingine watu wanaweza kukuchukia bila sababu, wanasema maneno mabaya dhidi yako au wanakuzushia, au unakuwa wimbo kwenye vinywa vyao, unakataliwa, unadharauliwa, unasemwa na kusengenywa kila mahali, maneno ya watu yanakuvunja moyo unasikia jinsi wanavyokushutumu na kukusimanga na kukusema vibaya inasababisha shinikizo la maisha na kumvunja vunja mtu wa ndani na nasfi inainama

Zaburi 42:10-11 “Watesi wangu hunitukana mithili ya kuniponda mifupa yangu, Pindi wanaponiambia mchana kutwa, Yuko wapi Mungu wako? Nafsi yangu, kwa nini kuinama, Na kufadhaika ndani yangu? Umtumaini Mungu; Kwa maana nitakuja kumsifu, Aliye afya ya uso wangu, Na Mungu wangu.”

Kukumbuka nyakati nzuri zilizopita – Kuna nyakati ambapo tunakumbuka nyakati nzuri tulizokuwa nazo, nyakati za furaha na vicheko, nyakati za amani na furaha ya moyo, nyakati  huru, Mwandishi ni kama anakumbuka nyakati hizo, alikuwa anaenda Hekaluni tena akiwa kiongozi wa ibada ulikuwa ni wakati wa furaha lakini sasa wakati huo anaukosa, unaweza kukumbuka nyakati ambazo ulikuwa uko vizuri, ukilinganisha na hali ya sasa, mambo yako yalikuwa mazuri, ujana wako ulikuwa bomba na ni kama nyakati hizo zimepita haraka unakosa yale uliyokuwa ukiyatamani  na nafsi yako inainama

Zaburi 42:4-5 “Nayakumbuka hayo nikiweka wazi nafsi yangu ndani yangu, Jinsi nilivyokuwa nikienda na mkutano, Na kuwaongoza nyumbani kwa Mungu, Kwa sauti ya furaha na kusifu, mkutano wa sikukuu. Nafsi yangu, kwa nini kuinama, Na kufadhaika ndani yangu? Umtumaini Mungu; Kwa maana nitakuja kumsifu, Aliye afya ya uso wangu, Na Mungu wangu.”

Hali ya uchovu wa kiroho – Ziko nyakati ambapo kimsingi mambo yanapokuwa hayaendi uko mpweke unachoka sana unachoka kuomba, unachoka kusubiri na unaweza kuchoka hata kupigana vita nafsi inashuka na unamuhitaji Mungu, nafsi inakosa nguvu na ni mpaka Bwana akutegemeze na kukuinua kutoka hapo ulipoinama ndipo unapoweza kupenya  mwandishi alikuwa anapitia hali  hii.

Zaburi 145:13-14 “Ufalme wako ni ufalme wa zamani zote, Na mamlaka yako ni ya vizazi vyote. Bwana huwategemeza wote waangukao, Huwainua wote walioinama chini.”

Nafsi yangu kwa nini kuinama?

Mwandishi wa zaburi hii hakubaliani na hali anayoipitia na badala yake anaihoji nafsi yake kwanini kuinama? Kwanini upate shida, kwanini uteseke? Kwanini ufadhaike, yeye anaamini ya kuwa atamsifu Mungu aliye afya ya uso wake, yaani uso wake hautakuja kukunjamana kamwe, yeye ataendelea kufurahia uzuri wa Bwana kwani anaziona njia za huzuni kuwa ni swala la Muda tu  na anajua ya kuwa, Mungu huwa hakai kimya wakati nafsi zetu zinapoinama, yeye kama baba anayejali huwahurumia wamchao na kuwaokoa, Neno la Mungu linaonyesha wazi kuwa Mungu hutoa faraja ya kipekee pale watu wake wanapochoka na kuelemewa kwa hivyo badala ya kufikiri kuwa uko peke yako Neno la Mungu linaonyesha kuwa yeye atajitokeza na kutoa msaada hivyo lazima uikumbushe nafsi yako wajibu wake kwa Bwana na neno la Mungu linasema nini kukuhusu au kuihusu ili usiiname unapoikumbusha nafsi yako kuendelea kumtegema Bwana haitokuja itokee ukazimia kupitiliza:-

1.       Anaalika wote waliochoka wanaolemewa wamjie na kuwa atawapa pumziko na raha nafsini mwao. - Mathayo 11:28-30 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”

 

2.       Mungu huwapa nguvu wale waliochoka wale wanaomtumaini kama ilivyokuwa kwa mwandishi wa Zaburi hii - Isaya 40:29-31 “Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo. Hata vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana wataanguka; bali wao wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia.”

 

3.       Tunaweza kumuomba Mungu atutie nguvu pale nafsi zetu zinapochoka na kuelemewa - Zaburi 119:25-28 “Nafsi yangu imeambatana na mavumbi, Unihuishe sawasawa na neno lako. Nalizisimulia njia zangu ukanijibu, Unifundishe amri zako. Unifahamishe njia ya mausia yako, Nami nitayatafakari maajabu yako. Nafsi yangu imeyeyuka kwa uzito, Unitie nguvu sawasawa na neno lako.”

 

4.       Iambie nafsi yako imsubiri Bwana kwa kimya maana yeye hatakuangusha - Zaburi 62:1-6 “Nafsi yangu yamngoja Mungu peke yake kwa kimya, Wokovu wangu hutoka kwake. Yeye tu ndiye mwamba wangu na wokovu wangu, Ngome yangu, sitatikisika sana. Hata lini mtamshambulia mtu, Mpate kumwua ninyi nyote pamoja? Kama ukuta unaoinama, Kama kitalu kilicho tayari kuanguka,Hufanya shauri kumwangusha tu katika cheo chake; Huufurahia uongo. Kwa kinywa chao hubariki; Kwa moyo wao hulaani. Nafsi yangu, umngoje Mungu peke yake kwa kimya. Tumaini langu hutoka kwake. Yeye tu ndiye mwamba wangu na wokovu wangu, Ngome yangu, sitatikisika sana.”

 

5.       Iamuru nasfi yako kumuhimidi Bwana na kutokusahau fadhili zake - Zaburi 103:1-5 “Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana. Naam, vyote vilivyo ndani yangu Vilihimidi jina lake takatifu. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana, Wala usizisahau fadhili zake zote. Akusamehe maovu yako yote, Akuponya magonjwa yako yote, Aukomboa uhai wako na kaburi, Akutia taji ya fadhili na rehema, Aushibisha mema uzee wako, Ujana wako ukarejezwa kama tai;”

Ikumbushe nafsi yako kuwa haitakiwi kubaki chini hata kama kuna changamoto za aina gani zinakukabili, Mungu yuko kwa hiyo kama nafsi yako inaweza kuinama yuko Mungu mwenye uwezo wa kuiinua, kama nafsi yako inaweza kulia yuko Mungu anayeweza kuifanya ikaimba sifa, kama nafsi yako inaweza kukata tamaa yuko Mungu mwamba wa wokovu wako anaweza kuleta tumanini, kama nafsi yako inaweza kusumbuka na kuelemewa yuko Mungu anayeweza kuleta furaha na kuipa raha nafsi yako, Neno la Mungu linakutaka umtumainie Bwana na kumsifu hata wakati wa changamoto kali za maisha inuka acha kuketi chini tunaye Mungu aliye karibu wala hajakuacha yeye ni kimbilio na nguvu na msaada uonekanao tele wakati wa mateso hivyo hupaswi kuogopa lolote, hata nchi itetemeke, hata milima itikisike, hata moyo wa bahari uumuke yuko Mungu ambaye ukimtegemea na kumtumaini Moyo wako hauwezi kufadhaika kamwe yeye hatakuangusha  kamwe hatakuacha wala hatakupungukia, usikate tamaa, usione kuwa mazingira ni magumu, Mungu yuko kila mahali sio Yerusalem peke yake uwepo wa Mungu uko hata mapangoni, hata ukimbizini atakushika, utainuka.

“Mungu yuko hapa, Yesu Kristo  naye yuko hapa, Roho wake Mungu  yuko hapa na malaika wako hapa,x2 kwa nini mimi niteseke  na hali wewe uko hapa, usiniache uniguse mana Mungu yuko hapa, kwanini mimi nipate tabu, nidharauliwe na kutupwa hovyo usiniache uniguse, maana Mungu yuko hapa” 

Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Hakuna maoni: