Alhamisi, 6 Oktoba 2016

Nabii Hagai



HAGGAI: MTIA MOYO WA UJENZI WA HEKALU

A.      Mwandishi
-          Hagai ni moja ya vitabu vitatu vya kinabii vya Agano la Kale vilivyoandikwa baada ya uhamisho ambavyo ni Hagai, Zekaria na Malaki.
-          Hagai anatajwa kwa jina mara mbili katika kitabu cha Ezra (Ezr 5:1,6:14) kama “mjumbe wa Bwana” (1: 13). Inawezekana alikuwa mmoja wa wale waliorudi kutoka uhamishoni waliorudi Yerusalemu, walioweza kulikumbuka hekalu la Solomoni lilivyokuwa kabla halijaharibiwa na majeshi ya Nebukadneza mwaka 586 K.K. (2:3). Hagai na Zekaria ndio waliowatia moyo wale watu waliorudi kutoka uhamishoni kujenga upya hekalu.
-          Ilikuwa ni mnamo mwaka 538 K.K., miaka kumi na minane ilikuwa imepita tangu Dario alipopitisha amri kuwaruhusu Wayahudi kurudi Yerusalemu kutoka uhamishoni. Watu walikuwa bado wanashughulika kujenga nyumba zao, hivyo ujenzi wa hekalu la Mungu ulikuwa bado haujakamilika.
-          Kundi la kwanza la Wayahudi lililorudi Yerusalemu liliweka msingi wa hekalu jipya.mnamo mwaka 536 K.K.wakiwa na furaha na matumaini makubwa (Ezr 3:8-10).
-          Hata hivyo Wasamaria na majirani wengine walipinga ujenzi huo kwa nguvu nyingi na kuwakatisha tamaa wafanya kazi hata ikafanya ujenzi huo usimame mwaka 534 K.K..
-          Watu waliacha ujenzi wa hekalu, wakageukia ujenzi wa nyumba zao wenyewe. Ujumbe wa Hagai ulikuwa kwamba ni wakati wa kujenga nyumba ya Mungu. Hagai akiwa amefuatana na Zekaria (taz.utangulizi wa kitabu cha Zekaria), yeye alianza kumhimiza Zerubabeli na watu wote kuanza tena kujenga nyumba ya BWANA. Chini ya uongozi wa Zerubabeli mtawala na Yoshua kuhani mkuu na kule kuhimiza kwa Nabii Hagai hekalu lilijengwa mnamo 520 K.K. Miaka minane baadaye hekalu lilimalizika kujengwa na kuwekwa wakfu (ling.Ezr 4-6). 

B.      Kiini cha ujumbe wa Haggai

-         Hagai aliwaambia watu kwamba utukufu wa hekalu walilokuwa wanajenga ungekuwa mkubwa kuliko ule wa hekalu lililotangulia, ingawaje halingekuwa imara kama la kwanza. Hili hekalu lingekuwa bora zaidi kwa sababu Mungu angelijaza utukufu Wake ndani yake.

-          Kuwahimiza watu kujenga upya hekalu la BWANA na kuwahamasiaha kuyatengeneza maisha yao upya na Mungu ili waweze kupata baraka Zake.

C.      Historia ya nyuma ya mambo
-          Hekalu la Yerusalemu lilibomolewa mnamo mwaka 586 K.K. Mwaka wa 538 K.K,
-          Mfalme Koreshi wa Uajemi alitoa amri Wayahudi warudi ili kujenga upya mji wa Yerusalemu na hekalu.Mwaka 536 K.K.walianza kujenga hekalu lakini ilikuwa vigumu kumalizia kutokana na upinzani waliokutana nao kutoka kwa Wasamaria na mataifa ya jirani.
-          Kupitia huduma ya Hagai Zekaria na Yoshua, mwaka 520 K.K., walianza kujenga tena hekalu.Miaka minane baadaye kazi hiyo ya ujenzi wa hekalu ilimalizika.

                           

Mabaki ya ikulu ya Mfalme Dario Mmedi /Mmuajemi ni katika utawala wake ndipo Nabii Haggai aliandika kitabu chake cha kuhamasisha ujenzi wa Nyumba ya bwana makazi haya ya iliyokuwa ikulu yako mahali paitwapo Persepolis Nyakati za Leo Picha na maelezo kwa hisani ya Maktaba ya mwalimu Innocent KamoteMchungaji.

D.      Tarehe  ya uandishi
-          Tarehe ya kuandikwa kwa kitabu kwa hiki ni ya uhakika, yaani, mwaka wa pili wa Mfalme Dario wa Uajemi (mwaka 520 K.K. (1:1).
-          Mpangilio wa kihistoria ni wa muhimu sana ili kuuelewa ujumbe wa kitabu hiki. Mnamo mwaka 538 K.K., Mfalme Koreshi wa Uajemi alitoa amri ikiwaruhusu Wayahudi waaliokuwa uhamishoni kurudi nchini mwao ili kuujenga upya Yerusalemu na hekalu katika kutimiza unabii wa Isaya na wa Yeremia (Isa45:1,3; Yer 25:11-12; 29:10-14) na maombezi ya Danieli (Dan 9). 

E.       Wahusika Wakuu 

-          Hagai, Zerubabel, Yoshua.

F.       Mgawanyo
-          Wito wa kujenga hekalu. (1:1-15)
-          Matumaini ya hekalu jipya. (2:1-9)
-          Baraka zilizoahidiwa. (2:10-19)
-          Ushindi wa mwisho wa Mungu. (2:20-23)

Nabii Habbakuki


A.      Mwandishi wa Kitabu cha Habakuki
 
-          Aliyeandika kitabu hiki anajitambulisha kama Nabii Habakuk i(1:1 ; 3: 1). Hakuna maelezo mengine ya ziada kuhusu maisha ya binafsi au ya familia ya huyu mwandishi yaliyopo po pote katika Maandiko. Alikuwa nabii wa Yuda na inajulikana kutokana na zaburi yake (sura ya tatu) na kwenye maelekezo kwa mkuu wa waimbaji (3:19) kwamba alikuwa wa kabila la Lawi, mmoja wa waimbaji wa hekaluni. Habakuki maana yake Kumbatia
-          .Kitabu cha Habakuki kimeandikwa kwa mtindo wa mazungumzo kati ya Mungu na Nabii.
-          Habakuki aliona kwamba viongozi wa Yuda walikuwa wanawaonea maskini, kwa hiyo aliuliza swali kwamba ni kwa nini Mungu anawaruhusu watu hawa waovu kustawi.
-          Mungu alipomwambia kwamba Wakaldayo wangekuja kuwaadhibu Yuda, Habakuki aliumia zaidi. Hakuelewa ni kwa jinsi gani Mungu angeweza kuwatumia Wakaldayo ambao walikuwa waovu kuliko Wayahudi waovu, ili kutekeleza hukumu dhidi ya watu walikuwa watu waliochaguliwa na Mungu. Jibu la Mungu lilikuwa kwamba wenye haki wangeishi kwa imani kwa Mungu na kwamba walikuwa na uhakika kwamba Mungu alikuwa anafanya lililo sahihi. Mungu alimwambia Habakuki kwamba punde si punde Wakaldayo wangehukumiwa na kwamba hatimaye haki ingeshinda kwa ajili ya watu wa Mungu. Habakuki anamalizia kitabu kwa zaburi ya sifa. 

B.      Kiini Cha kitabu cha Habakuki.
-          Mungu anavyotumia waovu kuadhibu watu wake wanapotenda uovu kwa nia ya kuwarudisha ili wamrudie, lakini hao waovu wakiisha kutimiza kusudi la Mungu, wao huadhibiwa zaidi.
-          Yuda walitenda dhambi ikiwa ni pamoja na kuabudu sanamu, lakini Mungu anatumia Wakaldayo walio waovu zaidi kuwaadhibu na hatimaye Mungu anawaadhibu Wakaldayo.
-           Ilimshangaza Habakuki kuona waovu wakistawi huku wakiendelea kutenda dhambi nyingi wala Mungu hawaadhibu upesi! Habakuki anaelezea imani yake katika mamlaka ya Mungu na katika uhakika kwamba Mungu ana haki katika njia Zake zote.
-           Ufunuo wa Mungu kwa wenye haki na nia Yake ya kuiangamiza Babeli iliyokuwa ovu iliamsha wimbo wa sifa wa kinabii na ahadi kuhusuwokovu katika Sayuni (3:1-19)
C.      Kusudi
-          Kuonyesha kwamba bado Mungu anaitawala dunia hata kama tunaona kwamba uovu unashamiri na ya kwamba iko siku Mungu atauhukumu na kuadhibu huo uovu hatimye kuuangamiza kabisa usiwepo tena.
D.      Wahusika Wakuu
-          Habakuki, Wababeli.
E.       Tarehe
-          Kitabu hiki hakikuwekewa tarehe, lakini bila shaka kilikuwa kipindi cha Wakaldayo.
-           1.Hekalu bado limesimama (2 :20) na huduma ya uimbaji inafanyika (3 :19),
-          2. Kuinuka kwa Wakaldayo kuwa dola inayotisha miongoni mwa mataifa kunatokea wakati wa kizazi hicho (1 :5,6) na kuchinjwa kwa mataifa na Wakaldayo tayari kulishaanza
-          (1 :6,7).Wakaldayo walijulikana na Wayahudi muda mrefu kwa kuyashinda mataifa mengine hadi kuongoza katika dola za ulimwengu wakati wa kuanguka kwa Ninawi 612 K.K. au 606 K.K. na kwa ushindi wao juu ya Wamisri huko Kerkemishi mwaka 605 K.K.
F.       Mgawanyo
-          Swali la Habakuki na jibu la Mungu. (1 :1-11)
-          Swali la pili la Habakuki na jibu la Mungu. (1 :12-2 :20)
-          Maombi ya Habakuki. (3 :1-19) 

                                                           
Hekalu lililokarabatiwa wakati wa Herode na kutumiwa Na Yesu na wanafunzi wake kama linavyoonekana katika Nyumba za mfano za kale hii ilitiza kwa sehemu unabii  utukufu wa mwisho wa nyumba hii utakuwa mkuu kuliko ule wa kwanza kama alivyotia Moyo Nabii Haggai na Zekaria Picha na maelezo kwa hisani ya Mwalimu wa somo Rev.Innocent Kamote Home Bible library 2007

Nabii Nahumu


Nabii wa Kuanguka kwa Ninawi yaani Ashuru (Syria)

 Hali ya Syria leo!


      Mwandishi wa kitabu cha Nahumu 

-          Nahumu maana yake ni mwenye kufariji
-          Hakuna linalofahamika kuhusu wazazi wake au historia yake wala mafunzo yake lakini ukweli unabaki kuwa kwa kuwa ujumbe wake unahusu hukumu  ni wazi kuwa ulitolewa wakati mfupi  kabla ya Uamsho mkubwa uliokuja wakati wa Yosia 627-621
-          Nahumu anajulikana kama Nabii wa kisasi au Nabii wa kuanguka kwa Ninawi  kinakisiwa kuwa kiliandikwa 621 K.K. katika mwaka wa 18  wa Yosia mfalme wa Yuda na kabla ya anguko la Ninawi la mwaka 612 K.K
-          Nahumu anajiita mwekloshi 1;1 na Ekloshi yenyewe Haijulikani iko upane gani ila kuna wanaodhani kuwa  ni kijiji kidogo mashariki ya mto Tigrisi sio mbali kutoka Ninawi na wengine wanafikiri kuwa ni kijiji kidogo huko Galilaya karibu na Kapernaumu jina Kapernaumu maana yake ni kijiji cha Nahumu
B.       Kiini cha kitabu
-          Kiini cha ujumbe wa kitabu hiki ni anguko la Ninawi katika Septuagint kitabu hiki kimewekwa mara tu baada ya kitabu cha Yona  ikifikiriwa kuwa ni ukamilisho wa kitabu cha Yona
C.      Historia ya nyuma ya mambo
-          Ninawi ulikuwa ni mji mkuu wa waashuru
-          Kwa karne nyingi waashuru waliwaonea sana watu wa mashariki ya kati na kumuka ukatili waliokuwa nao katika kitabu cha Yona na angalia Isaya 37
-          Lakini kwa huruma zake Mungu alimtumia Yona Ninawi na watu walitubu na kuokolewa hata hivyo baada ya Muda watu walirudi katika njia zao za uovu vilevile
D.      Mistari ya msingi
-          1;3    - Bwana si mwepesi wa hasira lakini ana nguvu
-          2;13 – Niko kinyume nawe asema Bwana
-          1;7 – Bwana ni mwema kimbilio wakati wa Taabu
-          1;15 – Angalia huko milimani miguu yake yeye aletaye habari njema
E.       Uchanganuzi
-          Hasira ya Bwana 1;1-8 Kuna Maneno sita ya nguvu katika Nahumu  yanayoelezea hisia za Mungu  na majibu yake kwa waninawi Wivu, Kisasi, Hasira, Ukali, Ghadhabu, Kumwagwa  Nahumu 1;6. Ingawa nahumu amesema wazi kuwa mungu ni mwingi wa huruma 1;7 na hivyo rehema zake na upendo wake humfanya asihukumu kwa haraka dhidi yao wamtendao mabaya  lakini wakati unakuja ambapo hulazimika kuadhibu maovu
-          Hasira ya Mungu ni Tofauti na ya wanadamu ya wanadamu huchanganyika chuki kwa waliomuuzi na mwanadamu hawezi kujizuia katika hasira yake  yenye ubinafsi, Hasira ya mungu  haina haraka wala ubinafsi, au isiyozuilika kama ya wanadamu 1;3, haki yake na kisasi chake kiko katika kanini ya kupenda na kuvuna wanadamu na mataifa yote yatavuna kile walichokipanda.
-          Wivu wa mungu ni wa haki unasukumwa na upendo wake kwa watu  na unakusudia kuwalinda kutoka kwao wanapojaribu kuwapeleka watu wake mbali na yeye na furaha aliyoikusudia kwao kumbuka alivyomwambia “Sauli Mbaona waniudhi”
-          Kabla ya hasira za mungu milima ilitetemeka  na vilima viliyeyuka na nchi ilitetemeka 1;6
F.       Upekee wa kitabu cha Nahumu na ujumbe wake
-          Nahumu ndiye Nabii pekee anayeuita ujumbe wake kitabu 1;1
-          Nahumu kama Yona na Obadia wanashughulika na  mataifa adui  waliozionea Israel na Yuda
-          Yona aliwahubiri waninawi huko ninawi lakini Nahumu aliizungumzia Ninawi kwa Yuda hivyo ujumbe wake ulikuwa ni faraja kwa Yuda juu ya ukombozi toka kwa adui zao na watesi wao na hakuna mashitaka kuhusu yuda wala wito wa toba
-          Nahumu kinasisitiza Anguko la Ninawi na kinakazia juu ya Hasira takatifu ya Mungu dhidi ya dhambi
-          Kumbuka kuwa ujumbe wa Ninawi kwa Yuda haukutokana na chuki binafsi za Nahumu kwa adui zao Lakini mungu alimpa ili kuthibitisha agano lake dhidi ya Yuda na kuwakumbusha kuwa Mungu atawapigania dhidi ya adui zao Kumbukumbu 28;1,7.
G.      Mgawanyo
-          1  Anguko la Ninawi linatangazwa sura ya 11;1-15
-          2 Anguko la Ninawi lina changanuliwa sura ya 2;1-13
-          3 Anguko la ninawi  linathibitishwa Sura ya 3;1-19