Jumapili, 16 Oktoba 2016

“Kama utakuwa mtumwa wa watu hawa leo, watakuwa watumwa wako siku zote”


“If today you will be a servant to these People, they will always be your servants” 

Lengo: kufanya maamuzi yenye Busara.

Andiko: 1Wafalme 12:1-15 “1. Rehoboamu akaenda Shekemu; maana Israeli wote walikuwa wamekwenda Shekemu, ili kumfanya mfalme. 2. Ikawa Yeroboamu mwana wa Nebati alipopata habari (maana alikuwa akaliko Misri, huko alikokimbilia awe mbali na mfalme Sulemani; Yeroboamu akakaa huko Misri, 3. wakapeleka watu kwenda kumwita); basi Yeroboamu na jamii yote ya Israeli wakaenda, wakamwambia Rehoboamu, wakasema, 4. Baba yako alilifanya zito kongwa letu; basi sasa utupunguzie utumwa mzito tuliotumikishwa na baba yako, na lile kongwa zito alilotutwika, nasi tutakutumikia. 5. Akawaambia, Enendeni zenu hata siku ya tatu, kisha mnirudie tena. Watu wakaenda zao. 6. Mfalme Rehoboamu akataka shauri kwa wazee waliokuwa wakisimama mbele ya Sulemani, baba yake, alipokuwa hai, akasema, Mwanipa shauri gani ili niwajibu watu hawa? 7. Wakamwambia wakasema, Ukikubali kuwa mtumishi wa watu hawa leo, na kuwatumikia, na kuwajibu, na kuwapa maneno mazuri, basi watakuwa watumishi wako daima.   8. Lakini akaliacha shauri lile la wazee, walilompa, akataka shauri kwa wale vijana waliokua pamoja naye, na kusimama mbele yake. 9. Akawaambia, Mwanipa shauri gani ili tuwajibu watu hawa, waliosema nami, wakinena Utufanyie jepesi kongwa lile alilotutwika baba yako? 10. Na wale vijana waliokua pamoja naye wakamwambia, wakasema, Uwaambie hivi watu wale waliokuambia, wakisema, Baba yako alilifanya zito kongwa letu, bali wewe utufanyie jepesi, uwaambie hivi, Kidole changu cha mwisho ni kinene kuliko kiuno cha baba yangu. 11. Basi kama vile baba yangu alivyowatwika kongwa zito, mimi nitaongeza kongwa lenu; baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, bali mimi nitawapigeni kwa nge. 12. Basi, Yeroboamu na watu wote wakamfikia Rehoboamu siku ya tatu, kama mfalme alivyoamuru, akisema, Mnirudie siku ya tatu. 13. Mfalme akawajibu watu wale kwa ukali, akaliacha shauri lile wazee walilompa; 14. akawajibu kama vile walivyomshauri vijana, akasema, Baba yangu alilifanya zito kongwa lenu, bali mimi nitaongeza kongwa lenu; baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, bali mimi nitawapigeni kwa nge. 15. Basi mfalme hakuwasikia wale watu; maana jambo hili lilitoka kwa Bwana, ili alitimize neno lake, Bwana alilomwambia Yeroboamu mwana wa Nebati kwa kinywa cha Ahiya Mshiloni.



Utangulizi.

Somo letu leo linahusu tukio hili kubwa kabisa la kusikitisha ambalo lilitokea mapema sana mara baada ya utawala wa Rehoboamu mwana wa Sulemani kuingia Madarakani!
Jina Rehoboamu maana yake “Mwenye kuwaongeza watu” Lakini hata hivyo maisha yake yalijawa na wingi wa majanga yenye kuhuzunisha na kusikitisha sana, na Moja ya janga kubwa ni kugawanyika kwa Ufalme wa Israel na kujitenga kutoka kabila la Yuda, jambo hili linatupelekea leo kuchukua Muda mfupi ili kujifunza mengi kutoka kwa Rehoboamu.

Katika kujifunza somo hili tutaangalia mambo muhimu yafuatayo:-

1.       Ushauri kutoka kwa wazee 1Falme 12:6-7
2.       Ushauri kutoka kwa vijana 1Falme 12:8-11
3.       Muitikio wa watu baada ya Uamuzi 1Falme 12:13-14a, 16

Ushauri kutoka kwa wazee IFalme 12:6-7

Inaonekana mfalme Rehoboamu alisikiliza ombi la watu, na jamii kubwa ya watu waliomshauri katika kundi la Kwanza walikuwa ni wazee, hawa walikuwa ni Makuhani, makamanda, washauri na magavana, hawa walikuwa ni watu wenye ujuzi na ufahamu kuhusu utaratibu wa Israel na tamaduni zake. Lakini pia walifahamu athari za utawala wa kifalme hasa wakati wa Sulemani na jinsi utawala wake ulivyoacha athari mbaya kwa raia wake.

Wazee hawa walichokifanya kwa Rehoboamu ilikuwa ni kuweka wazi udhaifu wa Mfalme aliyetangulia, Ufalme wa Sulemani ambaye aliitwa mwenye hekima kubwa kuliko watu wote Duniani katika nyakati zile, ulikuwa umeacha athari kubwa na makovu makubwa sana kwa watu wake na hata kwa Mungu pia, Sulemani alikosa muda wa kushughulika hata na familia yake, alikuwa akishughulika na mambo ya watu wengine Wimbo uliobora 1:5-6, Sulemani katika utawala wake alijishughulisha kushauri wafalme wa maytaifa mengine, alijishughulisha kujenga utukufu wake na sifa zake, aliiigeuza jamii yote kuwa watumwa wake, alisahau hata kumuweka Mungu mbele, alioa wanawake wengi ambao waliingiza ibada za miungu katika Israel, Mahitaji ya Sulemani yalikuwa makubwa sana kiasi ambacho aliongeza kodi kwa raia wake na kila mmoja alijihisi kuwa ni mtumwa, watu walikaa kimya, waliojaribu kumpinga walitaka kuuawa na hivyo walikimbia uhamishoni, Mungu alikwisha kukusudia mapema kuwa atausambaratisha utawala wa Sulemani na kuugawa na atabakiza kabila moja tu kwaajili ya Daudi mtumishi wake, Mungu alikwishakuupima moyo wa Sulemani nakuona kuwa ameshindwa kuiendea njia ya Daudi baba yake.

Wazee waliona nafasi ya magezi ilikuwa moja tu, ni Mara alipotawazwa Rehoboamu kuwa mfalme, hapo ndipo walipojua kuwa watapata Nafuu hivyo walimsihi mfalme.

1.       Utupunguzie utumwa mzito tuliotumikishwa na baba yako
2.       Kubali kuwa mtumwa wa watu hawa ( hapa wazee walikuwa wanamaanisha Unyenyekevu,Utu, Huruma na kujali)
3.       Wape maneno mazuri (Jibu watu vizuri, jali watu ona watu kuwa wathamani, kuwa mwema kwao na wakati mwingine wasikilize na kuwajibu watu vizuri) “Mithali 15:1-4
4.       Watu watakutumikia daima, walikuwa tayari kumtumikia mfalme anayejali
Rehoboamu alifanya maamuzi ya busara, alitulia na alitoa siku tatu kuwa atatoa jibu ni maamuzi gani atafanya.

Ushauri kutoka kwa vijana 1Falme 12:8-11.

Hata hivyo ilikuweko nafasi nyingine, hii ilikuwa ni kuwasikiliza vijana wanasema nini? Na hata hivyo hakuweza kuukubali ushauri wa wazee mapema kwani aliona hawezi kuwa mnyenyekevu na kuwatumikia watu wanaostahili kutawaliwa tu majibu ya Rehoboamu yalikuwa ya Ujeuri zaidi
1.       “Kidole changu cha mwisho ni kinene kuliko kiuno cha baba yangu” “loins – sex organ
Haya yalikuwa ni majivuno na kiburi cha hali ya juu, Rehoboamu alitaka kuonyesha kuwa ana nguvu kuliko aliyemtangulia, utawala wake ni superior kuliko ule wa Sulemani yeye ni super power
2.       Rehoboamu alishauriwa kuongeza utumwa na kodi na kuifanya nzito zaidi, alisema kama Baba aliwapiga kwa mijeledi mimi nitawapiga kwa nge (Scorpion) hiki ni chombo chenye vipande vya chuma vyenye uwezo wa kukatakata, ujumbe aliokuwa akiutoa hapa ni wazi kuwa nitaongeza machungu yenu hasa kuliko ilivyokuwa kwa Sulemani
3.        Alizungumza na watu kwa ukali sana Mstari 13. Hakuna kubembeleza mtu,Hakuna maneno mazuri wala ya Heshima
4.       Watu wakaasi na kumuacha Rehoboamu.

Muitikio wa watu baada ya Uamuzi 1Falme 12:13-14a, 16

1.       Watu waliona kuwa hawana urithi wowote katika Yuda waliamua kujitenga 15-16
2.       Watu waliamua kuangalia maisha yao wenyewe na nyumba zao wenyewe 16
3.       Watu waliingiwa na roho ya ukatili, walimuuamsimamizi wa utumwa 18
4.       Na Israel waliasi 19. Sio tu waliasi ufalme wa Yuda bali pia walimchukia Mungu wa Israel na katika utawala wao waliona waabudu miungu mingine (watu wakikasirishwa nawe hata Mungu unayemuamini hawatamuamini)
5.       Rehoboamu alitaka kupigana na Ndugu zake Mungu akamkemea 1Wafalme 12:21-24

Hitimisho.

Nini cha kujifunza kutoka katika somo hili.

1.       Kuzaliwa na mwenye Hekima hakukufanyi uwe na Hekima, wengine wameshindwa kupata japo nusu ya akili za Baba zao
2.       Tukiisha kumuacha Mungu na kumdaharu utukufu wake unaondoka
3.       Namna yoyote ile ya kutaka kuwa na nguvu na utukufu bila kutanguliza Mungu na utu utatupa kuishia kwenye wakati mgumu
4.       Bila uongozi wa kiroho au wa Roho wa Mungu hatuwezi kufanya maamuzi ya Busara
5.       Ni lazima tuwe na huruma kwa wanadamu, na kuonyesha kujali ubinadamu kwanza kabla ya mambo mengine
6.       Manabii walikuweko na makuhani, ambao waliweza hata kuepusha vita kati ya ndugu na ndugu, walitakiwa kusikilizwa kwanza
7.       Rehoboamu alilijua wazi kabisa tatizo lakini, alikataa kabisa kulishughulikia na hivyo watu walimuasi na Mungu aliruhusu
8.       Mgawanyiko na udhaifu huu uliwapa nguvu maadui wa Israel kuwamaliza na kupelekwa utumwani
9.       Lazima wakati wote tufanye maamuzi yenye busara na kukataa ushauri mbaya, lakini pia kama wazazi wetu hawakufanya vema tusiiifuate njia yao.

Mkiyajua hayo Heri ninyi mkiyatenda! Yohana 13:17

Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Rev. Innocent Kamote.

Alhamisi, 6 Oktoba 2016

Nabii Malaki



MALACHI: NABII WA SIKU ZA UAMSHO
A.       Mwandishi


-          Malaki aliishi katika nusu ya pili ya karne ya tano Kabla ya Kristo, baada ya ujenzi wa hekalu kumalizika. Malaki ambalo ni neno la Kiebrania ‘‘Malaki’’ kama lilivyo kwenye Kiswahili, maana yake ‘‘Mjumbe wangu.’’. Jina hili ni kifupi cha ‘‘Malakia’’ ambalo maana yake ni ‘‘Mjumbe wa Bwana‘’ (1:1).
-          Jina hili la kitabu limetumika vivyo hivyo kwenye maandiko ya Kiebrania na Kiyunani likionyesha kwamba hili likuwa jina la nabii ambaye ujumbe wake umenukuliwa humu. Hakuna habari nyingine zo zote za kibinafsi zinazofahamika za huyu nabii. Maisha ya kidini ya Wayahudi yalikuwa mabaya :
-           Walikuwa wamekengeuka, wakawa wameoa wanawake wa mataifa mengine, wakaacha kutoa zaka (fungu la kumi) na dhabihu ambayo na sehemu ya Mungu, hata wakawa wamemwacha Mungu, hali ambayo ilifanana sana na ile iliyokuwepo wakati wa Nehemia (444-432 K.K.). 

B.      Kiini cha ujumbe wa kitabu cha Malaki

-          Masikitiko makubwa ya Malaki ni uhusiano kati ya Waisraeli na Mungu haukuwa kama ulivyopaswa uwe. Walimwacha Mungu na kumdharau, wala hawakumheshimu inavyostahili, wakashindwa kufuata yale Mungu aliyowaagiza. Matokeo yake hukumu ikawa inawangoja, lakini watu wanaomcha Mungu wamehakikishiwa kuwa wameandikwa kwenye kitabu cha Mungu, nao watafuhia wokovu wa Mungu milele. 

C.      Kusudi
-          Kuwahimiza watu wafanye mabadiliko thabiti ya kimsingi katika maisha yao, kwa kuwakumbusha upendo wa Mungu (1:1-5) na pia kwamba adhabu yake iko karibu (2:17; 3:13)

D.      Mchanganuo wa kitabu cha malaki

-          Kitabu hiki kinaonyesha kuwa:(1)Hekalu lilijengwa tena (516/515 K.K.), dhabihu na sikukuu zilirudishwa. (2)Ufahamu wa jumla wa sheria ulirudishwa tena na Ezra (kama 457-455 K.K. ; tazama Ezra 7 :10, 14, 25-26) na (3).Kurudi nyuma kimaadili kulikofuatia kulitokea miongoni mwa makuhani na mwa watu pia (kama mwaka 433K.K.). Kutokana na hali hii hali ya kiroho na upuzi Malaki anaouzungumzia kwa karibu vilifanana sana n aile hali aliyoikuta Nehemia aliporudi kutoka uhamishoni Uajemi (kama 433-425 K.K.) ili kuwa mtawala wa Yerusalemu (ling. 13 :4-30).
E.       Mahali
-          Yerusalemu. Malaki, Hagai na Zekaria walikuwa manabii katika Yuda (Ufalme wa kusini) baada ya watu kurudi kutoka uhamishoni.. Hagai na Zakaria waliwakemea watu kwa kutokumalizia ujenzi wa hekalu. Malaki alipambana nao kwa sababu walipuuzia hekalu na kutokumjali Mungu.
F.       Tarehe
-          Yale yaliyomo kwenye kitabu hiki yanaonyesha kwamba huduma ya Malaki ilikuwa kwenye utendaji mnamo sehemu ya pili ya karne ya tano Kabla ya Kristo. Hekalu lilikuwa tayari limeshajengwa tena upya. Kutokana na wakati alioishi Malaki na yale yaliyomo kwenye kitabu hiki, inawezekana kiliandikwa 557- 525 K.K.
G.      Wahusika wakuu
-          Malaki na makuhani
H.       Mgawanyo
-          Upendo wa Mungu kwa Israeli. (1:1-5)
-          Israeli yamtukana Mungu. (1:6-2:16)
-          Hukumu ya Mungu na ahadi yake. (2:17-4:6)

Nabii Zakaria



ZECHARIA: NABII WA MAONO KUHUSU MASIHI;
A.      Mwandishi 
-          Zekaria alianza huduma yake mnamo mwezi wa nane wa mwaka wa pili wa Dario (520 K.K.), miezi miwili baada ya ujumbe wa kwanza wa Hagai. Maana ya jina Zekaria ni “BWANA amekumbuka.”
-          Haijulikani kwa uhakika Zekaria aliendelea kufanya huduma hiyo kwa muda gani.Kwa kadiri ionekanavyo alikuwa kijana (2:4) wakati alipoanza huduma yake.
-           Ido, ambaye ni babu yake (Zek 1:1) alikuwa miongoni mwa wale waliorudi kutoka uhamishoni mwaka 538 K.K.
-          Katika ujumbe wake wa kwanza (1:1-6) Zekaria anawaonya watu ambao ndio kwanza tu walikuwa wameanza kujenga upya hekalu kwamba inawapasa kusikiliza ujumbe wa Mungu kupitia manabii na kudumisha uhusiano wa muhimu na Mungu, wasije wakaharakisha hukumu ya Mungu.
-          Mfululizo wa maono ya usiku (1:7-6:8) yanatia moyo wajenzi ule wakati mgumu katika hatua ya kukata tamaa.
-          Ule utaratibu wa ujenzi ulikuwa umesababisha maafisa wa Kiajemi kufanya uchunguzi na kuandika taarifa ya malalamiko kwa Dario (Ezr 5-6). Huenda Wayahudi walikuwa wakingojea hukumu ya Dario wakati Zekaria akitoa ujumbe wake uliowekewa msingi katika haya maono ya usiku. Mtazamo wa jumla wa mfululizo wa maono haya manane yanawahakikishia wajenzi kwamba Mungu anao mpango wa muda mrefu kwa ajili ya Israeli. Miaka miwili baadaye, (518 K.K.) suala la kutia katika matendo kutii kufunga liliibuka (7:1-8:23). Zekaria kwa mara nyingine anaangaliza watu kwamba njia ya kudumisha uhusiano sahihi na Mungu ni utii. Kule kufunga ili tu kwamba mtu amefunga ni ubatili.Utaratibu wa kushika sheria kamwe hauwezi kutumika kama njia mbadala ya kuonyesha upendo wa Mungu katika maisha ya kila siku. Sehemu ya mwisho ya ujumbe wa Zekaria (9-14) haukuonyeshwa tarehe. Uwezekano mkubwa ni kwamba ulitolewa baadaye, huenda mnamo mwaka 480 K.K. Hapa mkazo uko katika mpango wa maendeleo wa muda mrefu ukionyesha kusimamishwa kwa ufalme wa mwisho. Mfalme anatambulishwa kama anayekuja kwa tabia ya unyenyekevu akileta wokovu lakini akikataliwa na watu wake mwenyewe, yaani, Waisraeli, ambao baadaye wanaachwa kwenye hukumu ya mataifa. Mataifa yatakapokusanyika kwa ajili ya vita dhidi ya Yerusalemu, Waisreli watamtambua Yeye “Yule waliomchoma mkuki” (Zek.12:10) na wataibuka na ushindi. Ndipo mataifa yote yatakuja Yerusalemu kumwabudu Mfalme, Bwana wa Majeshi.

B.      Kiini cha kitabu cha Zekaria
-          Zekaria anaonyesha kwamba Mungu ana mpango wa muda mrefu na Israeli, hivyo anaita mwito wa utii.
-          Anaonyesha jinsi ambavyo watu wanaweza kufanya mambo Si kwa nguvu wala kwa uwezo bali kwa Roho Yangu ”asema.( 4:6)..
-           Kuwapa watu wa Mungu matumaini kwa kuwajulisha watu mpango wa Mungu wa baadaye wa ukombozi kupitia kwa Masihi.
C.      Historia ya Nyuma ya mambo
-          Huu ujumbe wa mwanzoni unafuatiliwa na maono ambayo yaliwatia moyo wajenzi ambao Zekaria aliwatia moyo kwa kuwaambia kwamba Mungu alikuwa na mpango mrefu kwa ajili ya Israeli.
-          Katika sura ya 7 na 8 Zekaria aliwataka watu wamtii Mungu, hii ikiwa ni njia ya kila mtu kumjali na kumhurumia mwenzake. Mungu alitaka utii kwao katika kuhusiana naye.
-          Sura ya 9 mpaka 14 inazungumzia habari za miezi inayokuja, hukumu ya mwisho na kukua kwa muda mrefu kwa ufalme wa mwisho.
D.      Mahali
-          Yerusalemu
E.       Tarehe
-          520-470 K.K.
F.       Wahusika
-          Hagai, Zerubabeli, Yoshua na waliorudi kutoka uhamishoni.

G.      Mgawanyo

-          Wito wa kuwa watiifu. (1:1-6)
-          Maono. (1:7-6:15)
-          Hukumu dhidi ya maadui wa Israeli. (9:1-8)