Jumapili, 3 Mei 2026

Ndoa na iheshimiwe na watu wote!


Waebrania 13:4. “Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu.”




Utangulizi:

Leo tutachukua muda kujifunza kwa kina na mapana na marefu undani wa mafundisho ya Biblia kuhusiana na swala la kuheshimu ndoa, tukio ambalo nyakati za leo, limekuwa likichukuliwa si kwa uzito ule ambao Mungu mwenyewe anautoa katika ndoa, Ndoa za siku hizi zimepoteza heshima kuanzia kwa wanandoa wenyewe na mpaka katika jamii inayozizunguka ndoa kutokana na maarifa katika eneo hili kuwa finyu, Agizo la kuheshimiwa kwa ndoa ni agizo zito linalopewa kipaumbele na Mungu, Neno Iheshimiwe katika lugha ya kiyunani yaani Kigiriki(Koine Greek) linasomeka kama neno “timios” likimaanisha kuwa ndoa ni ya thamani sana, ndoa ni ya heshima kubwa sana, ndoa haipaswi kutiwa unajisi, ndoa inatakiwa kuchukuliwa kwa uzito na kwa utukufu wa Mungu, ndoa haipaswi kuchukuliwa kwa wepesi, kwa hiyo hii ina naana ya kuwa Ndoa sio swala la kuchukuliwa kawaida, bali ni swala la kiadilifu na ni takatifu kwa sababu ndoa ilianzishwa na Mungu mwenyewe kama yanenavyo maandiko:-

Mwanzo 2:18-24 “BWANA Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye. BWANA Mungu akafanyiza kutoka katika ardhi kila mnyama wa msituni, na kila ndege wa angani, akamletea Adamu ili aone atawaitaje; kila kiumbe hai, jina alilokiita Adamu likawa ndilo jina lake. Adamu akawapa majina yao kila mnyama wa kufugwa, na ndege wa angani, na kila mnyama wa mwituni; lakini hakuonekana wa kumsaidia Adamu aliyefanana naye. BWANA Mungu akamletea Adamu usingizi mzito, naye akalala; kisha akatwaa ubavu wake mmoja, akafunika nyama mahali pake, na ule ubavu alioutwaa katika Adamu BWANA Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu. Adamu akasema, Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume. Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.”

Kwa msingi huo swala la kuiheshimu ndoa ni agizo la Mungu kwa watu wote waliomo katika ndoa wenyewe na wale ambao bado hawajaingia katika ndoa, na wanajamii wote wanapaswa kuiheshimu, kuithamini na kuepuka kwa namna yoyote ile kuiharibu na kuipotosha ndoa, Kimsingi Mungu anaonya jamii iache kuichezea ndoa, kuidharau na hata kuiharibu, kwa sababu zozote zile yakiwemo majungu, uchochezi na ushawishi mbaya na usiofaa, au kuitia unajisi. Tutajifunza somo hili Ndoa na iheshimiwe na watu wote kwa kuzingatia vipengele vikuu muhimu vitatu vifatavyo:-


·         Maana ya kuheshimiwa kwa ndoa.

·         Kwa nini kuna ulazima na umuhimu wa kuheshimu ndoa.

·         Ndoa na iheshimiwe na watu wote.


Maana ya kuheshimiwa kwa ndoa.

Ili tuweze kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu agizo la kibiblia kuhusiana na andiko Ndoa na iheshimiwe na watu wote na malazi yawe safi ni muhimu kwetu tukaangalia andiko hili kwanza kutoka katika lugha yake ya asili ya Kiyunani yaani Kigiriki kisha tulifanyie uchambuzi yakinifu, ili tupate maana na msisitizo ulio wazi kutoka kwenye maandiko hayo. Andiko hili linaweza kuwa na tafasiri hii katika lugha ya Kiswahili, Kiyunani na Kiingereza maandiko yanasomeka kama ifuatavyo:-

Kiswahili: Waebrania 13:4. “Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu.”

Kiyunani: (Timios ho gamos en pasin, kai hē koitē amiantos; pornous gar kai monoecious krinei ho Theos)

Kiingereza: (Hebrews 13:4 Marriage should be honoured by all and the marriage bed kept pure, for God will judge the adulterer and all the sexually immoral) NIV.

Neno ho gamous – Neno hilo maana yake ni Ndoa ni Muungano halali unaojumuisha mwanamke na mwanaume unaokubalika na kubarikiwa na Mungu, kwa hiyo Biblia haitambui ndoa za jinsia zinazofanana, kwa hiyo kuheshimu ndoa ni pamoja na kuheshimu jinsia husika, na kuunganisha wana ndoa wenye jinsia zinafananazo au waliobadili jinsia katika maisha yao baada ya kuzaliwa ni kufuru! na ni kuivunjia ndoa heshima yake katika ngazi ya juu sana

Neno hē koitē – Neno hili ambalo maana yake limetajwa kama kitanda cha ndoa au marriage bed Kiyunani linamaanisha tendo la ndoa, yaani tendo halali ambalo limehalalishwa kwa wana ndoa, kwa hiyo usafi unaotajwa hapo sio wa kitanda na Godoro, bali Mwandishi anazungumzia uadilifu wa tendo la ndoa katika agano halali la ndoa, kwa hiyo kuingilia ndoa ya mtu na kuitia unajisi ni kosa kubwa linalomuuzunisha Mungu, na sio hivyo tu kutoka nje ya ndoa nalo ni kosa kubwa kwa Mungu

Mwanzo 39:7-9 “Ikawa baada ya mambo hayo, mke wa bwana wake akamtamani Yusufu, akamwambia, Lala nami. Lakini akakataa, akamwambia mke wa bwana wake, Tazama, bwana wangu hajui kitu kilichowekwa kwangu nyumbani, na vyote alivyo navyo amevitia mkononi mwangu. Hakuna mkuu katika nyumba hii kuliko mimi, wala hakunizuilia kitu cho chote ila wewe, kwa kuwa wewe u mkewe. Nifanyeje ubaya huu mkubwa nikamkose Mungu?

Ayubu 31:9-12 “Kama moyo wangu ulishawishwa kwa mwanamke, Nami nimeotea mlangoni pa jirani yangu; Ndipo hapo mke wangu na asage kwa mwingine, Na wengine na wainame juu yake. Kwani hilo lingekuwa kosa kuu; Naam, lingekuwa ni uovu wa kuadhibiwa na waamuzi; Kwa kuwa ni moto uteketezao hata Uharibifu, Nao ungeyang'oa maongeo yangu yote.”  

Neno amiantos – maana yake isiyo na doa, isiyotiwa unajisi, isiyochafuliwa, au isiyosababisha madhara kwa tafasiri ya moja kwa moja ni safi yaani isiyochafuliwa kwa dhambi kwa msingi huo tafasiri ya moja kwa moja ya mstari huu wa msingi maana yake ni kwamba ndoa haipaswi kuwa iliyochafuliwa amiantos kwa kiingereza  “undefiled”, “pure” or “unpolluted” au “harmless”. Isitiwe unajisi wala wewe usijitie unajisi kwa kuingia katika ndoa ya mtu, yaani unaichafua na wewe unachafuka

Walawi 19:20 “Nawe usimkaribie mwanamke kufunua utupu wake wakati wa kutengwa kwa ajili ya unajisi wake. Usilale na mke wa mwenzio, ukajitia unajisi naye.”

Neno monoeciousmaana yake ni tendo la ndoa linalofanyika nje ya agano la ndoa uzinzi, au kuchanganya mbegu za uzazi baina ya wanandoa, kuingizia mtoto asiye halali, katika ndoa ya mtu mwingine, au kuchanganya viungo vya uzazi vya aina mbili katika kiungo kimoja, kuchangia mke, Katika mimea tendo hili linaitwa “hermaphrodite”,ambalo linatafasiriwa hivi kwa kiingereza Hermaphrodite which means male and female reproductive organs in the same individual msichangine mke au mume,

Neno Porneia – Lina maana tendo la ndoa linalofanyika kabla ya agano la ndoa au kwa kuhusisha tamaa au kumtumia mwenzi wako vibaya uchafu au uasherati.  

“Kwa hiyo Muungano halali wa ndoa uheshimiwe na watu wote na tendo la ndoa kati ya wanandoa lisiwe linalotiwa unajisi kwa sababu wazinzi na waasharati Mungu atawahukumia adhabu”

Kwa msingi huo Mstari huu wa msingi na unaojitegemea unahimiza wana ndoa kujitunza kwa uaminifu katika ndoa, wao wenyewe wakiwa mstari wa mbele kuheshimu makubaliano yote ya ndoa yaani lile agano na kuepuka kwa sababu zozote zile za kuleteana uchafu wa kingono, picha chafu za ngono, tamaa mbaya na udanganyifu, huku wanandoa wakionywa kutokuutumia mwili wa mwenzi wako vibaya au kumtumia vibaya, kuishi kwa kuheshimiana, kutokuzaliana watoto haramu, kusikilizana, kujaliana, kupendana na kuwa na nia moja kiroho, kuepuka kufanya au kusababisha tendo la ndoa lifanyike nje ya mapenzi na makusudi ya Mungu au nje ya agano, huku wana jamii wakiagizwa kuheshimu sana ndoa takatifu, na kutokuiingilia ndoa ya mtu mwingine au kuwa sababu ya ndoa takatifu kuvunjika, kuichukulia ndoa kwa heshima kubwa na kutokuvunja viwango vya uadilifu katika ndoa, kutokuingilia na kuharibu, kuingilia na kuvuruga, kuwachafua wana ndoa na kuwaletea fitina ama sababu zozote zile zitakazopelekea kuachana kwao, hiyana wivu, uchonganishi majungu na maneno ya kuwakatisha tamaa au kuwashauri vibaya.

Kwa nini kuna ulazima na umuhimu wa kuheshimu ndoa.

Ndoa ni lazima iheshimiwe kwa sababu imeanzishwa na Mungu mwenyewe kama agano la kudumu ambalo linatupa picha ya uhusiano wa Kristo na Kanisa, Ndoa ndio msingi wa Familia jamii na taifa lolote lile, Kamwe hakuwezi kuwa na jamii duniani bila kuweko kwa ndoa, Katika ndoa ndiko Mungu anakotarajia watoto wakue katika Imani nidhamu na ustaarabu, huwezi kuwa na jamii bora kama hakuna ndoa zilizo bora, kama jamii haiheshimu ndoa tutajipatia jamii zilizo hovyo sana duniani.

Katika nyakati hizi za sasa kwa mujibu wa tafiti za karibuni imebainika kuwa heshima kwa ndoa imeshuka kwa kiwango kikubwa kwa asilimia sitini na nne 64% kwa tafiti za kati ya mwaka 1970 mpaka 2024 watu wengi sana katika nyakati za leo hawajiheshimu wala hawaheshimu ndoa, kuanzia kwa wananandoa wenyewe na kwa jamii nzima, bila kujali umri, heshima au cheo, hofu kuhusu mke wa mtu au mume wa mtu katika jamii imeshuka na jambo hili liko mpaka katika makanisa ya Mungu, wanandoa wa siku hizi wanagombania kwenye mitandao ya kijamii, wazee wa zamani wakati mwingine waliweza kuhitilafiana na hata kuachana na jamii isijue siku hizi kuachana ni matangazo, ni fahari na imefikia hatua hata sasa zimekuwepo sherehe za kuadhimisha talaka, mlipendana wenyewe huko sirini mkaona wenyewe huko mitandaoni mnaenda kuanikana na kupata maoni ya watu wapuuzi wa dunia hii ili iweje? 

Ni kwa nini Jamii inapaswa kuheshimu ndoa kama agizo la kibiblia linavyosema hapa ziko sababu kadhaa

1.       Ndoa ni mpango wa Mungu -  Wazo la ndoa kamwe sio la kibinadamu, Ni Mungu ndiye aliyeanzisha ndoa na Ndoa inaonekana mwanzo kabisa wa uumbaji wa Mungu,  katika agano la kale huu ulikuwa ni mpango halali na kamili wa Mungu katika kuanzisha jamii yenye uadilifu kuelekea kwake kwa hiyo halikuwa wazo la Mwanadamu

Mathayo 19:4-6 “Akajibu, akawaambia, Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke, akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja? Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe.”

Kwa maelezo hayo ya Bwana wetu Yesu Kristo na hitimisho lake Alichokiunganisha Mungu mwanadamu asikitenganishe maana yake Mungu anapowakutanisha watu na wakafanikiwa kuoana hawana sababu wala hakuna sababu zinazokubalika kwa wao kuachana mpaka Mungu mwenyewe atakapoamua kumchukua mmoja nyumbani, maana yake ni kuwa Ndoa imeanzishwa na Mungu na inatoka kwa Mungu  na hakuna mwanadamu aliye na kibali cha kuimaliza au kuiachanisha, hili linatakiwa kufahamika hivyo kwa wanandoa wenyewe na wana jamii, unapoingilia mke wa mtu au mume wa mtu maana yake wewe utakuwa na adhabu kubwa sana kwa Mungu na laana kwa sababu unataka kuwa sababu ya watu kutengana, au unaweza kusababisha watu kuachana,kufarakana, Yesu anatufundisha hapa kuwa hata talaka sio mpango wa Mungu iwe watu hao waliooana wameokoka au hawajaokoka Mungu anatambua muungano huo na ameufanya.

2.       Ndoa ni eneo la kukua kiroho na kiadilifu – Mungu ameikusudia ndoa kutokuwa swala la uhusiano pekee bali eneo la ukuaji wa kiroho na maadil na uvumilivui, Ndoa ni njia ya kukua na kumfikia Mungu kwa hiyo mojawapo ya sehemu ya ukuaji wa kiroho na kimaadili ni pamoja na kujenga uhusiano wa karibu kati ya wanandoa na hivyo kusababisha ukaribu na Mungu, ndoa zenye msingi imara wa kiroho na uadilifu zinatengeneza jamii yenye uadilifu na uhusiano mzuri na Mungu, Adam na Hawa walipokosea katika maswala ya kiroho na uadilifu uzao wote wa mwanamke ulipata changamoto zinazoathiri jamii mpaka leo.

Mwanzo 3:1-6 “Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwitu aliowafanya BWANA Mungu. Akamwambia mwanamke, Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani? Mwanamke akamwambia nyoka, Matunda ya miti ya bustanini twaweza kula; lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu amesema, Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa. Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya. Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala.”

3.       Ndoa imewekwa kwa kusudi la kuzuia zinaa – Mojawapo ya sababu za kibiblia ya kuwapo kwa ndoa ni kwaajili ya kuzuia zinaa, na Paulo mtume analizungungumzia hili kwa uwazi kwamba ndoa imewekwa kwaajili ya kuzuia uzinzi na uchafu kwa sababu hiyo sababu zozote zile zinazopelekea uchafu ufanyike na zinaa ifanyike Mungu atahukumu, na ndio maana wana ndoa wanapaswa kuhakikisha amani inakuwepo, na shetani hapati nafasi ya kuharibu ndoa, katika namna ya kushanganza sana nyakati za leo hata pamoja na maandiko kuonya wanandoa wamekuwa wakikomoana kwa kunyimana na kutokuridhishana na kupelekea shetani kupata nafasi ya kuharibu ndoa hii ni namna nyingine pia ya kutokuheshimu ndoa.

 

1Wakoritho 7:2-5 “Lakini kwa sababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe. Mume na ampe mkewe haki yake, na vivyo hivyo mke na ampe mumewe haki yake. Mke hana amri juu ya mwili wake, bali mumewe; vivyo hivyo mume hana amri juu ya mwili wake, bali mkewe. Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu.”

 

4.        Ndoa ndio eneo la kwanza la mahusiano na upendo -   Mungu alikusudia ndoa iwe eneo la kwanza la mahusiano na upendo, Mwanadamu ni kiumbe cha kijamii, moja ya changamoto iliyoonekana kabla ya anguko la mwanadamu ilikuwa sio vema mtu huyu awe peke yake kwa hiyo Mungu alitaka awepo mtu mwenye kumfaa Adamu na kutoa huduma ya ushirika na kuanzisha jamii, Uhusiano huu wa ndoa unaruhusu wanandoa kukua katika uhusiano na upendo na imani kwa pamoja kuingilia ndoa ya watu ni kuharibu mpango huu wa upendo wa Mungu na ustawi wa ndoa hizo na kuleta vurugu katika jamii, ndoa iheshimiwe, kuingilia mahusiano ya wengine ni wizi, unaingia kuiba upendo usiokuwa wako, jenga wako acha kuharibu wa wengine, heshimu wako wacha kuharibu wa watu wengine  

Mwanzo 2:18. “BWANA Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye.”

Waefeso 5:22-33 “Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili. Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo. Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno; apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa. Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe. Maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake po pote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa. Kwa kuwa tu viungo vya mwili wake. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja. Siri hiyo ni kubwa; ila mimi nanena habari ya Kristo na Kanisa. Lakini kila mtu ampende mke wake kama nafsi yake mwenyewe; wala mke asikose kumstahi mumewe.”

5.       Ndoa ni agano takatifu – Ndoa sio tu ushirika wa kawaida wa kijamii ni agano, Ni agano takatifu linaloapwa au linalomuhusisha Mungu, likiwa limekusudiwa kuwa agano la kudumu na lisilovunjika, kuharibu ndoa kwa sababu zozote zile ikiwepo swala la zinaa na uasherati au talaka, linamleta Mungu katika kuingilia na kuhukumu kwa sababu ya kupuuziwa kwa agano lake, Agano ambalo Mungu ni shahidi

Malaki 2:13-16 “Tena mnatenda haya nayo; mnaifunikiza madhabahu ya Bwana kwa machozi, kwa kulia na kwa kuugua, hata asiiangalie tena hiyo dhabihu, wala kuitakabali mikononi mwenu na kuiridhia. Lakini ninyi mwasema, Ni kwa sababu gani? Ni kwa sababu Bwana amekuwa shahidi kati ya wewe na mke wa ujana wako, uliyemtenda mambo ya hiana, angawa yeye ni mwenzako, na mke wa agano lako. Hakuna mtu mmoja aliyetenda hivi, ambaye alikuwa na ufahamu kidogo. Au je! Kuna mtu mmoja atafutaye mzao mwenye kumcha Mungu? Kwa hiyo jihadharini roho zenu; mtu awaye yote asimtende mke wa ujana wake mambo ya hiana. Maana mimi nakuchukia kuachana, asema Bwana, Mungu wa Israeli; naye aifunikizaye nguo yake kwa udhalimu namchukia, asema Bwana wa majeshi; basi jihadharini roho zenu, msije mkatenda kwa hiana.”                      

6.       Kwa sababu Mungu atahukumu wasioheshimu ndoa – Neno la Mungu katika msingi wa andiko tunalojifunza katika somo hili limetoa onyo kali kwa kosa lolote lile litakalohusika katika kuharibu ndoa, Mungu anaona na atahukumu kama alivyosema kwa hiyo hata kama jamii itapotoka na ikapuuzia mpango huu wa Mungu, Mungu mwenyewe atahukumu vikali Katika amri zake za uadilifu ziko amri mbili ambazo zimewekwa na Mungu kwa kusudi la kuilinda ndoa ndani ya zile amri kumi za uadilifu. Kutoka 20:14. “Usizini.”

Kutoka 20:17 “Usiitamani nyumba ya jirani yako, usimtamani mke wa jirani yako; wala mtumwa wake, wala mjakazi wake, wala ng'ombe wake, wala punda wake, wala cho chote alicho nacho jirani yako.”

Waebrania 13:4. “Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu.”

Jamii inapaswa kukumbuka kuwa ndoa ni muungano wa Mke na Mume uliowekwa na Mungu, Ndoa ni mali ya wenye ndoa, watu wanapaswa kuiheshimu na kuiogopa ndoa, miaka ya zamani jamii ilikuwa inaogopa sana kusikia mke wa mtu au mume wa mtu anatoka nje ya ndoa yake, miaka ya siku hizi watu wanajionea fahari kutoka nje ya ndoa, upofu wa kijamii umeingia na hawaoni tena uzito wa dhambi ya zinaa, agano la ndoa halijaliwi, hakuna heshima, kwa ndoa nyakati za leo na labda kanisa pia limeacha wajibu wake wa kufundisha na kuonya, Bwana atupe neema kutubu na kukaa katika mstari ulionyooka ambao umekusudiwa na Mungu kwaajili ya ndoa, vijana kwa wazee katika jamii wafundishwe na kuelekezwa kuwa jambo hili litaumiza wengi na kuondoa Baraka za Mungu katika maisha yao endapo watachukulia ndoa kama jambo jepesi na la kawaida na kuzivunjia ndoa heshima.

Ndoa na iheshimiwe na watu wote.

Waebrania 13:4. “Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu.”

Maandiko yanapoagiza swala zima la kuiheshimu ndoa, yanaagiza kuwa ndoa na iheshimiwe na watu wote, neno watu wote katika Biblia ya kiyunani linasomeka kama neno “Pántōn”  ikimaanisha kuwa ndoa na iheshimiwe na watu wote bila kumtenga yeyoye, hii maana yake wanaopaswa kuiheshimu ndoa ni wana jamii wote ambao kimsingi tunaweza kuwaelezea katika makundi kama sita hivi, yaani wanandoa wenyewe, wasio na ndoa, wazazi wa wana ndoa, Jamii kwa ujumla yaani majirani marafiki na watu wote katika jamii wakiwemo viongozi wa mila na desturi, Kanisa na viongozi wa kiroho, na mifumo yote ya Serikali na utawala wa nchi, makundi hayo yote yanajumuishwa katika agizo la kuiheshimu ndoa kila kundi kwa jinsi yake na kwa namna yake kama neno la Mungu linavyoagiza.

1.       Wanandoa wenyewe – Katika agizo la kuiheshimu ndoa kundi la kwanza kabisa linalopaswa kuiheshimu Ndoa ni wana ndoa wenyewe, ni lazima kila mwanadamu mwanamke na mwanamume wanaoingia kwenye ndoa wawe na ufahamu wa kutosha na akili ya kutosha na ujuzi wa kutosha na hekima ya kutosha kuelewa kuhusu ndoa, ndoa ni nini na kwa nini wameacha wazazi wao na kuanza jumuia mpya ndani yake kuna wajibu gani na ni namna gani wanapaswa kuiheshimu sana ndoa, Kabla hujataka watu wengine waiheshimu ndoa yako kwanza wewe mwenyewe uliyeko kwenye ndoa ni lazima uwe unaiheshimu na kujiheshimu, ziko kanuni zinazoiongoza ndoa na kama wana ndoa wenyewe watakuwa wapumbavu na kutokuziheshimu na kujiheshimu ndoa hiyo itashambuliwa na shetani na kuwa na wavamizi

a.       Lazima wanandoa watoshelezane – Moja ya jambo kubwa na la muhimu linalowaunganisha wana ndoa ni tendo lenyewe la ndoa, tendo hili likifanyika kwa ubora na kwa utoshelevu linaleta amani na utulivu na kuleta utoshelevu, tafiti ziko wazi kuwa changamoto zote au nyingi zinazopelekea kuwako kwa migogoro ya ndoa zimebainisha kuwa ni tendo la Ndoa lenyewe kutokufanyika kwa utoshelevu au wanandoa kutokutoshelezana, wana ndoa wengi hawatoshelezani katika tendo la ndoa, na wengi hawana muda hata wa kufanya maandalizi na wala hawafurahii jambo hili linapelekea mmomonyoko wa uadilifu na kushuka kwa heshima ya ndoa, wanawake kwa wanaume wanapaswa kuhakikisha kuwa wanatoshelezana.  

Wimbo uliobora 5:15-19 “Unywe maji ya birika lako mwenyewe, Na maji yenye kububujika katika kisima chako. Je! Chemchemi zako zitawanyike mbali, Na mito ya maji katika njia kuu? Yawe yako mwenyewe peke yako, Wala si ya wageni pamoja nawe. Chemchemi yako ibarikiwe; Nawe umfurahie mke wa ujana wako. Ni ayala apendaye na paa apendezaye; Maziwa yake yakutoshe sikuzote; Na kwa upendo wake ushangilie daima.”

b.      Wananandoa hawapaswi kunyimana – Ndoa inapoteza heshima yake sio tu kwa sababu ya kutokutoshelezana lakini pia kwa sababu ya kunyimana, na changamoto hii katika tafiti za ndoa hujitokeza hasa kwa wanawake na baadae wanaume hujibu mapigo kwa kunyimana ni jambo la kusikitisha na kufedhehesha kuwa hata wanawake waliookoka na kupata mafundisho mara kwa mara bado pia huwa wanampa ibilisi nafasi na kuharibu ndoa zao kwa sababu ya tabia endelevu za kunyimana na kutopeana haki ya ndoa bila sababu za msingi, mioyo ya wanaume wengi sana imeumizwa na matukio ya aina hii ambayo kimsingi ni hujuma iliyo wazi kwa ndoa nadhani ni mwanamke mpumbavu tu ndiye anayeweza kumnyima mumewe kinyume na maandiko na kwa kufanya hivyo huyo anakuwa ndio wa kwanza kulivunja agano. Aidha ni marufuku kwa wanandoa kuuziana tendo la ndoa yaani kulitumia tendo hilo kamammadai kuwa usiponifanyia hiki hutapata hii, jambo hili la kuifanyia ndoa biashara ni kosa kama kosa la kunyimana

1Wakorintho 7:3-5 “Mume na ampe mkewe haki yake, na vivyo hivyo mke na ampe mumewe haki yake. Mke hana amri juu ya mwili wake, bali mumewe; vivyo hivyo mume hana amri juu ya mwili wake, bali mkewe. Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu.”

c.       Wanandoa wenyewe hawapaswi kutendeana mambo ya hiyana – Maandiko yanawaonya wana ndoa kuokutendeana  mambo ya hiyana, kimsingi mambo ya hiyana ni maswala yote ambayo Mungu anachukizwa nayo kwani yanatikisa na kuharibu misingi ya ndoa, na kuharibu uhusiano, kimsingi kama wana ndoa wanaheshimu Ndoa basi hawapaswi kutendeana mambo hayo ambayo nabii Malaki anayatilia mkazo katika agizo la kiungu.

Malaki 2:13-16 “Tena mnatenda haya nayo; mnaifunikiza madhabahu ya Bwana kwa machozi, kwa kulia na kwa kuugua, hata asiiangalie tena hiyo dhabihu, wala kuitakabali mikononi mwenu na kuiridhia. Lakini ninyi mwasema, Ni kwa sababu gani? Ni kwa sababu Bwana amekuwa shahidi kati ya wewe na mke wa ujana wako, uliyemtenda mambo ya hiana, angawa yeye ni mwenzako, na mke wa agano lako. Hakuna mtu mmoja aliyetenda hivi, ambaye alikuwa na ufahamu kidogo. Au je! Kuna mtu mmoja atafutaye mzao mwenye kumcha Mungu? Kwa hiyo jihadharini roho zenu; mtu awaye yote asimtende mke wa ujana wake mambo ya hiana. Maana mimi nakuchukia kuachana, asema Bwana, Mungu wa Israeli; naye aifunikizaye nguo yake kwa udhalimu namchukia, asema Bwana wa majeshi; basi jihadharini roho zenu, msije mkatenda kwa hiana.”

Mambo ya hiyana ambayo tunaweza kuyabainisha ambayo wana ndoa wasioheshimiana huyafanya au huweza kuyafanya na yakazuia maombi yao na ibada zao ni pamoja na kukoseana adabu au heshima, wanandoa wanapaswa kuheshimiana, na kutengeneza mazingira ya kujenga upendo na ushirikiano, lakini wakiwa wanafarakana na kugombana kukoseana heshima jambo hilo linavunja uadilifu wa ndoa na heshima ya ndoa na kuiharibu, sio hivyo tu kila mwanandoa anapaswa kutimiza wajibu wake na majukumu yake, kujali watoto, kujenga familia yenye afya, kujenga Imani thabiti na utii heshima na upendo, wanandoa wanapaswa kuwa mbali kabisa na usaliti, na kuvunja uaminifu, kuwa na mahusiano na wanawake au wanaume wengine kinyume na uadilifu wa ndoa, kupeana talaka, aidha kwa mwanamke kuidai talaka au kwa mwanaume kutoa talaka, Katika nyakati za leo wanawake katika nchi zilizoendelea wameitumia ndoa sio kwa upendo bali kama mtaji ya kwamba akiolewa na mwanaume tajiri ataachana naye baadae ili apate malipo ya kugawana nusu ya mali ya mwanaume ya utajiri wake Mungu alikusudia ndoa ziwe za kudumu na Mungu anachukia kuachana, pia kufunika nguo kwa udhalimu maana yake ni kunyimana tendo la ndoa, au kufanya zinaa na kadhalika haya yote yote pamoja na migogoro, na kukomoana Malaki anayaita mambo ya hiyana kila mmoja katika ndoa ana wajibu wa kuhakikisha kuwa ndoa inaheshimika na inadumu kama Mungu anavyotaka, wote tuna wajibu wa kuzuia mambo yanayoleta migogoro na uharibifu katika ndoa.

d.      Wanandoa wanapaswa kuhakikisha kuwa malazi yanakuwa safi - Neno hē koitē – Neno hili ambalo maana yake limetajwa kama kitanda cha ndoa au marriage bed Kiyunani linamaanisha tendo la ndoa, linapaswa kuwa safi, Usafi unaotajwa hapo ni kutokutiwa unajisi kwa kitanda cha ndoa kwa wana ndoa wenyewe lakini pia inazungumzia usafi wa kawaida na usafi wa tendo lenyewe hii ikiwa na maana ya kuwa lazima tendo la ndoa lifanyike kwa ufasaha, wanandoa wajifunze namna ya kufurahishana kwa kulifanya tendo hili kwa uhodari hii ikiwa ni pamoja na kutumia mitindo tofauti tofauti, “styles” za tendo la ndoa maadamu tu hazihitilafiani na mapenzi ya Mungu, wanandoa wanapaswa kuhakikisha kuwa wanabadilisha mitindo ya kushirikiana tendo hilo, ili kuondoa uchovu na mazoea ya aina moja ya mitindo, wakati mwingine ikibidi hata eneo, wako watu wengine ambao hufikiri kuwa mitindo hii ni dhambi, Lakini Mungu alimuumba mwanadamu na kumpa tendo hili kwa kusudi la kuongezeka na pia kwa kusudi la kufurahia na kuondoa migandamizo ya mawazo ya safari na uchovu wa dunia na kuleta usingizi mzuri Isaka na Rebeka walikuwa na ndoa yenye furaha kwa sababu walikuwa na mitindo tofauti, walikuwa marafiki walikuwa wakicheza pamoja na kutekenyana na kuchezeana michezo ambayo watu walipoona walijua kuwa huyu alikuwa mke na mume  

Mwanzo 26:6-9 “Isaka akakaa katika Gerari. Watu wa mahali hapo wakamwuliza habari za mkewe. Akasema, Ni ndugu yangu huyu maana aliogopa kusema, Ni mke wangu, watu wa nchi wasije wakamwua kwa ajili ya Rebeka; kwa maana alikuwa mzuri wa uso. Ikawa alipokuwa amekaa huko siku nyingi, Abimeleki, mfalme wa Wafilisti, akachungulia dirishani, akamwona Isaka anacheza-cheza na Rebeka mkewe.Abimeleki akamwita Isaka, akasema, Yakini huyu ni mkeo, mbona ulisema, Ni ndugu yangu huyu? Isaka akamwambia, Kwa sababu nalisema, Nisife kwa ajili yake.”

2.       Wasio na Ndoa – Agizo la kuheshimu ndoa pia linawahusu pia wasiokuwa na ndoa hawa nao wameamriwa katika andiko hili la msingi kuithamini na kutokuhusika kuichezea ndoa, Neno la Mungu linawataka wasiooa na wasiolewa kutokutamani mke wa mtu au mume wa mtu, lakini sio hiyo tu wanapaswa kuepuka ngono kabla ya ndoa kwa hiyo hawapaswi kufanya uasherati, tendo la ndoa linapaswa kufanyika ndani ya ndoa halali tu, kulifanya tendo hili kabla ya wakati wake ni dhambi na kunapelekea kutokuwa na heshima katika ndoa, zaidi hawapaswi kuivamia ndoa ya mtu mwingine na hawapaswi kuitumia miili yao kuharibu ndoa, wasiooa au kuolewa wanapaswa kujiepusha na kuufanya uchafu wa aina yoyote ile unaoharibu ndoa hata kama wewe hauko kwenye ndoa waogope wenye ndoa kama tatizo ili usije ukaadhibiwa na Mungu.

Kutoka 20:17 “Usiitamani nyumba ya jirani yako, usimtamani mke wa jirani yako; wala mtumwa wake, wala mjakazi wake, wala ng'ombe wake, wala punda wake, wala cho chote alicho nacho jirani yako.”

Wathesalonike 4:3-4 “Maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu, kutakaswa kwenu, mwepukane na uasherati; kila mmoja wenu ajue kuuweza mwili wake katika utakatifu na heshima;”

3.       Wazazi wa wenye ndoa – Mojawapo ya watu wanaoonywa pia na kuagizwa kuiheshimu ndoa ni pamoja na wazazi, wazazi wengi wasio na ufahamu wameharibu sana ndoa za watoto wao kwa sababu ya tabia ya kuingilia uongozi wa wanandoa na kwa sababu hiyo kuchochea migogoro, au wakati mwingine kwa kushindwa kuwasaidia wana ndoa na kutokuwaambia ukweli au kuamua changamoto zao kwa upendeleo, wanandoa wanapoambiwa kuwa mtu atamuacha baba yake na mama yake maana yake, maana yake wao wanapaswa kuanza serikali yao na hivyo wazazi wanapaswa kuwa walezi na washauri wa mbali na sio wenye kuingilia maamuzi  ya wanandoa na kuendelea kuwafanya wachanga siku zote, wazazi wanaosababisha migongano kwa wana ndoa wanavunja moja kwa moja agizo la ndoa na iheshimiwe na watu wote.

Mwanzo 2:23-24 “Adamu akasema, Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume. Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.”

4.       Jamii kwa ujumla, marafiki, majirani, viongozi wa mila na desturi – Maandiko yapoagiza kuwa ndoa na iheshimiwe na watu wote inawataka wana jamii wote kuheshimu ndoa wakiwemo marafiki, majirani, viongozi wa mila na desturi, wote wanapaswa kuiheshimu ndoa, Viongozi wa kimila ni lazima wasimamie haki na kuondoa mila zote potofu zinazoeneza uzinzi na uasherati kupitia tamaduni za aina mbalimbali, wana jamii wanapaswa kuiheshimu ndoa kwa kutokueneza udaku, habari mbaya na fitina au taariza zinazoweza kuihatarisha ndoa, jamii inapaswa kujiepusha na ushauri mbaya kwa wana ndoa, wanajamii waache maneno maneno na kuwaacha wenye ndoa waishi kwa amani, mtu yeyote anayesambaza habari za kuharibu ndoa ya mtu anafanya dhambi na haiweki ndoa katika vipimo vya Mungu, ziko mila ambazo kundi rika la aina fulani lina uwezo wa kutembea na wake wa wenzake wa rika hilo mila hizo zikomeshwe na hazifai kwani ni kinyume na uadilifu wa ndoa uliowekwa na Mungu, mila zinaweza kuwa bora kama tu hazivunji kanuni na utaratibu uliowekwa na Mungu

Mithali 6:16-19 “Kuna vitu sita anavyovichukia Bwana; Naam, viko saba vilivyo chukizo kwake. Macho ya kiburi, ulimi wa uongo, Na mikono imwagayo damu isiyo na hatia; Moyo uwazao mawazo mabaya; Miguu iliyo myepesi kukimbilia maovu; Shahidi wa uongo asemaye uongo; Naye apandaye mbegu za fitina kati ya ndugu.”

Mithali 12:22-23 “Midomo ya uongo ni chukizo kwa Bwana; Bali watendao uaminifu ndio furaha yake. Mwanadamu mwenye busara husitiri maarifa; Bali moyo wa wapumbavu hutangaza upumbavu

5.       Kanisa na viongozi wa kirohoKanisa na viongozi wa kiroho wanapaswa kukazia na kutokuwa lele mama katika kufundisha uadilifu na uaminifu na utakatifu katika ndoa ni lazima kanisa lisimame katika zamu yake na kuhakikisha ya kuwa maagizo ya Mungu yanafanyiwa kazi katika jamii, na kuwasaidia wana ndoa bila kuziingilia na kuziharibu viongozi wa kanisa ni lazima watumie mamlaka yao vizuri na sio kuharibu ndoa za watu kwani ni makosa kiroho.

Mathayo 19:4-6 “Akajibu, akawaambia, Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke, akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja? Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe.”

6.       Serikali na watawala watunga sheria za nchi – Serikali inawajibika kuziheshimu ndoa kwa kuweka taratibu nzuri na kutunga sheria zenye kuilinda jamii na kuilinda ndoa, kwa kuzuia vitendo vya kimapenzi vyenye kusababisha uhalifu ndani yake mfano uzinzi, ubakaji, ulawiti na matendo ya nguvu au uingiliaji wa kingono wa watoto wadogo na kuzuia matendo ya ukahaba mitaani, serikali lazima ilinde Ndoa kwa sheria, mamlaka inapaswa kuisimamia mema kwa mujibu wa neno la Mungu

Warumi 13:1-4 “Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na ile iliyopo umeamriwa na Mungu. Hivyo amwasiye mwenye mamlaka hushindana na agizo la Mungu; nao washindanao watajipatia hukumu. Kwa maana watawalao hawatishi watu kwa sababu ya matendo mema, bali kwa sababu ya matendo mabaya. Basi, wataka usimwogope mwenye mamlaka? Fanya mema, nawe utapata sifa kwake; kwa kuwa yeye ni mtumishi wa Mungu kwako kwa ajili ya mema. Lakini ufanyapo mabaya, ogopa; kwa maana hauchukui upanga bure; kwa kuwa ni mtumishi wa Mungu, amlipizaye kisasi mtenda mabaya kwa ajili ya ghadhabu.”

Hitimisho:

Neno la Mungu linatoa wito wa kuiheshimu ndoa, wito huu nunaihusua jamii nzima kila mtu anapaswa kutambua kuwa ndoa ni Muungano unaotokana na Mungu  na sio wa kibinadamu, kila mtu anapaswa kuishi kwa uaminifu, usafi, na kuepuka dhambi zinazolichafua agano la ndoa, kuhakikisha kuwa unakuwa mfano wa heshima na upendo wa Kristo na kuhakikisa ya kuwa hugusi mali za watu ili kuepusha laana na kifo katika maisha yako, kila mtu anayegusa ndoa za mtu mwingine anajiweka katika hatari ya hukumu ya Mungu na kifo

Mwanzo 20:1-9 “Ibrahimu akaondoka huko kwenda nchi ya kusini, akakaa kati ya Kadeshi na Shuri, naye akatembea katika Gerari. Ibrahimu akamnena Sara mkewe, Huyu ni ndugu yangu. Basi Abimeleki mfalme wa Gerari akapeleka watu akamtwaa Sara. Lakini Mungu akamjia Abimeleki katika ndoto ya usiku, akamwambia, Umekuwa mfu wewe kwa sababu ya mwanamke huyu uliyemtwaa, maana ni mkewe mtu. Basi Abimeleki alikuwa hakumkaribia, akasema, Ee BWANA, Je! Utaua hata taifa lenye haki? Je! Hakuniambia mwenyewe, Huyu ni ndugu yangu? Na mwanamke mwenyewe naye alisema, Huyu ni ndugu yangu. Kwa ukamilifu wa moyo wangu, na kwa kuwa safi mikono yangu, nimefanya hivi. Mungu akamwambia katika ndoto, Nami nimejua ya kwamba kwa ukamilifu wa moyo wako umefanya hivi, ndipo nami nikakuzuia usinitendee dhambi, kwa hiyo sikukuacha umguse. Basi sasa umrudishe mwanamke kwa mtu huyo, maana yeye ni nabii, naye atakuombea, upate kuishi. Bali usipomrudisha, fahamu ya kwamba kwa hakika utakufa wewe na watu wote ulio nao. Abimeleki akaamka asubuhi na mapema, akawaita watumwa wake wote, akawaambia maneno hayo yote masikioni mwao, nao watu hao wakaogopa sana. Kisha Abimeleki akamwita Ibrahimu, akamwambia, Umetutenda nini? Nimekukosa nini, hata ukaleta juu yangu na juu ya ufalme wangu dhambi kuu? Umenitenda matendo yasiyotendeka.”

Wanandoa wanapaswa kujiepusha kwa namna yoyote ile kujitangaza katika mitandao ya kijamii kama wanaachana, kufanya hivyo kunafungua mlango wa mmomonyoko wa uadilifu, kufungua mlango wa maoni maovu kutoka kwa watu wenye nia mbaya, Kumpa ibilisi nafsi na kupanua wigo wa mashambulizi zaidi, ni jambo la kusikitisha sana kuwa watu waliokuwa wanaishi chumba kimoja na wakati mwingine wana watoto unasikia mitandaoni kuwa wameachana wana simu za mkononi lakini wanajibizania mitandaoni, upumbavu  na ushamba wa namna hii unaweza kufanywa na mabaradhuli tu au watu wasiomjua Mungu, kwa ndoa ya kikristo  na hata isiyo ya kikristo ni muhimu kuweka akiba ya maneno kwani wanandoa wanaweza kurudiana baada ya kuhitilafiana sasa ikiwa mliweka ugomvi wenu na mafarakano yenu mtandaoni ikitokea mnarudiana mtatangaza? Mtataka tena maoni ya jamii nzima yaje kwenye stutus zenu hasa kama ninyi ni wakristo basi tuwe na adabu!

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima.              

Hakuna maoni: