Alhamisi, 6 Oktoba 2016

Nabii Zakaria



ZECHARIA: NABII WA MAONO KUHUSU MASIHI;
A.      Mwandishi 
-          Zekaria alianza huduma yake mnamo mwezi wa nane wa mwaka wa pili wa Dario (520 K.K.), miezi miwili baada ya ujumbe wa kwanza wa Hagai. Maana ya jina Zekaria ni “BWANA amekumbuka.”
-          Haijulikani kwa uhakika Zekaria aliendelea kufanya huduma hiyo kwa muda gani.Kwa kadiri ionekanavyo alikuwa kijana (2:4) wakati alipoanza huduma yake.
-           Ido, ambaye ni babu yake (Zek 1:1) alikuwa miongoni mwa wale waliorudi kutoka uhamishoni mwaka 538 K.K.
-          Katika ujumbe wake wa kwanza (1:1-6) Zekaria anawaonya watu ambao ndio kwanza tu walikuwa wameanza kujenga upya hekalu kwamba inawapasa kusikiliza ujumbe wa Mungu kupitia manabii na kudumisha uhusiano wa muhimu na Mungu, wasije wakaharakisha hukumu ya Mungu.
-          Mfululizo wa maono ya usiku (1:7-6:8) yanatia moyo wajenzi ule wakati mgumu katika hatua ya kukata tamaa.
-          Ule utaratibu wa ujenzi ulikuwa umesababisha maafisa wa Kiajemi kufanya uchunguzi na kuandika taarifa ya malalamiko kwa Dario (Ezr 5-6). Huenda Wayahudi walikuwa wakingojea hukumu ya Dario wakati Zekaria akitoa ujumbe wake uliowekewa msingi katika haya maono ya usiku. Mtazamo wa jumla wa mfululizo wa maono haya manane yanawahakikishia wajenzi kwamba Mungu anao mpango wa muda mrefu kwa ajili ya Israeli. Miaka miwili baadaye, (518 K.K.) suala la kutia katika matendo kutii kufunga liliibuka (7:1-8:23). Zekaria kwa mara nyingine anaangaliza watu kwamba njia ya kudumisha uhusiano sahihi na Mungu ni utii. Kule kufunga ili tu kwamba mtu amefunga ni ubatili.Utaratibu wa kushika sheria kamwe hauwezi kutumika kama njia mbadala ya kuonyesha upendo wa Mungu katika maisha ya kila siku. Sehemu ya mwisho ya ujumbe wa Zekaria (9-14) haukuonyeshwa tarehe. Uwezekano mkubwa ni kwamba ulitolewa baadaye, huenda mnamo mwaka 480 K.K. Hapa mkazo uko katika mpango wa maendeleo wa muda mrefu ukionyesha kusimamishwa kwa ufalme wa mwisho. Mfalme anatambulishwa kama anayekuja kwa tabia ya unyenyekevu akileta wokovu lakini akikataliwa na watu wake mwenyewe, yaani, Waisraeli, ambao baadaye wanaachwa kwenye hukumu ya mataifa. Mataifa yatakapokusanyika kwa ajili ya vita dhidi ya Yerusalemu, Waisreli watamtambua Yeye “Yule waliomchoma mkuki” (Zek.12:10) na wataibuka na ushindi. Ndipo mataifa yote yatakuja Yerusalemu kumwabudu Mfalme, Bwana wa Majeshi.

B.      Kiini cha kitabu cha Zekaria
-          Zekaria anaonyesha kwamba Mungu ana mpango wa muda mrefu na Israeli, hivyo anaita mwito wa utii.
-          Anaonyesha jinsi ambavyo watu wanaweza kufanya mambo Si kwa nguvu wala kwa uwezo bali kwa Roho Yangu ”asema.( 4:6)..
-           Kuwapa watu wa Mungu matumaini kwa kuwajulisha watu mpango wa Mungu wa baadaye wa ukombozi kupitia kwa Masihi.
C.      Historia ya Nyuma ya mambo
-          Huu ujumbe wa mwanzoni unafuatiliwa na maono ambayo yaliwatia moyo wajenzi ambao Zekaria aliwatia moyo kwa kuwaambia kwamba Mungu alikuwa na mpango mrefu kwa ajili ya Israeli.
-          Katika sura ya 7 na 8 Zekaria aliwataka watu wamtii Mungu, hii ikiwa ni njia ya kila mtu kumjali na kumhurumia mwenzake. Mungu alitaka utii kwao katika kuhusiana naye.
-          Sura ya 9 mpaka 14 inazungumzia habari za miezi inayokuja, hukumu ya mwisho na kukua kwa muda mrefu kwa ufalme wa mwisho.
D.      Mahali
-          Yerusalemu
E.       Tarehe
-          520-470 K.K.
F.       Wahusika
-          Hagai, Zerubabeli, Yoshua na waliorudi kutoka uhamishoni.

G.      Mgawanyo

-          Wito wa kuwa watiifu. (1:1-6)
-          Maono. (1:7-6:15)
-          Hukumu dhidi ya maadui wa Israeli. (9:1-8)

Hakuna maoni: