Jumapili, 16 Oktoba 2016

“Kama utakuwa mtumwa wa watu hawa leo, watakuwa watumwa wako siku zote”


“If today you will be a servant to these People, they will always be your servants” 

Lengo: kufanya maamuzi yenye Busara.

Andiko: 1Wafalme 12:1-15 “1. Rehoboamu akaenda Shekemu; maana Israeli wote walikuwa wamekwenda Shekemu, ili kumfanya mfalme. 2. Ikawa Yeroboamu mwana wa Nebati alipopata habari (maana alikuwa akaliko Misri, huko alikokimbilia awe mbali na mfalme Sulemani; Yeroboamu akakaa huko Misri, 3. wakapeleka watu kwenda kumwita); basi Yeroboamu na jamii yote ya Israeli wakaenda, wakamwambia Rehoboamu, wakasema, 4. Baba yako alilifanya zito kongwa letu; basi sasa utupunguzie utumwa mzito tuliotumikishwa na baba yako, na lile kongwa zito alilotutwika, nasi tutakutumikia. 5. Akawaambia, Enendeni zenu hata siku ya tatu, kisha mnirudie tena. Watu wakaenda zao. 6. Mfalme Rehoboamu akataka shauri kwa wazee waliokuwa wakisimama mbele ya Sulemani, baba yake, alipokuwa hai, akasema, Mwanipa shauri gani ili niwajibu watu hawa? 7. Wakamwambia wakasema, Ukikubali kuwa mtumishi wa watu hawa leo, na kuwatumikia, na kuwajibu, na kuwapa maneno mazuri, basi watakuwa watumishi wako daima.   8. Lakini akaliacha shauri lile la wazee, walilompa, akataka shauri kwa wale vijana waliokua pamoja naye, na kusimama mbele yake. 9. Akawaambia, Mwanipa shauri gani ili tuwajibu watu hawa, waliosema nami, wakinena Utufanyie jepesi kongwa lile alilotutwika baba yako? 10. Na wale vijana waliokua pamoja naye wakamwambia, wakasema, Uwaambie hivi watu wale waliokuambia, wakisema, Baba yako alilifanya zito kongwa letu, bali wewe utufanyie jepesi, uwaambie hivi, Kidole changu cha mwisho ni kinene kuliko kiuno cha baba yangu. 11. Basi kama vile baba yangu alivyowatwika kongwa zito, mimi nitaongeza kongwa lenu; baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, bali mimi nitawapigeni kwa nge. 12. Basi, Yeroboamu na watu wote wakamfikia Rehoboamu siku ya tatu, kama mfalme alivyoamuru, akisema, Mnirudie siku ya tatu. 13. Mfalme akawajibu watu wale kwa ukali, akaliacha shauri lile wazee walilompa; 14. akawajibu kama vile walivyomshauri vijana, akasema, Baba yangu alilifanya zito kongwa lenu, bali mimi nitaongeza kongwa lenu; baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, bali mimi nitawapigeni kwa nge. 15. Basi mfalme hakuwasikia wale watu; maana jambo hili lilitoka kwa Bwana, ili alitimize neno lake, Bwana alilomwambia Yeroboamu mwana wa Nebati kwa kinywa cha Ahiya Mshiloni.



Utangulizi.

Somo letu leo linahusu tukio hili kubwa kabisa la kusikitisha ambalo lilitokea mapema sana mara baada ya utawala wa Rehoboamu mwana wa Sulemani kuingia Madarakani!
Jina Rehoboamu maana yake “Mwenye kuwaongeza watu” Lakini hata hivyo maisha yake yalijawa na wingi wa majanga yenye kuhuzunisha na kusikitisha sana, na Moja ya janga kubwa ni kugawanyika kwa Ufalme wa Israel na kujitenga kutoka kabila la Yuda, jambo hili linatupelekea leo kuchukua Muda mfupi ili kujifunza mengi kutoka kwa Rehoboamu.

Katika kujifunza somo hili tutaangalia mambo muhimu yafuatayo:-

1.       Ushauri kutoka kwa wazee 1Falme 12:6-7
2.       Ushauri kutoka kwa vijana 1Falme 12:8-11
3.       Muitikio wa watu baada ya Uamuzi 1Falme 12:13-14a, 16

Ushauri kutoka kwa wazee IFalme 12:6-7

Inaonekana mfalme Rehoboamu alisikiliza ombi la watu, na jamii kubwa ya watu waliomshauri katika kundi la Kwanza walikuwa ni wazee, hawa walikuwa ni Makuhani, makamanda, washauri na magavana, hawa walikuwa ni watu wenye ujuzi na ufahamu kuhusu utaratibu wa Israel na tamaduni zake. Lakini pia walifahamu athari za utawala wa kifalme hasa wakati wa Sulemani na jinsi utawala wake ulivyoacha athari mbaya kwa raia wake.

Wazee hawa walichokifanya kwa Rehoboamu ilikuwa ni kuweka wazi udhaifu wa Mfalme aliyetangulia, Ufalme wa Sulemani ambaye aliitwa mwenye hekima kubwa kuliko watu wote Duniani katika nyakati zile, ulikuwa umeacha athari kubwa na makovu makubwa sana kwa watu wake na hata kwa Mungu pia, Sulemani alikosa muda wa kushughulika hata na familia yake, alikuwa akishughulika na mambo ya watu wengine Wimbo uliobora 1:5-6, Sulemani katika utawala wake alijishughulisha kushauri wafalme wa maytaifa mengine, alijishughulisha kujenga utukufu wake na sifa zake, aliiigeuza jamii yote kuwa watumwa wake, alisahau hata kumuweka Mungu mbele, alioa wanawake wengi ambao waliingiza ibada za miungu katika Israel, Mahitaji ya Sulemani yalikuwa makubwa sana kiasi ambacho aliongeza kodi kwa raia wake na kila mmoja alijihisi kuwa ni mtumwa, watu walikaa kimya, waliojaribu kumpinga walitaka kuuawa na hivyo walikimbia uhamishoni, Mungu alikwisha kukusudia mapema kuwa atausambaratisha utawala wa Sulemani na kuugawa na atabakiza kabila moja tu kwaajili ya Daudi mtumishi wake, Mungu alikwishakuupima moyo wa Sulemani nakuona kuwa ameshindwa kuiendea njia ya Daudi baba yake.

Wazee waliona nafasi ya magezi ilikuwa moja tu, ni Mara alipotawazwa Rehoboamu kuwa mfalme, hapo ndipo walipojua kuwa watapata Nafuu hivyo walimsihi mfalme.

1.       Utupunguzie utumwa mzito tuliotumikishwa na baba yako
2.       Kubali kuwa mtumwa wa watu hawa ( hapa wazee walikuwa wanamaanisha Unyenyekevu,Utu, Huruma na kujali)
3.       Wape maneno mazuri (Jibu watu vizuri, jali watu ona watu kuwa wathamani, kuwa mwema kwao na wakati mwingine wasikilize na kuwajibu watu vizuri) “Mithali 15:1-4
4.       Watu watakutumikia daima, walikuwa tayari kumtumikia mfalme anayejali
Rehoboamu alifanya maamuzi ya busara, alitulia na alitoa siku tatu kuwa atatoa jibu ni maamuzi gani atafanya.

Ushauri kutoka kwa vijana 1Falme 12:8-11.

Hata hivyo ilikuweko nafasi nyingine, hii ilikuwa ni kuwasikiliza vijana wanasema nini? Na hata hivyo hakuweza kuukubali ushauri wa wazee mapema kwani aliona hawezi kuwa mnyenyekevu na kuwatumikia watu wanaostahili kutawaliwa tu majibu ya Rehoboamu yalikuwa ya Ujeuri zaidi
1.       “Kidole changu cha mwisho ni kinene kuliko kiuno cha baba yangu” “loins – sex organ
Haya yalikuwa ni majivuno na kiburi cha hali ya juu, Rehoboamu alitaka kuonyesha kuwa ana nguvu kuliko aliyemtangulia, utawala wake ni superior kuliko ule wa Sulemani yeye ni super power
2.       Rehoboamu alishauriwa kuongeza utumwa na kodi na kuifanya nzito zaidi, alisema kama Baba aliwapiga kwa mijeledi mimi nitawapiga kwa nge (Scorpion) hiki ni chombo chenye vipande vya chuma vyenye uwezo wa kukatakata, ujumbe aliokuwa akiutoa hapa ni wazi kuwa nitaongeza machungu yenu hasa kuliko ilivyokuwa kwa Sulemani
3.        Alizungumza na watu kwa ukali sana Mstari 13. Hakuna kubembeleza mtu,Hakuna maneno mazuri wala ya Heshima
4.       Watu wakaasi na kumuacha Rehoboamu.

Muitikio wa watu baada ya Uamuzi 1Falme 12:13-14a, 16

1.       Watu waliona kuwa hawana urithi wowote katika Yuda waliamua kujitenga 15-16
2.       Watu waliamua kuangalia maisha yao wenyewe na nyumba zao wenyewe 16
3.       Watu waliingiwa na roho ya ukatili, walimuuamsimamizi wa utumwa 18
4.       Na Israel waliasi 19. Sio tu waliasi ufalme wa Yuda bali pia walimchukia Mungu wa Israel na katika utawala wao waliona waabudu miungu mingine (watu wakikasirishwa nawe hata Mungu unayemuamini hawatamuamini)
5.       Rehoboamu alitaka kupigana na Ndugu zake Mungu akamkemea 1Wafalme 12:21-24

Hitimisho.

Nini cha kujifunza kutoka katika somo hili.

1.       Kuzaliwa na mwenye Hekima hakukufanyi uwe na Hekima, wengine wameshindwa kupata japo nusu ya akili za Baba zao
2.       Tukiisha kumuacha Mungu na kumdaharu utukufu wake unaondoka
3.       Namna yoyote ile ya kutaka kuwa na nguvu na utukufu bila kutanguliza Mungu na utu utatupa kuishia kwenye wakati mgumu
4.       Bila uongozi wa kiroho au wa Roho wa Mungu hatuwezi kufanya maamuzi ya Busara
5.       Ni lazima tuwe na huruma kwa wanadamu, na kuonyesha kujali ubinadamu kwanza kabla ya mambo mengine
6.       Manabii walikuweko na makuhani, ambao waliweza hata kuepusha vita kati ya ndugu na ndugu, walitakiwa kusikilizwa kwanza
7.       Rehoboamu alilijua wazi kabisa tatizo lakini, alikataa kabisa kulishughulikia na hivyo watu walimuasi na Mungu aliruhusu
8.       Mgawanyiko na udhaifu huu uliwapa nguvu maadui wa Israel kuwamaliza na kupelekwa utumwani
9.       Lazima wakati wote tufanye maamuzi yenye busara na kukataa ushauri mbaya, lakini pia kama wazazi wetu hawakufanya vema tusiiifuate njia yao.

Mkiyajua hayo Heri ninyi mkiyatenda! Yohana 13:17

Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Rev. Innocent Kamote.

Hakuna maoni: