Jumatano, 26 Oktoba 2016

Kila amwaminiye Hatatahayarika!


Mstari wa msingi: 1Petro 2:6-8
 
6. Kwa kuwa imeandikwa katika maandiko Tazama, naweka katika Sayuni jiwe kuu la pembeni, teule, lenye heshima, Na kila amwaminiye hatatahayarika. 7. Basi, heshima hii ni kwenu ninyi mnaoamini. Bali kwao wasioamini, Jiwe walilolikataa waashi, Limekuwa jiwe kuu la pembeni.8. Tena, Jiwe la kujikwaza mguu, na mwamba wa kuangusha, Kwa maana hujikwaza kwa neno lile, wasiliamini, nao waliwekwa kusudi wapate hayo.”

 "Naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni."

Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele viwili muhimu vifuatavyo

·         Maana ya jiwe kuu la Pembeni
·         Kila amwaminiye Hatatahayarika

Utangulizi:

Leo katika Mistari hii kuna mambo ya msingi sana ya kujifunza ambayo tunayapata kutoka kwa Petro, kimsingi Petro mahali hapa alinukuu maandiko kwa kusudi la kuwatia moyo wote waliomuamini Yesu Kristo, na kulikubali neno lake, Petro anatuhakikishia kuwa hatutaaibika katika wakati huu wa sasa na hata wakati wa kuja kwake Bwana na wakati wa hukumu. Kila amwaminiye Hatatahayarika!

Jiwe kuu la Pembeni.

Nataka kwanza kuweka wazi maana ya Neno Jiwe kuu la Pembeni Yesu Kristo anaitwa jiwe kuu la Pembeni, katika taratibu za ujenzi za zamani jiwe hilo lilichongwa kwa umakini sana ili liwe limenyooka na lilitumika kutafuta unyoofu wa mawe au matofali mengine, jiwe hili kwa kawaida lilitumika kujengwa katika kona ya jingo na ndipo mawe au matofali mengine yangefuata, licha ya kuitwa jiwe kuu la Pembeni pia liliitwa Jiwe la Msingi jiwe hilo kwa mujibu wa masimulizi ya kale liliwekwa kwa vigelegele na shangwe na ndio ulikuwa msingi muhimu wa nyumba ulioshika jingo zima, Mara nyingi hasa jiwe hili la Msingi au la pembeni lilikuwa na Heshima zaidi lilipotumika kujenga Hekalu ambao kwa sasa unazungumzia kanisa au watu wa Mungu 

Waefeso 2:20-22 “20. Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni. 21. Katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana. 22. Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho.”

Maandiko yanamtaja Yesu Kristo kuwa ndio jiwe kuu la Pembeni au jiwe la msingi, maandiko yanaonyesha kuwa wale wanaomuamini na kumtegemea watakuwa na heshima kuu lakini wasiomuamini na wanaomkataa watakumbwa na mwakwazo ya ajabu sana katika maisha yao, wataainbika katika ulimwengu huu na ule ujao

Biblia inapomtaja Yesu kama Jiwe katika sayuni inatabiri pia kuweko kwa watu watakaomkataa 

Zaburi 118: 22  Jiwe walilolikataa waashi Limekuwa jiwe kuu la pembeni.” Waashi wanaotajwa hapo ni wajenzi, Mafundi ujenzi Mason hili ni kundi la Makuhani wakuu, wazee na waandishi (waalimu wa torati) hawa ndio walikuwa na nafasi ya kwanza kulijenga Hekalu na kanisa kuanzia na jamii ya Wayahudi, lakini kupitia mafundisho yao hawakuwaelekeza watu kwa Yesu na walipinga kabisa mfumo mpya na msingi mpya wa Ujenzi wa Kanisa ambalo ni Yesu, Yesu kristo ni jiwe la kweli la Msingi wote wanaomkataa wataaibika, itakuwa bahati mbaya sana kwao kwani ni kama wameumbwa wapatwe na mabaya, Makunani wazee na waandishi ambao walitarajiwa kuwajenga watu na kuwaunga na Kristo na wamekataa itakuwa ni kama wale waangukao juu ya jiwe hilo ama wale ambao jiwe litawaangukia Mapema Mzee Simon alitambua unabii huu wa Isaya na Zaburi kuwa Yesu ndio jiwe lile na aliwaelekeza watu kwa kutoa habari zake

 Luka 2:34  Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa.”

Simeon alikuwa ameelewa kuwa Yesu angekataliwa Israel nzima sawa na unabii wa Isaya na wenyeji wa Yerusalem wangemkataa masihi na kujiletea hukumu kubwa sana

Isaya 8:14-15 “14. Naye atakuwa ni mahali patakatifu; bali ni jiwe la kujikwaza na mwamba wa kujikwaa kwa nyumba za Israeli zote mbili, na mtego na tanzi kwa wenyeji wa Yerusalemu. 15. Na wengi watajikwaa juu yake, na kuanguka na kuvunjika, na kunaswa na kukamatwa.”

Mungu ampe neema kila mmoja wetu kutokuwa miongoni mwa wajenzi, waashi waliomkataa Yesu au watakao mkataa Yesu na kujiletea hukumu kubwa nay a aibu

Kila amwaminiye Hatatahayarika!

1Petro 2:6 “Kwa kuwa imeandikwa katika maandiko Tazama, naweka katika Sayuni jiwe kuu la pembeni, teule, lenye heshima, Na kila amwaminiye hatatahayarika.”

ni muhimu kufahamu kuwa Petro anaponukuu neno Kila amwaminiye hatatahayarika!, Neno hilo limetokana na na unabii wa Isaya katika kitabu cha nabii Isaya 28:16 Mstari huo unasomeka 

“16. kwa ajili ya hayo Bwana, MUNGU, asema hivi, Tazama, naweka jiwe katika Sayuni, liwe msingi, jiwe lililojaribiwa, jiwe la pembeni lenye thamani, msingi ulio imara; yeye aaminiye hatafanya haraka.”

Kuna lugha mbili hapo zinatumika  

1.       Na kila amwaminiye hatatahayarika - Petro
2.       yeye aaminiye hatafanya haraka – Isaya

Biblia zote zimetumia neno katika Isaya “He who believe shall not make HASTE” Neno la asili la kiebrania HASTE ni “NADAD” ambalo maana yake ni kutoupigwa vitani, kutokuchanganyikiwa, kutokimbia mbele ya adui zako, kutowapa kisogo adui zako, kutokuwaogopa, kutokuwa mkimbizi, kutokufutiliwa mbali, kutokuhukumiwa na kutokuaibika ndio kutokutahayarika

Petro anamthibitishia kila amwaminiye Yesu ambaye ni jiwe kuu la Pembeni hatakatiliwa mbali, hatapata aibu, hatakimbia vitani, atahishimika, kuna ushindi mkubwa kwa kila aliyemwamini na kumtegemea Yesu, kila mtu na amfanye Yesu kuwa tumaini lake aweze kuyafaidi mema ya nchi.

Na Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Jumanne, 25 Oktoba 2016

Kuuona wema wa Bwana katika nchi ya walio hai!


 
Adniko la Msingi: Zaburi 27:13. “Naamini ya kuwa nitauona wema wa BWANA Katika nchi ya walio hai


Utangulizi:

Zaburi ya 27 ni wazi kabisa kuwa ni zaburi ya Daudi, Zaburi hii ina mambo mengi sana ya kutafakari, Muda hauwezi kutosha kutafakari mambo yote, lakini leo nataka tutafakari tumaini kuu la ajabu alilokuwa nalo Daudi, kuhusu ndoto yake na ahadi za Mungu kwake, Haikuwa wazi kabisa kuwa Daudi hapa alikuwa anapigana vita ya aina gani, au bwana alikuwa amempa ushindi wa namna gani ama bado adui walikuwa wakimtishia na ulifikia wakati akaogopa  lakini bado alisalia na tumaini moja tu kwamba yeye anaamini kuwa atauona wema wa Bwana katika nchi ya walio hai! Ni kitu gani kinampa Daudi moyo wa imani hii

1.       Mstari  1-3 Alikuwa na ujuzi kuwa Bwana ni Nuru yake. Kwamba hakuna giza mbele kama unamtumainia Mungu, hofu yote inaondoka na unaweza kuiona future ( kuwa na Maisha mazuri na ya furaha) hata kama kuna kila aina ya hila, wazushi, waongo, watenda mabaya, watesi, adui, majeshi ya maadui, hivi vyote haviwezi kumtisha Daudi kwa sababu Bwana ni Nuru yake, mtu asiye na Mungu yumo gizani, ataishi maisha ya hofu kuu sana kwa sababu.

·         Watenda mabaya, wenye dhambi, waovu, wicked or evil doer
·         Watesi, waonezi, wasengenyaji, wanyanyasaji
·         Adui, foes, enemies, wapinzani, wasiotaka ufanikiwe
·         Jeshi, wanaopigana nao kimwili na kiroho, kisaikolojia, kiakili na vyovyote vile

Daudi alisema hawaogopi hao kabisa kwa sababu Bwana ni ngome ya uzima wake, Huu ulikuwa ni uthibitisho ulio dhahiri kuwa Daudi alidumisha uhusiano wake na Mungu, mtu yeyote yule atakayedumisha uhusiano wake na Mungu hawezi kutembea gizani, hawawezi kupoteza tumaini hata kama wataogopa watajitia moyo, na Mungu kwa hakika atawapigania na kuwalinda hakuna adui anaweza kufanikiwa kwako kama ilivyokuwa kwa Daudi ndivyo itakavyokuwa kwa kila anayemtanguliza Mungu mbele

2.       Mstari 4-5 Daudi anaeleza sababu kubwa ya kumtegemea Mungu ni kwamba pia akipewa uhai na kulindwa na Mungu atautumia uhai huo kukaa nyumbani mwa Bwana, ana kiu na shauku ya kutaka kuendelea kumuabudu Mungu, ni kama anaweka Nadhiri kwa Mungu mradi Bwana atanisitiri siku ya Mabaya na kuniinua, basi katika maisha yangu nitamuabudu, nitamtafakari, hekaluni mwake nitamuimbia, Daudi aliongeza aina nyingine ya Mapito na maombi aliyotaka mungu amtendee lakini kubwa zaidi anahitimisha kwa imani kuwa

3.       Anaamini kuwa atauona wema wa Bwana katika nchi ya walio hai, katika eneo hili Daudi alimuomba Mungu Mstari 12, asimtie katika nia ya adui zake, nia ya adui zake ni kumuangusha ni kuona kuwa hafanikiwi, ni kutoa ushahidi wa uongo na maneno ya Jeuri sana, Lakini Daudi anaamini atauona wema wa Bwana katika inchi ya walio hai

Mstari 13 jambo gani kubwa tunajifunza, hapa Daudi alielewa wazi kuwa kuna maisha baada ya kufa, alijua kuna kuishi milele, alijua kuna kwenda Mbinguni, lakini hakufurahia kuishi kwa shida Duniani, hapa alimuamini Mungu kuwa hatamuacha afe bila kumuonyesha mema katika nchi ya walio hai yaani hapa Duniani,

Kuingia mbinguni sawa kupo, kula vizuri mbinguni sawa kupo, magari ya farasi mbinguni sawa yapo, maisha ya matanuzi huko mbinguni sawa yapo lakini Daudi aliomba auone wema wa Mungu hapa Duniani kwenye nchi ya walio hai, kuna nchi ya wafu sawa, lakini kabla ya kwenda huko je nisionje mema ? kuna kufaulu kule mbinguni sawa, lakini ndo nifeli na Duniani, kuna majumba mbiguni sawa lakini ndo niishi katika kijinyumba cha nyasi Duniani? Kuna magari ya farasi za moto mbinguni sawa lakini je hapa duniani nisiendeshe hata toyo?, kuna hali ya hewa nzuri Mbinguni sawa lakini ndio nisipigwe hata na kiyoyozi duniani Daudi alimuomba Mungu kwamba ni lazima ufikie wakati vita vimalizike, mapambano yaishe, awe na wakati wa starehe, afanye kazi ya kuabudu

ndugu ulivyopambana duniani inatosha sasa mwambie Mungu akufurahishe akuonyeshe wema wake sasa, lazima ufikie ndoto zako na kuepushwa na kila aina ya mabaya ya dunia hii na Mungu atakupa kustarehe Hatimaye daudi alistarehe

2Samuel 7:1-2 “1. Ikawa, mfalme alipokuwa akikaa katika nyumba yake, hapo Bwana alipomstarehesha, asiudhiwe na adui zake waliomzunguka pande zote, 2. mfalme akamwambia Nathani, nabii, Angalia sasa, mimi ninakaa katika nyumba ya mierezi, bali sanduku la Mungu linakaa ndani ya mapazia.

Uko wakati wa Mapambano lakini pia uko wakati wa kustarehe Mungu na akufanikishe katika vita vyako na pia akujaalie wakati wa Kustarehe kama ilivyokuwa kwa Daudi


Naamini ya kuwa nitauona wema wa BWANA Katika nchi ya walio hai
Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Jumatatu, 24 Oktoba 2016

Sisi tutalitaja jina la Bwana Mungu wetu!


Andiko Zaburi 20:7 “ Hawa wanataja magari na hawa farasi, Bali sisi tutalitaja BWANA, Mungu wetu


 Hawa wanataja magari na hawa farasi, Bali sisi tutalitaja BWANA, Mungu wetu

Utangulizi.

Ni muhimu kufahamu kuwa Zaburi hii chimbuko lake ni Mfalme Daudi, kiongozi wa nyimbo au kwaya wa Daudi aliimba wimbo huu, au Daudi alitunga na kuwapa watu wa sifa waimbe hivyo Zaburi hii inahesabika kama moja ya zaburi ya Daudi, Hata hivyo kihistoria Zaburi hii ilitumiwa sana na wafalme waliofuata baada ya Daudi kama njia ya maombi walipokuwa wanakwenda kupigana vita, Mfalme aliomba na kutoa sadaka kisha watu walisindikiza maombi na dua za mfalme wao kwa Zaburi hii, hivyo ni zaburi maarufu kama maombi kwaajili ya kukabiliana na mambo ya kutisha! Ilitumika wakati wa shida na wakati wa kuhitaji msaada.

Kuna mambo mengi sana yaliyomo katika zaburi hii, lakini kubwa likiwa ni Dua ya kumuombea Mfalme, kwa nini mfalme aliomewa sana kwa sababu yeye alitangulia mbele wakati wa vita, alikuwa ndio mpambanaji mkuu na hivyo waimbaji na waombaji walimuombea angalia Mstari wa 1-4 Biblia inasema

1. Bwana akujibu siku ya dhiki, Jina la Mungu wa Yakobo likuinue. 2. Akupelekee msaada toka patakatifu pake, Na kukutegemeza toka Sayuni. 3. Azikumbuke sadaka zako zote, Na kuzitakabali dhabihu zako. 4. Akujalie kwa kadiri ya haja ya moyo wako, Na kuyatimiza mashauri yako yote.”

Baada ya dua na maombi ya kumuombea Mfalme waliweka matumaini yao kuwa Mungu anakwenda kuwapa ushindi hivyo walianza kushangilia ushindi, walilitumia jina la bwana na waliweka bendera tayari kwa imani  na pia walimkumbusha Mungu kwa imani kuwa atamwokoa masihi wake na kumjibu Maombi yake walikuwa na ujasiri kuwa watajibiwa Mstari wa 5-6 na kuwa ni lazima Mungu atafanya mambo makubwa kwa mkono wake 

“5. Na tuushangilie wokovu wako, Kwa jina la Mungu wetu tuzitweke bendera zetu. Bwana akutimizie matakwa yako yote. 6. Sasa najua kuwa Bwana amwokoa masihi wake;Atamjibu kutoka mbingu zake takatifu.”

Katika mstari wa 7 na wa 8 waimbaji hawa walionyesha tofauti iliyoko kati ya wanaoamini na wasioamini lakini pia walionyesha kwamba ndipo mahali pa kuzingatiwa sana katika utendaji wa Mungu, “Hao (wasiamini) au wenye kiburi wanataja Magari na hawa wasiomtegemea Mungu wa kweli wanataja Farasi, Bali sisi tunaoliamini Jina la Mungu tutalitaja jina la bwana Mungu wetu! Ni muhimu kupaangalia mahali hapa kwa makini sana

Mungu alikuwa amewafundisha Isarael siku nyingi sana kumtegemea yeye na kumwangalia kwaajili ya ushindi na dhiki ya aina yoyote, na katika nyakati za vita moja ya vitu vilivyokuwa vinaogopewa sana katika nyakati za vita za zamani ni magari ya vita na magari ya wapiganaji walikuwa wakipigana juu ya farasi, watu hao walikuwa hodari hata kufukuzia na hivyo katika nyakati za biblia watu au mataifa yaliyokuwa na magari ya vita na wapanda farsi hodari waliogopwa zaidi kwani ndio waliokuwa hatari na wenye kutisha sana katika nyakati za leo Magari haya tungeweza kufananisha na tanks au vifaru wakati wa vita wote tunajua namna vinavyotisha sana

Mungu aliwaonya mapema Israel kutokuogopa Kumbukumbu la taorati 20: 1Utokapo kwenda vitani kupigana na adui zako na kuona farasi na magari na watu wengi sana kuliko wewe usiwaogope, kwa kuwa Bwana Mungu wako yu pamoja nawe aliyekukweza kutoka nchi ya Misri” pia Yoshua 17:16

Nchi ya Misri na Syria ndio zilikuwa hatari zaidi kwa aina hii ya vita katika nyakati hizo na makabila mengine pia Israel hawakuwa na aina hiyo ya silaha wakati huo, wala hawakuwa na jeshi kubwa sana, hivyo wale wasiomuamini Mungu waliweka tumainilao katika hayo magari ya chuma nay a farasi na wapanda farasi, Israel walikuwa wamekwisha kupata somo kubwa kwamba Misri ilifanywa nini pamoja na kuwa na Magari ya farasi na wapanda farasi Kutoka 15:1-4, Mungu alikwisha kuwafundisha kutokuyategemea magari na wapanda farasi, Mungu aliwajulisha kuwa hufanya mambo kwaajili ya jina lake na kwaajili ya utukufu wake, Mungu hatakuinamisha bali Mungu atakusimamisha mungu hatakuaibisha bali Mungu atakuokoa Mstari 8-9 waimbaji wanaonyesha kuwa hawataaibika na kuwa adui zao watainama

Ndugu yangu haijalishi ni hila kiasi gani adui anazo,

Haijalishi watakuwa na nguvu kiasi gani

Haijalishi magonjwa yamekutesa kiasi gani, yamekuandama na kukukandamiza kwa kiwango gani mtegemee Mungu tu

Haijalishi watakuwa na mbinu  za kibinadamu kiasi gani, wana silaha na magari ya chuma kiasi gani, wana watetezi kiasi gani, wana uzoefu kiasi gani, wana akili kiasi gani, wana mitego kiasi gani, wana nguvu kiasi gani tunachokiangalia wanatumainia nini, je wanatumainia fedha, majeshi, nguvu waimbaji wakasema wao wanataja Farasi namagari sisi tutalitaja jina la Bwana Mungu wetu, wapendwa na tuchangamke, tunaye Mungu, tunaye shujaa, anauwezo, ana nguvu, ni hodari wa vita atatupigania anakwenda kutupa ushindi anza kuufurahia ushidni wako leo yuko Mungu wa Yakobo atatuokoa na ataisikia sauti yetu,

Bwana Mungu nimekutegemea wewe, tumaini langu si kwa wanadamu Bali ni katika jina lako
Sasa najua kuwa Bwana amwokoa masihi wake*

Na. Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Hapana mfalme aokokaye kwa wingi wa uwezo!



Andiko la Msingi: Zaburi 33: 16—19 Biblia inasema “16. Hapana mfalme aokokaye kwa wingi wa uwezo, Wala shujaa haokoki kwa wingi wa nguvu. 17. Farasi hafai kitu kwa wokovu, Wala hamponyi mtu kwa wingi wa nguvu zake. 18. Tazama, jicho la Bwana li kwao wamchao, Wazingojeao fadhili zake. 19. Yeye huwaponya nafsi zao na mauti, Na kuwahuisha wakati wa njaa. 20. Nafsi zetu zinamngoja Bwana; Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu.”

 Hapana mfalme aokokaye kwa wingi wa uwezo, Wala shujaa hamponyi mtu kwa wingi wa nguvu zake
 
Utangulizi:

Zaburi hii ni zaburi inayokazia katika tabia ya kumtegemea Mungu na kupata Ushindi katika maisha yetu, ni zaburi ambayo haithibitiki kuwa ilikuwa ya Mfalme Daudi kama ilivyo kwa zaburi nyingine, lakini Zaburi hii inawezekana kabisa ni zaburi iliyoimbwa na kwaya ya Walawi, waliokuwa wakimsifu Mungu kwa Amri ya Daudi miaka mingi nyuma alimchagua kiongozi mkuu wa sifa aliyeitwa Asafuhuyu  alikuwa kiongozi wa sifa na nduguze na baadaye wana wa Asafu walirithi kazi hii ya kuimba na kumsifu Mungu

 1Nyakati 16:7-8, Ndipo siku hiyo Daudi alipoagiza kwanza kumshukuru Bwana, kwa mkono wa Asafu na nduguze. Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake; Wajulisheni watu matendo yake.” 

Na pia 1Nyakati 25:1  Tena Daudi na maakida wa jeshi wakatenga kwa utumishi baadhi ya wana wa Asafu, na wa Hemani, na wa Yeduthuni, watakaotabiri kwa vinubi na vinanda, na matoazi; hii ndiyo hesabu ya wafanya kazi sawasawa na utumishi wao;”

Hivyo wana wa Asafu ndio waliimba Zaburi hii na ni wazi kuwa Kiongozi wa ibada ya sifa aliimbisha kuanzia mstari wa 1-3 na kisha waimbaji wengine waliitikia katika mistari yote inayofuata, kwa vyoyote vile wimbo huu unaonekana kuitwa wimbo mpya na huenda ulizungumzia tukio la kuokolewa kwa taifa hususani ufalme wa Yuda

Wimbo unaonekana kudhihirisha tukio la ushindi wa kitaifa lililotokea wakati wa utawala wa Yehoshafati au wakati wa utawala wa Hezekia, Pia kidogo Ushindi wa Daudi dhidi ya Goliath, Nyakati za utawala wa wafalme hao Mungu alikwisha dhihirisha kuwa haokoi kwa wingi wa jeshi, wala shujaa hapati ushindi kwa wingi wa nguvu zake!

·         2Nyakati 20:1-30 Mungu alisambaratisha combine ya majeshi yote yaliyoinuka juu ya Yehoshafati na Yuda bila kupigana “mwaminini Mungu mtathibitika waaminini manabii wake mtafanikiwa”

·         2Wafalme 19:1-35 Malaika wa Bwana alipiga watu 185,000 mst 35 huu ulikuwa wakati wa Hezekia
Mungu alikuwa amekwisha wafundisha Israel kivitendo kuwa wokovu wake hautegemei wingi wa nguvu alizonazo mtu au wingi wa jeshi lake bali mtu akimtegemea Mungu na kumcha Mungu, Mungu huleta wokovu mkuu

Zaburi 33:16-19
1.       Inatoa somo kuu sana Mungu anaokoa kwa uweza wake si katika njia zinazotegemewa na wanadamu
2.       Yeye ndiye mlinzi mkuu sana wa maisha yetu na kuwa tusipomuhusisha yeye katika maisha yetu uwezekano wa kujilinda wenyewe ni hafifu

3.       Jeshi hata liwe kubwa kiasi gani na liwe na akili kiasi gani na vifaa kiasi gani, Mungu anaweza kuleta ugonjwa ukawapiga jeshi zima, anaweza kuwatia hofu wakaogopa wote na kutwawanyika kwa hofu

4.       Rehema zake zinao wamchao siku zote Muhubiri 9:11 si wenye mbio washindao, wala sio waliohodari washidao vita, wala sio wenye hekima wapatao chakula, wala si watu wa ufahamu wapatao mali, wala wenye ustadi wapatao upendeleo

5.       Goliath alikuwa na nguvu na uzoefu wa vita lakini alishindwa na Daudi kijana mororo.
Mafanikio yetu hayako katika ujanja na uweza wa kibinadamu yako katika kumtanguliza Mungu na kumtegemea, uwezo wetu wa kufaulu katika Mitihani utategemea na namna tunavyomtegemea Mungu na kujinyenyekeza kwake, Ufanisi wa kweli uko katika kumtegemea Mungu, kumfanya yeye kuwa kinga yetu, kumtanguliza Yesu mbele, kuhakikisha tunafanya mambo kwa utukufu wake, kuhakikisha kuwa hatutafuti utukufu wetu wenyewe bali tunatafauta utukufu wa Mungu, Daudi hakuwa anatafuta utukufu wake, alitaka Mungu ainuliwe, Tazama jicho la Bwana li kwao wamchao , wazingojeao fadhili zake’ huwaponya wakati wa mauti na kuwahuisha wakati wa njaa.

Wana wa Asafu walihitimisha kwa kusema nafsi zetu zinamngoja Bwana, yeye ndiye Msaada wetu na ngao yetu, mioyo yetu itanfurahia kwa kuwa tumelitumainia jina lake ee bwana fadhili zako zikae nasi kama vile tulivyokungoja wewe” 

16-17 hatuwezi kufanyo lolote bila Mungu
18 –19 Mungu mwenyewe huwaangalia wamchao na kuwasaidia wanaongoja msaada wake
20- wana wa Asafu na Israel wote waliamua kuwa watamngoja Bwana na kumtegemea yeye
21, walijua kuwa watafurahi walijitolea unabii kwa sababu wamelitumainia Jina lake
22 walijiombe fadhili za Mungu zikae nao milele.

Wema wako nimeungoja ee Bwana!

Na Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!