Jumatatu, 24 Oktoba 2016

Hapana mfalme aokokaye kwa wingi wa uwezo!



Andiko la Msingi: Zaburi 33: 16—19 Biblia inasema “16. Hapana mfalme aokokaye kwa wingi wa uwezo, Wala shujaa haokoki kwa wingi wa nguvu. 17. Farasi hafai kitu kwa wokovu, Wala hamponyi mtu kwa wingi wa nguvu zake. 18. Tazama, jicho la Bwana li kwao wamchao, Wazingojeao fadhili zake. 19. Yeye huwaponya nafsi zao na mauti, Na kuwahuisha wakati wa njaa. 20. Nafsi zetu zinamngoja Bwana; Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu.”

 Hapana mfalme aokokaye kwa wingi wa uwezo, Wala shujaa hamponyi mtu kwa wingi wa nguvu zake
 
Utangulizi:

Zaburi hii ni zaburi inayokazia katika tabia ya kumtegemea Mungu na kupata Ushindi katika maisha yetu, ni zaburi ambayo haithibitiki kuwa ilikuwa ya Mfalme Daudi kama ilivyo kwa zaburi nyingine, lakini Zaburi hii inawezekana kabisa ni zaburi iliyoimbwa na kwaya ya Walawi, waliokuwa wakimsifu Mungu kwa Amri ya Daudi miaka mingi nyuma alimchagua kiongozi mkuu wa sifa aliyeitwa Asafuhuyu  alikuwa kiongozi wa sifa na nduguze na baadaye wana wa Asafu walirithi kazi hii ya kuimba na kumsifu Mungu

 1Nyakati 16:7-8, Ndipo siku hiyo Daudi alipoagiza kwanza kumshukuru Bwana, kwa mkono wa Asafu na nduguze. Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake; Wajulisheni watu matendo yake.” 

Na pia 1Nyakati 25:1  Tena Daudi na maakida wa jeshi wakatenga kwa utumishi baadhi ya wana wa Asafu, na wa Hemani, na wa Yeduthuni, watakaotabiri kwa vinubi na vinanda, na matoazi; hii ndiyo hesabu ya wafanya kazi sawasawa na utumishi wao;”

Hivyo wana wa Asafu ndio waliimba Zaburi hii na ni wazi kuwa Kiongozi wa ibada ya sifa aliimbisha kuanzia mstari wa 1-3 na kisha waimbaji wengine waliitikia katika mistari yote inayofuata, kwa vyoyote vile wimbo huu unaonekana kuitwa wimbo mpya na huenda ulizungumzia tukio la kuokolewa kwa taifa hususani ufalme wa Yuda

Wimbo unaonekana kudhihirisha tukio la ushindi wa kitaifa lililotokea wakati wa utawala wa Yehoshafati au wakati wa utawala wa Hezekia, Pia kidogo Ushindi wa Daudi dhidi ya Goliath, Nyakati za utawala wa wafalme hao Mungu alikwisha dhihirisha kuwa haokoi kwa wingi wa jeshi, wala shujaa hapati ushindi kwa wingi wa nguvu zake!

·         2Nyakati 20:1-30 Mungu alisambaratisha combine ya majeshi yote yaliyoinuka juu ya Yehoshafati na Yuda bila kupigana “mwaminini Mungu mtathibitika waaminini manabii wake mtafanikiwa”

·         2Wafalme 19:1-35 Malaika wa Bwana alipiga watu 185,000 mst 35 huu ulikuwa wakati wa Hezekia
Mungu alikuwa amekwisha wafundisha Israel kivitendo kuwa wokovu wake hautegemei wingi wa nguvu alizonazo mtu au wingi wa jeshi lake bali mtu akimtegemea Mungu na kumcha Mungu, Mungu huleta wokovu mkuu

Zaburi 33:16-19
1.       Inatoa somo kuu sana Mungu anaokoa kwa uweza wake si katika njia zinazotegemewa na wanadamu
2.       Yeye ndiye mlinzi mkuu sana wa maisha yetu na kuwa tusipomuhusisha yeye katika maisha yetu uwezekano wa kujilinda wenyewe ni hafifu

3.       Jeshi hata liwe kubwa kiasi gani na liwe na akili kiasi gani na vifaa kiasi gani, Mungu anaweza kuleta ugonjwa ukawapiga jeshi zima, anaweza kuwatia hofu wakaogopa wote na kutwawanyika kwa hofu

4.       Rehema zake zinao wamchao siku zote Muhubiri 9:11 si wenye mbio washindao, wala sio waliohodari washidao vita, wala sio wenye hekima wapatao chakula, wala si watu wa ufahamu wapatao mali, wala wenye ustadi wapatao upendeleo

5.       Goliath alikuwa na nguvu na uzoefu wa vita lakini alishindwa na Daudi kijana mororo.
Mafanikio yetu hayako katika ujanja na uweza wa kibinadamu yako katika kumtanguliza Mungu na kumtegemea, uwezo wetu wa kufaulu katika Mitihani utategemea na namna tunavyomtegemea Mungu na kujinyenyekeza kwake, Ufanisi wa kweli uko katika kumtegemea Mungu, kumfanya yeye kuwa kinga yetu, kumtanguliza Yesu mbele, kuhakikisha tunafanya mambo kwa utukufu wake, kuhakikisha kuwa hatutafuti utukufu wetu wenyewe bali tunatafauta utukufu wa Mungu, Daudi hakuwa anatafuta utukufu wake, alitaka Mungu ainuliwe, Tazama jicho la Bwana li kwao wamchao , wazingojeao fadhili zake’ huwaponya wakati wa mauti na kuwahuisha wakati wa njaa.

Wana wa Asafu walihitimisha kwa kusema nafsi zetu zinamngoja Bwana, yeye ndiye Msaada wetu na ngao yetu, mioyo yetu itanfurahia kwa kuwa tumelitumainia jina lake ee bwana fadhili zako zikae nasi kama vile tulivyokungoja wewe” 

16-17 hatuwezi kufanyo lolote bila Mungu
18 –19 Mungu mwenyewe huwaangalia wamchao na kuwasaidia wanaongoja msaada wake
20- wana wa Asafu na Israel wote waliamua kuwa watamngoja Bwana na kumtegemea yeye
21, walijua kuwa watafurahi walijitolea unabii kwa sababu wamelitumainia Jina lake
22 walijiombe fadhili za Mungu zikae nao milele.

Wema wako nimeungoja ee Bwana!

Na Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Hakuna maoni: