Mstari wa msingi: 1Petro 2:6-8
“6. Kwa kuwa imeandikwa katika maandiko Tazama,
naweka katika Sayuni jiwe kuu la pembeni, teule, lenye heshima, Na kila
amwaminiye hatatahayarika. 7. Basi, heshima hii ni kwenu ninyi mnaoamini. Bali
kwao wasioamini, Jiwe walilolikataa waashi, Limekuwa jiwe kuu la pembeni.8.
Tena, Jiwe la kujikwaza mguu, na mwamba wa kuangusha, Kwa maana hujikwaza kwa
neno lile, wasiliamini, nao waliwekwa kusudi wapate hayo.”
"Naye
Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni."
Tutajifunza somo hili kwa
kuzingatia vipengele viwili muhimu vifuatavyo
·
Maana ya
jiwe kuu la Pembeni
·
Kila
amwaminiye Hatatahayarika
Utangulizi:
Leo katika Mistari hii kuna mambo
ya msingi sana ya kujifunza ambayo tunayapata kutoka kwa Petro, kimsingi Petro
mahali hapa alinukuu maandiko kwa kusudi la kuwatia moyo wote waliomuamini Yesu
Kristo, na kulikubali neno lake, Petro anatuhakikishia kuwa hatutaaibika katika
wakati huu wa sasa na hata wakati wa kuja kwake Bwana na wakati wa hukumu. Kila amwaminiye Hatatahayarika!
Jiwe kuu la Pembeni.
Nataka kwanza kuweka wazi maana
ya Neno Jiwe kuu la Pembeni Yesu
Kristo anaitwa jiwe kuu la Pembeni, katika taratibu za ujenzi za zamani jiwe
hilo lilichongwa kwa umakini sana ili liwe limenyooka na lilitumika kutafuta
unyoofu wa mawe au matofali mengine, jiwe hili kwa kawaida lilitumika kujengwa
katika kona ya jingo na ndipo mawe au matofali mengine yangefuata, licha ya
kuitwa jiwe kuu la Pembeni pia liliitwa Jiwe
la Msingi jiwe hilo kwa mujibu wa masimulizi ya kale liliwekwa kwa
vigelegele na shangwe na ndio ulikuwa msingi muhimu wa nyumba ulioshika jingo zima,
Mara nyingi hasa jiwe hili la Msingi au la pembeni lilikuwa na Heshima zaidi
lilipotumika kujenga Hekalu ambao kwa sasa unazungumzia kanisa au watu wa Mungu
Waefeso 2:20-22 “20. Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye
Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni. 21. Katika yeye jengo lote
linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana. 22.
Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho.”
Maandiko yanamtaja Yesu Kristo
kuwa ndio jiwe kuu la Pembeni au jiwe la msingi, maandiko yanaonyesha kuwa wale
wanaomuamini na kumtegemea watakuwa na heshima kuu lakini wasiomuamini na
wanaomkataa watakumbwa na mwakwazo ya ajabu sana katika maisha yao, wataainbika
katika ulimwengu huu na ule ujao
Biblia inapomtaja Yesu kama Jiwe katika sayuni inatabiri pia kuweko kwa
watu watakaomkataa
Zaburi 118: 22 “Jiwe walilolikataa waashi Limekuwa jiwe kuu la
pembeni.” Waashi wanaotajwa hapo ni wajenzi, Mafundi ujenzi Mason
hili ni kundi la Makuhani wakuu, wazee na waandishi (waalimu wa torati) hawa
ndio walikuwa na nafasi ya kwanza kulijenga Hekalu na kanisa kuanzia na jamii
ya Wayahudi, lakini kupitia mafundisho yao hawakuwaelekeza watu kwa Yesu na
walipinga kabisa mfumo mpya na msingi mpya wa Ujenzi wa Kanisa ambalo ni Yesu,
Yesu kristo ni jiwe la kweli la Msingi wote wanaomkataa wataaibika, itakuwa
bahati mbaya sana kwao kwani ni kama wameumbwa wapatwe na mabaya, Makunani
wazee na waandishi ambao walitarajiwa kuwajenga watu na kuwaunga na Kristo na
wamekataa itakuwa ni kama wale waangukao juu ya jiwe hilo ama wale ambao jiwe
litawaangukia Mapema Mzee Simon alitambua unabii huu wa Isaya na Zaburi kuwa
Yesu ndio jiwe lile na aliwaelekeza watu kwa kutoa habari zake
Luka 2:34 “Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake,
Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na
kuwa ishara itakayonenewa.”
Simeon alikuwa ameelewa kuwa Yesu angekataliwa Israel nzima sawa na
unabii wa Isaya na wenyeji wa Yerusalem wangemkataa masihi na kujiletea hukumu
kubwa sana
Isaya 8:14-15 “14. Naye atakuwa ni mahali patakatifu; bali ni jiwe la
kujikwaza na mwamba wa kujikwaa kwa nyumba za Israeli zote mbili, na mtego na
tanzi kwa wenyeji wa Yerusalemu. 15. Na wengi watajikwaa juu yake, na kuanguka
na kuvunjika, na kunaswa na kukamatwa.”
Mungu ampe neema kila mmoja wetu
kutokuwa miongoni mwa wajenzi, waashi waliomkataa Yesu au watakao mkataa Yesu
na kujiletea hukumu kubwa nay a aibu
Kila amwaminiye Hatatahayarika!
1Petro 2:6 “Kwa kuwa imeandikwa katika maandiko Tazama, naweka katika
Sayuni jiwe kuu la pembeni, teule, lenye heshima, Na kila amwaminiye
hatatahayarika.”
ni muhimu kufahamu kuwa Petro anaponukuu neno Kila amwaminiye
hatatahayarika!, Neno hilo limetokana na na unabii wa Isaya katika kitabu cha
nabii Isaya 28:16 Mstari huo unasomeka
“16. kwa ajili ya hayo Bwana, MUNGU, asema hivi, Tazama, naweka jiwe katika
Sayuni, liwe msingi, jiwe lililojaribiwa, jiwe la pembeni lenye thamani, msingi
ulio imara; yeye aaminiye hatafanya haraka.”
Kuna lugha mbili hapo zinatumika
1.
Na
kila amwaminiye hatatahayarika - Petro
2.
yeye
aaminiye hatafanya haraka – Isaya
Biblia zote zimetumia neno katika
Isaya “He who believe shall not make
HASTE” Neno la asili la kiebrania HASTE ni “NADAD” ambalo maana yake ni kutoupigwa
vitani, kutokuchanganyikiwa, kutokimbia mbele ya adui zako, kutowapa kisogo adui zako, kutokuwaogopa, kutokuwa mkimbizi, kutokufutiliwa
mbali, kutokuhukumiwa na kutokuaibika ndio kutokutahayarika
Petro anamthibitishia kila
amwaminiye Yesu ambaye ni jiwe kuu la Pembeni hatakatiliwa mbali, hatapata
aibu, hatakimbia vitani, atahishimika, kuna ushindi mkubwa kwa kila
aliyemwamini na kumtegemea Yesu, kila mtu na amfanye Yesu kuwa tumaini lake
aweze kuyafaidi mema ya nchi.
Na Rev. Innocent Kamote
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni