Jumanne, 17 Oktoba 2017

Kama sisi ni mwili mmoja basi tuheshimiane!



Mstari wa Msingi: Warumi 12:4-5Kwa kuwa kama vile katika mwili mmoja tuna viungo vingi, wala viungo vyote havitendi kazi moja; Vivyo hivyo na sisi tulio wengi tu mwili mmoja katika Kristo, na viungo, kila mmoja kwa mwenzake.”

 Ndege wa ajabu aliyekuwa na vichwa viwili

Utangulizi.

Neno la Mungu linatufundisha kuwa na ushirika wenye mshikamano wa kipekee kama vile ulivyo mwili wa mwanadamu,tutakuwa tunafikiri vema na kwa unyenyekevu kama tutakuwa tunatambua kuwa sisi ni sehemu tu ya huo mwili wa Kristo, yaani sisi ni kiungo kimojawapo katika mwili wa Kristo, kwa sababu hiyo kila tutendapo jambo lolote ni muhimu kulitenda kwa kuzingatia na wengine pia, kwa kuzingatia kuwa hatuko peke yetu, kwa kuzingatia kuwa kila mmoja ni wa muhimu, kwa kuzingatia kuwa hakuna wa kupuuzwa, hii sio katika kanisa peke yake lakini na katika ndoa pia na katika mashirika pia, na katika sehemu yoyote ambapo watu hufanya kazi kwa pamoja kwa kusudi moja kanuni ya kuheshimiana itatusaidia kuwa na mafanikio makubwa sana na ufanisi.  

Kwa mujibu wa Mwana theolojia Gene Getz wMwandishi wa kitabu kiitwachoi Kujengana, kwa kiingereza (Building Up One Another [Victor Books, 1976]) anaeleza kuwa Neno kila mmoja na mwenzake limetajwa katika Agano jipya nje ya Injili mara 58 ili kukazia kujaliaana kwenye nia ya viwango vya juu sana na ametaja mara 12 neno KILA MTU NA MWENZAKE LINAVYOJITOKEZA KATIKA AYA KADHAA ZA BIBLIA YA KIYUNANI.  Nazinukuu:-

1.      Tu viungo kila mmoja na mwenzake Warumi 12:5
2.      Tupendane kila mmoja na mwenzake Warumi 12:10
3.      Tuheshimiana kila mmoja na mwenzake Warumi 12:10
4.      Kunai mamoja kila mmoja na mwenzake Warumi 15:5
5.      Kukaribishana kila moja na mwenzake Warumi 15:7
6.      Kuonyana kila mmoja na mwenzake Warumi 15:14
7.      Kusalimiana kila mmoja na mwenzake Warumi 16:3-16
8.      Tumikianeni kila mmoja na mwenzake ninyi ni ndugu Wagalatia 5:13
9.      Mchukuliane mizigo kila mmoja na mwenzake Wagalatia 6:2-3
10.  Kwa kuvumilina na kuchukuliana katika upendo kila mmoja na mwenzake Waefeso 4:2-4
11.  Kwa kunyenyekeeana  kila mmoja na mwenzake Waefeso 5:11
12.  Kwa kutiana moyo kila mmoja na mwenzake 1Wathesalonike 5:11

Aya zote hizi hapo juu zinakazia ukweli kwamba Mungu anataka tuwe na ushirikiano usiokuwa wa kawaida na kwamba ni muhimu kila mmoja akajifunza kuwa mbali na ubinafsi na kuwajali wengine hasa kama tumeungwa katika imani moja.

Mfano:-

Wakati fulani katika hali ye kushangaza sana aliwahi kutokea ndege mmoja ambaye alikuwa na vichwa viwili kimoa kiliangalia kulia na kingine kiliangalia kushoto, Hata hivyo ndege huyu mwenye mwili mmoja vichwa viwili, vichwa vyao havikuwa na maelewano mazuri na mara kwa mara waligombana na kubishana, hata kwa mambo ambayo yalkikuwa rahisi sana ingawa kumbka walikuwa wanamwili mmoja.

Ndege huyu wa ajabu aliishi katika mti mmoja mkubwa uliokuwa kando ya mto

Siku moja alipokuwa akiruka kuvuka nga’mbo ya mto kichwa cha kushoto kiliona mti mzuri sana uliokuwa na tunda zuri, kichwa cha kushoto kilitamani kula tunda lile na hivyo alitua kwaajili ya kula tunda kichwa cha kushoto kilikula tunda hilo ambalo lilikuwa linanukia vizuri sana, wakati kicha cha kushoto kinakula kichwa cha kulia kiliuliza ndugu unaweza kuniachia na mimi nijaribu ladha la hilo tunda?

Kichwa cha kushoto kikajibu “ Ndugu una wasiwasi gani tuna tumo moja tu kwa hiyo hata kama mimi nitakula kwa mdomo wangu vitaelekea kwenye tumbo letu tu” “ lakini nataka kuonja tu utamu wa hilo tunda tafadhali naomba na mimi” kilijibu kichwa cha kulia.

Kichwa cha kushoto kilijibu kwa kupuuzia bwana ee tuna tumbo moja tu kwa hiyo hata nikila mimi vitaelekea kwenye tumbo letu nina haki nya kula hata bila kukushirikisha kikala chenyewe!
Kichwa cha kulia kilijisikia vibaya na kikanyamaza kimya.

Siku chache baadaye wakati ndege alipokuwa katika safari zake kichwa cha kulia kiliona tuna la rangi ya manjano katika mojawapo ya mti hivyo ndege alitua na kujaribu kulichuma tunda hilo 

Ndege wengine wanaoishi karibu na mti huo walisema kwa sauti USILE USILE tafadhali tunda hilo lina sumu kali litakuua.

Kichwa cha kushoto kiliposikia kiasema USILE, USILE  Bwana!

Hata hivyo kichwa cha kulia hakikusikiliza yanayosemwa na kichwa cha kushoto, Kichwa cha kulia kilijibu kuwa Nina haki ya kula hata bila kukushirikisha kwa hiyo huna haki ya kunizuia

Kichwa cha kushoto kilipiga kelele tafadhali usile tutakufaa!

Kichwa cha kulia kilijibu kwa kuwa nimeliona nina haki ya kula bila kukushirikisha, kichwa cha kulia kilikuwa kinalipa kisasi kwa kichwa cha kushoto kutokaa na choyo chake dhidi ya lile tunda la kwanza

Hatimaye kichwa cha kulia kilikula lile tunda lenye sumu na baada ya sekunde chache ndege huyu wa ajabu mwenye vichwa viwili alifariki dunia.

Ndugu zangu hakuna sumu kali, kama mafarakano, mafarakano katika taifa, katikafamilia, katika mashirika, katika kazi, katika kanisa, katika misikiti yanaharibu ustawi na maendeleo ya kila mmoja wetu 

Ni muhimu kuzingatia kama mafundisho ya biblia yanavyokazia umoja na mshikamano sisi nasi tukaendelea kuwa na umoja na mshikamano katika kila Nyanja ya maisha yetu, tusikubali watu wakatugawanga, tusikubalia mafarakanano ya sisi kwa sisi ni sumu na itaua na kuharibu umoja na mshikamano na ustawi wetu, kiungo kimoja kikiumia vyote huumia hivyo kama sisi ni mwili mmoja basi tuheshimiane.
.
Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Rev. Innocent Kamote.

Jumapili, 15 Oktoba 2017

Bwana Mungu wako Ndiye atakayevuka mbele yako!


Kumbukumbu 31:3-6 
 
Bwana Mungu wako, ndiye atakayevuka mbele yako, atawaangamiza mataifa haya mbele yako, nawe utawamiliki; na Yoshua atavuka mbele yako, kama Bwana alivyonena. Na Bwana atawatenda hao kama vile alivyowatenda Sihoni na Ogu, wafalme wa Waamori, na nchi yao, ambao aliwaharibu.  Naye Bwana atawatia mikononi mwenu, nanyi mtawatenda kadiri ya amri ile niliyowaamuru. Iweni hodari na moyo wa ushujaa, msiogope wala msiwahofu; kwa maana Bwana, Mungu wako, yeye ndiye anayekwenda pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha.”



Utangulizi.

Hivi karibuni sasa tunaelekea ukingoni au mwishoni kabisa mwa mwaka 2017, kila mara unapofika wakati kama huu unakuwa ni wakati wa wanafunzi kukabiliwa na mitihani yao ya mwisho, mitihani hii ni moja wapo ya changamoto kwa wanafunzi wote, kwa kidato cha pilina cha nne watakuwa na mitihani yao ya mwisho, hali kadhalika na mitihani ya kitaifa, na madarasa mengine watakuwa na mitihani ya aina mbalimbali ya mwisho kwaajili ya kuwapima ili wavukekuingia darasa lingine, katika wakati kama huu wanafunzi wengi hata wale wenye uwezo huanza kuinhgia hofu kwa vile hawajui mtihani utaamua nini katika maisha yao.

Wakati huu ni wakati wa muhimu sana kwao na kwetu pia sisi walimu na shule kwa ujumla hivyo katika majira kama haya ni muhimu kila mmoja akiutafuta uso wa Mungu na kujisomea kwa bidii sana lakini hali kadhalika kuwa na neno la ushindi litakaloongoza maisha yetu wakati huu unapokaribia.

Kumbukumbu 31:3-6 Mungu anataka kututia moyo kupitia torati ya Musa kwa wana wa Israel, kuna maswala kadhaa ambayo Musa alikuwa akiwaambia Israel kama siri ya ushindi wao

1.      Bwana Mungu wako ndiye atakayevuka mbele yako, 

Kuna uwezekano wa kuwa umesoma kwa bidii, umekuwa na ratiba yako ya kujisomea na umetumia akili yako yote na hekima yako yote kujiandaa ilivyo jambo hjilo ni jema lakini inawezekana pamoja na maandalizi hayo ukawa unaogopa Biblia inatupa njia ya ushindi kwamba ni lazima tumuombe Mungu aweze kwenda pamoja nasi na kututangulia Kutoka 33:14-15 “Akasema, Uso wangu utakwenda pamoja nawe, nami nitakupa raha. Naye akamwambia, Uso wako usipokwenda pamoja nami, usituchukue kutoka hapa.” Musa alimweleza Mungu kuwa hawezi kwenda bila uso wa Mungu neno uso wa Mungu maana yake ni uwepo wa Mungu maana yake ni Kumpa Roho wa Mungu nafasi ya kukuongoza katika masomo yako na maandalizi ya mitihani yako Yohana 16:13 “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.”

2.      Iweni hodari na moyo wa ushujaa, msiogope wala msiwahofu,

Neno la Mungu hapa linatutaka tusiogope linatutaka tuendelee kuwa na imani na kuweka hofu mbali Israel waliahidiwa inchi ya kanaani ambayo ndani yake ilikuwa ikikaliwa na majitu hodari, lakini Israel walipaswa kutokuwaogopa na kuwakabili na kuwashinda, wanafunzi mnaokabiliwa na mitihani, huu ni wakatoi muhimu sana kwenu, mitihani Inasimama kama majitu inasimama kama tishio la kufanikiwa katika masomo yako, Lakini unapaswa kuishinda na kufanikiwa kabisa kwaajili ya Maendeleo yako mbeleni 

Joshua 1:5-9 “Hapatakuwa mtu ye yote atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako; kama nilivyokuwa pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe; sitakupungukia wala sitakuacha. Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa. Uwe hodari tu na ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na sheria yote aliyokuamuru Musa mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kuume, au wa kushoto, upate kufanikiwa sana kila uendako.Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana. Je! Si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako.” 

3.      Tamka Neno la Mungu.

Tamka neno la Mungu kwa kuliamini na kwa ujasiri Yohana 6:63Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima” kumbuka kuwa hofu ni roho hivyo ili kuishinda unapaswa kuwa na ujasiri na hivyo ni muhimu kwako kuliangalia neno na kulitamka hata ndani ya moyo wako kwa ujasiri  Matendo 4:29 “Basi sasa, Bwana, yaangalie matisho yao; ukawajalie watumwa wako kunena neno lako kwa ujasiri wote,”

4.      Uwe na Moyo wa Ushujaa (Imani).

Tendo lolote lile lisilotokana na imani ni dhambi, Warumi 14:23 “Lakini aliye na shaka, kama akila, amehukumiwa kuwa ana hatia, kwa maana hakula kwa imani. Na kila tendo lisilotoka katika imani ni dhambimara tunaporuhusu mashaka katika maisha yetu ndipo ytunapoanza kuzama Mathayo 14:30-31 “Lakini alipouona upepo, akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe, akisema, Bwana, niokoe. Mara Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka?” Ni muhimu kwetu tukimuamini Mungu kwa yasiyowezekana, Luka 1:37 “kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu.” 

Kila mwanafunzi anayetarajia kufanya Mitihani hivi karibuni tafadhali omba Maombi haya pamoja na Mkuuwa wajenzi.

Mungu wa Rehema ni wewe utakayevuka mbele yangu katika nyakati hizi za mitihani, ni wewe utakayetengeneza future yangu kupitia ushindi wakati wa mitihani yangu nya mwisho na mitihani ya kitaifa najiweka katika mikono yako nikikutegemea wewe, niweke mbali na hofu zote maana wewe hukutupa roho ya woga, Nisaidie kwa Roho wako Mtakatifu na uwepo wako ukawe pamoja name katika mitihani yangu sawasawa na Mapenzi yako Katika jina la Yesu amen!  

Nakutabiria ushindi, nakutabiria mafanikio makubwa katika mitihani yako, natabiri ufaulu wa kupita kawaida katika mitihani yako ya mwaka huu katika jina la Yesu amen!

Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Rev. Innocent Kamote.

Ijumaa, 13 Oktoba 2017

Jua lisichwe !



“Do not let The sun go down”
Waefeso 4:26Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka;”


Utangulizi.

Maisha ya mwanadamu ni mafupi sana na yamejawa na taabu na changamoto za aina mbalimbali  na yanapita upesi sana Zaburi 90:10Siku za miaka yetu ni miaka sabini, Na ikiwa tuna nguvu miaka themanini; Na kiburi chake ni taabu na ubatili, Maana chapita upesi tukatokomea mara.” Biblia inaonyesha kuwa siku za mwanadamu kuishi ni chache na zinapita haraka lakini pia zimejaa taabu unaweza pia kuona katika Ayubu 14:1-2Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke Siku zake za kuishi si nyingi, naye hujaa taabu. Yeye huchanua kama vile ua, kisha hukatwa; Hukimbia kama kivuli, wala hakai kamwe

Kutokana na hali hiyo Maandiko yanatutaka kila mmoja wetu kujifunza jinsi ya kuishi kwa furaha na kuacha kufadhaika kabisa Wafilipi 4:4-7. Furahini katika Bwana sikuzote; tena nasema, Furahini. Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yu karibu. Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.”

Ni jinsi gani tunaweza kuishi maisha ya furaha na amani, jinsi gani tunaweza kuwa mbali na masumbufu ya ulimwengu huu maisha ni mafupi sawa lakini kama mtutaishi kwa huzuni na kukosa amani yatakuwa mabaya zaidi, ni lazima tukubali kujifunza kuishi kwa furaha na amani na kutokuweka Uchungu moyoni Biblia inapotuamuru kufurahi na kuachilia mamnbo kwa haraka kabla ya kwenda kulala au kabla jua halijachwa inajua kuwa uwezo huo uko katika maamuzi yetu, tunaweza kuamua kuwa wenye furaha na tunaweza kuamua kuwa wenye huzuni ni vema kuamua kuwa wenye furaha muda wote na kutokuogopa.

Mfano

Profesa mmoja wa saikolojia alikuwa akitembea mbele ya jukwaa akiwafundishwa watu jinsi ya kuwa mbali na stresses na migandamizo ya maisha, ukumbi ulikuwa umejaa wanafunzi wengi sana , aliposimama aliagiza glasi ya maji ya kunywa ambayo ilikuwa na maji nusu, pia aliagiza nyingne iliyokuwa imejaa na akazishika mikononi mwake , wanafunzi wote walikodoa macho wakimuangalia kwa mshangao

Profesa aliuliza swali je hizi glasi nilizoshika zina uzito kiasi gani, wanafunzi waliinua sauti zao na kujibu huyu hivi na huyi hivi huku wakitaja uzito wa aina mbalimbali

Kisha profesa yule alijibuna kuwaambia kwa mtazamo wangu kwa hakika kabisa uzito wa glasi hizi hauna maana yoyote “Haujalishi” lakini jambo kubwa la maana ni muda ninaotumia kuzishika glasi hizi, endapo nitazishika kwa muda mfupi mikono yangu haitaumia, lakini kama nitazishika kwa muda mrefu sana mikono yangu itaumia na hatimaye nitachoka na mwisho nitalazimika kuzivunja glasi hizi, kwa sababu hiyo uzito wa glasi hapa hauna maana lakini muda ninaoutumia kuzishika ndio utakaonifanya nione uzito wa glasi hizi

Wanafunzi walishangaa sana na walikubaliana na mafundisho yake , ndipo alipowaambia unapokuwa na migandamizo na unapoendelea kuwa na hofu katika maisha yako ndivyo unavyoendelea kujiumiza moyo wako, unapofikiri chanhgamoto unazazipitia kwa muda kisha ukaziondoa moyoni hakuna kitakachotokea lakini ukifikiri kwa undani sana utashindwa kuendelea na hatimaye madhara yatatokea

Ni kwaajili ya swala kama hili Biblia inatukumbusha kuondoa uchungu mioyni mwetu kabla jua halijachwa, Mungu hapendi tutale na uchungu na hofu, haijalishi nini kinatutokea mchana, ikifikia jioni yatupe yote yaliyokuwa yanakusumbua , usiyabebe usiku nkucha na kuamka nayo,  kama utaamka nayo basi kumbuka ni wakati wa kuweka Glassi chini

Biblia pia inatushauri Kuomba na kumsihi Mungu atupe amani naye atatupa kamwe tusigope! Kuna Baraka kubwa sana katika kuwasamehe wengine na kuondoa kila kitu mioyoni mwetu Mathayo 6:14-15Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao na Baba wenu wa mbinguni atawasamehe ninyi bali msipowasamehe watu makosa yao wala Baba yenu hatawasamehe makosa yenu”.

Na Rev. Innocent Kamote.

Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima!.