Mstari wa
Msingi: Yoshua 1:5-8 “Hapatakuwa mtu ye yote
atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako; kama nilivyokuwa
pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe; sitakupungukia wala
sitakuacha. Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu
hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa. Uwe hodari tu na
ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na sheria yote aliyokuamuru Musa
mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kuume, au wa kushoto, upate
kufanikiwa sana kila uendako. Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako,
bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa
na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako,
kisha ndipo utakapositawi sana. Je! Si
mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike;
kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako”.
Jumatatu ijayo kidato cha sita kote Nchini wanatarajia kuanza mitihani yao
ya kumaliza Elimu ya juu ya sekondari, nafahamu sana katika wakati huu wengi
watakuwa wana hofu kwamba mambo yatakuwaje japo kweli wengi wamejiandaa vizuri
na hawana wasowasi kabisa kukabiliana na mtihani huo, lakini hata hivyo Mungu
alinipa neno hili maalumu kwaajili yao kwamba “Naye Bwana, yeye ndiye
atakayekutangulia, atakuwa pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha; usiogope wala usifadhaike.” Kumbukumbu
la Torati 31:8
Ni muhimu
kufahamu kuwa katika maisha wakati mwingine tutakabiliana na changamoto za aina
mbalimbali, ziko changamoto nyingi lakini mojawapo ya changamoto kubwa ni pale
unapodhani kuwa uko peke yako au unakabiliana na muda ambao utabaki mwenyewe na
wakati huo utapaswa kutatua changamoto zinazokukabili ukiwa peke yako, Bila mtu
aliyekuwa anakupa msaada wa karibu, Mungu alifanya kazi na Musa kwa kiwango
kikubwa na cha ajabu, Mungu pia alifanya kazi na Yesu Kristo kwa uweza mkubwa na
waajabu, Musa alipokuwa ameondoka Yoshua alibaki mwenyewe na hivyo alikuwa na
mashaka makubwa kuwa itakuwaje endapo atakabiliwa na changamoto nzito zilizoko
mbele yake, sio hivyo tu hata wakati Yesu anaondoka wanafunzi wake walikuwa na
wasiwasi mkubwa sana kwamba itakuwaje Jibu sahihi katika wakati huu lilikuwa ni
kuwahakikishia kuwa nitakuwa pamoja nanyi, Mungu alimuhakikishia Yoshua kuwa
atakuwa pamoja naye hatampungukia wala hatamuacha
Ni rahisi
kwetu wanadamu tunapopita katika changamoto ngumu huku tukifikiri kuwa hakuna
msaada ni rahisi kwetu kupiga kelele za kibinadamu kama zile alizopiga Yesu
Kristo pale msalabani baada ya mateso mazito “Mungu wangu mungu wangu mbona
umeniacha?” Mungu katika neno lake ameahidi mara kadhaa kwani anatujua vema
umbo letu anajua udhaifu wetu na ameahidi kuwa hatatuacha kamwe, ushindi wetu
katika maisha yetu unaanza na ujasiri huu kwamba Mungu yuko Pamoja nasi,
Hatatuacha wala hatatupungukia.
Tunapokaribia
kuingia katika vyumba vya mitihani wiki ijayo, ni kweli kuwa tutakaa wenyewe
mbali na wenzetu mbali na walimu, tutakuwa tukikabiliana na maswali
yaliyotungwa na watu tusiowajua sisi, wasio walimu wetu sisi na hivyo ni rahisi
kuogopa mtihani kwa sababu tu umepewa jina la mtihani wa kitaifa, lakini hata
ujapokuwa peke yako katika chumba chako cha mtihani kumbuka kuwa Bwana
anatangulia mbele yako hatakuacha kabisa wala kukupungukia kabisa. Hakuna mtu
alipewa wajibu wa kufanya na Mungu kisha Mungu asiwe pamoja nae, mmepewa wajibu
wa kusoma kwa sasa na hilo ndio kusudi la Mungu kwaajili yenu katika kusudi
hilo Bwana atakuwa pamoja nanyi, MSIOGOPE.
Mathayo 28:18-20 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka
yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa
wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na
kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; NA TAZAMA, MIMI NIPO PAMOJA
NANYI SIKU ZOTE, HATA UKAMILIFU WA DAHARI”
Hakuna
maneno ya muhimu kama haya wakati tunakabiliana na changamoto yoyote mbeleni
Mungu akikuambia kuwa yuko pamoja nawe tayari hii ni alama kubwa sana ya
ushindi, lakini akikuambia kuwa hatakuacha wala nhatakupungukia ni zaidi ya
ushindi, yeye atakuwa pamoja nawe ahadi hii imerejewa mara kadhaa katika
maandiko kwa kusudi la kutuondolea woga na kutupa ujasiri na moyo wa kujiamini,
kwamba atakuwa pamoja nasi, katikwa wakati wa msahaka na wasoiwasi kumbuka
atakuwa pamoja nasi kwa uwepo mkubwa sana.
Mungu
alimwambia Yakobo katika Mwanzo 28:11-17 “Akafika
mahali fulani akakaa huko usiku kucha, maana jua lilikuwa limekuchwa; akatwaa
jiwe moja la mahali pale akaliweka chini ya kichwa chake, akalala usingizi pale
pale. Akaota ndoto; na tazama, ngazi imesimamishwa juu ya nchi, na ncha yake
yafika mbinguni. Tena, tazama, malaika wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake.
Na tazama, BWANA amesimama juu yake, akasema, Mimi ni BWANA, Mungu wa Ibrahimu
baba yako, na Mungu wa Isaka; nchi hii uilalayo nitakupa wewe na uzao wako. Na
uzao wako utakuwa kama mavumbi ya nchi, nawe utaenea upande wa magharibi, na
mashariki, na kaskazini, na kusini; na katika wewe, na katika uzao wako, jamaa
zote za dunia watabarikiwa. NA TAZAMA, MIMI NIPO PAMOJA NAWE, nitakulinda kila
uendako, nami nitakuleta tena mpaka nchi hii, kwa maana sitakuacha, hata
nitakapokufanyia hayo niliyokuambia. Yakobo akaamka katika usingizi wake,
akasema, Kweli BWANA yupo mahali hapa, wala mimi sikujua. Naye akaogopa
akasema, Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka, hapa ni nyumba ya Mungu,
napo ndipo lango la mbinguni.”
Mungu
anataka tuwe na ujuzi huu, kwamba yuko pamoja nasi, ujuzi wa aina hii ukiwa
wazi mbele yetu hatutaogopa, tutakuwa na ujasiri, kwamba hata iweje yuko Mungu
ambaye ni Mchungaji mwema na hivyo hatutapungukiwa na kitu, kwa vyovyote vile
hatatupungukia wala hatakuacha hata tujapopita katika uvuli wa mauti
Daudi
alipoifahamu siri hii hakuogopa alimtegemea Mungu na alijua wazi kuwa Mungu ni
Mchungaji wake na kwamba hatapungukiwa, wala hataogopa mabaya au vitisho kwa
maana yeye yupo pamoja naye, Hofu ni adui mkubwa wa mafanikio yetu, wanafunzi
wengi wenye akili na uwezo wanaweza kufanya vema siku zote lakini wanaweza
kuharibu wakati wa mitihani kwa sababu shetani huwatia hofu huwaogopesha lakini
leo Bwana amenituma nikuamnbie kuwa usiogope Bwana yu pamoja nawe
Zaburi 23: 1-6 “Bwana ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu. Katika
malisho ya majani mabichi hunilaza, Kando ya maji ya utulivu huniongoza.
Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza Katika njia za haki kwa ajili ya jina
lake. Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa
maana WEWE UPO PAMOJA NAMI, Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. Waandaa meza
mbele yangu, Machoni pa watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, Na
kikombe changu kinafurika. Hakika wema
na fadhili zitanifuata Siku zote za maisha yangu; Nami nitakaa nyumbani mwa
Bwana milele.”
Yoshua alichoambiwa na Mungu ni kuliamini neno lake
tu, kwamba alisome, alitafakari na kulitii na kulifuata na kuwa akifanya hivyo
haitakuja itokee amepungukiwa na kitu, Hutapungukiwa na kitu Yesu akikutuma,
hii ni ahadi katika neno lake anapokuagiza Yesu hata kama huna kitu mfukoni
hutapungukiwa
Luka
22:35 “Akawauliza, Je! Hapo nilipowatuma hamna
mfuko, wala mkoba, wala viatu, mlipungukiwa na kitu? Wakasema, La!”
Waebrania 13:5-6 “Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo
navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha
kabisa. Hata twathubutu kusema, Bwana ndiye anisaidiaye, sitaogopa; Mwanadamu
atanitenda nini?”
Jambo
kubwa na la msingi ni kuamini neno lake, na kulitendea kazi, na ndio maana,
Mungu alimwambia Yoshua aliangalie neno la kulitafakari na kulishika
atafanikiwa katika kila alifanyalo na kila aendako na kuwa hakuna kiti au mtu
atakayeweza kusimamam mbele yake siku zote za maisha yake, Hitler Dikteta
mkubwa sana alikuwa ni mtu asiye na hofu askari wake pia hawakuogopa walikuwa
watii mno kwa neno la Hitler kwa kiwango cha kufa lakini Hitler anasema alikuwa
anaogopa mitihani, sisis hatupaswi kuogopa kwa sababu Mungu ameahidi kwamaba
atakuwa pamoja nasi, hii ni ahadi yake kwetu, na ni neno lake kwetu tuamini tu
na utaona mafanikio makubwa katika mitihani itakayoanza jumatatu ijayo ya
tarehe 6/05/2019 Bwana hatakupungukia wala hatakuacha amini tu neno lake.
Mathayo 7:24-27 “Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya,
atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; mvua
ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa
maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba. Na kila asikiaye hayo maneno yangu
asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya
mchanga; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile,
ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa.”
Sisi ni
warithi wa Baraka zake Ibrahimu, Ibrahimu baba yetu wa imani alikuwa rafiki wa
Mungu, Ibrahimu hakuishi maisha ya hofu Mungu alimtokea na kumwambia wazi kuwa
yeye ni thawabu yake kubwa sana na Ngao yake
Mwanzo 15:1 “Baada ya mambo hayo neno la BWANA likamjia Abramu katika njozi, likinena,
Usiogope, Abramu, Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana.”
Baba
katika jina la Yesu nawasogeza kidato cha sita nchi nzima nawaombea mtihani
mwema, naamini neno lako litawafikia hata kama wengine wako shule za Bweni na
hawajui Mungu amesema nao nini lakini mimi mtumwa wako kwa nenolako ulilonipa
nawaombea wote uwe pamoja nao kama ulivyoahidi, katika neno lako, uwasaidie wote
wanaokutegemea wewe Bwana nakuomba usiwaangushe ukawafanikishe na uwepo wako
ukawe pamoja nao katika vyumba vyao vya mitihani kwaajili ya utukufu wako,
asiwepo awaye yote wa kuwatisha wala kuwaingizia hofu, nawakinga kwa jina lako
kutoka katika mashambulizi yote ya yule muovu nakusihi ukawe pamoja nao, Katika
jina la Yesu Kristo wa Nazareth aliye hai, Amen!
Na. Rev Innocent Kamote.
Mkuu wa wajenzi mwenye hekima.