Jumamosi, 11 Mei 2019

Aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia.

1Yohana 4:4Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na Mungu nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia.”


Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa sasa tunaishi katika nyakati za mwisho zaidi, kuliko tunavyoweza kufikiri, mwisho wa mambo yote umekaribia, kila kilichokuwa kimeahidiwa katika maandiko kimetimia na kinaendelea kutimia kwa kasi kubwa sana, Petro anasema mwisho wa mambo yote umekaribia 1Petro 4:7Lakini mwisho wa mambo yote umekaribia; basi, iweni na akili, mkeshe katika sala.Sio tu kukesha katika sala kunakoweza kutusaidia lakini hatuna budi kuwa na ufahamu mkubwa sana wa kujifunza na kulijua neno la Mungu ili tusiwe miongoni mwa watu wanaopotea, Katika nyakati hizi za mwisho shetani atafanya kazi kubwa sana kutupinga au kulipinga kanisa kwa nguvu zake zote alitumia manabii wa uongo na mafundisho potofu hizi ndio silaha zake kuu alizozitumia nyakati za kanisa la kwanza kulishambulia kanisa, hata hivyo nyakati za kanisa la kwanza mitume waliwasaidia wakristo kulijua neno na kuwatia moyo kusimama imara katika Bwana na wakafanikiwa sana.

·         Ninyi watoto wadogo mwatokana na Mungu
·         Nanyi mmewashinda
·         Yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia

Ninyi watoto wadogo mwatokana na Mungu.


Haya yalikuwa maneno ya faraja kuu kwa wanafunzi wa Yesu nyakati za Kanisa la Kwanza, Yohana anatumia maneno haya kuwatoa hofu na kuwafariji wanafunzi wa nyakati za kanisa la kwanza kwa sababu walikuwa wanakabiliwa na masambulizi ya shetani kwa njia ya Mateso, Mafundisho potofu na manabii wa uongo, hili lilikuwa jambo lenye kulitishia kanisa, wanafunzi wachanga wa kiroho walikuwa na hofu kubwa sana kuhusu mafundiho potofu pia uvumi kuhusu roho ya Mpinga Kristo, kutokana na hofu hiyo  Yohana aliwaambia kuwa wasiwe na hofu kwa sababu wao wanatokana na Mungu, 1Yohana 4:1-4 1 Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani. 2. Katika hili mwamjua Roho wa Mungu; kila roho ikiriyo kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili yatokana na Mungu. 3. Na kila roho isiyomkiri Yesu haitokani na Mungu. Na hii ndiyo roho ya mpinga Kristo ambayo mmesikia kwamba yaja; na sasa imekwisha kuwako duniani. 4. Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na Mungu nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia.” 

Kwa vile wanafunzi wachanga nyakati za kanisa la kwanza walikuwa na hofu kuhusu manabii wa uongo, mafundishi ya uongo na roho ya mpinga Kristo kwa ujumla walikuwa na hofu na kazi hizi za shetani kinyume na Kanisa yaani watu wa Mungu Yohana alikuwa anataka kuwakumbusha kuwa wao hawakuzaliwa kwa mapenzi ya damu na nyama wao ni uzao unaotoka na Mapenzi ya Mungu, wao wako tofauti na wale wa upande wa ibilisi kwa hiyo hawapaswi kuogopa, Maandiko yanaonyesha wazi kuwa ni vigumu sana kushindana na kile ambacho kimeatokana na Mungu au kimeanzishwa na Mungu, Kanisa ni mali ya Mungu, Israel ni mali ya Mungu na Biblia ni neno lake, kweli ni ya Mungu na watu wake hakuna uongo unaweza kulifanya kanisa likashindwa, kwa sababu limeanzishwa na Mungu mwenyewe,

Matendo ya Mitume 5:34-3934. Lakini mtu mmoja, Farisayo, jina lake Gamalieli, mwalimu wa torati, mwenye kuheshimiwa na watu wote, akasimama katika baraza, akaamuru mitume wawekwe nje kitambo kidogo, 35. akawaambia, Enyi waume wa Israeli, jihadharini jinsi mtakavyowatenda watu hawa. 36. Kwa sababu kabla ya siku hizi aliondoka Theuda, akijidai ya kuwa yeye ni mtu mkuu, watu wapata mia nne wakashikamana naye; naye aliuawa na wote waliomsadiki wakatawanyika wakawa si kitu. 37. Baada ya mtu huyo aliondoka Yuda Mgalilaya, siku zile za kuandikiwa orodha, akawavuta watu kadha wa kadha nyuma yake, naye pia akapotea na wote waliomsadiki wakatawanyika. 38. Basi sasa nawaambia, Jiepusheni na watu hawa, waacheni; kwa kuwa shauri hili au kazi hii ikiwa imetoka kwa binadamu, itavunjwa, 39. lakini ikiwa imetoka kwa Mungu hamwezi kuivunja; msije mkaonekana kuwa mnapigana na Mungu.No one can defeat what has originated from God! At all !” Hakuna awaye yote anayeweza kushindana na kile ambacho kimeanzishwa na Mungu hata kidogo, Mtume analikumbusha kanisa kuwa wao wanatokana na Mungu, kamwe Mungu hajawahi na haitakuja itokee akaanzisha kitu dhaifu kitu kikiwa kimetoka kwa mwanadamu kitavunjwa lakini kikiwa kimetoka kwa Mungu hakuna awezaye kukivunja.

Kanisa linatokana na Mungu na hivyo kazi za kishetani na malango yote ya ibilisi hayataliweza wala kulishinda Mathayo 16: 17-1817. Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni. 18. Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.”

Yesu aliahidi kuwa atalijenga kanisa lake na kuwa malango ya kuzimu hatyatalishinda, Mateso na upinzani dhidi ya kila mtu wa Mungu kutoka kwa wale wasio wa Mungu hayawezi kufanikiwa katika maisha yetu, nguvu za giza, nguvu za kichawi na upinzani kutoka kwa waganga wa kienyeji na maajenti wote wa shetani wachawi na mafundishi ya uongo na manabii wa uongo na roho ya mpinga Kristo havuiwezi kufanikiwa dhidi ya kitu chochote ambacho chanzo chake ni Mungu,Kumbuka ninyi watoto, wadogo mwatokana na Mungu. Mungu ametupa neema ametupa Roho wake na ametupa uwezo wa kupambanua kamwe hatutaweza kudanganywa na yule muovu wala hatutashindwa maana tumetokana na Mungu.


Nanyi mmewashinda.


Biblia ya kilatini ijulikanayo kama Vulgate maneno haya Nanyi mmewashinda yanasomeka “…And have overcome him” na Biblia ya kiethiopia Ethiopic Version inasomeka “…And have overcome the evil one” Yohana mtume anaendelea kuonyesha uweza mkubwa sana wa wana wa Mungu, kuwa sio tu kule kutokana na Mungu kunatuwezesha kumshinda Mpinga Kristo na manabii wa uongo pamoja na mafundisho potofu na adui yetu shetani na maajenti wake wote, lakini pia sisi tumewashinda tayari, mara mtu anapokuwa Mkristo tayari kuna ushindi ndani yetu, tunaweza kabisa kupigana vita vilivyo vizuri vya imani, tunalo neno la Mungu ambalo ni upanga wa roho, Kila mkristo anazaliwa kiroho akiwa na ushindi tayari ndani yake 1Yohana 2:13 “Nawaandikia ninyi, akina baba, kwa sababu mmemjua yeye aliye tangu mwanzo. Nawaandikia ninyi, vijana, kwa sababu mmemshinda yule mwovu. Nimewaandikia ninyi, watoto, kwa sababu mmemjua Baba.Ziko nguvu ndani yako nguvu za ushindi na hakuna kinachoweza kushindana na wewe, kwa sababu ndani yako kuna ushindi, iko siri ya ushindi imefichwa ndani yako wewe ni mshindi na zaidi ya mshindi


Yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia.


Siri nyingine kuu ambayo Yohana anatupa ambayo ni kuuna inayotuthibitishia ushindi ni Yeye aliye ndani yetu Biblia ya Kiarabu Arabic version inasema wazi “The Spirit that is in you” ni wazi Roho Mtakatifu ndiye aliye ndani yetu yeye ana nguvu kuliko yeye aliye katika dunia, aliye katika dunia ni Ibilisi, pamoja na majeshi yake yote, Hatupaswi kuogopa upinzani wa aina yoyote ile, hatupaswi kuogopa nguvu za mpinga Kristo, wala manabii wa uongo, wala maajenti wa ibilisi, wala nguvu za giza, wala falme na mamlaka, wala majeshi ya pepo katika ulimwengu war oho kwa vile aliye ndani yetu ni mkuu kuliko aliye duniani aliye ndani yetu ni Mungu mwenyewe ni muhimu kufahamu kuwa mara mtu anapomkriri Yesu kuwa Bwana na mwokozi wake Mungu hukaa ndani yetu, huwezi kushindwa, kushindwa kwetu ni sawa na kushindwa kwa Mungu 1Yohana 4:15 “Kila akiriye ya kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu, Mungu hukaa ndani yake, naye ndani ya Mungu”. Mungu ni mwenye nguvu na uweza kuliko aina yoyote ya upinzani inayotenda kazi nje ya maisha yetu, Mungu aliye ndani yetu ana uwezo wa kutuokoa na kila aina ya hila zote za maadui zetu, Mungu hakuandaa mpango dhaifu kwamba awe na watu ambao watakuwa ni wenye kushindwa, kudanganywa na kumpa adui utukufu hata kidogo, sisitunatokana na Mungu na mungu ameweka ushindi ndani yetu nay eye anaishi ndani yetu hivyo kila tunapotembea tunaye Mungu, ushindi wetu upo kama Mungu yuko pamoja nasi, hata kama tutashambuliwa Mungu yuko pamoja nasi na ushindi kwetu ni dhahiri.  

Zaburi 124:1-8Kama si Bwana aliyekuwa pamoja nasi, Israeli na aseme sasa, Kama si Bwana aliyekuwa pamoja nasi, Wanadamu walipotushambulia. Papo hapo wangalitumeza hai, Hasira yao ilipowaka juu yetu Papo hapo maji yangalitugharikisha, Mto ungalipita juu ya roho zetu; Papo hapo yangalipita juu ya nafsi zetu Maji yafurikayo. Na ahimidiwe Bwana; Asiyetutoa kuwa mawindo kwa meno yao. Nafsi yetu imeokoka kama ndege Katika mtego wa wawindaji, Mtego umevunjika, nasi tumeokoka. Msaada wetu u katika jina la Bwana, Aliyezifanya mbingu na nchi. 

Msikilizaji wangu na msomaji wangu haijalishi ni vita ya aina gani inayokuzunguka, haijalishi ni nani anakupoinga na ana jina kiasi gani, haijalishi ni mchawi kiasi gani, haijalishi ni mtu wa namna gani, ana cheo gani, haijalishi wana akili kiasi gani, haijalishi wamejipanga kukushambulia kwa kiasi gani unachoatakiwa kufahamu ni kuwa Aliye ndani yetu ni mkuu kuliko aliye katika dunia, aliye ndani yetu ni mwenye nguvu kuliko nguvu zote, haijalishi Yohana alikuwa anataka kuhakikisha kuwa hakuna hofu ya aina yoyote inawatawala watu wa Mungu, nah ii sio kwaajili ya kufariji tu bali ni kwaajili kutuhakikishia uhalisia wa kweli kuu kabisa kuwa hatuna cha kuogopa kwa sababu.

1.       Tunatokana na Mungu
2.       Tunaushindi ndani yetu
3.       Aliye ndani yetu ni mkuu kuliko aliye katika dunia

Rev. Innocent Kamote.
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Jumamosi, 4 Mei 2019

Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu!

Mstari wa Msingi:- Matendo 5:29Petro na mitume wakajibu, wakisema, Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu.”


Mstari wa Somo:- Kutoka 1:15-21Kisha mfalme wa Misri akasema na wazalisha wa Waebrania, mmoja jina lake aliitwa Shifra, na wa pili jina lake aliitwa Pua;  akasema, Wakati mwazalishapo wanawake wa Kiebrania na kuwaona wa katika kuzaa, ikiwa ni mtoto mwanamume, basi mwueni, bali ikiwa ni mtoto mwanamke, na aishi. Lakini wale wazalisha walikuwa wakimcha Mungu, wasifanye kama walivyoamriwa na huyo mfalme wa Misri, lakini wakawahifadhi hai wale wanaume. Basi mfalme wa Misri akawaita wale wazalisha na kuwauliza, Kwa nini kufanya jambo hili, na kuwahifadhi watoto waume wawe hai? Wazalisha wakamwambia Farao, Ni kwa sababu hao wanawake wa Kiebrania si kama wanawake wa Kimisri; kwa kuwa ni hodari hao, nao huzaa kabla mzalisha hajapata kuwafikilia. Basi Mungu akawatendea mema wale wazalisha; na hao watu wakaongezeka sana, wakaendelea na kuzidi kuwa na nguvu nyingi. Ilikuwa kwa sababu wale wazalisha walikuwa wakimcha Mungu, akawasimamishia nyumba.”


Utangulizi:


Ni muhimu kufahamu kuwa wako watu ambao wametajwa katika maandiko kwa ufupi sana lakini wanatufundisha somo pana sana lenye kuweza kutufaa katika nyakati zetu, Miongoni mwa watu hao ni Shiphrah na Puah ambao wanatufundisha mambo ya msingi katika kumpendeza Mungu, Leo tutachukua muda kujifunza kuwa wao ni nani na mambo muhimu ya kujifunza kutoka kwao:-

Shiphra na Puah ni nani?

Tofauti na Mashujaa wengine katika maandiko Shiphra na Puah wanatajwa kwa kifupi sana katika maandiko katika kitabu cha Kutoka 1:15-21, Hawa walikuwa wanawake waliookoa maisha ya wengi kabla ya kuzaliwa kwa Musa huko Misri, wanawake hawa walikuwa ni wakunga, (Wauguzi wanaohusika na kuzalisha wanawake wajawazito)

Wanatheolojia wanapata utata mkubwa sana kugundua asili ya Shiphrah na Puah kwamba walikuwa Waebrania au walikuwa Wamisri, hii ni kwa sababu Biblia ya kiyahudi inawaita wazalisha wa kiibrania “Hebrew Midwives” kwa kiibrania “ Meyaldot Haiviyot  Meyaldot Haiviyot” Wataalamu wa maandiko wa kiyahudi akiwemo Rabbi Abrabanel  ameweka wazi katika mawazo yake kuwa wanawake hao walikuwa wamisri isipokuwa waliokuwa wanamcha Mungu, kama wangekuwa waebrania neno Mcha Mungu lisingeliweza kutumika hapo, lakini neno hilo ndilo linalosaidia kujua kuwa wanawake hao walikuwa wamisri, kwa vile neno wacha Mungu mara nyingi lilitumika katika biblia kumaanisha mataifa waliomuamini au waliomcha Mungu wa waebrania, sasa swali linaweza kuja kwa nini waliitwa wazalisha wa kiibrania lugha hii inaweza kuwa na maana ya “Wakunga waliokuwa wakiwazalisha waebrania” na kwa sababu hiyo haikuwa na ulazima sana wao wenyewe wawe waebrania Kama hivyo ndivyo basi, Shiphra na Puah wanakuwa watu wa kwanza wasiokuwa waenrabia kuhatarisha maisha yao kwaajili ya Wayahudi. Msomi mmoja wa kiyahudi ambaye ni mwalimu mwenye kuheshimika sana ajulikanaye kama Nechama Leibowitaz  anasema kama wanawake hao walikuwa wamisri hapo ndipo somo hili linapokuwa tamu na kupata maana iliyo njema zaidi, na somo kuu tunajifunza kuwa mtu yeyote yule wa taifa lolote lile na jamii yeyote ile anaweza kusimama katika kweli linapokuja sala la kusimamia haki, bila kujali kuwa anatoka katika historia gani.


Ni wanawake waliompendeza Mungu.


Wanawake hawa mashujaa waliagizwa kwa amri ya mfalme katika Kutoka 1:15-17 “Kisha mfalme wa Misri akasema na wazalisha wa Waebrania, mmoja jina lake aliitwa Shifra, na wa pili jina lake aliitwa Pua; akasema, Wakati mwazalishapo wanawake wa Kiebrania na kuwaona wa katika kuzaa, ikiwa ni mtoto mwanamume, basi mwueni, bali ikiwa ni mtoto mwanamke, na aishi. Lakini wale wazalisha walikuwa wakimcha Mungu, wasifanye kama walivyoamriwa na huyo mfalme wa Misri, lakini wakawahifadhi hai wale wanaume.Unaona Maandiko yanasema wanawake wale walikuwa wacha Mungu na hivyo hawakufanya kama ilivyokuwa amri ya mfalme, wao kwa imani waliamua kumtii Mungu kuliko kuwatii wanadamu waliwatunza wayahudi bila kujalia amri ya mfalme jambo hili lilihatarisha sana maisha yao, zamani ilikuwa usipotii amri ya mfalme ilikuwa lazima uuawe, lakini wanwake hawa walisimama katika kweli walisimama katika haki na Mungu aliwatetea, Ziko nyakati katika maisha yetu ambazo tunatakiwa kuwa na msimamo thabiti kwamba heri ya lawama kuliko fedhea kuwa tayari kuhatarisha maisha yetu kwaajili ya utii wetu kwa Mungu, hili ni somo ambalo wanawake hao wanatufunza leo, walikuwa na ujasiri, hawakuogopa, walifanya yaliyo wajibu wao, sawa na Petro alivyojibu wakati baraza la wazee wa kiyahudi wakiwapiga marufuku wasihubiri injili, Petro alijibu kwa ujasiri “Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu

Somo kutoka kwa Shiphra na Puah


1.       Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu – wanawake hao walihatarisha maisha yao kwaajili ya kuikiuka amri ya mfalme kwa kweli walipaswa kukatwa shingo, lakini walikuwa tayari kupoteza kila kitu kwa sababu WALIKUWA WANAMCHA MUNGU tunajifunza kuwa kama tunamcha Mungu kama tunamuogopa Mungu tunaweza kusimama na kupingana na dhuluma na udhalilishaji wa aina yoyote ile bila kujali nini kitatukuta ila kwa sababu kubwa moja tu tunamcha Mungu.


2.       Walitamini umuhimu wa uhai na maisha - Bila kujali kuwa wanaozalishwa ni wamisri au wayahudi wanawake hawa walionyesha kuwa wanathamini uhai na kuwa wako tayari kutoa uhai kwaajili ya uhai, hawakuogopa waliwahurumia watoto hao wachanga walioma huruma jinsi ambavyo mama amebeba mimba miezi tisa na sasa anataka kuunganishwa na mwanaye na kitoto kipya kinakuja ulimwenguni bado hakujaunganishwa na mama yake, bila kujali ni wa aina gani ni wakabila gani uhai wa mwanadamu una thamani kuwa sana, wao walijua kuwa wameapa kuokoa uhai wa mwanadamu na hivyo walikuwa wana haki ya kuhakikisha kuwa wanafanya hivyo bila kujali nani ameagiza vitoto visivyo na hatia viuawe, siku nhizi watu hawathamini uhai unaweza kusikia watu wakiwaxchinja wake zao, au kuua vitoto na kuwachoma moto wezi kabla hata ya kuwafikisha katika vyombo vya kisheria kuua limekuwa jambo la kawaida tu Mithali 31:8-9 inasema “Fumbua kinywa chako kwa ajili yake aliye bubu; Uwatetee watu wote walioachwa peke yao; Fumbua kinywa chako, uhukumu kwa haki; Uwapatie maskini na wahitaji haki yao” Neno la Mungu linatutaka tuseme kwa aajili ya wale wasiosema, tuwatetee wasioweza kujitetea, tusimame katika haki na kuhakikisha kuwa masikini wanapata haki zao, Hii ndio kazi iliyofanywa na Shiphrah na Puah, walisimama kwa niaba ya wanyonge na masikini vitoto visivyoweza kujitetea, watu wengine kwa kuwa Mungu amekuweka katika mikono yake basi ndio utaipata fresh. 


3.       Mungu anaona Mawazo yetu na Matendo yetu – Hwa wanawake wakunga walikataa kutii amri ya mfalme wao muovu, na kutokukubalia kuuwa watoto wasio na hatia na Mungu aliona na kuwabariki, Sio tu kuwa mungu aliona matendo yao hapa lakini pia aliisoma nia yao namawazo yao, Zaburi 139:1-4 “Ee Bwana, umenichunguza na kunijua. Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu; Umelifahamu wazo langu tokea mbali. Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu, Umeelewa na njia zangu zote.  Maana hamna neno ulimini mwangu Usilolijua kabisa, Bwana.” Kumbe Mungu anaona na anayajua mawazo yetu anatufahamu kwa undani zaidi hakuna cha kujificha katika mawazo yetu wala katika ulimi wetu, hivyo ni muhimu katika maisha yetu kuishi maisha ya kupendeza yeye popote tulipo na kisimama upande wake hata kama lile tunalolisimamia litahatarisha maisha yetu, hatuna budi kuisimiamia kwaajili ya Mungu.


4.       Lazima tusimame na Israel. – Shiphra na Puah hawakuwa Wayahudi, lakini waliwahudumia waliwalinda na kutokana na matendo yao mema Mungu aliwabariki aliwasimamishia nyumba , walipate neema waliolewa, walikuwa na familia nzuri. Walibarikiwa, Bilia ina ahadi nyingi kuhusu kusimama na Israel, Bila kujali wewe ni mtu wa namna gani, ni wa asili ipi ni wa imani ipi linapokuja swala la mtu anataka kuiharibu Israel simama na Israel simama na watu wa Mungu, hata siku moja usithubutu kuwashutumu na kuwazomea na kuwalaani


Mwanzo 12: 1-3 “BWANA akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha; nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka; nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa.”

Isaya 62:1 “Kwa ajili ya Sayuni sitanyamaza, na kwa ajili ya Yerusalemu sitatulia, hata haki yake itakapotokea kama mwangaza, na wokovu wake kama taa iwakayo.”

Isaya 62:6-7 “Nimeweka walinzi juu ya kuta zako, Ee Yerusalemu; hawatanyamaza mchana wala usiku; ninyi wenye kumkumbusha Bwana, msiwe na kimya;  wala msimwache akae kimya, mpaka atakapoufanya imara Yerusalemu, na kuufanya kuwa sifa duniani.”

Zaburi 122:6 “Utakieni Yerusalemu amani; Na wafanikiwe wakupendao;

Warumi 15:27 “Naam, imewapendeza, tena wamekuwa wadeni wao. Kwa maana ikiwa Mataifa wameyashiriki mambo yao ya roho, imewabidi kuwahudumu kwa mambo yao ya mwili.

Shiphrah na Puah walisimam na wayahudi na wakabarikiwa, kila taifa linapaswa kuwa na uelewa na kujifunza na kufahamu kuwa mataifa mengi yaliyobarikiwa na Mungu na watu wengi waliofanikiwa sana ni wale wanaosimama na Israel, viongozi wa taifa letu ni lazima wahakikishe kuwa linapokuja swala la Israel kama huna cha kusema ni afadhali kunyamaza kimya, kuna uhusiano mkubwa wa Baraka za watu wote Duniani na mataifa yote Duniani kubarikiwa kutokana na msimamo wako katika Israel, Marekani na mataifa mengine makubwa yanaifahamu siri hii na ndio maana unawaona kama wanaojipendekeza kwa wayahudi, Kupitia wanawake wale wakunga waliosiamama na Waisrael nataka kumuonya kila mtu kuhakikisha kuwa katika maisha yake ili kuzivuta Baraka waza mema na watakie heri Israel waombee amani, fanya amani nao na utaona Baraka alizoahidiwa Ibrahimu zikimiminika katika maisha yako Shipra na pua walifanya hivyo walisimama na Israel licha ya kuwa wao hawakuwa waebrania.

I stand with Israel forever
Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Jumatatu, 29 Aprili 2019

Imekwisha !



Yohana 19:28-30Baada ya hayo Yesu, hali akijua ya kuwa yote yamekwisha kumalizika ili andiko litimizwe, akasema, Naona kiu. Kulikuwako huko chombo kimejaa siki; basi wakatia sifongo iliyojaa siki juu ya ufito wa hisopo, wakampelekea kinywani.  Basi Yesu alipokwisha kuipokea ile siki, alisema, IMEKWISHA. Akainama kichwa, akaisalimu roho yake.


Utangulizi:
Mojawapo kati ya usemi wenye maana sana kati ya semi saba za Yesu alizozisema akiwa msalabani na ambazo zinatajwa katika sehemu mbalimbali za injili, moja ya usemi huo wa muhimu ni usemi wa sita wenye Neno IMEKWISHA  ambalo leo katika siku ya pasaka tutachukua muda kulijadili kwa undani na kupata maana iliyokusudiwa, maneno mengine kati ya maneno saba aliyoyasema Yesu msalabani ni pamoja na:-
·         Baba uwasamehe kwa maana hawajui walitendalo Luka 23:34
·         Amin nakuambia leo hii utakuwa pamoja nani peponi Luka 23:43
·         Mama tazama mwanao, mwana tazama mama yako Yohana 19:26-27
·         Mungu wangu Mungu wangu mbona umeniacha Mathayo 27:46
·         Nina kiu Yohana 19:28
·         Imekwisha Yohana 19:30
·         Baba mikononi mwako naiweka roho yangu Luka 23:46
Maana ya neno IMEKWISHA
Ni muhimu kufahamu kuwa Neno IMEKWISHA ambalo katika kiingereza kiingereza linasomeka “IT IS FINISHED  katika Biblia ya kiyunani yaani Kigiriki linasomeka kama “TETELESTAI  Neno hili ndio neno la Mwisho kabisa katika maneno aliyoyatamka Yesu pale msalabani kabla ya kutamka neno “Baba mikononi mwako naiweka roho yangu” na kufariki dunia pale msalabani, Neno hili Imekwisha TETELESTAI limetokana na neno TELEO la kiyunani ambalo maana yake ni Kukamilisha kazi, kumaliza kazi, kutimiza kazi, to complete or to accomplish, neno hili lina umuhimu mkubwa kwa sababu linazungumzia kumaliza kazi kwa furaha, au kwa mafanikio, utamu wa neno hili ni kama vile mtu anapokuwa amemaliza mtihani wa mwisho katika kozi ya mwisho, au mtihani wa mwisho kabisa wa kumaliza shule au chuo au kama vile mtu aliyekamilisha malipo ya mwisho ya ununuzi wa nyumba au gari, (Paid in Full) au kukamilisha kwa usahihi kile ulichowaza au kufikiri kuwa utakifanya na ukakifanya kwa usahihi kabisa, Kama vile Mungu alivyosema tazama kila kitu kimekuwa chema, well done, kazi imefanyika kwa ufasaha.

Lakini ni muhimu kufahamu kuwa neno hili IMEKWISHA liko katika wakati uliopita kwa namna linavyoonekana hapa  lakini katika kiyunani ni sentensi kamili Perfect tense na kwa sababu hiyo neno hili linapata umuhimu mkubwa kwa sababu lina maanisha imekwisha katika wakati uliopita, uliopo na ujao kwa msingi huo neno hili linaendelea kufanya kazi kila siku na kila wakati, Neno hili pia lilimaanisha kuwa kama kulikuwa na deni, basi deni hilo limelipwa milele, wale wamuaminio Yesu hawana wanachodaiwa, kama ilikuwa ni kesi imefutwa na hati za mashitaka zimeharibiwa kabisa Wakolosai 2:14-15 akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani; akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo”.Neno hili ni kama kupewa ruhusa kutoka hospitalini baada ya kuugua kwa muda na kulazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi kila mtu akijua umekwisha kisha ukainuka tena ukiwa mzima wa afya. Ni neno muhimu sana katika kazi ya ukombozi wa mwanadamu na wokovu wetu.

Umuhimu wa neno IMEKWISHA.

Yesu alipolia kwa sauti kuu IMEKWISHA alimaanisha katika wakati uliopita, sasa na itaendelea kuwa imekwisha hata baadaye. Kumbuka kuwa hakusema nimekwisha hii ingemaanisha kuwa ameshindwa na kifo, lakini alilia akisema IMEKWISHA! maana yake nimeikamilisha kwa ufasaha kazi niliyokuja kuifanya. Kwa msingi huo neno imekwisha lina maana ya hakuna kilichosazwa katika kazi ya ukombozi aliyokuja kuifanya na hivyo alikuwa akizungumza ukweli kuwa kila kitu kimekamilishwa sasa ni mambo gani Yesu aliyakamilisha yako mengi mno lakini baadhi ni pamoja na:-
1.       Alikamilisha kazi yote aliyokuwa ametumwa na baba yake kuja kuifanya duniani Yohana 17:4 “Mimi nimekutukuza duniani, hali nimeimaliza kazi ile uliyonipa niifanye.

2.       Alikamilisha kazi ya kuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea Luka 19:10 “Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.”

3.       Alikamilisha kazi ya kutukomboa sisi na adui zetu Luka 1:68-74 “Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli, Kwa kuwa amewajia watu wake, na kuwakomboa. Ametusimamishia pembe ya wokovu Katika mlango wa Daudi, mtumishi wake. Kama alivyosema tangu mwanzo Kwa kinywa cha manabii wake watakatifu; Tuokolewe na adui zetu Na mikononi mwao wote wanaotuchukia; Ili kuwatendea rehema baba zetu, Na kulikumbuka agano lake takatifu; Uapo aliomwapia Ibrahimu, baba yetu, Ya kwamba atatujalia sisi, Tuokoke mikononi mwa adui zetu, Na kumwabudu pasipo hofu,

4.       Alikamilisha unabii katika torati na manabii uliozungumza kumuhusu yeye kwa unabii, ishara, alama na vivuli kuhusu ujio wake na kazi zake kutoka kitabu cha Mwanzo mpaka kitabu cha Malaki ambako kuna nabii zaidi ya 300 kuhusu Masihi Mwanzo 3:15 na Isaya 53

Kwa msingi huo hatupaswi tena kuteseka, kuwa watumwa, kukandamizwa, kuonewa, kuugua na kuteswa na magonjwa, kuwa watumwa wa dhambi na shetani, hatupaswi kumuogopa awaye yote, Nguvu za giza, na wachawi na washirikina na waganga, na mapepo na majini na mashetani na shetani hazina uwezo juu yetu kwa imani katika kazi aliyoifanya Bwana Yesu pale msalabani, laana ya torati, na sheria, hatuna deni, hatuna deni la jana wala la leo wala la kesho kazi imekamilika yakikutokea majanga angalia msalaba kumbuka kazi iliyofanyika msalabani, kumbuka kuwa mwanaume huyu amemaliza amakamilisha kazi ya ukombozi huna hatia hata kidogo hakuna wa kukuhukumu, wewe hata kama ulikuwa na historia mbaya sana yeye anawweza kuifuta na kuiandika upya endapo utamwamini Bwan Yesu, Neno imekwisha ni neno lenye nguvu kama vile siku unapotangazwa uhuru wa taifa lililotawaliwa na wakoloni, tunapoadhimisha siku ya kufa na kufufuka kwa Yesu Kristo yaani katika siku hii ya pasaka ni lazima tujikumbushe kuwa Yesu amekamilisha kazi ya kutuweka huru na kuvitangazia vifungo vinavyotuzunguka kwa kuvitangazia kuwa imekwisha, Mateso yamekwisha, kazi za shetani zimekwisha, majini na mapepo kazi zao zimekwisha kila aina ya vifungo na utumwa wa ibilisi ni lazima zisikie na kukumbuka kuwa imekwisha

Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!