Andiko la Msingi: Tito 2:11-12 “Maana neema
ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya
na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika
ulimwengu huu wa sasa;”
Utangulizi:
Leo hii tutachukua Muda kujifunza
kwa undani kuhusu Uadilifu, (Ethics).
Moja ya maswala ya msingi sana ambayo kila mwanadamu anapaswa kuwa nayo awapo
Duniani ni pamoja na kuwa na uadilifu, uadilifu sio agizo la Dini Fulani au
mafundisho ya watu Fulani tu lakini somo kuhusu uadilifu linawahusu wanadamu
wote, Mungu anapendezwa na uadilifu, na dunia itakuwa mahali salama na pazuri
kama watu watajifunza kuishi kwa uadilifu, Uadilifu unafanya kazi katika Nyanja
zote na watu wanaozingatia uadilifu wanakuwa na mafanikio makubwa sana na ustawi
katika maeneo yote, kwa ujumla jamii yenye uadilifu watu wake wanaishi kwa
amani na utulivu na kwa kumpendeza Mungu na watu wote!
Uadilifu ni nini hasa! Neno
uadilifu katika lugha ya kiyunani husomeka kama neno “ETHOS” kwa kiingereza ETHICS na kwa kilatini MORES Maana yake CHARACTER au BEHAVIOR au Attitude ambalo katika Falsafa tunalielezea neno
hili kama Mfumo wa kanuni unaotusaidia kujua jema na baya, na kutusaidia namna
ya kuendesha maisha yetu. Kwa kikristo tunaita “Moral Theology”
Kwa kiingereza Ethos/Ethics are system of Principles that helps our
life to determine what is wrong and what right is, what is good and what is Bad.
Uadilifu pia ni kanuni
zinazotuelekeza namna na jinsi ya kuenenda na kufanya kazi Fulani! kwa hiyo,
walimu wana aina zao za uadilifu, Wauguzi wana aina zao za uadilifu, wanasiasa
wana aina zao za uadilifu, Polisi wana aina zao za uadilifu, wachungaji wana
aina zao za uadilifu, Lakini wakristo nao wana aina yao ya uadilifu, Kimsingi
uadilifu ni kanuni zinazotuongoza kujua neno na tendo na sifa ambazo zinatupa
kukubaliika mbele za Mungu na wanadamu!
Wakolosai
1:9-11 “Kwa sababu hiyo sisi nasi, tangu siku ile
tuliposikia, hatuachi kufanya maombi na dua kwa ajili yenu, ili mjazwe maarifa
ya mapenzi yake katika hekima yote na ufahamu wa rohoni; mwenende kama ulivyo
wajibu wenu kwa Bwana, mkimpendeza kabisa; mkizaa matunda kwa kila kazi njema,
na kuzidi katika maarifa ya Mungu; mkiwezeshwa kwa uwezo wote, kwa kadiri ya
nguvu ya utukufu wake, mpate kuwa na saburi ya kila namna na uvumilivu pamoja
na furaha;”
Ki msingi wakristo ndio wanapaswa
kuwa taa u nuru ya uadilifu kote duniani na watu wengine wote wanapaswa
kujifunza na kutuiga,lazima sisi tuwe mstari wa mbele katika swala zima la
kuishi kwa uadilifu, kwa sababu tuna Mungu, tuna mwokozi na tuna Mafundisho
yaliyo bora zaidiyanayotokana na kiongozi mwadilifu zaidi kuliko wote Yesu
Kristo Bwana na Mwokozi wangu!,
katika somo hili tutaangalia eneo kubwa kwa sehemu ule umuhimu tu wa mafundisho
kuhusu uadilifu!
Umuhimu wa Mafundisho kuhusu Uadilifu!
1.
# Uadilifu
unatufanya sisi kumpendeza Mungu na wanadamu
Kwa mujibu wa
maadili ya Kikristo, mtu anayekuwa vizuri katika uadilifu atalenga siku zote
kumpendeza Mungu na wanadamu, sio wakati wote jambo hili linaweza kuwa jepesi
lakini ni amri ya Mungu kumpenda Mungu na kuwapenda jirani zetu kama nafsi zetu
kwa msingi huo neno la Mungu linatuamuru tumpendeze Mungu lakini vilevile tuwapendeze
na wanadamu ona
Mathayo 22:36-40 “Mwalimu,
katika torati ni amri ipi iliyo kuu? Akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa
moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri
iliyo kuu, tena ni ya kwanza. Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende
jirani yako kama nafsi yako. Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na
manabii.”
Kwa msingi huo
basi kila mwanadamu anayekua katika uadilifu atashuhudiwa kuwa mwema kwa Mungu
na wanadamu, Mwanadamu atakayeishi akiwa na madai kuwa ana mpendeza Mungu na
huku anawakwaza wanadamu wenzake, hatuwezi kusema kuwa anampenda Mungu pia
1Yohana 2:9-11 “Yeye
asemaye kwamba yumo nuruni, naye amchukia ndugu yake, yumo gizani hata sasa.
Yeye ampendaye ndugu yake, akaa katika nuru, wala ndani yake hamna kikwazo.
Bali yeye amchukiaye ndugu yake, yu katika giza, tena anakwenda katika giza,
wala hajui aendako, kwa sababu giza imempofusha macho.”
Kwa hivyo
kiuadilifu tunapaswa kuhakikisha kuwa tunakuwa sahihi mbele za Mungu na
wanadamu, tunampendeza Mungu na wanadamu na hili ndio moja ya somo kuu sana la
kibiblia, hakikisha kuwa unamtendea mema kila mmoja na hakikisha kuwa unakuwa
mbali na ubinafsi na kuwa kila unalotaka wewe kutendewa unawatendea na wengine
na kile usichotaka wewe kutendewa usiwatendee wengine
Mathayo 7:12 “Basi
yo yote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo
ndiyo torati na manabii.”
Ni mafundisho ya
Msingi ya kibiblia kuhakikisha kuwa tunakuwa sawa pande zote kwa Mungu na kwa
wanadamu, lazima tuwe na amani pande zote
Waebrania 12:14 “Tafuteni
kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu
atakayemwona Bwana asipokuwa nao;”
Maisha ya aina
hii ndiyo maisha anayopaswa kuishi mtu muadilifu na anayemcha Mungu hatupaswi
kuwa sawa upande mmoja tu Kristo Yesu Mwikozi wetu na kiongozi mkuu wa wokovu
wetu ametuachia kielelezo cha maisha ya uadilfu kwa sababu katika maisha yake
alimpoendeza Mungu na wanadamu ona
Luka 2:51-52 “Akashuka
pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii; na mamaye aliyaweka hayo yote
moyoni mwake. Naye Yesu akazidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza
Mungu na wanadamu.”
Kwa msingi huo
basi tunapojifunza kuhusu somo la Uadilifu maana yake tunajikumbusha namna
inavyotupasa kutenda na kueneda mbele za Mungu na wanadamu, na kuwapendeza
katika kiwango kinachopaswa ona
2Wakoritho 8:20-21 “Tukijiepusha na neno hili, mtu asije akatulaumu kwa habari ya karama
hii tunayoitumikia; tukitangulia kufikiri yaliyo mema, si mbele za Bwana tu,
ila na mbele ya wanadamu.”
2.
# Uadilifu
unatufanya sisi kuishi kwa utaratibu.
Kuishi kwa
uadilifu vilevile maana yake ni kujifunza kuishi kwa utaratibu, kama Mungu
hangetoa maelekezo au sharia na kanuni watu wangeishi bila kufuata utaratibu,
moja ya vita kubwa sana iaisyoonekana duniani ni pamoja na vita ya Utaratibu na
Machafuko (Order and Chaos) hii ni vita inayopiganwa kila siku na nadhani
utaratibu unamwakilisha Mungu na machafuko yanamwakilisha shetani, watu wenye
maadili wanaishi kwa kufuata utaratibu hatuwezi kuacha mambo yaende kama
yanavyokwenda Mungu si Mungu wa
machafuko bali ni Mungu wa utaratibu
1Wakoritho 14:33 “Kwa
maana Mungu si Mungu wa machafuko, bali wa amani; vile vile kama ilivyo katika
makanisa yote ya watakatifu.”
Unaweza kuona
sasa basi kama Mungu sio Mungu wa machafuko ni Mungu wa namna gani ni Mungu wa
utaratibu na anataka mambo yote yatendeke kwa uzuri na utaratibu
1Wakoritho 14:40 “Lakini
mambo yote na yatendeke kwa uzuri na kwa utaratibu”. Mungu alipokuwa
anauumba ulimwengu alikuwa anaumba kwa kufuata utaratibu hakutanka tu kwa ufupi
historia ya uumbaji nni historia ya utaratibu kutoka katika machafuko ona Mwanzo 1:1-8 “Hapo
mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi. Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na
giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso
wa maji. Mungu akasema, Iwe nuru; ikawa nuru. Mungu akaiona nuru, ya kuwa ni
njema; Mungu akatenga nuru na giza. Mungu akaiita nuru Mchana, na giza akaliita
Usiku. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku moja. Mungu akasema, Na liwe anga
katikati ya maji, likayatenge maji na maji. Mungu akalifanya anga, akayatenga
yale maji yaliyo juu ya anga na yale maji yaliyo chini ya anga; ikawa hivyo.
Mungu akaliita lile anga Mbingu. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya pili.”
Mpaka Mungu
anakamilisha nuumbaji maana yake alikuwa anakamilisha utaratibu, hakuna nchi au
taifa au taasisi inaweza kuendelea ikiwa watu wanaishi vile watakavyo, hakuna
nidhamu hakuna utaratibu watu wanaishi hovyo hovyo tu au bila kufuata utaratibu
maandiko yanaionyesha kuwa Mungu anataka kila mahali kuwe na utaratibu na watu
waadilifu huishi kwa utaratibu na kwa kufuata utaratibu, unaposikia
kuhusunutawala wa sharia maana yake ni utawala wa utaratibu, sio mwizi amekamatwa
watu wanapiga moto na kiberiti, Mungu anapoweka viongozi maana yake Mungu anawataka
wao wahakikishe kuwa wanasimamia utaratibu na kukemea wale wote wasioenedna kwa
utaratibu ona
Tito 1:5 “Kwa
sababu hii nalikuacha Krete, ili uyatengeneze yaliyopunguka, na kuweka wazee
katika kila mji kama vile nilivyokuamuru;” unaona meneno hayo
uyatengeneze yaliyopunguka katika Biblia ya kiingereza KJV yanasomeka hivi Titus 1:5 “For this Cause left I thee in Crete, that thou shouldest set in order the
things that are wanting, and ordain elders in every city as I had appointed
thee” Kwa hiyo Paulo mtume alimpeleka Tito awe askofu katikamkiswa
cha crete ili kuweka utaratibu unaona
kwa hiyo kimsingi mtu hawezi kuwa mwadilifu alafu wakati huo akakosa kuwa mtu
wa utaratibu mambo haya yanaenda pamoja
1Timotheo
3:1-6 “Ni
neno la kuaminiwa; mtu akitaka kazi ya askofu, atamani kazi njema. Basi
imempasa askofu awe mtu asiyelaumika, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi na
busara, mtu wa utaratibu, mkaribishaji, ajuaye kufundisha; si mtu wa kuzoelea
ulevi, si mpiga watu; bali awe mpole; si mtu wa kujadiliana, wala asiwe mwenye
kupenda fedha; mwenye kuisimamia nyumba yake vema, ajuaye kutiisha watoto
katika ustahivu; (yaani, mtu asiyejua kuisimamia nyumba yake mwenyewe,
atalitunzaje Kanisa la Mungu?) Wala asiwe mtu aliyeongoka karibu, asije
akajivuna akaanguka katika hukumu ya Ibilisi.”
Watu wale
waliojiita wakristo na wakashindwa kuishi kwa kufuata kanuni ya kufanya kazi na
kujipatia chakula chao wenyewe Paulo mtume aliwakemea na kuwaita watu
wasioenenda kwa utaratibu
1Wathesalonike 5:14 “Ndugu, twawasihi, waonyeni wale wasiokaa kwa utaratibu;
watieni moyo walio dhaifu; watieni nguvu wanyonge; vumilieni na watu wote.”
Watu wasiokaa kwa utaratibu wanaitwa
unruly maandiko yanakemea na kuwataka watu wote wawe wenye kuishi kwa utaratibu
kwa msingi huo somo la maadili linakazia watu kuishi kwa kufuata utaratibu na
kujihami kwa kujichukulia sharia mkononi au kufanya kila tunaloliona
wenyewekuwa jema na ili kwamba watu waishi kwa utaratibu na kuepuka machafuko,
ulimwengu wa sasa unakwenda mbio mno na watu wanaishi bila kufuata utaratibu
hawajali kanuni na utaratibu ambapo Mungu ameuweka na ndio maana Isaya
nabii anaiona kama kitu kinachoharibika haraka kwa sababu utaratibu umetoweka !
Isaya 24:19-20“Dunia
kuvunjika, inavunjika sana; dunia kupasuka, imepasuka sana; dunia kutikisika,
imetikisika sana. Dunia inalewa-lewa kama mlevi, nayo inawaya-waya kama
machela; na mzigo wa dhambi zake utailemea; nayo itaanguka, wala haitainuka
tena”
3.
# Uadilifu
humfanya mtu aone kuwa watu wote ni sawa au bora
Maandiko yanatufundisha
kuwa Mungu hana upendeleo kwa lugha nyingine Mungu hana ubaguzi.
Warumi 2:11 “kwa
maana hakuna upendeleo kwa Mungu” Kwa msingi huo Mungu humkubali mtu
yeyote yule katika kila taifa anayemkubali yeye
Matendo 10:34-35 “Petro
akafumbua kinywa chake, akasema, Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo;
bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye.”
Hii maana yake
kila mwanadamu ana haki sawa kwa Mungu binadamu wote ni sawa Ni kweli
Mungualiichagua Israel ili kuleta Baraka kwa mataifa byote na sasa mtu
akimkubali Yesu anakuwa na kibali kwa Mungu bila ubaguzi wa aina yoyote katika
Kristo kila mtu ni sawa kila mtu ni uzao wa Ibrahimu na mrithi wa ahadi zile ona
Wagalatia 3:27-29 “Maana
ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo. Hapana Myahudi wala
Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke. Maana ninyi
nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu. Na kama ninyi ni wa Kristo, basi,
mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi sawasawa na ahadi.”
Kwa msingi huo
kama Mungu hana ubaguzi na tunajifunza kutoka kwake hii maana yake kila mtu
anayemcha Mungu hapaswi kuwa na upendeleo wala ubaguzi Swala la ubaguzi
limekuwa moja ya tatizo kubwa sana Duniani, mara kadhaa tumeona Africa na
Israel ikiwa ni jamii ambayo imeteseka sana duniani, wengi wakionewa wivu,
kubaguliwa kuawa na hata kukojolewa waafrika wakati mwingine wamezaniwa kama watu
wasio na akili na wasioweza kufanyololote bila kutumikishwa, wengi wametumiwa
kwa faida ya weupe, huku watu weupe wakijifikiri kuwa wao ni bora zaidi duniani
katika maadili ya kikristo maandiko matakatifu yanatukataza sio tu kuwabagua
watu kwa sababu ya rangi zao bali hata
kwa hali zao za kifedha hatupaswi kuwa na upendeleo
Yakobo 2:1-4 “Ndugu
zangu, imani ya Bwana wetu Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwe nayo kwa
kupendelea watu. Maana akiingia katika sinagogi lenu mtu mwenye pete ya dhahabu
na mavazi mazuri; kisha akiingia na maskini, mwenye mavazi mabovu; nanyi
mkimstahi yule aliyevaa mavazi mazuri, na kumwambia, Keti wewe hapa mahali
pazuri; na kumwambia yule maskini, Simama wewe pale, au keti miguuni pangu, je!
Hamkufanya hitilafu mioyoni mwenu, mkawa waamuzi wenye mawazo mabovu? ”
Ubaguzi ni mwiko
katika Tamko la umoja wa mataifa la haki za binadamu lililotolewa huko Paris December 10 mwaka 1948 ambalo
linaitwa kwa kiingereza Universal Declaration of Human Rights UDHR tamko lake
la kwanza linasema hivi nanukuu
“All human beings are born free and equal
in dignity and rights, they are endowed with reason and conscience and should
act toward one another in spirit of brotherhood”
“Kwamba watu wote huzaliwa huru wakiwa sawa
na katika haki na heshima na wamepewa akili na dhamiri nani juu yao
kushirikiana wana na wengine kwa roho ya udugu”
Matamko haya
pamoja na mengine mengi yanayofuata yalikuwa na lengo la kukomesha hali ya
kujiona mabwana na wengine watumwa au hali ya kuwabaguwa wanadamu kwa sababu
zozote zile maandiko yanamtaka kila
mmoja amuhesabu mweznie kuwa ni bora kuliko nansi yake ona
Wafilipi 2:3 “Msitende
neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu
na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake.”
Watu wenye
uadilifu hawana ubaguzi, hawapokei uso wa mwanadamu kwa mitazamo ya upendeleo,
wanawaona wanadamu wote kuwa ni sawa hawana upendeleo wala hawana ubaguzi kama
alivyo baba wa Mbinguni ambayo hutoa haki sawa kwa watu wema na wabaya kwa
kuwapa jua lake na mvua
Mathayo 5:44-46 “lakini
mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, ili mpate kuwa wana
wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema,
huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi
mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo?”
4.
Uadilifu
unatufanya sisi tuwe mfano wa kuigwa.
Tunajifunza
kuhusu uadilifu katika neno la Mungu ili kwamba tuwe kielelezo au mfano kwa
watu wengine hususani watu wa ulimwengu huu wasio na uadilifu, Mungu
alipowaokoa wana wa Israel kule Misri aliwafundisha uadilifu kupiti Musa
mtumishi wake ili Israel liwe taifa litakalokuwa kielelezo kwa Mataifa yote
Kumbukumbu 4:5-8 “Angalieni
nimewafundisha amri na hukumu, vile vile kama Bwana, Mungu wangu,
alivyoniamuru, ili mzitende katika nchi mwingiayo ili kuimiliki. Zishikeni
basi, mkazitende, maana hii ndiyo hekima yenu na akili zenu, machoni pa mataifa
watakaozisikia amri hizi zote, nao watasema, Hakika taifa hili kubwa ni watu
wenye hekima na akili. Kwa maana liko taifa gani kubwa, lililo na Mungu aliye
karibu nao, kama Bwana, Mungu wetu, alivyo, kila tumwitapo? Tena liko taifa
gani kubwa, lililo na amri na hukumu zenye haki kama torati hii yote,
ninayoiweka mbele yenu leo.”
Ni katika hali
kama hii Yesu alipokuja ulimwenguni alikuja kama Mwalimu wa kutufundisha mambo
mengi sana ili tuweze kuuiga mfano wake yeye ametuachia mifano mingi ya kuiga
na kuishi kwa uadilifu ona
Yohana 13:15 “Kwa
kuwa nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo.”
Unaona Yesu
ametuachia kielelezo ili kwamba na sisi tuweze kumfuata na kutenda kama
alivyotenda, aidha Paulo mtume pia alipokuwa duniani alijitajitahidi sana kuwa
kielelezo na aliwataka watu wamfuate yeye vilevile kama anavyomfuata Kristo ona
1Wakoritho 11:1 “Mnifuate
mimi kama mimi ninavyomfuata Kristo.” Makusudi makubwa ya Bwana Yesu
ni kuwa tutakapoishi kwa kufuata mfano wake watu wa ulimwengu watajua kuwa sisi
ni wanafunzi wa Yesu ona
Yohana 13:35 “Hivyo
watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo
ninyi kwa ninyi”, kwaajili ya haya mitume walisisitiza sana
wanafunzi wa Yesu wote waishi kwa kufuata kielelezo
Wafilipi 3:17 “Ndugu
zangu, mnifuate mimi, mkawatazame wao waendao kwa kuufuata mfano tuliowapa
ninyi.”
Wafilipi 4:9 “Mambo
mliyojifunza kwangu na kuyapokea, na kuyasikia na kuyaona kwangu, yatendeni
hayo; na Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi.” Tunapoishi kwa
uadilifu moja ya faida kubwa sana ni kuwa watu watayaona matendo mema na
kumtukuza Mungu, lakini hata wale wenye kulaumu watakosa sababu zenye mashiko
kutokana na kuwa waadilifu ona
1Petro 2:12 “Mwe
na mwenendo mzuri kati ya Mataifa, ili, iwapo huwasingizia kuwa watenda mabaya,
wayatazamapo matendo yenu mazuri, wamtukuze Mungu siku ya kujiliwa.”
Neno la Mungu
linatoa maonyo makali sana kwa watu wasiojua kupambanua mema na mabaya na hata
wale amabao kwa kusudi wanageuza na kuona kuwa mabaya ndio mema na mema ndio
mabaya ona
Isaya 5:20-23 “Ole
wao wasemao kwamba uovu ni wema, na kwamba wema ni uovu; watiao giza badala ya
nuru, na nuru badala ya giza; watiao uchungu badala ya utamu, na utamu badala
ya uchungu! Ole wao walio wenye hekima katika macho yao wenyewe, na wenye
busara katika fikira zao wenyewe! Ole wao walio hodari kunywa kileo chenye
nguvu, watu waume wenye nguvu kuchanganya vileo; wampao haki mwenye uovu, ili
wapewe ijara, na kumwondolea mwenye haki haki yake!”
5.
Uadilifu
hutusaidia kuepuka Kanuni ya kupanda na kuvuna
Wagalatia 6;7-8 “Msidanganyike,
Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna. Maana
yeye apandaye kwa mwili wake, katika mwili wake atavuna uharibifu; bali yeye
apandaye kwa Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele.”
Kanuni ya
kupanda na kuvuna ni moja ya kanuni yenye nguvu nay a ajabu sana Duniani na
kanuni hii inafanya kazi, katika dini ya kihindu na Kibudha kanuni hii huitwa
Karma – ambayo maana yake ni mjumuisho
wa matendo ya awali yanayoamua matukio yako ya sasa na baadaye, kanuni hii
inatisha sana kwa sababu huwa
haidanganyi na infanya kazi mno, Na ndio
maana Paulo mtume anausema mstari huu kwa maonyo makali neno hilo
Msidanganyioke kwa kiibrania ni (Planao)
ambalo maana yake kuchezea pua ya Mungu au kuugeuza ukweli wa Mungu, au
kufanya mzaha na kanuni za Mungu, kwa hiyo Paulo anaonya kuwa tusifanya mzaha
na Kanuni za Mungu zinafanya kazi yeye anachokisema amekisema
Mwanzo 3:4-5 “Nyoka
akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku
mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu,
mkijua mema na mabaya.”
Hapa Eva alikuwa anajaribiwa achezee
kanuni za kiungu na unajua yaliyotukia, Kanuni za kiungu zinafanya kazi na
hazina mzaha, Yakobo ni mfano mzuri wa kuigwa katika maandiko alidanganya kuwa
yeye ni Esau ona
Mwanzo 27:18-22 “Akaja
kwa baba yake, akasema, Babangu. Akasema, Mimi hapa, U nani wewe, mwanangu?
Yakobo akamwambia babaye, Mimi ni Esau, mzaliwa wako wa kwanza, nimefanya kama
ulivyoniambia. Ondoka, tafadhali, ukae kitako, ule mawindo yangu, ili roho yako
inibariki.Isaka akamwuliza mwanawe, Imekuwaje umepata upesi namna hii,
mwanangu? Akasema, Kwa sababu BWANA, Mungu wako, amenifanikisha. Isaka
akamwambia Yakobo, Karibu, tafadhali, ili nikupapase, mwanangu, nione kwamba
wewe ndiwe mwanangu Esau, ama siyo. Basi Yakobo akamkaribia Isaka, babaye, naye
akampapasa, akasema, Sauti ni sauti ya Yakobo, lakini mikono ni mikono ya Esau.”
Baada ya yeye kudanganya alisababisha
machozi makubwa sana kwa kaka yake Esau ona Mwanzo 27:34-35 “Esau aliposikia maneno ya babaye, akalia kilio kikubwa
cha uchungu sana, akamwambia babaye, Nibariki na mimi, mimi nami, Ee babangu.
Akasema, Nduguyo amekuja kwa hila, akauchukua mbaraka wako.” Baada
ya wakati mwingi hiki kilikuja kutokea katiika maisha ya Yakobo
Mwanzo 29:15-26 “Labani
akamwambia Yakobo, Kwa sababu wewe ni ndugu yangu, basi, je! Unitumikie bure?
Niambie mshahara wako utakuwa nini? Labani alikuwa na binti wawili, jina la
mkubwa ni Lea, na jina la mdogo ni Raheli. Naye Lea macho yake yalikuwa dhaifu,
lakini Raheli alikuwa mzuri wa umbo, na mzuri uso.Yakobo akampenda Raheli
akasema, Nitakutumikia miaka saba kwa kumpata Raheli, binti yako mdogo. Labani
akasema, Afadhali nikupe wewe kuliko mtu mwingine; kaa kwangu. Yakobo akatumika
miaka saba kwa kumpata Raheli. Ikawa machoni pake kama siku chache tu kwa vile
alivyompenda. Yakobo akamwambia Labani, Nipe mke wangu, maana siku zangu
zimetimia; niingie kwake. Labani akakusanya watu wote wa mahali pale, akafanya
karamu. Ikawa wakati wa jioni akamtwaa Lea, binti yake, akamletea Yakobo, naye
akaingia kwake. Labani akampa Lea mjakazi wake Zilpa, awe mjakazi wake. Ikawa,
kulipokuwa asubuhi, kumbe! Ni Lea. Akamwambia Labani, Nini hii uliyonitenda?
Sikukutumikia kwa Raheli? Mbona umenidanganya? Labani akasema, Havitendeki hivi
kwetu, kumtoa mdogo kabla ya mkubwa”
Vile vile Yakobo
alidanganywa tena na vijana wake kuhusu ndugu yao Yusufu
Mwanzo 37:31-35 “Wakaitwaa
kanzu ya Yusufu, wakachinja mwana-mbuzi, na kuichovya kanzu katika damu.
Wakaenda nayo ile kanzu ndefu, wakamletea baba yao, wakasema, Tumeona hii;
basi, utambue kama kanzu hii ni ya mwanao, ama siyo. Akaitambua, akasema, Ndiyo
kanzu ya mwanangu, mnyama mkali amemla; bila shaka Yusufu ameraruliwa. Yakobo
akararua mavazi yake, akajivika gunia viunoni, na kumlilia mwanawe siku nyingi.
Wanawe wote, na binti zake wote, wakaondoka wamtulize, lakini akakataa
kutulizwa, akasema, La! Nitamshukia mwanangu, nikisikitika, hata kuzimu. Baba
yake akamlilia.”
Unaona huwezi
kupanda ubaya kisha uvune mema kanuni hii inafanya kazi kwa watu wote na kabila
zote na jamii zote za dunia kwa sababu ni kanuni ya Mungu, ni kanuni ya uadilifu pakee inayoweza
kukulinda na mavuno ndio maana ile sharia ya dhahabu ikatutahadharia kuwa
lolote lile ambalo hupendi wewe kutendewa usiwatendee wengine
Mathayo 7:12 “Basi
yo yote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo
ndiyo torati na manabii.”
Kanuni ya kula
mke wa mtu, malipizi yake ni kuliwa kwa mkeo Ayubu 31:9-11 “Kama moyo wangu
ulishawishwa kwa mwanamke, Nami nimeotea mlangoni pa jirani yangu; Ndipo hapo
mke wangu na asage kwa mwingine, Na wengine na wainame juu yake. Kwani hilo
lingekuwa kosa kuu; Naam, lingekuwa ni uovu wa kuadhibiwa na waamuzi;”
2.Samuel 11:2-4 “Ikawa
wakati wa jioni, Daudi akaondoka kitandani, akatembea juu ya dari ya jumba la
mfalme; na alipokuwa juu ya dari aliona mwanamke anaoga; naye huyo mwanamke
alikuwa mzuri sana, wa kupendeza macho. Naye Daudi akapeleka, akauliza habari
za yule mwanamke. Mtu mmoja akasema, Je! Huyu siye Bath-sheba, binti Eliamu,
mkewe Uria, Mhiti? Basi Daudi akapeleka wajumbe, akamtwaa; naye akaingia kwake;
naye akalala naye; (maana yule mwanamke amekwisha kutakasika unajisi wake);
kisha akarudi nyumbani kwake.”
Wote tunajua
kile Daudi alikifanya na matokeo yake Mungu alimuambiaje? Ona
2samuel 12:1-11 “Ndipo
Bwana akamtuma Nathani aende kwa Daudi. Naye akamwendea, akamwambia, Palikuwa
na watu wawili katika mji mmoja; mmoja wao alikuwa tajiri, wa pili maskini.Yule
tajiri alikuwa na kondoo na ng'ombe wengi sana; bali yule maskini hakuwa na
kitu, ila mwana kondoo mmoja, mdogo, ambaye amemnunua na kumlea; naye akakua
pamoja naye, na pamoja na wanawe; hula sehemu ya posho lake, na kukinywea
kikombe chake, na kulala kifuani mwake, akawa kwake kama binti. Hata msafiri
mmoja akamfikilia yule tajiri, naye akaacha kutwaa mmoja wa kondoo zake
mwenyewe au mmoja wa ng'ombe zake mwenyewe, ili kumwandalia yule msafiri aliyemfikilia,
bali alimnyang'anya yule maskini mwana-kondoo wake, akamwandalia yule mtu
aliyemfikilia. Ndipo hasira ya Daudi ikawaka sana juu ya mtu yule; akamwambia
Nathani, Aishivyo Bwana, mtu huyo aliyetenda jambo hili, hakika yake astahili
kufa; naye atamrudishia yule mwana-kondoo mara nne, kwa sababu ametenda neno
hili, na kwa sababu hakuwa na huruma. Basi Nathani akamwambia Daudi, Wewe ndiwe
mtu huyo. Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nalikutia mafuta, uwe mfalme juu
ya Israeli, nikakuokoa na mkono wa Sauli; nami nikakupa nyumba ya bwana wako,
na wake za bwana wako kifuani mwako; nikakupa nyumba ya Israeli na ya Yuda; na
kama hayo yangalikuwa machache, ningalikuongezea mambo kadha wa kadha. Kwa nini
umelidharau neno la Bwana, na kufanya yaliyo mabaya machoni pake? Umempiga
Uria, Mhiti, kwa upanga, nawe umemtwaa mkewe awe mke wako, nawe umemwua huyo
kwa upanga wa wana wa Amoni. Basi, sasa upanga hautaondoka nyumbani mwako, kwa
sababu umenidharau, ukamtwaa mkewe Uria, Mhiti, kuwa mke wako. Bwana asema hivi,
Angalia, nitakuondokeshea uovu katika nyumba yako, nami nitawatwaa wake zako
mbele ya macho yako, na kumpa jirani yako, naye atalala na wake zako mbele ya
jua hili. Maana wewe ulifanya jambo lile kwa siri; bali mimi nitalifanya jambo
hili mbele ya Israeli wote na mbele ya jua.”
Je Daudi alivuna kile alichokipanda ?
ona Samuel 16:20-23 “Kisha Absalomu akamwambia Ahithofeli, Haya, toa shauri
lako, tufanyeje. Naye Ahithofeli akamwambia Absalomu, Ingia wewe kwa masuria ya
baba yako, hao aliowaacha ili kutunza nyumba; na Israeli wote watasikia ya kuwa
umechukizwa kabisa na baba yako; ndipo itatiwa nguvu mikono yao wote walio
pamoja nawe. Basi wakamtandikia Absalomu hema juu ya nyumba darini; naye
Absalomu akaingia kwa masuria ya babaye machoni pa Israeli wote. Na shauri lake
Ahithofeli, alilokuwa akilitoa siku zile, lilikuwa kama mtu aulizapo kwa neno
la Mungu; ndivyo yalivyokuwa mashauri yote ya Ahithofeli, kwa Daudi, na kwa
Absalomu.”
Muda hauwezi
kutosha kuangalia kanuni ya kupanda na kuvuna namna inavyofanya kazi lakini kwa
ufupi ni kanuni yenye kutisha sana ukipanda mema utavuna mema na ukipanda
mabaya utavuna mabaya haijalishi ni katika siasa au kanisani au maisha ya
kawaida, hatuna budi kuwa makini na mbegu tunazozipanda. Somo kuhusu uadilifu
litatusaidia.
6.
Uadilifu
unatukumbusha sisi Kutunza Heshima ya wazazi
Uadilifu ni
pamoja na kutunza heshima ya wazazi Tangu mwanzo Mungu alikusudia wazazi wapewe
heshima kubwa nay a kipekee sana sharia za uadilifu zilikuwa zinakataza vikali
kuwavunjia heshima wazazi na hata wakati mwingine zilitoa maelekezo makali kwa
mtu aliyevunja heshima kwa wazazi ikiwezekana hata kuuawa ona Kutoka 20:12 neno
la Mungu linasema
Kutoka 20:12 12. Waheshimu
baba yako na mama yako; siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na
BWANA, Mungu wako.
Wakolosai 3:20 “Ninyi
watoto, watiini wazazi wenu katika mambo yote; maana jambo hili lapendeza
katika Bwana”
Waefeso 6:1-3 “Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika
Bwana, maana hii ndiyo haki. Waheshimu baba yako na mama yako; amri hii ndiyo
amri ya kwanza yenye ahadi, Upate heri, ukae siku nyingi katika dunia.”
Kwanini neno la
Mungu linakazia kuwaheshimu baba na mama kuna watu walijiletea laana kwa
kutokuwaheshimu wazazi wao, Biblia inaonyesha kuwa kuwadharau wazazi kuna
madhara makubwa na athari kubwa katika maisha yetu ona
Mwanzo 9:20-26 “Nuhu
akaanza kuwa mkulima, akapanda mizabibu; akanywa divai, akalewa; akawa uchi
katika hema yake. Hamu, baba wa Kanaani, akauona uchi wa baba yake, akawaeleza
ndugu zake wawili waliokuwa nje. Shemu na Yafethi wakatwaa vazi, wakalitanda
mabegani mwao wote wawili, wakaenda kinyumenyume, wakaufunika uchi wa baba yao;
na nyuso zao zilielekea nyuma, wala hawakuuona uchi wa baba yao.Nuhu akalevuka
katika ulevi wake, akajua mwana wake mdogo alivyomtendea.Akasema, Na alaaniwe
Kaanani; Atakuwa mtumwa kabisa kwa ndugu zake.Akasema, Na atukuzwe BWANA, Mungu
wa Shemu; Na Kaanani awe mtumwa wake.”
Hamu alijiletea
laana na kukosa Baraka za uzaliwa wa kwanza kwa sababu hakuufunika uchi wa baba
yake, utupu wa baba yako usiufunue, ni wazi kuwa wazazi wetu wanapaswa
kuheshimiwa sana ona pia
Mwanzo 39:3-4 “Reubeni,
u mzaliwa wangu wa kwanza, Nguvu zangu, na malimbuko ya uwezo wangu. Umewapita
wengine kwa ukuu na kwa nguvu.Umeruka mpaka kama maji, basi usiwe na ukuu, Kwa
sababu ulikipanda kitanda cha baba yako, Ukakitia unajisi; alikipandia kitanda
changu.”
Kimaadili
maswala haya hayakubaliki nani utovumkubwa sana wa kinidhamu na uadilifu kuna
maswala ambayo kiuadilifu yakifanyika yanaweza kuwashangaza hata wapagani hasa
kama yatafanywa na waaminio
1Wakoritho 5:1-5 “Yakini
habari imeenea ya kuwa kwenu kuna zinaa, na zinaa ya namna isiyokuwako hata
katika Mataifa, kwamba mtu awe na mke wa babaye. Nanyi mwajivuna, wala
hamkusikitika, ili kwamba aondolewe miongoni mwenu huyo aliyetenda jambo hilo. Kwa
maana kweli, nisipokuwapo kwa mwili, lakini nikiwapo kwa roho, mimi mwenyewe
nimekwisha kumhukumu yeye aliyetenda jambo hilo, kana kwamba nikiwapo. Katika
jina la Bwana wetu Yesu, ninyi mkiwa mmekusanyika pamoja na roho yangu, pamoja
na uweza wa Bwana wetu Yesu; kumtolea Shetani mtu huyo, ili mwili uadhibiwe,
ili na roho iokolewe katika siku ya Bwana Yesu”
Maandiko
yanaonya vikali kutokuwatendea wazazi mambo ya kijinga na ndio maana katika
amri za uadilifu swala la kuwaheshimu wazazi limewekwa katika amri za Mungu za
kutunza mahusiano, maandiko hayaruhusu hata kuwalaani wazazi Mafanikio hayawezi
kumjia mtu anayemlaani baba yake na mama yake Mithali 20:20 “Amlaaniye babaye au mamaye,
Taa yake itazimika katika giza kuu.” Maandiko pia yansisitiza
wasikilizwe na wasidharauliwe ona Mithali
23:22 “Msikilize baba yako aliyekuzaa, Wala
usimdharau mama yako akiwa mzee” Maandiko yanaonyesha wanaowadharau
wazazi wanaweza kufa kifo kibaya Mithali
30:17 “Jicho la mtu amdhihakiye babaye, Na kudharau
kumtii mamaye; Kunguru wa bondeni wataling'oa, Na vifaranga vya tai watalila.”
Mtu anayejaribu
kuwalaani au kuwasumbua alipaswa auawe ona Walawi 20:9 Kwa maana kila mtu
amlaaniye baba yake au mama yake hakika atauawa, amemlaani baba yake na mama
yake; damu yake itakuwa juu yake.
Torati 21:18-21 “Mtu
akiwa na mwana mkaidi, mshupavu, asiyetii sauti ya baba yake, wala sauti ya
mama yake, nao wajapomwadhibu hawasikizi, ndipo babaye na mamaye na wamkamate,
na kumpeleka kwa wazee wa mji wake, katika lango la mahali pake; wawaambie
wazee wa mji wake, Huyu mwana wetu ni mkaidi, mshupavu, hasikizi sauti yetu; ni
mwasherati, tena ni mlevi.Waume wote wa mji wake na wamtupie mawe, afe; ndivyo
utakavyoondoa uovu katikati yako; na Israeli wote watasikia na kuogopa.”
Kimsingi sio
kuwa maandiko yanafurahia kuuawa kwa watoto, wote tunajua kuwa ni jambo gumu
sana kuacha mwanao auawe lakini mpango wa Mungu ni usimamizi mahiri kuhusu
wazazi waheshimike kwa msingi huo basi neno la Mungu linatutaka tuwaheshimu
wazazi tena sio wet utu hata na wa wengine, tuwasalimie kwa heshima zote,
tuwapokee, tusiwapite tuwasaidie kazi mbalimbali na kuwatii na ikuwasikiliza katika
mahusia yao na maagizo yao hususani ambaye hayako kinyume na mapenzi ya Mungu.
7.
Uadilifu
unatukumbusha sisi Kutunza Heshima ya Mungu:
Somo kuhusu
maadili pia linamtaka kila mwanadamu duniani kutambua uwepo wa Mungu na kumpa
heshima yake katika amri za maadili amri kama tatu za mwanzoni ziko kwaajili ya
kuhakikisha kuwa heshima ya Mungu inatunzwa
Kutoka 20:1-7 “Mungu
akanena maneno haya yote akasema, Mimi ni BWANA, Mungu wako, niliyekutoa katika
nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa. Usiwe na miungu mingine ila mimi.
Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu
mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia.
Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, BWANA, Mungu wako, ni Mungu
mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha
nne cha wanichukiao, nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri
zangu. Usilitaje bure jina la BWANA, Mungu wako, maana BWANA hatamhesabia kuwa
hana hatia mtu alitajaye jina lake bure.”
Kwa kawaida neno
la Mungu linamuhesabia mtu yeyote asiyeamini katika kuwepo kwa Mungu kuwa ni
mpumbavu na kamwe maandiko hayana Muda wa kufanya kazi ya kutibitisha kuwa
Mungu yupo Lakini neno la Mungu lilianza kwa kusema hapo mwanzo Mungu kwa hiyo
kila anayewaza hata moyoni mwake kuwa hakuna Mungu anaitwa mpumbavu ona
Zaburi 53:1-3 “Mpumbavu
amesema moyoni, Hakuna Mungu; Wametenda uovu wa ufisadi na kuchukiza, Hakuna
atendaye mema. Toka mbinguni MUNGU aliwachungulia wanadamu, Aone kama yuko mtu
mwenye akili, Amtafutaye Mungu.Kila mtu amepotoka, wameoza wote pamoja, Hakuna
atendaye mema, La! Hata mmoja.”
Mungu anawajali
wanadamu na kuwapenda katika kiwango kikubwa sana na cha hali ya juu, lakini
kwa muda mrefu wanadamu wengo na mataifa mengi yamepuuza sana maswala
mbalimbali kuhusu Mungu na watu wengi wameshindwa kumuheshimu, unapoangalia
sera za kijamaa ni ukweli ulio wazi kuwa ni sera nzuri sana ukilinganisha na za
kibepari, hata hivyo tatizo kubwa la sera ya kijamaa ilitaka kuishi kwa ujamaa
bila kujali mambo ya Mungu, na hatimaye ujamaa ulianguka, Ujamaa wa kwanza ulifanyika
huko Babeli.
Mwanzo 10: 1-8. “Nchi yote ilikuwa na lugha moja na
usemi mmoja. Ikawa watu waliposafiri pande za mashariki waliona nchi tambarare
katika nchi ya Shinari; wakakaa huko. Wakaambiana, Haya, na tufanye matofali
tukayachome moto. Walikuwa na matofali badala ya mawe, na lami badala ya
chokaa. Wakasema, Haya, na tujijengee mji, na mnara, na kilele chake kifike
mbinguni, tujifanyie jina; ili tusipate kutawanyika usoni pa nchi yote. BWANA
akashuka ili auone mji na mnara waliokuwa wakiujenga wanadamu. BWANA akasema,
Tazama, watu hawa ni taifa moja, na lugha yao ni moja; na haya ndiyo wanayoanza
kuyafanya, wala sasa hawatazuiliwa neno wanalokusudia kulifanya. Haya, na tushuke
huko, tuwachafulie usemi wao ili wasisikilizane maneno wao kwa wao. Basi BWANA
akawatawanya kutoka huko waende usoni pa nchi yote; wakaacha kuujenga ule mji ”
Mungu huwa
anasikitishwa mno pale wanadamu wanapomdharau na kumsahau, kwa ujumla
tunapojifunza kuhusu uadilifu Mungu ndio mwalimu mkuu wa somo hilo hivyo ni
wazi kuwa uadilifu unatoka kwa Mungu,
Isaya 1: 3-5 “Ng'ombe
amjua bwana wake, Na punda ajua kibanda cha bwana wake; Bali Israeli hajui,
watu wangu hawafikiri. Ole wake, taifa lenye dhambi, watu wanaochukua mzigo wa
uovu, wazao wa watenda mabaya, watoto wanaoharibu; wamemwacha Bwana,
wamemdharau yeye aliye Mtakatifu wa Israeli, wamefarakana naye na kurudi nyuma.
Mbona mnataka kupigwa hata sasa, hata mkazidi kuasi? Kichwa chote ni kigonjwa,
moyo wote umezimia.”
Ukweli kuhusu
Mungu umedhihirishwa tangu mwanzo, lakini wanadamu kwa kujifikiri kuwa wana
akili walijipumbazika na kumvunjia Mungu heshima kwa kuendelea kuishi bila
uadilifu
Warumi 1:21-25 “Kwa kuwa mambo
ya Mungu yanayojulikana yamekuwa dhahiri ndani yao, kwa maana Mungu
aliwadhihirishia. Kwa sababu mambo yake yasiyoonekana tangu kuumbwa ulimwengu
yanaonekana, na kufahamika kwa kazi zake; yaani, uweza wake wa milele na Uungu
wake; hata wasiwe na udhuru; kwa sababu, walipomjua Mungu hawakumtukuza kama
ndiye Mungu wala kumshukuru; bali walipotea katika uzushi wao, na mioyo yao
yenye ujinga ikatiwa giza. Wakijinena kuwa wenye hekima walipumbazika; wakaubadili utukufu wa Mungu asiye na
uharibifu kwa mfano wa sura ya binadamu aliye na uharibifu, na ya ndege, na ya
wanyama, na ya vitambaavyo. Kwa ajili ya hayo Mungu aliwaacha katika tamaa za
mioyo yao, waufuate uchafu, hata wakavunjiana heshima miili yao.Kwa maana
waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakakisujudia kiumbe na kukiabudu badala
ya Muumba anayehimidiwa milele. Amina.”
Kwa msingi huo
sasa unaweza kuona mwenye uumbaji wake anataka aheshimiwe na anakasirishwa sana
na watu wanapoacha kujali na kupuuzia kuwa hakuna Mungu au kuzitegemea akili
zao wenyewe, watu wengi wanashindwa
Mithali 3:5-7 “Mtumaini
Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia
zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako. Usiwe mwenye hekima machoni
pako; Mche Bwana, ukajiepushe na uovu.”
Mmiliki wa Meli
ya Tutanic ambayo kihistoria ilikuwa meli kubwa sana ya kifahari iliyokuwa na
viwanja vya michezo, makasino, na hoteli na uwezo wa kubeba watu 1,500
alipoulizwa kuhusu uimara wa maeli hiyo alisema HATA MUNGU HAWEZI KUIZAMISHA, lakini habari mbaya ilipatikama siku
moja mara baada ya kuanza safari kwa meli hiyo kutoka uingereza kuelekea
Marekani Tarehe April 14-15, 1912 meli
hii kubwa ilipata ajali na kuzama baada ya kugonga mwamba wa barafu na kuzama
na watu wengi sana walikufa kwa nini bila
shaka kwa sababu ya kumdharau Mungu.
Mathayo 22;37-38 “Akamwambia,
Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili
zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza.”
Maandiko
yanatuamrisha kumpenda Mungu, hatuwezi kwa namna yoyote kuwa waadilifu kama
hatumpi Mungu nafasi ya kwanza, Mungu anapaswa kuheshimiwa kwa moyo, na kwa
matendo yetu na kwa mali zetu, na kwa ujumla
lakini sio hivyo tu hata mafanikio yetu yanapaswa kuonyesha kuwa
yanatokana na Mungu, vyeo na nafasi mbali mbali zinatokana na Mungu
Daniel 4: 29-37 “Baada ya miezi kumi na miwili, alikuwa
akitembea ndani ya jumba la kifalme katika Babeli. Mfalme akanena, akasema, Mji
huu sio Babeli mkubwa nilioujenga mimi, uwe kao langu la kifalme, kwa uwezo wa
nguvu zangu, ili uwe utukufu wa enzi yangu? Hata neno lile lilipokuwa katika
kinywa cha mfalme, sauti ilikuja kutoka mbinguni, ikisema, Ee mfalme
Nebukadreza, maneno haya unaambiwa wewe; Ufalme huu umeondoka kwako. Nawe
utafukuzwa mbali na wanadamu, na makao yako yatakuwa pamoja na wanyama wa
kondeni; utalishwa majani kama ng'ombe, na nyakati saba zitapita juu yako, hata
utakapojua ya kuwa Aliye juu ndiye anayemiliki katika ufalme wa wanadamu, naye
humpa amtakaye, awaye yote. Saa iyo hiyo jambo hilo likatimizwa, likampata
Nebukadreza; alifukuzwa mbali na wanadamu, akala majani kama ng'ombe, na mwili
wake ulilowa maji kwa umande wa mbinguni, hata nywele zake zikakua, zikawa kama
manyoya ya tai, na kucha zake kama kucha za ndege.Hata mwisho wa siku hizo,
mimi, Nebukadreza, nikainua macho yangu kuelekea mbingu, fahamu zangu
zikanirudia; nikamhimidi Yeye aliye juu, nikamsifu na kumheshimu Yeye aishiye
milele; kwa maana mamlaka yake ni mamlaka ya milele, na ufalme wake hudumu toka
kizazi hata kizazi; na watu wote wanaokaa duniani wamehesabiwa kuwa si kitu,
naye hufanya kama atakavyo, katika jeshi la mbinguni, na katika hao wanaokaa
duniani; wala hapana awezaye kuuzuia mkono wake, wala kumwuliza, Unafanya nini
wewe? Basi wakati uo huo fahamu zangu zikanirudia, na kwa ajili ya utukufu wa
ufalme wangu, enzi yangu na fahari yangu zikanirudia; na mawaziri wangu, na
madiwani wangu, wakaja kunitafuta; nami nikathibitika katika ufalme wangu,
nikaongezewa enzi kupita kiasi. Basi mimi, Nebukadreza, namhimidi Mfalme wa
mbinguni, namtukuza na kumheshimu; maana matendo yake yote ni kweli, na njia
zake ni za adili; na wale waendao kwa kutakabari, yeye aweza kuwadhili.”
Mungu
anawaheshimu wale wanaomuheshimu 1Samuel
2:30 “ Kwa sababu hiyo, Bwana, Mungu wa Israeli,
asema, Ni kweli, nalisema ya kuwa nyumba yako, na nyumba ya baba yako itakwenda
mbele zangu milele; lakini sasa Bwana asema, Jambo hili na liwe mbali nami; kwa
maana wao wanaoniheshimu nitawaheshimu, na wao wanaonidharau watahesabiwa kuwa
si kitu.” Kwa msingi huo katikanuadilifu wetu ni muhimu kwetu
kukumbuka kuliheshimu jina la Mungu wetu uadilifu ni pamoja na kumtanguliza
Mungu katika maisha yetu yote!
8.
Uadilifu
unatusaidia sisi Kufikiri kwa undani kila aina ya tendo.
Tunapojifunza
kuhusu uadlifu katika ukristo haimaanishi tu kujua mema na mabaya bali pia
kuangalia mambo ambayo kibnadamu yanaweza kuleta utata mkubwa katika maisha ya
kila siku na hata kutufarakanisha na Mungu, kwa hiyo tunapijifunza kuhusu
uadilifu hatuangalii tu tendo lenyewe bali pia mtazamo wa mtu kuhusu hilo
tendo, nia ya mtu kuhusu hilo tendon a matokeo ya mtu kuhusu hilo tendo, kwa
mfano wote tunafahamu kuwa kutoa mimba ni dhambi, lakini wakati mwingine mahospitalini
linaweza likatokea jambo lenye utata na kutaka kuamua kama mama afe ili mtoto
aishi au mtoto aishi ili mama afe, au mimba imetunga katika eneo lisilo sahihi
na hivyo inahatarisha maisha ya mama mjamzito, mguu ukatwe ili kuokoa maisha ya
mtu na kadhalika kwa hiyo yako mazingira ambayo unaweza kujikuta katika
mazingira magumu na ukashindwa ni jambo gani la kuamua,
Kutoka 1:15-17 “Kisha
mfalme wa Misri akasema na wazalisha wa Waebrania, mmoja jina lake aliitwa
Shifra, na wa pili jina lake aliitwa Pua; akasema, Wakati mwazalishapo wanawake
wa Kiebrania na kuwaona wa katika kuzaa, ikiwa ni mtoto mwanamume, basi mwueni,
bali ikiwa ni mtoto mwanamke, na aishi. Lakini wale wazalisha walikuwa wakimcha
Mungu, wasifanye kama walivyoamriwa na huyo mfalme wa Misri, lakini
wakawahifadhi hai wale wanaume.”
Shifra na Puah
wazalisha wa waebrania walikuwa na wakati Mgumu wa kuamua kutii amri ya kifalme
na Mungu kwa kutikuwaua watoto, waliamua kumtii Mungu na kuwaacha hai watoto,
kuna matukio mengine yanaweza kutokea na yakakupa wakati mgumu sana kujua
uadilifu wake unatakaje
Hesabu 15:32-36 “Kisha
wakati huo wana wa Israeli walipokuwako jangwani, wakamwona mtu mmoja
akikusanya kuni siku ya Sabato. Hao waliomwona akikusanya kuni wakamleta kwa
Musa na Haruni, na kwa mkutano wote. Nao wakamweka kifungoni, maana, lilikuwa
halijasemwa atakalotendwa. Bwana
akamwambia Musa, Mtu huyo lazima atauawa; mkutano wote watampiga kwa mawe huko
nje ya marago. Basi mkutano wote wakampeleka nje ya marago, nao wakampiga kwa
mawe, akafa; kama Bwana alivyomwagiza Musa”
Yako maswala
mengine yanahitaji sana kujua mapenzi ya Mungu ili kuweza kujua undani wake na
maamuzi ambayo tunaweza kuyachukua katika kuyatafuta mapenzi ya Mungu
tunahitaji wakati mwingine kuwa na Muda wa kutafakari, wakati wa kutafakari
hatuna budi kufikiri
1. Neno la Mungu linasema nini
2. Ufahamu kuhusu ukweli na hali halisi
3. Ufahamu wetu wenyewe
4. Ushauri wa wengine
5. Mabadiliko ya mazingira
6. Mioyo yetu na dhamiri zetu
7. Roho yetu na nafsi zetu kama wanadamu
8. Uongozi wa Roho Mtakatifu
Baada ya
kuyafikiri hayo kwa undani Hekima ya kiungu inatuongoza katika kujua jambo
Fulani ni dhambi au la.
9.
Uadilifu
unatuweka katika nafasi ya kupokea Baraka mbalimbali.
Kuishi kwa
uadilifu ni kuishi kwa kumtii Mungu na Baraka zote asili yake ni utii, maandiko
yanatuthibitishia ya kuwa Tunapokea Baraka kubwa sana kwa kumtii Mungu ona
Mwanzo 12:1-3 “BWANA
akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba
yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha; nami nitakufanya wewe kuwa taifa
kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka;nami nitawabariki
wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia
watabarikiwa”.
Baraka za Mungu
zitamiminika kwetu ikiwa tutaishi sawa na maagizo yake ya uadilifu, lakini
laana kubwa zitatupata ikiwa hatutafuata au kuishi sawa na maagizo yake ya
uadilifu
Kumbukumbu la Torati 28:1-6 “Itakuwa
utakaposikia sauti ya Bwana, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo
yake yote nikuagizayo leo, ndipo Bwana, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya
mataifa yote ya duniani; na baraka hizi zote zitakujilia na kukupata usikiapo
sauti ya Bwana, Mungu wako. Utabarikiwa mjini, utabarikiwa na mashambani.
Utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, na uzao wa wanyama wako
wa mifugo, maongeo ya ng'ombe wako, na wadogo wa kondoo zako. Litabarikiwa kapu
lako, na chombo chako cha kukandia unga. Utabarikiwa uingiapo, utabarikiwa na
utokapo.”
Maandiko pia
yameidhinisha wazi kuwa kama hatutatii maagizo ya Mungu kuna laana chungu nzima
zitaambatana nasi katika maisha yetu
Kumbukumbu la Torati 28:15-21 “Lakini itakuwa
usipotaka kuisikiza sauti ya Bwana, Mungu wako, usiyaangalie kufanya maagizo
yake yote na amri zake, nikuagizazo hivi leo, ndipo zitakapokujia laana hizi
zote na kukupata. Utalaaniwa mjini, utalaaniwa na mashambani. Litalaaniwa kapu
lako na chombo chako cha kukandia. Utalaaniwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa
nchi yako, maongeo ya ng'ombe wako, na wadogo wa kondoo zako. Utalaaniwa
uingiapo, utalaaniwa na utokapo, Bwana atakuletea laana na mashaka, na
kukemewa, katika yote utakayotia mkono wako kuyafanya, hata uangamie na kupotea
kwa upesi; kwa ule uovu wa matendo yako, uliyoniacha kwayo.Bwana
atakuambatanisha na tauni, hata atakapokwisha kukuondoa katika nchi uingiayo
kwa kuimiliki.”
Isaya 1:18-20 “Haya,
njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa
nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu.Kama
mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi; bali kama mkikataa na kuasi
mtaangamizwa kwa upanga; maana kinywa cha Bwana kimenena haya”
Agano jipya
linatufundisha kuwa kuna Baraka mbalimbali za kila namna zinazowajia watu
wanaoishi maisha ya utii yaani maisha ya uadilifu moja ya Baraka hiyo ni furaha Yohana 15:10-11 “Mkizishika
amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za
Baba yangu na kukaa katika pendo lake. Hayo nimewaambia, ili furaha yangu iwe
ndani yenu, na furaha yenu itimizwe.”
Lakini sio hivyo
tu kunakuwa na furaha kubwa sana ya kumtii na kumpendeza Mungu kwa sababu kuna
hukumu pia mbele za Mungu 2Wakoritho 5:9-10
“Kwa hiyo, tena, ikiwa tupo hapa, au ikiwa hatupo
hapa, twajitahidi kumpendeza yeye. Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa
mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee ijara ya mambo
aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya.” na
Wakolosai 1;10 “mwenende kama ulivyo wajibu wenu
kwa Bwana, mkimpendeza kabisa; mkizaa matunda kwa kila kazi njema, na kuzidi
katika maarifa ya Mungu;”
Na ndio maana
maandiko hayawataki wakristo waishi chini ya kiwango wala kufuatisha viwango
vya dunia hii, sisi tunapaswa kuwa mstari wa mbele Warumi 12:2 “Wala msiifuatishe namna ya
dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi
ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.”
Kuishi kwa
uadilifu kunatupa kumpendeza Mungu na kunaleta Baraka nyingi sana katika maisha
yetu.
10.
Uadilifu
unatufunza jinsi ya kuwa na tabia za uungu.
Wanadamu
wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu Mwanzo
1:27 “Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano
wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba”.
Kuumbwa kwa
mfano wa Mungu ni kuumbwa katika uadilifu na sifa kama za Mungu, baada ya
anguko uadilifu wa mwanadamu uliathiriwa, hata hivyo Mungu ametufunza mfano
wake ili tuufuate, Mungu anabaki pake yake mwema na asiyebadilika na wa milele,
kiwango chake cha uadilifu anachokidai kwa wanadamu ni kile ambacho yeye mwenyewe
anacho na kwa sababu hiyo anahaki ya kukidai kutoka kwa wanadamu wote wa
tamaduni yoyote ile na historia. Matakwa haya haya yako kwa wingi katika neno
lake ingawaje vilevile ziko amri nyingine amezidai kwa watu maalumu na kwa
wakati maalumu, Mungu ni Pendo na hivyo anawataka watu wote kuwa na upendo
1Yohana
4:19-21 “Sisi twapenda kwa maana yeye alitupenda
sisi kwanza. Mtu akisema, Nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake, ni
mwongo; kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi kumpenda Mungu
ambaye hakumwona. Na amri hii tumepewa na yeye, ya kwamba yeye ampendaye Mungu,
ampende na ndugu yake.”
Mungu ni
mtakatifu na kwa sababu hiyo anayo haki ya kutudai kuwa watakatifu katika
mwenedno wetu wote
1Peter 1:15 -16 “bali
kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika
mwenendo wenu wote; kwa maana
imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.” Hali
kadhalika Mungu ni mwingi wa rehema hivyo nasi tunaagizwa kuwa na rehema, Luka 6:36 “Basi,
iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma.” Yeye ni mwaminifu
na hivyo ni haki yake kutuagiza nasi kuwa waaminifu na kutokutoa ushuhuda wa
uongo Tito 1:2 katika
tumaini la uzima wa milele, ambao Mungu asiyeweza kusema uongo aliuahidi tangu
milele; Kutoka 20:16 “Usimshuhudie jirani
yako uongo”. Mungu ni mwadilifu kwa msingi huo anaagiza sisi tuwe
waadilifu kama yeye alivyo anachokiagiza sio kigumu kwetu Mungu anajua kuwa
tunaweza kwa sababu alituumba tuwe waadilifu, mwanadamu wa kwanza alikuwa
mwadilifu ni mpaka Shetani alipoharibu sifa za uadilifu kwa msingi huo ni madai
sahihi ya Mungu kwetu kutuagiza kuishi kwa uadilifu na kuudai uadilifu.
Hitimisho!
Uadilifu ndio asili kamili ya
uanadamu, kila mwanadamu aliumbwa awe mwema kwa asili, tabia mbaya na mambo
yasiyopendeza yalikuwa ni matokeo ya dhambi, na ndio maana sio msingi wa
kuokolewa kwetu lakini ni msingi wa ubinadamu wetu, hivyo uwe umeokolewa au la
kila mmoja anapaswa kuishi kwa uadilifu hili ni jukumu la dunia nzima bila kujali
unaamini nini
Waefeso 2:1-10 “Nanyi mlikuwa wafu kwa sababu
ya makosa na dhambi zenu; ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya
ulimwengu huu, na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi
sasa katika wana wa kuasi; ambao zamani, sisi sote nasi tulienenda kati yao,
katika tamaa za miili yetu, tulipoyatimiza mapenzi ya mwili na ya nia, tukawa
kwa tabia yetu watoto wa hasira kama na hao wengine. Lakini Mungu, kwa kuwa ni mwingi
wa rehema, kwa mapenzi yake makuu aliyotupenda; hata wakati ule tulipokuwa wafu
kwa sababu ya makosa yetu; alituhuisha pamoja na Kristo; yaani, tumeokolewa kwa
neema. Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa
roho, katika Kristo Yesu; ili katika zamani zinazokuja audhihirishe wingi wa
neema yake upitao kiasi kwa wema wake kwetu sisi katika Kristo Yesu. Kwa maana
mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu,
ni kipawa cha Mungu; wala si kwa
matendo, mtu awaye yote asije akajisifu. Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika
Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili
tuenende nayo.”
Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote.