1Wathesalonike 3:6-10 “Lakini Timotheo alipotujia hivi sasa kutoka kwenu,
alituletea habari njema za imani yenu na upendo wenu, na ya kwamba mnatukumbuka
vema siku zote; mkitamani kutuona sisi vile vile kama sisi kuwaona ninyi. Kwa
sababu hiyo, ndugu, tulifarijiwa kwa habari zenu, katika msiba na dhiki yetu
yote, kwa imani yenu. Kwa kuwa sasa twaishi, ikiwa ninyi mnasimama imara katika
Bwana. Maana ni shukrani gani tuwezayo kumlipa Mungu kwa ajili yenu, kwa furaha
ile yote tunayoifurahia, kwa sababu yenu mbele za Mungu wetu; usiku na mchana
tunapoomba kwa juhudi tupate kuwaona nyuso zenu, na kuyatengeneza mapungufu ya imani
yenu? ”
Utangulizi:
Katika
maandiko hayo hapo juu, Paulo mtume anamshukuru Mungu kwa habari alizopokea
kutoka kwa Timotheo kuhusu wanafunzi kule Thesalonike kwamba wanaendelea vizuri
katika imani, na upendo huku wakimkumbuka Paulo mtume na watenda kazi wengine
ambao kwa kiwango Fulani walilazimika kuondoka Thesalonike kwa sababu ya dhiki
na mateso makubwa yaliyokuwa yakiwakabili kwaajili ya injili yaliyolazimisha
Paulo na Sillas na watenda kazi wengine kwenda katika mji wa Beroya mbele ya Thesalonike
kwaajili ya usalama wao
Matendo ya Mitume
17: 1-10 “Wakiisha
kupita kati ya Amfipoli na Apolonia wakafika Thesalonike, ambapo palikuwa na
sinagogi la Wayahudi. Na Paulo, kama ilivyokuwa desturi yake, akaingia mle
walimo, akahojiana nao kwa maneno ya maandiko sabato tatu, akiyafunua na
kuwaeleza ya kwamba ilimpasa Kristo kuteswa, na kufufuka katika wafu; na ya
kwamba, Yesu huyu ninayewapasha ninyi habari zake ndiye Kristo. Wengine
miongoni mwao wakaamini, wakashikamana na Paulo na Sila; na Wayunani waliomcha
Mungu, wengi sana, na wanawake wenye cheo si wachache. Na Wayahudi wakaona
wivu, wakajitwalia watu kadha wa kadha katika watu ovyo wasio na sifa njema,
nao wakakutanisha mkutano, wakafanya ghasia mjini, wakawaendea watu wa nyumba
ya Yasoni, wakataka kuwapeleka mbele ya watu wa mji; na walipowakosa,
wakamkokota Yasoni na baadhi ya ndugu mbele ya wakubwa wa mji, wakipiga kelele,
wakisema, Watu hawa walioupindua ulimwengu wamefika huku nako, na Yasoni
amewakaribisha; na hawa wote wanatenda mambo yaliyo kinyume cha amri za
Kaisari, wakisema na kwamba yupo mfalme mwingine, aitwaye Yesu. Wakafadhaisha
ule mkutano na wakubwa wa mji walipoyasikia hayo. Nao walipokwisha kumtoza
dhamana Yasoni na wenziwe wakawaacha waende zao. Mara hao ndugu wakawapeleka
Paulo na Sila usiku hata Beroya. Nao walipofika huko wakaingia katika sinagogi
la Wayahudi”
Kutokana na fujo zilizojitokeza waliamua kumuacha Timotheo ili aweze kuimarisha kanisa lililokuweko Thesalonike, Hata Timotheo alipowajia Paulo mtume na kuwataarifu habari ya kanisa lililokuwako Thesalonike, na jinsi wanavyokua katika imani na upendo na ya kuwa wanawakumbuka sana mitume na kuwa wanatamani kumuona tena, habari hii ilikuwa njema sana kwa Paulo mtume na alifurahi sana ya kuwa pamoja na mapito yote waliyoyapitia na majaribu na dhiki ilifurahisha kuwa wathesalonike walisimama katika imani, Paulo alifurahi na aliwajulisha katika waraka wake kuwa anaendelea kuwaombea na kwamba iko siku atawatembelea ili aweze kuwaimarisha katika imani, Kanisa la leo tunapaswa kufurahia kuona watu hususani watoto wachanga kiroho wakidumu na kusimama katika imani, ni jambo lanye kutia moyo kuiona kazi uliyoianzisha ikiendelea vizuri, watoto wetu wa kiroho wakikua na kuhubiri kama sisi, na kuomba kama sisi na wakiitetea imani kuandaa na kuhubiri vilevile kama wanavyojifunza kutoka kwetu jambo hili linaleta furaha kubwa tunajifunza somo hili twaishi ikiwa ninyi mnasimama imara kwa Bwana kwa kuzingatia vipengele viwili vifuatavyo:-
1. Maana
ya kusimama Imara
2. Umuhimu
wa kusimama Imara
Maana ya Kusimama imara!
Moja
ya furaha kubwa sana aliykuwa nayo Paulo mtume ni kuona watu wa Mungu
waliozaliwa kiroho katika hali ya dhiki nyingi sana wakisimama imara katika
imani maneno yanayotumika kuelezea kusimama imara katika kiyunani ni “STEKETE” neno hili katika kiyunani ni
neno la kijeshi lenye maana ya kuwa tayari kwa mapambano, ni kusimama kama
anavyosimama askari aliyepewa amri ya
tahadhari kuwa tayari kukabiliana na adui, hii maana yake wathesalonike
walikuwa tayari wako imara tayari ka mapambano dhidi ya shetani aliyekuwa
akilishambulia kanisa kwa dhiki na kwa mafundisho ya kiyahudi ya walimu wa
uongo waliokuwa wakifundisha kinyume na injili ya mtume Paulo, Wathesalonike
walikuwa tayari wameshajifunza ile kweli na walikuwa wameipokea imani katika dhiki
na walikuwa wako tayari kikakamavu kukabiliana na upinzani wa aina yoyote STEKETE ni anchor au attention, wao walikuwa kama askari ambao wako tayari
sasa kumkabili adui wako tayari hata kufa na kupoteza maisha yao wakiitetea
kweli na hawakuwa tayari kurudi nyuma na kuiacha imani, Paulo mtume alifurahi na luha hii anayoitumia
aliwahi kuwaambia wakoritho vilevile kwamba waimarike, wasitikisike, na
wamtumikie Bwana siku zote ona
1Wakoritho 15:58 “Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike,
mkazidi sana kutenda kazi ya Bwana sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu
yenu siyo bure katika Bwana.”
Maneno
ya kiingereza yanayotumika ni kama “steadfast,
immovable” hii ni hali ya kusimama imara bila kuyumbishwa mara kwa mara
Mungu anatamani tuwe katika hali kama hiyo hatupaswi kubabaika kwa namna yoyote
ile.
Wafilipi 1:27-30 “Lakini mwenendo wenu na uwe kama inavyoipasa Injili ya
Kristo, ili, nikija na kuwaona ninyi, au nisipokuwapo, niyasikie mambo yenu,
kama mnasimama imara katika roho moja, kwa moyo mmoja mkiishindania imani ya
Injili; wala hamwaogopi adui zenu, katika neno lo lote; kwao hao ni ishara
mathubuti ya kupotea, bali kwenu ninyi ni ishara ya wokovu, huo utokao kwa
Mungu. Maana mmepewa kwa ajili ya Kristo, si kumwamini tu, ila na kuteswa kwa
ajili yake; mkiwa na mashindano yale yale mliyoyaona kwangu, na kusikia kwamba
ninayo hata sasa”
unaona
Yesu Kristo na mitume wanafurahi kuwa na wanafunzi imara, hata mimi nataka watu
imara watu wanaosimama imara na kuitetea imani, wakiishindania injili, watu
ambao wako tayari hata kwaajili ya mateso, wakitwaa mfano wa mitume na manabii
ambao walivumilia magumu, leo hii ukisikia mtu ameiacha imani unaweza
kushangaa, mtu anaiacha imani kwaajili ya mwanamke tu mwenye mapaja makubwa,
mtu anaisha imani kwaajili ya chipsi na soda, mtu anaiacha imani kwa kukosa
mume wa kumuoa, mtu anaiacha imani kwa sababu uchumba umevunjika, mtu anaiacha
imani kwa sababu za kipuuzi sana ambazo ni ngumu hata kumueleza Mungu na kujaza
katika faili lake Nyakati za kanisa la kwanza watu walipambana na kusimama
kidete wakiitetea imani, lugha ya ujenzi ya kanisa sio lele mama ni lugha ya
kivita nitalijenga kanisa langu juu ya mwamba na wala malango ya kuzimu
hayataliweza leo hii ni tofauti, watu hawamjui shetani wala hajawajui namna ya
kzuipinga nhila zake watu wamekuwa laini kama mlenda waklichukuliwa na upepo wa
kila aina wa imani, hawana hata uwezo wa kupambanua jema wala baya, Yesu
alikuwa hana mpango na watu dhaifu hata siku moja Yesu alikuwa ana mpango na
watu watakaojenga nyumba zao juu ya mwamba ambao hakuna upepo utaziangusha
nyumba hizo,
Mathayo 7:24-27 “Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya,
atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; mvua
ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa
maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba. Na kila asikiaye hayo maneno yangu
asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya
mchanga; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile,
ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa.”
Umuhimu wa kusimama imara
Lilikuwa
ni jambo la kufurahisha sana kwamba Kanisa la Thesalonike watu wanasimama imara
licha ya kuwa walizaliwa katika hali ya dhiki na majaribu makali, Lakini baada
ya kumuacha Timotheo na kuliimarisha kanisa anakuja na habari njema sio tu
imnaonekana kumfurahisa Paulo mtume bali inamfurahisha sana Mungu Mungu
hafurahishi na watu vuguvugu katika imani anataka watu wawe motoooo watu
wanaositasita Mungu hapendezwi nao ona
Waebrania 10:38-39 “Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani; Naye
akisita-sita, roho yangu haina furaha naye. Lakini sisi hatumo miongoni mwao
wasitao na kupotea, bali tumo miongoni mwa hao walio na imani ya kutuokoa roho
zetu.”
Wakristo
wa kweli hawapaswimkuwa watu wenye kusitasita Mungu hapandezwi na watu wasitao
mwandishi wa kitabu cha waebrania anaeleza kuwa sisi hatuko miongoni mwao
wasitao, Mungu ambariki kila mtu asiyesitasita katika imani na kuishi maisha ya
uvuguvugu ambayo yatapalekea kutapikwa na Yesu Kristo
Ufunuo 3:15-16 “Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto;
ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto. Basi, kwa sababu una uvuguvugu,
wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.”
Mungu
anataka mtu aliye moto, anayesimama imara, sio anayetetemeka vitani kama
hatutazingatia swala la kusimama imara tutatapikwa na mfumo utatukataa,
Wakristo bado tunakabiliwa na imani potofu, bado shetani analishambulia kanisa
kwa namna nyingi sana na leo tumekuwa na wakristo wepesi sana wepesi mno, Mungu
atupe neema ya kusimama imara katika bwana katika jina la Yesu Mwana wa Mungu
akliye hai amen!
Na Rev. Innocent Kamote.
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima! # 0718990796
#
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni