Mwanzo 15:1 “Baada ya mambo
hayo neno la BWANA likamjia Abramu katika njozi, likinena, Usiogope, Abramu,
Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana.”
Utangulizi:
Mojawapo ya
sehemu muhimu sana katika maandiko ambapo unaweza kupata faraja ya kiungu ni
pamoja na eneo hili ambapo tunasoma kuwa Mungu alisema na Abraham katika njozi
na kumtia Moyo kwa maneno makubwa matatu muhimu sana, USIOGOPE, MIMI NI NGAO
YAKO NA THAWABU YAKO KUBWA SANA, Maneno haya ya muhimu ambayo ndio sehemu kuu
ya somo letu kwa leo yana umuhimu mkubwa sana, Sio kwa Abrahamu tu bali na
kwetu sisi katika nyakati hizi za leo!
Mwanzo 15:1 “Baada ya mambo
hayo neno la BWANA likamjia Abramu katika njozi, likinena, Usiogope, Abramu,
Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana.”
Kimsingi Biblia
inapotumia maneno Neno la Bwana likamjia likisema, hapo maana yake Mungu
anazungumza na Abrahamu kama nabii, kwa hiyo kimsingi lugha hii ni ya kinabii
na unaweza kuiona Lugha hii ikitumika katika vitabu vya kinabii, lakini sio hivyo
tu Neno la Bwana pia hutumika kumwakilisha Kristo, na kwa sababu hiyo maneno
haya ya kutia moyo yanazungumza sio na Abraham tu bali na kila mmoja anayeisikia
sauti hii kwa msingi huo tutajifunza somo hili MIMI NI NGAO YAKO NA THAWABU YAKO KUBWA SANA Kwa kuzingatia
vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Kuondolewa kwa Hofu za maisha
·
Ahadi ya Ulinzi wa Mungu
·
Ahadi ya Mafanikio kwa kuwa na
Mungu
Kuondolewa kwa Hofu za Maisha!
Mwanzo 15:1 “Baada ya mambo
hayo neno la BWANA likamjia Abramu katika njozi, likinena, Usiogope, Abramu,
Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana.”
Ni neno lenye
kutia moyo kuliko namna tunavyoweza kufikiri, Katika maandiko haya kwanza
kabisa Mungu anataka kumuondoa hofu Abrahamu kutokana na hofu ya maisha yake.
Biblia inaanza kwa kusema “baada ya
mambo hayo…” Neno la bwana lilimjia
katika Njozi kusema Usiogope, hii maana yake ni kuwa kulikuwa na aina Fulani ya
hofu katika maisha ya Abrahamu, Biblia inasema baada ya mambo haya ni yepi?
Abrahamu alikuwa ametoka kupigana na wafalme kadhaa wa kanaani na kumuokoa
Nduguye Lutu, Pamoja na mfalme wa Sodoma, na Gomorah kwa kuwa Lutu aliishi huko
akamuokoa pamoja na mali zake zote,Lakini vilevile alimsaidia mfalme wa Salem na wengineo ona
Mwanzo 14:1-19 “Ikawa siku za
Amrafeli mfalme wa Shinari, na Arioko mfalme wa Elasari, na Kedorlaoma mfalme
wa Elamu na Tidali mfalme wa Goimu, walifanya vita na Bera mfalme wa Sodoma na
Birsha mfalme wa Gomora, na Shinabu mfalme wa Adma, na Shemeberi mfalme wa
Seboimu, na mfalme wa Bela, ndio Soari. Hawa wote wakakutana panapo bonde la
Sidimu, kwenye Bahari ya Chumvi. Miaka kumi na miwili walimtumikia Kedorlaoma,
hata mwaka wa kumi na tatu wakaasi. Na mwaka wa kumi na nne akaja Kedorlaoma na
wafalme waliokuwa pamoja naye, wakawapiga Warefai katika Ashteroth-karnaimu, na
Wazuzi katika Hamu, na Waemi katika Shawe-kiryathaimu, na Wahori katika mlima
wao Seiri, mpaka Elparani iliyo karibu na jangwa. Kisha wakarudi wakaja mpaka
Enmisfati, ndio Kadeshi, wakapiga nchi yote ya Waamaleki, na Waamori waliokaa
Hasason-tamari. Mfalme wa Sodoma, na mfalme wa Gomora, na mfalme wa Adma, na
mfalme wa Seboimu, na mfalme wa Bela, ndio Soari, wakatoka wakapanga vita
panapo bonde la Sidimu; wapigane na Kedorlaoma mfalme wa Elamu, na Tidali
mfalme wa Goimu, na Amrafeli mfalme wa Shinari, na Arioko mfalme wa Elasari,
wafalme wanne juu ya wale watano. Na bonde la Sidimu lilikuwa limejaa mashimo
ya lami. Nao wafalme wa Sodoma na Gomora wakakimbia, wakaanguka huko, nao
waliosalia wakakimbia milimani. Wakachukua mali zote za Sodoma na Gomora na vyakula
vyao vyote, wakaenda zao. Wakamtwaa Lutu, mwana wa nduguye Abramu, aliyekaa
huko Sodoma, na mali yake, wakaenda zao. Mtu mmoja aliyeponyoka akaenda,
akampasha habari Abramu Mwebrania; naye amekaa panapo mialoni ya Mamre, yule
Mwamori, ndugu ya Eshkoli, na ndugu ya Aneri, na hao walikuwa wamepatana na
Abramu. Abramu aliposikia ya kwamba nduguye ametekwa mateka, akawapa silaha
vijana wake, waliozaliwa katika nyumba yake, watu mia tatu na kumi na wanane,
akawafuata mpaka Dani. Akajipanga apigane nao usiku, yeye na watumwa wake,
akawapiga, akawafukuza mpaka Hoba, ulioko upande wa kushoto wa Dameski. Naye
akarudisha mali zote, akamrudisha na Lutu nduguye na mali zake, na wanawake
pia, na watu. Abramu aliporudi kutoka kumpiga Kedorlaoma na wale wafalme waliokuwa
pamoja naye, mfalme wa Sodoma akatoka amlaki katika bonde la Shawe, nalo ni
Bonde la Mfalme. Na Melkizedeki mfalme wa Salemu akaleta mkate na divai, naye
alikuwa kuhani wa Mungu Aliye juu sana.
Akambariki, akasema, Abramu na abarikiwe na Mungu Aliye juu sana, Muumba
mbingu na nchi ”
Abrahamu alikuwa amepata ushindi mkubwa sana
dhidi ya maadui zake, aliwashinda wafalme wenye nguvu na wakubwa sana tena
waliokuwa wameungana lakini nadhani alipokuwa ametulia tayari alikuwa na mawazo
kuwa hatakuwa na amani kwani adui zake watajipanga kwa vita tena dhidi yake na
hasa kwa sababu yeye ni mgeni katiika
incho ya wakanaani bila shaka akiwa na mawazo haya, Ni wazi sana katika vita za
kizamani katika biblia pale unapopata ushindi mkubwa haimaanishi kuwa uko
salama kwani ilikuwa lazima adui akajipange tena kwa mbinu nyingine na ili
aweze kuja tena kwa namna nyingine kivita, ni katika utaratibu kama huu adui
yetu shetani huwa ana jipanga tena anapokuwa ameshindwa vita ili kuja kwa mbinu
nyingine na kutushambulia kwa sababu kama hizi lazima Abrahamu alikuwa na
mawazo kuwa huenda vita kali zitamkabili tena, Kutoka kwa wapinzani wake na
huenda watakuja na timu kubwa zaidi,
sasa Neno la Mungu linamjia na kumtaka asiogope, aache kuwaza dhidi ya
vita kwani Mungu aliyempa ushindi
anamuhakikishia kuwa hakuna kitakachoweza kusimama mbele yake tena Mungu
alikuwa akimthibitishia Abrahamu kuwa yeye atakuwa pamoja naye na kuwa asiogope
sawa tu na namna alivyomwambia Yoshua, ona :-
Yoshua 1: 5-9 “Hapatakuwa mtu ye yote atakayeweza kusimama mbele yako
siku zote za maisha yako; kama nilivyokuwa pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa
pamoja na wewe; sitakupungukia wala sitakuacha. Uwe hodari na moyo wa ushujaa,
maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya
kwamba nitawapa. Uwe hodari tu na ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na
sheria yote aliyokuamuru Musa mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kuume,
au wa kushoto, upate kufanikiwa sana kila uendako. Kitabu hiki cha torati
kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate
kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo
utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana. Je! Si mimi
niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa
kuwa Bwana, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako.”
Wakati wote
Mungu anapotaka kuthibitisha kuwa yuko pamoja nasi anatuita kwa majina yetu ili
kwamba akutie Moyo haijalishi ni hofu ya aina gani iko mbele yako jambo kubwa
na la msingi ni kuwa usiogope haijalishi umezungukwa ana adui pande zote au
wanaojipanga kukushambulia ni wenye nguvu au ni wengi bado kwa Mungu hawawezi
kutoboa na kufanikiwa dhidi yako hivyo usiogope hapa Mungu hataki wewe na mimi
tuwe na hofu za maisha yetu, Yuko Mungu anayetulinda anayejishughulisha sana na
mambo yetu hivyo hatupaswi kuogopa, Mpenzi Mungu amenituma nikuhakikihie kuwa
usiogope, usiogope, usiogope.
Ahadi ya Ulinzi wa Mungu
Baada ya Mungu
kumuondolea Hofu Abrahamu kwa kumwambia asiogope Mungu anamuhakikishia Abrahamu
ulinzi, anamthibitishia kuwa yeye ni ngao yake na hivyo atamlinda dhidi ya adui
zake wote haijalishi ni wengi kiasi gani na wala haijalishi wana nguvu kwa
kiwango gani kama jinsi ambavyo Yesu Kristo ni ngao yetu ndivyo Mungu
anavyomthibitishia Abrahamu na sisi kuwa yeye ni ngao yetu na kuwa yuko pamoja
nasi Maandiko yanamtaja Mungu kama ngao yetu mara nyingi sana hususani katika
zaburi ona
Zaburi 3:1-3 “Bwana,
watesi wangu wamezidi kuwa wengi, Ni wengi wanaonishambulia, Ni wengi
wanaoiambia nafsi yangu, Hana wokovu huyu kwa Mungu. Na Wewe, Bwana, U ngao
yangu pande zote, Utukufu wangu na mwinua kichwa changu”
Zaburi 7:9-11 “Ubaya wao
wasio haki na ukome, Lakini umthibitishe mwenye haki. Kwa maana mjaribu mioyo
na viuno Ndiye Mungu aliye mwenye haki. Ngao yangu ina Mungu, Awaokoaye wanyofu
wa moyo. Mungu ni mwamuzi mwenye haki, Naam, Mungu aghadhibikaye kila siku.”
Zaburi 28:7-8 “Bwana ni
nguvu zangu na ngao yangu. Moyo wangu umemtumaini, Nami nimesaidiwa; Basi, moyo
wangu unashangilia, Na kwa wimbo wangu nitamshukuru. Bwana ni nguvu za watu
wake, Naye ni ngome ya wokovu kwa masihi wake”
Zaburi 33:19-21 “Yeye
huwaponya nafsi zao na mauti, Na kuwahuisha wakati wa njaa. Nafsi zetu
zinamngoja Bwana; Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu. Maana mioyo yetu
itamfurahia, Kwa kuwa tumelitumainia jina lake takatifu.”
Zaburi 84:9-12 “Ee Mungu,
ngao yetu, uangalie, Umtazame uso masihi wako.Hakika siku moja katika nyua zako
Ni bora kuliko siku elfu. Ningependa kuwa bawabu nyumbani mwa Mungu wangu,
Kuliko kukaa katika hema za uovu. Kwa kuwa Bwana, Mungu, ni jua na ngao, Bwana
atatoa neema na utukufu. Hatawanyima kitu chema Hao waendao kwa ukamilifu. Ee
Bwana wa majeshi, Heri mwanadamu anayekutumaini Wewe.”
Zaburi 89:18 “Maana ngao
yetu ina Bwana, Na mfalme wetu ni wake Mtakatifu wa Israeli.”
Muda usingeweza
kutosha kuziona ahadi za Mungu kwa kila Mtu amchaye na kumtegemea yeye kama
Mungu alivyomwambia Abrahamu na kumuahidi kuwa yeye ni ngao yeke, Mungu ni ngao
kwa kila anayemtegemea ukimtegemea yeye Mungu hatakuangusha wala hatakuacha
atakupa ushindi mmoja mpaka ushindi mwingine na atakulinda hakuna silaha
itafanikiwa juu yako, hakuna mbinu itatoboa dhidi yako Mungu atakutetea kama
alivyomthibitishia Abrahamu leo neno la Mungu linatuthibitishia ulinzi wetu na
kutueleza wazi kuwa tunalindwa na nguvu za Mungu
1Petro
1:5 “Nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya
imani hata mpate wokovu ulio tayari kufunuliwa wakati wa mwisho.”
Ahadi ya Mafanikio kwa kuwa na Mungu.
Mwanzo 15:1 “Baada ya mambo
hayo neno la BWANA likamjia Abramu katika njozi, likinena, Usiogope, Abramu,
Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana.” Licha ya Mungu
kumwambia Abrahamu asiogope na kuwa yeye ni ngao yake lakini Mungu vilevile
alimthibitishia Abrahamu kuwa yeye ni thawabu yake kubwa sana, kwa nini ?
Abrahamu aliteka nyara nyingi sana ambazo aliruhusu wafalme jirani wazichukue,
sio hivyo tu Abraham alihakikisha kuwa mali za wenyewe za wafalme wote
waliokuwa wamepora na mwana wa ndugu yake Lutu wote walirejeshewa mali zote
zilizotekwa nyara na maadui, Jambo hili lilionekana kama ujinga Abrahamu
hakutaka mwanadamu ajisifu kuwa ametajirishwa na wanadamu Abrahamu aliamua
kuacha mali na kijitegemeza kwa Mungu ona
Mwanzo 14:21-23 “Mfalme wa
Sodoma akamwambia Abramu, Nipe mimi hao watu, na hizo mali uchukue wewe. Abramu
akamwambia mfalme wa Sodoma, Nimeinua mkono wangu kwa BWANA, Mungu Aliye juu
sana, Muumba mbingu na nchi, ya kuwa sitatwaa uzi wala gidamu ya kiatu wala cho
chote kilicho chako, usije ukasema, Nimemtajirisha Abramu;”
Abrahamu alikuwa
amejiapiza kwa Mungu nimeinua mkono wangu kwa Mungu maana yake nimeapa,
hakutaka kuwa na mali ambazo asili yake ni wanadamu mali hizi zingeliweza
kuleta utajiri mkubwa sana huenda alionekana mjinga kwa kuzikataa, Abrahamu
hakutaka mali za udhalimu, Mungu alikuwa amemuahidi kuwa atambariki, kwa hiyo
asili ya Baraka zake ilipaswa kuwa Mungu mwenyewe na sio mali za udhalimu au
zinazotokana na kuteka nyara !
Mungu alimtia
Moyo Abrahamu kuwa Yeye ni thawabu yake kubwa sana hii ilikuwa ni ahadi kubwa
ya kuwa Mungu atamfanikisha Abrahamu kwa neema na utukufu mkubwa sana kwani
kuwa na Mungu ambaye ndio chanzo cha utajiri ni muhimu zaidi kuliko kuwa na
utajiri usiotokana na Mungu, chanzo
chake kikuu na mafanikio ni MUngu, Neno la Mungu leo linatukumbusha kuwa Yesu
kwetu ni thawabu yetu kubwa sana ni utajiri mkubwa sana ni utoshelevu wa hali
ya juu kuwa na Yesu kunalipa kuliko kuwa na mali, magari na nyumba na fedha
ambazo asili yake sio Yesu, kuwa na mali na kutokuwa na Yesu machoni pa Mungu
ni uduni,umasikini na uchi, Lakini kumpata Yesu ni zaidi
Ufunuo 3:17-18 “Kwa kuwa
wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya
kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi. Nakupa
shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na
mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya
kujipaka macho yako, upate kuona.”
Yesu anatushauri
kuwa utajiri wa kweli ni kununua kwake yaani ni kumuamini yeye ambaye ndio
chanzo cha utajiri wa kudumu, Mungu ametuahidi mafanikio makubwa sana hakuna
kitu atatunyima yeye anasema tafuteni kwanza ufalme wa Mungu na haki yake na
mengine yote mtazidishiwa Hakuna sababu ya kujisumbukia na kutafuta mali na
fedha na mavazi na chakula tusumbuke kumtafuta Yesu na mambo mengine yote
mtazidishiwa
Mathayo 6:25-33 “Kwa
sababu hiyo nawaambieni, Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini; wala
miili yenu, mvae nini. Maisha je! Si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya
mavazi? Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala
hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora
kupita hao? Ni yupi kwenu ambaye
akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja? Na mavazi, ya nini
kuyasumbukia? Fikirini maua ya mashamba, jinsi yameavyo; hayafanyi kazi, wala
hayasokoti nami nawaambia, ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote
hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo. Basi, ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya
kondeni, yaliyopo leo, na kesho hutupwa kalibuni, je! Hatazidi sana kuwavika
ninyi, enyi wa imani haba? Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe
nini? Au Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba
yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni kwanza
ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.”
Yesu ni thawabu yetu kubwa sana
Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni