Jumanne, 27 Juni 2023

Agano la Chumvi!


2Nyakati 13:5 “je! Haikuwapasa kujua ya kwamba Bwana, Mungu wa Israeli, alimpa Daudi ufalme juu ya Israeli milele, yeye na wanawe kwa agano la chumvi?” 



Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa Chumvi ni moja ya madini muhimu sana duniani, na kuwa chumvi ina matumizi mengi na makubwa zaidi ya kunogesha ladha ya chakula, Chumvi imekuwa ikitumika katika jamii na tamaduni mbalimbali duniani kwa matumizi mengi tofauti tofauti, Neno Mshahara kwa kiingereza ni “SALARY” inasemekana neno hili chimbuko lake ni neno “Salt – Money” likimaanisha fedha inayostahili hela ya chumvi kwa askari wa kirumi, yaani malipo ya mshahara yalikuwa ni kwaajili ya kununulia chumvi, Kutokana na umuhimu wa chumvi katika nyakati hizo!

Chumvi ilitumika nyakati za zamani kumaanisha urafiki wa kudumu, au kutimiza ahadi miongoni mwa watu na kwa wayunani (Greeks) waliihesabu chumvi kuwa ina asili ya uungu, Katika tamaduni za kiarabu hata sasa endapo watu wawili walipatana jambo walijiapiza na kulamba chumvi wakimaanisha ni patano la kulindana milele, ni ishara ya uaminifu wa kudumu na hata kama ikitokea kuwa wamekuwa maadui au walikuwa maadui walipaswa kuheshimu kulindana huko endapo walifanya patano au agano la chumvi.

Nyakati za agano la kale walipofanya agano la patano katika ya mtu na mtu mapatano hayo yaliweza kuthibitishwa na kulamba chumvi mbele ya mashahidi na tendo hili lingemaanisha kuwa ni patano la kudumu, Ahadi ya kudumu milele, ahadi isiyoweza kuvunjika na kama mtu ataivunja aharibikiwe vibaya na kupata madhara makubwa sana.

Kwa msingi huo unapoona katika maandiko 2Nyakati 13:5 “je! Haikuwapasa kujua ya kwamba Bwana, Mungu wa Israeli, alimpa Daudi ufalme juu ya Israeli milele, yeye na wanawe kwa agano la chumvi?Mfalme Abiya Hapa alikuwa akizungumza na Israel na Yeroboamu kuwaonya wasipigane naye na kuwajulisha kuwa Mungu yuko Pamoja na ufalme wa agano na Daudi kwa sababu lilikuwa ni agano la chumvi, Abiya aliwathibitishia Israel kuwa watapigwa Na kamwe hawataweza kushindana na ufalme wa ukoo wa Daudi kwa vile ana agano la chumvi na Mungu, akimaanisha agano thabiti, lisiloweza kubatilika la ahadi ya Mungu aliyoiweka kwa Daudi na uzao wake milele na kwamba hakuna mtu anaweza kuiharibu.

Nyakati za agano la kale maandiko yaliamuru kila aina ya sadaka za mbegu na nafaka ziambatanishwe na chumvi ili kufanya “agano la chumvi” kila aina ya sadaka ya nafaka iliambatanishwa na chumvi angalia

Mambo ya walawi 2:13 “Tena, kila toleo la sadaka yako ya unga utalitia chumvi; wala usiiache sadaka yako ya unga kupungukiwa na chumvi ya agano la Mungu wako; utatoa chumvi pamoja na matoleo yako yote.”  

Aidha Mungu alipowachagua wana wa walawi kuwa makuhani wake kwa vile hawakuwa na urithi Mungu aliwapatia chakula kupitia sadaka zilizoletwa na watu wake na jambo hili Mungu aliliita “Agano la Chumvi”

Hesabu 18:19 “Sadaka zote za kuinuliwa za vitu vitakatifu, wana wa Israeli wavisongezavyo kwa Bwana, nimekupa wewe na wanao na binti zako pamoja nawe, ni haki yenu ya milele; ni agano la chumvi la milele mbele za Bwana kwa ajili yako, na kizazi chako pamoja nawe.

Hapa Mungu alikuwa anamaanisha kuwa patano hilo au agizo hilo ni la kudumu na halitaweza kubatilishwa ni agano la chumvi! Vilevile ukuhani wake na kabila ya lawi ni wa milele. Kwa msingi huo utaweza kuona kuwa wzo kuhusu chumvi lilipewa umuhimu mkubwa sana katika maandiko, Leo chumvi inapatikana kwa urahisi katika tamaduni nyingi ikiwa na umuhimu uleule japo inaweza isihitajike sana katika uhifadhi kutokana na teknolojia ya kuwepo kwa mafriji majumbani, lakini nyakati za Biblia chumvi ilikuwa na umuhimu mkubwa sana kwaajili ya kutunzia vitu visiharibike kama tu ilivyokwa mafriji leo, na ndio maana utaweza kuona katika mifano ya Yesu aliwataja wanafunzi wake au kanisa kuwa ni chumvi ya ulimwengu akimaanisha vilevile kuwa usalama wa ulimwengu unategemea sana uwepo wa kanisa ili kuutunza usiharibiwe na uovu

Mathayo 5:13 “Ninyi ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu.” Kwa msingi huo neno la Mungu linapozungumzia kuhusu agano la chumvi linazungumzia katika uelewa kuwa ni uaminifu wa Mungu katika kutunza ahadi zake kwa mwanadamu bila kuvunjia, ni tabia ya Mungu kuendelea kuwa mwema hata katika mazingira ya udhaifu wa kibinadamu yeye anabaki kuwa mwaminifu.

Chumvi inahusishwa na umilele

Chumvi imekuwa ikijulikana tangu zamani kuwa inauwezo wa kutunza vitu visiharibike, ina uwezo wa kulinda, na inawezekana Mungu aliamuru matumizi ya chumvi katika kutunza nyama ili isiharibike idumu lakini iwe na ladha na hivyo chumvi ilikuwa kitu cha thamani kwa makuhani ambao waliishi kwa kuitegemea sadaka za kila siku.

Wazo la agano la Chumvi linabeba uthamani mkubwa kutokana na uwezo wake wa kutunza kitu kwa muda mrefu na wa kudumu bila kuharibika, Nyakati za Biblia na mpaka wakati wa Kristo Chumvi ilikuwa ni bidhaa ya thamani kubwa sana, Na kwa msingi huo ndio maana utaweza kuona Yesu akiwaambia wanafunzi wake kuwa ninyi ni “Chumvi ya ulimwengu” akimaanisha kuwa watu waliomuamini Yeye wanathamani kubwa sana Duniani kwaajili ya kuitunza na kuishawishi dunia kuishi katika haki sawa na injili yake aidha Yesu alitaka kuonyesha kuwa wanafunzi wake wanapaswa kuwa watu watakaodumu na ambao ni vigumu kuharibiwa! 

Mathayo 5:13 “Ninyi ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu.”

Yesu hatarajii awaye yote ambaye amemuamini aharibike na kufikia hatua ya kushindwa kabisa kuwa ladha kwa ulimwengu, Chumvi yenyewe ni ngumu sana kuharibika lakini vilevile hufanya vitu vingine visiharibike, chumvi inadumu, chumvi inazuia uharibifu, chumvi inaleta ladha, chumvi ni tiba inaleta uponyaji, chumvi inadumisha, ingawa tuna namna nyingine nyingi leo za kuzuia vitu visiharibike lakini bado chumvi imekuwa ni njia bora na ya kale zaidi ya kuhifadhi vitu visiharibike. Kwa msingi huo unapozungumza chimvi unazungumzia kudumu milele na kutokuharibiwa!

Chumvi pia katika mafundisho ya Yesu Kristo ilihusika kumaanisha agano la amani na watu wote, kwamba tuwe na moyo wa chumvi ndani yetu kwa kuwa na amani sisi kwa sisi, kuwa na uhusiano usioharibika, Kristo anatarajia kuwa wanafunzi wake watakuwa watu wenye amani ya kudumu na isiyoweza kuharibika kwa namna yoyote, kwa msingi huo kwa Mungu anashangaza sana pale wanafunzi wake wanapoharibu mahusiano, wanapokuwa na bifu la kudumu, wanaposhindwa kusameheana wanaposhindwa kupatana na wanaposhindwa kuwa na amani wao kwa wao na hata ndoa ya kikristo kuvunjika pia ni sawa na chumvi kuharibika ni jambo baya ambalo kimsingi ni jambo lisilotarajiwa litokee!

Marko 9: 50 “Chumvi ni njema; lakini chumvi ikiwa si chumvi tena, mtaitia nini ikolee? Mwe na chumvi ndani yenu, mkakae kwa amani ninyi kwa ninyi” 

Hivyo chumvi ni agano la Amani chumzvi haitarajiwi kuharibika hcumvi haitarajiwinkutikufaa tena chumvi haitarajiwi kuruhusu uharibifu.

AGANO LA CHUMVI.

Neno agano la chumvi limejitokeza mara tatu katika maandiko, huenda inamaanisha kuhusu utatu, kwa maana nyingine linamuhusisha Mungu, Ukiacha andiko la Msingi sehemu nyingine ni

Hesabu 18:19 “Sadaka zote za kuinuliwa za vitu vitakatifu, wana wa Israeli wavisongezavyo kwa Bwana, nimekupa wewe na wanao na binti zako pamoja nawe, ni haki yenu ya milele; ni AGANO LA CHUMVI LA MILELE mbele za Bwana kwa ajili yako, na kizazi chako pamoja nawe.

Na utaweza kuona tena katika Walawi 2:13 “Tena, kila toleo la sadaka yako ya unga utalitia chumvi; wala usiiache sadaka yako ya unga kupungukiwa na chumvi ya agano la Mungu wako; utatoa chumvi pamoja na matoleo yako yote.”

Mungu alifanya maagano kadhaa na watu wake mbalimbali akitumia alama mbalimbali muhimu za kupita kawaida.

·         Agano la Mungu na Nuhu lilihusisha upinde wa Mvua.

 

Mwanzo 9:15-17 “nami nitalikumbuka agano langu, lililoko kati yangu na ninyi, na kila kiumbe hai katika wote wenye mwili, wala maji hayatakuwa gharika tena kuwaharibu wote wenye mwili. Basi huo upinde utakuwa winguni; nami nitauangalia nipate kulikumbuka agano la milele lililoko kati ya Mungu na kila kiumbe hai katika wote wenye mwili kilichoko katika nchi. Mungu akamwambia Nuhu, Hii ndiyo ishara ya agano nililoliweka kati yangu na wote wenye mwili walioko katika nchi”.

               

·         Agano la Mungu na Ibrahimu lilihusisha Nyota na tohara ya govi

 

Mwanzo 15:5, 18 “Akamleta nje, akasema, Tazama sasa mbinguni, kazihesabu nyota, kama ukiweza kuzihesabu. Akamwambia, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako.”, Siku ile BWANA akafanya agano na Abramu, akasema, Uzao wako nimewapa nchi hii, kutoka mto wa Misri mpaka huo mto mkubwa, mto Frati,

 

Matendo 7:8 “Akampa agano la tohara; basi Ibrahimu akamzaa Isaka, akamtahiri siku ya nane. Isaka akamzaa Yakobo. Yakobo akawazaa wale kumi na wawili, wazee wetu.”

 

·         Agano la Mungu na wana wa Israel kupitia Musa lilihusisha  amri kumi katika Mawe.

 

Kutoka 34:28 “Naye alikuwa huko pamoja na BWANA siku arobaini na masiku yake; hakula chakula, wala hakunywa maji. Naye akaandika katika hizo mbao, hayo maneno ya maagano, hizo amri kumi.”

 

·         Agano la Mungu na Mfalme Daudi lilihusisha Chumvi.

 

2Nyakati 13:5 je! Haikuwapasa kujua ya kwamba Bwana, Mungu wa Israeli, alimpa Daudi ufalme juu ya Israeli milele, yeye na wanawe kwa agano la chumvi?

 

Makusudi makubwa ya somo hili ni kuzungumzia agano hili la chumvi na matumizi ya chumvi katika maeneo mbalimbali ya kiibada kama tunavyoweza kuona katika siku za karibuni kukiwa na matumizi makubwa sana ya chumvi maarufu kama chumvi ya upako!

Matumizi ya Chumvi.

Kwaajili ya kuleta ladha – Chumvi inatumika katika kuleta ladha na utamu katika chakula au kinywaji au kitu kingine kwa kuchanganya na chumvi na kuleta ladha

Kwaajili ya Kutunza – Chumvi inatumika kuhifadhi na kutunza nyama na samaki na kadhalika visioze

Kwaajili ya tiba – Chumvi hutumika kukausha, kuandaa kwaajili ya kutunza kitu kisiharibike, kwa kusafishia na kutakasa.

Kwaajili ya uwiano – ukiizidisha hainogi, ukiipunguza hainogi ni mpaka iwekwe kwa kiwango chenye kuwiana

Umuhimu wa chumvi katika maisha ya Ukristo.

Mathayo 5:13aNinyi ni chumvi ya ulimwengu” hii ina maana gani, Biblia inatufundisha sisi tuliomuamini Kristo kwamba tunapaswa kuwa chumvi ya ulimwengu, tupo hapa duniani kwa wakati kuhakikisha kuwa tunautunza ulimwengu uliooza kwa dhambi  na kuuponya kutoka katika chuki dhidi ya Mungu na mambo ya Mungu.

Sifa halisi za Chumvi na maana zake za kiroho.

Huwezi kuila Chumvi peke yake!

Jaribu kuchukua kijiko kimoja cha chumvi kisha dumbukiza mdomoni kwako, hutaweza kuimeza, Chumvi haiko kwaajili ya kuliwa yenyewe ni lazima uiweke katika kitu kingine ili uweze kuitumia pamoja na kitu hicho, Ni lazima uitumie chumvi kwa kiwango sahihi yaani kinachotosha kulingana na kitu unachokula na hapo ndipo unapoweza kukifurahia, ukiweka kidogo hutaweza kufurahia na ukizidisha utapoteza ladha lazima itumiwe vizuri kwa uwiano sahihi. Biblia inasema katika

Wakolosai 4:6Maneno yenu yawe na neema siku zote, yakikolea munyu, mpate kujua jinsi iwapasavyo kumjibu kila mtu.

Maneno yetu kukolea munyu yaani chumvi maana yake kujawa na kiasi, kuzungumza kwa upendo, Kufanya mambo yote tukiongozwa na upendo Maisha ya Ukristo yasipojawa na upendo yanakuwa hayana maana hata kama tumeajaliwa kila kitu 1Wakoritho 13:1Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao.”

Kama watu tuliookolewa kwa damu ya Yesu tunapaswa kuwa na ushuhuda, kwa hivyo maneno yetu ni mojawapo ya maneneo ambayo watu wasiookolewa hutafuta kutushambulia, wanasema kuwa tunapowazungumzia kuhusu neno la Mungu, tunawahukumu, Hatupaswi wakati wote tu kuhukumu mambo, kwani wakati tunapoonekana kuihukumu dhambi, ni lazima tuonyeshe kuwa tunawapenda na kwa sababu hiyo tutaweza kufanikiwa kuwaleta kwa Yesu kwa upendo na uvumilivu wala tusijinyeshe kuwa sisi ni wema zaidi kuliko wanadamu wa kawaida au kwa sababu ya wiokovu wetu kuwa labada sisi hatuwezi kukosea, kimsingi duniani tunajifunza sana kwa kukosea kwa hiyo wote tunakosea kama asemavyo Yakobo ndugu yake bwana ona

Yakobo 3:1-2 “Ndugu zangu, msiwe waalimu wengi, mkijua ya kuwa mtapata hukumu kubwa zaidi. Maana twajikwaa sisi sote pia katika mambo mengi. Mtu asiyejikwaa katika kunena, huyo ni mtu mkamilifu, awezaye kuuzuia na mwili wake wote kama kwa lijamu.”

Aidha hatuna budi kuvumiliana sisi kwa sisi, kutokana na uwezo wa chumvi kustahimili muda mrefu duniani bila kupoteza ladha chumvi inatufundisha uwezo wa kuvumilia na kuchukuliana

2Timothy 4:2lihubiri neno, uwe tayari, wakati ukufaao na wakati usiokufaa, karipia, kemea, na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho.”

Ni muhimu kushughulika na wengine kwa busara biblia inatoa muongozo kwa mfano namna na jinsi ya kushughulika na kiongozi katika kanisa 1Timotheo 5:1-3Mzee usimkemee, bali umwonye kama baba; na vijana kama ndugu; wanawake wazee kama mama; wanawake vijana kama ndugu wa kike; katika usafi wote. Uwaheshimu wajane walio wajane kweli kweli” unaweza kuona kuwa kuwa chumvi kunatupasa kuhakikisha kuwa tunawaheshimu wengine, tunakemea kwa uvumilivu, hatuwakemei wazee, tunawaheshimu wajane na kuzungumza na wengine kama dada na kaka zetu

Aidha wanawake pia wanapaswa kuwa makini na namna wanavyozungumza na waume zao 1Petro 3:1-2Kadhalika ninyi wake, watiini waume zenu; kusudi, ikiwa wako wasioliamini Neno, wavutwe kwa mwenendo wa wake zao, pasipo lile Neno; wakiutazama mwenendo wenu safi, na wa hofu.Hakuna jambo linatia maudhi kama kumsikia mwanamke akizungumza kama baharia. Biblia inapozungumia maneno kukolea munyu au chimvi ina maanisha pia namna bora ya uzungumzaji wa wanawake katika kutii kwao waume zao kimsingi Mungu hapendezwi na kelele na mafarakano katika ndoa ambayo yanaweza yakasababishwa na wanawake, ni matarajio ya kibiblia kuwa wanawake walioolewa watakuwa chumvi katika ndoa zao

Biblia pia inatuonya juu ya matumizi bora ya Meneno kwa maana kuwa sio vema kwetu kuapa, kulaani au kukufuru Yakobo 5:12 “Lakini zaidi ya yote, ndugu zangu, msiape, wala kwa mbingu wala kwa nchi; wala kwa kiapo kinginecho chote; bali ndiyo yenu na iwe ndiyo, na siyo yenu iwe siyo, msije mkaangukia hukumu.” Kumbe Mungu anachukizwa sana kumsikia Mkristo akitumia maneno yasiyojaa munyu.

Maneno yetu pia hayapaswi kuleta aibu na kuharibu ushuhuda wa Bwana wetu Yesu  Tito 2:7-8 “katika mambo yote ukijionyesha wewe mwenyewe kuwa kielelezo cha matendo mema, na katika mafundisho yako ukionyesha usahihi na ustahivu, na maneno yenye uzima yasiyoweza kuhukumiwa makosa, ili yule mwenye kupinga atahayarike, kwa kuwa hana neno baya la kunena juu yetu.” Chumvi ni fundisho kwetu sisi wahubiri wa injili katika kuhakikisha kuwa maisha yanakuwa kielelezo ambapo tutaweza kusababisha watu washindwe kutuhukumu na kupata sababu za kupinga hawa wale ambao wako kinyume na injili.

Chumvi inaweka ladha

Wote tunafahamu kuwa ni vigumu sana kufurahia chakula cha aina yoyote hususani mboga kama chumvi ikikosekana kwa hiyo ili mboga ziwe tamu ni lazima chumvi iwekwe katika uwiano husika ona Ayubu 6:6a “Je! Kitu kisicho na ladha yumkini kulika pasipo chumvi?ni rahisi watu kukubali ujumbe wetu wa injili ya wokovu kama ujumbe huo utatolewa katika roho sahihi, watu wamuelewe mwokozi na mpango na makusudi ya Mungu kabla ya kushawishika kumpokea Yesu kama Bwana na mwokozi wa maisha yao! Mahubiri yetu, maneno yetu na matendo yetu na mafundisho yetu yajawe na ladha ya hekima yenye kuwavutia watu kwa kuwaonjesha ile ladha ya wokovu na utamu tulio nao katika Kristo        

Chumvi hutumika kuyeyusha barafu.

Katika nchi ambazo wakati wa baridi kunakuwa na umende ujulikanao kama snow na barafu ambazo wakati mwingine hujikusanya hata kufikia futi sita na kadhalika mara nyingi wamekuwa wakitumia chumvi pia katika kuyeyusha barafu ili iwe rahisi kwa watu kupita na kuendelea na shughuli zao, kwa hivyo tunajifunza pia kuwa chumvi ina ngubu ya kutekebisha hali joto na kuhakikisha kuwa mambo yanakuwa sawa Neno la Mungu lina uwezo wa kuweka sawa mioyo ya watu kuliko kitu kingine chochote

Zaburi 147:16-18 “Ndiye atoaye theluji kama sufu, Huimwaga barafu yake kama majivu, Hutupa mvua ya mawe kama makombo, Mbele ya baridi yake ni nani awezaye kusimama? Hulituma neno lake na kuviyeyusha, Huuvumisha upepo wake, maji yakatiririka.”

Matumizi mazuri ya maneno yetu tunayoyatumia katika kuwajibu watu na kuzungumza nao yanatusaidia katika kuyeyusha mioyo ya watu kwa neno la Mungu ambalo lina nguvu ya kushughulika na watu wa kila aina na wenye mioyo migumu na wanaojihami tunapowahubiri Mithali 15:1 “Jawabu la upole hugeuza hasira; Bali neno liumizalo huchochea ghadhabu.”

Chumvi hutumika kama tiba.

Chumvi pia hutumika kama sehemu ya matibabu, watu wanaitumia chumvi kuiweka kwenye eneo la kidonda kilichotokana na kujikata, Wamisri pia waliitumia chumvi kama tiba na pia kwenye utunzaji wa maiti ili isharibike kazi kubwa ya chumvi katika tiba hufanya kazi ya kukausha majimaji yote na kuleta ukavu, Neno la Mungu linauwezo wa kukausha dhambi katika maisha ya watu, Roho Mtakatifu anaweza kuondoa mambo yasiyofaa katika maisha yetu  na kumfanya mtu kuwa kiumbe kipya

2Wakorintho 5:17 “Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.”

Endapo kuna eneo katika maisha yako linakupa changamoto na unapambana kubadilika ushindi wako unathibitishwa kupatiana kwa neno la Mungu, kila kitu uvutaji wa sigara, masengenyo, wivu, uchungu, kiburi,  na kadhalika Mungu yuko tayari kutoa msaada  na amini ya kuwa atakusaidia.

Maisha ya Mwanadamu ni chumvi.

Unapojaribu kuonja kila aina ya majimaji yanayotoka kwenye mwili wa mwanadamu yana ladha ya chumvi chumvi, chumvi inatufundisha kuwa Mungu Roho Mtakatifu anapokuwa ndani ya mtu humwezesha mtu huyo kuwa na ladha nzuri katika maeneo yake yote kila ulifanyalo katika maisha linatukuwa na ubora wenye kuleta radha kwaajili ya utukufu wa Mungu Luka 6:45 “Mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake.”

Maneno yako yatakuwa yanampa Mungu utukufu, japo wako wanaoweza kuchukizwa na jambo hili na kwao itakuwa ni kama chumvi inawekwa kwenye majeraha yao lakini neno la Mungu ndio lilivyo

Chumvi inatufundisha kuishi maisha ya kiasi.

Wote tunajua pale chumvi inapozidi na tunajua vilevile chumvi inapopungua, wakristo wameitwa kuishi maisha ya kiasi ili kila kit duniani kiwe kitamu ona

Tito 2:11-12 “Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa;”            

Maisha ya kiasi yana umuhimu mkubwa katika maeneo mengi, hata ya kiafya chumvi ikizidishwa sana inaweza hata kusababisha magonjwa kama shinikizo la juu la damu na kadhalika , kama maisha yetu hayana kiasi ni ngumu pia kwetu kuihubiri injili, Maisha ya kiasi ya na umuhimu mkubwa katika afya ya kimwili na kiroho, chumvi inatukumbusha kuishi maisha ya kiasi.

Agano la Chumvi.

2Nyakati 13:5 “je! Haikuwapasa kujua ya kwamba Bwana, Mungu wa Israeli, alimpa Daudi ufalme juu ya Israeli milele, yeye na wanawe kwa agano la chumvi?

Agano ni patano linalofanywa baina ya watu wawili, huku kila upande ukiahidi kuwa mwaminifu kwa mwingine, agano ni tofauti na mapatano, ni tofauti na kiapo, ni tofauti na nadhiri, kwa vile agano huwa linamuhushisha Mungu mwenyewe, Hata upande wa kibinadamu unapokuwa sio mwaminifu upande unaobaki wa Mungu unapaswa kuwa mwaminifu katika kulitimiza agano au patano, hata pale Daudi alipokesea pamoja na watoto wake wote ambao walishindwa kukaa katika njia yake  kiasi kwamba ilikuwa Mungu awaangamize lakini kwaajili ya agano lake na Daudi ilimpasa Mungu kuwa mwaminifu katika upande wake ili ahadi ile isianguke,

 1Wafalme 9:3-5 “Bwana akamwambia, Nimeyasikia maombi yako na dua zako, ulizotoa mbele zangu. Nimeitakasa nyumba hii uliyoijenga ili niweke jina langu humo milele; tena macho yangu na moyo wangu utakuwapo hapo siku zote; na wewe, ukienda mbele zangu kama alivyokwenda Daudi, baba yako, kwa ukamilifu wa moyo, na kwa adili, kufanya hayo yote niliyokuamuru, na kuzishika sheria zangu na hukumu zangu, ndipo nitakapokifanya imara kiti cha ufalme wako juu ya Israeli milele; kama nilivyomwahidia Daudi, baba yako, nikisema, Hutakosa kuwa na mtu wa kukaa katika kiti cha enzi cha Israeli.”             

Unaona Mungu alikuwa amemuahidi Daudi akimwambia ya kuwa “HUTAKOSA MTU WA KUKAA KATIKA KITI CHA ENZI CHA ISRAEL MILELE” Agano hili ndio linaitwa agano la chumvi, namna agano hili lilivyofanyika Nabii Nathan au Gadi mmojawapo aliyetumwa kuleta ujumbe huu ndiye aliyemfanyia Daudi na watoto wake wote agano la chumvi.

 

Jinsi ya kufanya agano la chumvi

Wakati wa kufanya agano la chumvi.

  1. Mizimu, mapepo, shetani na wachawi na waganga au makuhani wa kichawi huwaathiri watu katika maisha yao na kusababisha msongo wa mawazo, kwa kutumia nguvu za giza, kwa kutumia nguvu hizo za giza na za kichawi wanawasababishia watu kupoteza mwelekeom kuwa na bumbuwazi, kuteseka, kuelemewa, kuwa na uzito na kupata changamoto za kifedha na kiuchumi na changamoto nyinginezo nyingi.

 

Uchawi ni silaha ya giza inayotumiwa na wachawi kwa kusudi la kuharibu maisha ya watu wanaofanikiwa na kufanikiwa  katika mazingira mbalimbali, silaha hiyo ya giza ni silaha ya kiroho lakini matokoe yake hutokea katika hali halisi.kuteseka kwa watu waliorogwa au kuchawiwa kunategemeana na nguvu iliyotumika katika kunuiziwa nguvu za mashambulizi

Pepo watatafasiri uchawi na manuizo na kuyawasilisha kwa watu waliolengwa na kuwashambulia na matokeo yanaweza kutokea katika ulimwengu wa miili yao, mambo magumu na matukio ya ajabu huanza kutiokea katika maisha yao na njia pakee ya kuimarisha na kuleta ukombozi ni agano la chumvi

 

Ukombozi kupitia gano la chumvi ni rahisi sana kwa muonekano lakini una nguvu kubwa za ajabu sana, ukombozi huu una nguvu ya kuondoa kabisa maedhara ya nguvu zisizoonekana za kichawi na kuukausha au kuuondoa kabisa na kuondoa hali ya kushindwa kwa sababu zozote zile, kwa kufanya hivyo haimaanishi oia mkuwa tutaacha kabisa kuschughulikia nguvu za giza kwa namna za kawaida, lakini tutaendelea ili kuhakikisha kuwa tunaendelea kukua kiroho.

 

  1. Unafanya gano la Chumvi wakati gani?

 

Tunafanya agano la chumvi wakati tunapohisi kuwa kuna matukio ya vita za kiroho zilizohusisha nguvu za giza, ni kweli kwamba mtu aliyeokoka hawezi kushambuliwa na nguvu za giza kwa sababu imeandikwa hakuna ugaga wala uchawi juu ya Yakobo Hesabu 23:23  Hakika hapana uchawi juu ya Yakobo, Wala hapana uganga juu ya Israeli. Sasa habari za Yakobo na Israeli zitasemwa, Ni mambo gani aliyoyatenda Mungu!

 

Lakini kumbuka tuna mashambulizi kutoka kwa mamadui, tuko vitani, majeshi ya pepo yanatumwa kwetu kwa mauizo na sadaka za iana mbalimbali na kwa maelekezo ya aina mbalimbali kwa hiyi kuna kiwango cha mashambulizi ambayo tunakutana nayo wakati mwingine kwa asilimia 30 au 60 au 90 kwa hiyo wote kwa kiwango Fulani tunashambuliwa na nguvu za giza kulingana na kiwango za kuzaa kwetu matunda kumbuka mfano wa zile mbegu zilizoangukia kwenye udongo mzuri Marko 4:8 “Nyingine zikaanguka penye udongo ulio mzuri, zikazaa matunda, zikimea na kukua, na kuzaa, moja thelathini, moja sitini, na moja mia.” Kama ukuaji wetu wa kiroho unaweza kuzaa matunda kwa asilimia hizo zilizotajwa ni dhahiri na mashambulizia yanaweza kuwepo kutokana na kiwango kwa hiyo niia nyepesi ya kuondoa kiwango hicho cha mashambulizi ya nguvu za giza ni kwa kutumia ganano la chumvi  na ukifanya mara kwa mara unaziondoa kabisa katika mwili wako  tunaweza kujitibu kwa agano la chumvi mara unapohisi au kusikia changamoto hizi:-

 

-          Uchovu wa kimwili na kiroho

-          Kupoteza hamasa

-          Kupoteza uwezo wa kufikiri

-          Kuelemewa na mawazo

-          Hasira za kupita kawaida

-          Mgandamizo wa mawazo stresses

-          Aina yoyote ya ugonjwa na wakati wowote unapokuwa unahisi kuwa kuna uvamizi na hali isiyo ya kawaida katika mwili wako, uchumi wako, kazi yako, huduma yako na roho yako.

-          Lakini pia udhaifu wowowte wa kimwili, kiroho na kihisia ujue kuna mashambulizi ya mizimu, mapepo, wachawi na kadhalika basi unahitaji tiba ya agano la chumvi.

 

  1. Mambo unayohitaji kwaajili ya kutekeleza agano la chumvi

 

-          Utahitaji ndoo au beiseni

-          Utalijaza maji safi kwa asilimia 50% yaani nusu

-          Utahitaji chumvi yam awe kwa kiwango chochote kana huna ya mawe unaweza kutumia ya mezani lakini ya mezani uwezo wake utapungua kwa asilimia 30% ukilinganisha na ile ya mawe

-          Taulo la kujikaushia

-          Na sehemu ya kukanyajia

-           

  1. Jinsi ya kufanya ibada ya agano la chumvi.

 

1.       Weka maji kwenye ndoo yajae kwa asilimia 50% yaani nusu yake kwa kiwango tu cha kufunika enka za miguu

2.       Weka vijiko vidogo viwili vya chumvi ya mawe

3.       Omba kwa kumaanisha na kwa imani kwamba Mungu akuondolee nguvu zote za giza, pia omba maalumu kwaajili ya kuziharibu kabisa na kuzibomboa nguvu zote za mizimu, pepo, waganga na wachawi na kila manuizo yaliyofanywa kinyume nawe na kukuletea athari, omba maombi ni muhimu sana na yana uwezo mkubwa sana yanapofanyika sambaba na ibada hii ya ukombozi.

4.       Hakikisha umekaa sawa sawa na miguu yako hususani enka ziwe zimezama katika maji, miguu yako isigusane bali iwe mbalimbali kati ya sentimita 2-3 hii inasaidia kuodoa uchawi wote uliorogwa kwa nguvu za giza, kama miguu yako itagusana itakuwa kikwazo kwa ibada hii, 

5.       Hakikisha miguu inakaa kati ya dakika 10-15 na usizidishe zaidi ya dakika 15, ukizidisha nguvu za giza zinazotoka kwa njia ya miguu zinaweza kuingia mwilini mwako

6.       Wakati miguu yako inapokuwa katika maji yenye chumvi anza kuomba au kunuiza kwa jina la Yesu  Mungu au kuimba maombi

7.       Wote wenye pumzi wote waishio duniani wote wampendao  (Wamchao) Mungu na waseme fadhili zake ni za milele

8.       Wote wanaoeneza habari zake watangazao habari njema duniani kote na waseme fadhili zake ni za milele.

 

Kwa ufupi utaimba zaburi 118:1-14         

1. Haleluya. Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele.

2. Israeli na aseme sasa, Ya kwamba fadhili zake ni za milele.

3. Mlango wa Haruni na waseme sasa, Ya kwamba fadhili zake ni za milele.

4. Wamchao Bwana na waseme sasa, Ya kwamba fadhili zake ni za milele.

5. Katika shida yangu nalimwita Bwana; Bwana akanijibu akaniweka panapo nafasi.

6. Bwana yuko upande wangu, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini?

7. Bwana yuko upande wangu, msaidizi wangu, Kwa hiyo nitawaona wanaonichukia wameshindwa.

8. Ni heri kumkimbilia Bwana Kuliko kuwatumainia wanadamu.

 

9. Ni heri kumkimbilia Bwana. Kuliko kuwatumainia wakuu.

10. Mataifa yote walinizunguka; Kwa jina la Bwana naliwakatilia mbali.

11. Walinizunguka, naam, walinizunguka; Kwa jina la Bwana naliwakatilia mbali.

12. Walinizunguka kama nyuki, Walizimika kama moto wa miibani; Kwa jina la Bwana naliwakatilia mbali.

13. Ulinisukuma sana ili nianguke; Lakini Bwana akanisaidia.

14. Bwana ni nguvu zangu na wimbo wangu, Naye amekuwa wokovu wangu.

 

Hitimisho:

Baada ya kumaliza maombi haya ya ukombozi kulinga nan a mahitaji yako unaweza kuanza kumshukuru Mungu kwa ulinzi wake anaokupa na namna anavyokuzunguka

Utayamwaga maji yake chooni na kisha utasafisha ndoo na maji safi. Utakausha miguu yako vema kwa taulo na kisha utajipaka mafuta ya mzeituni na kuomba Mungu akupeleke kwenye kiwango kingine cha maswala mbalimbali uyatakayo. Ibada inaweza kufanyika pia kwa makusudi mbalimbali ambayo mengine hayajaainishwa katika somo hili mfano kuweka wakfu, kiongozi, kujilinda na cheo chako na kadhalika

Mwisho wa ibada hii.

Matokeo:

  1. Athari zote za nguvu za Giza na mashambulizi ya wachwi, waganga na mapepo na shetani zinaondoka
  2. Maji ya agano la chumvi yana nguvu kubwa sana yenyewe tu kunyonya nguvu zote za giza
  3. Nguvu za giza na magonjwa yote yanayoambatana na nguvu hizo yanaondoka na wakati mwingine maji yanaweza kuwa na rangi nyeusi kama ishara ya kuondoka kwa nguvu hizo, au yanaweza kuwa na uvuguvugu au yakawa na harufu mbaya hii ni shara ya vitu vibaya kuondoka mwilini mwako

KUMBUKA. Mafundisho haya ya katika shule za kinabii na kama imani yako inakinzana usitilie maanani wala usifundishe kanisani kwako!

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima

Jinsi ya kutengeneza Maji ya Baraka!


Ezekiel 36:25-27 “Nami nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi; nitawatakaseni na uchafu wenu wote, na vinyago vyenu vyote. Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama. Nami nitatia roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda.”

 


 

Utangulizi:

 

Nyakati za siku hizi kumekuwepo na mfumuko mkubwa sana wa matumizi ya maji pamoja na mafuta katiika maombezi, na watu wengi sana wamekuwa wakijiuliza kulikoni kuhusu matumizi ya maji, mafuta na au chumvi katika maombezi na shughuli za utatuaji wa maswala kadhaa ya kiroho, Katika somo hili leo nazungumzia tu kuhusu matumizi ya maji katika maombezi, ambayo ni maarufu kama maji ya Baraka, au maji matakatifu.

 

Kwanza ni muhimu kufahamu kuwa neno la Mungu liko kimyaa kuhusu namna maji ya Baraka au maji matakatifu na namna yanavyotumika leo, Maji yanayotajwa katika maandiko hususani agano jipya ni maji yanayohusika na ubatizo Mathayo 3:11 “Kweli mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba; bali yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, wala sistahili hata kuvichukua viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.”

 

Maandiko yanataja ubatizo wa maji kwa kusudi la toba, na hakuna ufafanuzi wowote kuhusu maji ya Baraka au maji matakatifu, Ubatizo wa maji mengi ni ishara ya kumkiri Bwana wetu Yesu kuwa bwana na mwokozi kwa kukubali hadharani kazi aliyoifanya pale msalabani kwa mateso yake, kifo na kuzikwa na kufufuka. Hicho ndicho kinaelezwa zaidi na kwa uwazi katika maandiko!

 

Swala la kunyunyizia maji ya Baraka au maji matakatifu kama tunavyoliona leo linaweza kufanana kliasi Fulani na ile dhana ya agano la kale la utakaso ambapo maji matakatifu yalitumika kutakasa vitu najisi endapo kimeguswa na kunajisiwa na mtu aliyevigusa aliyekuwa najisi, lakini pia maji matakatifu au maji ya Baraka yalitumika kama njia ya kuwatakasa watu waliokuwa najisi, kwa sababu mbalimbali ona mfano

 

Mambo ya walawi; 17:15 “Tena kila mtu atakayekula nyamafu, au nyama aliyeraruliwa na wanyama, kama ni mzalia, kama ni mgeni, atafua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni; ndipo atakapokuwa safi.”

 

Hesabu 19:17-19 “Na kwa huyo aliye najisi watatwaa katika majivu ya kuchomwa kwake hiyo sadaka ya dhambi, na maji ya mtoni yatachanganywa na majivu katika chombo; kisha mtu mmoja aliye safi atatwaa hisopo, na kuitia katika hayo maji naye atayanyunyiza juu ya hema, na juu ya vyombo vyote, na juu ya watu waliokuwapo, na juu yake yeye aliyeugusa mfupa, au mtu aliyeuawa, au mzoga, au kaburi; na yule aliye safi atamnyunyiza huyo aliye najisi siku ya tatu, na siku ya saba; na katika siku ya saba atamtakasa; naye atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa safi jioni.”

 

Andiko la msingi ambalo nimelitumia katika utangulizi wa somo langu kwa kiwango Fulani linazungumzia kinabii kile ambacho Mungu amekitabiri kupitia nabii Ezekiel kuhusu kuwanyunyizia watu wake maji safi kwa kusudi la kuwaondolea vitu vibaya na kutafuta ushirika naye, kwa hiyo tunaweza kuona kuwa maji yalitumika kuwatakasa wanadamu, waliokuwa na magonjwa au waliokuwa najisi au kuweka wakfu vyombo vitakatifu, hivyo kwa kiwango Fulani tunaweza kuona tu kwa umbali kwamba maji yanahusishwa na utakaso lakini huduma kuhusu maji ya Baraka na maji ya matakatifu kama yanavyotumika leo bado biblia iko kimya!

 

Maji ya Baraka katika makanisa makubwa ya kale

 

Katika makanisa makubwa namaanisha kwa umri yaa ni makanisa ya asili kama Orthodox, Roman Catholic na Anglican yapo matumizi ya maji ya Baraka au maji matakatifu, hivyo kimsingi makanisa hayo yalikuwa na utaratibu wa kutumia maji hayo, bila kuweka wazi sana chanzo cha matumizi ya maji hayo, hata hivyo katika kanisa la Orthodox kwa mfano matumizi ya maji matakatifu yalikuwa au hufanyiika katika siku za jumamosi kuu, yaani jumamozi kabla ya sikukuu ya pasaka, na vilevile katika sikukuu ya Pentekoste, Makuhani huyafanyia maombi maji machache na chumvi kisha wanachanganya na kuruhusu maji hayo kuongezewa na maji mengine na kuyasambaza katika maeneo husika ya kanisa hususani sehemu za kuingilia milangoni, waamini wangeingia na kuchovya vidole vyao na kupiga ishara ya msalaba, kama maji hayo yakuongezea yangekuwa mengi zaidi kuliko yale yaliyobnarikiwa makuhani wangeiongeza maji zaidi baada ya kuandaa, uandaaji wenyewe unafanywa na makuhani, kwa kuombea maji pamoja na chumvi na kuyaombea ili yakutane na mahitaji ya watu ikiwa ni pamoja na kufukuza mapepo,kuponya magonjwa,kutakasa, kuondoa nuksi, mikosi na balaa, na kuleta neema isiyokusudiwa, juu ya watu, wao wanaamini tu kuwa maji matakatifu ni zawadi nzuri ambayo Mungu amewapa watu wake kwa kusudi la kuwatakasa watu wake kutoka katika changamoto mbalimbali za kila siku,  na kuhakikisha kuwa tunakuwa vizuri kila siku kama tutayatumia mara kwa mara, wao wanaamini kuwa maji ni sacrament  Neno Sacrament limetokana na neno la asili la kihispania Sacramento kwa kiingereza sacrament ni tukio la kidini au la kiishara kama ilivyo ubatizo au meza ya bwana linaloaminika kuwa linabeba neema ya Mungu na kuleta maana Fulani ya kiroho

 

A Sacrament is a religious ceremony or rituals that stand as baptism or Lord Supper held to be a means of divine grace to be a symbol of a certain spiritual reality

 

Kwa hiyo matumizi ya maji matakatifu, au maji ya Baraka kwa mujibu wa Orthodox unaendana na habari ya ubatizo wa maji mengi aliofanyiwa Yesu Kristo, kupitia Yohana Mbatizaji katika mto wa Yordani, kwa mujibu wa Orthodox ingawa Yohana alikuwa anabatiza kwa maji kama ishara ya toba dhidi ya dhambi, na watu walikwenda ili watubu dhambi zao, wanaamini kwa kuwa Yesu hakuwa na dhambi na alikuwa ni Mungu, wanaamini kuwa Yesu aliyabariki maji,  na wanayahesabu maji kuwa ni matakatifu na kuwa Yesu aliyatakasa na kwaasili maji yaliumbwa na Mungu kwa makusudi hayo yatumike pia kwa kazi zake za kutakasa! Roho Mtakatifu alitulia juu ya uso wa maji wakati waa uumbaji na hivyo maji ni sababu ya uwepo wa uzima katika mwili na roho

 

Mwanzo 1:2  Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji.”      

 

Kwa mujibu wa kanisa Catholic wao maji ya Baraka au maji matakatifu wanayatumia kila siku na wanayaweka mlangoni mwa kanisa, wana wanaamini kuwa maji ya Baraka mwanzo ni yalitumiwa na watu walioabudu mwezi na yalitumiwa na makuhani wa dini za kienyeji walipokuwa wakiingia katika mahekalu yao, kwa hiyo swala la maji ya Baraka ni la asili ya dini za kipagani za waabudu miungu  na hasa mungu mwezi,  kwa mujibu wa kanuni ya 65 ya mkutano mkuu wa Constantinople (691). Na kwa mujibu wa Encyclopaedia ya wakatoliki inaeleza kuwa matumizi ya maji ya Baraka yalianza kutumika zaidi mnamo karne ya 19, pamoja na ukweli kuwa Agano jipya hakijasema chochote kuhusu matumizi ya maji, lakini waliitumia njia hii kama njia ya kuwashika wapagani na kuhakikisha kuwa wanaifuta ibada hiyo katika njia ya kipagani, kwa matumizi ya maandiko yanayoonyesha kuwa maji yanatakasa vilevile kama walivyokuwa wakiyatumia katika ibada zao za zamani.

 

Kanisa Anglikan wao hutumia maji vilevile kwa njia mbili, moja ikiwa ni kwa kuyaombea na kuchanganya na chumvi na kuyaweka katika milango ya kanisani ili washirika wanapoingia waweze kujibariki kupitia maji hayo, aidha pia kuhani wa kianglikan anaweza kupita katika baadhi ya ibada akiwanyunyizia maji, kama ishara ya kuwatakasa na washirika wangeitikia kwa kufanya ishara ya msalaba ili wakutane na mahitaji yao, tukio hili lilikuwa sawa na maombezi tu!

 

Wakatoliki na wanaamini kuwa tukio lolote ambalo linakufanya ujisikie ya kuwa Mungu yuko karibu nawe linapaswa kutiwa moyo  hii ni kwa mujibu wa Warumi 14:23  Lakini aliye na shaka, kama akila, amehukumiwa kuwa ana hatia, kwa maana hakula kwa imani. Na kila tendo lisilotoka katika imani ni dhambi.”        Na pia

 

1Wakorintho 6:12 “Vitu vyote ni halali kwangu, lakini si vyote vifaavyo; vitu vyote ni halali kwangu, lakini mimi sitatiwa chini ya uwezo wa kitu cho chote”.

               

Wanaamini kuwa kama jambo lolote ni jema katika kutufungamanisha na Mungu ni vema kulitunza, na akama linakwaza ni vema kulitupilia mbali, kwa hiyo ingawa maandiko hayajawahi kutoa maelekezo kuhusu matumizi ya maji ya Baraka kwa namna yoyote wana wanaona wayatumie tu japo sio agizo la kibiblia

 

Makanisa ya kiinjilisti na makanisa mengi ya kipentekoste sasa wamekuwa wakiyatumia maji vilevile kama makanisa makuu ya zamani, lakini sasa wao wamekuwa na msamiati mpya badala ya maji ya Baraka au maji matakatifu wao huyaita maji ya upako, matumizi haya ya maji ya upako yamepata mfumuko mkubwa wa kimatumizi katika dunia ya leo kuliko ilivyokua zamani na ni kwaajili ya haya ndio ilinipelekea kujaribu kufuatilia na kulifanyioa utafiti swala hili ili kuweza kuja na somo linaloweza kutusaidia katika kupanua ufahamu wetu kuhusu Maji ya Baraka na ikiwezekana tutengeneze wenyewe kama tunataka badala ya kuuziwa kwa vile pia yamekuwa na mfumuko mkubwa wa kibiashara na yamekuwa yakihusishwa katika kuuzwa

 

Jinsi ya kutumia maji ya Baraka.

 

Maji haya yanaombewa na kiongozi wa kiroho aliye na mamlaka ya kichungaji au kikuhani, au na mkristo yeyote anayeamini kwa maandalizi maalumu utakayoyaona baadaye katika kielelezo. Kuhani huyabariki maji hayo kwa kidole chake kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, baada ya maji kuwa tayari kwa kufuata hatua za maelekezo yaliyoko chini  katika somo hili  maji yatatumika aidha kwa kutumia ishara ya msalaba au kwa kunyunyizia watu katika ibada, yanaweza kutumika nyumbani, kwa kutakasa nyumba, kutakasa watu, kutakasa wanyama, kutakasa biashara, kutoa pepo, kuponya wagonjwa ulinzi,  kujipatia rehema za MUngu na matumizi mengine mengi zaidi kwa kadiri ya dhamiri inavyokushuhudia, wakati wote huwa unaweza kutumia jina la Baba, Mwana na Roho Mtakatifu au moja kwa mojwa kwa jina la Yesu Kristo., unaweza kuyatumia kubariki familia, watoto, ndoa, wakati wanapoenda kulala usiku au asubuhi watu wanapoenda kazini na shuleni, kama sehemu inautembeleo wa kishetani kama shule au uchawi unaweza kutatumia maji ya Baraka au maji ya upako kwa jina linalotumika siku za karibuni.

 

Jinsi ya kutengeneza maji ya Baraka/ maji ya uapako

1.   Chukua maji safi na uyaweke katika bakuli safi la aluminium inayong’aa, yashikilie maji yako na kwa unyenyekevu mkubwa sema Ewe Mungu uliyeumba Nchi na ardhi na maji na vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana nayabariki maji haya Katika jina la Baba na Mwana na Roho Mtakatifu!.

 

2.   Chukua chumvi ya aina yoyote ile ya mawe au ya kawaida nyeupe au ya bahari, Omba kwa unyenyekevu mkubwa na kusema Ewe Mungu uliyeumba Nchi na ardhi na maji na vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana naibariki chumvi hii Katika jina la baba na la mwana na la Roho Mtakatifu! 



3.   Chukua chimvi iliyoombewa sasa na utainyunyizia katika maji na pia utakoroga maji hayo ili yachanganyike na chumvi na utaichanganya kwa kutumia jina la Yesu au kwa jina la Baba na Mwana na Roho Mtakatifu!

 


 

4.   Sasa Mchanganyiko wa Maji ya Baraka uko tayari, lakini unasubiri dua maalumu ambayo utayaombea kwa kusema Baba wa Mbinguni, nayaweka maji haya wakfu katika jina la baba na Mwana na Roho Mtakatifu, Nikiomba kwa maji haya utakase kila kitakachoguswa na maji haya, utaondoa nuksi, mikosi na balaa na kila jicho baya na maneno mabaya dhidi ya kitakachoguswa na maji haya kiwe batili na manuizo yote ya kiganga na kichawi yaharibike,  nawe utakibariki kila kitakachoguswa na maji haya kwaajili ya utukufu wako ili wewe utukuzwe sawa na mapenzi yako Katika jina la Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai amen!

 


Baada ya dua na maombi hayo na maandalizi hayo yote muhimu tayari una maji ya Baraka, una maji matakakatifu una maji ya upako na unaweza kuyatumia kwa sababu zozote zile kwa kusudi la kumpa Mungu utukufu, mashambani kwaajili ya mavuno, kwenye biashara kwaajili ya mafanikio, kazini, ofisini au maeneo unayohisi kuwa yamevamiwa kishirikina

 

Mafundisho haya ni kwawale tu wanaomini katika fundisho hilo au utamaduni huo, lakini wakati wote nguvu ya vifaa hivi vya kiroho ni jina la Yesu Kristo.

 

KUMBUKA: Mafundisho haya ya katika shule za kinabii na kama imani yako inakinzana usitilie maanani wala usifundishe kanisani kwako!

 

Na. Rev. Innocent Kamote.

 

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!.

Inzi wanaposumbua Nyumba yako.


Kutoka 8:20-22 “BWANA akamwambia Musa, Inuka asubuhi na mapema usimame mbele ya Farao; angalia! Atoka aende majini; kamwambie, BWANA asema, Wape watu wangu ruhusa waende zao, ili wanitumikie mimi. Au kwamba huwapi ruhusa watu wangu, tazama, nitaleta wingi wa mainzi juu yako wewe, na juu ya watumishi wako, na juu ya watu wako, nao wataingia ndani ya nyumba zako; na nyumba za Wamisri zitajawa na wingi wa mainzi, na nchi nayo ambayo wa juu yake. Nami siku hiyo nitatenga nchi ya Gosheni, watu wangu wanayokaa, ili hao mainzi wasiwe huko; ili kwamba upate kujua wewe ya kuwa mimi ndimi BWANA kati ya dunia.” 

 




Utangulizi:

Watu wengi sana huwa wanachukizwa sana na wakati mwingine wanapata hasira wanaposumbuliwa na Inzi katika nyumba zao, hii ni kwa sababu inzi katiika jamii nyingi wanahusishwa na uchafu, na wakati mwingine pia kusambaza magonjwa hivyo kimsingi inzi hawapendwi na ni machukizo kwa watu wengi sana duniani, wakati mwingine nzi wanaweza hata kutoa milio Fulani ya kuudhi au kujazana mahali, Jambo ambalo linakera na linaleta maudhi na wakati mwingine kuruka ruka katiika miili ya watu! Hata hivyo katika lugha ya kinabii inzi wanapotokea katika nyumba yako wana habari Fulani njema au mbaya ya kukupasha, katika ulimwengu wa kiroho, na hivyo ni muhimu kuwa na usikivu wa rohoni mainzi yanapotawala katika nyumba yako! Tutajifunza somo hili Inzi wanaposumbua nyumba yako kwa kuzingatia maeneo manne yafuatayo:-

i.                    Inzi katika mtazamo wa kibiblia

ii.                  Inzi wakiwa ni ishara njema

iii.                Inzi wakiwa ni ishara mbaya

iv.                 Mambo ya msingi yakupasayo kufanya

Inzi katika Mtazamo wa kibiblia

Hatunabudi kufahamu kuwa nzi ukiacha kwamba ni wadudu wa kawaida lakini pia wanatazamwa tofauti katika mtazamo wa kibiblia kwanza wanawakilisha malaika waovu au pepo wachafu, na dhana hii iko katika maandiko agano la kale na jipya ambapo hata mkuu wao aliitwa Beelzebubu ona mfano katika

Luka 11:14-15 “Naye alikuwa akitoa pepo bubu; ikawa pepo alipotoka, yule bubu akanena, makutano wakastaajabu. Wengine wao wakasema, Atoa pepo kwa Beelzebuli, mkuu wa pepo.”

Katika kifungu hicho cha maandiko Wayahudi walimshutumu Yesu wakidhani ya kuwa anatumia nguvu za mkuu wa pepo Beelzebuli kutoa Pepo, kumbe yeye alitoa pepo kwa uweza wa Roho Mtakatifu na alifafanua kuwa shetani hawezi kumtoa shetani, sio kusudi langu kufafanua jambo hilo kwa undani kwani ninachikitaka hapa ni kufafanua tu huyu BEELZEBULI ni nani ?  Kimsingi jina hili Wayahudi walitoka nalo huko ukaldayo na hapa limeandikwa kwa lugha ya Kiyunani, kiyunani ni BEELZEBOUL ambalo tafasiri yake ni mkuu wa Pepo wachafu, au mfalme wa pepo wachafu jina ambalo kimsingi linamuhusu shetani,  aidha katika maandiko pia huko katika nchi ya wafilisti katika mji ulioitwa Ekron kulikuwa na mungu baali ambaye alikuwa anahusishwa na swala la kufukuza Inzi huyu aliitwa Baal-Zebub mungu wa Ekron ona katika

2Wafalme 1:2-4 “Na Ahazia akaanguka katika dirisha la chumba chake orofani, katika Samaria, akaugua; akatuma wajumbe, akawaambia, Enendeni mkaulize kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni, kwamba nitapona ugonjwa huu. Lakini malaika wa Bwana akamwambia Eliya Mtishbi, Ondoka, uende ukaonane na wale wajumbe wa mfalme wa Samaria, ukawaambie, Je! Ni kwa sababu hapana Mungu katika Israeli, hata mnakwenda kuuliza kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni? Basi sasa, Bwana asema hivi, Hutashuka katika kile kitanda ulichokipanda, bali hakika utakufa. Eliya akaondoka.”

Mungu huyu wa wafilisti aliitwa BAAL ZEBUBU jina ambalo kwa kiingereza humaanisha “BAAL OF FLIES”  yaani mungu wa mainzi, mungu huyu alisadikiwa kuwa na uwezo wa kufukuza mainzi, Hakuna uhakika sana kama kuna muununganiko wa kimaana kwa majina hayo na lile la agano jipya lakini huyu pia alikuwa ni shetani kwa hiyo bado tunaweza kuona Mapepo na mashatani yakihusishwa na mainzi, kwa sababu ya uchafu. Au jina lile pepo wachafu.

Huko Misri nako wakati wa hukumu ya Mungu dhidi ya Farao ili awaachie wana wa Israel Mungu aliipiga Misri kwa hukumu ya pigo la mainzi

Kutoka 8:20-22 “BWANA akamwambia Musa, Inuka asubuhi na mapema usimame mbele ya Farao; angalia! Atoka aende majini; kamwambie, BWANA asema, Wape watu wangu ruhusa waende zao, ili wanitumikie mimi. Au kwamba huwapi ruhusa watu wangu, tazama, nitaleta wingi wa mainzi juu yako wewe, na juu ya watumishi wako, na juu ya watu wako, nao wataingia ndani ya nyumba zako; na nyumba za Wamisri zitajawa na wingi wa mainzi, na nchi nayo ambayo wa juu yake. Nami siku hiyo nitatenga nchi ya Gosheni, watu wangu wanayokaa, ili hao mainzi wasiwe huko; ili kwamba upate kujua wewe ya kuwa mimi ndimi BWANA kati ya dunia.”

Kimsingi pigo hili pia ilikuwa sio hukumu kwa Farao na wamisri tu bali pia kwa miungu ya wamisri, mungu aliyekuwa anahukumiwa hapa kwa wamisri ambao walikuwa na miungu wengi mmoja wapo ni  mungu aliyekuwa anajihusisha na kufukuza inzi, kwa uweza wa Mungu alikuwa akionyesha kuwa kama Mungu akiwatumia inzi kama sehemu ya hukumu miungu hiyo haiwezi kuzuia kusudi kuu likiwa lile lile Farao aweze kujua ya kuwa Yehova ndiye Mungu pekee duniani.

Kwa hiyo tunaweza kukubaliana wazi na wazo la kibiblia kuwa inzi wanawakilisha pepo wabaya na mkuu wao ni shetani, katika lugha ya kinabii, hata hivyo ni muhimu kufahamu kuwa kinabii inzi wa kawaida wanapoanza kuiandama nyumba yako huwa kunakuwa na maana za msingi za kiroho zinazowakilishwa maana hiyo inaweza kuwa ya hatari na mbaya au maonyo ya kutokupuuzia maeneo Fulani muhimu katika maisha yetu. Inzi kinabii pia wanawakilisha chuki, uovu, au lawama kwa sababu wanaruka ruka hovyo na kubughudhi watu, wanawakilisha pia tabia mbaya, kukosa kiasi na hisia mbaya, lakini pia wanawakilisha mambo mazuri kama tunavyoweza kujifunza katika vipengele vifuatavyo:-

Inzi wakiwa ni ishara njema

Inzi wakiwa na ishara njema huwa wanabeba maana zifuatazo:-

1.       Inzi wanashiria kuwa kuna mambo unapaswa kuyafanyia maamuzi magumu  - Inzi wanapokufuata futa katika nyumba yako wanakupa ujumbe kuwa kuna maamuzi magumu unapaswa kuyafanya ili kuleta mabadiliko makubwa katika maisha yako, yako mambo aidha unapaswa kuachana nayo, au kuna jambo unapaswa kuliachia kabisa katika maisha yako, kama iko tabia mbaya ambayo inachangia kwa kiwango kikubwa kuharibu maisha yako tabia hiyo iachwe mara moja, kama yuko mtu anakusababishia kufanya mambo mabaya mtu huyo uachane naye haraka, au mara moja, kuna ujumbe wanaokupa nzi kuwa kitu hicho kibaya kiondoke katika maisha yako, hivyo utapaswa kujitafakari na kuangalia ndani yako na mazingira yako na kile utagundua kuwa ni sababu ya wewe kutokuendelea au kuharibikiwa basi utapata jibu kuwa unatakiwa kukifukuzilia mbali kama vile tunavyotafuta kuachana na nzi, tahadhari hapa usichukue maamuzi bila kufikiri kwa kina na ukijisikilizia kwa ndani ndipo utagundua ni kitu gani watu au mtu gani mbaya anakusababishia mkwamo katika maisha kisha utatafuta njia mbadala za kuachana na jambo hilo kwa amani!

 

2.       Inzi wanakupa taarifa ya jambo jipya kutokea katika maisha yako – Ishara ya nzi sio tu wakati wote ni mbaya kama watu wanavyodhani lakini wanapokuandama inamaanisha kuwa kuwa kuna kitu kinaenda kuisha au kufikia mwisho katika maisha yako  na jambo jipya kabisa linaenda kutokea katika maisha yako, ni ishara ya kuisha kwa jambo Fulani katika maisha yako na kuanza kwa jambo jipya kabisa, hivyo kuwaona inzi wazi wazi kabisa au kwenye ndoto  ni ujumbe ambao unakueleza kuangalia jambo jipya kabisa katika maisha yako, a kulipokea vizuri kwani mabadiliko hayo yanaweza kuleta  nafasi usiyoitarajia.

 

3.       Inzi wanakupa taarifa ya kwamba kuna jambo linalokuondolea umakini - aidha unalijua au hulijui kama ni mtu aidha unamjua au humjui anakunyima usingizi, anakusumbua au ndio sababu ya kuharibikiwa kwako na kukuletea migandamizo katika moyo , unapoona inzi fikiria kwa kina kama kuna mtu katika maisha yako uwe unamjua au humjui anasababisha mabaya katika maisha yako iwe unajua au hujui, mtu huyo lazima umfanyie mkakati wa kumuacha au kuharibu nguvu anayoitumia kuharibu maisha yako mtu huyo aondoke au uache mawasiliano naye katika maisha yako kabisa. Kumbuka isiwe kwa ugomvi Mungu ametuita katiia mani.

 

4.       Inzi wana ujumbe kuwa kuna watu au mtu unampuuzia  kama unavyoona inzi wanapotusumbua huwa tunawapuuza, na kuwafukuza kwa dharau japo nzi hao hawataenda mbali na wataendelea kutusumbua hii ni ishara kuwa kuna watu wanakuhitaji lakini unawapuuzia hujawapa kipaumbele, ni mtu au watu wanaokupenda sana lakini umewapuuzia, au ni marafiki wa maana sana lakini umewapuuzia, inawezekana hata wakituma ujumbe unawapuuzia hujibu,  anza kujihoji kwa makini, na kwa uangalifu mkubwa kama umepuuzia na kuharibu urafiki na watu muhimu katika maisha yako au umeshindwakugundua umuhimu wa watu hao tunza na kurudisha urafiki haraka imarisha mahusiano na wote walio muhimu kwenye maisha yako

 

5.       Inzi wanakupa taarifa wazi kuwa unakabiliwa na hofu – Hofu hii ni hofu ya kupoteza mtu wa karibu sana umpendaye au kupoteza kazi, labda mambo hayaendi vizuri kazini na una mashaka ya kupoteza kazi hivyo kuna hofu inaanza kujengeka ndani yako, inzi wanakutaarifu kuhusu hofu yako ili uweze kujihami mapema kwa kufikiri kuondoka kazini au kutafuta kazi nyingine ambayo itaendana na hisia zako na kuachana na ile inayokupa mikandamizo ya moyo.

 

6.       Inzi wanawakilisha uwezo wako wa kukabiliana na mazingira – Inzi wanakupa ujumbe kwamba wewe sio wa kupuuzwa kuna nguvu kubwa ndani yako ya kukabiliana na mazingira nzi wanauwezo wa kuishi kokote na katika mazingira yoyote yawe mazuri au mabaya, wanauwezo wa kujipatia chakula hata katika mazingira yanayofikiriwa kuwa hayafai,  wana wanakupa ujumbe kuwa hata wakikutupa kama taka taka wewe ni hazina kwa wengine, inzi wanakupa ujumbe wa kufanikiwa, kuwa na vingi sana kuwa tajiri, kuwa na uwezo mkubwa wa kuhamasisha watu kuwa na uwezo wa kuishi katika mazingira hata ya kukataliwa, uwezo mkubwa wa kuvumilia magumu, huku ukiendelea na maisha na kujitafutia chakula , inzi wanakukumbusha kuwa wewe ni mtu mgumu sana  na unaweza kukabiliana na mazingira yoyote yanayobadilika, yawe mazuri au mabaya.

 

7.       Inzi wanakukumbusha kuwa una hasira -  na kwamba unatakiwa kumudu hasira yako, katika maisha, inzi hatuwezi kuwadhibiti sisi wenyewe  kwa msingi huo, hata hasira lazima tujifunze namna ya kuidhibiti ili isituletee madhara

Inzi wakiwa ni ishara mbaya

Inzi pia wana ujumbe mbaya na wa kuvunja moyo

1.       Inzi wanaujumbe wa kukutaarifu kuwa kuna jambo baya. – kuna jambo baya lisilopendeza, la kuudhi au lenye kuingilia mipango yako na kukuharibia kama vilevile tunavyoona inzi wakiwa wasumbufu, wenye maudhi na kutua tua katika mazingira tusiyoyapenda ndivyo wanavyoashiria kuwa kuna tukio litaingilia kati katika maisha yako kulete usumbufu, kukuharibia kukukatisha kukuudhi na kadhalika au jambo la kukuondolea amani, na au kukupa fadhaa, kiroho unajua nini unachopaswa kukifanya kuifuta hali hiyo.

 

2.       Inzi ni taarifa ya kifo – Kwa kawaida inzi pia wanapenda kitu kilichokufa au kilichooza au chenye harufu mbaya au shombo, nzi wanapoonekana katika ndoto au halisi wakiwa nyumbani kwako huashirikia kifo cha mtu aliye karibu sana na wewe ambaye hungependa afe  hata hivyo Inzi pia wana ishara ya ufufuo, kwa kuwa huzaliwa kama yai kisha buu kisha inzi hutokea kwa hiyo kuna ishara ya maisha mapya.

 

3.       Uwepo wa Inzi pia huashiria kuvunjika kwa mahusiano, - kwa hiyo watu wanapaswa kuzungumzia mahusiano yao ili ikiwezekana wayajenge kama wanaweza kuimarisha uhusiano wao na kila mmoja ajali hisia za mwenzake, kama watu hawataimarisha mahusiano yao ni dalili inayoonywa na nzi kuwa uhusiano unakwenda kuvunjika, inzi wanakupa ishara mbaya ya matukio mabaya ya kiroho, hivyo tunapowaona tunaweza kurekebisha hali ya mambo isiwe mbaya vinginevyo kitu kibaya kinakwenda kutokea na watu watafukuzana kama unavyofukuza inzi.

 

4.       Inzi wanashirikia haribiko – inaweza kuwa haribiko ambalo limekwishatokea au linalokwenda kutokea, labda ulikuwa ukifanya kazi na kuwafurahisha wanaokuzunguka na kukuajiri na umesahahu jambo muhimu sana unalotakiwa kulifanya sasa unapaswa kuangalia kile unachotakiwa kukifanyia kazi na kile kinachohusina na maisha yako, panga mipango yako mwenyewe na kaa katika hiyo ili uweze kufikia malengo, vunja malengo makubwa na angalia madogo ambayo unayamudu inaweza kuwa jambo sahihi kwako, kama unagundua kuwa umetoka katika mpango  anza kujipanga sasa panga mpango utakaokufaa ni rahisi kuwa kutokujisikia vizuri lakini itakusaidia kufanya mambo ya muhimu.

 

 

5.       Huwezi kufanya lolote – Inzi wanakupa ujumbe kuwa mambo yanayokutokea au yatakayokutokea  yako nje ya uwezo wako huwezi kuyadhibiti kinachokutokea kiko nje ya uwezo wako kama unavyoona inzi hujawaleta wewe unawaona tu na wanakuletea usumbufu ndivyo ilivyo katika maswala yanayokutokea au yatakayokutokea  kwa imani kumbuka tu kuwa Mungu anatawala.

Mambo ya msingi yakupasayo kufanya

Hakuna sababu ya kuogopa unapoona inzi katika nyumba yako, hawako hapo kwa makusudi ya kukutisha lakini wako hapo kukupa ujumbe kuhusu mambo yajayo, hivyo jipange jipe moyo kaa tayari kukabiliana na lolote litakalokusibu, weka moyo wako kwenye mipango yako, wasiliana na watu muhimu sana katika maisha yako, fanya kazi kwa bidii weka mahusiano yako vizuri, usiogope jambo baya wala taarifa mbaya jiandae kukabiliana na lolote gumu litakalokukabili, Muombe sana Mungu kwa kuahirisha mambo mabaya na kumshihi Mungu alete mambo mema siku zote za maisha yako, hakikisha kuwa unakuwa safi kwani kama jinsi ambavyo inzi wanavutiwa na uchafu, lisiwepo ovu katika maisha yako litakalokuchafua.

KUMBUKA. Mafundisho haya ya katika shule za kinabii na kama imani yako inakinzana usitilie maanani wala usifundishe kanisani kwako!

Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!