Wafilipi 4:4-7 “Furahini katika Bwana
sikuzote; tena nasema, Furahini. Upole
wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yu karibu. Msijisumbue kwa neno lo lote;
bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na
zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo
yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.”
Utangulizi:
Yesu Kristo alisema Ulimwenguni mnayo
dhiki lakini jipeni moyo Mimi nimeushinda ulimwengu Yohana 16:33 “Hayo nimewaambieni mpate
kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi
nimeushinda ulimwengu.”,
Kwa kawaida tunapokuwa taabuni,
yaani tunapokutana na changamoto mbalimbali katika maisha yaani ile hali ya
changamoto zenye kuumiza au kukosesha Amani, au kuogopa au kuhisi kuwa
umeharibu, umeshuka moyo, umeumizwa, umepotezewa Amani una msongo wa Mawazo,
hasira na mashaka hali zote hizi zinatuweka katika taabu, na kwa mujibu wa
Biblia tunajifunza ya kuwa tuna uwezo wa kutawala na kuchukuliana na hali hizo
zote endapo tutaamua kufurahi na kujiendeleza katika tabia kujenga afya ya
kukabiliana na hali zote hizi ambazo ni kikwazo cha maendeleo yetu kimwili,
kiroho na kisaikolojia, maandiko yanasema tunaweza kuzitawala hali hizo. Ni
katika mazingira ya wakati mgumu kama huo Mungu anatufundisha namna tunavyoweza
sasa kujitawala wakati wa taabu, tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele
vitatu vifuatavyo:-
·
Agizo la kufurahi katika Bwana.
·
Mfano wa Paulo mtume kwa Wafilipi.
·
Unapokuwa katika wakati Mgumu.
Agizo la kufurahi katika Bwana.
Wafilipi 4:4-7 “Furahini katika Bwana
sikuzote; tena nasema, Furahini. Upole
wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yu karibu. Msijisumbue kwa neno lo lote;
bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na
zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo
yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.”
Kwa kawaida ni vigumu sana
kumwambia mtu afurahi hususani anapokuwa katika changamoto mbalimbali
nilizoziainisha hapo juu, unawezaje kufurahi, ukiwa unapitia taabu? Nawezaje
kufurahi ilihali ukweli niko taabuni sio swala jepesi, na Paulo mtume anawaagi
za Wafilipi wafurahi tena kwa msisitizo, Ni muhimu kufahamu kuwa Agizo la
Kufurahi kimsingi sio la Paulo Mtume, ni Agizo la kibiblia ni Agizo la Yesu
Kristo Mwenyewe Paulo mtume alirejea tu kile ambacho Kristo alikuwa amekiagiza
katika injili ya Yohana 16:33 kwa kawaida
unaposoma andiko hilo kidogo hususani katika lugha yetu ya Kiswahili
iliyotumika kutafasiri mstari huo badala ya kujipa moyo unaweza kukata tamaa
zaidi kwanini Kwa sababu Yesu au Mungu hawezi kutuambia TUJIPE MOYO Lugha hiyo ni lugha ya kibinadamu kwenda kwa mwanadamu
mwenzake, Mungu hana neno JIPE MOYO hana utakubaliana name tunapoangalia Mstari huu
tena na kuungalia kwa kina ona
Yohana 16:33 “Hayo nimewaambieni mpate kuwa
na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini JIPENI MOYO; mimi
nimeushinda ulimwengu.”,
John 16:33 “These things I have spoken unto
you that in me ye might have peace. In the world ye shall have tribulation but
BE OF A GOOD CHEER Ihave overcome the world”
Unapoyaangalia maandiko haya
katika tafasiri nyingine za kimaandiko huzusani Biblia ya kiyunani ambayo ndio
Lugha ya asili iliyotafasiri agano jipya katika Kiingereza na kisha Kiswahili
neno JIPE MOYO linasomeka kama
THARSEO ambalo tafasiri yake katika kiingereza ni BE OF A GOOD CHEER yaani FURAHINI AU CHANGAMKENI na
hiki ndicho ambacho Paulo anakisema sasa kwa wafilipi katika njia ambayo sasa
iko wazi zaidi kwa msingi huo sasa tafasiri halisi ya andiko hili la Yohana 16:33 ilitakiwa kuwa hivi “Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu.
Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini FURAHINI (CHANGAMKENI) (MSIOGOPE); mimi
nimeushinda ulimwengu.”,
Unaona hii inakubaliana kabisa na
tafasiri ya kiingreza ya Amplified Bible
ambapo mstari huo unasomeka “I have told you these things that in me you may have
peace. In the world you have trouble; but CHEER UP! I have overcome the world”
kwa msingi huo maandiko yanaagiza wakati wote kwamba tuchangamke, tusiogope
tufurahi tunapioangukia katika changamoto za aina mbalimbali hili lilikuwa
agizo la Bwana mwenyewe na mitume walifanya tu rejea ya mafundhisho ya Bwana,
Kumbuka atakapokuja roho mtakatifu atawakumbusha yote atatwaa katika yaliyo
yangu na kuwafundisha kwa hiyo agizo la kibiblia linatutaka tufurahi tunapokuwa
katika taabu na majaribu ya aina mbalimbali
Yakobo 1:2-4 “Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa
ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali; mkifahamu ya kuwa
kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi. Saburi na iwe na kazi kamilifu, mpate
kuwa wakamilifu na watimilifu bila kupungukiwa na neno.”
Marko 6:46-50 “Hata alipokwisha kuagana nao
akaenda zake mlimani kuomba. Na kulipokuwa jioni mashua ilikuwa katikati ya
bahari, na yeye yu peke yake katika nchi kavu. Akawaona wakitaabika kwa kuvuta
makasia, kwa maana upepo ulikuwa wa mbisho; hata ilipopata kama zamu ya nne ya
usiku akawaendea, akitembea juu ya bahari; akataka kuwapita. Nao walipomwona
anatembea juu ya bahari, walidhani ya kuwa ni kivuli, wakapiga yowe, kwa kuwa
wote walimwona, wakafadhaika. Mara akasema nao, akawaambia, Changamkeni; ni
mimi, msiogope.”
Kwa hiyo katika lugha halisi ya
kimaandiko Neno la Mungu halijawahi kuagiza tujipe moyo na badala yake
tuchangamke tusiogope na tufurahi na katika namna kama hiyo Paulo mtume
anawambia Wafilipi wafurahi tena nsema furahini hivyo tunapokuwa taabuni agizo
la kibiblia linatutaka tufurahi na kuchangamka, Bwana ampe neema kila mmoja
wetu kuwa na uwezo wa kuchangamka anapopita katika magumu sawa na mapenzi ya
Mungu katika jina la Yesu amen.
Mfano wa Paulo Mtume kwa Wafilipi.
Paulo mtume ni mfani hai unaoweza
kuigwa wa jinsi na namna ya kuwa wakati unapokuwa katika wakati mgumu, yeye sio
tu anawaagiza wafilipi wafurahi wakati wa changamoto, lakini yeye mwenyewe ni
mfano wa kuigwa wa kushangaza wakati kanisa hilo lilipokuwa linafunguliwa,
Paulo Mtume na rafiki yake Sila walipotembelea Filipi kwa mara ya Kwanza
kwaajili ya kuihubiri injili, walikamatwa na kupigwa mijeledi na kuvuliwa ngyo
zao mbele ya umati wa watu na kupigwa kinyama ona
Matendo 16:20-24 “wakawachukua kwa makadhi,
wakasema, Watu hawa wanachafua sana mji wetu, nao ni Wayahudi; tena wanatangaza
habari ya desturi zisizokuwa halali kwetu kuzipokea wala kuzifuata, kwa kuwa
sisi tu Warumi. Makutano wote wakaondoka wakawaendea, makadhi wakawavua nguo
zao kwa nguvu, wakatoa amri wapigwe kwa bakora. Na walipokwisha kuwapiga mapigo
mengi, wakawatupa gerezani, wakamwamuru mlinzi wa gereza awalinde sana. Naye
akiisha kupata amri hii akawatupa katika chumba cha ndani, akawafunga miguu kwa
mkatale.”
Unapoangalia kifungu hicho
unaweza kupata picha ya kuwa walikuwa katika wakati mgumu sana, wameaibishwa na
wamefedheheshwa na kupigwa bakora na kufungwa kama wahalifu, wakiwa na madonda
na wamewekwa gerezani katika gereza chafu, lililokuwa limechongwa juu ya kilima
pale Filipi, na kufungwa kwa mikatale
maana yake bado walikuwa katika wakati mgumu, lakini mwitikio wa matukio hayo
kwao na katika mioyo yao iilikuwaje? Na baada ya haya yote eti wao Paulo na
sila waliokuwa katika wakati Mgumu walianza kuomba na kisha kumsifu Mungu huku
wakisikilizwa na wafungwa wengine ona
Matendo 16:25-31 “Lakini panapo usiku wa
manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu,
na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. Ghafula pakawa tetemeko kuu la
nchi, hata misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka,
vifungo vya wote vikalegezwa. Yule mlinzi wa gereza akaamka, naye alipoona ya
kuwa milango ya gereza imefunguka, alifuta upanga, akataka kujiua, akidhani ya
kuwa wafungwa wamekimbia. Ila Paulo akapaza sauti yake kwa nguvu, akisema,
Usijidhuru, kwa maana sisi sote tupo hapa. Akataka taa ziletwe, akarukia ndani,
akitetemeka kwa hofu, akawaangukia Paulo na Sila; kisha akawaleta nje akasema,
Bwana zangu, yanipasa nifanye nini nipate kuokoka? Wakamwambia, Mwamini Bwana
Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako.”
Kama haya yangekuwa yamenipata
mimi au wewe Mungu angekuwa mahakamani, na angekula maswala makali sana
tungewezaje kumsifu Mungu katika hali kama ile?
Unakumbuka wana wa Israel walipochukuliwa utumwani kule Babeli kisha
waliowachukua mateka wakataka waimbe je waliweza?
Zaburi 137:1-4 “Kando ya mito ya Babeli
ndiko tulikoketi, Tukalia tulipoikumbuka Sayuni. Katika miti iliyo katikati
yake Tulivitundika vinubi vyetu. Maana huko waliotuchukua mateka Walitaka
tuwaimbie; Na waliotuonea walitaka furaha; Tuimbieni baadhi ya nyimbo za
Sayuni. Tuuimbeje wimbo wa Bwana Katika
nchi ya ugeni?”
Sio rahisi kama tunavyoweza
kudhani kile ambacho Mtume Paulo alikifanya na Sila wakiwa gerezani katika hali
kama ile sio rahisi, wana wa Israel walishindwa walipochukuliwa mateka, na
ugomzi mkubwa kweli ungekuwa kati yetu na Mungu, kwamba Mungu ee cha unafiki?
Unawezaje kuacha tumevuliwa nguo, unawezaje kuacha tunacharazwa bakora,
unawezaje kuacha tunapigwa na kuhukumiwa kwenda jela bila hatia? Unawezaje
kuwaacha wacheza disko huko nje afu sisi wamisionari unatuacha tunateseka hivi?
Alafu baadaye ndio unakuja kutikisha magereza kwa tetemeko kubwa na kuzifanya
pingu ziachie zenyewe? Lakini siri ya hekima
ya Mungu ni kubwa mno unaweza kuyatukuza matendo makuu ya Mungu kama ukielewa
njia zake angalia kwamba Mungu alikuwa na mpango wa kuokoa na kuliongeza kanisa
la filipi kwa kumuokoa mkuu wa gereza wafungwa na familia yake
Maana yake kila linapokuja swala
gumu katika maisha yetu, maswala hayo magumu yanakuja na majibu mazuri kutoka
kwa Mungu, kwa msingi huo ni muhimu kuyapokea majaribu yetu kwa furaha na Amani
ya Kristo, hivyo baadaye Paulo alipokuwa akiwaandikia waraka huu aliwaamuru
wafilipi wafurahi katika Bwana tena wafurahi.
Unapokuwa na magumu katika maisha
yako, msongo wa mawazo, kukata tamaa, kuchanganyikiwa, hofu za maisha, kazi,
ndoa, watoto na kila aina ya changamoto inayokukabili katika maisha yako
huipaswi kuogopa wala kukata tamaa na badala yake mtukuze Mungu, mshukur,
mwambie Mungu namna unavyompenda bado chagua kufurahi wakati wa changamoto zako
kwani kuchagua kufurahi maana yake ni kuchakua kumuamini Mungu na hapo Amani ya
Mungu itakuwa pamoja nasi.
Unapokuwa katika wakati mgumu!
Kwa hiyo tayari tuna majibu
kwamba wakati mambo magumu yanatupata tunapaswa kufurahi, lakini kwa nini
tufurahi hili ni jambo muhimu sana kulijibu, kwa sababu wote tunafahamu madhara
yanayosababishwa na huzuni, Huzuni ni kinyume cha furaha ni upande wa pili wa
maisha kama jinsi ambavyo kuna uzima na mauti, kuchagua huzuni ni kuchagua
mauti, kuchagua huzuni ni kuchagua kushindwa, kuchagua furaha ni kuchagua
ushindi, kuchagua huzuni ni kurudi nyuma kuchagua furaha ni kusonga mbele,
tunaweza kuutafasiri ulimwengu au maisha katima mitazamo tofauti kama tukiwa na
huzuni tunaweza kufikiri kuwa hatustahili tena, tumekataliwa, hatuna bahati,
mamb hayawezi kuwa, hatuwezi kusonga mbele, hatuwezi kuwa na Imani, hatuwezi
kuwa na matumaini tunakuwa na hisia za kupoteza lakini kuna athari nyingi za
kisaokolojia na kupoteza baadhi ya homoni katika wili wetu kama tukichagua
huzuni, ndio maana maandiko yanatutaka tufurahi unaona kwa hiyo unapohhisi
mambo sio mazuri
1.
Ingia
katika toba, usijali kuwa umemkosea Mtu au hujamkosea mtu, umemkosea Mungu
au hujamkosea Mungu lakini omba msamaha kwa Mungu.
2.
Omba
msamaha watu wote ambao u nadhani kuwa umehitilafiana nao hakikisha kuwa
uko vizuri na Mungu na wanadamu lakini
pia kama moyoni mwako kuna watu hujawasamehe samehe na au waweke mbali kabisa
na maisha yako kama watu waliopoteza thamani katika maisha yako, sio kila mtu
anakufaa katika maisha yako, wengine hawakufai na hivyo hupaswi kuwa nao
hususani kama kuwaacha hakuleti madhara katika maisha yako
Waebrania 12:14 “Tafuteni
kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu
atakayemwona Bwana asipokuwa nao;”
3.
Fanya
matengenezo, wakati wa mambo magumu kama tulizidiwa na maswala mbalimbali
tunaweza kujikuta tuliumiza watu wengine au tulichukua mali zao au kuharibu
vitu vyao au kutokuwalipa fedha zao hebu walipe
Luka 19:8 “Zakayo akasimama, akamwambia Bwana, Tazama,
Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang'anya mtu kitu kwa
hila namrudishia mara nne”.
4.
Furahia
siku zote na uwe mwenye mawazo chanya, Mwamini Mungu ukijua kuwa katika
kila jambo Mungu hufanya mambo yote yaani mema na hata mabaya kuwapatia mema
wale wampendao
Warumi 8:28 “Nasi
twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao
katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.”
Na. Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!