Ayubu 16:1-6 “Ndipo Ayubu akajibu, na
kusema, Nimesikia maneno mengi mfano wa hayo; Ninyi nyote ni wafariji wenye
kutaabisha. Je! Maneno yasiyo faida yatakuwa na mwisho? Au, kuna nini
kinachokukasirisha, hata ukajibu? Mimi nami ningeweza kunena kama ninyi; Kama
roho zenu zingekuwa mahali pa roho yangu, Ningeweza kutunga maneno juu yenu, Na
kuwatikisia ninyi kichwa changu. Lakini ningewatia nguvu kwa kinywa changu, Na
utuzo wa midomo yangu ungetuliza. Nijapokuwa nanena, huzuni yangu haitulizwi;
Nijapokuwa najizuia, nimepunguziwa kitu gani? ”
Utangulizi:
Kitabu cha Ayubu ni moja ya
kitabu kilichoandikwa kwaajili ya kutoa majibu kwa ulimwengu kuhusu falsafa ya
mateso, kwanini maisha ya mwanadamu hukutana na changamoto za aina mbalimbali,
lakini sio hivyo tu kujibu pia swali kwanini wenye haki nao wanateseka? Ayubu alikuwa mtu mwenye haki mbele za Mungu,
hata hivyo alikumbana na mateso makubwa ya aina mbalimbali, ambayo aliyavumilia
na mwisho wake ukawa mwema, Ayubu leo amekuwa mfano mzuri na mwema wa kuigwa
katika swala zima la kuvumilia mateso na kuonyesha wema wa Mungu kwetu pale
tunapovumilia, Mungu ni mwingi wa rehema na mwenye huruma
Yakobo 5:10-11 “Ndugu, watwaeni manabii
walionena kwa jina la Bwana, wawe mfano wa kustahimili mabaya, na wa uvumilivu.
Angalieni, twawaita heri wao waliosubiri. Mmesikia habari ya subira yake Ayubu,
mmeuona mwisho wa Bwana ya kwamba Bwana ni mwingi wa rehema, mwenye huruma.”
Pamoja na mapito aliyokuwa
akiyapitia Ayubu lakini vilevile Maandiko yanatufundisha kuwa wakati tunapopitia
mambo magumu kwa kawaida wanakuwepo watu wanaokuja katika maisha yetu na kutoa
ushauri/kufariji au kusema hili au lile kutokana na mapito tunayoyapitia wakati
mwingine watu hao wakiwa na nia njema na wakati mwingine wakiwa hawajui
wanachoweza kusema kuhusiana na mapito yako kama kiko sahihi au la kama ni
mapenzi ya Mungu au la, na wakati
mwingine sio rahisi kujua siri ya mapito anayoyapitia mtu isipokuwa Mungu
mwenyewe, wakati Ayubu alipokuwa akipitia wakati Mgumu neno linatueleza kuwa
alitembelewa na rafiki zake watatu ambao walikuja kwa kusudi la kumfariji
kutokana na mapito aliyokuwa anayapitia ona:-
Ayubu 2:11-13 “Basi ikawa hao rafikize Ayubu watatu walipopata habari ya
mabaya hayo yote yaliyomfikilia, wakaja kila mtu kutoka mahali pake; nao ni
Elifazi Mtemani, na Bildadi Mshuhi, na Sofari Mnaamathi; wakapatana pamoja ili
waende kumlilia Ayubu na kumtuliza moyo. Basi walipovua macho yao, nao wakali
mbali, wasimtambue, wakainua sauti zao na kulia; kila mmoja akararua joho yake,
wakarusha mavumbi juu ya vichwa vyao kuelekea mbinguni. Kisha wakaketi nchi
pamoja naye muda wa siku saba, mchana na usiku, wala hapana mmoja aliyenena naye
neno lo lote; kwa maana waliona ya kuwa mashaka yake aliyo nayo ni makuu mno.”
Elifazi Mtemani, Bildadi Mshuhi
na Sofari mnaamathi walikuwa na nia njema na nzuri kabisa ya kumfariji Ayubu na
mioyo yao na matendo yao yanadhihirisha kuwa walikuwa wako sahihi katika
kutafuta namna ya kumfariji ndugu yao kutokana na mambo magumu aliyoyapitia,
hata hivyo katika namna ya kushangaza sana baada ya wao kutoa hoja mbalimbali
Ayubu aliwaita watu hao au rafiki zake kuwa ni WAFARIJI WENYE KUTAABISHA angalia hapa Ayubu 16:2 “Nimesikia maneno mengi mfano
wa hayo; Ninyi nyote ni wafariji wenye kutaabisha.” sasa swali kubwa
kwetu na macho yetu ni kuliangalia jambo hili kwa kina na mapana na marefu kuwa
wafariji wenye kutaabisha ni watu wa namna gani ? na ni vipi tunaweza kukabiliana nao
wanapojitokeza katika maisha yetu, na kama sisi nasi tunataka kuwa wafariji na
washauri wa wengine ni tahadhari gani tunapaswa kuzizingatia. Tutajifunza somo
hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Maana ya Wafariji wenye kutaabisha
·
Jinsi Mtu anavyoweza kuwa mfariji mwenye
kutaabisha
·
Namna ya kujiepusha na wafariji wenye kutaabisha
au kuwa wafariji wenye kutaabisha
Maana ya Wafariji wenye kutaabisha:
Ayubu 16:1-6 “Ndipo Ayubu akajibu, na
kusema, Nimesikia maneno mengi mfano wa hayo; Ninyi nyote ni wafariji wenye
kutaabisha. Je! Maneno yasiyo faida yatakuwa na mwisho? Au, kuna nini
kinachokukasirisha, hata ukajibu? Mimi nami ningeweza kunena kama ninyi; Kama
roho zenu zingekuwa mahali pa roho yangu, Ningeweza kutunga maneno juu yenu, Na
kuwatikisia ninyi kichwa changu. Lakini ningewatia nguvu kwa kinywa changu, Na
utuzo wa midomo yangu ungetuliza. Nijapokuwa nanena, huzuni yangu haitulizwi;
Nijapokuwa najizuia, nimepunguziwa kitu gani? ”
Moja ya swali muhimu la kujiuliza
hapa ni kwanini Ayubu anawaita watu hawa kama wafariji wenye kutaabisha japo
tunaweza kuwa na ufahamu kuwa walikuwa na nia nzuri na walijitahidi kwa kadiri
ya hekima waliyokuwa nayo, kumtia moyo lakini mwisho wa yote walikuwa ni
wafariji wenye kutaabisha na Mungu aliwakemea kuwa hawakunena sawasawa na Mungu
wala sawasawa na Mtumishi wake Ayubu na hivyo walitakiwa kutoa dhabihu kuomba
radhi kwa uovu wao!
Neno wafariji wenye kutaabisha
kimsingi katika biblia ya kiingereza Mstari wa pili ambao ni wa msingi katika
somo letu unasomeka hivi
“I have heard many such things MISERABLE
COMFORTERS are ye all” neno
MISERABLE kwa kiibrania ni “AMAL”
ambalo maana yake ni wenye kulaumu, wenye kukutendea vibaya, wenye unyanyasaji,
wenye kuchosha, wenye kuumiza, wenye kuhuzunisha, wenye maumivu, wenye
kuogopesha, wenye uovu, wenye kuchosha, wenye kutia uvivu, wenye kukatisha
tamaa, wenye kuvunja moyo, wenye uovu, wasiyo na kweli, wenye kupotosha. Neno hilo AMAL
limetumika mara 55 Katika Biblia
na katika mistari tofauti 54
Kwa msingi huo Ayubu alikuwa
anamaanisha kuwa ameshawasikia watu wengi kama hawa na kuwa katika faraja na ushauri
waliokuwa wakijaribu kuutoa walikuwa wametoka nje ya makusudi na mpango wa
Mungu kwa sababu hiyo badala ya kumfariji, walikuwa wakizungumza tu na kwa
kweli walikuwa wametoka pia nje ya
kusudi na ukweli kuhusu mtazamo wa Mungu, kwa ujumla walikuwa nje ya kweli ya
Mungu, tena wala walikuwa hawawakilishi mfumo na sifa za Mungu, kwa hiyo Ayubu
alipowasikiliza aliona wazi kuwa wanamkosea Mungu mno, walikuwa wanahisi tu
jambo Fulani kuhusu utendaji wa Mungu wakati wa majaribu ya mtu lakini haikuwa
kweli ya Mungu wala kusudi la Mungu na pia walikuwa wakimshutumu Mtumishi wa
Mungu Ayubu kwamba ana kesi ya kujibu katika mabaya aliyokuwa anayapitia n
ahata watoto wake waliokufa vibaya walikuwa na makosa Fulani na kwa sababu hiyo
ingawa walikuja kwa wakati kwa kusudi la kumfariji na kumshauri Ayubu walijikuta wanapotosha, wanamuumiza
zaidi, wanamvunja moyo, wananena uovu, wanasema yasiyo kweli, wanamchosha na
wanamuumiza hali kama hii inaweza kuwepo kwa watu wengi wanaotuzunguka katika
nyakati zetu hata siku za leo!
Ayubu alikuwa amepitia majaribu
makubwa na mazito mno kiasi cha kupatwa na mashaka makubwa sana, rafiki zake
waliojitokeza kumfariji badala ya kumpunguzia maumivu aliyokuwa akiyapitia wao
waliongeza huzuni na maumivu mtazamo wao kuhusu majaribu ulikuwa ukimtaka Ayubu
akiri na kutubu dhambi zake ili Mungu aondoe adhabu aliyoiweka juu yake
Ayubu 11:14-17. “Ikiwa una uovu mkononi
mwako, uweke mbali nawe, Wala usikubali upuzi kukaa hemani mwako; Hakika ndipo
utakapopata kuinua uso pasipo ila; Naam, utathibitika, wala hutakuwa na hofu;
Kwa kuwa utasahau mashaka yako; Utayakumbuka kama maji yaliyokwisha pita; Na
maisha yako yatakuwa meupe kuliko adhuhuri; Lijapokuwa ni giza, litakuwa kama
alfajiri.”
Ayubu 22:4-7 “Je! Ni kwa wewe kumcha yeye
anakukemea? Na kuingia hukumuni nawe? Je! Uovu wako si mkuu? Wala maovu yako
hayana mwisho. Kwa kuwa umetwaa dhamana kwa nduguyo bure, Na kuwavua nguo zao
walio uchi. Hukumpa maji ya kunywa huyo aliyechoka, Nawe umemnyima chakula huyo
mwenye njaa.”
Sio jambo la kushangaza hata
katika siku zetu leo, pale tunapopatwa na mapito magumu, majaribu magumu na
mitihani ya aina mbalimbali, wafariji wengi na washauri hukimbilia katika hatima
ya kusema kuwa ni kwa sababu tu mefanya dhambi, au kuna kosa kubwa sana ambalo
mtu amelifanya na sio hivyo tu hata
katika nyakati zetu leo watu wengi sana hufikiri kuwa mtu akiwa na mafanikio ya
mwilini basi yuko vizuri na Mungu na mtu akiwa na majanga basi kutakuwa kuna
shida katika mahusiano yake na Mungu
fikira za namna hii sio tu zinawakosesha amani wanaopita katika mapito
bali pia zinaharibu mtazamo wa utendaji wa Mungu na kupotosha ukweli kuhusu
utendaji wa Mungu!, badala ya watu kushauri vema na kukujenga wanakubomoa na
kuichoma nafsi yako kiasi ambacho wanataka kukugombanisha wewe na Mungu,
Wafariji wa namna hii huongezea Msiba wakati wa matatizo badala ya kukusaidia
hao ndio wanaitwa wafariji wenye kutaabisha!
Jinsi Mtu anavyoweza kuwa mfariji mwenye kutaabisha
1.
Mtu
anayefikiri kila mwanadamu anayeteseka ni kwa sababu amefanya dhambi - Mfariji mwenye kutaabisha ni mtu awaye yote
anayedhani kuwa kila taabu anayoipitia mtu ni kwa sababu aidha mtu huyo
amefanya dhambi au wazazi wake, haya ndio yalikuwa mawazo ya wanafalsafa
waliokwenda kumshauri na kumfariji Ayubu wao walikuwa na dhana inayoathiri
wengi hata katika nyakati za leo, miongoni mwa watu wengi sana waliookoka leo
wakiona mtu aliyeokoka anapatwa na mabaya wanadani kuwa mtu huyo ni mbaya au
kuna dhambi ameifanya hajaitubia, au Mungu anashughulika naye anamuadhibu aina
hii ya dhana ilikuwepo pia miongoni mwa wanafunzi wa Yesu na Yesu alikuwa
tofauti na mtazamo wao?
Yohana 9:1-3 “Hata
alipokuwa akipita alimwona mtu, kipofu tangu kuzaliwa. Wanafunzi wake wakamwuliza wakisema, Rabi, ni
yupi aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake, hata azaliwe kipofu? Yesu
akajibu, Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake; bali kazi za Mungu
zidhihirishwe ndani yake.”
2.
Mtu
anayefikiri kuwa kila mwanadamu anayeteseka anavuna alichokipanda – Ni
ukweli ulio wazi kuwa maandiko yanazungumza juu ya kuwepo kwa kanuni ya kupanda
na kuvuna
Wagalatia 6:7-9 “Msidanganyike,
Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna. Maana
yeye apandaye kwa mwili wake, katika mwili wake atavuna uharibifu; bali yeye
apandaye kwa Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele. Tena tusichoke katika
kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho.”
Wako watu
duniani ambao wanadhani ya kuwa unapopita katika mapito Fulani basi ni kwa
sababu ulipanda au kuna mtu kwenye ukoo wenu au baba zako alipanda ubaya Fulani
na sasa unateseka kwa sababu unavuna au wewe ulifanya uovu Fulani na sasa
unakujilia juu yako na wanaweza kumuhusisha Mungu katika jambo hilo kwamba
Mungu analeta mabaya juu yako kwa sababu ya ubaya Fulani ulioutenda hii pia
ilikuwa falsafa ya rafiki zake Ayubu walipokuja kumfariji, na watu wengi leo
wana mtazamo kama huo wa KARMA lakini sio kila mapito yanatokana na Karma au
mavuno Fulani.
3.
Mtu
anayefikiri kuwa wewe hufanikiwi au
hupati muujiza kwa sababu huna Imani - wako
watu wengi sana ambao wakati mwingine wanaweza kuhukumu wenzao kuwa wewe hupati
muujiza wako au Mungu hakufanyii jambo Fulani kwa sababu huna Imani, wakati
wote wao wanafikiri tu kuwa Imani yao ndio imewasaidia kufikia hali
waliyoifikia na wale wasio na imani wamebaki na michangamoto yao, falsafa na
dhana ya namna hii pia inamuweka Mungu katika nafasi ya kufikiriwa kuwa
anahusiana na wenye Imani pekee lakini maandiko yanamaanisha Imani ina pande
mbili, na zote ni Imani.
Waebrania 11:35-39 “Wanawake walipokea wafu wao waliofufuliwa. Lakini wengine waliumizwa
vibaya hata kuuawa, wasikubali ukombozi, ili wapate ufufuo ulio bora; wengine
walijaribiwa kwa dhihaka na mapigo, naam, kwa mafungo, na kwa kutiwa gerezani; walipigwa
kwa mawe, walikatwa kwa misumeno, walijaribiwa, waliuawa kwa upanga; walizunguka-zunguka
wakivaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi; walikuwa wahitaji, wakiteswa,
wakitendwa mabaya; (watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao), walikuwa
wakizunguka-zunguka katika nyika na katika milima na katika mapango na katika
mashimo ya nchi. Na watu hao wote wakiisha kushuhudiwa kwa sababu ya imani yao,
hawakuipokea ahadi;”
Je watakatifu
waliouawa kwaajili ya Imani, kina Stefano waliopigwa mawe na kufa kwaajili ya
neno la uzima je walikuwa hawana Imani? Au Kristo mwenyewe mwenye haki
aliyesulubiwa na kufa kifo kibaya msalabani je hakuwa na Imani? Watakatifu waliopitia mateso na changamoto
mbalimbali je walikuwa wamemkosea Mungu kuna haja ya kupanua mtazamo wako
kuhusu changamoto mbalimbali wanazopitia watu wote duniani!
4.
Mfariji
mwenye kutaabisha huzungumza zaidi ya kile anachokijua – Wafariji wengi
wenye kutaabisha ni wepesi kuzungumza na ni wepesi kufikiri na kutoa maoni, na sio wepesi kusikiliza, unaweza kuwa kwenye
ndoa kama ya kwangu ina miaka 22 mimi ndio naishi na mke wangu, lakini kuna mtu
anaweza kuja tu na kujifanya anatujua vizuri kuliko tunavyojijua kwa habari za
kusikia tu, wafariji wenye kutaabisha hujifanya wanajua kila kitu, wanaweza
kujifanya wanamjua mumeo kuliko wewe au wanamjua mkeo kuliko wewe au wanajua
sana maisha yako au wana taarifa zako za miaka na siku nyingi au wanajua hata
dhambi zako za zamani, hawajui kama ulitubu au la hawajui uhusiano wako na
Mungu lakini wanaweza kujifanya wanajua na wakakizungumza kwa kujiamini na kwa
uhakika kumbe wako mbali sana na mapenzi ya Mungu, Wako watu wanaweza kujua hata kwanini unaugua figo, na
wakawa na majibu yao, wanaweza kujua hata kwanini uliachishwa kazi na wakawa na
majibu yao, wanaweza wakawa na jibu la kila kitu, Rafiki za Ayubu walikuwa na
dhana kuwa dhambi inaleta changamoto za kila aina na haki inaleta thawabu na
Baraka tele na mafanikio kwa hiyo hata kufa kwa watoto kumi wa Ayubu wao
waliona kuwa huenda watoto hao walikuwa wamefanya dhambi na wakazungumza kwa uhakika ona
Ayubu 8:2-4 “Wewe
utanena maneno haya hata lini? Maneno ya kinywa chako yatakuwa kama upepo mkuu
hata lini? Je! Mungu hupotosha hukumu? Au, huyo Mwenyezi hupotosha yaliyo ya
haki? Kwamba watoto wako wamemfanyia dhambi, Naye amewatia mkononi mwa kosa lao;”
Unaona Wafariji
na washauri wa Ayubu walimwambia kuwa Mungu amewaua watoto wako kwa sababu
walikuwa wamemfanyia Mungu dhambi na Mungu amewashughulikia kwaajili ya makossa
yao! Wafariji wenye kutaabisha kwa ujumla huwa hawajui hata wanayoyazungumza,
wao wanazungumza kwa uzoefu wa falsafa za dunia na hawawezi kuingia kwenye
mashauri ya Mungu na kujua Mungu alikuwa anamaanisha nini na kwanini mambo
yanatokea katika namna yanayotokea, lakini pia walikuwa wanadhani tu kwa
kuunganisha mambo, na badala ya kumfariji Ayubu katika mapito yake walimuhukumu
yeye na familia yake ! na badala ya kumpunguzia Msiba wake waliongeza huzuni
zake!
5. Mtu anayefikiri kuwa kikombe chako kimejaa
- Kwamba Mungu huwa anahifadhi maovu anaandika
mahali anakuangaliaaaaa afu kuna mstari mwekundu, kuna kikombe chako mahali
siku kikijaaa sasa hasira zake zinawaka na anaanza kukushughulikia hii ni dhana
ambayo imejengeka sana kwa watu wa Mungu kama wanajadili jambo kuhusu mapito
yako wanaweza kusikika na kusema aaa
jamaa bhana kikombe chake kimejaa!:, Hata sijui imeandikwa wapi au iko eneo gani
katika maandiko ambapo Mungu emeeleza kuwa kuna matone ya dhambi yanaingia afu
kikombe chako kikijaa anakushughulikia! Yaani tunaye baba Mbinguni ambaye
anavizia maovu yetu yafikie kiwango Fulani alafu anamwaga mihasira yake ahaaaa
ee kikombe kimejaa yaani kuna mambo kadhaa ulikuwa huyafanyi sasa Mungu ndio
anashughulikna na wewe ulikuwa hutoi zaka, uliwaabisha wengine, uliwanyima
chakula wenye njaa, hukuwajali wajane, hukuwajali yatima, hukwenda kuona
wafungwa, uliwanyima maji wenye kiu, ulipendelea watu, uliwapuuzia yatima na
wajane, ulikuwa na hiki ama kile kwa hiyo baada ya mlolongo huo mkubwa Mungu
alikuwa anakucheki tu sasa kikombe kimejaa anakushughulikia ahaaa ona dhana kama hii ilikuwa katika mioyo ya
wafariji wa Ayubu waliokuja kumfariji na kumshauri n ahata leo wako watu wenye
mitazamo kama hiyo
Ayubu 22::5-10 “Je!
Uovu wako si mkuu? Wala maovu yako hayana mwisho. Kwa kuwa umetwaa dhamana kwa
nduguyo bure, Na kuwavua nguo zao walio uchi. Hukumpa maji ya kunywa huyo
aliyechoka, Nawe umemnyima chakula huyo mwenye njaa. Lakini huyo shujaa, nchi
ilikuwa yake; Na huyo mwenye kusifiwa, yeye aliikaa. Umewafukuza wanawake
wajane hali ya utupu, Na mikono ya mayatima imevunjwa. Kwa hiyo umezungukwa na
mitego, Na hofu ya ghafula yakutaabisha,”
6.
Wafariji
wenye kutaabisha hujiweka katika nafasi ya Mungu kuhukumu - wakati ukiwa katika changamoto mbalimbali
za maisha saa ya kujaribiwa kwako wafariji wenye kutaabisha hujisahau na kukaa
katika nafasi ya Mungu wakijifanya
kuamua hatima ya maisha yako, au wakitaka kumsaidia Mungu kukuonjesha machungu
zaidi, kumbe badala yake wanamkosea Mungu, waliokuja kumfariji Ayubu wote
walihukumiwa na Mungu na ukweli ni kuwa Mungu alikasirishwa nao sana kwa kuwa hawakuwa sahihi kwa jinsi na
namna walivyoshughulika na Ayubu
Ayubu 42:7-10 “Basi
ikawa, baada ya Bwana kumwambia Ayubu maneno hayo, Bwana akamwambia huyo
Elifazi Mtemani, Hasira zangu zinawaka juu yako, na juu ya hao rafiki zako
wawili; kwa kuwa ninyi hamkunena yaliyo sawa katika habari zangu, kama
alivyonena mtumishi wangu Ayubu. Basi sasa, jitwalieni ng'ombe waume saba, na
kondoo waume saba, mkamwendee mtumishi wangu Ayubu, mjisongezee sadaka ya
kuteketezwa; na huyo mtumishi wangu Ayubu atawaombea ninyi; kwa kuwa
nitamridhia yeye, nisiwatende sawasawa na upumbavu wenu; kwani ninyi hamkunena
maneno yaliyonyoka katika habari zangu, kama alivyonena mtumishi wangu Ayubu.
Basi Elifazi, Mtemani, na Bildadi, Mshuhi, na Sofari, Mnaamathi, wakaenda,
wakafanya kama vile Bwana alivyowaamuru; naye Bwana akamridhia Ayubu. Kisha
Bwana akaugeuza uteka wa Ayubu, hapo alipowaombea rafiki zake; Bwana naye
akampa Ayubu mara mbili kuliko hayo aliyokuwa nayo kwanza.”
Wafariji hawa
walikosea hawakusema sawasawa kwa habari ya Mungu wala kwa habari za mtumishi
wake Ayubu, na hivyo walikuwa na hatia walipata dhambi ambayo ilihitaji tena
watoe dhabihu kisha waombewe na Ayubu ili Mungu aweze kuwarehemu! Je unapenda
sana kujishaua shaua na kuingilia mambo ya watu katika maisha yao? Je unadhani
uko sahihi kila wakati unaponena neno juu ya Masihi wa Bwana na mapito
yake? Je unadhani uko salama
unapoongezea mateso juu ya watu wa Mungu, Je unadhani uko sahihi wakati wote
unapojifanya unatoa ushauri kuhusu maisha na huduma ya Mtu wa Mungu? Je wewe
ndio Mungu je wewe ndiye uliyemuita, je wewe ndio unajua anakokokwenda? Je wewe unajifanya una uelewa mkubwa sana wa
neno la Mungu kuliko mtu anayepitia mateso? Je wewe kwenye raha zako unadhani
una ukaribu na Mungu kuliko mtu anayepitia kwenye mateso? Au mtu aliyevunjika
moyo? Wengi wa watu wanaojifanya
wafariji, au washauri ndio wanaoharibu maisha ya watu zaidi na kumkosea Mungu
kuliko unavyodhani kwa msingi huo lazima kila mmoja achukue tahadhari na kuacha
kuingilia mapito na njia za mtu, tuwe marafiki tu, tuombeane tu lakini huna
mamlaka ya kuingilia na kumuamulia mtu mpango wa Mungu alioukusudia kwa watu
wake na maisha yake na mapito yake, Mungu akulinde wewe na mimi ili tusiwe miongoni
mwa watu watakaokuwa wafariji wenye kutaabisha
Namna ya kujiepusha na wafariji wenye kutaabisha au kuwa wafariji wenye
kutaabisha
1. Acha kumuwazia Mungu kwa upumbavu!
Ni vizuri kukaa
kimya wakati changamoto zinapozuka katika maisha yetu na kuacha kabisa
kumuwazia Mungu kwa upumbavu, hakuna jambo linaweza kuhatarisha maisha yetu
kama kukimbilia kuzungumza mambo kana kwamba tunajua sana, duniani kuna watu ni
wajuaji kila kitu wanadhani wanakijua na wana majibu ya kila kitu, maandiko
yanatufundisha kuwa ni vizuri kukaa kimya na kujichunga sana tunapozungumza
mambo na zaidi pia tunaloliwaza kuhusu Mungu.
Ayubu 1:20-22 “Ndipo
Ayubu akainuka, akalirarua joho lake, kisha akanyoa kichwa chake, na kuanguka
chini, na kusujudia; akasema, Mimi nilitoka tumboni mwa mama yangu nili uchi, nami
nitarudi tena huko uchi vilevile; Bwana alitoa, na Bwana ametwaa; jina la Bwana
na libarikiwe. Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi, wala hakumwazia
Mungu kwa upumbavu.”
Kufikiri kuwa
kila mwanadamua aneyeteseka duniani ni kwa sababu ametenda dhambi ni kumwazia
Mungu kwa upumbavu, hivi wewe ni mkamilifu kiasi ya kwamba Mungu anakuacha?
Kama Mungu anagekuwa anamtesa kila mtu kwa sababu ya dhambi basi wanadamu wote
wangekuwa walelazwa kwa mateso na magonjwa kutokana na uovu tulio nao maandiko
yanaonyesha kuwa watu wote wamefanya dhambi na hakuna mwenye haki hata mmoja
wala hakuna anayemtafuta Mungu Ayubu anatajwa kuwa alikuwa Mcha Mungu
Warumi 3:10-12 “kama
ilivyoandikwa, ya kwamba, Hakuna mwenye haki hata mmoja. Hakuna afahamuye;
Hakuna amtafutaye Mungu. Wote wamepotoka, wameoza wote pia; Hakuna mtenda mema,
la! Hata mmoja.”
Kama unataka
kuwa mshauri mzuri na mfariji mzuri uwe na uwezo mkubwa wa kulijua neno la
Mungu na kumjua Mungu, na kuyajua mapenzi yake na njia zake, huwezi kuwa
mfariji sahihi kama humjui Mungu wala neno lake na tabia zake na njia zake,
tukilijua neno vema na tabia za Mungu na mapenzi yake tunaweza kufaa kuwa
wafariji wazuri kwa kuwa tutawaelekeza watu katika kumuamini Mungu na kuwatia
moyo wanapopitia katika changamoto mbali mbali, Mungu hana mahali ambapo
anaweka rekodi ya uovu na kusubiri kikombe kijae, wala alishasema watoti
hawatateseka kwa sababu ya dhambi za baba zao
Zaburi 130:3-4 “Bwana,
kama Wewe ungehesabu maovu, Ee Bwana, nani angesimama? Lakini kwako kuna
msamaha, Ili Wewe uogopwe.”
Ezekiel 18:20 “Roho
itendayo dhambi, ndiyo itakayokufa; mwana hatauchukua uovu wa baba yake, wala
baba hatauchukua uovu wa mwanawe, haki yake mwenye haki itakuwa juu yake, na
uovu wake mwenye uovu utakuwa juu yake.”
2. Usiwe na majibu ya suluhisho la tatizo
moyoni mwako
Marafiki wa
Ayubu walifanya mambo mazuri kama matatu hivi waliposikia kuwa Ayubu amepatwa
na majanga walimtembelea ni tofauti kidogo na nyakati za leo ambapo watu
hukukimbia kama walivyomkimbia watu wengine, pili walilia kwa sauti kuu na
kurarua mavazi yao kuonyesha kuwa waliguswa na changamoto alizopitia jamaa yao na mwisho walikaa pamoja naye tena walikaa
kimya kwa siku saba.
Tatizo lao ni
kuwa hawakuweza kukaa kimya walikuwa na tafasiri yao kuhusu mateso yaliyompata
Ayubu na walikuwa wanamtaka atubu ili kwamba Mungu aweze kumsamehe na kumbariki
tena hii ilikuwa ushauri na suluhisho, nimeshakutana na watu wengi sana ambao
unapokutana na changamoto wao wanakuambia UTUBU
ni kana kwamba wewe kuna makosa Fulani makubwaaa umemfanyia Mungu na ndio maana
unapitia hali unayoipitia, wanadhani kuwa sifahamu umuhimu wa toba wanadhani
labda ninajihesabia haki kama ilivyo kwa Ayubu maandiko yalionyesha wazi kuwa
Ayubu alikuwa safi, na Mungu mwenyewe alikuwa amejivunia kuhusu Ayubu na
Shetani pia alikiri kuwa Ayubu alikuwa mwadilifu, kwa msingi huo basi ni wazi
kuwa mapito ya Ayubu hayakuwa na uhusiano wowote na tabia zake, aidha wako watu
ambao ukikosea wanataka kuona unaadhibiwa na Mungu na unapitia mambo magumu
hata adhabu wanatoa wao haya ni makosa makubwa sana ya kitheolojia na ujuzi
hafifu kuhusu Mungu, na neno lake, Mungu ni mwema na huwapa jua lake na mvua
yake wema na waovu, linapokuja swala la
mapito huwa halichagui
Ayubu 2:9-10 “Ndipo
mkewe akamwambia, Je! Wewe hata sasa washikamana na utimilifu wako? Umkufuru
Mungu, ukafe. Lakini yeye akamwambia, Wewe wanena kama mmoja wa hao wanawake
wapumbavu anenavyo. Je! Tupate mema mkononi mwa Mungu, nasi tusipate na mabaya?
Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi kwa midomo yake.”
Hatupaswi
kuhisi tu kuwa mtu Fulani anapitia hali Fulani kwa sababu Fulani kwani kufanya
hivyo pia ni kuingilia UBWANA wa Mungu, na hili ndio sababu iliyopelekea Mungu
akawakemea Rafiki za Ayubu
3. Zingatia kanuni za ushauri au kufariji
Ziko kanuni
ambazo mfariji anapaswa kuzizingatia anapokwenda kumfariji mtu na kumshauri
ikiwa ni pamoja na kuvaa kiatu na yeye
aliyepatwa na majanga Warumi 12:15 “Furahini pamoja nao wafurahio; lieni pamoja nao waliao.”
Kila mfariji lazima awe na uelewa wa kutosha kuhusu mapito na njia za Mungu,
achana kabisa na mitazamo yenye kuhukumu achana nayo, hakikisha unakuwa na
usiri na sio kutangaza siri za Muhusika, zingatia tamaduni za wahusika, acha
kwenda kuwasanifu, watie moyo unaowafariji sawa sawa na mtazamo wao au wa neno
la Mungu na mapenzi ya Mungu, waunge mkono isipikuwa tu kama fikira zao haziko
sawa na Mapenzi ya Mungu, hakikisha unamjua Mungu vizuri na njia zake, kumbuka
kuna wanaopatwa na ubaya kwa sababu ya mabaya lakini si kila anayepatwa na
mabaya ni mbaya, Panua mtazamo wako wa kitheolojia na upana wa mapito katika
mtazamo wa Mungu, Inua macho yako na kuchukua tahadhari kuhusu wema wa Mungu.
Hitimisho:
Hatuna budi
kumuomba Mungu ili siku zote tuweze kuwa marafiki wazuri, wafariji wasioleta misiba,
na washauri wenye weledi ili kwamba wale wote wanaopitia mapito ya aina
mbalimbali na huzuni na magumu na maumivu tuweze kujua namna ya kuwatia moyo
katika Mungu, wakati mwingine kama hatuna ufumbuzi wa jambo ni vema kukaa kimya
usijitie kimbelembele kama mzungumzaji, Tumuombe Mungu atusaidie kama tunataka
kusema tuseme yaliyo kweli na yale tunayoyajua na yaliyoko kwenye mapenzi yake,
kama watu wana dhambi tuwaongoze kwenye mema, tuwe wafariji wenye haki, na sio
wafariji wenye kutaabisha.
Na Rev. Innocent
Mkombozi Kamote
Mkuu wa
Wajenzi mwenye Hekima!